KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 20, 2013

BILIONI 32 KUJENGA UWANJA WA KAUNDA

KLABU ya Yanga inatarajia kutumia sh. bilioni 32 kwa ajili ya kujenga uwanja wake mpya na wa kisasa katika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji, aliwaambia wanachama wa klabu hiyo jana kuwa, ujenzi wa uwanja huo unatarajia kuanza Juni mwaka huu chini ya usimamizi wa kampumi ya Beijing Constructinon Engineering ya China.

Manji alisema uongozi wa Yanga unatarajia kufanya mazungumzo na Kampuni ya Unit Trust Fund Tanzania, ambayo ni wataalamu wa uchumi na kufanya mipango ya upatikanaji wa fedha za ujenzi wa uwanja huo.

Mwenyekiti huyo alisema, jukumu la kampuni hiyo litakuwa kutafuta benki au taasisi, ambayo itaikopesha Yanga fedha za kujenga uwanja huo na kuongeza kuwa, wanatarajia kufikia Mei mwaka huu, fedha hizo zitakuwa zimepatikana.

Alisema licha ya kutumia sh. bilioni 32 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja, pia wanatarajia kutumia dola za Marekani milioni 21 kwa ajili ya kugharamia vifaa vya ujenzi huo.

Manji alisema pia kuwa, uongozi unatarajia kuwaomba wanachama wao 210,000 kuchangia sh. 250 kwa wiki ili kwa mwaka zipatikane sh. bilioni nane kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa uwanja huo.

Alisema mbali ya wanachama kuchangia, wanatarajia kuendesha harambee ya kukusanya fedha za ujenzi wa uwanja huo, itakayofanyika baadae mwaka huu.

No comments:

Post a Comment