KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

BASATA yahimiza usajili wa kumbi na wasanii

ANGELO Luhala


BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wamiliki wa kumbi za burudani nchini kuzisajili ili ziweze kutambulika kisheria.
Baraza hilo pia limewataka wasanii na wadau wa sanaa nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kujisajili.
Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya BASATA, Angelo Luhala wakati wa Jukwaa la Sanaa lililofanyika kwenye ofisi za baraza hilo zilizopo Ilala Sharifu Shamba, Dar es Salaam.
Jukwaa hilo huandaliwa kila Jumatatu na BASATA kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz).
Luhala alisema, kwa mujibu wa sheria, suala la kujisajili kwa wasanii na wadau wa sanaa ni la lazima na si hiyari.
“Naanzia kusema hapa, kila anayefanya kazi yoyote ya sanaa ni wajibu ajisajili, kujihusisha na shughuli za sanaa. Bila kujisajili ni kuvunja sheria,kanuni na taratibu za nchi,” alisema.
Luhala alisema, kwa mujibu wa sheria ya nchi namba 23 ya mwaka 1984, BASATA imepewa mamlaka ya kusajili na kusimamia sekta ya sanaa nchini, hivyo mtu yeyote anayefanya shughuli za sanaa, anapaswa kusajiliwa na kupewa kibali cha kufanya shughuli hizo.
Aliongeza kuwa, sanaa ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, hivyo kila anayefanya kazi ya sanaa, anapaswa kutambuliwa na serikali na baraza kwa niaba ya serikali limepewa kazi hiyo.
Kwa mujibu wa Luhala, wadau wanaopaswa kujisajili BASATA ni pamoja na wasanii wa fani zote, wakuzaji sanaa (mapromota), vikundi vya wasanii, kumbi zote za burudani, wafanyabiashara wa sanaa, vyama na asasi mbalimbali za sanaa.
Akizungumzia faida za kujisajili, Luhala alisema ni pamoja na kufuata sheria na taratibu za nchi, kutambuliwa na serikali na pia kupata utambulisho wa baraza katika mahitaji mbalimbali. Alizitaja faida zingine kuwa ni kupata fursa za kushiriki maonyesho, taifa kuwa na takwimu sahihi za wadau wanaojihusisha na shughuli za sanaa na nyinginezo.
“Kuna watu wanajiuliza kwa nini wasajiliwe, lazima ieleweke kwamba, kila anayejihusisha na shughuli za sanaa, lazima atambuliwe na serikali. Hapa ndipo tunapata takwimu pia,” alisisitiza.
Wadau mbalimbali waliohudhuria programu hiyo, walionekana kuwa na shauku kubwa kwani mbali na suala la usajili, baraza lilitoa elimu kwa wasanii juu ya kulinda haki zao ikiwa ni pamoja na wasanii kutakiwa kujisajili kwenye chombo kinacholinda Hakimiliki na Shiriki cha Cosota.

No comments:

Post a Comment