KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 23, 2011

VIINGILIO SIMBA NA MTIBWA

Mechi namba 50 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Mtibwa Sugar itachezwa Jumapili (Septemba 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa ifuatavyo; viti vya kijani na bluu sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 7,000, VIP B na C sh. 15,000 wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.

Mauzo ya tiketi yatafanyika siku ya mchezo kwenye magari mbalimbali yatakayokuwa yameegeshwa nje ya Uwanja wa Taifa.

Uwanja wa Taifa pia utakuwa mwenyeji wa mechi nyingine ya ligi hiyo kati ya Yanga na Coastal Union. Mechi hiyo itachezwa Jumatano (Septemba 28 mwaka huu).

MBWA WA POLISI CCM KIRUMBA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko tukio la mbwa wa polisi kukata kamba na kusababisha mtafaruku kwa wachezaji wakati wa mechi kati ya Toto Africans na Simba iliyochezwa Septemba 21 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba.

Tunafanya mawasiliano na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza ili kujua chanzo cha tukio hilo, na hatua ambazo jeshi hilo limechukua kwa mhusika iwapo itathibitika kuwa kitendo hicho kilisababishwa na uzembe. Pia tunaamini kuwa tukio hilo litakuwa ni fundisho kwa askari polisi ambao badala ya kufanya shughuli iliyowapeleka uwanjani ya kulinda usalama ugeuka kuwa watazamaji wa mpira.

MAPATO TOTO AFRICANS v SIMBA

Pambano namba 44 la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Toto Africans na Simba lililochezwa Septemba 21 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza limeingiza sh. 24,044,000. Viingilio katika mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3 vilikuwa sh. 2,000 kwa mzunguko na sh. 10,000 kwa jukwaa kuu.

LIGI DARAJA LA KWANZA

Timu saba kati ya 18 za Ligi Daraja la Kwanza bado hazijawasilisha usajili wao wakati ligi hiyo inatarajia kuanza mapema mwezi ujao. Timu hizo ni Temeke United, 94 KJ, Polisi Morogoro, Samaria FC, Rhino FC ya Tabora, Morani FC ya Manyara na AFC ya Arusha.

Ingawa timu kumi na moja zimewasilisha usajili wao, lakini ni sita tu ambazo zimelipa ada ya ushiriki ya sh. 200,000. Timu zilizolipa ni Polisi Iringa, Burkina Faso ya Morogoro, Mlale JKT ya Ruvuma, Morani FC ya Manyara, Mgambo Shooting, Samaria FC na Transit Camp. Timu nyingine za Daraja la Kwanza ni Polisi Dar es Salaam, Tanzania Prisons, Mbeya City Council, Polisi Tabora, Small Kids ya Rukwa na Majimaji.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

MBWA WA POLISI ALIYEINGIA UWANJANIHuyu ndiye mbwa wa polisi aliyemponyoka polisi na kuingia uwanjani wakati za soka za Simba na Toto African zilipokuwa zikimenyana katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. Timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3. Je, ni nani wa kulaumiwa?


Jeshi la Polisi mjini Mwanza limesema limeshamuhoji askari aliyekuwa na mbwa huyo na litamchukulia hatua kulingana na taratibu za kijeshi. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo limeomba maelezo kutoka Polisi kuhusu tukio hilo. Tusubiri tuone.

Thursday, September 22, 2011

Kanakamfumu aikosoa ligi kuuAdai kuna matatizo kibao ya kiuendeshaji

Awaponda baadhi ya maproo kutoka nje

Asema Polisi Dodoma haijamtimua

SWALI: Umepokeaje taarifa za kuondolewa kwako katika kazi ya ukocha wa timu ya Polisi Tanzania?
JIBU: Binafsi nilikuwa nina mkataba wa muda mfupi na viongozi wa Polisi na mkataba huo umeshamalizika na tayari nimerudi katika shughuli zangu za kawaida.
Kwa ujumla, nimeondoka pale bila matatizo yoyote na hivi sasa ninaendelea na kazi yangu ya kufundisha soka sehemu nyingine.
SWALI: Ni sababu gani iliyoufanya uongozi wa Polisi Dodoma kutangaza kuwa umekuondoa? Na je, umejifunza nini katika kipindi chote ulichokuwa ukiinoa Polisi?
JIBU: Kama nilivyoeleza awali, nimeondoka Polisi baada ya mkataba wangu wa muda mfupi kumalizika na sipendi kuzungumza zaidi juu ya jambo hilo.
Lakini kama wao wanadai wameniondoa baada ya kugundua mwenendo wa timu hiyo sio mzuri, sawa lakini hiyo ni juu yao.
Kuhusu vitu, ambavyo nimejifunza kwa kweli ni vingi, kuanzia ndani ya ligi kuu na kwenye klabu hiyo. Sio siri, hivi sasa timu nyingi za ligi kuu zimejiandaa vizuri na kuifanya iwe na ushindani mkali wa kusaka ubingwa.
Maandalizi yamefanywa vizuri na kila timu na usajili umekuwa wa makini sana. Baadhi ya timu zimeweza kuibua vipaji, ambavyo vimeanza kutisha katika ligi hiyo.
Binafsi niliweza kusajili baadhi ya wachezaji chipukizi, ambao wameonyesha uwezo mkubwa na hivi sasa ni wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza.
SWALI: Ni mapungufu yepi uliyoweza kuyabaini katika ligi hiyo?
JIBU: Mapungufu ni mengi na makubwa kwa vile zipo baadhi ya timu zinategemea zaidi udhamini wa Vodacom, ambao bado ni mdogo ikilinganishwa na hali halisi ya michuano hiyo.
Timu zinapewa sh. milioni karibu 26 kwa mwaka, lakini maandalizi ya ligi hiyo yanaweza kuigharimu timu zaidi ya sh. milioni 200.
Bado kuna mapungufu mengine yakiwemo vifaa vya kufanyia mazoezi, uwezeshaji kwa wachezaji na vifaa duni, ambavyo ukiangalia, wachezaji mara nyingi kabla ya kumalizika ligi, viatu vyao navyo vinakuwa vimekwisha, inabidi wanunue vingine.
Hiyo yote inatokana na kuwepo vifaa visivyo na kiwango na kusababisha baadhi ya wachezaji kushindwa kuonyesha uwezo wao kutokana na kuvaa viatu vibovu.
SWALI: Vipi kuhusu uwezo wa waamuzi wa ligi kuu?
JIBU: Baadhi yao wanazingatia vyema sheria 17 za soka, lakiniwengine wanashindwa na kusababisha matatizo, ikiwemo kutaka kupigwa na wengine kuzinufaisha baadhi ya timu, hasa zenye uwezo kifedha.
Lakini kwa ujumla, inabidi TFF iangalie mwenendo wa baadhi ya waamuzi kwa vile wanakiuka miiko ya kazi hiyo.
SWALI: Vipi kuhusu mchuano wa kusaka namba katika vikosi vya kwanza?
JIBU: Kwa kweli mchuano ni mkali sana na katika baadhi ya timu, makocha wana kazi kubwa kutokana na kusajili wachezaji wengi wazuri.
Napenda kuwapongeza wachezaji wengi, ambao wamekuwa wakijituma katika ligi hiyo ili waweze kupata nafasi ya kucheza kwenye vikosi vya kwanza.
Hili jambo ni zuri kwa vile litachangia kwa asilimia nyingi kupatikana kwa vipaji zaidi ili viweze kushindana na wageni. Kwa sasa makocha wana kazi kubwa ya kuhitaji muda kuangalia uwezo wa kila mchezaji ili kujenga timu ya kwanza tofauti na zamani.
Pia inabidi makocha wafanyekazi ya ziada kufuatilia mienendo ya wachezaji nje ya dimba ili kuhakikisha wanafuata miiko ya soka.Mchezaji akimaliza mazoezi, inabidi atulie na wala asijihusishe na starehe, ikiwemo ya ngono kwa vile inaua uwezo wa mchezaji.
SWALI: Unawazungumziaje wanasoka wa kulipwa kutoka nje waliopo nchini?
JIBU: Kwa kweli wana mchango mdogo sana katika soka ya Tanzania tofauti na ule wa wachezaji wazawa, ambao wamekuwa wakionyesha uwezo mkubwa kuliko wao.
Hii yote inatokana na viongozi wa kamati za usajili, kusajili wachezaji kwa kuangalia majina au umaarufu wa nchi wanazotoka wachezaji hao. Hili jambo kwa kweli linaua uwezo wa timu kwa vile wanasajili wachezaji wenye uwezo mdogo.
Ukiangalia kwenye ligi kuu msimu huu, wapo baadhi ya wachezaji wazuri kutoka nje kama vile Yaw Berko, Haruna Niyonzima, Jerry Santo na Patrick Mafisango, ambao wanaonyesha uwezo mkubwa.
Lakini wengine kwa kweli wana uwezo mdogo,ingawa napenda kueleza kwamba, mchango wa wachezaji wa nje ni mzuri kwa vile utaweza kuwashtua wachezaji wetu.
SWALI: Unazungumziaje kuhusu kuwepo mabadiliko ya viwanja kila kukicha kwa baadhi ya timu?
JIBU: Nilichogundua ni kwamba, kuna athari kubwa kwa vile timu nyingi zimekuwa zikilalamika kuingia gharama kubwa na wakati mwingine wachezaji kuchanganyikiwa.
Licha ya jambo hilo, baadhi ya wachezaji wanashindwa kuonyesha uwezo wao kutokana na kuhamishiwa katika viwanja vibovu.
Naliomba Shirikisho la Soka nchini (TFF), kubadili mfumo wa ligi kuchezwa katikati ya wiki kwa vile unawachosha sana wachezaji.
Angalia mchezaji mwishoni mwa wiki anacheza Dar es Salaam, na katikati ya wiki anatakiwa akacheze Bukoba katika mchezo mwingine.Ni vyema TFF ikalitazama jambo hilo kwa umakini mkubwa ili kupunguza athari na uwezo wa wachezaji.

Uzinduzi Chupa Nyeusi wafunika Burundi


UZINDUZI wa filamu mpya ya Chupa Nyeusi, uliofanyika mjini mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Bujumbura, nchini Burundi, ulifunika kutokana na kuhudhuriwa na watu kedekede.
Mbali na uzinduzi huo kuhudhuriwa na mashabiki lukuki, baadhi ya washiriki waliocheza filamu hiyo walikuwa kivutio cha aina yake kila walipokatika katika mitaa ya jiji hilo.
Baadhi ya mashabiki hao walikuwa wakigombea kupiga picha na wacheza filamu hao wa kitanzania kwa ajili ya ukumbusho wao na wengine kuzungumza nao.
Mtayarishaji wa filamu hiyo, Husna Poshi ‘Dotnata’ alisema wiki hii kuwa, hawakutarajia kupata mapokezi makubwa kiasi hicho, ambayo aliyalinganisha na yale wanayopewa viongozi wa kiserikali.
Alisema tangu walipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Bujumbura, msafara wao ulikuwa na msururu mkubwa wa magari na uliongozwa na mkuu wa Jeshi la Polisi, aliyemtaja kwa jina moja la Mohamed.
Dotnata alisema heshima waliyoipata kutoka kwa wananchi wa Burundi ni kubwa na imeonyesha wazi jinsi wasanii wa Tanzania wanavyothaminiwa na kupendwa wanapokuwa nje ya nchi yao.
“Kwa kweli tunajisikia faraja kubwa kutokana na mapokezi tuliyoyapata katika Jiji la Bujumbura. Wananchi walitupokea kwa shangwe, kila mtu alikuwa akitaka kupiga picha na sisi,”alisema.
Dotnata alitoa shukurani za pekee kwa Meya wa Jiji hilo, ambaye hamkumbuki kwa jina, ambaye alisema aliwakaribisha ofisini kwake na kuzungumza nao kwa dakika kadhaa kwa lengo la kubadilishana mawazo.
Baadhi ya wasanii waliocheza filamu hiyo, walioshiriki kwenye uzinduzi huo ni Irene Uwoya, Mohamed Posh, Hisani Muya ‘Tino’, Patcho Mwamba na muongozaji wao, Moses Mwanyilu.

