NA VICTOR MKUMBO
SHIRIKISHO la Soka
Tanzania (TFF), limesema kuwa ni marufuku kwa klabu za ligi kuu kuwachezesha
wachezaji wa kimataifa katika michuano ya ligi kuu msimu huu iwapo hazitawalipia
ada ya Dola za Kimarekani 2,000 (sawa na sh. milioni 4.6).
Katika mkutano wa
Kamati ya Utendaji uliofanyika mwaka huu, Zanzibar, kamati ilikubaliana kuwa
kila mchezaji ambaye atasajiliwa na klabu ya ligi kuu msimu huu, atalipiwa ada
ya Dola 2,000 kabla ya kuanza kwa ligi hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya
klabu zimeshatangaza kugomea kulipa ada hiyo kwa madai kuwa uamuzi huo
umechukuliwa kwa kushtukiza.
Kamati ya Utendaji ya
TFF ilifikia makubaliano hayo ili wachezaji wa kimataifa waliosajiliwa
Tanzania, waweze kuchangia fedha hizo kwa ajili ya maendeleo ya soka ya
wanawake na vijana.
Akizungumza Dar es
Salaam, jana, Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, alisema wameamua
kuzikumbusha klabu zote zilizosajili wachezaji wa kigeni ili kuwalipia ada hiyo.
Alisema katika ligi kuu
msimu huu, wapo wachezaji 27 wa kigeni, waliosajiliwa na timu mbalimbali,
zikiwemo Simba, Yanga na Azam. Klabu
hizo zimesajili wachezaji saba kila moja.
Kizuguto alisema wachezaji wengine wa kigeni wamesajiliwa katika
timu za Mbeya City, Stand United, African Sports na Coastal Union.
“Tunazikumbusha klabu
za Ligi Kuu Bara zilizosajili wachezaji kutoka nje ya nchi, kuwalipia ada ya Dola
2,000 kwa kila mchezaji kabla ya ligi kuanza,” alisema.
Aliongeza kuwa klabu
itakayolipia idadi ndogo ya wachezaji au wote saba, ndio itakaowatumia kwa msimu huu na si vinginevyo.
Ofisa huyo alisema
wanatarajia kutoa majina ya timu na orodha ya wachezaji waliolipiwa ada baada
ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Bara, Jumamosi wiki hii.
No comments:
Post a Comment