KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 30, 2015

NYOSO AFUNGIWA KUCHEZA SOKA MIAKA MIWILI, ATOZWA FAINI SH. MILIONI MBILI


Kamati ya masaa 72 ya uendeshaji wa Ligi Kuu iliyokutana leo kupitia ripoti mbalimbali za michezo iliyochezwa ya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza nchini imemfungia mchezji Juma Nyoso wa timu ya Mbeya City kucheza mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka miwili na faini ya shilingi milioni mbili (2,000,000) kufutia kitendo cha udhalilishaji alichomfanyia mchezaji wa Azam FC John Bocco.

Nyoso alifanya kitendo hicho katika mchezo no namba 32 wa VPL kati ya Azam FC na Mbeya City uliofanyika kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, kutokana na kuwa tabia ya kufanya vitendo hivyo vya utovu wa nidhamu mara kwa mara kwenye michezo ya Ligi Kuu.

Klabu ya Young Africans imepigwa faini ya shiligi laki tano (500,000) kufutia wachezaji wake watano kuonyeshwa kadi za njano katika mchezo dhidi ya Simba SC. Kwa mujibu wa kanunu namba 42 (11) timu ambayo wachezaji wake watapata kadi zaidi ya tabo katika mchezo mmoja itapigwa faini ya shilingi laki tano.

Wachezaji waliopata kadi za njano wa Young Africans katika mchezo huo ni ni Salum Telela, Mbuyu Twite, Malimi Busungu, Ali Mustafa na Mbuyu Twite.

Aidha klabu ya Yanga imepigwa faini nyingine ya shilingi laki tano (500,000) kufutia wachezaji wake kwenda kushangilia upande wa Simba SC mara baada ya mchezo kumalizika.

Mchezo utatazamwa tena ili kuangalia malalamiko ya Simba SC dhidi ya mwamuzi.

Simba pia inapigwa faini baada ya wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kuwashambulia waamuzi baada ya mchezo ambapo waliwarushia chupa za maji ambazo nyingine ziliwakosa waamuzi na kumpata kocha wa Yanga Hans Van Pluijm.

Mchezo namba 26 wa VPL kati ya Coastal Union na Mwadui uliofanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Chumba cha Coastal Union kilikuwa na harufu kali sana. Baadhi ya mashabiki wa Coastal Union waliokuwa nyuma ya goli la upande wa kaskazini walitoa  lugha ya matusi kwa waamuzi na kutishia kuwapiga na pia walimrushia mawe mwamuzi msaidizi wa pili Shafii Mohamed na jiwe moja lilimpiga mgongoni na kumjeruhi kidogo mwamuzi na aliomba msaada wa jeshi la polisi kutuliza ghasia, mchezo ulisimama kwa dakika 3.

Kwa mujibu wa kanuni namba 42 (1) ya udhibiti wa wachezaji Coastal Union itatozwa faini ya Tsh 500,000/=

Mchezo namba 22 wa VPL kati ya Mtibwa Sugar na Ndanda uliofanyika kwenye uwanja wa Manungu, Turiani. Ndanda hawakuleta watu wa kutosha kwenye pre match meeting hivyo wanapigwa faini ya shilingi laki mbili (200,000/=)

Mchezo namba 23 wa VPL kati ya Simba SC na Kagera Sugar uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa, Dar es salaam. Simba walikuwa na wajumbe watatu na Kagera Sugar walikuwa na mtu mmoja tu tena hakuja na vifaa. Timu zote zimepigwa faini ya shilingi laki mbili (200,000).

Mchezo namba 17 wa VPL kati ya Stand united na African Sports kocha wa Stand United alitolewa nje ya eneo la ufundi kwa kutoheshimu taratibu za eneo hilo na pia alikataa kuongea na vyombo vya habari kwa hiyo kwa mujibu wa kanuni namba 40 (11) anafungiwa kukaa kwenye benchi la ufundi kwa mechi mbili na faini ya sh 500,000/= kwa kila kosa jumla 1,000,000/=.

Friends Rangers na KMC Mechi Na 8 Kundi A iliyofanyika uwanja wa Karume 27.9.2015. Timu ya KMC ya kinondoni ilifanya mabadiliko kwa kuingiza wachezaji 4 ambao ni kinyume cha kanuni. Kwa mujibu wa taarifa ya mwamuzi wachezaji waliofanyiwa mabadiliko ni

i. Frank Mashoto badala ya Kudra Omari

ii. Kamongo Morris badala ya Mrisho Simon

iii. Mfanyeje Musa badala ya Kabange Mgunda na

iv. Sultani Kasiras badala ya Adam Said

Kwa mujibu wa kanuni namba 14 (25) KMC imepoteza mechi na kupigwa faini ya Tsh 200,000/=. Mwamuzi wa akiba anafutwa kuchezesha ligi msimu huu na mwamuzi wa kati anapewa onyo.

KIKOSI CHA U-15 CHAENDA TANGA KUJIPIMA NGUVUKikosi cha Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U15) kinatarajiwa kusafiri kesho Jumatano kuelekea jijini Tanga kwa ajili ya mchezo wa kirafiki na kombani ya U15 ya jijini humo.

U15 ambayo iliingia kambini siku ya Ijumaa katika hosteli za TFF zilizopo Karume imekua ikifanya mazoezi asubuhi na jioni katika uwanja wa Karume kujiandaa na michezo hiyo ya kirafiki itakayofanyika siku ya Alhamis na Ijumaa.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Sebastian Nkoma anatarajiwa kutumia michezo hiyo ya kirafiki jijni Tanga kuona maendeleo ya vijana wake na kupata kung’amua vipaji vingine atakavyoviona katika mchezo kwa ajili ya kuboresha kikosi chake.

Program hiyo ya vijana ilianza mwezi Juni mwaka huu ambapo kila mwisho wa mwezi, wachezaji hao hukutana jijini Dar es salaam kwa ajili ya kambi kabla ya kusafiri mikoani kucheza michezo ya kirafiki.

Mpaka sasa kikosi hicho cha vijana wenye umri chini ya miaka 15 kimecheza michezo ya kirafiki na kushinda michezo yote katika mikoa ya Mbeya, Zanzibar, na kutoka sare na kombaini ya Morogoro.

Wachezaji waliopo kambini wanaotarajiwa kusafiri kesho ni Josephat Mbokiwe, Anthony Shilole, Kelvin Deogratius, Maziku Amede, Hamis Juma, David Julius, Kibwana Ally, Mohamed Ally, Ibrahim Ramadhan, Frank George, Maulid Salum.

Wengine ni Faraji John, Athuman Maulid, Mwinjuma Abdallah, Alex Peter, Ibrahim Abdallah, Rashid Kilongora, Casto Issa, Ally Hussein, Jama Idd, Asad Ally na Issa Abdi.

SIMBA, YANGA MAJARIBUNI TENA LEO


Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara inatarajiwa kuendelea leo Jumatano kwa timu 14 kucheza katika viwanja saba nchini, ikiwa ni raundi ya tano ya ligi hiyo iliyoanza kutimua vumbi Septemba 12, 2015.

Simba SC watakua wenyeji wa Stand United katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Azam FC watawakaribisha Coastal Union kwenye uwanja wa Azam Complex – Chamazi jijini Dar es salaam.

Mjini Morogoro vinara wa ligi hiyo Young Africans watakua ugenini kuwakabili wenyeji Mtibwa Sugar ambapo timu zote zikiwa na alama 12 baada ya kucheza michezo minne zikipishana kwa tofauti ya magoli, Wana Lizombe Majimaji FC watakua wenyeji wa Ndanda FC kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Wakata Miwa wa Kagera Sugar watawakaribisha maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, African Sports wakiwakaribisha wa Mgambo Shooting uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Tanzania Prisons wakiwa wenyeji wa Mwadui FC katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Ligi hiyo ya Vodacom itaendelea siku ya Alhamis kwa mchezo mmoja ambapo Toto Africans watakuwa wenyeji wa Mbeya City katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Monday, September 28, 2015

DIAMOND APASUA JIPU SAKATA LA MWANAWENA NASRA KITANA

WATANZANIA wengi walikuwa wanaisubiri siku maalumu ambayo staa wa muziki nchini na Afrika, Nassib Abdul 'Diamond Platinum' ataweka hadharani sura ya mtoto wake.

Pia wapenzi wa burudani walikuwa na shauku ya kuona sura ya mtoto huyo ambaye alizua gumzo tangu mama yake Zarina Hassan 'Zari The Boss Lady' akiwa mjamzito.

Shauku hiyo iliongezwa kasi baada ya kuenea tetesi kuwa Diamond alibambikiwa ujauzito huo lakini yeye hakujali na aliendelea na maandalizi ya kumpokea mwanawe mtarajiwa.

Baada ya mtoto wa kike kuzaliwa, yaliibuka maneno lukuki kuwa si mwanawe na baadhi ya wadau walitaka apimwe vinasaba (DNA) ili kupata ukweli.

Septemba 20, mwaka huu mtoto wa mastaa hao alipewa jina la Latiffah 'Tiffah', alitimiza siku 40 na nyota hao waliamua kufanya sherehe kamambe ya kumkaribisha rasmi duniani.