Viongozi Yanga wasikwepe lawama timu kuvurunda


HALI imeendelea kuwa si shwari ndani ya klabu ya Yanga, kufuatia timu hiyo kuchapwa bao 1-0 na Azam katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kipigo hicho kilikuwa cha pili kwa Yanga katika mechi sita ilizocheza hadi sasa katika ligi hiyo. Kabla ya mechi ya jana dhidi ya Villa Squad, Yanga ilikuwa na pointi sita baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare mechi tatu.
Ushindi wa Yanga dhidi ya African Lyon wiki iliyopita, ulionekana kuleta ahueni kubwa kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, huku vyombo vya habari vikiipamba kwa vichwa mbalimbali vya habari vyenye mvuto, vikiwemo vile vilivyosema ‘Yanga yaanza ligi’ , ‘Timbe aanza kazi’ na ‘Yanga yaona mwezi’.
Lakini kipigo ilichokipata kutoka kwa Azam kimezusha mambo mengine mapya. Wapo wanaoendelea kuamini kuwa, hizo ni hujuma zinazoendelea kufanywa na baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo na wengine wameutupia lawama uongozi kwa kushindwa kujali maslahi ya wachezaji.
Pia wapo wanaowatuhumu baadhi ya viongozi wa zamani wa klabu hiyo kwamba, wamekuwa wakiwatumia wachezaji kuuhujumu uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti Lloyd Nchunga ili kuufanya uonekane haufai. Hizo zote ni tetesi.
Vilevile kuna habari kuwa, wachezaji wa Yanga wanaudai uongozi sh. milioni 30 walizopewa na mfadhili mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Yusuf Manji baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu na ule wa Kombe la Kagame. Pia kuna habari kuwa, wachezaji wa Yanga hawajalipwa mishahara yao kwa miezi kadhaa.
Sina hakika na madai hayo ya wachezaji kwa sababu hakuna kiongozi yeyote wa Yanga aliyewahi kukiri hadharani iwapo ni kweli hawajawalipa wachezaji pesa hizo, ambazo ni haki yao. Swali la msingi la kujiuliza ni je, ni kipi kilichoisibu Yanga na kuifanya ivurunde katika mechi hizo za mwanzo za ligi kuu?
Suala la kufungwa kwa Yanga katika mechi za ligi kuu si la ajabu. Timu hiyo kongwe imewahi kufungwa katika mechi kadhaa miaka ya nyuma kama ilivyo kwa watani wao wa jadi Simba, lakini hazikuwahi kutolewa tuhuma kama zinazotolewa sasa.
Kocha Mkuu wa Yanga, Sam Timbe alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari wiki hii akidai kuwa, kuvurunda kwa timu hiyo kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na udhaifu wa safu yake ya ushambuliaji.
Timbe alinukuliwa akisema kuwa, washambuliaji wa timu hiyo, wakiwemo maproo wanne, wamekuwa wakifika mara kwa mara kwenye eneo la hatari la timu pinzani, lakini wanashindwa kufunga mabao. Alidai huo ni upungufu katika kitu kinachoitwa uwezo binafsi wa mchezaji.
Lakini baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wamemtupia lawama kocha huyo kwa madai kuwa, amekuwa akipanga kikosi chake kwa upendeleo huku akiwapa kipaumbele zaidi baadhi ya wachezaji, hasa maproo, hata kama uwezo wao umeshuka.
Wachezaji hao walisema pia kuwa, kocha huyo amekuwa akiwanyima nafasi ya kucheza baadhi ya wachezaji, ambao wamekuwa wakionyesha uwezo wa juu mazoezini na kusababisha kuwepo kwa makundi mawili ndani ya timu hiyo. Kwamba wale, ambao hawajawahi kucheza hata mechi moja, wamekuwa wakiwachukia wale wanaochezeshwa mara kwa mara.
Inawezekana ni kweli kwamba wachezaji wa Yanga wanaudai uongozi fedha zao, lakini je, kucheza chini ya kiwango ndio suluhisho la kupatiwa fedha hizo? Je, timu itakaposhindwa kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ama kuteremka daraja, hasara itakuwa kwa nani?
Na ni kwa nini Kocha Timbe apange timu kwa kubagua wachezaji? Iweje kocha huyo ang’ang’anie kuwachezesha baadhi ya wachezaji hata kama uwezo wao ni mdogo?
Yapo maswali mengi ya kujiuliza, lakini majibu wanayo wenyewe wachezaji wa Yanga, uongozi pamoja na benchi la ufundi. Cha msingi ni pande hizo tatu kukutana na kujadiliana ili kujua tatizo ni nini ili waweze kulipatia ufumbuzi.
Kinachotokea hivi sasa kwa Yanga hakina tofauti na kile kinachotokea kwa klabu ya Arsenal katika michuano ya ligi kuu ya England msimu huu. Timu hiyo imevurunda katika mechi zake kadhaa, lakini lawama kubwa zimeelekezwa kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Arsene Wenger.
Pamoja na kuvurunda huko, Wenger ambaye amekuwa kocha wa Arsenal kwa miaka 15 sasa, amekaririwa akisema kuwa, hana wasiwasi wa kutimuliwa na kusisitiza kuwa, anaamini ataendelea kubaki klabu hiyo.
Lakini hali ni tofauti kwa Yanga. Kuna tetesi kuwa, kamati ya utendaji ya klabu hiyo huenda ikafikia uamuzi wa kumtimua kutokana na uwezo mdogo aliouonyesha katika kukisuka kikosi cha timu hiyo.
Iwapo ni kweli uongozi wa Yanga umefikia uamuzi huo, inaonekana umesahau kwamba, Timbe ndiye aliyeiwezesha timu kutwaa ubingwa wa ligi kuu dakika za mwisho msimu uliopita na pia kutwaa Kombe la Kagame.
Sasa iweje kocha aliyeiwezesha Yanga kutwaa mataji hayo, aonekane hafai msimu huu kutokana na timu kufanya vibaya katika mechi chache za mwanzo wa ligi? Ni wazi kwamba, lipo tatizo lingine kubwa na Timbe anabebeshwa msalaba usiomuhusu.
Ni vyema viongozi wa Yanga watafakari kwa makini nini kiini cha timu yao kuvurunda katika ligi na kuchukua hatua zinazostahili badala ya kuwabebesha lawama Timbe na wachezaji.
Kama ni kweli wachezaji wanaudai uongozi malipo yao, ni dhahiri kwamba, hilo linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kushusha ari yao uwanjani. Mchezaji atachezaje kwa moyo wakati hajalipwa madai yake? Na kwa nini uongozi umeshindwa kuwalipa madai yao, ambayo ni haki yao ya msingi? Tatizo lipo wapi?
Kama ni pesa, tayari Manji alishazikabidhi kwa uongozi. Na kama ni mishahara, inatoka moja kwa moja kwa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambayo pia inaidhamini Simba. Sasa tatizo ni nini?
Nawashauri viongozi wa Yanga wasikwepe lawama moja kwa moja. Lazima wawaeleze ukweli watanzania kuhusu sababu za timu yao kuvurunda badala ya kuwabebesha lawama kocha na wachezaji.

Wadau Z'bar walilia udhamini wa TBL

BAADHI ya wadau wa michezo wa Zanzibar wameiomba serikali iruhusu Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na ile ya Serengeti (SBL) kudhamini michezo visiwani humo.
Wadau hao walitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki iliyopita, kufuatia serikali kupokea msaada wa sh. milioni 20 kutoka TBL kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika kutokana na ajali ya meli ya MV Spice Islander.
Katika ajali hiyo iliyotokea wiki iliyopita eneo la Nungwi, watu zaidi ya 200 walipoteza maisha wakati wengine 600 waliokolewa. Meli hiyo ilikuwa ikitoka Unguja kwenda Pemba.
Wadau hao walisema, iwapo serikali imekubali kupokea msaada wa fedha kutoka TBL, hawaoni kwa nini iizuie kampuni hiyo na zinginezo zinazotengeneza pombe, kudhamini michezo visiwani humo.
“Kwanza tunaipongeza TBL kwa mchango wake huo kwa serikali. Lakini pili tunahoji kwa nini serikali yetu imekubali kupokea msaada huo, lakini inaizuia TBL kudhamini michezo,” alihoji mdau, aliyejitambulisha kwa jina la Issa Jecha.
Mdau huyo alisema, ameshangaa kusikia serikali imekataa kupokea msaada kutoka Vodacom kwa ajili ya kuwachangia wahanga wa ajali hiyo, lakini imepokea msaada huo kutoka TBL.
“Kwa kweli hapo serikali inatuchanganya. Imeikatalia Vodacom kwa sababu iliendesha mashindano ya Miss Tanzania mara tu baada ya ajali. Sasa iweje ipokee msaada wa TBL wakati haitaki matangazo ya pombe?” Alihoji Jecha.
Mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jacob Masanja alisema, ipo haja kwa serikali kutafakari kwa makini uamuzi wake wa kuzuia udhamini wa kampuni zinazotengeneza pombe katika michezo visiwani Zanzibar.
“Kama kweli serikali imedhamiria kwa dhati kukataa udhamini wa pombe katika michezo, basi isikubali kupokea misaada ya kampuni hizo katika miradi ya maendeleo na ile ya kuchangia matatizo,”alisema.
Alisema huu ni wakati mwafaka kwa serikali kuziruhusu TBL na SBL kudhamini michezo ili kusaidia kuinua viwango mbalimbali vya michezo visiwani humo.
Mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Samir Habibu alisema, bila udhamini, haitakuwa rahisi kwa Zanzibar kupata maendeleo katika michezo kwa sababu uendeshaji wake ni gharama kubwa.

BASATA yahimiza usajili wa kumbi na wasanii

ANGELO Luhala


BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wamiliki wa kumbi za burudani nchini kuzisajili ili ziweze kutambulika kisheria.
Baraza hilo pia limewataka wasanii na wadau wa sanaa nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kujisajili.
Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya BASATA, Angelo Luhala wakati wa Jukwaa la Sanaa lililofanyika kwenye ofisi za baraza hilo zilizopo Ilala Sharifu Shamba, Dar es Salaam.
Jukwaa hilo huandaliwa kila Jumatatu na BASATA kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz).
Luhala alisema, kwa mujibu wa sheria, suala la kujisajili kwa wasanii na wadau wa sanaa ni la lazima na si hiyari.
“Naanzia kusema hapa, kila anayefanya kazi yoyote ya sanaa ni wajibu ajisajili, kujihusisha na shughuli za sanaa. Bila kujisajili ni kuvunja sheria,kanuni na taratibu za nchi,” alisema.
Luhala alisema, kwa mujibu wa sheria ya nchi namba 23 ya mwaka 1984, BASATA imepewa mamlaka ya kusajili na kusimamia sekta ya sanaa nchini, hivyo mtu yeyote anayefanya shughuli za sanaa, anapaswa kusajiliwa na kupewa kibali cha kufanya shughuli hizo.
Aliongeza kuwa, sanaa ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, hivyo kila anayefanya kazi ya sanaa, anapaswa kutambuliwa na serikali na baraza kwa niaba ya serikali limepewa kazi hiyo.
Kwa mujibu wa Luhala, wadau wanaopaswa kujisajili BASATA ni pamoja na wasanii wa fani zote, wakuzaji sanaa (mapromota), vikundi vya wasanii, kumbi zote za burudani, wafanyabiashara wa sanaa, vyama na asasi mbalimbali za sanaa.
Akizungumzia faida za kujisajili, Luhala alisema ni pamoja na kufuata sheria na taratibu za nchi, kutambuliwa na serikali na pia kupata utambulisho wa baraza katika mahitaji mbalimbali. Alizitaja faida zingine kuwa ni kupata fursa za kushiriki maonyesho, taifa kuwa na takwimu sahihi za wadau wanaojihusisha na shughuli za sanaa na nyinginezo.
“Kuna watu wanajiuliza kwa nini wasajiliwe, lazima ieleweke kwamba, kila anayejihusisha na shughuli za sanaa, lazima atambuliwe na serikali. Hapa ndipo tunapata takwimu pia,” alisisitiza.
Wadau mbalimbali waliohudhuria programu hiyo, walionekana kuwa na shauku kubwa kwani mbali na suala la usajili, baraza lilitoa elimu kwa wasanii juu ya kulinda haki zao ikiwa ni pamoja na wasanii kutakiwa kujisajili kwenye chombo kinacholinda Hakimiliki na Shiriki cha Cosota.

