KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 31, 2017

MAYANGA AMWONGEZA EMMANUEL MARTIN KIKOSI CHA TAIFA STARS



Kocha Mkuu wa timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Mayanga amemwongeza Kiugo wa Young Africans, Emmanuel Martin kwenye kikosi chake kinachojindaa kucheza na Botswana Jumamosi Septemba 2, mwaka huu.

Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam chini ya utaratibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Emmanuel Martin anatarajiwa kujiunga na kambi ya Taifa Stars mara moja leo Agosti 30, mwaka huu na kuanza na mazoezi na wenzake yatakayofanyika jioni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Emmanuel Martin ameongezwa na Mayanga baada ya mawasiliano kuonesha kwamba huenda akawakosa nyota wa kimataifa Simon Msuva kutoka Difaa El Jadidah ya Morocco na Orgenes Mollel wa FC Famalicao ya Ureno.

Taarifa kutoka Morocco inaonesha kwamba Msuva ana kibali cha muda cha kuingia na kutoka Morocco ‘visa’ ambacho kinamnyima haki ya kutoka na kuingia Morocco mara kwa mara.

Kuna juhudi zinafanywa na timu yake kadhalika Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco kumfanikishia kupata kibali cha muda mrefu ili iwe rahisi kwa mchezaji kutoka na kuingia kama anahitaji katika timu ya taifa.

Kuhusu Mollel taratibu za ruhusa za kimataifa zinafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria za nchi ya Ureno ambako anacheza soka la kulipwa.

Nyota wengine wote wameripoti Taifa Stars wakiwamo wale wa kutoka nje ya mipaka ya Tanzania kama vile Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Elias Maguli (Dhofar FC/Oman), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya) wakati Farid Mussa wa CD Tenerif ya Hispania anatarajiwa kutua leo.

Wengine ambao wako kambini Hoteli ya Sea Scape iliyoko Kunduchi, Dar es Salaam ni makipa Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Young Africans).

Pia wamo Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphas Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).

Viungo ni Himid Mao – Nahodha Msaidizi (Azam FC), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Shiza Kichuya (Simba SC), wakati Washambuliaji ni Raphael Daud (Young Africans) na Kelvin Sabato (Azam FC).

Benchi la Ufundi la Mayanga linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).

KESI YA AVEVA, KABURU YAZIDI KUPIGWA KALENDA



UPANDE wa Jamhuri katika kesi inayowakabili   Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange 'Kaburu' umedai unaendelea na uchunguzi wa nyaraka zilizokusanywa ambazo zimepelekwa kwa mtaalamu wa maandishi.

Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson alidai hayo jama katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Esterzia alidai hayo wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa kutajwa ambapo aliieleza mahakama kuwa bado wanaendelea na uchunguzi wa nyaraka mbalimbali zilizokusanywa ambazo zimepelekwa kwa mtaalamu wa maandishi, hivyo wanasubiria ripoti.

Kutokana na hilo, Esterzia aliomba shauri hilo liahirishwe hadi tarehe nyingine kwa kutajwa. Hakimu Victoria aliuhimiza upande wa jamhuri kujitahidi ili ripoti hiyo itoke mapema na kesi iweze kuendelea.

Shauri hilo liliahirishwa hadi Septemba 8, mwaka huu, kwa kutajwa na washitakiwa walirudishwa mahabusu kwa kuwa miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni ya kutakatisha fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, viongozi hao wa klabu ya Simba, wanakabiliwa na mashitaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha Dola za Marekani (USD) 300,000.

Washitakiwa hao   walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa  USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.

Aveva anadaiwa  Machi 15,2016, katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala, huku akijua   alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.

Aveva na Nyange wanadaiwa tarehe tofauti  kati ya Machi 15 na Juni 29,2016, mkoani Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000, wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Aveva anadaiwa  Machi 15,2016, katika benki ya Baclays, Mikocheni alijipatia USD 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Nyange anadaiwa Machi 15,2016, katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva kujipatia USD 300,000, wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

Wednesday, August 30, 2017

KAMATI YA NIDHAMU TFF KUKUTANA LEO


Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake Tarimba Abbas, kinatarajiwa kuketi kesho Jumatato Agosti 30, mwaka huu.

Kamati hiyo itakuwa na ajenda kadhaa ikiwamo ya mashauri yanayohusu wachezaji mbalimbali, viongozi na klabu.

Shauri mojawapo linahusu ripoti ya Mechi namba 236 ya Ligi Kuu ya Vodacom uliokutanisha timu za Mbao FC na Yanga uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Yanga ikipoteza kwa bao 1-0.

Mara baada ya mchezo huo, Kamati ya 72 ya Bodi ya Ligi ilipitia matukio mbalimbali na kufikia uamuzi wa kuwasimamisha wachezaji Deus Kaseke, Simon Msuva na Obrey Chirwa wa Yanga kucheza mechi za Ligi Kuu.

Walisimamishwa wakisubiri suala lao la kumsukuma na kumwangusha Mwamuzi Ludovic Charles kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Wachezaji hao walidaiwa kufanya kitendo hicho katika mechi hiyo dhidi ya Mbao FC iliyofanyika Mei 20, 2017 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijni Mwanza. Uamuzi wa Kamati ya Saa 72 ulizingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.

Mwamuzi Ludovic Charles amepewa onyo kali kwa kutodhibiti vizuri mchezo. Uamuzi dhidi yake ni kwa mujibu w Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.

KIKAO CHA KAMATI YA TIBA KUFANYIKA LEO


Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Dkt. Paul Marealle ameitisha kikao cha Kamati ya Tiba kitakachofanyika kesho Jumatano Agosti 30, mwaka huu kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Kikao hicho kitakachofanyika Ukumbi wa Ofisi za Makao Makuu TFF, yaliyoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam kitarejea shughuli zake kwa mujibu wa Katiba ya TFF sambamba na Kanuni zinazoongoza mashindano mbalimbali ya TFF.

Katika kikao hicho, pia kamati itapitia fomu za afya za utimamu wa mwili za wachezaji wote wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL); Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL).

Miongoni mwa majukumu ya kamati hiyo ni kupitisha wachezaji wanaopaswa kucheza/kushiriki katika ligi baada ya kujirisha juu ya utimamu wa mwili wa wachezaji kwa michuano tajwa hapo juu.

WANANE WAPITISHWA KUWANIA UONGOZI BODI YA LIGI


Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imetangaza majina manane ya wagombea ambao yamepita katika mchujo wa awali kuwania nafasi mbalimbali katika Kamati ya Uongozi (Management Committee) ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Waliopitishwa ni kuwania uenyekiti wa Management Committee ni Clement Sanga na Ahmed Yahya wakati Shan Crysostoms ameiptishwa kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, Ramadhan Mahano na Hamisi Madaki wamepitishwa kuwania nafasi ya Ujumbe wakitokea klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

James Bwire na Almas Kasongo wamepitishwa kuwania Ujumbe wakitokea klabu za Ligi Daraja la Kwanza. Brown Ernest hakupitishwa kwa sababu hakuthibitishwa na klabu yake.

Edga Chubura amepitishwa kuwania ujumbe akitokea klabu za Ligi Ligi Daraja la Pili.

Wagombea kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Bodi ya Ligi Kuu ni marais au wenyeviti wa klabu husika. Wagombea wanatakiwa kuwa wenyeviti au Marais wa klabu husika.

Nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inagombewa na klabu za Ligi Kuu pekee.

Uchaguzi huo wa kamati hiyo utafanyika Jumapili Oktoba 15, 2017 jijini Dar es Salaam na unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.

TAIFA STARS YAANZA MAZOEZI


Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imeanza kujifua leo asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Wachezaji wote kutoka klabu za Tanzania wamefika kadhalika baadhi kutoka nje ya mipaka ya Tanzania kama vile Nahodha Mbwana Samatta na Elias Maguli. Mazoezi hayo yataendelea kila siku hadi Ijumaa wiki hii.

Kikosi hicho kinachofanya mazoezi chini ya Kocha Mkuu, Salum Shabani Mayanga kinajindaa kucheza na Botswana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa chini ya utaratibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Wiki ya FIFA kwa mechi za kimataifa inatarajiwa kuanza Jumatatu Agosti 28 hadi Septemba 5, mwaka huu ambako Tanzania imekubaliana kucheza Botswana kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Jumamosi ya Septemba 2, 2017.

Katika kikosi hicho cha wachezaji 21, Kocha Mayanga amemwita upya Mlinzi wa Young Africans, Kelvin Yondani huku nyota kutoka nje ya mipaka ya Tanzania wakiwa ni saba.

Kikosi hicho kinachopiga kambi hoteli ya Sea Scape iliyoko Kunduchi, Dar es Salaam kina makipa Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Young Africans).

Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphas Maganga (Mbao FC), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Kelvin Yondani (Young Africans), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).

Viungo ni Himid Mao - Nahodha Msaidizi (Azam FC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Saimon Msuva (Difaa El Jadidah/Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Farid Mussa (CD Tenerif/Hispania) na Orgenes Mollel (FC Famalicao/Ureno).

Washambuliaji ni Raphael Daud (Young Africans), Kelvin Sabato (Azam FC), Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji) na Elias Maguli (Dhofar FC/Oman).

Benchi la Ufundi la Mayanga linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).

Monday, August 28, 2017

SIMBA, AZAM SASA KUKIPIGA SEPTEMBA 6


Bodi ya Ligi (TPLB) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limefanya mabadiliko kidogo katika michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kama ifuatavyo.
 

Michezo ambayo imefanyiwa mabadiliko ni kati ya Tanzania Prisons na Majimaji ya Songea; Azam FC na Simba, Njombe Mji na  Young Africans; Mtibwa Sugar na Mwadui FC ambayo sasa itachezwa Septemba 6, 2017.

Pia tarehe hiyo ya Septemba 6, mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Lipuli na Stand United; Singida United na Mbao; Kagera Sugar na Ruvu Shooting wakati Mbeya City na Ndanda FC .


