KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, February 28, 2017

WAZIRI NAPE ATANGAZA KAMATI YA HAMASA SERENGETI BOYS


Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye (Mb), ametangaza Kamati ya watu 10 watakaohamasisha kuwaunganisha Watanzania kwa pamoja ili kuichangia timu ya Tanzania ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys.

Mheshimiwa Nape alitangaza kamati hiyo itakayoongozwa na Mtangazaji mkongwe wa habari na Mpira wa miguu nchini, Charles Hilary mbele ya wanafamilia ya mpira wa miguu waliohudhuria kongamano ya kujadili juu ya ushiriki wa Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Mada ilikuwa ni Tanzania kushiriki michuano ya Olimpiki Tanzania, lakini kwa kuwa kuna jambo la usoni la timu ya Serengeti Boys kucheza fainali za Kombe la Dunia huko Gabon kuanzia Mei 21, mwaka huu, Waziri Nape atakatangaza kamati ya kuhamamsisha ili Watanzania kwa pamoja waweze kuchangia.

Akitangaza kamati hiyo, Nape alisema kwamba Katibu wa Kamati hiyo atakuwa Mwesigwa Selestine ambaye ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakati wajumbe ni Mtangazaji wa Radio ya EFM, Maulidi Kitenge; Mkurugenzi wa Mahusiano wa kampuni ya Airtel Tanzania, Beatrice Singano na Mrembo wa Tanzania wa mwaka 1999, Hoyce Temu.

Pia wamo Mkurugenzi wa Habari katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hassan Abbas; Mkurugenzi wa Global Publishers Limited, Eric Shigongo; bosi wa radio Clous, Ruge Mutahaba pamoja wa wasanii wa kizazi kipya Diamond Platnums na Ally ‘King’ Kiba.

Pamoja na hayo, katika kongamano hilo na wadau wa soka wadau ikiwamo Serikali iliridhia kuwa mshiriki wa karibu kwa kila hatua kuanzia Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya timu za taifa, Kamati ya Hamasa kwa lengo la kupanga pamoja na kushirikiana kwa pamoja.

Wameazimia kuwa na chanzo cha fedha cha kueleweka ili kufanikisha program mbalimbali za timu za taifa ikiwamo ya U23 ambayo inatakiwa kushiriki kwenye michuano ya Olimpiki. Serikali imepanga kuwa pamoja badala ya kile kinachoitwa kudandia matokeo mafanikio bila kushiriki maandalizi.

Kadhalika wameazimia mpira kuwa jambo la nchi ili hamasa inayotangazwa iguse wadau wote kwa maana ya Watanzania wote.

Pia chanzo cha kupata vipaji kiwe pia kutoka mashuleni (Umitashumta na Umiseta) ambako Mheshimiwa Waziri Nape mbali ya kuthibitisha kuwa mwaka huu itafanyika tofauti na mwaka jana, pia aliagiza kuwa isiwe kama matamasha.

WAAMUZI WA TANZANIA KUCHEZESHA LIGI YA MABINGWA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limeteua waamuzi wanne wa Tanzania watakaochezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu za AS Porto Louis 2000 ya Mauritius na El Hilal ya Sudan wikiendi ijayo.

Katika mchezo huo ambao utafanyika ama Machi 17, 18 au 19 Mwamuzi wa kati atakuwa Israel Mujuni Nkongo wakati wasaidizi wake watakuwa ni Samuel Hudson Mpenzu na Josephat Deu Bulali huku Mwamuzi wa akiba akiwa ni Elly Ally Sasii.

Kamisha katika mchezo huo Na. 78 atakuwa Jerome Kelvyn Damon kutoka Afrika Kusini.

Wakati huo huo, waamuzi watakaochezesha mchezo kati ya Young Africans ya Tanzania na Zanaco FC ya Zambia wamefahamika. Waamuzi kutoka Djibouti ni Djamal Aden Abdi ambaye atapuliza kipenga wakati wasaidizi wake ni Hassan Yacin na Farhan Salime ilihali mwamuzi wa akiba atakuwa Souleiman Djamal.

Kamisha katika mchezo huo Na. 61 atakuwa Luleseged Asfaw kutoka Ethiopia.

Pia CAF imetanga waamuzi watakochezesha mnchezo kati ya Azam FC ya Tanzania na Mbabane Swallows. Mchezo huo wa kuwania Kombe la Shirikisho utachezeshwa na waamuzi kutoka nchi ya Benin.

Mwamuzi wa kati atakuwa Addissa Abdul Ligali wakati wasaidizi wake watakuwa Medegnonwa Romains Agbodjogbe na Babadjide Bienvenu Dina huku Mwamuzi wa akiba akiwa Moumouni Kiagou na kamisha wa mchezo atakuwa Mohamed Omar Yusud wa Kenya.