REDONDO: Moto wa Azam hauzimikiKIUNGO Ramadhani Chombo ‘Redondo’ wa timu ya soka ya Azam, amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kwa kuwahakikishia ushindi katika mechi zijazo za ligi kuu ya Tanzania Bara.
Redondo alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, ushindi walioupata dhidi ya Yanga ni salamu tosha kwa timu zingine watakazocheza nazo katika ligi hiyo.
Azam iliichapa Yanga bao 1-0 katika mechi iliyochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na kuchupa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi sita, sawa na Mtibwa Sugar.
Azam ilitarajiwa kushuka tena dimbani jana kumenyana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Redondo aliieleza tovuti ya klabu hiyo kuwa, wamefanya maandalizi ya kutosha kupambana na timu yoyote watakayokutana nayo kwenye ligi hiyo.
“Timu ina hari nzuri na ari kubwa, kwa kuwa tumekuwa pamoja muda mrefu, tunahitaji ushindi kwa kila mechi tutakayocheza ili kufikia malengo yetu,” alisema.
Kiungo huyo wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars alisema, wanapigana kadri wawezavyo ili waweze kuchupa nafasi za juu zaidi katika msimamo wa ligi hiyo.
Nahodha msaidizi wa timu hiyo, Aggrey Morris alisema baada ya kutoka sare na Simba na kuichapa Yanga bao 1-0, hawaoni ni timu ipi inayoweza kuwazuia.
Amewataka wapenzi wa Azam wasiwe na wasiwasi kwa sababu wachezaji wote wapo makini, hivyo wajitokeze kwa wingi kwa sababu hawatawaangusha.

Mchezaji wa Coastal Union alazwa Bombo


MSHAMBULIAJI wa timu ya Coastal Union, Shafii Kaluani(pichani) amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Tanga ya Bombo kufuatia mguu wake wa kulia kuvunjika mara mbili.
Mshambuliaji huyo machachari alivunjika mguu wakati wa mchezo baina ya timu hiyo na Ruvu Shooting uliofanyika wiki mbili zilizopita kwenye uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani.
Mwandishi wa habari hizi alifika katika hospitali ya Bombo na kumkuta mchezaji huyo akiwa amelazwa kwenye wodi ya majeruhi ya Galanos akiuguza mguu wake.
“Nina maumivu makali sana hapa nilipo, sijui hatma yangu itakuwaje,”alisema mchezaji huyo, ambaye amefungwa plasta ngumu mguuni (POP).
Kocha Mkuu wa Coastal Union, Hafidh Badru alisema Kaluani alivunjwa mguu na beki mmoja wa Ruvu Shooting wakati walipokuwa wakigombea mpira.
Badru alisema wakati Kaluani alipokuwa akitolewa uwanjani, hawakuweza kutambua iwapo alivunjika mguu, lakini hali ilipozidi kuwa mbaya, ilibidi wamsafirishe haraka kumpeleka Bombo.
Alisema kuumia kwa mchezaji huyo kumeongeza pengo la wachezaji kwenye kikosi chake, ambapo idadi yao imefikia watatu wakati mchezaji mwingine mmoja anajiandaa kwa mitihani ya kidato cha nne.
Aliwataja majeruhi wengine kwenye kikosi chake kuwa ni Salum Juma na Benard Mwalala wakati Daniel Lianga amekwenda kwao Moshi kujiandaa kwa mitihani ya kidato cha nne.

UCHE JOMBO: Nitapambana hadi nipate haki ninayostahili


Aenda mahakamani kudai fidia dhidi ya gazeti lililomchafua

Asema si kweli kwamba alitoa mimba yenye umri wa miezi sita

Asema alipungua uzito sababu ya kucheza nafasi ya mgonjwa wa kansa
LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nollywood, Uche Jombo ameeleza kukerwa kwake na taarifa zilizoripotiwa hivi karibuni na baadhi ya vyombo vya habari nchini Nigeria kuwa, ametoa mimba yenye umri wa miezi sita.
Akizungumza kwa uchungu wiki iliyopita mjini hapa, Uche alisema habari hizo si tu kwamba zimemkera, bali zimemvunjia heshima na kumjengea taswira mbaya mbele ya jamii.
Uche alisema ni wazi mwandishi wa habari aliyeandika habari hizo, alidhamiria kumdhalilisha na kumpa machungu moyoni.
Alisema habari hizo zimesababisha apatwe na uchungu muda wote huku baadhi ya wakati akitokwa na machozi na aliapa lazima awashughulikie waliomchafua.
“Unafahamu jinsi nilivyoguswa na habari hizi. Nimewahi kulia kwa sababu ya masuala madogo, lakini kwa hili, nimekerwa na mtu huyu na itaendelea kuwa hivi kwa siku nyingi zijazo. Nitamuomba Mungu anikutanishe na mtu huyu na si kumdhuru,”alisema nyota huyo wa Nollywood.
Uche, ambaye hivi karibuni alifanya uzinduzi wa filamu yake mpya ya ‘Damage’ alisema, yupo tayari kupambana na watu waliomchafua hadi pale atakapohakikisha anapata haki anayostahili.
Alisema ameshafungua kesi mahakamani dhidi ya chombo kilichochapisha habari hizo pamoja na mwandishi aliyeziandika kwa sababu ni za uzushi na hazina ukweli wowote.
Uche alisema habari hizo, ambazo zilichapishwa ukurasa wa mbele wa chombo hizo, bado zinaendelea kumfanya asiwe na raha ndio sababu ameamua kutafuta haki yake mahakamani.
“Kwangu mimi, hii ilikuwa skendo kubwa kutokea. Iliniathiri hasa na siwezi kuacha kupambana hadi nitakapopata haki,”alisisitiza mcheza filamu huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto huku akitokwa na machozi.
Alisema habari zilizochapishwa na gazeti hilo ni mbaya kuliko zote katika maisha yake na uigizaji wa filamu na kusisitiza kuwa, zilikuwa za kuchukiza na hazikuwa na ukweli wowote.
Uche alisema wakati wa uzinduzi wa filamu yake ya pili ya Holding Hope mwaka jana, alipoteza uzito mwingi kutokana na nafasi aliyocheza ya mgonjwa wa kansa, lakini inashangaza kuona gazeti hilo likiripoti kwamba alitoa uja uzito wa miezi sita na ndio sababu mwili wake ulipungua.
“Habari hizi zimetapakaa kila sehemu duniani. Ukifungua tu mtandao wa Google na kuandika Uche atoa mimba, utaona zaidi ya kurasa 500. Habari hizo karibu ziyavuruge maisha yangu,”alisema.
“Ukweli ni kwamba ilikuwa karibu ziniue na kuchafua kila nilichokifanya katika maisha yangu ya kiusanii. Unaposema mtu fulani ametoa mimba ya miezi sita, husemi tu ametoa mimba, ni sawa na kusema mtu fulani ni muuaji kwa sababu mimba ya miezi sita tayari kiumbe kinakuwa kimekamilika,”aliongeza.
Mwanadada huyo alisema, haelewi kwa nini inafikiriwa kwamba, mwanamke anaweza kupungua uzito kwa sababu ya kutoa mimba.
Uche alizaliwa katika mji wa Enugu uliopo mashariki mwa Nigeria na kukulia katika mjini wa Aba, ambao upo kwenye jimbo la Abia. Ni mhitimu wa masomo ya hesabu na takwimu katika Chuo Kikuu cha Calabar na pia amehitimu masomo ya sayansi ya kompyuta katika chuo kikuu cha Minna kilichopo jimbo la Niger.
Alijitosa kwenye fani ya uigizaji filamu mwaka 1999 na tangu wakati huo amecheza zaidi ya filamu 60. Pia ni mwandishi mzuri wa miswada ya filamu na ameandika miswada ya filamu nyingi, zikiwemo The Celebrity, Games Men Play, Girls in the Hood, A Time to Love , Be my wife, Perfect Planner, Price of Fame na To Love Forever.
Filamu yake ya kwanza kuitengeneza yeye mwenyewe inajulikana kwa jina la Ibinabo. Filamu zingine alizozitengeneza ni pamoja na Nollywood Hustlers, Holding Hope na Damage.
Uche amewahi kushinda tuzo nyingi kutokana na umahiri wake katika kucheza filamu na pia mchango wake katika maendeleo ya fani hiyo nchini Nigeria.

Kipre Tchetche nje wiki mbili

MSHAMBULIAJI Kipre Tchetche wa Azam ametakiwa kupumzika kucheza soka kwa muda wa wiki mbili kufuatia kuumia mguu hivi karibuni.
Mratibu wa Azam, Nassor Idrisa alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Tchetche anasumbuliwa na maumivu ya misuli.
Nassor alisema tayari mchezaji huyo kutoka Ivory Coasta ameshafanyiwa uchunguzi wa tatizo hilo na kuanza kupatiwa matibabu.
Alisema kutocheza kwa mchezaji huyo katika mechi kati ya Azam na Yanga kulitokana na maumivu hayo na si vinginevyo.
Akizungumzia mwenendo wa ligi ulivyo hivi sasa, Nassor alikiri kuwa, ligi ya msimu huu ni ngumu kwa vile kila timu imepania kushinda.
Wakati huo huo, uongozi wa klabu ya Simba umesema, beki Amir Maftah anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina katika kifundo chake cha mguu.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Maftah aliumia mguu mwishoni mwa wiki iliyopita wakati timu hiyo ilipomenyana na Kagera Sugar mjini Bukoba.
Kaburu alisema tayari mchezaji huyo ameshaanza kupatiwa matibabu, lakini atafanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini ukubwa wa tatizo hilo.

Vodacom Mwanza Chalenji mwezi ujao

Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom, Rukia Mtingwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mbio za baiskeli za Vodacom Mwanza Chalenji uliofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Katikati ni Mwenyekiti wa Chama cha Baiskeli mkoa wa Shinyanga, Elisha Eliasi na kulia ni Katibu wa chama hicho, Lukas Bupilipili.


KAMPUNI ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania imetangaza kuandaa na kudhamini mashindano ya mbio za baiskeli ya Vodacom Mwanza Chalenji yanayotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom, Rukia Mtingwa aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa, mbio hizo zitakazogharimu sh. milioni 50, zitaanzia Shinyanga na kumalizikia Mwanza.
Rukia alisema mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na amewaomba waendesha baiskeli wa miji hiyo miwili kujitokeza kwa wingi. Alisema washindi katika kila kundi watapewa zawadi mbalimbali, ambazo zitatangazwa baadaye.
“Mashindano haya yameboreshwa kwa zawadi, ubora na viwango, tofauti na miaka ya nyuma. Mashindano ya mwaka huu yatahusisha mikoa miwili muhimu kwa mchezo wa baiskeli katika kanda ya ziwa, yani Shinyanga na Mwanza,”alisema.
Rukia alisema mashindano hayo yatafanyika Oktoba 22 mwaka huu na yatakuwa ya kilomita 196 kwa wanaume na kilometa 80 kwa wanawake. Alisema kwa upande wa walemavu, mbio hizo zitakuwa za kilometa 15 kwa wanaume na kilomita 10 kwa wanawake.
Kwa mujibu wa Rukia, mashindano hayo, ambayo yamekuwa yakiandaliwa na Vodacom kwa miaka mitano sasa, yamelenga kukuza mchezo huo ili Tanzania iweze kujulikana zaidi kimataifa.
Alisema kwa kuzingatia kuwa mwaka huu, Tanganyika inasherehekea kutimiza miaka 50 ya uhuru, Vodacom imepanga kutoa zawadi ya mshiriki mwenye umri wa kuanzia miaka 50, atakayemaliza wa kwanza katika kundi la washiriki 50 wa kwanza.
Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Baiskeli mkoa wa Shinyanga, Elisha Eliya alisema,ili kuleta mabadiliko na kuboresha zaidi mashindano hayo, mbioza mwaka huu zitaanzia mkoa wa Shinyanga na kumalizikia Mwanza.
Amewataka wanamichezo wote wanaoshiriki katika mashindano hayo, kuanza kujiandaa mapema ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa vyao wenyewe vya mchezo huo ili waweze kuwa katika hali nzuri ya kiushindani zaidi.