Sherehe hiyo iliyojumuisha nyota mbalimbali wakiwemo wa filamu, ilifanyika nyumbani kwake Madale-Tegeta, Dar es Salaam.

Diamond na Zari wamezishawishi baadhi ya kampuni kubwa za biashara kuingia mkataba wa malipo kutumia jina na picha za Tiffah kibiashara.

Tayari kinda huyo ni balozi wa maduka ya nguo za watoto Dar es salaam na pia picha yake ya kwanza ilioneshwa hadharani ikiambatana na udhamini wa benki ya NMB.

Diamond anasema mtoto wake Tiffah ni 'photocopy' ya sura yake na anashukuru mtoto huyo amefuata rangi ya urembo wa mama yake.

Anasema anashukuru Mungu kupata mtoto ambaye ilikuwa ndoto ambapo ameahidi kumtunza na kumpa malezi bora katika maadili ya Afrika.

"Kwanza nimefurahi kwa sababu mtoto ni kopi yangu kabisa huwezi kukataa na wale waliokuwa wanadai kwamba nimesingiziwa nadhani wamethibitisha hilo baada ya kuona piacha zake,"alisema Diamond.

“Unajua mtoto kama si wako ni rahisi tu kujua. Na unajua mzazi anakuwa mtu wa kwanza kugundua kama mtoto si wako.

Kuhusu kauli zinazoenezwa kuwa mtoto huyo si wake, Diamond, anasema wabaya wake wamekuwa wakimfuatilia muda mrefu lakini wameshindwa.

“Mimi nasema jamani nyinyi mnadai mna hela, matajiri mmeshamwacha mwanamke mbona mmekuwa mnafuatilia.Fanyeni shughuli zingine, tafuteni wanawake wengine wazuri zaidi yake mfanye vitu vingine," anasema Diamond.

Mwimbaji huyo anasema matarajio yao ni kupata mtoto wa pili ambaye atazaa na Zari baada ya mtoto wao Tiffah 'kuchangamka'.

Akizungumzia mustakabali wa maisha yao, Diamond, anasema wanatarajia kufunga ndoa hivi karibuni kwa sababu hakuna kikwazo baina yao.

WASANII KIBAO KUKAMUA TAMASHA LA AMANI TAIFA

UPENDO Nkone
ROSE Muhando


NA MWANDISHI WETU

MACHO na masikio ya Watanzania yanatarajiwa kuelekezwa katika tamasha kamambe la kuombea amani ambalo limepangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Tamasha hilo ni maalumu kwa ajili ya kuwaombea amani Watanzania wanaotarajia kupiga kura za kumchagua rais wa awamu ya tano, wabunge na madiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo litakalofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pia waimbaji mbalimbali maarufu kutoka Afrika watanogesha tamasha hilo kupitia vipaji vyao vya kuimba nyimbo za kumsifu Mungu.

Ingawa mfumo wa vyama vingi ulianza mwaka 1992, lakini uchaguzi wa Oktoba 25 una mvuto wa aina yake, hivyo tamasha hilo linafanyika katika muda mwafaka.

Tanzania inafanya uchaguzi wake wa tano ukitanguliwa na uchaguzi wa mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 ambao ulimuweka Rais Kikwete madarakani.

Kampuni ya Msama Promotions imeandaa tamasha hilo ili kuomba uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu ili kulinda maslahi ya Taifa na mali za Watanzania.

Tamasha hilo linatarajia kufanyika katika mikoa 10 ya Tanzania Bara ikiwemo Morogoro, Iringa, Mbeya, Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga.

Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, anasema tamasha hilo lina lengo la kuwaleta pamoja Watanzania kuombea amani nchi yao katika kipindi cha uchaguzi mkuu.

"Kutokana na umuhimu wa amani kampuni ya Msama Promotins inayoratibu matamasha ya muziki wa injili wakati wa Pasaka na Krismasi kila mwaka, tumeona ni vyema kuandaa tamasha hili kusisitiza amani kwa kila Mtanzania," anasema Msama.

Anasema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika na amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi ili kumuunga mkono Rais Kikwete ambaye amekuwa mstari wa mbele kusisitiza amani.

Msama anadokeza kuwa tamasha la mwaka huu litakuwa na ujumbe “Tanzania ni ya Kwetu, Tuilinde na Kuitunza Amani Yetu.’

Anasema mustakabali wa amani ya nchi iko mikononi mwa Watanzania na kila mmoja ana wajibu wa kuilinda kwa nguvu zote ili kuepuka vurugu zinazoendelea katika baadhi ya nchi duniani.

Juhudi hizi za kusisitiza amani na utulivu wa nchi hasa katika kipindi  cha uchaguzi, kinapaswa kuungwa mkono na kila mmoja kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu.

Anasema waimbaji wa nyimbo za injili wa nafasi kubwa ya kutoa mchango wao kupitia tungo za nyimbo zao zenye kujenga na kudumisha amani ya nchi.

"Waimbaji wana fursa nzuri ya kutoa mchango wao kupitia neno la Mungu, naomba Watanzania wote bila kujadili itikadi za nyama kujitokeza kwa wingi katika tamasha hili,"anasema Msama.

Mkurugenzi huyo ametoa rai kwa wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi kupiga kura kwa amani ili kulinda umoja na mshikamano wa Watanzania.

Viongozi mbalimbali wamepongeza uwepo wa tamasha hilo kwa kuwa linaitakia mema Tanzania ambapo iko katika harakati za kuchagua viongozi ambao watakaa madarakani kwa miaka mitano ijayo.

Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo kwa kuwa lina maslahi makubwa kwa Taifa.

“Viongozi wa dini ni watu muhimu katika jamii na Taifa kwa ujumla, wao ndio mwongozo wetu bila kuwapo wao sijui Tanzania yetu ingekuwaje”, anasema Azzan.

Waimbaji mashuhuri kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Zambia, Jamhuri ya Congo na Afrika Kusini, wanatarajia 'kuchuana' vikali na wenzao wa Tanzania katika tamasha hilo.

Mwimbaji nguli wa muziki wa injili mwenye maskani yake Uingereza, Ifeanyi Kelechi, anatarajia kukonga nyoyo za Watanzania katika tamasha hilo.

Baadhi ya waimbaji watakaopanda jukwaani kutoka nje ni Anastazia Mukabwa (Kenya), Sipho Makhabane, Glorius Celebrations ‘Kwetu Pazuri’, Ephraim Sekeleti, Solomon Mukubwa na Sara K.

Kwa upande wa waimbaji wa Tanzania ni John Lissu, Boniface Mwaitege, Martha Mwaipaja, Beatrice Mwaipaja, Rose Muhando, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Joshua Mlelwa na Christopher Mwahangila.

Sunday, September 27, 2015

K-ONE AIBUKA NA NGOMA NYINGINE MPYA KALI


Na Mwandishi Wetu

BAADA ya ukimya wa muda mrefu, hatimaye msanii nyota na chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini, Karim Othman ameibuka na kibao kingine kipya.

Kibao hicho kinachokwenda kwa jina la Nilikuchora, kimerekodiwa kwenye studio za Truck Music zilizoko Mbagala, Dar es Salaam, chini ya usimamizi wa prodyuza Rise Clever.

Akizungumza na Dawati la Michezo la Uhuru, mjini Dar es Salaam jana, Karim, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la K-One, alisema video ya wimbo huo imetengenezwa na Fadhili Ngoma.

Alisema video hiyo ni ya kwanza kuitoa akiwa msanii wa kujitegemea, baada ya mkataba wake na kampuni ya Baucha Records kumalizika tangu mwaka jana.

Awali, K-One aling'ara kwa kibao chake kinachojulikana kwa jina la Yule, ambacho alikirekodi kwa kushirikiana na Maunda Zorro. Alirekodi kibao hicho kwa usimamizi wa Baucha Records.

Kibao hicho ambacho kimepigwa katika miondoko ya zouk, kilitamba katika vituo mbalimbali vya televisheni pamoja na kupigwa kwenye vituo vya radio nchini.

K-One alisema baada ya kibao cha Nilikuchora, ambacho kinatarajiwa kuanza kupigwa kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni hivi karibuni, amejipanga kurekodi kibao kingine kitakachojulikana kwa jina la Sijadili mapenzi.

Mbali na vibao hivyo vitatu, K-One pia amewahi kurekodi vibao vingine kadhaa, kikiwemo Ngoja niseme, alichomshirikisha mkongwe wa muziki wa kizazi kipya nchini, Chege Chigunda.

Vibao vingine vya msanii huyo machachari ni Dhahabu alichomshirikisha Ali Kiba, Niwaambie alichorekodi na Madee, Muelewe alichoimba na Tundaman, Bora alichomshirikisha Top C, Weekend Special alichompa shavu Baker na Sina hakika.

Hata hivyo, K-One alishindwa kutoa video za nyimbo hizo kutokana na kukosa mdhamini baada ya mkataba wake na Baucha Records kumalizika.

“Namshukuru Mungu kwamba vibao vyangu vyote hadi sasa ni moto wa kuotea mbali, kinachonikwamisha ni kukosa wadhamini kwa ajili ya kutengeneza video,"alisema.

