KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, January 7, 2013

YANGA KUKIPIGA NA WATURUKI KESHO



TIMU ya soka ya Yanga kesho inashuka tena dimbani kukipiga na timu ya Denizlispor FC ya Uturuki, inayoshiriki michuano ya ligi daraja la kwanza katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika katika uwanja wa Selen Football -Kalimya Complex pembeni kidogo ya mji wa Antlaya.


Yanga, ambayo imeweka kambi ya mafunzo jijini Antalya, itautumia mchezo huo kama fursa ya kujipima nguvu na timu hiyo, ambayo  imeshuka kutoka ligi kuu ya Uturuki mwaka jana na hivi sasa inapambana kurudi tena katika ligi kuu ya Uturuki.

Kocha Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts amesema kwao ni furaha kupata nafasi ya kucheza na timu kubwa kama ya Denizlispor FC, ambayo inaundwa na wachezaji wa kiwango cha kimataifa hivyo anaamini utakuwa mchezo safi na wa kuwavutia.

"Baada ya kuwa na wiki moja ya mazoezi na mechi moja ya kirafiki dhidi ya Armini Bielefeld ya Ujerumani mwishoni mwa wiki iliyopita, hii itakuwa fursa nyingine nzuri ya kucheza mchezo wa kirafiki na timu nyingine, hii itanisadia kuona maendeleo ya kikosi changu kutokana na mazoezi ambayo tumekuwa tukiyafanya tangu tulipofika hapa," alisema Brandts.

Denizlispor FC ni miongoni mwa timu zaidi ya 200 kutoka sehemu tofauti duniani, ambazo zimeweka kambi katika mji wa Antlaya kwa ajili ya maandilizi ya mzunguko wa pili wa ligi daraja la kwanza nchini Uturuki.

Mchezaji wa zamani wa Leicester City ya Uingereza, Dundee United ya Scotland na Ivernes ya Uholanzi, mtanzania mzaliwa wa Uingereza, Eric Odhiambo ni miongoni mwa washambuliaji wa kutegemewa wa timu ya Denizlispor FC.

Kikosi cha wachezaji 27 wa Yanga waliopo mjini Antalya wote wako katika hali nzuri na hakuna majeruhi hata mmoja, hali itakayomfanya Brandts kuamua kumtumia mchezaji yoyote katika mchezo huo.

Athumani Idd 'Chuji' na Hamis Kiiza waliokuwa wakijisikia vibaya kabla ya mchezo wa juzi dhidi ya Amrnini Bielefeld wanaendelea vizuri kwani wanaendelea na mazoezi pamoja na wachezaji wengine waliopo na timu mjini Antalya.
Kuhusu hali ya hewa ya leo, haijaonekana kuwa tatizo kwa wachezaji kwani wanaonekana kuimudu na muda mwingi kwa sasa kumekuwa na jua linalowaka kuanzia asubuhu wakati wa mazoezi mpaka mida ya jioni. Kwa leo hali ya hewa ni nyuzi joto 17 - 21, hivyoni nzuri na jua linawaka muda wote.

No comments:

Post a Comment