YANGA, RUVU SHOOTING KUVAANA KESHO




Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), inatarajiwa kuendelea keshokutwa Jumatano ambako mabingwa watetezi wa taji hilo, Young Africans itaalikwa na Ruvu Shooting kwenye mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali ya mchezo huo mmoja kwa siku ya Jumatano, ligi hiyo ambayo ni michuano mikubwa nchini, itaendelea mwishoni mwa wiki hii ambako kwa siku ya Jumamosi Machi 4, mwaka huu Simba itacheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ukiacha mchezo huo, michezo mingine ya Jumamosi Machi 4, mwaka huu itakuwa ni kati ya Toto Africans na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza huku Kagera Sugar ikiikaribisha Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Azam FC pia itacheza Jumamosi Machi 4, mwaka huu na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Chamazi. Mchezo huo utaanza saa 1.00 jioni wakati mechi nyingine zitaanza saa 10.00 jioni.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limerejesha tena mechi za Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Jumapili Machi 5, mwaka huu Mtibwa Sugar itaialika Young Africans kwenye uwanja huo katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Vodacom utachezwa Uwanja wa Uhuru ambako African Lyon itaialika Mwadui ya Shinyanga wakati Ndanda FC itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

RATIBA KAMILI YA MECHI ZA LIGI KUU YA WANAWAKE TANZANIA BARA


Ligi Kuu ya Mpira wa Wanawake, hatua ya timu sita Bora (6), ilianza rasmi jana kwa Mlandizi Queens ya Pwani kuilaza JKT Queens ya Dar es Salaam mabao 3-2 katika mchezo wa awali mchana kabla ya ule wa jioni Sisterz ya Kigoma kuifunga Fair Play ya Tanga mabao 5-1.

 Ligi hiyo inayochezwa Kituo kimoja cha Uwanja wa Karume, Ilala Dar es Salaam inakutanisha timu sita zinazowania ubingwa wa ligi hiyo ya wanawake ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania. Pia ni ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki.

Timu sita zilizofanikiwa kufika hatua ya Sita Bora ni JKT Queens ya Dar es Salaam, Mlandizi Queens ya Pwani na Fair Play ya Tanga kutoka Kundi “A” wakati kutoka Kundi “B” zimo Marsh Acedemy ya Mwanza, Sisterz ya Kigoma na Panama ya Iringa.

Mara baada ya mechi za jana Februari 26, 2017; ligi hiyo sasa itaendelea kesho Februari 28, mwaka huu ambako kwa michezo ifuatayo:  

Februari 28, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Marsh Academy na Panama saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Mlandizi na Fair Play.

Machi 2, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Sisterz na Marsh Academy saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Panama na JKT Queens.

Machi 4, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Fair Play na JKT Queens saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Marsh Academy na Mlandizi Queens.

Machi 6, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Panama na Sisters saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya JKT Queens na Marsh Academy.

Machi 8, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Sisters na Mlandizi Queens saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Panama na Fair Play.

Machi 10, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Marsh Academy na Fair Play saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Mlandizi na Panama.

Machi 11, mwaka huu kutakuwa na mchezo mmoja tu saa 10.00 jioni ambako JKT Queens watamaliza na Sisterz.

NNE BORA YA LIGI DARAJA LA PILI KUANZA KESHO

Timu nne vinara wa Ligi Daraja la Pili kutoka makundi manne, zinatarajiwa kuanza kupambana keshokutwa Jumatano - Machi mosi, mwaka huu ‘Play off’ kutafuta timu Tatu Bora, zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2017/2018.

Timu hizo zilizofanya vema ni pamoja na JKT Oljoro ya Arusha, Cosmopolitan ya Dar es Salaam, Mawenzi ya Morogoro na Transit Camp ya Shinyanga. Ziliibuka vinara katika makundi yao.

Ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi, inaonesha kuwa Ratiba ya Nne Bora itakuwa na raundi mbili ambazo kwa pamoja zitacheza kwa mwezi mmoja kuanzia Machi mosi hadi Aprili mosi, mwaka huu.