Licha ya kushindwa kuongeza mkataba na Baucha Records, K-One amemshukuru mmiliki wa studio hiyo, Ally Baucha kwa kumruhusu kutumia nembo yake kwa kipindi cha miaka miwili waliyokuwa pamoja.

Ameitaja sababu kubwa iliyomfanya ajitoe katika udhamini wa Baucha Records kuwa ni kushindwa kutoa albamu kama walivyokuwa wamekubaliana kwenye mkataba kati yao.

Kwa mujibu wa K-One, amerekodi zaidi ya nyimbo 12 katika studio za Baucha, lakini hadi sasa ameshindwa kumtolea albamu.

"Nimesikitishwa sana na hali hii, ndio sababu niliamua kutosaini mkataba mwingine na Baucha Records kwa sababu sioni faida yoyote ya kuendelea kufanyakazi chini yake,"alisema K-One.

Msanii huyo aliyetengeneza nywele zake kwa mtindo wa rasta, alisema licha ya wimbo wake wa kwanza wa Yule, kumpatia sifa na umaarufu mkubwa na pia kukubalika kwa mashabiki, Baucha hakuweza kuzisambaza nyimbo zake nyingine kwenye vituo vya redio na televisheni.

"Nyimbo zangu nyingine nazo ni kali sana. Fikiria nimerekodi na Ali Kiba, Chege, Tundaman, Madee, Top C na Becka Suspender, lakini nyimbo zote bado zipo kabatini," alilalamika msanii huyo, ambaye pia ni mtaalamu wa mambo ya kompyuta.

K-One alisema haelewi ni kipi kilichomsibu Baucha na kumfanya ashindwe kutimiza makubaliano yao kwa vitendo, hali inayomfanya ajione mnyonge kwa sababu wasanii wenzake wengi wamekuwa wakimkubali kutokana na kazi zake.

Mbali na kushindwa kusambaza kazi zake kwenye vituo vya redio na televisheni, K-One alisema Baucha alishindwa kumwandalia maonyesho ya muziki kwa ajili ya kutangaza kazi zake.

Alisema kwa sasa yupo huru kwa vile hafungwi na mkataba wa Baucha Records na kwamba ameshaanza mikakati ya kumsaka meneja mpya kwa ajili ya kusimamia kazi zake.

"Ni kweli Baucha alikuwa na mipango mizuri ya kuniendeleza, lakini sielewi ni kipi kilichomsibu. Labda mambo yake hayakuwa mazuri, huwezi kujua, maana siku zote alikuwa akinipa ahadi za subiri kidogo,"alisema.

Hata hivyo, alimshukuru Baucha kwa kuishi naye kama mdogo wake na kumsaidia katika mambo mengi madogo madogo.

"Namshukuru sana Baucha kwa sababu amenisaidia kwa mambo mengi. Tatizo pekee ni kwamba nimeshindwa kutimiza ndoto zangu chini yake,"alisema K-One.

"Lengo langu ni kuwa msanii bora. Nahitaji kuwa na meneja aliye makini na mwenye malengo makubwa zaidi kwa sababu uwezo nilionao kiusanii ni mkubwa,"aliongeza.

K-One alianza kuchomoza kimuziki baada ya kuibuka na vibao vyake viwili vya mwanzo, vinavyojulikana kwa majina ya Bila wewe na Sema baby, alivyorekodi na Ney wa Mitego na Pasha. Alirekodi vibao hivyo katika studio za Brain Trust, zilizoko Temeke, Dar es Salaam kwa udhamini wa dada yake.

Mbali na kurekodi vibao hivyo, K-One pia alikuwa akishirikishwa kuimba viitikio katika nyimbo za wasanii mbali mbali maarufu wa muziki hao. Baadhi ya wasanii hao ni JB wa kundi la Mabaga Fresh na Mood Kibra.

Vibao vingine vya awali vya K-One ni pamoja na Valentine, Kwa nini, Mpenzi sasa why na Fau.

K-One amewaomba mapromota wa muziki wa kizazi kipya kujitokeza kumsaidia kurekodi albamu yake kwa vile anazo nyimbo za kutosha, zikiwa tayari zimesharekodiwa. Amewahakikishia mapromota hao kwamba hawatajutia kutumia fedha zao kwa kazi hiyo.

Ametoa wito kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, wapendane, kusaidiana na kuaminiana ili waweze kupiga hatua za juu zaidi kimaendeleo.

Amesema miongoni mwa sababu zinazochangia kuwakwamisha wasanii chipukizi wa muziki huo, ni kutokuwepo kwa umoja miongoni mwao, kuchukiana na kutosaidiana.

“Wasanii walio juu wanapaswa kukumbuka kuwa kabla ya kufika huko waliko hivi sasa, nao walianzia chini, hivyo wasikwepe kuwasaidia wenzao wanaohitaji msaada kutoka kwao, hata kama wa kurekodi pamoja,”alisema.


Saturday, September 26, 2015

KING MAJUTO, SUNDAY MANARA WAKUTANA MAKKA

MSANII nyota wa filamu na maigizo nchini, Amri Athumani 'King Majuto' akiwa na mwanasoka nyota wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars, Sunday Manara walipokutana katika mji wa Makka wakati wa ibada ya Hijja.

YANGA WAIZIBA MDOMO SIMBA, TAMBWE, BUSUNGU WAPELEKA KILIO MSIMBAZI


MSHAMBULIAJI Malimi Busungu leo amekuwa shujaa baada ya kutoa pasi ya bao na kufunga Yanga SC ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Malimi aliyesajiliwa kutoka Mgambo JKT ya Tanga msimu huu, alimpa pasi Amissi Joselyn Tambwe kufunga baada ya kutokea benchi kipindi cha kwanza- kabla ya yeye mwenyewe kufunga la pili kipindi cha pili.
Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliochezeshwa na refa wa FIFA, Israel Nkongo, hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Tambwe.
Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 44 kwa ustadi mkubwa, akigeuka baada ya pasi ya Malimi Busungu aliyepokea krosi ya Haruna Niyonzima na kumchambua kipa Peter Manyika.
Pamoja na kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa wanaongoza, Yanga SC hawakucheza vizuri kipindi cha kwanza na walikoswa mabao mawili ya wazi.
Simba SC walitawala mchezo kipindi cha kwanza na kuwafanya Yanga SC wapoteane kabisa uwanjani, kiasi cha kucheza kwa kujihami muda mrefu zaidi.
Dakika ya kwanza tu, Mwinyi Kazimoto alitia krosi maridadi, lakini mshambuliaji Hamisi Kiiza ‘Diego’ akachelewa na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ akadaka.
Beki Mkongo wa Yanga SC, Mbuyu Twite alifanya kazi nzuri dakika ya tano, baada ya kuokoa krosi nzuri ya beki wa kulia wa Simba SC, Hassan Kessy.
Dakika ya tisa, Nahodha wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi alishindwa kumalizia kazi nzuri ya kiungo Mwinyi Kazimoto na dakika ya 24 Kiiza alifumua shuti kali baada ya pasi ya Said Ndemla na Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akaokoa
Shambulizi la kwanza la maana la Yanga SC lilikuja dakika ya 41, baada ya Tambwe kupiga shuti lililokwenda nje akiwa kwenye nafasi nzuri.
Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm alimtoa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, Simon Msuva dakika ya 34 na kumuingiza Malimi Busungu aliyekwenda kuongeza uhai katika safu ya ushambuliaji ya Yanga SC
Kipindi cha pili Yanga SC walibadilika na kuanza kushambulia moja kwa moja, huku Simba SC nao wakiendelea kuzuia na kusaka bao la pili.
Lakini ni nyota ya vijana wa Jangwani iliyoendelea kung’ara baada ya kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 79 kupitia kwa Busungu aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twite.
Baada ya bao hilo, Simba SC walipoteana na kuwaacha Yanga SC kutawala zaidi mchezo.
Kuingia kwa mshambuliaji Msenegali, Pape Abdoulaye N’daw kidogo kuliipa uhai safu ya ushambuliaji ya Simba SC na kuanza kufika langoni mwa Yanga SC, ingawa hawakufanikiwa kupata bao.
Refa Nkongo alimuonyesha kadi ya pili ya njano Mbuyu Twite dakika ya 90+2 kwa kujichelewesha kurusha mpira na Simba SC walitumia dakika hizo za majeruhi kufanya shambulizi moja la maana langoni mwa Yanga SC.
Ushindi huo, unaifanya Yanga SC ijinafasi kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikitimiza pointi 12 baada ya mechi nne, wakati Simba SC inaanza kuporomoka.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi Kazimoto, Kevin Yondan, Thabani Kamusoko, Simon Msuva/Malimi Busungu dk34, Salum Telela/Said Juma ‘Makapu’ dk82, Amissi Tambwe/Deus Kaseke dk87, Donald Ngoma na Haruna Niyonzima.
Simba SC;Peter Manyika, Hassan Kessy/Pape Abdoulaye N’daw dk84, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Justice Majabvi, Awadh Juma, Said Ndemla, Hamisi Kiiza, Mwinyi Kazimoto na Mussa Hassan Mgosi/Ibrahim Hajib dk62.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

TANZANIA MWENYEJI WA KOZI YA KIMATAIFA YA WAAMUZI


Jumla ya waamuzi chipukizi 29 wasiokua na beji za FIFA kutoka nchi 28 barani Afrika wanatarajiwa kuhudhuria kozi ya waamuzi inayoandaliwa na FIFA kwa kushirikiana na CAF itakayofanyika kuanzia kesho Jumamosi tarehe 26 –30 Septemba mwaka huu jijini Dra es salaam.

