KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 27, 2015

K-ONE AIBUKA NA NGOMA NYINGINE MPYA KALI


Na Mwandishi Wetu

BAADA ya ukimya wa muda mrefu, hatimaye msanii nyota na chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini, Karim Othman ameibuka na kibao kingine kipya.

Kibao hicho kinachokwenda kwa jina la Nilikuchora, kimerekodiwa kwenye studio za Truck Music zilizoko Mbagala, Dar es Salaam, chini ya usimamizi wa prodyuza Rise Clever.

Akizungumza na Dawati la Michezo la Uhuru, mjini Dar es Salaam jana, Karim, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la K-One, alisema video ya wimbo huo imetengenezwa na Fadhili Ngoma.

Alisema video hiyo ni ya kwanza kuitoa akiwa msanii wa kujitegemea, baada ya mkataba wake na kampuni ya Baucha Records kumalizika tangu mwaka jana.

Awali, K-One aling'ara kwa kibao chake kinachojulikana kwa jina la Yule, ambacho alikirekodi kwa kushirikiana na Maunda Zorro. Alirekodi kibao hicho kwa usimamizi wa Baucha Records.

Kibao hicho ambacho kimepigwa katika miondoko ya zouk, kilitamba katika vituo mbalimbali vya televisheni pamoja na kupigwa kwenye vituo vya radio nchini.

K-One alisema baada ya kibao cha Nilikuchora, ambacho kinatarajiwa kuanza kupigwa kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni hivi karibuni, amejipanga kurekodi kibao kingine kitakachojulikana kwa jina la Sijadili mapenzi.

Mbali na vibao hivyo vitatu, K-One pia amewahi kurekodi vibao vingine kadhaa, kikiwemo Ngoja niseme, alichomshirikisha mkongwe wa muziki wa kizazi kipya nchini, Chege Chigunda.

Vibao vingine vya msanii huyo machachari ni Dhahabu alichomshirikisha Ali Kiba, Niwaambie alichorekodi na Madee, Muelewe alichoimba na Tundaman, Bora alichomshirikisha Top C, Weekend Special alichompa shavu Baker na Sina hakika.

Hata hivyo, K-One alishindwa kutoa video za nyimbo hizo kutokana na kukosa mdhamini baada ya mkataba wake na Baucha Records kumalizika.

“Namshukuru Mungu kwamba vibao vyangu vyote hadi sasa ni moto wa kuotea mbali, kinachonikwamisha ni kukosa wadhamini kwa ajili ya kutengeneza video,"alisema.

Licha ya kushindwa kuongeza mkataba na Baucha Records, K-One amemshukuru mmiliki wa studio hiyo, Ally Baucha kwa kumruhusu kutumia nembo yake kwa kipindi cha miaka miwili waliyokuwa pamoja.

Ameitaja sababu kubwa iliyomfanya ajitoe katika udhamini wa Baucha Records kuwa ni kushindwa kutoa albamu kama walivyokuwa wamekubaliana kwenye mkataba kati yao.

Kwa mujibu wa K-One, amerekodi zaidi ya nyimbo 12 katika studio za Baucha, lakini hadi sasa ameshindwa kumtolea albamu.

"Nimesikitishwa sana na hali hii, ndio sababu niliamua kutosaini mkataba mwingine na Baucha Records kwa sababu sioni faida yoyote ya kuendelea kufanyakazi chini yake,"alisema K-One.

Msanii huyo aliyetengeneza nywele zake kwa mtindo wa rasta, alisema licha ya wimbo wake wa kwanza wa Yule, kumpatia sifa na umaarufu mkubwa na pia kukubalika kwa mashabiki, Baucha hakuweza kuzisambaza nyimbo zake nyingine kwenye vituo vya redio na televisheni.

"Nyimbo zangu nyingine nazo ni kali sana. Fikiria nimerekodi na Ali Kiba, Chege, Tundaman, Madee, Top C na Becka Suspender, lakini nyimbo zote bado zipo kabatini," alilalamika msanii huyo, ambaye pia ni mtaalamu wa mambo ya kompyuta.

K-One alisema haelewi ni kipi kilichomsibu Baucha na kumfanya ashindwe kutimiza makubaliano yao kwa vitendo, hali inayomfanya ajione mnyonge kwa sababu wasanii wenzake wengi wamekuwa wakimkubali kutokana na kazi zake.

Mbali na kushindwa kusambaza kazi zake kwenye vituo vya redio na televisheni, K-One alisema Baucha alishindwa kumwandalia maonyesho ya muziki kwa ajili ya kutangaza kazi zake.

Alisema kwa sasa yupo huru kwa vile hafungwi na mkataba wa Baucha Records na kwamba ameshaanza mikakati ya kumsaka meneja mpya kwa ajili ya kusimamia kazi zake.

"Ni kweli Baucha alikuwa na mipango mizuri ya kuniendeleza, lakini sielewi ni kipi kilichomsibu. Labda mambo yake hayakuwa mazuri, huwezi kujua, maana siku zote alikuwa akinipa ahadi za subiri kidogo,"alisema.

Hata hivyo, alimshukuru Baucha kwa kuishi naye kama mdogo wake na kumsaidia katika mambo mengi madogo madogo.

"Namshukuru sana Baucha kwa sababu amenisaidia kwa mambo mengi. Tatizo pekee ni kwamba nimeshindwa kutimiza ndoto zangu chini yake,"alisema K-One.

"Lengo langu ni kuwa msanii bora. Nahitaji kuwa na meneja aliye makini na mwenye malengo makubwa zaidi kwa sababu uwezo nilionao kiusanii ni mkubwa,"aliongeza.

K-One alianza kuchomoza kimuziki baada ya kuibuka na vibao vyake viwili vya mwanzo, vinavyojulikana kwa majina ya Bila wewe na Sema baby, alivyorekodi na Ney wa Mitego na Pasha. Alirekodi vibao hivyo katika studio za Brain Trust, zilizoko Temeke, Dar es Salaam kwa udhamini wa dada yake.

Mbali na kurekodi vibao hivyo, K-One pia alikuwa akishirikishwa kuimba viitikio katika nyimbo za wasanii mbali mbali maarufu wa muziki hao. Baadhi ya wasanii hao ni JB wa kundi la Mabaga Fresh na Mood Kibra.

Vibao vingine vya awali vya K-One ni pamoja na Valentine, Kwa nini, Mpenzi sasa why na Fau.

K-One amewaomba mapromota wa muziki wa kizazi kipya kujitokeza kumsaidia kurekodi albamu yake kwa vile anazo nyimbo za kutosha, zikiwa tayari zimesharekodiwa. Amewahakikishia mapromota hao kwamba hawatajutia kutumia fedha zao kwa kazi hiyo.

Ametoa wito kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, wapendane, kusaidiana na kuaminiana ili waweze kupiga hatua za juu zaidi kimaendeleo.

Amesema miongoni mwa sababu zinazochangia kuwakwamisha wasanii chipukizi wa muziki huo, ni kutokuwepo kwa umoja miongoni mwao, kuchukiana na kutosaidiana.

“Wasanii walio juu wanapaswa kukumbuka kuwa kabla ya kufika huko waliko hivi sasa, nao walianzia chini, hivyo wasikwepe kuwasaidia wenzao wanaohitaji msaada kutoka kwao, hata kama wa kurekodi pamoja,”alisema.


No comments:

Post a Comment