Michezo mingine ambayo imesogezwa hadi Septemba 11, 2017 ni kati ya Azam na Kagera Sugar wakati Mbao na Tanzania Prisons utachezwa Septemba 21, mwaka huu.


Kadhalika mechi nyingine zitachezwa Oktoba 11, mwaka huu ni kati ya Mbao na Azam FC; Kagera Sugar na Mwadui; Mbeya City na Ruvu Shooting; Ndanda na Singida United.

Tarehe hiyo pia Oktoba 11, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Njombe Mji na Simba; Mtibwa na Tanzania Prisons; Lipuli na Majimaji wakati Stand United na Young Africans watacheza Oktoba 12, mwaka huu.

Novemba 15, 2017 Mbao itacheza na Young Africans; Kagera na Mbeya City; Stand United na Azam; Mwadui na Ruvu Shooting; Singida na Njombe Mji; Lipuli na Tanzania Prisons; Mtibwa Sugar na Majimaji wakati Novemba 16, Ndanda itacheza na Simba.

YANGA YABANWA MBAVU NA LIPULI


MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana waliianza vibaya ligi hiyo baada ya kulazimishwa sareya bao 1-1 na Lipuli.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Lipuli inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Selemani Matola, ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Seif Abdalla dakika ya 44.

Yanga ilisawazisha dakika moja baadaye kwa bao lililofungwa na Donaldo Ngoma, kufuatia mpira wa kona uliopigwa na beki Juma Abdul.

Lipuli ililazimika kumaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji 10, baada ya nahodha wake, Asante Kwasi kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Awali, alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano.

SIMBA YAANZA LIGI KUU KWA KISHINDO, YAIBAMIZA RUVU SHOOTING 7-0



SIMBA imeanza michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara kwa kishindo baada ya kuibamiza Ruvu Shooting mabao 7-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi aliibuka shujaa wa Simba baada ya kuifungia mabao manne kati ya saba.

Kutokana na kufunga idadi hiyo ya mabao, Okwi alizaliwadiwa mpira uliotumika katika mechi hiyo baada ya pambano kumalizika.

Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Shiza Kichuya, Juma Luizio na Erasto Nyoni.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Azam iliichapa Ndanda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Mwadui ilishinda 2-1 dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wakati Mtibwa Sugar wameilaza Stand United 1-0 kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Timu machachari ya Mbao FC nayo iliibuka na ushindi ugenini baada ya kuichapa Kagera Sugar 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Tanzania Prisons iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mji Njombe wakati Mbeya City iliilaza Majimaji ya Songea 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Sokoine, mjini Mbeya.

Saturday, August 26, 2017

STAND UNITED YAPATA MKATABA WA MILIONI 100 KUTOKA BIKO



Wakati pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2017-2018 likitarajiwa kufunguliwa rasmi kesho Agosti 27, mwaka huu kwa timu zote 16 kuingia viwanjani,Kampuni ya Michezo ya Bahati Nasibu Mtandaoni – BIKO imeidhamini Klabu ya Stand United ‘Chama la Wana’ shilingi milioni 100 kuanzia mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Ijumaa,Agosti 25,2017mjini Shinyanga, Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mheshimiwa Stephen Masele (CCM) alisema BIKO wameamua kuidhamini timu hiyo baada ya kuridhishwa na mwenendo wa timu hiyo.
“Baada ya Stand United kupoteza mwelekeo na wadhamini wake Kampuni ya Acacia kujiondoa katika udhamini,hivi sasa nimeamua kuwa msimamizi mkuu wa timu hii,nimetafuta udhamini mwingine,nimeiomba kampuni ya Kitanzania ya BIKO,imekubali kuwa wadhamini wakuu na imetupatia shilingi milioni 100 kwa mwaka huu”,alieleza Masele.
Mbunge huyo alisema ameamua kuwa msimamizi mkuu wa timu hiyo ili kuhakikisha kuwa timu hiyo inafanya vyema katika michezo mbalimbali.

“Najua mnaelewa uhusika wangu katika Stand United,mnafahamu jitihada nilizofanya kuhakikisha timu hii inafanya vizuri,ili timu hii iwe ya kimataifa na timu hii baada ya kupata matatizo yaliyotokea,ilikuwa kama timu yatima,haina ulezi,haina msaada,na mimi kama mbunge nilikuwa nimekasirika na nikasema Maeja na wenzake wasinisumbue katika mambo ya mpira”,alisema.
“Nilitafuta ufadhili wa shilingi bilioni 2.4 kutoka Acacia,lakini tuliuchezea,na baada ya kujiridhisha na uongozi mpya ulioingia ukiongozwa na Dk. Maeja nimetafuta wadhamini wengine ambao ni kampuni ya BIKO ili kuisadia timu yetu,naomba fedha hizi zitumike vizuri”,alisema Masele.

Masele alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha viongozi wa timu kuhusu matumizi mabaya na ubadhirifu wa fedha zilizotolewa na wadhamini hao na kuwa hawatasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.
“BIKO itapenda kuona fedha hizi zinatumikaje na kuanzia sasa mtu yeyote atakayejihusisha na ubadhirifu tutamfikisha katika vyombo vya sheria kwa sababu wanaumiza hisia za watu wengi”,aliongeza Masele.
“Nataka niwahikikishie kuwa timu hii haitashuka daraja kinatochotakiwa ni kutoa msaada kwa timu hii ikiwemo kuishangilia,jambo jingine naomba mjitahidi kubana matumizi katika masuala mbalimbali ikiwemo pale mnaposafiri punguzeni idadi ya watu wa kusafiri lakini pia lipeni mishahara ambayo haiumizi sana”,aliongeza.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Klabu ya Stand United,Dkt. Ellyson Maeja alisema Klabu hiyo ya Stand United imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa inafanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2017-2018.

“Hivi sasa timu imetulia kiuongozi tatizo ni bajeti,mpira ni pesa,bila pesa hakuna timu,lakini pia hatuna usafiri wala hosteli kwa ajili ya wachezaji,tunaomba wadau waendelee kujitokeza kuisaidia timu hii,tumesajili wachezaji wapya 19,jumla sasa wapo 30,tunaye kocha mzuri,walimu wazuri,malengo yetu ni kushika nafasi ya kwanza hadi ya tatu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu wa 2017-2018?,alisema Dkt.Maeja.

YANGA WAMWONGEZEA LWANDAMINA MKATABA WA MWAKA MMOJA


Kocha wa Yanga, George Lwandamina hana mpango wa kuondoka, maana tayari ameongezewa muda wa kuendelea kufanya kazi Jangwani.
Uongozi wa Yanga umeamua kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja kocha wake George Lwandamina raia wa Zambia baada ya ule wa awali kumalizika Julai 16, mwaka huu.
Katika mkataba wake uliopita, Lwandamina aliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kuifikisha katika nusu fainali ya Kombe la FA kabla ya kutolewa na Mbao FC ya Mwanza.
Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa amesema  mchana kuwa, wameamua kumuongezea mkataba Lwandamina baada ya kuridhishwa na kazi yake.
“Tunaingia mkataba mwingine wa mwaka mmoja na Lwandamina kwani ule wa mwanzo umeisha na sasa kila kitu kipo tayari hivyo muda wowote tena kwa uwazi kabisa atasaini mkataba mpya.
“Tumejitahidi kwa uwezo wetu kuboresha mkataba wake mpya kwa kumuongezea maslahi kidogo ili apate motisha ya kufanya kazi yake ipasavyo,” alisema Mkwasa.
Lwandamina alitarajiwa kusaini mkataba huo muda wowote kuanzia jana mchana ili awe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi yake kwa uhuru na kujiamini.

MAYANGA ATAJA TAIFA STARS MPYA KUIVAA BOTSWANA


Kocha Mkuu wa timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Shabani Mayanga ametangaza kikosi kipya kitakachocheza na Botswana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa chini ya utaratibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).


Wiki ya FIFA kwa mechi za kimataifa inatarajiwa kuanza Jumatatu Agosti 28 hadi Septemba 2, mwaka huu ambako Tanzania imekubaliana kucheza na Botswana kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Jumamosi ya Septemba 2, 2017.


Katika kikosi hicho cha wachezaji 21, Kocha Mayanga amemwita upya Mlinzi wa Young Africans, Kelvin Yondani huku nyota kutoka nje ya mipaka ya Tanzania wakiwa saba, akiwamo nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Ally Samatta.


Kikosi hicho kinachotarajia kuingia kambini kesho Jumapili kuanzia saa 2.00 usiku ni makipa Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Young Africans).


Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphas Maganga (Mbao FC), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Kelvin Yondani (Young Africans), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).


Viungo ni Himid Mao - Nahodha Msaidizi (Azam FC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Saimon Msuva (Difaa El Jadidah/Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Farid Mussa (CD Tenerif/Hispania) na Orgenes Mollel (FC Famalicao/Ureno).


Washambuliaji ni Raphael Daud (Young Africans), Kelvin Sabato (Azam FC), Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji) na Elias Maguli (Dhofar FC/Oman).


Benchi la Ufundi la Mayanga linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).

LIGI KUU TANZANIA BARA KUANZA KUTIMUA VUMBI LEO



Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), msimu wa 2017/18 inaanza rasmi leo Jumamosi Agosti 26, 2017 kwa michezo saba itayochezwa katika viwanja tofauti nchini.
 
Ni msimu mpya utakaotoa timu bingwa mpya itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), msimu wa 2019.


Itakumbukwa, msimu wa CAF wa 2018, timu itakayoiwakilisha nchi ni Young Africans SC ambayo ni Bingwa wa VPL msimu 2016/17 wakati michuano ya Kombe la Shirikisho, Tanzania itawakilishwa na Simba SC.


TFF tunazitakia kila la kheri timu zote zinazoshiriki ligi hii, tukiamini kwamba uadilifu utaongoza mbele ya taratibu, kanuni na sheria zinazosimamia mpira wa miguu hapa nchini na kwingineko.