Kozi hiyo itaendeshwa na wakufunzi kutoka katika nchi za Afrika Kusini, Malawi, Misri na Mauritius itafanyika katika hoteli ya Holiday Inn iliyopo jijini Dar es salaam ambapo waamuzi chipukizi kutoka Tanzania watakohudhuria ni Abdallah Kambuzi (Shinyanga) na Shomari Lawi (Kigoma).

Lengo la kozi hiyo ni kuwaanda waamuzi wanaochipukia ili baadae kuweza kuwa waamuzi wa FIFA ambao watatumika kwa michuano mbalimbali.

TFF YATUMA RAMBIRAMBI BAKWATA


Rais wa Shrikisho la Mpira wa Migu nchini (TFF), Jamal Malinzi ametuma salam za rambirambi kwa Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubeiry kufuatia vifo vya mahujaji zaidi ya 700 vilivyotokea Maka wakati wa kuhiji.

Katika salam zake kwenda kwa mufti mkuu, Malinzi amewapa pole waislam wote duniani kufuatia vifo vya mahujaji hao zaidi ya 700 vilivyotokea juzi na majeruhi zaidi ya 400 wakati wa ibada ya hija.

Malinzi amesema kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini TFF inawapa pole wafiwa wote, ndugu jamaa na marafiki na kuwatakia majeruhi afya njema na kusema ipo pamoja nao katika kipindi hichi kigumu cha maombelezo.

Wednesday, September 23, 2015

KUZIONA SIMBA NA YANGA BUKU SABA


Viingilio vya mchezo wa watani wa jadi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania utakaochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam vimetangazwa leo ambapo kiingilio cha chini kitakua ni shilingi elfu saba (7,000).

Katika mchezo huo kiingilio cha juu kitakua ni shilingi Elfu Thelathini (30,000) kwa viti vya VIP A, Elfu Ishirini (20,000) kwa viti vya VIP B & C, huku kiingilio cha shilingi Elfu Saba (7,000) kikiwa ni kwa viti vyenye rangi ya Blu, Kijani na Orange.

Tiketi za mchezo ho zitaanza kuuzwa siku ya Ijumaa saa 2 kamili asubuhi katika vituo vifuatavyo: Karume – Ofisi za TFF, Buguruni – Oilcom, Dar Live – Mbagala, Uwanja wa Taifa, Luther House – Posta, Ferry – Kivukoni, Mnazi Mmoja, Ubungo – Oilcom na Makumbusho – Standi ya mabasi ya daladala.

TFF inawaomba wapenzi, wadau na washabiki wa mpira wa miguu nchin kununua tiketi katika magari yaliyopo kwenye vituo vya kuuzia tiketi ili kuondokana na kuuziwa tiketi zisizo sahihi.

Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi wa kimataifa mwenye beji ya FIFA, Israel Nkongo (Dsm) akisaidiwa na Josephat Bulali (Tanga), Ferdinand Chacha (Mwanza) mwamuzi wa akiba Soud Lila (Dsm) wakati kamisaa wa mchezo huo atakua Charles Mchau kutoka Kilimanjaro.

Michezo mingine ya Ligi Kuu ya Vodacom siku hiyo ya Jumamosi itakua ni kati ya Coastal Union dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Maafande wa jeshi la Magereza (Tanzania Prisons) watawakaribisha maafande wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Maafande wa JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Stand United katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, huku wakata miwa wa Turiani Mtibwa Sugar watawakaribisha Majimjaji ya Songea katika uwanja wa Manungu wakati Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Toto Africans katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Ligi hiyo itaendelea siku ya Jumapili kwa michezo miwili ambapo waoka mikate wa Azam FC watawakaribisha Mbeya City katika uwanja wa Chamazi Complex, huku African Sports wakiwa wenyeji wa Ndanda FC kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

TWIGA STARS KUJIPIMA NA MALAWI


Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya Wanawake ya Malawi tarehe 24 Oktoba, mwaka huu nchini Malawi.

Mechi hiyo kati ya Twiga Stars dhidi ya Malawi itachezwa jijini Lilongwe kufuatia mwaliko wa chama cha soka nchini Malawi (FAM) kuialika Twiga Stars kwenda nchini Malawi kwa ajili ya mchezo huo

Mchezo huo wa kirafiki ni sehemu ya maandalizi ya vikosi vya timu zote mbili za Wanawake Tanzania na Malawi kwa ajili ya michuano mbalimbali.

MALINZI AFUNGA KOZI YA MAKOCHA


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi amefunga kozi ya makocha ya leseni C inayotolewa na CAF, iliyowashirikisha makocha 31 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Akifungua kozi hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Soka mkoa wa Dar es salaam (DRFA), Malinzi amewaomba washiriki wa kozi hiyo kwenda kutumuia ujuzi walioupata kwa kufundisha timu na vituo vya vijana vilivyopo seheu mbalimbali.

“Naimani wote hapa mlioshirki kozi hii ni watu wa mpira, ombi langu kwenu ni kwenda kufundisha mpira na sio kwenda kuviweka vyeti hivi hivi makabatini, mtusaidie kuandaa vijana kama tulivyo TFF na mipango mziuri ya kuendeleza vijana kwa ajili ya ushirki wa vijana kwenye fainali za Mataifa Afrika kwa vijaa wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2017 nchini Madagascar, mwaka 2019 Tanzania na baadae tuweze kushiriki fainali za Olimpiki mwama 2010 Tokyo nchini Japan.

Aidha Mwenyekiti wa DRFA Almasi Kasongo akiongea wakati wa kumkaribsisha Rais wa TFF, alisema DRFA wamejitahid kuendesha kozi hiyo yenye washiriki 31 lakini chnagamoto kubwa ni gharama za uendeshaji kwani kozi moja kama hiyo inahitaji fedha zaidi ya shilingi milioni 15 za Kitanzania jambo ambalo vyama vingine vya mikoa vinashindwa kumudu.

STAR TIMES KUDHAMINI LIGI YA FDLKampuni ya StarTimes Media ya jijini Dar es salaam leo imeingia mkataba wa udhamini na TFF kudhamini Ligi Daraja la Kwanza nchini (FDL) inayoshirikisha timu 24 kutoka katika mikoa 16 ya Tanzania bara.

Akiongea na waandishi wa habari wakai uwekaji sahihi mkataba huo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi ameshukuru kituo cha Star Times kwa kuamua kuwekeza katika mpira wa miguu na hasa kwenye chimbuko la vipaji na wachezaji wengie nchini.

Malinzi amesema udhamini huo wa shilingi milioni 900 kwa kipindi cha miaka mitatu, unatarajiwa kuongezeka wiki ijayo baada ya kuingia mkataba na mdhamini mwingine wa kurusha matangazo ya ligi hiyo kwa shilingi milioni 450 na kufikia jumla ya udhamini wa shilingi bilioni 1.3.

Aidha Malinzi amesema TFF inaendelea na mipango ya kuhakikisha inavisaidia vilabu vya madaraja ya chini, timu za wanawake na vijana kuona vinapata udhamini na kuweza kushirki vyema michuano mbalimbali.

Naye Mkurugenzi wa StarTimes Media nchini, Lanfang Liao amepongeza ushirikiano mpya ulioanzishwa kati ya kampuni yake na TFF na kuahidi kudumisha ushirkiano huo kwa faida ya maendeleo ya mpira wa Tanzania.

Mwenyekiti wa timu ya Kinondoni Municipal Council (MKC), John Njunde akiongea kwa niaba ya vilabu vya ligi daraja la kwanza, amesema anaishukru TFF kwa kuweza kuvitafutia udhamini vilabu na sasa wataweza kushiriki vizuri ligi hiyo inayotoa timu tatu zitakazopanda ligi kuu msimu ujao.

VYAMA VYA MIKOA VYATAKIWA KUANZISHA LIGI ZA WANAWAKE


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TF) limeviagiza vyama vya mpira wa miguu vya mikoa (FA’s) kuendesha mashindano ya ligi ya mabingwa wa mikoa kwa wanawake (Region Womens Champion League) kabla ya tarehe 31, Disemba mwaka huu.

Kila chama cha mkoa cha mpira wa miguu nchini kinapaswa kuwasilisha jina la bingwa wa mkoa mwishoni wa mwezi Disemba mwaka huu, kwa ajili ya maandalizi ya Ligi ya Taifa ya Wanawake inayotarajiwa kufanyika mwakani.

Ligi ya Taifa ya Wanawake inatarajiwa kuanza mapema mwakani baada ya kupatikana mabingwa wa mikoa 27 nchini ikijumuisha mkoa wa Dar es salaam utakaokuwa na timu tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke.