SIMBA CHUPUCHUPUSIMBA jana ilipunguzwa kasi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kulazimishwa kutoka sare ya mabao 3-3 na Toto African katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini hapa.
Sare hiyo ilikuwa ya pili mfululizo kwa Simba baada ya wiki iliyopita kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar katika mechi iliyochezwa mjini Bukoba.
Pamoja na kulazimishwa kutoka sare, Simba bado inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi saba wakati Toto African inaendelea kushika nafasi ya tano ikiwa na pointi tisa sawa na Yanga, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Simba ililianza pambano hilo kwa kasi na kubisha hodi kwenye lango la Toto African dakika ya saba wakati Emmanuel Okwi alipotanguliziwa mpira mrefu, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Maganga Seif.
Mshambuliaji Felix Sunzu aliifungia Simba bao la kuongoza dakika ya nane alipounganisha kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Juma Jabu kutoka pembeni ya uwanja.
Darlington Enyima aliisawazishia Toto African dakika ya 19 kwa njia ya penalti baada ya beki Obadia Mungusa wa Simba kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari wakati wa harakati za kuokoa.
Pambano hilo lililazimika kusimama kwa muda dakika ya 29 baada ya mbwa wa polisi kuingia katikati ya uwanja na kusababisha wachezaji Haruna Moshi na Sunzu kukimbilia kwenye benchi la Toto kwa lengo la kujiokoa.
Toto iliongeza bao la pili dakika ya 37 lililofungwa na Mohamed Sudi kwa shuti kali la mbali lililotinga moja kwa moja wavuni.
Dakika nane baadaye, Enyima nusura aiongezee Toto bao la pili baada ya kufumua shuti kali lililomshinda kipa Juma Kaseja na mpira kurudi uwanjani. Timu hizo zilikwenda mapumziko Toto ikiwa mbele kwa mabao 2-1.
Timu zote mbili zilikianza kipindi cha pili kwa kushambuliana kwa zamu, Simba wakicheza pasi ndefu huku Toto wakigongeana pasi fupi fupi.
Simba ilisawazisha dakika ya 59 kwa bao lililofungwa na Sunzu baada ya kuunganisha wavuni kwa shuti krosi kutoka kwa Okwi.
Dakika moja baadaye, Iddi Mobb aliiongezea Toto bao la tatu baada ya kudokolewa mpira na Sudi huku mabeki wa Simba wakizembea kumfuata kwa kudhani ameotea.
Patrick Mafisango aliisawazishia Simba dakika ya 65 kwa kiki kali iliyomshinda kipa Maganga wa Toto.
Toto ilipata pigo dakika ya 70 baada ya beki wake, Philemon Mwendasile kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Mafisango.
Katika pambano hilo, mashabiki wapatao 100, baadhi wakiwa na tiketi, walivunja geti kuu la kuingilia uwanjani kutokana na kukosa uvumilivu wa kupanga foleni.
SIMBA: Juma Kaseja, Nassoro Cholo, Juma Jabu, Obadia Mungusa, Victor Costa, Patrick Mafisango, Ulimboka Mwakingwe/Gervas Kago, Jerry Santo, Felix Sunzu, Haruna Moshi, Amri Kiemba na Emmanuel Okwi.
TOTO AFRICAN: Maganga Seif, John Bosco, Philemon Mwendasile, Laban Kambole, Ladslaus Mbogo, Lulanga Mapunda, Emmanuel Swita, Mohamed Sudi, Darlington Enyima/ Mwita Kemronge, Iddi Mobb na Fabian James.

YANGA RAHA TUPU

HARUNA Niyonzima

MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga jana walituliza mzuka wa mashabiki wa klabu hiyo, baada ya kuifunga Villa Squad mabao 3-2 katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Mashabiki wa Yanga waliofurika kwenye uwanja huo uliopo nje kidogo ya Dar es Salaam, walitoka uwanjani roho kwatu baada ya kushuhudia timu hiyo ikicheza soka ya kuvutia na kupata ushindi huo ulioifanya kufikisha pointi tisa katika mechi saba ilizocheza.
Yanga ilianza mchezo kwa kasi na mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Kenneth Asamoah, alikosa bao dakika ya 10 kabla ya Villa Squad kujibu shambulizi hilo dakika ya 11 na kufanikiwa kufunga bao kupitia kwa winga wa zamani wa timu hiyo, Nsa Job aliyepokea pasi ya Mohamed Kijuso.
Kuingia kwa bao hilo kuliamsha hasira za Yanga, ambayo ilijipanga vizuri na kusukuma mashambulizi langoni mwa Villa Squad. Juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 15 baada ya kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima kufunga kwa mkwaju wa adhabu ndogo.
Dakika ya 27, Yanga ilizidisha kasi ya mchezo na kupata bao la pili kupitia kwa Asamoah, aliyefunga baada ya kupata pasi ya winga, Idrissa Senga. Nurdin Bakari alikosa bao dakika ya 36 licha ya kubaki na kipa Mohamed Bambino kabla ya Asamoah kupiga shuti nje dakika ya 43.
Kipindi cha pili timu hizo zilishambuliana kwa zamu kabla ya Villa Squad kupata pigo dakika ya 57 baada ya mchezaji wake, Stamili Mbonde kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumtolea lugha mbaya mwamuzi Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga.
Yanga ilipata bao la tatu lililofungwa na Hamis Kiiza, aliyeingia kuchukua nafasi ya Shamte Ally dakika ya 63, akiunganisha mpira wa krosi ya Senga. Villa Squad ilipata bao la pili kupitia kwa Kigi Lusekelo dakika ya 72 kwa shuti kali.
Ushindi huo umeifanya Yanga kupoza machungu baada ya kufanya vibaya katika mechi za awali, ambapo ilianza ligi vibaya kwa kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu, ilitoka sare 1-1 na Moro United, ilitoka suluhu na Mtibwa Sugar, ilitoka sare 1-1 na Ruvu Shooting, ilishinda 2-1 dhidi ya African Lyon kabla ya kuchapwa 1-0 na Azam.
Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Chacha Marwa, Nurdin Bakari, Shamte Ally/Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima, David Mwape, Kenneth Asamoah/ Rashid Gumbo na Idrissa Senga.
Villa Squad: Mohamed Bambino, Haruna Shamte/Evarist Maganga, Yassin Juma, Shai Mpala, Mohamed Lupatu, Zuebr Dabi, Mussa Nampaka, Stamil Mbonde, Mohamed Kijuso, Nsa Job na Lameck Dayton/Kigi Lusekelo. 72
Kutoka Tanga, mwandishi Sophia Wakati, anaripoti kuwa timu ya Azam ilitoka uwanja wa Mkwakwani kifua mbele baada ya kuilaza Coastal Union bao 1-0 lililofungwa na John Bocco dakika ya 32 kwa mpira wa kichwa.

Friday, September 16, 2011

SEMINA YA COM-UNITY

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira Duniani (FIFA) wameandaa semina ya siku tatu itakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Oktoba 25-28, 2011 kwenye hoteli ya Peacock.

Semina hiyo inalenga kuwaleta pamoja wadau wote muhimu katika maendeleo ya mpira wa miguu kwa wanawake. Wadau wakuu ni Serikali, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, wadhamini na wanahabari.

Lengo kuu ni kutoa mwamko na kujenga uelewa zaidi wa mchango wa mpira wa miguu kwa wanawake katika jamii. Pia kutambua nafasi na umuhimu wa wadau mbalimbali katika maendeleo ya mpira wa miguu kwa wanawake na pia kujadili na kubaini mipango, mikakati na michango mbalimbali inayotolewa/inayoweza kutolewa na wadau hao katika kumwendeleza mtoto wa kike na ushiriki wake katika mpira wa miguu.

Semina hii inalenga kujenga stadi za mawasiliano na udhamini/masoko (marketing) ili kuliwezesha shirikisho kuzitumia na kuwavutia wadhamini na wadau wengi zaidi. Semina ya Com –Unity itatoa nafasi kwa Serikali, NGOs wadhamini na wanahabari kutoa mada mbalimbali kuhusiana na michango yao na nafasi zao katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wanawake.

Itahitimishwa kwa Tamasha la watoto wa kike watakaocheza katika mfumo wa wachezaji watano watano Oktoba 28 mwaka huu katika viwanja vya Karume kuanzia saa tatu asubuhi. Shule zifuatazo zitashiriki;

SOS·
Ilala Boma Shule ya Msingi ·
Kurasini mahitaji maalum ·
Uhuru Mchanganyiko/Uhuru Girls·
International School of Tanganyika·
Almuntazir Girls Primary School

Mchana tunatarajia kuwa na tamasha la wazazi/akina mama kutoka timu mbalimbali zitakazoshiriki. Timu hizo zitajumuisha timu ya wanakamati wa maandalizi ya Com –Unity, viongozi wa mpira wa wanawake na wanahabari toka vyombo vyetu vya habari.

FIFA itagharamia wawezeshaji, wawakilishi wake, ukumbi na vifaa vitakavyotumika na maandalizi ya Tamasha. TFF itagharamia usafiri wa ndani, gharama za ushuru na kodi na gharama nyingine.

Kamati za Maandalizi
Kutakuwa na kamati nne za maandalizi ya Semina na Tamasha. Kamati hizo ni za uratibu wa washiriki, uandaaji na uwasilishaji wa mada, udhamini na tamasha na kamati ya habari.
Wenyeviti wa kamati hizo wataunda kamati kuu.

Kamati ya Uratibu wa Washiriki
Amina Karuma– Mwenyekiti
Michael Bundala– Katibu
Rose Kisiwa – Mjumbe

Kamati ya Udhamini na Tamasha
Rukia Mtingwa- Mwenyekiti
Jimmy Kabwe- Katibu
Devota Komba-Ikandiro – Mjumbe
Irene Mwasanga – Mjumbe

Kamati ya Habari
Joyce Mhaville/Deo Rweyunga- Mwenyekiti
Boniface Wambura– Katibu
Zena Chande – Mjumbe
Somoe Ngitu - Mjumbe

Kamati ya Uratibu wa Uandaaji wa Mada
Sunday Kayuni- Mwenyekiti
Juliana Yassoda- Katibu
Devota John – Mjumbe
Joan Minja – Mjumbe

Kamati Kuu
Lina Mhando – Mwenyekiti
Devota John Marwa – Katibu
Amina Karuma – Mjumbe
Rukia Mtingwa – Mjumbe
Joyce Mhaville/Deo Rweyunga - Mjumbe
Sunday Kayuni – Mjumbe

Mshauri na Mwezeshaji wa FIFA: Henry Tandau
Tunaomba kutoa mwito kwa wadau wa mpira wa miguu wanawake watuunge mkono. Kamati ziko tayari kupokea ushauri, misaada ya hali na mali ili kufanikisha tamasha la watoto.

Lina Mhando
Mwenyekiti
Kamati ya Semina ya Com-Unity

Thursday, September 15, 2011

Yanga yaona mweziMABINGWA watetezi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga leo wamepata ushindi wao wa kwanza katika ligi hiyo baada ya kuifunga African Lyon mabao 2 – 1 katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Davis Mwape dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza na Rashid Gumbo dakika ya 66 ya kipindi cha pili.

Bao la kujifariji la Lyon lilifungwa na Shengo kwa mpira uliokufa (freekick) dakika ya 44 kipindi cha kwanza.

Kwa ushindi huo, mabingwa hao watetezi sasa wamefikisha pointi sita katika michezo mitano waliyocheza hadi sasa.

Ushindi huo umeleta ahueni kubwa kwa Yanga kwani iwapo ingepoteza mechi hiyo ama kutoka sare, huenda mgogoro uliopo sasa kati ya uongozi na wachezaji ungeongezeka zaidi.

Katika mechi za awali, Yanga ilipoteza mechi moja na kuambilia sare katika mechi tatu, hali iliyosababisha baadhi ya wachezaji watuhumiwe kwamba walicheza chini ya kiwango kutokana na uongozi kushindwa kuwalipa fedha wanazodai.

Nelly Kamwelu arejea nchini leoMWAKILISHI wa Tanzania katika shindano la Miss Universe 2011, Nelly Kamwelu amerejea nchini leo akitokea Sao Paolo, Brazil ambako mwishoni mwa wiki iliyopita alikuwa miongoni mwa washiriki 88 kutoka nchi mbalimbali duniani waliowania taji hilo. Hata hivyo, Nelly hakufanikiwa kuingia kwenye hatua ya warembo 16 bora, lakini alifanya vizuri katika vazi la kitaifa. Pichani, mrembo huyo akiwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam mara baada ya kurejea nchini leo.