Raundi ya kwanza itaanza siku ya Machi mosi, mwaka huu ambako kutakuwa na mechi mbili ambazo Transit Camp itacheza na Mawenzi kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati Cosmopolitan itacheza na JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Machi 5, mwaka huu kutakuwa pia na michezo miwili ambako JKT Oljoro itacheza na Transit Camp kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Mawenzi Market itacheza Cosmopolitan kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Machi 12, mwaka huu JKT Oljoro itacheza na Mawenzi Market kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Cosmopolitan itacheza na Transit Camp kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Raundi ya Pili ya ligi hiyo, itaanza Machi 18, mwaka huu kwa timu za Mawenzi Market itacheza na Transit Camp kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati siku hiyo, JKT Oljoro itacheza na Cosmopolitan katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Machi 25, mwaka huu Cosmopolitan itapambana na Mawenzi Market kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam ilihali Transit Camp itacheza na JKT Oljoro Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

Funga dimba la hatua hiyo, itakuwa Aprili mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambako Mawenzi itakuwa mwenyeji wa JKT Oljoro wakati Cosmopolitan itakuwa mgeni wa Transit Camp kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Sunday, February 26, 2017

KAPUMZIKE KWA AMANI MUSSA SORAGA



ILIKUWA saa tano usiku wa kuamkia jana, wakati nilipopokea ujumbe wa maandishi kupitia simu yangu ya mkononi kutoka kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Habari Leo, kituo cha Zanzibar, Khatib Suleiman, ukinijulisha msiba wa mwanahabari mwenzetu mkongwe Mussa Soraga.

Kwa mujibu wa Khatib, Soraga alifariki dunia juzi (Jumamosi), saa 12 jioni, akiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) cha Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, ambako alilazwa akiwa chini ya uangalizi maalumu baada ya kupata ajali ya pikipiki.

Ajali hiyo ilitokea siku hiyo hiyo saa tano asubuhi, wakati Soraga akiwa anaendesha pikipiki yake aina ya Vespa, akitokea nyumbani kwake kwenda mjini, alipogongwa na mwendesha pikipiki mwingine maeneo ya barabara ya Dole na kuumia vibaya kichwani.

Wote wawili walikimbizwa Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kupatiwa matibabu, lakini Soraga alipoteza maisha ilipofika saa nne usiku akiwa ICU. Mwenzake bado anaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali hiyo.

Marehemu Soraga, ambaye asili yake ni mkoa wa Morogoro, alizikwa jana, saa nne asubuhi, kwenye makaburi ya Dole.

Nilipokea taarifa hizo za kifo cha Soraga kwa uchungu mkubwa. Nilipatwa na uchungu kwa sababu tangu nilipofahamiana naye miaka ya mwishoni mwa 1980, alikuwa kama ndugu na kaka yangu.

Wakati huo Soraga alikuwa mwandishi wa habari za michezo wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, kituo chake cha kazi kikiwa Zanzibar, nami nikiwa mwandishi wa kujitegemea wa magazeti hayo. Mbali na uandishi, Soraga pia alikuwa mwajiriwa wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM).

Nilianza kuwa karibu na Soraga baada ya kuajiriwa na Kampuni ya Uhuru Publications Ltd, mwanzoni mwa miaka ya 1990. Kila nilipopangiwa safari za kikazi kwenda Zanzibar, Soraga ndiye alikuwa mwenyeji wangu.

Alizoea kuja kunipokea bandarini, kunitafutia hoteli na pia kuhakikisha ananifikisha katika maeneo yote niliyotakiwa kufika kwa ajili ya kupata habari. Alikuwa zaidi ya mfanyakazi mwenzangu.

Ndio sababu haikuwa ajabu kwa Khatib, aliponitumia ujumbe ule juu ya kifo cha Soraga, kuandika: 'Zahor, rafiki yako Sogara amefariki kwa ajali'. Alikuwa na kila sababu ya kuandika hivyo kwa sababu waandishi wengi wa habari wa Zanzibar, hasa wakongwe, walikuwa wakiufahamu ukaribu niliokuwa naye.

Wakati nilipokuwa nikienda Zanzibar kwa ajili ya kuandika makala za michezo na burudani, Soraga ndiye aliyenifikisha kwa wanasoka wengi nyota wa zamani visiwani humo kama vile marehemu Mcha Khamis, marehemu Ali Issa, Ibrahim Kapenta na wengineo. Pia alinitembeza kwa waimbaji wengi wakongwe wa taarab visiwani humo na kunikutanisha na viongozi wa kikundi cha taarab cha Culture. Ama kwa hakika nilijifunza na kupata vitu vingi kutoka kwake.

Mbali na hayo, Soraga alikuwa mwandishi wa aina ya pekee visiwani Zanzibar. Haikuwa ikipita siku bila habari zake zinazohusu michezo na burudani kuwemo kwenye magazeti ya Uhuru na Mzalendo. Aliitendea haki tasnia hii kwa kufanya kile ambacho wanahabari wengi wa kizazi cha sasa wanashindwa kukifanya.