Jumla ya timu 10 zinatarajiwa kupanda Ligi Kuu ya Wanawake Taifa baada ya timu za mikoa 27 kucheza ligi ya mabingwa na kupata timu 10 zitakazoanza kwenye ligi hiyo ya wanawake mwakani.

Tuesday, September 22, 2015

MALINZI AFUNGA KOZI YA MAKOCHA, AWAPA ANGALIZO
RAIS wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Jamal Malinzi, amefunga kozi ya wiki mbili ya makocha lesseni C inayotambuliwa na Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) na kuwataka wahitimu hao kufanyia kazi mafunzo waliyoyapata.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kufunga mafunzo hayo, Malinzi amesema kuwa anasikitika kuona makocha wanapata mafunzo kama hayo lakini wanaenda kuweka vyeti vyao ‘makabatini’ na kuacha kufanyia kazi walichojifunza.

“Hiki mlichokipata kwenye mafunzo haya mnatakiwa muende mkafanyie kazi kwa kutafuta timu za kufundisha na baada ya mwaka mmoja ni vizuri mkajiendeleza zaidi ya hapa,” alisema Malinzi

Amesema kuwa Shirikisho lake limepanga kuhakikisha baada ya muda litafuta utaratibu wa makocha wenye lesseni C kuwa kwenye benchi la ufundi la timu za daraja la kwanza na kuwa wasaidizi kwenye benchi la ufundi la timu za ligi kuu.

“Kwa sasa hivi makocha wa ligi kuu wanatakiwa kuwa na leseni ya daraja B na wasaidizi angalau leseni daraja C, ila kuanzia msimu wa 2017-2018 mambo yatabadilika na lessen I C aizataruhusiwa kwenye mabenchi ya ufunzi kwa timu za ligi kuu, mambo yataendelea hivyo mpaka mwisho tutakuwa na leseni za daraja A,” alisema Malinzi.

Aidha, aliwataka wahitimu hao ambao wengi wao wanatoka kwenye klabu za daraja la kwanza na wengine wakiwa makocha wasaidizi kwenye klabu za ligi kuu, kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata kwenye mafunzo hayo kuzisaidia timu zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha soka mkoa wa Dar es Salaam, Almas Kasongo, ameishukuru TFF kwa jitihada za kuendeleza mchezo wa soka nchini na kuelelezea changamoto wanazokutana nazo katika kuandaa kozi kama hizo kwa vyama vya soka vya mikoa nchini.

“Sisi DRFA tumefanikiwa kuendesha kozi hii kwa sababu ya uwepo wa timu za Simba, Yanga na Azam kwenye ligi kuu ambazo ni sehemu ya mapato kwa chama chetu, ila kwa vyama vingine hali inakuwa ngumu kuandaa na kuendesha mafunzo kama hayo,” alisema Kasongo.

Kozi hiyo ya wiki mbili ilikuwa ikifanyika kwenye ukumbi wa TFF na kuendeshwa na mkufunzi anayetambulika na CAF, Salum Madadi ambaye pia ni Mkurugenzi wa ufundi wa TFF.

TFF YAISHITAKI ETOILE DU SAHEL FIFA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limefungua kesi kwenye Kamati ya Nidhamu ya FIFA dhidi ya klabu ya Etoile Sportive du Saleh ya Tunisa kutokana na klabu hiyo kushindwa kuilipa klabu ya Simba SC ya Tanzania pesa za mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi.

Kwa mujibu wa barua ya FIFA kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Tunisia (FTF) na nakala yake kwenda TFF, klabu hiyo inashitakiwa  kwa kuvunja kanuni kwa mujibu wa ibara ya 64 ya kanuni za nidhamu za FIFA (Fifa Disciplinary Code).

Kwa kuzingatia hilo, agenda hii itakuwa kwenye kikao kijacho cha kamati ya nidhamu.

Etoile Sportive du Sahel wametakiwa kulipa mara moja kiasi cha dola za kimarekani laki 3 na riba ya asilimia 2% kwa kila mwaka kama ilivyoelekezwa na maamuzi ya Jaji mmoja wa Kamati ya Nidhamu za Wachezaji mnamo tarehe 20 Novemba 2014.

Tangu wakati huo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekua likiwasiliana na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Tunisia (FTF) na FIFA kwa niaba ya klabu ya Simba amabye ni mwanachama wa TFF.

Ikiwa klabu hiyo ya Tunisia itafanya malipo kwa klabu ya Simba na kupelekea ushahidi wa malipo kwa FIFA basi suala hilo litafutwa.

Aidha klabu hiyo iko kwenye hatari ya kushushwa daraja au kupokwa alama  kwenye ligi (League Point) iwapo haitalishughulikia suala hilo mara moja.

MALINZI AFUNGA FAINALI ZA AIRTEL RISING STARS


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi leo amefunga fainali za michuano ya kombe la Airtel Rising Stars katika uwanja Karume jijini Dar es salaam.

Akiongea kwakati wa ufungaji michuano ya airtel mbele ya halaiki ya vijana walioshirki michuano hiyo, Malinzi ameishukuru kampuni ya simu ya Airtel kwa kuendelea kudhamini michuano hiyo ambayo inawapa nafasi vijana ya kucheza mpira na kuonekana na baadae kujipatia ajira.

“Lengo la TFF ni kushirki fainali za Olimpiki za Dunia mwaka 2020 Tokyo –Japan hivyo wachezaji wenye vipaji kutoka kwenye michuano hii ya Airtel na vijana wengine wataendelea kutunzwa kwa ajili ya timu ya Taifa ya baadae” Alisema Malinzi.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel ambao ndio wadhamini wakuu wa michuano hiyo, amesema airtel wataendelea na program hiyo ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 kwa wanawake na wanaume, na kuahidi kuendelea koboresha michuano hiyo kila mwaka.

Michuano ya Airtel Rising Stars iliyomalizika leo, ilizisihirkisha timu za wanaume na wanawake kutoka mikoa saba nchini, huku mashindano hayo yakiwa yanafanyika kwa msimu wa tano sasa tangu kuanzishwa mwaka 2011.

Kwa upande wa wanaume, timu ya Ilala imeibuka mabingwa baada ya kuifunga Mbeya kwa mabao 4-0 katika mchezo wa fainali ulochezewa jioni ya leo, huku timu ya wanawake ya Temeke wakiibuka washindi baaada ya kuibwaga Kinondoni mwa mikwaju ya penati 5-4.

Monday, September 21, 2015

SIMBA YAITUMIA SALAMU YANGA, YAICHAPA KAGERA SUGAR MABAO 3-1TIMU kongwe ya soka nchini, Simba jana iliendelea kuchanua katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuitandika Kagera Sugar mabao 3-1.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mshambuliaji Hamisi Kiiza ndiye aliyeibeba Simba baada ya kuifungia mabao yote matatu.

Kutokana na kuzitikisa nyavu za Kagera Sugar mara tatu, Kiiza sasa ameweka rekodi ya kuifungia Simba mabao matano katika mechi tatu ilizocheza za ligi hiyo.

Simba sasa imefikisha pointi tisa sawa na Yanga na Azam, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa. Yanga inaongoza kwa mabao mengi ya kufunga.

Kiiza alifunga bao la kwanza katika kipindicha kwanza, alipounganisha wavuni kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Awadh Juma. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipa Manyika Peter wa Simba alistahili pongezi kutokana na kuzuia mipira mingi ya hatari iliyopigwa na washambuliaji wa Kagera Sugar.

Kiiza aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 46 baada ya kumalizia krosi safi kutoka kwa beki wa kushoto, Mohamed Hussein Tshabalala.

Kagera Sugar ilipata bao la kujifariji dakika ya 50 lililofungwa na Mbaraka Yussuf baada ya mabeki wa Simba kujichanganya katika eneo lao la hatari.

Kiiza alihitimisha karamu ya magoli dakika ya 90 baada ya kuifungia Simba bao la tatu kwa shuti kali, baada ya kupokea krosi kutoka kwa Mwinyi Kazimoto.

Simba wanatarajiwa kushuka tena dimbani Septemba 26, mwaka huu, kuvaana na mahasimu wao Yanga katika mechi inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.