Vodacom kudhamini semina ya TASWAMENEJA Uhusiano na Habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusiana na udhamini wa Vodacom kwa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo na Burudani Tanzania(TASWA) kwa ajili ya semina kwa wanachama wake. Katikati ni Katibu Mkuu wa Taswa, Amiri Mhando na kulia ni Katibu Mkuu Msaidizi, George John. (Na Mpiga Picha Wetu)


MAFUNZO kwa ajili ya waandishi wa habari za michezo nchini yaliyopangwa kufanyika mkoani Morogoro, Oktoba Mosi na pili mwaka huu, yatadhaminiwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Amir Mhando, alisema, maandalizi ya mafunzo hayo yanakwenda vizuri na wana matumaini yatakuwa na manufaa makubwa.
Mhando aliishukuru Vodacom Tanzania kwa kudhamini mafunzo hayo na kuongeza kuwa, ni hatua nzuri katika kutekeleza mikakati ya TASWA kuendesha mafunzo kwa wanachama wake na waandishi wa habari za michezo kwa ujumla chini ya kauli mbiu ya chama hicho isemayo: TASWA Mafunzo Zaidi.
Alisema mafunzo hayo yatahusisha washiriki 40 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani na kuongeza kuwa, mwanzoni mwa Novemba mwaka huu, wataendesha mafunzo kama hayo mkoani Arusha, yakihusisha washiriki kutoka Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyra na baadhi ya washiriki kutoka Dar es Salaan.
Mhando alisema mwishoni mwa Novemba mwaka huu, TASWA pia itaendesha mafunzo kwa wahariri wa habari za michezo, ambayo yatakuwa nje ya Dar es Salaam na kwamba mkoa husika utatangazwa baadaye.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa TASWA, mafunzo ya Morogoro na Arusha yatahusisha masuala ya maadili ya uandishi wa habari,, masuala ya sheria za mambo ya habari na sheria za michezo mbalimbali.
Alisema washiriki wataelimishwa namna ya kuripoti habari za michezo ya mpira wa wavu, kikapu na riadha na kwamba kama mambo yataenda vizuri, pia utaingizwa na mchezo wa ngumi.
Aliongeza kuwa, wakufunzi katika mafunzo hayo ni baadhi ya walimu wa mambo ya habari, wahariri wazoefu, wanasheria na pia wakufunzi wa michezo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu, alisema kampuni yake inajisikia fahari kubwa kudhamini mafunzo hayo na kwamba itaendelea kufanya hivyo kadri itakavyoweza na kwamba, mafunzo ya Morogoro yatagharimu kiasi cha sh. milioni saba.
“Vodacom Tanzania inajisikia fahari kwa kudhamini mafunzo haya kwani hii siyo mara ya kwanza kwa Vodacom kudhamini mafunzo ya aina hii, mwaka jana tuliendesha mafunzo ya wahariri wa habari za michezo. Mwaka huu tunadhamini mafunzo ya TASWA, yote haya tukiwa na lengo la kuboresha tasnia ya habari. Mafunzo ya Arusha pia tutadhamini, lakini bajeti yake itaangaliwa baadaye,” alisema Nkurlu.
Naye Katibu Msaidizi wa TASWA, George John alisema katika mkutano huo kuwa, chama chake kimeamua kuendesha mafunzo hayo kwa ajili ya kuwoangezea uelewa zaidi waandishi wa habari za michezo.
“Mafunzo yatasaidia sana kwani kwenye ripotingi yetu, mfano mchezo wa mpira wavu, huwa wengine wanauliza wameshinda kwa mabao mangapi? Wakati kule huwa ni mambo ya seti si mabao,” alisema John, ambaye pia ni Katibu Msaidizi wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA).

Kamati ya Tibaigana kukutana Sept 24

Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakutana tena Septemba 24 mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza mashauri matatu dhidi ya Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage na Ofisa Habari wa klabu ya Yanga, Louis Sendeu.
Awali kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alfred Tibaigana ilikuwa ikutane Agosti 29 mwaka huu kusikiliza malalamiko ya TFF dhidi ya viongozi hao, lakini kikao kiliahirishwa kutokana na Kamati kutotimiza akidi (column) kwa wajumbe wake.
Pia TFF imewasilisha kwa kamati hiyo shauri jipya dhidi ya Sendeu kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi aliyechezesha mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Sendeu alimshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao, na anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba na kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima haikuwa halali.

SIMBA, POLISI ZAINGIZA MIL 16/-

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Polisi Dodoma iliyochezwa Septemba 14 mwaka huu Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 16,839,000.
Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 2,257 ambapo kiingilio kilikuwa sh, 7,000 kwa mzunguko na sh. 20,000 kwa VIP.
Waliokata tiketi za sh. 20,000 walikuwa 80. Baada ya kuondoa gharama za mchezo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 2,568,661.02 kila timu ilipata sh. 3,546,671.90. Mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja (sh. 1,162,893.90), TFF (sh. 1,162,893.90), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 581,446.95), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 465,157.56) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 116,289.39).

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Tonto Dikeh azusha tafrani GhanaLAGOS, Nigeria
BAADHI ya waongozaji filamu wa Ghana wamemtaka mcheza sinema wa Kinigeria, Tonto Dikeh amwombe radhi Van Vicker, vinginevyo asahau kucheza filamu za nchi hiyo.
Kwa mujibu wa blogu moja ya mastaa wa Ghana, Van Vicker ni mmoja wa watu wanaoheshimika katika tasnia ya filamu nchini humo hivyo hawako tayari kuona akidhalilishwa kwa namna yoyote ile.
Uamuzi huo wa waongoza filamu hao umekuja baada ya kuwepo na taarifa kuwa, Tonto na Van Vicker, ambao wana uhusiano wa kimapenzi, walipigana wakiwa kwenye eneo la kutengeneza filamu.
“Hivi anaweza kumdhalilisha RMD kama vile,” alihoji mmoja wa waongoza filamu hao, ambao hakutaka jina lake litajwe.
Wameonya kuwa, watamfungia mwongoza filamu yeyote, ambaye atamshirikisha Tonto katika filamu yake. Pia wamesema wataandika barua ya malalamiko kwa Chama cha Waigizaji Filamu cha Nigeria.
Hadi sasa, Tonto hajasema lolote kuhusu onyo hilo na iwapo atakuwa tayari kumuomba radhi Van Vicker.
Mzozo kati ya Tonto na Van Vicker ulianza wakati wa mazoezi ya upigaji wa picha za filamu yao mpya, ambapo kila mmoja alikuwa akifanya mazoezi kivyake.
Baada ya muongozaji wa filamu hiyo kugundua kasoro hiyo, aliamua kuwafuata kwa lengo la kuwaweka sawa, lakini Tonto alionekana kupandwa na hasira na kuanza kusema hovyo.
Hali ilikuwa mbaya baada ya Tonto kuwasha sigara na kumpulizia moshi Van Vicker, ambaye kwa sauti ya upole, alimwomba aache kufanya hivyo ama aende kuvutia nje.
Tonto aliichukulia kauli hiyo ya Van Vicker kama kumtusi na kuanza kumtukana matusi ya nguoni. Ilibidi watayarishaji wa filamu hiyo waingilie kati kuwasuluhisha.

Vidume wamuibukia Funke Akindele


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Funke Akindele amezua tafrani kubwa baada ya wanaume zaidi ya 119 kutoka ndani na nje ya nchi hiyo kujitokeza kutaka kumuoa.
Kujitokeza kwa vidume hao, kumekuja baada ya mwanadada huyo kuripotiwa hivi karibuni na mtandao mmoja akisema kuwa, anahitaji mwanaume bora wa kumuoa.
Tangu taarifa hizo ziliporipotiwa na mtandao huo, vidume wengi wamekuwa wakiandika ujumbe kwa njia ya barua pepe, sms na hata kupiga simu wakieleza kuwa wapo tayari kumuoa mwanadada huyo.
Baadhi ya vidume hao wamemweleza Funke kuwa, wapo tayari kufunga naye ndoa na wengine wamejipa ujiko zaidi kwa mweleza ndio chaguo lake alilopangiwa na Jalali.
Vidume hao wanatoka katika majimbo mbalimbali ya Nigeria na wengine walithubutu kufika hadi kwenye makao makuu ya mtandao uliochapisha habari za mwanadada huyo ili kupata uthibitisho.
Mtandao huo hivi karibuni ulichapisha meseji za sms kutoka kwa vidume wote waliojitokeza kutaka kumuoa mwigizaji huyo, huku meseji nyingi zaidi zikiendelea kumiminika.

Clarion aweka kando uigizaji filamuLAGOS, Nigeria
BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mcheza filamu nyota wa Nollywood, Clarion Chukwurah amesema ameamua kujiweka kando na fani hiyo ili apate muda wa kutosha wa kushughulikia taasisi yake binafsi.
Clarion alisema wiki hii kuwa, amekuwa akipata ofa nyingi za kucheza filamu mpya kwa malipo makubwa, lakini kwa sasa ameamua kutumia muda wake mwingi kushughulikia taasisi hiyo, inayojulikana kwa jina la Clarion Initiative.
Mwanamama huyo mwenye mtoto mmoja, wiki iliyopita alisherehekea kutimiza miaka 32 tangu alipojitosa kwenye fani hiyo na kujizolea sifa lukuki.
Kwa mujibu wa Clarion, taasisi yake hiyo inajihusisha na masuala ya kutoa elimu ya uongozi kwa vijana waliopo kwenye shule za sekondari nchini Nigeria kuhusu mambo mbalimbali.
“Tunataka kuwaandaa vijana ili waweze kujiajiri baada ya kumaliza masomo yao badala ya kusubiri ajira za serikali,” alisema na kuongeza kuwa, taasisi hiyo inafanyakazi kwa karibu na USAID, British Council na Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa.
Clarion alisema taasisi yake hiyo ilianza kufanyakazi tangu mwaka 1999 na inajulikana katika nchi za Cameroon, Uingereza, Canada na zinginezo duniani.
Hata hivyo, Clarion hakuwa tayari kuzungumza lolote kuhusu mumewe, ambaye wametengana. Alisema masuala yafamilia yake yanawahusu wao binafsi.
Mcheza filamu huyo alisema ni vigumu kuwalinganisha waigizaji wa Nigeria na nchi kama Marekani kimalipo kwa sababu hata bajeti za kuandaa filamu katika nchi hizo zinatofautiana.
Alisema hafikirii kwenda kuishi nje ya Nigeria kwa sababu moja ya malengo yake ni kujiendeleza zaidi kimaisha na pia kuvisaidia vizazi vijavyo katika mambo mbalimbali.

Oge: Sina matatizo na mume wangu


LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI machachari wa Nigeria, Oge Okoye amekanusha madai kuwa, ndoa yake na mumewe imevunjika ama ipo hatarini kuvunjika.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari wiki hii, Oge amesema madai hayo si ya kweli na yamelenga kuchafua jina lake.
Oge amesema amechoka kupokea simu na meseji nyingi kutoka kwa ndugu, jamaa na rafiki zake wakimuuliza iwapo taarifa hizo zilizotolewa na vyombo vya habari ni za kweli.
“Mimi na mume wangu wiki chache zilizopita tulisherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wetu wa mwisho, hivyo sielewi kwa nini watu wanaeneza tuhuma ambazo hazipo,”alisema.
“Najisikia vibaya ninaposoma taarifa hizi na inaonekana kama vile yupo Oge Okeye mwingine. Mimi nipo salama na hakuna chochote kilichotokea baina yangu na mume wangu,”aliongeza.
Oge alisema ndoa yake haijawahi kukumbwa na matatizo yoyote na kusisitiza kuwa, mumewe na wifi zake wanafurahia maisha yao na kumuonyesha upendo mkubwa.
Amewataka waandishi wa habari na wanaoeneza uvumi huo kwenda kutafuta kazi zingine za kufanya ili wawe bize kwa sababu yeye na mumewe hawana muda wa kupoteza kusoma taarifa zao.
Katika hatua nyingine, Oge amesema anatarajia kuigiza filamu mpya hivi karibuni, ambayo picha zake zitapigwa nchini Canada. Pia alisema amepata nafasi ya kucheza filamu na waigizaji kadhaa nyota kutoka Hollywood.

Msondo, Sikinde zapigana madongo


BENDI kongwe za muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma na Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ wiki hii zimeibuka na vibao vipya vyenye mwelekeo wa kupigana madongo.
Wakati Msondo Ngoma imeibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Lakuvunda halina ubani’, Sikinde wameipua kibao kinachojulikana kwa jina la ‘Bundi’.
Kibao cha Lakuvunda halina ubani kimetungwa na mwimbaji machachari wa bendi hiyo, Shabani Dede wakati kibao cha Bundi kimetungwa na Abdalla Hemba.
Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Katibu wa Sikinde, Hamisi Milambo alisema kibao cha Bundi ni miongoni mwa vibao sita vitakavyokuwemo kwenye albamu mpya ya bendi hiyo.
Milambo alisema wapo katika maandalizi ya mwisho ya kurekodi kibao hicho baada ya kibao chao kilichopita cha ‘Jinamizi la talaka’ kupata mafanikio makubwa.
Kibao cha Jinamizi la talaka, kilichotungwa kwa ushirikiano wa wanamuziki wote wa Sikinde, kilirekodiwa mwezi mmoja uliopita na hivi sasa kimekuwa kikipigwa mara kwa mara kwenye vituo mbalimbali vya radio nchini.
Kufuatia kutamba kwa kibao hicho, Milambo alisema hivi sasa wapo katika hatua za mwisho za kurekodi video ya wimbo huo kwa lengo la kuwapa uhondo zaidi mashabiki. Alivitaja vibao vingine vitakavyokuwemo kwenye albamu yao mpya, watunzi wakiwa kwenye mabano kuwa ni ‘Nitalipa deni’ (wanamuziki wote), ‘Kilio cha kazi’ (Hassan Bitchuka), ‘Nisamehe’ (Hemba) na ‘Asali na shubiri’ (Shukuru Majaliwa).
Milambo alisema albamu yao mpya, itakayokuwa na vibao sita, inatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu kabla ya kuanza kuuzwa kwa mashabiki.
Wakati huo huo, mwimbaji mpya wa Msondo Ngoma, Dede amesema kibao chake kipya cha Lakuvunda halina ubani kimeshakamilika na kuanza kupigwa kwenye maonyesho ya bendi hiyo.
Dede alisema kibao hicho ni cha pili kwake tangu alipojiunga na bendi hiyo miezi minne iliyopita. Kibao chake cha kwanza kinajulikana kwa jina la ‘Suluhu’.
Mwimbaji huyo wa zamani wa Sikinde ametamba kuwa, kibao hicho kipya kitawadhihirishia mashabiki kwamba hana mpinzani katika utunzi na uimbaji wa nyimbo mwanana.
Dede alisema vibao alivyovitunga akiwa Msondo Ngoma havina lengo la kuwasema wanamuziki wa Sikinde kwa vile hana ugomvi nao, bali amevitunga kutokana na hisia zake.
“Sina ubaya wowote na wanamuziki wa Sikinde kwa sababu kuondoka kwangu kule kulilenga kuongeza changamoto na ushindani wa kimuziki.