Kwa mechi za kesho Jumamosi, Simba inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati Mbao watakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.


Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Majimaji ya Songea itakayosafiri hadi Mbeya kucheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini humo huku Njombe Mji ikiialika Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sabasaba huko Makambako.


Kadhalika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani, Mtibwa mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar itaikaribisha Stand United ya Shinyanga kwenye mchezo mwingine wa VPL ilihali Azam atakuwa mgeni wa Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.


Mwadui watakuwa wenyeji wa Singida United ya Singida kwenye Uwanja wa Mwadui huko Shinyanga na Jumapili kutakuwa na Mchezo mmoja utakaokutanisha Young Africans na Lipuli kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.

RAIS WA FIFA AMPONGEZA KARIA, AMWALIKA ZURICH

Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Gianni Infantino, ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Wallace Karia kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa TFF kwa kipindi cha miaka minne ijayo ya 2017-2021.


Rais Infantino katika barua yake ya Agosti 14, 2017 aliyoiandika kutoka Zurich, amesema: “Ningependa kuchukua nafasi hii kukupa pongezi zangu dhati. Nakutakia kila la kheri katika majukumu yako.”


Rais wa FIFA amesema kwamba hana shaka na uwezo wa Karia hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa Makamu wa Rais wa kipindi kilichopita, hivyo atakuwa fursa thabiti ya kuiletea nchi maendeleo ya mchezo soka.


“Kwa wakati wote, nakuhakikishia ushirikiano wa kutosha kutoka FIFA katika malengo yako. Milango ya FIFA iko wazi wakati wowote wewe kuja kujadili masuala ya mchezo wa mpira wa miguu hasa eneo la utawala.


“Ningependa kuchukua nafasi hii kukualika kuja hapa Zurich wakati wowote kuanzia sasa ambako nitapata  fursa ya kukutambulisha maeneo mbalimbali ya FIFA. Nimeagiza upande wa utawala kuwasiliana nawe kuona na kupanga tarehe rasmi ya safari,” amesema na kuongeza:
 
“Nikutakie tena kheri na fanaka, nguvu na kila aina ya mafanikio katika majukumu yako mapya huku nikitarajia ujio wa kuonana nawe haraka.”


Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Rwanda (FERWAFA) nalo kwa upande wake wamempongeza Rais wa TFF, Wallace Karia kwa kuchaguliwa kuwa kiongozi mpya wa shirikisho.


Katika barua ya FERWAFA iliyosainiwa na Rais wa shirikisho hilo, Nzamwita Vincent imesema kwamba Rwanda itaendelea kuwa bega kwa bega na Tanzania katika maendeleo ya mpira wa miguu kwa ushirikiano baina ya nchi mbili kadhalika ukanda wa Afrika Mashariki unaounda Baraza la Sola la nchi za Afrika Mashariki.

Thursday, August 24, 2017

TFF YAWAOMBA RADHI WADAU WA SOKA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linaomba radhi wanafamilia wote wa mpira wa miguu kutokana na makosa ya maandishi yaliyoonekana kwenye utambulisho wa Ngao ya Jamii iliyotolewa Jumatano Agosti 23, 2017.

Ngao hiyo ilitolewa mara baada ya mchezo uliokutanisha timu za Simba SC na Yanga SC za Dar es Salaam kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa jijini. Katika mchezo huo, Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya Yanga na kutwaa Ngao hiyo.

Watanzania hususani wanafamilia ya mpira wa miguu popote pale, TFF hatujapokea vizuri mwonekana wenye makosa kwenye Ngao hiyo ya Jamii kama ambavyo wadau hawajapokea vema suala hili.

Kutokana na makosa hayo, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, tayari amechukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliohusika kadhalika kuwasiliana na uongozi wa Simba SC kuirejesha Ngao hiyo ili kufanyiwa marekebisho yatakayobaki kwenye kumbukumbu sahihi.

Hatutegemei tukio kama hili kujirudia tena.

SIMBA SIMBA SIMBA


NGEBE, tambo na majivuno baina ya mashabiki wa klabu za Yanga na Simba zimemalizika. Jana ilikuwa hukumu kwa timu hizo kongwe katika mchezo wa Ngao ya Jamii.

Timu ya Simba ilitwaa Ngao ya Jamii, baada ya kushinda mabao 5-4 kwa penalti.

Mchezo huo wa kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ulichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mikwaju ya penalti ilitumika ili kupata bingwa, baada ya miamba hiyo ya kandanda kumaliza ndani ya dakika 90.

Penalti za Yanga zilifungwa na Papy Tshishimbi, Thabani Kamusoko, Ibrahim Ajibu, Donald Ngoma wakati Kelvin Yondani, Juma Mahadhi walikosa.

Simba ilipata penalti zake kupitia kwa Method Mwanjali, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim 'Mo' wakati Mohammed Hussein 'Tshabalala' walikosa.


Mchezo huo ulikuwa ni moja ya ‘derby’ maarufu Afrika ikishika nafasi ya tatu baada ya Al Ahly vs Zamalek za Misri inayotajwa namba moja.

Nyingine ni ‘Soweto Derby’ baina ya Orlando Pirates vs Keizer Chiefs za Afrika Kusini ikifuatiwa na Simba dhidi ya Yanga.

Awali, mpira ulianza kwa kasi hasa ukichezwa zaidi katikati kwa takribani dakika 10 huku wachezaji wa kimataifa Haruna Niyonzima wa Simba na Papy Tshishimbi, wakionyesha ufundi.

Niyonzima aliyejiunga na Simba kutoka Yanga, alicheza kwa ustadi katika eneo la katikati akisaidiana na Mzamiru Yassin.

Tshishimbi, kiungo wa kimataifa aliyetua Yanga kutoka Mbabane Swallors, aling'ara katika dimba la kati akigawa mipira maridadi kwa washambuliaji wake.

Kiungo huyo raia wa Swaziland mwenye asili ya Jamhuri ya Congo, alicheza pacha na nahodha wake Thabani Kamusoko.

Licha ya kujiunga na Yanga muda mfupi, Tshishimbi, alicheza kwa ustadi kulinganisha na Niyonzima katika mchezo huo.

Simba ilifanya shambulizi la kushitukiza dakika ya 15, lakini Laudit Mavugo, alikosa bao akiwa ndani ya eneo la hatari.

Mavugo, alishindwa kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Niyonzima kutoka upande wa kulia mwa uwanja.

Ibrahim Ajibu, mmoja wa washambuliaji hatari nchini, alikosa bao dakika ya 24 kwa kupiga shuti lililotoka pembeni kidogo mwa lango la Simba.

Ajibu ametua Yanga kutoka Simba na jana alicheza kwa kiwango bora na kuwa tishio kwa safu ya ulinzi ya Simba iliyokuwa chini ya mabeki wa kati nahodha Method Mwanjali na Salim Mbonde.

Yanga ilikosa bao dakika ya 30 baada ya Donald Ngoma, kupiga mpira wa krosi uliotua mikononi kwa kipa Aishi Manula.

Simba ilijibu shambulizi dakika tatu baadaye kwa shuti la kiungo wa pembeni Shiza Kichuya kupiga mkwaju uliozuiwa na beki Vincent Andrew 'Dante'.

Niyonzima alikosa bao dakika ya 40, alipounganisha mpira wa kona uliochongwa na Kichuya lakini alifumua shuti juu.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku timu zote zikikosa mabao licha ya kutengeneza nafasi za kufunga.

Laudit Mavugo wa Simba nusura afunge bao baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga, lakini shuti lake lilitoka nje kabla ya Kamusoko kukosa bao dakika ya 53.

Lango la Simba lilikuwa katika hatari ya kufungwa bao, baada ya Yanga kufanya shambulizi lakini mabeki waliokoa.

Juma Liuzio alikosa bao dakika ya 75 baada ya kupiga shuti ambalo mabeki wa Yanga walikaa imara kuokoa.

Pia Ajibu alikosa bao dakika ya 77 kwa shuti lake kupaa kabla ya Tshishimbi kufumua shuti dakika mbili baadaye lililokosa mwelekeo.

Niyonzima aliyepewa kadi ya njano na mwamuzi wa mchezo, Elly Sasi, alionekana mara kwa mara akilalamika uwanjani.

Dakika ya 86 Ajibu alikosa bao baada ya kupiga mpira wa krosi kuokolewa na libero Salim Mbonde.

Yanga: Youthe Rostand, Juma Abdul/Hassani Kessy, Gadiel Michael, Vincent Andrew, Kelvin Yondani, Papy Tshishimbi, Thabani Kamusoko, Raphael Daudi/Juma Mahadhi, Donald Ngoma, Ibrahim Ajibu na Emmanuel Martin.

Simba: Aishi Manula, Ali Shomari, Erasto Nyoni/Mohammed Hussein, Method Mwanjali, Salim Mbonde, James Kotei, Mzamiru Yassin/Mohammed Ibrahim, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Laudit Mavugo/Juma Liuzio na Shiza Kichuya.

Wednesday, August 23, 2017

KIDAU KATIBU MKUU MPYA TFF




Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imepitisha jina la Kidao Wilfred kuwa Kaimu Katibu Mkuu.

Kidao ambaye ni mchezaji wa zamani wa Taifa Stars ambaye pia Mwenyekiti wa Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA), ameteuliwa rasmi jana Agosti 22, 2017 na Kamati ya Utendaji ya TFF. Wasifu wa Kidao utawajia punde.

KIUNGO YANGA AFUNGIWA MWAKA MMOJA


Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, iliyokutana kwa siku mbili mfululizo Agosti 20 na 21, 2017, jijini Dar es Salaam, imepitia usajili wa majina ya klabu 40.

Katika idadi hiyo ya timu 40, kamati imepitia klabu 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa mujibu wa katiba na kanuni za mashindano yanayosimamiwa na kuendeshwa na TFF.

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, inayoongozwa na Wakili Richard Sinamtwa, imegundua na kubaini kuwa mchezaji Pius Busita amesaini mikataba ya klabu mbili tofauti katika msimu mmoja wa 2017/18.