Kutokana na ukereketwa wake katika mchezo wa soka, Soraga aliwahi kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa timu ya KMKM na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa ligi Kuu ya Zanzibar, mwanzoni mwa 2000. Pia alisafiri na timu hiyo katika nchi mbalimbali za Afrika kwa ajili ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Kama hiyo haikutosha, uongozi wake thabiti ulimwezesha kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), akiiwakilisha wilaya ya Magharibi B, wadhifa ambao aliendelea kuutumikia hadi mauti yalipomfika.

Ninayo mengi ya kumuelezea Soraga, lakini kwa sababu ya mshtuko na uchungu nilioupata kutokana na kifo chake, inaniwia vigumu kuyaeleza. Hakika sisi sote ni waja wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.

Nakumbuka siku mbili kabla ya Soraga kufikwa na mauti, niliposti kwenye mtandao wa facebook, makala zangu kadhaa za wachezaji wa zamani na wanamuziki nyota wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), waliowahi kutembelea Tanzania, ambazo niliandika miaka mingi ya nyuma.
Soraga alikuwa mmoja wa marafiki zangu wa FB waliochangia kwenye post hizo.

"Bosi wangu, hiki ndicho ninachokupendea. Unatukumbusha vitu vingi vya zamani," aliandika Soraga kwenye moja ya posti hizo.

Katika moja ya maandishi yangu kwenye posti hizo, nilimkumbusha Soraga vijiwe vya chakula, alivyokuwa akinipeleka kupata ugali, chakula ambacho ni adimu na ghali sana visiwani Zanzibar. Akaishia kucheka.

Pia, nikampa neno la shukurani, nikimueleza kuwa kamwe siwezi kumsahau katika maisha yangu kutokana na msaada mkubwa aliokuwa akinipatia kila nilipokwenda Zanzibar kikazi.

Katika majibu yake aliandika hivi: "Hata nami nakushukuru sana bosi wangu. Kwa ujumla tulisaidiana sana kikazi, kiasi kwamba tuliyafanya magazeti ya Uhuru na Mzalendo kupata chati huku Zanzibar kwa habari za michezo."

Pia aliandika: "Rafiki zetu uliowaulizia Mcha Khamis na Ali Issa walishatangulia mbele ya haki. Hawakupishana sana. Nasi sote ndio njia yetu." Kumbe ndio alikuwa akiniaga.

Marehemu Soraga alikuwa akipenda kuniita bosi kwa sababu miaka kadhaa ya nyuma nilikuwa Mhariri wa Michezo katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo, hivyo kila alipoandika habari au makala zinazohusu michezo na burudani, ilikuwa lazima zipitie kwangu. Hata nami nilipenda kumwita bosi kwa sababu ya uzoefu na ukongwe wake katika tasnia hii na pia ukweli kwamba, alinizidi kiumri.

Buriani Soraga. Umetangulia kwenda kule ambako kila mmoja wetu lazima atafika. Maana ishi vyovyote utakavyoishi, fanya chochote utakachokifanya, lakini hakuna atakayeweza kukiepuka kifo. Kila mmoja wetu atakumbana nacho kwa wakati na siku aliyopangiwa na Mungu. Ni siri kubwa ya Allah.

Japokuwa mauti huuwa mwili wa binadamu ukabaki kuwa vumbi kaburini, lakini yale yote aliyoyafanya hapa duniani, yatabaki kuwa kumbukumbu katika maisha ya wengine.

Pumzika kwa amani Bradha Soraga.

STEVE NYERERE ALIPUA BOMU, ASEMA HAKUNA MSANII ANAYEIDAI CCM


MSANII wa maigizo nchini Steven Mangele (Steven Nyerere), amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni sawa na bahari, haiwezi kuyumba kwa kuondoka kwa msanii Wema Sepetu, lakini amesikitishwa na kujitoa kwake kutumia kwa uongo kuwa anakidai Chama.

Amesema jitihada zake za kumnusuru Wema, asijiunge na chama kisichoeleweka, zimemsababishia matatizo kutokana na sauti ya maridhiano kati yake na Mama, Mariam Sepetu, kumchonganisha na wanasiasa.

Steve alisema mama yake Wema, mbali na kumuharibia maisha, amejivua nguo kama mzazi aliyeaminika katika jamii na kumtaka Wema kukumbuka mazuri ya CCM, badala ya kusema uongo, kwa kuwa wasanii wote waliokuwa katika kampeni na Chama, walilipwa na kumaliza mkataba wao.

Akizungumza jana, jijini Dar es Salaam, Steve alikiri sauti iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ni yake na alitumia mbinu za propaganda na usanii kueleza uongo na kuwasingizia viongozi mbalimbali ili kumridhisha mama Wema ili ashughulikie tatizo la mwanawe bila ya jazba.