Kuziruhusu Simba na Yanga kucheza Chamazi ni kuhatarisha usalama

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) iliyopita lilitangaza kuziruhusu timu za Simba na Yanga kuutumia uwanja wa Chamazi, unaomilikiwa na klabu ya Azam kwa ajili ya baadhi ya mechi zao za ligi.
Uamuzi huo wa TFF umetokana na agizo la serikali kutaka uwanja mpya wa Taifa uliopo Dar es Salaam kutumika kwa mechi mbili tu za ligi kwa wiki.
Serikali ililazimika kutoa agizo hilo ili kuepuka uwanja huo kuharibika iwapo utachezewa mechi nyingi za ligi kama ilivyokuwa wakati wa michuano ya Kombe la Kagame, iliyofanyika nchini mapema mwaka huu.
Awali, Simba na Yanga zililazimika kuhamishia mechi zake kwenye viwanja vya Jamhuri mjini Morogoro na Mkwakwani mjini Tanga baada ya serikali kuufunga uwanja wa Taifa usitumike kwa mechi za ligi.
Lakini baada ya maombi ya TFF, serikali imekubali uwanja huo uendelee kutumika, lakini kwa masharti ya mechi mbili kwa wiki. Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyozifanya Simba na Yanga ziombe kucheza Chamazi kwa ajili ya mechi zingine.
Kwa mujibu wa ratiba, Simba ilianza kuutumia uwanja huo jana kwa mechi kati yake na Polisi Dodoma wakati Yanga itaanza kuutumia leo kwa mechi kati yake na African Lyon.
Uamuzi wa TFF kuziruhusu Simba na Yanga zicheze Chamazi ni wa kushangaza kidogo. Hii ni kutokana na mazingira halisi ya uwanja huo pamoja na wingi wa mashabiki wa klabu hizo.
Kwa mujibu wa taarifa za TFF, uwanja wa Chamazi una uwezo wa kuchukua mashabiki 5000 na kwamba tiketi zitakazouzwa kwa mashabiki, hazitazidi idadi hiyo.
Lakini shirikisho hilo limesahau kuwa, halina uwezo wa kuwadhibiti mashabiki kuingia kwenye uwanja huo kuziona Simba na Yanga. Kazi hiyo itakuwa ngumu na inahitaji nguvu ya ziada ya Jeshi la Polisi.
Licha ya uwanja huo kuwa na maeneo machache ya kukaa mashabiki, hakuna uzio wa kuwazuia kuingia uwanjani. Hali hiyo inaweza kusababisha maisha ya waamuzi, viongozi na wachezaji kuwa hatarini.
Kwa mfano, katika kipindi hiki ambacho viongozi wa Yanga wamekuwa wakiwatuhumu wachezaji wao kucheza chini ya kiwango, inaweza kuwa hatari kwao kwa sababu mashabiki watakuwa na uwezo wa kuingia uwanjani na kuwashughulikia kwa sababu ya hisia hizo.
Vivyo hivyo kwa waamuzi watakaochezesha mechi za timu hizo mbili kongwe, ambapo tayari Yanga imeanza kuwatuhumu vibaya baadhi yao kwa madai kuwa, hawaitendei haki timu yao na kwamba wanachezesha kwa lengo la ‘kuinyonga’.
Kwa kuzingatia ukweli huo, nadhani TFF imefanya kosa kubwa kukubali Simba na Yanga zicheze uwanja huo. Na huenda imefanya hivyo kwa lengo la kuzifurahisha klabu hizo mbili, lakini madhara yake yanaweza kuwa makubwa.
Kama viwanja vingi vilivyopo sasa hapa nchini si salama kwa wachezaji, viongozi na mashabiki, sidhani kama uwanja wa Chamazi unaweza kuzifaa Simba na Yanga katika ligi. Ipo hatari ya mashabiki kushuhudia matukio ya ajabu ajabu, ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wao.
Lakini kikubwa zaidi ni kwamba, hii ni aibu na fedheha kwa Simba na Yanga, zilizoanzishwa miaka zaidi ya 70 iliyopita kutangatanga bila kuwa na viwanja vyao vya soka. Je, viongozi waliowahi kuziongoza klabu hizo, wataacha kumbukumbu gani kwa vizazi vijavyo? Na je, watakumbukwa kwa mambo gani waliyotenda kwa klabu hizo?
Klabu ya Yanga iliwahi kutangaza kuwa, itaufanyia ukarabati mkubwa uwanja wake wa Jangwani, ikiwa ni pamoja na kuuwekea nyasi za bandia na kujenga majukwaa ili utumike kwa mechi za ligi, lakini hadi sasa hakuna lolote la maana lililofanyika.
Alichoweza kukifanya mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji ni kufanya ukarabati mkubwa kwenye jengo la makao makuu, ambapo kwa sasa linatumika kama ofisi za viongozi na hosteli kwa wachezaji. Kwa hilo, Manji anastahili pongezi.
Kwa upande wa Simba, uongozi wake uliopo sasa madarakani umeahidi kujenga uwanja mpya wa kisasa maeneo ya Bunju, Dar es Salaam, ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000. Ni vigumu kuamini iwapo ahadi hii itatekelezwa ama itakuwa ni blabla za viongozi wanapoingia madarakani. Tusubiri tuone.

Kristine (Ella) ameolewa mara mbili

Christine Hermosa

JerichoWengi wanaulizia kuhusiana na Miguel na Ella kuwa wapenzi na kuwa na mtoto kutokana na taarifa za ndani kutoka nchini kwao Ufilipino kwamba wawili hao waliwahi kuwa wapenzi miaka ya nyuma hasa baada ya kuigiza tamthilia iliyowapa umaarufu mkubwa.


Licha ya simu nyingi kuulizia kuhusiana na mambo mbalimbali juu ya tamthilia hii, lakini wengi wanarudia kuuliza mara kwa mara swali kuhusiana na Jericho kama yu hai ama ameshafariki.


Tarifa za kuhusiana na kifo chake, ambazo zilivumishwa kuanzia mwaka 2000, lakini picha zake zinaendelea kuonekana na bendi yake ya muziki inapiga huku yeye akiimba na kuburudisha wapenzi wake katika kumbi mbalimbali hivyo jibu unalo.


Licha ya swali hilo, pia kuna swali lingine watu wakitaka kujua kuhusiana na mahusiano yake na Kristine Hermosa (Ella). Ukweli ni kwamba mwaka 2010, mwenyewe kwa mdomo wake alitamka kuwa na mpango wa kumuoa aliyekuwa mtangazaji wa Televisioni ya CNN, anayeitwa Cesca Litton huku akidai kufika hapo kwa kuwa kuna tofauti kubwa na alikowahi kupita.


Alisema kuwa wakati alipokuwa katika uhusiano na wapenzi anaodaiwa alikuwa nao kimapenzi, ambao ni Kristine Hermosa (Ella), Heart Evangelista, Gabby Conception, Lorna Tolentino na Mmalasia, Carmen Soo alijikuta akikumbwa na mambo mengi ya hapa na pale kutokana na umaarufu wa wasichana hao, lakini tangu afike kwa Cesca, amekuwa akijisikia huru zaidi na kufurahia mapenzi yake.


"Huku sifichi kitu, najisikia huru kueleza uhusiano wangu na Litton tofauti na nilipotoka kwani kulikuwa na mambo mengi yaliyokuwa yakiibuka kila siku, hivyo huku kuna tofauti kubwa na nilikotoka,'' alinukuliwa hivyo.


Jericho amezaliwa Septemba 22, 1970 katika mji wa Quezon na kuanza kazi ya uigizaji mwaka 1996, ambapo alichukuliwa kuwa mwanaume mwenye mvuto katika sanaa hiyo na kuanzia hapo alizidi kujizolea tuzo mbalimbali kwa kila tamthilia aliyokuwa akicheza.


Sasa licha ya kuigiza ni mmiliki wa bendi ya muziki aliyoipa jina la 'The Hunks', ambayo anashirikiana na wasanii Carlos Agassi, Piolo Pakual na wengineo.


Kwa upande wa Kristine Hermosa, ambaye ameigiza kama Angela (Ella) Alferos katika tamthilia hii, alizaliwa Septemba 9,1983 huko Quezon City, ambapo mji na mwenzi wa kuzaliwa unafanana na wa Jericho.


Kristine alipata bahati ya kuingia katika uigizaji baada ya mtayarishaji wa tamthilia kutoka kampuni ya picha za Televisioni ya ABS-CBN kuvutiwa naye na kumwacha dada wa Kristine, Kathleen ambaye sura yake haikumvutia mtayarishaji huyo.


Mwigizaji huyo amechanganyika kwani baba yake ni raia wa Ufilipino wakati mama yake ni raia wa Hispania. Kristine aliwahi kuolewa na Diether Ocampo na kuachana kwa madai ya wivu kwa Jericho.


Baada ya kuachana na Ocampo, Januari 12, 2011, Kristine aliolewa tena kwa ndoa na Oyo Sotto, ndoa ambayo ilisherehekewa majira ya saa tano usiku katika ukumbi wa Umbu Balai Isabel katika mji wa Talisay Batangas na sherehe hizo zilihudhuriwa na wageni 150 tu walioalikwa.


Licha ya hayo, ndoa hiyo pia iliripotiwa na kituo cha televisioni cha nchini Filipino cha SNN, ambapo sherehe za harusi hiyo zilitajwa kufadhiliwa na Rais wa Kampuni ya ABS-CBN, prodyuza pamoja na mtaalamu wa ufundi wa kampuni hiyo, ambapo dada wa Kristine, Katheleen na dada wa Oyo walikuwa wasimamizi wakuu wa harusi hiyo.

Wachezaji Yanga kuwekwa kiti moto


UONGOZI wa klabu ya Yanga umepanga kuwaweka kiti moto wachezaji kwa kuwahoji mmoja mmoja ili kubaini sababu za timu hiyo kufanya vibaya katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Habari kutoka ndani ya Yanga zilieleza juzi kuwa, kikao hicho kilipangwa kufanyika jana makao makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuwahoji wachezaji hao ulifikiwa baada ya kikao kizito kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kati ya uongozi na benchi la ufundi la timu hiyo.
Awali, uongozi wa Yanga uliwahoji makocha wa timu hiyo kuhusu sababu za kuboronga kwa timu hiyo na jana ulipanga kuwahoji wachezaji.
Mmoja wa viongozi wa Yanga, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alidokeza kuwa, wamefikia uamuzi huo ili kuhakikisha kuwa, wanapata ushahidi wa kutosha kabla ya kuwachukulia hatua wahusika.
Kiongozi huyo alisema wana hakika baada ya kumaliza kuwahoji wachezaji, watapata kiini cha tatizo hilo na hivyo kuamua hatua za kuchukua.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kikao hicho pia kitawahusisha wazee wa klabu hiyo kwa lengo la kupata busara zao kabla ya kuwachukulia hatua watu watakaobainika kuihujumu Yanga.
“Hatuwezi kuwachukulia hatua makocha au wachezaji kabla ya kuwahoji wahusika. Tunachotaka ni kujiridhisha kwa kupata ushahidi wa kutosha,”alisema.
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alithibitisha jana kufanyika kwa uchunguzi huo, ikiwa ni pamoja na kuwahoji wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi.
Katika hatua nyingine, Nchunga alisema jana kuwa, kamati ya utendaji ya Yanga inatarajiwa kukutana hivi karibuni kuwajadili wanachama waliofungua kesi mahakamani kuupinga uongozi uliopo madarakani.
Nchunga alisema tayari wameshapokea maelekezo kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya wanachama hao.
"Hatuwezi kuwaacha waendelee kutuharibia klabu yetu, tutakutana na viongozi wa matawi ili kuwajadili vinara wa wanachama hao na kutoa uamuzi mbele ya wanachama,”alisema.