Kamati imebaini kwamba mchezaji huyo aliyechezea Mbao FC ya Mwanza msimu uliopita, amevunja Kanuni ya 66 ya Ligi Kuu ya Vodacom ambayo inaelekeza adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja. Mchezaji huyo amefungiwa kucheza mpira wa miguu kwa mwaka mmoja.

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya  TFF, imebaini upungufu katika uwasilishaji wa majina ya wachezaji wa msimu wa 2017/18 kwa timu zote.

Klabu imeagiza klabu zote kuleta majina matatu ya wachezaji wasiopungua 18 na wasiozidi 30 wa kikosi cha timu ya vijana (U20).

Klabu zote zimeagizwa kuanisha wachezaji wa zamani na wapya na klabu wakakotoka kwa timu zote mbili za wakubwa na vijana.

Kamati imezitaka klabu hizo pia kuzingatia matakwa ya kanuni kwa kila mchezaji ambaye atapewa leseni ya kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi daraja la Kwanza.

Matakwa hayo ambayo ambayo yamesisitizwa ni kila mchezaji kujaziwa fomu ya utimamu wa mwili ‘Medical Form’ ya TFF.

Pia Klabu zinatakiwa kuwasilisha nakala tatu za mikataba (Contracts) ya kila mchezaji katika Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Uthibitisho wa kukatiwa Bima ‘Insurance’, Barua ya Uhamisho ‘Release Letter’ kutoka timu ambayo ametoka.

Kadhalika sharti jingine linahusu wachezaji wa kigeni ambako kila mchezaji hana budi kuwa na Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na kulipwa Ada ya ushiriki ya msimu Sh. 2,000,000.

Klabu zimeagizwa kikamilisha utaratibu wa usajili kabla ya Agosti 24, 2017.

KARIA ATEUA KAMATI MPYA TFF, NYAMLANI NA MGOYI WAPEWA SHAVU


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Wallace Karia amewateua Makamu wa Rais wa zamani wa TFF, Athuman Nyamlani na Ahmed Mgoyi kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.

Rais Karia ameteua kwa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo katika Katiba ya TFF ikiwa ni wiki moja baada ya kupatikana kwa viongozi wa shirikisho katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 12, mwaka huu.

Rais Karia aliwatambulisha viongozi hao kwenye Kikao cha Kamati ya Utendaji iliyofanyika Jumanne Agosti 22, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho pia Rais Karia alitumia fursa hiyo kutangaza viongozi wa kamati mbalimbali za TFF zikiwamo za kinidhamu na kisheria.

Kamati ya Nidhamu: Mwenyekiti Tarimba Abbas, Makamu Mwenyekiti, Peter Hella wakati wajumbe ni Boniface Lyamwike, Dk. Bill Haonga na Kassim Dau.

Kamati ya Rufani za Nidhamu: Mwenyekiti ni Wakili Rahim Zuber Shaban; Makamu Mwenyekiti, Stella Mwakingwe wakati Wajumbe ni Abbas Mtemvu, Amani Mulika na Siza Chenja.

Kamati ya Maadili: Mwenyekiti ni Wakili Hamidu Mbwezeleni, Makamu Mwenyekiti ni Wakili Steven Zangira wakati Wajumbe ni Glorious Luoga, Walter Lungu na Amin Bakhressa.

Kamati ya Rufaa ya Maadili: Mwenyekiti ni Wakili Ebenezer Mshana; Makamu Mwenyekiti ni DCP. Mohammed Mpinga na wajumbe  ni Wakili Benjamin Karume, George Mayawa na ASP. Benedict Nyagabona.

Kamati ya Uchaguzi: Mwenyekiti ni Revocatus Kuuli; Makamu Mwenyekiti ni Wakili Mohammed Mchengerwa; Wakili Edwin Mgendera; Wakili Kiomoni Kibamba na Wakili Thadeus Karua.

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi: Mwenyekiti ni Kenneth Mwenda; Makamu Mwenyekiti ni Jabir Shekimweri na Wajumbe ni Wakili Rashid Sadalla, Irene Kadushi na Mohammed Gombati.

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji: Mwenyekiti ni Elias Mwanjala; Makamu Mwenyekiti ni Wakili Malangwe Mchungahela wakati Wajumbe ni Zakaria Hanspope, Robert Selasela, Goodluck Moshi, Mhandisi Issa Batenga na Hamis Semka.

Kamati ya Fedha na Mipango: Mwenyekiti ni Michael Wambura; Makamu Mwenyekiti ni Francis Ndulane na Wajumbe ni Almas Kasongo, Pascal Kihanga, Maximillian Tabonwa, Paul Bilabaye na Farid Abeid.

Kamati ya Mashindano: Mwenyekiti ni Ahmed Mgoyi; Makamu Mwenyekiti ni James Mhagama wakati Wajumbe ni Kenneth Pesambili, Shafii Dauda, Fortunatus Kalewa na Mhandisi Andrew Makota.

Kamati ya Ufundi: Mwenyekiti ni Vedastus Lufano; Makamu Mwenyekiti ni Issa Bukuku na wajumbe ni Sarah Chao, Ally Mayay, Michael Bundala, Omar Abdulkadir na Israel Mujuni.

Kamati ya Soka la Vijana: Mwenyekiti ni Khalid Abdallah; Makamu Mwenyekiti ni Lameck Nyambaya na Wajumbe ni Mohammed Aden, Ramadhani Nassib, Salim Kibwana na Vicent Majili.

Kamati ya Mpira wa Wanawake: Mwenyekiti ni Amina Karuma; Makamu Mwenyekiti ni Rose Kissiwa na Katibu wa Kamati hiyo ni Somoe Ng’itu wakati Wajumbe ni Zena Chande, Beatrice Mgaya, Sofia Tigalyoma, Zuhura Kapama na Nia Mjengwa.

Kamati ya Waamuzi: Mwenyekiti ni Saloum Chama; Makamu Mwenyekiti Joseph Mapunda wakati Wajumbe ni Nassib Mabrouk, Leslie Liunda na Soud Abdi.

Kamati ya Habari na Masoko: Mwenyekiti ni Dunstan Mkundi; Makamu Mwenyekiti ni Mbasha Matutu wakati Wajumbe ni Imani Kajura, Mgaya Kingoba, Godfrey Dilunga na Samson Mbamba.

Kamati ya Ukaguzi wa Fedha: Mwenyekiti ni Yahya Hamad; Makamu Mwenyekiti ni Athuman Nyamlani na Wajumbe ni Khalifa Mgonja, Japhary Kachenje, Jackson Songoro na Benesta Rugora.

Kamati ya Tiba: Mwenyekiti ni Dkt. Paulo Marealle; Makamu Mwenyekiti ni Dkt. Fred Limbanga Wakati wajumbe ni Dkt. Norman Sabun, Dkt. Lisobina Kisongo, Dkt. Eliezer Ndalama, Dkt. Elson Maeja na Violet Lupondo.

Kamati ya Futsal na Beach Soccer: Mwenyekiti ni Ahmed Mgoyi; Makamu Mwenyekiti ni Hussein Mwamba na Wajumbe ni Blassy Kiondo, Isaac Munisi, Didas Zimbihile na Aaron Nyanda.

Kamati ya Ajira: Mwenyekiti ni Issa Bukuku; Makamu Mwenyekiti ni Saloum Chama wakati Wajumbe ni Athuman Kihamia, Mtemi Ramadhani, Noel Kazimoto na Hawa Mniga.

Kamati ya Leseni za Klabu: Mwenyekiti ni Wakili Lloyd Nchunga; Makamu Mwenyekiti Wakili Emmanuel Matondo wakati Wajumbe ni Profesa Mshindo Msolla, Hamisi Kissiwa na David Kivembele.

Kamati ya Rufaa za Leseni: Mwenyekiti Wakili Dk. Damas Ndumbaro; Makamu Mwenyekiti ni Wakili Alex Mngongolwa Wajumbe ni Meneja wa zamani wa Uwanja wa Taifa, Charles Matoke, Tumainiel Mlango na Ahmed Menye.

TIMU SITA DARAJA LA KWANZA SASA KUPANDA LIGI KUU


Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litapandisha idadi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu msimu ujao wa 2018/19 kutoka 16 za sasa hadi 20, imefahamika.

Uamuzi huo umefanyika Jumanne Agosti 22, 2017 wakati Kamati ya Utendaji inafanya marekebisho ya Kanuni za Ligi Daraja la Kwanza inayotarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu.

Kwa marekebisho hayo, timu zitakazoshuka daraja msimu ujao kutoka Ligi Kuu ya Vodacom ya sasa ni mbili hivyo kubaki 14. Na ili kufikia timu 20, timu sita (6) za Ligi Daraja la Kwanza zitapanda daraja.

Kwa mujibu wa utaratibu wa Ligi Daraja la Kwanza, timu, ina maana kwamba msimu huu timu mbili zitapanda kutoka katika kila kundi katika ligi hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu.

Makundi ya Daraja, kundi ‘A’ lina timu za African Lyon, Ashanti United, Friends Rangers za Dar es Salaam, JKT Ruvu na Kiluvya United za Pwani, Mgambo JKT ya Tanga, Mvuvumwa ya Kigoma na Polisi Moro ya Morogoro.

Kundi ‘B’ ziko za Coastal Union ya Tanga; JKT Mlale ya Ruvuma; KMC ya Dar es Salam, Mawezi Market ya Morogoro, Mbeya Kwanza ya Mbeya, Mufundi United ya Iringa, Mshikamano na Polisi Dar za Dar es Salaam.

Kundi ‘C’ lina timu za Alliance School, Pamba na Toto

African za Mwanza, Rihno Rangers ya  Tabora, Polisi Mara ya Mara, Polisi Dodoma ya Dodoma, Transit Camp ya Shinyanga na JKT Oljoro ya Arusha.