Sunday, September 20, 2015

YANGA HII WEEE ACHA TU, YAIBAMIZA JKT RUVU 4-1


YANGA SC imetoa onyo kwa mahasimu wao, Simba SC kuelelea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuwatandika JKT Ruvu mabao 4-1 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo wa tatu mfululizo unaifanya Yanga SC itimize pointi tisa na kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayoonyeshwa moja kwa moja na Azam TV.
Hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma dakika ya 30 akimalizia pasi fupi ya Amissi Tambwe baada ya kazi nzuri ya kiungo wa kulia Deus Kaseke.
Yanga SC ilitawala mchezo kipindi cha kwanza, lakini haikuweza kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao, wakati JKT walicheza kwa kujihami zaidi kipindi hicho.
Kipindi cha pili, Yanga SC walirudi na kasi ya kusaka mabao zaidi na iliwachukua dakika tatu tu kupata bao la pili, lililofungwa na Mrundi, Amissi Tambwe aliyemalizia krosi ya Kaseke.
JKT wakafanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 49, kupitia kwa beki na Nahodha wake, Geogre Minja aliyetumia mwanya wa wachezaji wa Yanga SC kuzubaa baada ya kupata bao la pili.
Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara misimu miwili iliyopita, Amissi Tambwe akaifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 62 kwa kichwa akimalizia krosi ya Simon Msuva. 
Kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko akahitimisha sherehe za mabao Yanga SC kwa kufunga bao la nne, dakika ya 87 kwa shuti la nje ya boksi baada ya kukutana na mpira uliookolewa na Michael Aidan kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Mbuyu Twite baada ya Msuva kuangushwa.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo jioni ya leo, Stand United imeshinda 2-0 dhidi ya African Sports ya Tanga Uwanja wa Kambarage, Shinyanga mabao yote yakifungwa na Elias Maguri, wakati Uwanja wa Mkwakwani, Tanga bao pekee Fully Maganga limeipa Mgambo Shooting ushindi wa 1-0 dhidi ya Majimaji FC na Uwanja wa Sokoine, Mbeya Prisons imeshinda 1-0 dhidi ya Mbeya City bao pekee la Jumanne Elfadhil.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi nne, Mwadui FC na Azam FC Uwanja wa Mwadui Complex, Mtibwa Sugar na Ndanda FC Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Simba SC na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Coastal Union na Toto Africans Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Salum Telela dk78, Amksi tambwe, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya dk61.
JKT Ruvu; Tony Kavishe, Michael Aidan, Napho Zuberi, Martin Kazila, Ramadhani Madenge, George Minja, Ismail Aziz/Abdulrahman Mussa dk57, Nashon Naftali, Samule Kamuntu/Gaudence Mwaikimba dk57, Saad Kipanga/Emmanuel Pius dk77 na Mussa Juma.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY

Saturday, September 19, 2015

VIJANA WALIOKWENDA ORLANDO PIRATES WAREJEAKufuatia safari ya vijana watano wa U15 Asaad Ali Juma, Maziku Aman, Issa Abdi, Kelvin Deogratias, Athumani Maulid waliokwenda kufanya mazoezi kwenye klabu ya Orlando Pirates kufuatia mwaliko uliotolewa na TFF na klabu hiyo, safari hiyo ilikamilika na vijana wamerejea nyumbani.

Vijana hawa waliongozana na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi wakiwa Afrika Kusini walifanya mazoezi ya wiki moja kuanzia Septemba Mosi mpaka tarehe 7 Septemba, 2015 chini ya uangalizi wa Augusto Placious ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Orlando Pirates.

Idara ya ufundi ya Orlando Pirates imejiridhisha na kiwango kilichoonyeshwa na vijana hao.

Hatua inayofuata ni mawasiliano kati ya shule wanazosoma hao vijana hapa Tanzania na klabu ya Orlando Pirates ili kutafutiwa nafasi za masomo kwenye shule za Afrika Kusini.

Jambo hili likikamilika vijana hao watakwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya masomo na kufundishwa mpira.

TFF inamshukuru Dr. Irvin Khoza Rais na mmiliki wa klabu ya Orlando Pirates kwa ushirkiano na kutoa nafasi kwa vijana wa U15 Tanzania kwenda kufanya mazoezi kwenye klabu hiyo kongwe nchini Afrik Kusini na kuendelezea

Wednesday, September 16, 2015

AZAM YAENDELEA KUCHANUAAZAM FC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada kuwalaza mabao 2-0 wenyeji Stand United Uwanja wa Kambarage, Shinyanga jioni ya leo.
Shukrani kwao, wafungaji wa mabao hayo, mshambuliaji wa Kenya, Alan Watende Wanga na kiungo mzalendo Frank Rymond Domayo.
Huo ushindi wa pili mfululizo kwa Azam FC ya kocha Muingereza Stewart Hall, baada ya awali kuichapa Prisons ya Mbeya 2-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Katika mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Yanga SC imeialza 3-0 Prisons Dar es Salaam, Simba SC imeifunga 2-0 Mgambo JKT Tanga, Majimaji FC imeifunga 1-0 Kagera Sugar Songea, Mbeya City imeichapa 3-0 JKT Ruvu Mbeya, Toto Africans imefungwa 2-1 na Mtibwa Sugar Mwanza, Ndanda FC imeialza 1-0 Coastal Union Mtwara na Mwadui FC imeshinda 2-0 dhidi ya African Sports.

MATOKEO MECHI ZA LIGI KUU TZ BARA LEO
Yanga SC 3-0 Prisons
Mgambo JKT 0-2 Simba SC
Majimaji FC 1-0 Kagera Sugar
Mbeya City 3-0 JKT Ruvu
Stand United 0-2 Azam FC
Toto Africans 1-2 Mtibwa Sugar
Ndanda FC 1-0 Coastal Union
Mwadui FC 2-0 African Sports
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

YANGA MBELE KWA MBELE LIGI KUUYANGA SC imeendelea kung’ara katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuichapa mabao 3-0 Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
Mabingwa hao watetezi, sasa wanafikisha pointi sita na mabao matano, baada ya awali kushinda pia nyumbani 2-0 dhidi ya Coastal Union.
Hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na kiungo Mkongo, Mbuyu Twite dakika ya 27 baada ya kipa wa Prisons, Mohammed Yussuf kushindwa kuokoa mpira wa adhabu uliopigwa na Simon Msuva, kufuatia Deus Kaseke kuangushwa nje ya boksi.
Mrundi Amissi Tambwe aliifungia Yanga SC bao la pili dakika 45 akiumalizia mpira uliopanguliwa na kipa wa Prison, Yussuf baada ya mpira wa adhabu wa kiungo wa Rwanda, Haruna Niyonzima kufuatia Msuva tena kuangushwa.
Mshambiliaji wa Prisons Jeremiah Juma alipoteza nafasi nzuri ya kufunga kipindi cha kwanza baada ya kupia juu la lango. Kipindi cha pili, kocha wa Prisons, Salum Mayanga alianza kwa kumpumzisha kipa Yussuf na kumuingiza Aron Kalambo
Refa Alex Mahagi wa Mwanza alimtoa kwa kadi nyekundu James Josephat dakika ya 59 baada ya kumdondosha Msuva kwenye boksi na Mzimbabwe Donald Ngoma akaifungia Yanga SC bao la tatu kwa penalti dakika ya 60.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi Haji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Thabani Kamusoko, Deus Kaseke/Salum Telela dk66
Simon Msuva, Haruna Niyonzima Geoffrey Mwashiuya dk79, Amissi Tambwe/Malimi Busungu dk84, Donald Ngoma na Deus Kaseke.
Prisons: Mohammed Yussuf/ Aron Kalambo dk46, Salum Kimenya, Laurian Mpalile, James Josephat, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Lambert Sabianka, Juma Seif, Mohammed Mkopi/Cosmas Ader dk47, Boniface Hau Ally Manzi dk64 na Jeremiah Juma.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

SIMBA YAIBANJUA MGAMBO SHOOTING 2-0SIMBA SC imetimiza dhamira ya kukusanya pointi zote sita katika mechi zake mbili za awali za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara- baada ya jioni ya leo kuilaza mabao 2-0 JKT Mgambo.
Huo ni mwanzo mzuri kwa kocha Muingereza Dylan Kerr Simba SC, kwani sasa Wekundu wa Msimbazi nao wamo kwenye mbio za ubingwa.
Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na kiungo Mzimbabwe Justuce Majabvi dakika ya 27 baada ya krosi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuzua kizazaa langoni mwa Mgambo
Mgambo walikosa bao la wazi dakika ya 19 baada ya shuti la Salim Aziz Gillah kupaa juu kidogo ya lango.
Said Ndemla alikaribia kufunga dakika ya 35 kwa kichwa akimaizia krosi ya Hassan Kessy lakini mpira ukatoka nje kidogo ya lango.
Mgambo tena wakakosa bao la wazi baada ya shuti la Nassor Gumbo aliyeingia akichukua nafasi ya Salim Gillah kugonga mwamba na kurudi uwanjani dakika tano baaadye.
Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliifungia Simba SC bao la pili dakika ya 73 akimalizia pasi Ibrahim Hajibu baada ya gonga safi baina yao.
Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Simba SC baada ya awali kuifunga African Sports 1-0, bao pekee la Kiiza.
Kikosi  cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Mohamed Hussein, Hassan Ramadhani, Murushid Juuko, Hassan  Isihaka, Justuce Majabvi, Awadh Juma, Said Ndemla/Abdoulaye Pape N’daw dk69, Mussa Mgosi/Ibrahim Habib dk67, Mwinyi Kazimoto/Hamisi Kiiza dk46 na Peter Mwalianzi.
Mgambo JKT; Said Abdi, Bashiru Chanache, Salim Mlima, Salim Kipaga, Ramadhani Malima/Athanas Chacha, Bakari Mtama, Salim Gillah, Mohammed Samatta, Helbert Charles, Fullu Zulu Maganga/Bolly Shaibu dk68 na Chande Magoja.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

TFF YAFANYA MABADILIKO YA KAMATI NDOGOKikao cha Kamati ya Utendaji cha Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kilichofanyika Septemba 06, mwaka huu kilifanya mabadiliko madogo ya kamati zake ndogo ndogo.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Blassy Kiondo aliyekua Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Wanawake ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Ufukweni na Sakafuni (Beach Soccer and Futsal).