Alisema CCM ni kama bahari na ndio maana wametoka vigogo nguli, lakini
Chama hakikuyumba na wapo waliowahi kuwa viongozi wakuu, wameshitakiwa na kuhukumiwa, lakini hawakurudisha kadi za chama hivyo ni vyema Wema angejitathimini.

“Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anayo haki ya kusafisha mji wake kwani ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama. Katika majina ya walengwa, alitajwa dada yangu, swahiba wangu, rafiki yangu kipenzi Wema Sepetu na mtu wa kwanza kupigiwa nilikuwa mimi,”alisema.

Alisema hana mamlaka na uwezo wa kuwafikia viongozi wakuu
na pia hakuweza kusema jambo hilo jema au sio jema, lakini alikuwa akiangalia upande wa mwenzake aliyekata waliyekata kuni pamoja, akiamini wataota moto pamoja.

Steve alisema alishangaa kuanza kupokea simu za vitisho kuwa yeye ndiye anayetoa majina wakati hakuwepo Dar es Salaam, alikuwa Mwanza na kabla ya kurekodiwa, mama Wema alimpigia simu mara kwa mara na kumuahidi kama mzazi kuwa, yote hayo yanawezekana na yataisha.

“Lakini tena zikaanza simu za kunitukana kuwa nimemkimbia Wema akiwa ndani siku ya tatu na mama kuanza kunitisha kuwa atanifanya kitu kibaya na Wema atahama chama. Nilimuamini mama huyo ni mzazi bila kuwa na  shaka  na nikatumia sifa za chama changu kutetea chama na kutumia sanaa kumridhisha mzazi wangu na hili lilifanyika siku tano kabla, sasa kwa nini itolewe wakati huu,"alihoji.

Steve alisema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka juzi, wasanii wote walioshiriki walilipwa vizuri na kama yupo ambaye hakulipwa, ajitokeze. Alisema Wema ndiye aliyelipwa vizuri zaidi kwa kuwa alikuwa makamu mwenyekiti wa wasanii.

"Tulijitosa kwenye kampeni sisi wenyewe. Tuliifuata CCM na kuiomba tushiriki kwenye kampeni, sio kwamba wao ndio waliotufuata na wazo hilo nililitoa mimi. Hakuna msanii anayeidai CCM tusichume dhambi bure,"alisisitiza.

SIMBA PUNGUFU YAIDUWAZA YANGA






LICHA ya kucheza ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja, Simba jana ilionyesha maajabu baada ya kusawazisha na kuibwaga Yanga mabao 2-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10, baada ya beki wake wa kushoto, Javier Bokungu kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Mathew Akrama kutoka Mwanza kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Obrey Chirwa wa Yanga.

Kabla ya Bokungu kutolewa, Yanga ilitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na kuifanya Simba iwe kwenye wakati mgumu wa kutafuta bao la kusawazisha huku mashabiki wake wakiwa wamenyong'onyea.

Iliwachukua Yanga dakika tano kuhesabu bao kwa njia ya penalti baada ya beki Novatus Lufunga wa Simba kumkwatua Chirwa ndani ya eneo la hatari. Bao hilo lilifungwa na Simon Msuva.

Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Joseph Omog wa Simba kipindi cha pili, yaliongeza uhai kwa timu hiyo licha ya kubaki ikiwa na wachezaji 10. Kocha huyo aliwaingiza Jonas Mkude, Saidi Ndemla na Shiza Kichuya.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo aliisawazishia Simba dakika ya 66 baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa Kichuya.

Kichuya aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 80 kwa shuti kali la mbali lililompita kipa Deo Munishi wa Yanga na mpira kujaa wavuni.

Kutokana na ushindi huo, Simba inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 54, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 49, huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.


HATA KWA BAO LA MKONO LAZIMA TUIBUKE WASHINDI GABON-NAPE




WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema hata kwa goili la mkono ni lazima Serengeti Boys warejee nyumbani wakiwa ama na kombe au wakiwa wamefuzu kushiriki kombe la dunia kwa kuwa moja ya timu mbili zinazohitajika.

Kauli ya Waziri Nape ameitoa leo asubuhi wakati akifungua mashindano ya Kombe la Standard Chartered 2017 safari kuelekea Anfield ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 tangu benki hiyo kuanzishwa mwaka 1917 yaliyoanza kutimua vumbi katika viwanja vya JK Park Kidongo Chekundu, Gerezani.

Alisema haiwezekani taifa hili kuwa na Waziri mjanja kama Nape halafu Serengeti Boys inakosa kombe huko Gabon na nafasi ya ushiriki Kombe la dunia.