Sunday, August 20, 2017

WACHEZAJI SIMBA, YANGA KUPIMWA MKOJO



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema wachezaji wa klabu za Simba na Yanga, watafanyiwa vipimo vya mkojo kabla ya mechi yao ya kuwania Ngao ya Jamii, itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Saaam.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema mjini Dar es Salaam, jana, kuwa upimaji huo umelenga kubaini iwapo kuna baadhi ya wachezaji wa timu hizo wanatumia dawa za kuongeza nguvu.

Alfred alisema upimaji wa aina hiyo ni wa kawaida kwa timu zote zinazoshiriki katika michuano ya ligi kuu na hufanyika wakati wowote.

Alisema kitakachofanyika ni madaktari kuchukua vipimo vya mchezaji yeyote watakayemuhitaji kutoka katika kila timu na utasimamiwa na TFF.

"Tumekuwa tukifanya hivi kila mwaka, kabla ya ligi kuanza na zoezi hili hufanywa na madaktari maalumu chini ya usimamizi wa TFF. Huu ni muendelezo wa upimaji huo, haitakuwa mara ya kwanza,"alisema Alfred.

Kwa mujibu wa Alfred, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mechi hiyo yanakwenda vizuri na tiketi zimeshaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali ili kuwapa fursa mashabiki kununua mapema, hivyo kujiepusha na usumbufu.

Viingilio katika mchezo huo vimepangwa katika makundi manne. Sehemu ya VIP A tiketi ni sh. 25,000; VIP B na C sh. 20,000; Viti vya rangi ya chungwa sh. 10,000 na mzunguko kwa viti vya rangi za bluu na kijani ni sh. 7,000.

Katika kujiandaa na mechi hiyo, Simba na Yanga zimekwenda Unguja na Pemba kwa ajili ya kuweka kambi, ikiwa ni pamoja na kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu.

Wakati huo huo, habari za kuaminika kutoka ndani ya TFF, zimeeleza kuwa, mwamuzi bora wa ligi kuu msimu uliopita, Elly Sassi, mwenye umri wa miaka 28, ndiye atakayechezesha mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba.

Sassi ndiye aliyeibuka mwamuzi bora wa ligi hiyo msimu uliopita na amekuwa akitabiriwa kufika mbali kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha katika kuchezesha soka.

Mwamuzi huyo kijana pia amekuwa akitajwa kuwa ni mwenye msimamo, anayefuata sheria na kanuni zote za kuchezesha soka, jambo ambalo limemfanya amudu michezo mingi mikubwa, ndani na nje ya nchi.

YANGA YAMALIZA KAMBI PEMBA KWA USHINDI


Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara Yanga wamemaliza Kambi yao Visiwani Pemba kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Jamhuri mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na msimu pamoja na Mechi ya Ngao ya Hisani utakaowakutanisha na mahasimu wao Simba Agosti 23 mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Wakicheza katika uwanja wa Gombani uliopo visiwani humo Yanga walipata bao hilo kupitia kwa beki wao wa kushoto,Mwinyi Hajji kwa shuti kali lililoenda moja kwa moja na unakuwa ushindi wa tatu wakiwa Zanzibara na ukiwa wa pili visiwani Pemba baada ya Jumatano kuwafunga timu ya Chipukizi bao 1-0 ambalo lilifungwa na Ibrahim Ajibu.

Baada ya hapo walipita visiwani Unguja na kucheza na Mlandege na kupata ushindi wa jumla ya mabao 2-0 yakifungwa na Ibrahimu Ajibu na Emmanuel Martin huku kocha Mkuu George Lwandamina akianza na vikosi viwili kipindi cha kwanza kilikuwa hiki Kabwili, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Abdallah Hajji ‘Ninja’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Pato Ngonyani dk34, Maka Edward, Pius Buswita, Said Juma ‘Makapu’, Amissi Tambwe/Said Mussa dk34, Matheo Anthony na Juma Mahadhi/Yussuf Mhilu dk34.

Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko kwa kukitoa kikosi kizima na kuingiza hiki Youthe Rostand, Hassan Kessy/Juma Abdul dk70, Gardiel Michael, Kevin Yondan, Andrew Vincent ‘Dante’, Papy Kabamba Tshisbimbi, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Ibrahim Hajib, Emmanuel Martin na Raphael Daudi.

Hata hivyo hakikuweza kubadili matokeo na kubaki kuwa bao moja hilo na kujiweka mguu sawa kuwavaa watani wao wa Jadi Simba kwenye ngao ya hisani Mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani Mkubwa hii inatokana na usajili uliofanywa na timu hizo.

Yanga wanatarajia kuingia jijini Dar es salaam Siku ya Jumanne ya wiki inayoanza kesho tayari kwa vita ya Ngao ya Hisani pamoja na kuanza Mikikimikiki ya Ligi Kuu ya Tanzania bara linalotanzamiwa kufunguliwa Agosti 26 huku Mabingwa hao watetezi wakitaraajia kutupa karata yao siku ya Jumapili ya Agosti 27 kuvaana na wageni wa Ligi timu ya Lipuli FC kutoka Iringa.

YAMETIMIA SIMBA


Wanachama 1,216 wa klabu ya Simba, leo wameridhia mfumo wa klabu yao kuuza Hisa baada ya Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (MNICC), Dar es Salaam.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Afya Jinsia na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala, Kaimu Mwenyekiti wa klabu, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kwamba asilimia 50 ya hisa zitauzwa kwa mwekezaji yeyote au wowote watakaoungana wasiozidi watatu, kwa sharti moja tu la kuwa wanachama wa klabu hiyo.

Abdallah alisema mwekezaji huyo au hao, wanatakiwa kuweka dau lisilopungua Sh. Bilioni 20 ili kupatiwa asilimia 50 ya hisa za klabu, wakati kwa kuanzia wanachama wote wa Simba wamepewa asilimia 10 ya hisa.

Alisema asilimia nyingine 40 zitawekwa kama mtaji wa klabu na zitauzwa kwa wanachama baadaye, lakini wale wawekezaji walionunua asilimia 50 awali, hawataruhusiwa kununua hata hisa moja kwenye asilimia 40 za mtaji.

Na baada ya mkutano wa leo, zoezi litakalofuata ni uhakiki wa wanachama wa klabu hiyo ili kuweza kujua mgawanyo wa asilimia 10 za hisa utakavyokuwa – na itaundwa Kamati maalum ya kupitia maombi ya wawekezaji wanaotaka kununua asilimia 50 ya hisa.

Mgeni rasmi, Dk Kigwangala ameunga mkono mabadiliko hayo na kuwaambia wanachama wa Simba wamechelewa kufanya uamuzi wa mabadiliko hayo, kwani walipaswa kufanya hivyo miaka mingi iliyopita na anaamini klabu nyingine zitafuata nyayo hizo.

“Leo Agosti 20 klabu ya Simba imetengeneza rekodi nyingine baada ya ile ya mwaka 1977 ya kuwafunga Yanga 6-0, na sisi kama Serikali chini ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli tunaunga mkono mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu ya Simba,”amesema Dk. Kigwangala.

Kigwangala alisema serikali ya Rais Magufuli inaelewa changamoto za maendeleo ya soka na imekwishaanza kukarabati viwanja vya soka ili kukuza na kuendeleza vipaji na kuviendeleza huku ikijipanga kukusanya kodi.

Alisema rais Magufuli anapenda michezo, amefanikisha hatua za ujenzi wa uwanja wa michezo mkoani Dodoma kwa ufadhili wa Mfalme wa Morocco, Mohammed VI ambao ni zaidi ya Dola za Marekani milioni 100.

Kwa upande wake Mwanasheria aliyefanikisha muundo huo mpya, Evodius Mtawala ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa klabu hiyo, alisema kwamba baada ya taratibu hizo kukamilika kinachofuata ni Kamati ya Utendaji kutengeneza kamati huru itakayosimamia tenda ambako pia baadaye itatangazwa tenda.

Naye Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura alisema mfumo uliopo katika soka la sasa ni kuendesha mchezo huo kibiashara na kuachana na mfumo wa kisiasa.

Wambura alisema wanachama wakiingia kwenye mfumo wa hisa, wataziingiza familia zao kwenye urithi endelevu hali ambayo ni tofauti na ilivyokuwa awali kwenye uanchama.

“Simba mara nyingi ndio wanakuwa wa kwanza kutekeleza maendeleo na hata ile migogoro ya mara kwa mara haitokuwepo tena na hata makomandoo hawatokuwepo, utakaposababisha Simba ipoteze mapato unajitakia njaa, mpango uliofanikishwa na Simba umeishitua TFF,” alisema Wambura.

WANACHAMA COASTAL UNION WAZIKA TOFAUTI ZAO



KLABU ya Coastal Union ya Jijini Tanga, imezika tofauti walizokuwa nazo awali zilizosababisha timu hiyo ishuke kutoka Ligi kuu ya Tanzania Bara msimu wa mwaka 2014/ 2015, na sasa timu hiyo imeunda umoja wa viongozi utakaokuwa na lengo la kuirejesha Ligi Kuu msimu ujao.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa wanachama uliofanyika makaomakuu ya klabuhiyo barabara ya 11 Jijini hapa, Mwenyekiti wa kamati ya mashindano, Ahmed Hilal ‘Aurora’ alisema kutokana na kikao kilichofanyika katika hoteli ya Mkonge, kimezika tofauti hizo na sasa wapo pamoja.

Alisema miongoni mwa watu waliohudhuria mkutano huo uliorudisha umoja ni pamojana Nassor Binslum ambaye ataisaidia tena kalbu hiyo pamoja na watu wengine ili kuhakikisha timu hiyo itakayoshiriki Ligi Daraja la kwanza iweze kurejea Ligi Kuu.

“Mkutano uliofanyika Mkonge Hoteli umezika yote yaliyotokea na tumeunda umoja ambao umewezesha timue yetu kusajili wachezaji watakaokuwa na uwezo wa kupanda daraja…Tunachotaka sasa watu wote wajali Coastal kwanza mambo mengine baadaye,” alisema Aurora.