Simba kama Man UnitedSIMBA jana iliendelea kung’ara katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Polisi Dodoma bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yaliiwezesha Simba kuendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi tano, ikifuatiwa na JKT Ruvu yenye pointi tisa.
Mshambuliaji Gervas Kago ndiye aliyeiwezesha Simba kutoka uwanjani na pointi zote tatu baada ya kuifungia bao hilo la pekee na la ushindi dakika ya tatu.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi ya kifua kutoka kwa Felix Sunzu. Lilikuwa bao la kwanza kwa Sunzu tangu ligi hiyo ilipoanza mwezi uliopita.
Ushindi wa Simba unafanana na ule wa Manchester United ya England, ambayo haijapoteza mechi hata moja tangu ligi kuu ya nchi hiyo ilipoanza. Hadi sasa, Simba imeshinda mechi tano na kutoka sare moja.
Simba ilianza ligi kwa ushindi wa mabao 2-0 ilipovaana na JKT Oljoro, ilishinda bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, iliilaza Villa Squad bao 1-0 kabla ya kutoka suluhu na Azam.
Timu hizo zilianza mchezo huo kwa kasi na Simba ilionekana kupania zaidi kufunga mabao ya mapema baada ya washambuliaji wake Ulimbokwa Mwakingwe, Kago na Okwi kuitoka mara kadhaa ngome ya wapinzani wao, lakini mashuti yao yalitoka nje na mengine kuokolewa.
Mwakingwe nusura afunge bao dakika 20 baada ya kufumua shuti kali lililotoka pembeni kidogo mwa lango kabla ya kiungo Patrick Mafisango kupiga mkwaju mkali uliwababatiza mabeki wa Polisi Dodoma na baadaye kuokolewa.
Dakika 34, Polisi Dodoma walifanya shambulizi langoni mwa Simba baada ya winga Bantu Admini kupata pasi ya Ibrahim Masawe, lakini kipa Juma Kaseja aliokoa. Mafisango aliyecheza vyema nafasi ya kiungo, aliitoka ngome ya Polisi Dodoma dakika 37 na kufumua shuti lilitoka nje ya lango.
Hamadi Kambangwa alifanikiwa kumtoka beki Juma Nyoso wa Simba na kutoa pasi nzuri kwa Admini dakika ya 56, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango kabla ya Kago kupiga mkwaju uliotoka nje kidogo ya lango la Polisi dakika mbili baadaye.
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Cholo/Selemani Kapombe, Juma Jabu, Juma Nyoso, Victor Costa, Patrick Mafisango, Ulimboka Mwakingwe/Uhuru Selemani, Jerry Santo, Felix Sunzu, Gervas Kago, Emmanuel Okwi.
Polisi: Agathon Mkwandiko, Salmin Kisikisi, Nassoro Mhagama, Frank Sindato, Elias Maftah, Ibrahim Masawe, Brighton Mponzi, Haruna Hassan, Kulwa Mfaume, Hamad Kambangwa, Bantu Admini.

Tuesday, September 13, 2011

MISS ANGOLA WINS MISS UNIVERSE 2011

A contestant from Africa- representing Angola has emerged the winner at the 60th edition of the world biggest beauty pageant, Miss Universe that was held in Sao Paulo, Brazil yesterday Sept 12 .


Leila Lopes beat 88 other contestants to win the title.


Ukraine's Olesia Stefanko became first runner-up of Ukraine while the second runner-up was Priscila Machado from Brazil. The third and fourth were Miss Philippines and Miss China respectively.


Leila of Cape Verdean descent is a student in Great Britain. She was crowned Miss Angola after representing the Angolan community in Great Britain at the pageant.


Leila is the fourth African to be crowned Miss Universe in the pageant's history. Miss South Africa (1978), Miss Namibia (1992), Bostwana (1999) and now Miss Angola (2011).


The 22 year old Tanzanian contestant, Nelly Kamwelu didn't make the cut into the top 16.

TIKETI MECHI ZA SIMBA NA YANGA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Septemba 13, 2011


TIKETI MECHI ZA SIMBA, YANGA CHAMAZI
Tiketi kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zinazohusisha timu za Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam hazitauzwa uwanjani. Lengo ni kuwaondolea usumbufu mashabiki ambao wanakwenda kwenye mechi hizo na kukuta tiketi zimekwisha, hivyo kuweza kuwa chanzo cha vurugu.

Ili kujiridhisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilifanya uhakiki na kubaini Uwanja wa Azam una uwezo wa kuchukua watazamaji 5,000 tu na si 7,000 kama ilivyoelezwa awali. Hata hivyo lengo la mmiliki wa uwanja huo ni kuongeza viti hadi kufikia 7,500.

Kwa mantiki hiyo tiketi zitakazouzwa kwa mechi za Yanga na Simba kwenye uwanja huo ni 5,000 tu. Vituo vya kuuzia tiketi hizo siku moja kabla ya mchezo na siku yenyewe ya mchezo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha Mafuta cha OilCom kilichoko Ubungo na Mbagala Rangitatu.

Viingilio kwa mechi za timu hizo zitakazochezwa Uwanja wa Azam ni sh. 20,000 kwa jukwaa kuu lenye uwezo wa kuchukua watazamaji 400 wakati majukwaa ya kawaida itakuwa sh. 7,000. Ili kuhakikisha idadi ya mashabiki haizidi uwezo wa uwanja hakutakuwa na tiketi za bure (complimentary).

Hivyo kutokana na kuwepo vituo vya kuuzia tiketi katika maeneo yaliyotajwa, mashabiki ambao watakosa tiketi hawana sababu ya kwenda uwanjani. Simba na Yanga zitaanza kuutumia uwanja huo kesho (Septemba 14 mwaka huu) kwa Simba kuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma wakati siku inayofuata Yanga itakuwa mgeni wa African Lyon.

MASHTAKA DHIDI YA LOUIS SENDEU
Sekretarieti ya TFF itawasilisha mashtaka dhidi ya Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi inayoongozwa na Kamishna wa Polisi mstaafu Alfred Tibaigana kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi.

Mara baada ya mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Sendeu aliita mkutano na waandishi wa habari na kumshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao.

Aliongeza kuwa anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba, kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima si halali na alifanya hivyo kwa lengo la kuisadia Simba ili iendelee kukaa kileleni mwa ligi.

Kauli ya Sendeu ililenga kumjengea chuki Mahagi mbele ya mashabiki wa Yanga kama ilivyo kwa viongozi na watendaji wa TFF. Ni wazi Sendeu akiwa ofisa wa Yanga anajua taratibu za kufanya pale klabu yake isiporidhishwa na uamuzi wa mwamuzi au suala lingine lolote.

Matamshi ya Sendeu yanalenga kuchochea chuki na vurugu katika mpira wa miguu ambapo ni kinyume na Ibara ya 53(1) na (2) ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Monday, September 12, 2011

SALHA NDIYE MISS TANZANIA 2011

Warembo watano walioingia hatua ya fainali ya shindano la Miss Tanzania 2011

MREMBO wa Tanzania wa mwaka 2011, Salha Israel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na mshindi wa pili, Tracy Sospeter (kushoto) na mshindi wa tatu, Alexia Williams (kulia) mara baada ya kutangazwa matokeo ya shindano hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.Friday, September 9, 2011

Kasaloo Kyanga afariki dunia, kuzikwa kesho makaburi ya SinzaMWANAMUZIKI mkongwe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Kasaloo Kyanga amefariki dunia.

Kasaloo amefariki dunia leo asubuhi katika hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam, ambako alikuwa amelazwa siku mbili zilizopita.

Mwanamuziki huyu ni pacha wa mwanamuziki mwingine, Kyanga Songa, ambaye alifariki miaka kadhaa iliyopita akiwa nchini Kenya.

Marehemu Kasaloo atakumbukwa sana kwa vibao vyake mbalimbali alivyowahi kuvitunga na kuviimba akiwa na bendi za Super Matimila, Maquis Original na Tuncat Almasi Orchestra.
Miongoni mwa vibao vilivyompatia umaarufu ni pamoja na Kalubandika, alichokiimba akiwa Maquiz, ambacho jina lake lilitumika sana katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kuwakebehi wanaume ambao ni laghai wa mapenzi.
Kibao kingine kilichomfanya mwanamuziki huyo aheshimika katika anga la muziki hapa nchini ni Masafa Marefu, alichokiimba akiwa na bendi ya Tancut.

Kasaloo aliletwa hapa nchini kwa mara ya kwanza miaka ya mwishoni mwa 1980 na mmiliki wa bendi ya Super Matimila. Wakati akija nchini, Kasaloo alifuatana na mwimbaji mwenzake kutoka Congo, Skassy Kasambula.

Kwa sasa, Kasambula yupo nchini akitokea Kenya, ambako amekuwa akiishi na kupiga muziki kwa miaka kadhaa sasa. Kasambula alirejea nchini kuja kumuuguza Kasaloo.

Kwa mujibu wa mwanamuziki mkongwe nchini, John Kitime, msiba wa Kasaloo upo nyumbani kwake Manzese jirani na baa ya Sandton na Tip Top na mazishi yake yamepangwa kufanyika kesho kwenye makaburi ya Sinza, Dar es Salaam.

Wadau wa muziki nchini watamkosa marehemu Kasaloo, lakini sauti yake maridhawa na tungo zake tamu zitaendelea kudumu masikioni mwa mashabiki wa muziki.

Mungu alitoa, Mungu ametwaa, jina lake litukuzwe. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema, peponi.

Mrembo yupi kutwaa taji la Miss TZ kesho?


WAREMBO 30 kutoka mikoa mbalimbali nchini, keshokutwa wanatarajiwa kupanda ulingoni kuwania taji la Vodacom Miss Tanzania 2011 katika shindano litakalofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Washiriki hao walipata tiketi ya kuwania taji hilo baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya mikoa na kanda. Mashindano hayo yalianza Juni mwaka huu na yanafikia tamati kesho.
Mshindi wa taji hilo mwaka huu atazawadiwa gari aina ya Jeep Patriot lenye thamani ya sh. milioni 72. Gari hilo limetolewa na Kampuni ya CFAO Motors na lilionyeshwa kwa warembo hao Jumatatu iliyopita.
Tofauti na mashindano yaliyopita, shindano la mwaka huu lilikuwa na mabadiliko makubwa, ambapo washiriki badala ya kukaa hotelini, walikwenda ndani ya nyumba moja, iliyofahamika kwa jina la Vodacom House.
Wakiwa ndani ya nyumba hiyo, mbali ya kufanya mazoezi ya miondoko ya kwenye steji, washiriki walipata mafunzo mbalimbali kuhusu maisha na jamii kwa ujumla.
Miongoni mwa mafunzo yaliyotolewa kwa washiriki hao ni pamoja na ujasiliamali, kujitambua wao ni nani na pia tahadhari ya ugonjwa hatari wa ukimwi.
Warembo hao pia walipata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya kitalii vilivyopo mjini Arusha, kupiga picha na wenyeji, kutembelea vituo kadhaa vya kulea watoto yatima vya mjini Dar es Salaam na kushiriki kwenye maonyesho ya mavazi.
Kwa mujibu wa utaratibu mpya wa mashindano hayo uliobuniwa na Vodacom, shindano la mwaka huu lilitanguliwa na mashindano madogo manne, ambapo washindi walipata tiketi ya kuingia moja kwa moja hatua ya nusu fainali.
Mashindano hayo madogo, ambayo pia hufanyika wakati wa shindano la kumsaka mrembo wa dunia ni ya mrembo mwenye kipaji, mrembo mwenye mvuto wa picha, mrembo mwanamichezo na mwanamitindo bora.
Mshindi wa taji la mrembo mwanamichezo alikuwa Loveness Flavian wakati taji la mrembo mwenye mvuto wa picha lilinyakuliwa na Tracy Mabula. Mwajabu Juma aliibuka mshindi wa taji la mwanamitindo bora wakati Rose Albert alishinda taji la mrembo mwenye kipaji.
Warembo 15 wanatarajiwa kuingia katika hatua ya nusu fainali kabla ya kupatikana warembo watano watakaoingia fainali. Warembo hao watano ndio watakaoulizwa maswali ili kupimwa ufahamu wao juu ya mambo mbalimbali na hatimaye kutangazwa mshindi.
Warembo watakaowania taji hilo mwaka huu, kanda wanazotoka zikiwa kwenye mabano ni Jenifer Kakolaki (Ilala), Leyla Juma (Nyanda za Juu), Mwajabu Juma (Temeke), Mariaclara Mathayo (Mashariki), Cynthia Kimasha (Temeke), Christina William (Nyanda za Juu Kusini), Hamisa Hassan (Kinondoni), Alexia Williams (Ilala), Stacy Alfred (Kaskazini) na Asha Saleh (Mashariki).
Wengine ni Zubeda Seif (Kaskazini), Rose Hubert (Kaskazini), Maua Kimambo (Kati), Glory Samuel (Ziwa), Neema Mtitu (Chuo Kikuu Huria), Atu Daniel (Nyanda za Juu Kusini), Blessing Ngowi (Elimu ya Juu), Weirungu David (Chuo Kikuu Huria), Chiary Masonobo (Chuo Kikuu DSM), Irene Karugaba (Ziwa).
Washiriki wengine ni Delilah Gharib (Kati), Tracy Sospeter (Ziwa), Husna Twalib (Temeke), Loveness Flavian (Mashariki), Christine Mwegoha (Kati), Husna Maulid (Kinondoni), Zerulia Manoko (Kati), Salha Israel (Ilala), Glory Lory (Vyuo Vikuu) na Stella Mbuga (Kinondoni).