Pamoja na kauli yake hiyo Waziri Nape aliiomba Benki ya Standard Chartered kushiriki katika jukumu la kuhakikisha kwamba Serengeti Boys ama inarejea na kombe au inafuzu miongoni mwa timu mbili zitakashiriki Kombe la Dunia.

Wednesday, February 22, 2017

KESI YA WEMA SEPETU KUTAJWA TENA MACHI 15 2017.


Msanii Wema Sepetu akitoka katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi yake ya kuahirishwa hadi March 15 mwaka huu.Kesi hiyo imeaihirishwa na Hakimu Mkazi Thomas Simna baada ya wakili wa Serikali Constantine Kakula kuieleza mahakama kuwa upelelezi dhidi ya kesi hiyo bado haujakamilika.

MASOGANGE APANDISHWA MAHAKAMA YA KISUTU,AACHIWA KWA DHAMANA




Mrembo anayepamba video za wasanii nchini, Agnes Gerald Waya maarufu kama Masogange au Deal (28), amepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kutumia dawa za kulevya.

Mrembo huyo anayeishi Makongo Juu ambaye alikuwa akitumia muda mwingi kujiziba sura yake kwa mtandio na miwani ya Giza alisomewa tuhuma zake mbele ya Hakimu Mkazi Willbard Mashauri. Hata hivyo, ameachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama.

Mahakama ilimtaka Masogange kuwekwa dhamana ya milioni kumi hali kadhalika na wadhamini wake wawili nao walitakiwa kuwekwa kiasi hicho cha fedha.

Aidha mahakama imemuamuru kutosafiri nje ya Dar ea Salaam bila ya kupata kibali cha Mahakama.Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa serikali, Constantine Kakula amedai kuwa kati ya Februari 7 na 14 mwaka huu katika Eneo na Wilaya isiyojulikana lakini ndani ya jiji la Dar es salaam, Masogange alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).

Katika hatua ya pili, Mshtakiwa Masogange siku na mahali pasipojulikana alitumia dawa za kulevya aina ya OXazempam.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.Masogange amekana kujihusisha na tuhuma hizo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 21, mwaka huu.

KASEJA MCHEZAJI BORA WA JANUARI LIGI KUU YA VODACOM


Golikipa wa timu ya Kagera Sugar, Juma Kaseja Juma amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom wa mwezi Januari kwa msimu wa 2016/2017.

Kaseja aliwashinda wachezaji Mbaraka Abeid pia wa Kagera Sugar na Jamal S. Mtengeta wa Toto African.

Katika mechi tatu ambazo timu ya Kagera ilicheza kwa mwezi huo, Kaseja ambaye alicheza kwa dakika zote 270 alikuwa kiongozi na mhimili wa timu na aliisaidia timu yake kupata ushindi katika michezo yote ambapo ilikusanya jumla ya pointi 9 zilizoifanya timu hiyo kupanda nafasi mbili katika msimamo wa ligi kwa mwezi huo wa Januari (kutoka nafasi ya 5 hadi ya 3).

Katika michezo hiyo mitatu, Kagera Sugar ilifunga mabao sita na Kaseja alifungwa bao moja tu na alionesha nidhamu ya hali ya juu ikiwemo kutopata onyo lolote (kadi).

Kwa kushinda tuzo hiyo, Kaseja atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.

WAZIRI WA MICHEZO NAPE KUZINDUA MFUKO WA KUSAIDIA SERENGETI BOYS


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Nape Nnauye (Mb) kesho Februari 23, 2017 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa miguu kwa vijana na wanawake.

Uzinduzi huo utakaofanyika saa 5.00 asubuhi, utahudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Mkurugenzi wa Michezo, Yussuph Singo. Utafanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Courtyard, Upanga jijini Dar es Salaam.

Mfuko huo uko chini ya Mwenyekiti Bw. Tido Mhando ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Azam Media wakati Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo ni Bw. Dereck Murusuri.

Wajumbe wake ni Bi. Beatrice Singano, Bw. Ephraim Mafuru, Bw. Tarimba Abbas, Bw. Joseph Kahama, Bw. Salum Rupia na Bw. Meshack Bandawe. Majukumu ya Kamati ya Mfuko huo ni kukusanya rasilimali kwa ajili ya kuendeshea program za TFF za maendeleo ya mpira wa vijana wa wanawake.

Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, mfuko huu ni huru, una sekretariet yake, akaunti yake benki na ofisi zake zinazotarajiwa kuwa Mikocheni, Dar es Salaam.