Coastal iliteremka daraja baada ya viongozi kuhitafiliana na  Aurora akiwa Mwenyekiti aliyeipandisha daraja timu hiyo msimu wa 2011-2012 alijiuzulu wadhifa huo na baadaye timu kufanya uchaguzi uliomweka madarakani Dkt Ahmed Twaha ambaye aliishusha daraja akiwa na katibu wake Kassim El-Siagi na Akida Machai.

Mgogoro huo ulisababisha baadhi ya watu kwenda kujiunga na timu ya Mgambo JKT ambayo nayo ilishuka daraja hadi la kwanza huku wanachama wengine wakienda katika timu hiyo ambapo zote mwaja jana zilizoposhiriki ligi daraja la kwanza hazikufanya vizuri.

“Tumesamuheana kabisa na sasa tupo pamoja, tusianze kunyoosheana vidole na kufukua makaburi yaliyipita hatutafika tunapotaka kwenda lakini lazima mkumbuke mpira sasa ni fedha…Nawakumbusha pia lipeni ada zenu muwe na sauti kwa viongozi hawa,” alisema Aurora.

Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo Mohamed Musni, alisema kwamba hivisasa uongozi wa klabu hiyo umepanga kuhakikisha inafanya vizuri katika Ligi daraja la kwanza itakayoanzamwezi ujao ili wawqeze kurejea kwa kishindo Ligi Kuu.

Mjumbe wa kamati ya utendaji ya timu hiyo Abdallah Zuberi ‘Unenge’, aliwataka wanachama kuhakikisha wanaacha majungu ya kupeleka habari zitakazowarudisha kule walipotoka na badala yake wahubiri umoja kwa faida ya timu hiyo.

Kaimu Katibu Mkuu Nassoro Kibabedi, aliwataka wanachama waisaidie timu hiyo katika kipindi hiki na kamwe wasibweteke wakiamini kwamba wafadhili watafanya kila kitu hivyo walipeada zao ili ziweze kuisaidia klabu hiyo.

KIKAO CHA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI KUFANYIKA KWA SIKU MBILI


Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), inatarajiwa kuketi kwa siku mbili Agosti 20 na 21, 2017 kupitisha usajili, lakini kabla kupitisha itasikiliza malalamiko kutoka baadhi ya timu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji vya soka zinazodai fidia baada ya wachezaji wao kusajiliwa na klabu nyingine msimu wa 2017/18.

Viongozi au Wawakilishi wa Klabu zifuatazo hawana budi kufika Azam FC, Pamba FC, African Lyon, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Singida United, Tusker FC, Young Africans, Njombe Mji, Majimaji, KMC, Ndanda FC, Coastal Union,  Stand United, Rhino FC, Mbao FC, Toto Africans, Stand United, Mbeya City na Lipuli. Pia wameitwa wachezaji Mbaraka Yussuf na Frank Hamisi.

Klabu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji vilileta malalamiko yao TFF kudai fidia mbalimbali kama vile za mafunzo; ada ya usajili; ada za maendeleo na kuvunjwa kwa mikataba kutoka katika timu walizochezea hadi msimu uliopita.

Baadhi ya malalamiko yaliyopokelwa TFF ni ya Majimaji ya Songea dhidi ya Azam FC ya Dar es Salaam kuhusu mchezaji Idd Kipangwile.

Alliance ya Mwanza imelalamikia Pamba pia ya Mwanza kuhusu mchezaji Juma Nyangi ambako madai hayo yamekwenda mbali zaidi yakisema kuwa mchezaji husika amebadili jina kwa lengo la kudanganya.

Kwa upande wake, African Lyon imeondokewa na wachezaji 19 na inadai fidia katika timu, wachezaji kwenye mabano za Majimaji (Saleh Malande); Lipuli (Hamad Manzi, Lambele Reuben na Mussa Nampoka); Young Africans (Rostand Youthe Jehu); Tusker FC (Abdul Hilal) na Ndanda kwa wachezaji Hamad Tajiri na Baraka Majogoo.

Madai mengine ni dhidi ya Coastal Union kwa wachezaji Baraka Jaffary, Omary Salum, Raizen Hafidh na Fred Lewis huku madai mengine ni kwa Kagera Sugar kwa wachezaji Omar Abdallah, Abdallah Mguhi na Vicent Ludovic na Alhaji Zege .

Madai mengine ni dhidi ya timu ya Kinondoni Municipality Council (KMC) ambayo imewasajili Halfan Twenye, Yussuf Abdul na Rehani Kibingu wakati Singida United inalalamikiwa kumsajili Miraji Adam ilihali Njombe Mji inadaiwa fidia kwa kumsajili mchezaji Salum Juma.

Malalamiko mengine ni ya Kisa Academy ya Kinondoni, Dar es Salaam dhidi ya timu za Mbeya City (Idd Seleman); Majimaji (Jafar Mohammed); Mbao (Ally Rashid); Stand United (Said Mbati) na Friends Rangers (Hassan Abubakar).

Madai mengine dhidi ya timu za Coastal Union (Abubakar Nyakarungi na Ahmed George); The Mighty Elephant (Maliki Hamad); Kagera Sugar (Hussein Idd) na Azam FC (Omary Maunda).

Tuesday, August 15, 2017

MAANDALIZI MECHI YA NGAO YA HISANI YAKAMILIKA


Maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii utakaowakutanisha Mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2016/17, Young Africans na Mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup), Simba yanakwenda vema.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linapenda kuwatangazia umma kuwa viingilio katika mchezo huo vimepangwa katika makundi manne.

Sehemu ya VIP ‘A’ tiketi zake ni Sh 25,000; sehemu ya VIP ‘B’ na ‘C’ Sh 20,000; Viti vya Rangi la Chungwa Sh 10,000 na mzunguko kwa vitu vya rangi za bluu na kijani ni Sh 7,000.

Tiketi zimeanza kuuzwa leo Jumanne Agosti 15, 2017 ili kuwapa fursa wadau wa mpira wa miguu kununua tiketi mapema kujipeusha na usumbufu.

LYON YAWAWEKEA PIGAMIZI WACHEZAJI 19 AKIWEMO GOLIKIPA WA YANGA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea malalamiko kutoka baadhi ya timu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji vya soka zikidai fidia baada ya wachezaji wao kusajiliwa na klabu nyingine msimu wa 2017/18.

Jana Agosti 14, 2017 ilikuwa siku ya mwisho kwa timu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji kuwasilisha malalamiko yao TFF kuhusu fidia za mafunzo; ada ya usajili; ada za maendeleo na kuvunjwa kwa mikataba kutoka katika timu walizochezea hadi msimu uliopita.

TFF imepokea malalamiko ya Kagera Sugar ya Kagera dhidi ya Azam FC ya Dar es Salaam kuhusu mchezaji Mbaraka Yussuf wakati Majimaji ya Songea pia imelalamika Azam kuhusu mchezaji Idd Kipangwile.

Alliance ya Mwanza imelalamikia Pamba pia ya Mwanza kuhusu mchezaji Juma Nyangi ambako madai hayo yamekwenda mbali zaidi yakisema kuwa mchezaji husika amebadili jina kwa lengo la kudanganya.

Kwa upande wake, African Lyon imeondokewa na wachezaji 19 na inadai fidia katika timu, wachezaji kwenye mabano za Majimaji (Saleh Malande); Lipuli (Hamad Manzi, Lambele Reuben na Mussa Nampoka); Young Africans (Rostand Youthe Jehu); Tusker FC (Abdul Hilal) na Ndanda kwa wachezaji Hamad Tajiri na Baraka Majogoo.

Madai mengine ni dhidi ya Coastal Union kwa wachezaji Baraka Jaffary, Omary Salum, Raizen Hafidh na Fred Lewis huku madai mengine ni kwa Kagera Sugar kwa wachezaji Omar Abdallah, Abdallah Mguhi na Vicent Ludovic na Alhaji Zege .

Madai mengine ni dhidi ya timu ya Kinondoni Municipality Council (KMC) ambayo imewasajili Halfan Twenye, Yussuf Abdul na Rehani Kibingu wakati Singida United inalalamikiwa kumsajili Miraji Adam ilihali Njombe Mji inadaiwa fidia kwa kumsajili mchezaji Salum Juma.

Malalamiko mengine ni ya Kisa Academy ya Kinondoni, Dar es Salaam dhidi ya timu za Mbeya City (Idd Seleman); Majimaji (Jafar Mohammed); Mbao (Ally Rashid); Stand United (Said Mbati) na Friends Rangers (Hassan Abubakar).

Madai mengine dhidi ya timu za Coastal Union (Abubakar Nyakarungi na Ahmed George); The Mighty Elephant (Maliki Hamad); Kagera Sugar (Hussein Idd) na Azam FC (Omary Maunda).

Kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kinatarajiwa kuketi Jumapili kupitisha usajili lakini kabla kitapitia malalamiko hayo na kuchukua uamuzi.

UCHAGUZI WA KAMATI YA UONGOZI TPLB KUFANYIKA JUMAPILI YA OKTOBA 15,2017 JIJINI DAR


Uchaguzi wa Kamati ya Uongozi (Management Committee) ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara utafanyika Jumapili Oktoba 15, 2017 jijini Dar es Salaam.

Fomu kwa ajili ya wagombea zitaanza kutolewa Agosti 17, 2017 kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu kwa wagombea ni saa 10.00 jioni Agosti 23, mwaka huu.

Nafasi zitakazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watatu kuwakilisha klabu za Ligi (PL), Wajumbe wawili wa kuwakilisha klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na Mjumbe mmoja wa kuwakilisha klabu za Ligi Daraja la Pili (SDL).

Ada ya fomu kwa nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ni Sh 200,000 (Shilingi lakini mbili) wakati nafasi nyingine zilizobaki ni Sh 100,000 (Shilingi laki moja).

Uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.