Amina Karuma ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake nchini (TWFA) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Wanawake.

Mashindano ya Copa Coca Cola yanayodhaminiwa na Kampuni ya Vinywaji ya Coca Cola yaliyokuwa yafanyike katikati ya mwaka huu, sasa yatafanyika mapema mwakani mwezi Februari kuanzia ngazi ya Wilaya na fainali zake kufanyika mwezi Juni na Julai 2016.

Michuano hiyo ambayo hushirikisha timu za mikoa yote Tanzania kuanzia katka ngazi ya Wilaya, hufanyika kila mwaka kwa kuwashirkisha vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U15).

Taarifa ya Idara ya Masoko ya Coca Cola imesema kampuni hiyo imeahirisha kufanyika kwa michuano hiyo wa mwaka huu, na sasa itafanyika mwakani ili waweze kupata nafasi ya kuandaa vizuri mashindano hayo.

Tuna uzoefu na mashindano hayo, ni vyema tukaifanya wakati wa likizo wakati vijana wakiwa mapumziko, sababu wachezaji wote wa michuano ya Copa Coca Cola ni wanafunzi hivyo ni vizuri tukaandaa mashindano hayo wakati wanafunzi wakiwa likizo.

Michuano ya Copa Coca Cola ilianza mwaka 2007 kwa kushirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U17) na baadae mwaka 2012 kubadilishwa na kuwa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U15).

Baadhi ya wachezaji waliopatikana katika mashindano hayo kwa sasa wanacheza katika vilabu vikubwa vya Ligi Kuu ya Vodacom nchini na wengine wamepata naafasi ya kucheza soka nje ya nchi.

LIGI YA FDL KUANZA SEPT 19


Ligi Daraja la Kwanza nchini (FDL) inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Jumamosi Septemba 19 kwa michezo 10 kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini, ambapo jumla ya timu 24 zinashirki ligi hiyo ambayo washindi wa tatu watapanda ligi kuu ya Vodacom msimu ujao.

Kundi A, Polisi Dar watakuwa wenyeji wa Friends Rangers kwenye uwanja Mabatini mkoani Pwani, Mjii Mkuu ya Dodoma watapambana na  Polisi Dodoma kwenye uwanja wa Jamhuri mjini humo.

Kundi B, Polisi Morogoro watacheza na Burkina Faso uwanja wa Jamhuri Morogoro, Njombe Mji FC watacheza na Kurugenzi uwanja wa Amani mjini Njombe, Lipuli ya Iringa watawaribisha Kimondo FC uwanja wa Wambi- Iringa na JKT Mlale watakua wenyeji wa Ruvu Shooting katika uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.

Kundi C, Mbao FC watawakaribisha Geita Gold uwanja wa CCM Kirumba, Rhino Rangers watacheza dhidi ya Polisi Tabora uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Panone FC watawakaribisha JKT Oljoro katika uwanja wa Ushirka mjini Moshi na Polisi Mara watakua wenyeji wa JKT Kanembwa kwenye uwanja wa Karume mkoani Mara.

YANGA KUCHAGUA VIONGOZI WAPYA BAADA YA UCHAGUZI MKUU


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limepokea maombi ya klabu ya Young Africans (Yanga SC) ya kutaka kufanya uchaguzi wake mkuu wa viongozi wa klabu hiyo kwa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya Utendaji.

TFF imeiomba klabu hiyo kufanya mkutano wake wa Uchaguzi wa viongozi baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Rais, Wabunge na Madiwani) utakaofanyika Oktoba 25, 2015.

Hii ni kutokana na unyeti wa uchaguzi wa klabu ya Yanga yenye matawi nchini kote.

TFF KUFANYA MAREKEBISHO YA KANUNI ZAKEShirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limebaini kuwepo kwa vitendo vyaa wanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania kujihusisha na masuala ya Siasa wakiwa katika mavazi rasmi ya mpira ambayo yana nembo za vilabu na wadhamini wa Ligi.

Katiba ya TFF ibara ya I (4) inatamka “TFF is neutral in matters of politics and religion. Discrimination of any kind against a country, private person or group of people on account race, skin colour, ethnic, national or social origin, gender, language, religion, political opinion or any other opinion, wealth, birth or any other status is strictly prohibited and punishable by suspension or expulsion.”

Aidha kanuni za Ligi, Kanuni ya 14(40) inatamka: “ Hairuhusiwi kwa mchezaji, mwamuzi au kiongozi wa timu kuonyesha kwa njia yeyote tangazo au ujumbe unaohusiana na dini yeyote au ulio na madhumuni maalum bila idhini ya TFF/TPLB”.

TFF inachukua fursa kuwakumbusha wana familia wote wa mpira wakiwemo viongozi, wachezaji, waamuzi, makocha na madaktari wa michezo kuwa ni marufuku kuelezea hisia zao za kisiasa au kujihusisha katika kampeni za kisiasa wakiwa katika mavazi rasmi ya mpira zikiwemo jezi na track suites zenye nembo za TFF, vilabu wadhamini na ligi, Taifa stars au za washirika wa TFF wakiwemo wadhamini.

Aidha ni marufuku kwa mashabiki wa mpira kutumia fursa ya mechi za mpira wa miguu kubeba mabango au kusambaza ujumbe wa kisiasa.

Hatua kali zitachukuliwa kwa wataokiuka mahitaji ya katiba na kanuni za mashindano. TFF inatambua haki za wanamichezo kushiriki katika siasa ili mradi ushiriki wao hazikiuki kanuni na mahitaji ya katiba za TFF na FIFA

Tuesday, September 15, 2015

MALINZI AZINDUA KAMBI YA U-13Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi leo amezindua rasmi kambi ya kikosi cha timu ya Taifa umri chini ya miaka 13 ambacho kitakua pamoja kuelekea fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 17  (U17) zitakazofanyika nchini Tanzania mwaka 2019.

Kikosi hicho ni cha vijana 20 ambao waliteuliwa tokana na mashindano ya vijana ya umri chini ya miaka 13 (U13) yaliyofanyika Mwanza mwezi Juni mwaka huu.

Malinzi amezindua kambi hiyo itakayodumu kwa muda wa miaka mitano hadi mwaka 2019. Kambi hiyo itakuwa  kwenye shule ya kulea na kukuza vipaji vya mpira ya Alliance iliyopo jijini Mwanza.

Wakiwa Alliance vijana hao gharama za masomo, matunzo na vifaa zitatolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).

Akizindua kambi hiyo Malinzi aliongea na wazazi wa watoto hao na kuwaahidi kuwa TFF kwa kushirikiana na shule ya Alliance itahakikisha vijana hao wanapewa elimu nzuri itakayozingatia maadili.

Wazazi wa watoto wametoa shukrani kwa uteuzi huu wa watoto wao na Mkurugenzi wa shule ya Alliance Bw James Bwire ameahidi kutoa elimu bora na mafunzo mazuri kwa vijana.

Jumla ya vijana 455 toka mikoa yote ya Tanzania walishiriki mashindano hayo

Sunday, September 13, 2015

OLE GABRIEL AFUNGUA MICHUANO YA AIRTEL RISING STARNaibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Elisante Ole Gabriel leo Jumapili, Septemba 13, amezindua rasmi michuano ya Airtel Rising Stars kitaifa kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa michuano hiyo, Ole Gabreil ameipongeza kampuni ya simu za mkononi ya Airtel nchini kwa kuendesha michuano hiyo, ambayo inawapa nafasi vijana wa kike na kiume kuonyesha vipaji vyao vya kucheza mpira wa miguu.

Ole Gabriel ameiomba Airtel kuendelea kudhamini michuano hiyo na kutanua wigo zaidi kwa mikoa mingi kuweza kushiriki kwenye mashindano hayo.

Aidha Ole Gabriel ameiitaka TFF kuwasiliana na Wizara yake pindi wanapoagiza vifaa vya michezo nje ya nchi mapema, ili ofisi yake iweze kulisadia Shirikisho katika suala la ushuru wa vifaa vya michezo vinapoingia nchini.

Naibu katibu mkuu huyo aliyasema hayo wakati akijibu ombi la Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia aliyeiomba Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kuisaidia TFF kupata msamaha wa kodi pindi inapoingiza vifaa vya michezo nchini kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu.

Jumla ya timu saba za vijana wa kike na kiume zinashiriki fainali hizo za Taifa za Airtel Rising Stars zinazodhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, ambapo vijana wenye vipaji huchaguliwa na kupata nafasi ya kujiunga na vituo vya michezo (Academy) za Dakara – Senegal na Doha – Qutar zinazomilikiwa na kampuni hiyo.