Tuesday, February 21, 2017

SERIKALI YAZIONYA SIMBA NA YANGA


Ndugu Watanzania Jumamosi, tarehe 25/02/2017 saa 10.00 jioni Uwanja wa Taifa tutakuwa na mchezo mkubwa wa kati ya Simba SC na Yanga FC.

Ikumbukwe kuwa mchezo uliopita wa timu hizi uliochezwa kwenye uwanja huu tarehe 1/10/2016 zilitokea vurumai zilizosababisha Serikali kuufungia Uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu.Vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa miundombinu ikiwemo uvunjifu wa viti,mageti na mbaya zaidi baadhi ya watu walijerehuliwa.

Tunaomba waandishi na wadau wote tushirikiane kuelimisha umma wa wapenda michezo kuwa Michezo ni Furaha, Amani na Upendo.

Kuelekea mchezo ujao tungependa kueleza yafuatayo:-

Tunawaomba wadau wote tujenge utamaduni wa kununua tiketi mapema kwani mpaka sasa tiketi zinapatikana kupitia SELCOM. Hii itaondoa msongamano na lawama zisizo za lazima.

Tunafahamu kuwa kuna changamoto za matumizi ya mfumo wa Ki- elektroniki lakini hatuna budi kuendelea kuelimishana na kujifunza kwani huko ndiko Dunia ilipo,tutakua watu wa ajabu leo tukisema hatuwezi kutumia mfumo huu kisa changamoto hizi ndogondogo zinazojitokeza.

Tujiepushe na vurugu za aina yoyote siku ya mchezo kwani Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayepelekea uvunjifu wa amani siku ya mchezo.

Kutakua na ulinzi wa kutosha ndani na nje ya Uwanja hasa ukichukulia kuwa kuna kamera zenye uwezo wa kumuona kila mtu anayeingia Uwanjani na kila anachokifanya.Tutapiga picha na kuzirusha kwenye TV kubwa ya Uwanja kwa wale wote watakaobainika kuashiria/kutenda vurugu sheria itachukua mkondo wake.

Tunatoa rai kwa waamuzi waliopewa dhamana ya kuchezesha mchezo huu,wajue kuwa wana dhamana kubwa hivyo ni vyema wakafuata kanuni na sheria za mchezo husika ili kuepusha malalamiko.

Mwisho napenda niwatakie mchezo mwema kwa timu zote wajue kuwa Watanzania wanategemea burudani nzuri kutoka kwao,na niwaombe mashabiki wakumbuke kuwa wajibu wao mkuu ni kuzishangilia na kuzipa hamasa timu zao na si vinginevyo.

HUSSEIN MACHOZI KUVUNJA UKIMYA NA ‘NIPE SIKUACHI’ CHINI YA COMBINATION SOUND


Baada ya kukaa kimya kwa miezi mingi bila kuachia wimbo, Hussein Machozi anatarajia kuachia wimbo mpya wiki chache zijazo. Wimbo huo unajulikana kwa jina la ‘Nipe Sikuachi.’

Wimbo huo umetayarishwa na mshindi wa tuzo ya mtayarishaji bora wa Bongo Flava katika miaka tofauti, Man Walter kupitia studio zake za Combination Sound.

“Combination yangu ya mimi na Man Walter, sidhani kama kuna kitu cha mchezo hapo,” anasema Machozi ambaye amethibitisha kuanza kufanya kazi rasmi kwa uangalizi wa label ya mtayarishaji huyo mashuhuri nchini Tanzania.

“Man Walter ni mshkaji kitambo, tumekutana tukakubaliana kufanya kazi na tukaona kabisa kwamba sisi tukifanya kazi wawili itakuwa kazi na ndicho kilichofanyika japo tuna makubaliano ya kusaini. Kwahiyo ni mimi tu nirudi Tanzania tuje tukae tusaini, lakini ukweli ni kwamba mimi nafanya kazi chini ya uongozi wa Kombinega,” amesema.

“Video pia imefanyika Italy, Gressoney Italy. Kuna mabadiliko makubwa ukiangalia location ambazo tumezizoea, ukiangalia video ambazo kila siku tunaziona Tanzania za magari na majumba,” amesisitiza muimbaji huyo.

Machozi ambaye anafahamika kwa vibao vingi vilivyowahi kufanya vizuri kwenye vituo vya redio na runinga ndani na nje ya Tanzania vikiwemo ‘Utaipenda’, ‘Kwaajili Yako’, ‘Addicted’ na zingine, amedai kuwa ukimya wake ulitokana na majukumu mengine ya kimaisha.

“Kama unavyojua, hakuna mtu anapenda kuwa kimya, na ukifuatilia vizuri kuna kazi kadhaa nilishawahi kuziachia lakini hazikufika nilikotarajia nadhani kwasababu ya ukosefu wa management.