Wagombea kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Bodi ya Ligi Kuu ni marais au wenyeviti wa klabu husika.

Wagombea wanatakiwa kuwa wenyeviti au Marais wa klabu husika.

Nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inagombewa na klabu za Ligi Kuu pekee.

VIONGOZI WA VILABU VYA LIGI DARAJA LA KWANZA KUFANYA KIKAO AGOSTI 18,2017

Viongozi wa Klabu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), wanatarajiwa kuwa na kikao na uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB), kitakachofanyika Ijumaa Agosti 18, 2017 kuanzia saa 3.00 asubuhi kwenye Hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kitakuwa maalumu kwa ajili ya kujadili Ligi Daraja la Kwanza lakini pia kutoa semina kwa viongozi hao kuhusu Leseni za Klabu (Club License).

TFF inatoa wito kwa viongozi wa juu wa klabu kuhudhuria kikao hicho muhimu . TFF ingependa kusisitiza kuzingatia muda wa kuanza kikao.

SEMINA YA WANACHAMA WA SIMBA KUELEKEA KWENYE MFUMO WA HISA KUFANYIKA KESHO


SIMBA SPORTS CLUB
DAR ES SALAAM
15-8-2017
            TAARIFA KWA UMMA

Klabu ya Simba kesho inatarajiwa kufanya Semina kubwa ya Wanachama wote wa klabu hiyo.
Semina hiyo inalenga kujenga uelewa mpana zaid juu ya muundo mpya wa klabu, uliotokana na mabadiliko ya katiba yaliyofanywa na wanachama hao,na kusajiliwa na Msajili wa Vilabu nchini.
Maandalizi yote ya Semina hiyo yamekamilika,na itafanyika kesho tarehe 16-8-2017,Jumatano Saa Nane na Nusu mchana(8.30) na itafanyikia kwenye ukumbi wa Mikumi uliopo kwenye eneo la maonyesho ya kimataifa ya biashara ya Sabasaba (PTA) kurasini hapa jijini Dar es salaam.
Tunawaomba wanachama wote popote walipo waje kwa wingi hapo kesho, huku klabu ikiwaomba viongozi wa Simba Wilaya ya Temeke waandae utaratibu mzuri wa kuwapokea wageni.
IMETOLEWA NA….
HAJI S MANARA
MKUU WA HABARI SIMBA SC
SIMBA NGUVU MOJA

Monday, August 14, 2017

TFF YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA DYAMWALE


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa kilichokuwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT), Chabanga Hassan Dyamwale (76).

Mbali wa wadhifa huo katika eneo la mpira wa miguu,  pia Dyamwale atakumbukwa zaidi akiwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na kwa miaka ya hivi karibu alikuwa Mjumbe wa Kamati huru ya uchaguzi TFF tangu 2004 mpaka 2012.

Hayati Dyamwale aliyezaliwa Juni 01, 1941, aliondoka FAT mwaka 1978, lakini pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Michezo nchini miaka ya mwanzo ya 1980 kabla ya kuhamishiwa Handeni mkoani Tanga kuwa Ofisa Utamaduni, lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere akamrudisha Dar es Salaam.

“Nimeguswa na kifo cha Mzee Chabanga Hassan Dyamwale. Inna Lillah wainaillah Rajauun. Natuma salamu zangu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, majirani na marafiki wa hayati Mzee Dyamwale ambaye nimetaarifiwa kuwa amefariki dunia Agosti 13, mwaka huu kwenye Hospitali ya Muhimbili,” amesema Karia.

“Ni msiba mkubwa kwa wanafamilia ya michezo hususani soka,” amesisitiza Rais Karia na kuomba  familia, ndugu, jamaa, marafiki kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu baada ya kumpoteza mpendwa Dyamwale.

Rais Karia amesema: “Namfahamu Mzee wetu huyu tangu miaka mingi akiwa mteuliwa kutoka serikalini kushika wadhifa wa utendaji ndani ya FAT wakati ule (Kwa sasa ni TFF), alifanya kazi kwa uhodari mkubwa na uadilifu,” amesema Rais Karia.

Rais Karia amesema kwamba mbali ya kuwa mtendaji ambaye alifanya mabadiliko makubwa katika soka la Tanzania kutoka ligi ya kituo kimoja hadi ligi ya mikondo miwili (nyumbani na ugenini). Taarifa zinasema kwamba alifanya kazi hiyo akiwa kwenye hema.

Pia Rais Karia alimfahamu Mzee Dyamwale alipokuwa Meneja wa Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) aliyekuwa mtaalamu wa masuala ya ujenzi wa viwanja.

Rais Karia amesema kwamba atambukuka zaidi hayati Dyamwale kwa uhodari wake wa kazi na msimamo kwenye jambo aliloliamini lilileta mafanikio makubwa katika soka la Tanzania.

Kumbukumbu nyingine zinaonesha kuwa Dyamwale ndiye aliyebuni mpango wa watoto kuingia bure uwanjani miaka ya 1980 maarufu yosso.

AJIBU AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO YANGA



MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Ibrahim Hajib, jana, alifunga bao lake la kwanza wakati timu yake hiyo ikiichapa Mlandege ya Zanzibar mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Ajibu, aliyesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Simba, alifunga bao hilo dakika ya 50, akimalizia krosi safi kutoka kwa Donald Ngoma.

Ajibu pia alitoa pasi iliyozaa bao la pili lililofungwa na Emmanuel Martin dakika ya 73.

Katika mechi hiyo, Kocha George Lwandamina wa Yanga, aliwabadilisha wachezaji wote kipindi cha pili, isipokuwa kipa Kabwili. Mabadiliko hayo ndiyo yaliyozaa mabao hayo mawili.

OKWI AONGEZA RAHA SIMBA



MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, ameongeza furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuifungia bao pekee na la ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar.

Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ilikuwa ya kujipima nguvu kwa timu zote mbili kwa ajili ya msimu huu wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Kocha Joseph Omog kutoka Cameroon, baada ya Jumanne iliyopita, kuwalaza mabingwa wa Ligi ya Rwanda,
Rayon Sport idadi hiyo ya bao kwenye uwanja huo.

Okwi alifunga bao hilo la pekee na ushindi dakika ya 44 baada ya kumalizia pasi kutoka kwa John Bocco.

Katika mechi hiyo, Mtibwa Sugar ilipata pigo dakika ya 30 baada ya kipa wake namba moja, Shabani Kado kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Abdalla Makangana.

KILOMONI AVULIWA UDHAMINI SIMBA, BILIONI 1.3 ZATUMIKA KUSAJILI WACHEZAJI



MKUTANO Mkuu wa klabu ya Simba, umetangaza kumvua wadhifa wa mjumbe wa baraza la wadhamini, mwanachama mkongwe, Hamisi Kilomoni.

Uamuzi wa kumvua nafasi hiyo Kilomoni, ulifikiwa katika mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika jana, kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdalla, alipendekeza mbele ya wanachama 927, waliohudhuria mkutano huo, Kilomoni aondolewe katika Baraza la Wadhamini kutokana na kitendo chake cha kufungua kesi mahakamani kupinga mkutano huo.

Kwa mujibu wa Salim, kwa kufanya hivyo, Kilomoni alivunja Katiba ya Simba
Ibara ya 18 kifungu cha 15 (b), ambayo hairuhusu masuala ya klabu hiyo
kufikishwa mahakamani.

Kilomini ametakiwa kuandika barua ya utetezi na kufuta kesi aliyofungua Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kinyume chake atafutwa kabisa uanachama.

Aidha, mkutano huo ulimpitisha Waziri wa zamani wa Michezo, Profesa Juma Kapuya, kuziba pengo la Ally Sykes katika Baraza la Wadhamini, huku Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Adam Mgoyi, akiteuliwa kuziba nafasi ya Kilomoni.    


Katika hatua nyingine, klabu ya Simba imetumia sh. bilioni 1.3, kwa ajili ya usajili wa kikosi cha Simba msimu huu.

Hayo yalisemwa na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah, katika mkutano uliofanyika jana.

Abdallah alisema wamesajili kikosi madhubuti kwa gharama kubwa, lengo likiwa ni kurejesha heshima ya klabu yao na kwamba, wachezaji wa kigeni pekee wamegharimu sh. milioni 679, zikiwemo sh. milioni 226, zilizotumika katika dirisha dogo, Desemba, mwaka jana.

YANGA YAPIGWA 1-0 NA RUVU SHOOTING


MABINGWA watetezi Yanga wamepigwa bao 1-0 na Ruvu Shooting katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Bao pekee la Ruvu Shooting lilitokana na uzembe wa beki Abdalla Haji 'Ninja' wa Yanga, kujifunga wakati akiwa katika harakati za kuokoa mpira kwenye lango la timu yake.

Mpira uliozaa bao hilo ulitokana na krosi iliyopigwa na Shalla Juma wa Ruvu Shooting, ambapo wakati Ninja akijaribu kuiokoa kwa kichwa, mpira ulielekea langoni na kumpita kipa Ramadhani Kabwili.

KARIA RAIS MPYA TFF, WAMBURA MAKAMU WAKE


WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wamemchagua Wallace Karia kuwa mwenyekiti mpya wa shirikisho hilo.

Katika uongozi uliopita, Karia alikuwa makamu wa rais chini ya Jamal Malinzi, anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha.

Karia alishinda wadhifa huo baada ya kuwabwaga Ally Mayay, Frederick Mwakalebela, Imani Madeha, Shija Richard na Emmanuel Kimbe.

Katika uchaguzi huo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa St. Gasper, Dodoma, Michael Wambura alichaguliwa kuwa makamu wa rais.

Wambura, ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT) na pia klabu ya Simba, aliwabwaga Mulamu Nghambi, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.