Nchunga kiongozi halali Jangwani


KAMATI ya Sheria, Katiba, Maadili na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema uongozi wa klabu ya Yanga uliopo madarakani ni halali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa kamati hiyo, Alex Mgongolwa, alisema uongozi huo chini ya Lloyd Nchunga, uko madarakani kihalali, kwa mujibu wa katiba ya Yanga ya mwaka 2010.
Kamati hiyo ilikutana Septemba 3, mwaka huu, katika Ofisi za TFF kujadili mgogoro wa kikatiba uliopo ndani ya klabu ya Yanga na kuridhia kuwa ni viongozi halali.
Mgongolwa alisema baada ya kupokea nyaraka zilizowasilishwa mbele ya kamati, wamebaini kwamba katiba ya Yanga ya mwaka 2010 iliyosajiliwa katika ofisi ya msajili wa vyama vya michezo, inatambulika kisheria.
“Mchakato wa kupata katiba hiyo, ulifuata maagizo sahihi ya FIFA (Shirikisho la Soka Duniani) na TFF,” alisema.
Mgogoro wa uongozi wa Yanga, uliibuka ghivi karibuni baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam kukubaliana na ombi la wanachama waliofungua kesi kuwapinga Nchunga na wenzake.
Wanachama hao, wakiongozwa na Juma Mwambelo, walifungua kesi Na. 98 ya mwaka 2010 katika mahakama hiyo wakidai kuwa uongozi wa Yanga chini ya Nchunga, uliwekwa madarakani na katiba ambayo ni batili, hivyo hawaopaswi kuongoza klabu hiyo.
Walidai kuwa katiba hiyo ni batili kwa kuwa haitambuliwi na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA- zamani Kabidhi Wasii Mkuu), badala yake katiba inayotambulika ni ile ya mwaka 1968, ambayo ilisajiliwa rasmi mwaka 1972.
Uamuzi wa wanachama hao, ulikuwa kinyume na sheria na kanuni za FIFA ambazo zinakataza mashauri ya michezo kufikishwa mahakamani, bali yanapaswa kufuata ngazi husika katika vyama na mashirikisho ya michezo kuanzia ngazi ya nchi hadi FIFA.
Kutokana na hatua hiyo, kamati ya Mgongolwa imeuagiza uongozi wa Yanga kuwachukulia hatua za kikatiba wanachama hao waliopeleka shauri hilo mahakamani.
“Iwapo klabu ya Yanga itashindwa kutekeleza agizo hilo, TFF haitasita kuichukulia hatua za kikatiba kwa mujibu wa katiba ya TFF na ya FIFA,” alisema Mgongolwa katika taarifa yake. Hatua hiyo ya wanachama ilishaanza kuathiri maendeleo na shughuli za klabu. Uamuzi huo wa mahakama ulizuia mkutano wa wanachama, uliokuwa umepangwa kufanyika Jumapili iliyopita kwenye bwalo la maofisa wa polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

GENEVIEVE: Nimejifunza mengi Miss TZ


MREMBO wa Tanzania wa mwaka jana, Genevieve Emmanuel amesema, amejifunza mengi kutokana na kushikilia taji hilo kwa mwaka mmoja.
Genevieve, ambaye anajiandaa kumkabidhi taji mrembo wa mwaka huu, atakayepatikana keshokutwa, amesema kwa sasa anajiamini zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya kushinda shindano hilo.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Genevieve alisema taji hilo limemwezesha kupata uzoefu mkubwa katika mambo mbalimbali.
“Mimi kama Vodacom Miss Tanzania ninayemaliza muda wangu, nimejifunza namna ya kushirikiana na kujichanganya na watu, na pia nimeongeza uwezo wa kujiamini,”alisema.
Genevieve alisema changamoto pekee kubwa aliyoipata ni kukosa ushirikiano mzuri wa wadhamini, hasa katika azma ya kusaidia jamii.
Kutokana na kujitokeza kwa tatizo hilo, mrembo huyo amezishauri kampuni, taasisi na watu binafsi wenye uwezo kifedha, kuwaunga mkono warembo na kuwatumia katika kazi zao.
Akizungumzia ushiriki wake katika shindano la kumsaka mrembo wa dunia mwaka jana, Genevieve alisema japokuwa hakufanya vizuri, anaamini aliipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
“Nina hakika niliiwakilisha vizuri nchi yangu ya Tanzania na kupeperusha vyema bendera yetu. Tulikuwa washiriki 105 na mshindi aliyehitajika ni mmoja. Hivyo kwa jumla nami ni mshindi,”alisema.
Alipoulizwa mtazamo wake kuhusu shindano la mwaka huu, Genevieve alisema washiriki wengi ni wazuri na wanakidhi vigezo vinavyotakiwa, lakini uamuzi wa mwisho utakuwa wa majaji.
Alisema anashukuru kwa kumaliza muda wake salama bila kuandamwa na kashfa zozote kama ilivyokuwa kwa baadhi ya warembo waliopita na anamini mrembo mpya atakayepatikana keshokutwa atatekeleza vyema majukumu yake.

Nelly Kamwelu kuwania taji la Miss Universe J'pili
MWAKILISHI wa Tanzania katika shindano la Miss Universe 2011, Nelly Kamwelu mwishoni mwa wiki hii anatarajiwa kupanda ulingoni mjini Brasilia nchini Brazil kuwania taji hilo.
Nelly, ambaye ni mshindi wa taji hilo mwaka huu hapa nchini, atapanda jukwaani pamoja na washiriki wengine zaidi ya 100 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Habari kutoka nchini Brazil zimeeleza kuwa, Nelly ni miongoni mwa warembo waliofanya vizuri katika hatua za awali za shindano hilo. Hatua hizo ni shindano la mrembo mwenye kipaji na mwanamichezo bora.
Picha kadhaa za mtandao wa Miss Universe zimekuwa zikimuonyesha Mtanzania huyo akishirki katika kucheza soka ya wanawake wakati wa shindano la mwanamichezo bora.
Kadhalika mrembo huyo alitia fora katika shindano la kumsaka mrembo mwenye kipaji kutokana na kuonyesha umahiri mkubwa wa kucheza ngoma za utamaduni za makabila ya Tanzania.
Shindano la Miss Universe ndilo kongwe kuliko yote duniani, likifuatiwa na lile la kumsaka mrembo wa dunia. Mashindano hayo mawili hufanyika kila mwaka.
Nelly ni mrembo wa tano kuiwakilisha Tanzania katika shindano hilo. Wa kwanza alikuwa Flaviana Matata mwaka 2007, ambaye alifanikiwa kuingia hatua ya 15 bora katika shindano la Miss Universe na kushika nafasi ya sita.
Flaviana, ambaye alishiriki kwenye shindano hilo nchini Mexico,aliibuka kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki kutokana na kunyoa nywele zake zote na kubaki upara. Kwa sasa, Flaviana ni mwanamitindo maarufu nchini Marekani.
Amanda Ole Sululu, msichana wa kabila la kimasai kutoka Arusha, aliibuka mshindi wa taji hilo mwaka 2008, lakini hakuweza kufanya vizuri katika shindano la Miss Universe baada ya kutolewa hatua za awali.
Pamoja na kuvurunda katika shindano la dunia, Amanda aliweka rekodi ya kuwa kivutio kwa mashabiki wakati wa shindano la hapa nchini. Kabla ya matokeo kutangazwa wakati wa fainali, mashabiki walilipuka mayowe ya kumshangilia huku wakilitaja jina lake kabla ya jaji mkuu kumtangaza mshindi.
Illuminata James kutoka mkoani Mwanza, aliibuka mshindi wa taji hilo mwaka 2009 na kushiriki kwenye shindano la Miss Universe mjini Nassau, Bahamas.
Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa washiriki wenzake waliotangulia, Illuminata hakuweza kufanya vizuri katika shindano hilo. Alitolewa hatua za awali.
Mwaka jana, taji hilo lilinyakuliwa na Hellen Dausen kutoka mkoani Arusha, ambaye naye alishindwa kufanya vizuri katika shindano la Miss Universe baada ya kutolewa hatua za awali.
Na sasa macho na masikio yote ya watanzania yapo kwa Nelly, ambaye amekabidhiwa dhamana ya kupeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano hayo keshokutwa.
Je, Nelly ataweza kufuata nyayo za Flamiana ama atafika mbali zaidi. Tusubiri tuone.

Simba yatesa, Yanga nywii


Na Sophia Wakati, Tanga na Mwandishi Wetu, Morogoro
SIMBA jana iliendelea kung’ara katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Villa Squad bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Wakati Simba ikiwa imetoka uwanjani na ushindi, mabingwa watetezi Yanga waliendelea kuvurunda baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Mtibwa Sugar katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Ushindi ilioupata Simba, ambao ni wa tatu mfululizo, uliiwezesha kuchupa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi tatu. JKT Ruvu inaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na Simba.
Katika mechi yake ya kwanza, Simba iliilaza JKT Oljoro mabao 2-0 kabla ya kuichapa Coastal Union bao 1-0.
Dalili za ushindi kwa Simba zilionekana mapema baada ya kulishambulia kwa nguvu lango la Villa Squad kwa lengo la kusaka mabao ya mapema, kupitia kwa Haruna Moshi, Gervas Kago na Ulimboka Mwakingwe, ambao walifumua mashuti makali langoni mwa wapinzani wao.
Jitihada zao zilizaa matunda dakika ya saba baada ya kupata bao pekee, lililofungwa na mchezaji wa kimataifa kutoka Jamhuri ya Kati, Kago aliyefunga kwa shuti baada ya kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa pembeni na Haruna Moshi 'Boban'.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuongeza kasi langoni mwa Villa Squad, lakini wapinzani wao walisimama kidete kuokoa hatari. Mwakingwe nusura afunge bao dakika 62, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango akiwa ana kwa ana na kipa Abbas Nassoro.
Villa Squad imepoteza mchezo wa pili tangu kuanza ligi msimu huu.Ilifungwa mabao 3-0 na Toto African katika mchezo wa ufunguzi kabla ya kulazimisha sare bao 1-1 na Kagera Sugar.
Simba: Juma Kaseja, Said Nassor, Amir Maftah, Juma Nyoso, Victor Costa, Jerry Santo, Haruna Moshi, Shija Mkina, Amri Ramadhani, Gervas Kago na Ulimboka Mwakingwe.
Villa Squad: Abbas Nasoro, Haruna Shamte, Yassin Majota, Shai Mpala, Menrad Mbunguza, Zuberi Dabi, Lameck Mbonde, Mussa Nampaka, Mohamed Binslum, Mohamed Kijuso na Nsa Job.
Katika hatua nyingine, timu ya Yanga jana ililazimishwa kutoka suluhu na Mtibwa Sugar katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi mbili baada ya kucheza michezo mitatu. Ilianza vibaya ligi kwa kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Moro United.
Yanga itabidi ijilaumu kwa kushindwa kupata bao, kwani ilifanya mashambulizi mengi kwenye lango la Mtibwa kipindi cha pili, lakini washambuliaji wake, Jerry Tegete, Davies Mwape na Kenneth Asamoah hawakuwa makini.