Mikoa inayoshiriki fainali hizo ni Arusha, Ilala, Kinondoni, Temeke, Mbeya, Morogoro, Mwanza na Mbeya

KING MAJUTO YUKO HIJJA MAKKA

MSANII maarufu wa filamu na vichekesho nchini, Amri Athumani 'King Majuto' (kulia) akiwa na mahujaji wenzake katika mji wa Madina juzi kabla ya kwenda Makka, ikiwa ni mwendelezo wa ibada ya hija.

NGOMA, MSUVA WAIUA COASTAL UNION
NA AMINA ATHUMAN
MABAO mawili yaliyofungwa na Simon Msuva na Donald Ngoma yameiwezesha Yanga kuibuka na ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliandika bao lake la kwanza dakika ya saba kupitia kwa Msuva aliyeachia shuti kali akiunganisha pasi ya Kelvin Yondan.
Bao la pili lilipatikana dakika ya 42 baada ya Ngoma kuunganisha mpira uliorudi uwanjani baada ya kipa wa Coastal Union kupangua mpira wa krosi iliyochongwa na Msuva.
Katika mchezo huo, Yanga ilianza mchezo kwa kasi na kushambulia lango la wapinzani wao kama nyuki ikitafuta mabao ya kufunga.
Dakika ya 12 Coastal Union ilibadilisha mfumo wa uchezaji na wachezaji wake kurudi nyuma kwa ajili ya kuzuia mashambulizi.
Hali hiyo ilisaidia kupunguza kasi ya Yanga lakini dakika ya 18 Niyonzima alibaki na kipa Sebwato Nicholas, lakini shuti alilopiga lilitoka pembeni kidogo ya goli.
Coastal Union ilijibu shambulizi hilo dakika ya 23 ambalo halikuzaa matunda kabla ya kufanya mabadiliko na kumtoa Adeyum Ahmed na kuingia Twaha Ibrahim
Mabadiliko hayo yaliamsha ari ya wachezaji wa Coastal Union ambapo dakika ya 29 Ali Ahmed alipata nafasi ya kufunga na kuachia shuti kali lililopaa mita chache na kutoka nje.
Coastal Union ilipata nafasi nyingine dakika ya 76 kupitia kwa Patrick Protas baada ya kubaki na kipa lakini mpira aliopiga ulitoka pembeni kidogo ya goli.
Timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu lakini hadi dakika 90 zinamalizika Yanga ndiyo iliyoondoka uwanjani na kicheko baada ya kupata pointi tatu.

Ali Mustapha, Mbuyu Twite, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Thaban Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amis Tambwe/Malimi Busungu, Donald Ngoma na Godfrey Mwashiuya/Deus Kaseke.
Coastal Union:Sebwato Nicholas, Hamad Juma, Yasin Mustapha, Ernest Joseph, Tumba Sued, Said Jeilan/Patrick Protas , Ali Ahmed, Yousoufa Sabo, Nasoro Kapama, Godfrey Wambura na Adeyum Ahmed.

MABAO 10 YATINGA MECHI ZA AWALI LIGI KUU, AZAM YAILAZA PRISONS 2-1


MABAO 10 tu yametinga nyavuni katika mechi  saba za ufunguzi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo, huku kipa mpya wa Mbeya City, Juma Kaseja akianza vibaya Uwanja wa Sokoine.
Kaseja amefungwa bao moja  na timu yake mpya ikilala 1-0 nyumbani mbele ya Kagera Sugar kutoka Bukoba na hakuna timu iliyoshinda kwa wastani wa zaidi ya bao 1-0 dhidi ya wapinzani wake.
Timu zote zote zimeshinda 1-0 na 2-1 baada ya mechi zote saba leo.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Simba SC imewafunga bao 1-0 wakati Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Ndanda FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Mgambo Shooting ya Tanga.
Uwanja wa Majimaji, Songea  wenyeji Majimaji FC wameshinda 1-0 dhidi ya JKT Ruvu, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Azam FC imeshinda 2-1 dhidi ya Prisons wakati Toto Africans imeshinda 1-0 dhidi ya Mwadui FC.
Timu zilizoanza kwa ‘mikosi’ zaidi Ligi ya msimu huu ni Stand United iliyofungwa 1-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na Mbeya City iliyofungwa 1-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania itaendelea kesho wakati mabingwa watetezi, Yanga SC watakapomenyana na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

SIMBA YAANZA VYEMA LIGI KUU, YAICHAPA AFRICAN SPORTS 1-0


SIMBA SC imeanza vyema Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo.
Shukrani kwake mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Friday Kiiza ‘Diego’ aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 56, akimalizia kwa kichwa krosi maridadi ya Nahodha Mussa Hassan Mgosi.
Simba SC ilicheza vizuri tangu mwanzo wa mchezo na kukaribia lango la wapinzani mara kadhaa, lakini uhodari wa kipa wa zamani wa Yanga SC, Yussuf Abdul uliwanyima mabao zaidi Wekundu hao wa Msimbazi.
Pamoja na kwamba imepanda msimu huu, African Sports maarufu kama Wana Kimanumanu walionyesha upinzani kwa Simba SC
Mshambuliaji Boniphace Maganga aliyesajiliwa msimu huu kutoka Marsh Academy ya Mwanza, alikosa bao la wazi baada ya kuunganishia juu ya lango krosi nzuri ya Simon Sserunkuma dakika ya 89.
Hussein Amir aliinyima Sports bao la kusawazisha dakika ya 90, baada ya kuunganishia juu ya lango krosi nzuri ya Ayoub Masoud.
Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Azam FC imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Prisons ya Mbeya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Shukrani kwake Farid Mussa aliyefunga bao la ushindi dakika ya 86 baada ya Jeremiah kuisawazishia Prisons dakika ya 60, kufuatia
Kipre Herman Tchetche kuanza kuifungia Azam FC dakika ya 42.
Kikosi cha African Sports kilikuwa; Yusuph Yusuph, Ayubu Masoud, Mwaita Gereza, Juma Shemvuni, Rahm Abdallah, Novat Lufungo, Jemes Mendi/Ally Ramadhani dk83, Husein Amiri, Hasani Matemema, Omary Issa, Pera Mavuo/Bakari Masoud dk53.
Simba SC; Peter Manyika, Mohamed Husei ‘Shabalala’ Hassan Kessy, Jjuko, Majabvi, Awadh Juma, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto/Simon Sserunkuma dk89, Mussa Hassan ‘Mgosi’,Hamisi Kiiza/Boniphace Maganga dk75 na Peter Mwalinyanzi.
IMETOLEWA BLOGU YA BINZUBEIRY

DK. FEENELLA KUZINDUA MICHUANO YA AIRTEL RISING STAR Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dr. Fenella Mkangara leo Jumapili, Septemba 13, 2015 saa 8 kamili mchana anatarajiwa kuzindua rasmi fainali za michuano ya Airtel Rising Star katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Jumla ya timu sita zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo ambayo imekua ikifanyika kila mwaka nchini kwa udhamini wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, ambapo vijana wenye vipaji huchaguliwa na kupata nafasi ya kujiunga na vituo vya michezo (Academy) za Dakara – Senegal na Doha – Qutar zinazomilikiwa na kampuni hiyo.

Katika uzinduzi huo wa leo, timu za mkoa wa Ilala, Kinondoni, Mbeya, Morogoro, Mwanza na Temeke zinatarajiwa kupambana kusaka mshindi kwa fainali hizo za kitaifa.

Shirikisho la Mpira Miguu nchini (TFF), limetuma salamu za rambirambi kwa familia za Lubawa,  kufutia kifo cha mwamuzi mstaafu na kamishina wa TFF Saleh Lubawa kilichotokea jana jioni.

Katika salam zake kwenda kwa familia ya marehemu, TFF imesema inawapa pole wafiwa, ndugu jamaa na marafiki na kwa niaba ya familia ya mpira miguu nchini wapo pamoja na familia katika kipindi hichi cha maombolezo.

Mazishi ya marehemu Saleh Lubawa yanatarajiwa kufanyika leo jioni nyumbani kwake eneo la Kongowe – Kibaha.

MALINZI KUKUTANA NA WAZAZI WA U-13


Rais wa Shirikisho la Mpira Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi anatarajiwa kukutana wazazi wa vijana wenye umri chini ya miaka 13 (U-13) waliochaguliwa kujiunga na kituo cha michezo cha Alliance kilichopo jijini Mwanza.

Malinzi anatarajiwa kukutana na wazazi wa vijana hao siku ya jumatatu ya tarehe 14, Septemba 2015 saa 5 kamili asubuhi katika shule ya Alliance, kabla ya taratibu za kuwakabidhi vijana hao kwa uongozi wa kituo hicho.

Mapema mwezi Juni mwaka huu TFF iliendesha mashindano ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 13 (U-13) yaliyofanyika jijini Mwanza, ambapo jopo la makocha liliweza kuchagua wachezaji 20 wenye vipaji ambao watajiunga na kituo hicho kwa ajili ya masomo ya kawaida na kufundishwa michezo.

Mpango huo wa kuwaweka vijana katika kituo cha Alliance una lengo la kuandaa timu bora ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, itakayoshiriki kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana wenye umri huo zitakazofanyika nchini Tanzania mwaka 2019.