Wednesday, August 9, 2017

'SIMBA DAY' HAIJAPATA KUTOKEA, NIYONZIMA NA OKWI WALITEKA JIJI



SIMBA jana ilisherehekea vyema siku yake baada ya kuichapa Rayon Sports ya Rwanda bao 1-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo iliyohudhuriwa na maelfu ya mashabiki, wengi wakiwa wa Simba, ilitawaliwa na matukio mengi, likiwemo utambulisho wa wachezaji wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu huu wa ligi.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, ndiye aliyepewa jukumu la kuwatambulisha wachezaji hao mmoja baada ya mwingine, huku mashabiki wakilipuka mayowe ya kuwashangilia.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi na kipa wa zamani wa Azam, Aishi Manula, ndio walioongoza kwa kushangiliwa kwa mayowe mengi ya mashabiki hao.

Mbali na tukio hilo, mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Mohamed Dewji alipewa heshima ya kuzindua App ya klabu hiyo, ambayo itakuwa na habari zinazoihusu klabu hiyo.

Katika kuongeza shamrashamra, klabu hiyo pia ilitoa tuzo maalumu kwa nyota wa zamani wa timu hiyo, Abdalla Kibadeni, ambaye aliweka rekodi ya kutwaa mataji mbalimbali akiwa kocha na mchezaji.

Kabla ya kuanza kwa pambano hilo, timu hizo zilikaguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, January Makamba, aliyeongozana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Mchemba na Dewji.

Katika mechi hiyo, Simba ilionyesha kiwango kizuri katika safu zake zote tatu za ulinzi, kiungo na ushambuliaji, huku ikifanya mashambulizi mazuri na kwa mpangilio maalumu.

Bao pekee na la ushindi la Simba lilifungwa na mshambuliaji Mohamed Ibrahim, baada ya kupokea pasi maridhawa kutoka kwa Okwi.

USAJILI 2017/18 WAKAMILIKA, KANUNI ZASHUSHA TIMU MBILI

Usajili wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kwa msimu wa 2017/18, umekamilika kwa timu 62 tu na timu mbili zimeshindwa kufanya usajili.


Tayari toleo la awali (First Draft) la majina ya timu zote na namna zilivyosajili, tumebandika katika mbao za matangazo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Karume Dar es Salaam tangu jana kadhalika nimeunganisha (attach) usajili huo kwenye taarifa hii kwa vyombo vya habari kwa timu zote kwa kufuata alphabeti.


Kubandikwa huko na kusambaza kwenye vyombo vya habari kunalenga kuwapa fursa timu zote kukagua majina ya wachezaji wa kila timu ili kuona kama kuna klabu au mchezaji amefanya udanganyifu wa kusajili wa timu zaidi ya moja, ziweze kuona.


Kama kuna dosari hiyo, TFF imefungua milango ya kupokea pingamizi la usajili wa wachezaji hao kuanzia leo Agosti 8, 2017 hadi Jumatatu Agosti 14, mwaka huu saa 10.00 jioni (16h00).


Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji inatarajiwa kuwa na kikao ama Agosti 16 au 17, mwaka huu kupitia mapingamizi hayo pamoja na usajili wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Usajili wa timu za Daraja la Kwanza na Pili, utapitiwa baadaye mwezi huu.


Timu hizo 62 kati ya 64 zimefanya usajili na kuingiza majina ya wachezaji, viongozi wa benchi la ufundi kwenye mfumo wa mtandao wa TMS - Transfer Matching System.


Timu ambazo zimeshindwa kufanya hivyo yaani usajili kwa mfumo wa TMS ni za Ligi Daraja la Pili (SDL) ambazo ni Pepsi ya Arusha na Bulyanhulu ya Shinyanga.
 

Na kwa msingi huo, timu hizo za Pepsi na Bulyanhulu zimejitoa kushiriki ligi kwa msimu wa 2017/18 na zinashushwa daraja hadi ligi ya wilaya kuanza upya kutafuta nafasi za juu kupanda daraja.

KAMPENI UCHAGUZI TFF ZAENDELEA, WALIOKATWA WAREJESHWA



Kampeni za wagombea mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika shirikisho, zinaendelea.
 

Kwa mujibu wa kanuni 11.10 ya uchagizi wa TFF, kampeni hizo za wiki moja hadi Ijumaa wiki hii ambako Uchaguzi Mkuu utafanyika Agosti 12, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Hosteli ya Mtakatifu Gasper mjini Dodoma.
 

Kwa mujibu wa kamati hiyo iliyokutana Jumamosi Agosti 5 2017, wagombea ambao wanawania urais ni pamoja na  Wallace Karia, Imani Madega, Fredrick Mwakalebela, Ally Mayay, Shija Richard na Emmanuel Kimbe.
 

Katika nafasi ya Makamu wa Rais wanaowania ni Mulamu Ng’hambi, Michael Wambura, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.

 Kanda namba 1 ya Mikoa ya Kagera na Geita: waliopitishwa ni Saloum Chama, Leopold Mukebezi na Kaliro Samson wakati Kanda namba 2 inayounganisha mikoa ya Mara na Mwanza wamo Aaron Nyanda, Vedastus Lufano, Samwel Daniel na Ephraim Majinge.
 

Kanda namba 3 (Mikoa ya Shinyanga na Simiyu) wanaowania nafasi hiyo ni Stanslaus Nyongo, Bannista Rogora na Mbasha Matutu ilihali Kanda namba 4 (Mikoa ya Arusha na Manyara) waliopitishwa ni Omar Walii, Sarah Chao na Peter Temu.
 

Katika Kanda namba 5 inayounganisha mikoa ya Kigoma na Tabora waliopitishwa ni John Kadutu, Issa Bukuku, Abubakar Zebo na Francis Michael wakati Kenneth Pesambili na Baraka Mazengo – wote wamepitishwa kuwania ujumbe kupitia Kanda namba 6 yenye mikoa ya Katavi na Rukwa.
 

Kanda namba 7 inayounganisha mikoa ya Mbeya na Iringa waliopitishwa ni Elias Mwanjala, Cyprian Kuyava na Erick Ambakisye huku Kanda namba 8 yenye mikoa ya Njombe na Ruvuma waliopitishwa ni James Mhagama, Golden Sanga, Vicent Majili na Yono Kevela.
 

Kanda namba 9 Lindi na Mtwara Athumani Kambi na Dunstan Mkundi (wamepitishwa) wakati Kanda namba 10 Dodoma na Singida waliopitishwa ni Hussein Mwamba, Steward Masima, Ally Suru na George Komba.
 

Kanda namba 11, mikoa ya Pwani na Morogoro waliopitishwa ni Charles Mwakambaya, Gabriel Mkwawe na Francis Ndulane wakati Kanda namba 12 Kilimanjaro na Tanga waliopitishwa ni Khalid Mohamed na Godluck Moshi.
 

Kanda namba 13 Dar es Salaam: waliopitishwa ni Emmanuel Kazimoto, Abdul Sauko, Ayoub Nyenzi, Shaffi Dauda, Peter Mhinzi, Lameck Nyambaya, Mussa Kissoky, Said Tully, Ally Kamtande, Aziz Khalfan, Ramadhani Nassib na Saad Kawemba.
 

Hii sasa ni orodha ya mwisho baada ya baadhi ya wagombea kufanikiwa kushinda rufaa zao katika Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wakipinga kuondolewa na Kamati ya Uchaguzi.
 

Kamati ya Uchaguzi ilipokea taarifa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kueleza kuwa iliwakamata viongozi wa soka kutoka mikoa mbalimbali katika mazingira ya kuvunja sheria za nchi na kanuni za uchaguzi.
 

Kamati iliamua kuwaondoa wagombea hao ambao ni Shafii Dauda wa Dar es Salaam; Banista Rugora wa Shinyanga; Ephraim Majinge wa Mara na Elias Mwanjala wa Mbeya katika kuwania nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi ujao wa TFF unatarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu kwa ukikwaji wa Kanuni ya 14 (3) inayozungumzia kampeni kabla ya wakati.

MAJIBU KAMATI YA RUFAA ZA UCHAGUZI

Kamati ya Rufaa za Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania pia imetoa matokeo ya rufaa nne ilizosikiliza Jumamosi Agosti 5, 2017 zilizokatwa dhidi ya Kamati ya Uchaguzi katika mchakato wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya TFF.

Waliokata Rufaa ni Fredrick Masolwa ambaye awali hakupitishwa kuwania nafasi ya urais kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa kanuni ya 9 (3) ya kanuni za uchaguzi za TFF. Kamati ya Rufaa ilitupilia mbali hoja hiyo kwa sababu ya rufaa kukosa kigezo cha kutolipia kwa mujibu wa katiba ya TFF.
 

Mwingine ni Mgombea Ujumbe wa Kamati ya Utendaji Kanda namba 7 (Mikoa ya Mbeya na Iringa), Abdusuphyan Sillah awali hakupitishwa kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa kanuni ya 9 (3) ya kanuni za uchaguzi za TFF.
 

Rufaa yake ilikuwa na vigezo, lakini ilikosa hoja za uadilifu kwa mujibu wa Kanuni ya 9 (7) kwani mrufani alikosa uadilifu kwa kutoa taarifa za uongo mbele ya kamati.
 

Kanda namba 11 (Mikoa ya Pwani na Morogoro), Hassan Othuman awali hajapitishwa kwa kukosa uadilifu jambo ambalo alilikatia rufaa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF. Hata hivyo, alituma ujumbe mbele ya Kamati ya Rufaa akitangaza kujitoa.
 

Kanda namba 13 Dar es Salaam: Saleh Abdallah awali hakupitishwa kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa kanuni ya 9 (3) ya kanuni za uchaguzi za TFF. Kamati ilitupilia mbali rufaa yake kwa sababu kwanza hakulipia hivyo kukosa vigezo pia hata mrufani mwenyewe hakutokea kutetea rufaa yake.

Monday, August 7, 2017

NIYONZIMA AANZA RASMI MAZOEZI SIMBA

MSHAMBULIAJI mpya wa klabu ya Simba, Haruna Niyonzima (kushoto) akizungumza na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog wakati wa mazoezi yaliyofanyika leo kwenye uwanja wa Bunju, ulioko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.