Kwa sasa Hussein anaishi nchini Italia baada ya kuwa ameenda kusoma, lakini hiyo haimaanishi kuwa ameupa kisogo muziki, kitu anachoamini alizaliwa kukifanya.

“Ilikuwa ni kozi fupi ambayo kwa sasa imeisha na nafanya shughuli za kawaida kujipatia riziki,” anaeleza.

Machozi anakikisha kuwa ujio wake mpya utakuwa wa tofauti.

“Kinachokuja kuonekana sasa hivi, hakijawahi kuonekana katika macho ya watu na nimejaribu kufanya hivyo kwasababu mimi mwenyewe nahitaji mabadiliko, nifanye kitu ambacho ni kipya zaidi hata kwenye macho yangu mimi, kwahiyo nimekikubali kwamba  ni kipya, video ni mpya, audio ni mpya kabisa.”

Anasema tarehe rasmi ya kutoka kwa video na wimbo itatangazwa hivi karibuni.

Thursday, February 16, 2017

DIAMOND AKAMATWA NA POLISI, ATOZWA FAINI


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond', jana alitiwa mbaroni na kikosi cha polisi cha usalama barabarani.

Manji alifikishwa kwenye kituo hicho kwa kosa la kuendesha gari huku akiimba wimbo wake wa Marry You' huku akiwa akiachia usukani mara kwa mara, akiwa hajafunga mkanda wa gari.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye kituo hicho cha polisi, Diamond anadaiwa kutenda kosa hilo Jumamosi iliyopita, siku ambayo mwanawe wa pili wa kike alikuwa akitimiza umri wa siku 40.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mohamed Mpinga, alikuwa miongoni mwa maofisa wa polisi walioshiriki kumuhoji msanii huyo.

Kamanda Mpinga alikiri kukamatwa kwa msanii huyo na kutiwa hatiani kwa makosa mawili, moja la kuendesha gari akiwa ameachia usukani na la pili kutofunga mkanda.

"Imebidi alipe faini kwa sababu makosa hayo mawili adhabu yake ni kulipa faini. Amelipa faini shilingi 60,000 kwa sababu kila kosa adhabu yake ni faini ya shilingi 30, 000,"alisema.

Kamanda Mpinga alisema makosa aliyokutwa nayo Diamond, yamekuwa yakifanywa na watu wengi wanapoendesha magari hivyo kukabiliwa na adhabu hizo.


Wednesday, February 15, 2017

MALINZI AIPONGEZA LIPULI KUPANDA DARAJA



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameuandikia barua uongozi wa Lipuli ya Iringa kwa mafanikio ya kupanda daraja msimu huu kutoka Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimuwa 2017/18.

Lipuli ya Iringa imepanda daraja baada ya kupita miaka 17 na Rais Malinzi amesema katika barua yake hiyo kwenda kwa Katibu Mkuu wa Lipuli, akisema: “Nitumie fursa hii kukupongeza wewe, uongozi wa klabuy ako, benchi la ufundi na wadau wote wa timu ya Lipuli kufuatia kupanda daraja kwenda Ligi Kuu.

“Bila shaka ni kazi kubwa imefanyika ikihusisha kujitolea kwa ari na mali kuhakikisha mnafika hapa mlipo,” ilisema barua hiyo na kuongeza: “Rai yangu kwenu ni kuongeza juhudi na kuendesha klabu kwa weledi mkubwa zaidi ili muweze kuwa washindani wa kweli katikal igi.”

Lipuli iliyo kuwa kundi “A” imepanda daraja na kuzipiku timu zaK iluvya United ya Pwani, Pamba ya Mwanza, African  Sports yaTanga, Polisi Dar, Ashanti United, Friends Rangers, Mshikamano za Dar es Salaam.

LIGI YA WANAWAKE SITA BORA TANZANIA BARA KUANZA FEBRUARI 18


Baada ya timu sita (6) kutinga hatua ya Sita Bora yaLigi Kuu ya Wanawake ya Shirilkisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kufahamika,ratiba rasmi ya michuano hiyo, imetoka na inaonyesha kuwa hatua hiyo ya kutafuta bingwa wa msimu, itaanza Februari 18, mwaka huu.

Timu sita zilizofanikiwa kufika hatua ya Sita Bora ni JKT Queens ya Dar es Salaam, Mlandizi Queens ya Pwanina Fair Play ya Tanga kutoka Kundi “A” wakati kutoka Kundi “B” zimo Marsh Acedemy ya Mwanza, Sisterz ya Kigoma na Panama ya Iringa.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kutakuwa na mechi mbili kila siku katika kituo kimoja kwa mujibu wa kanuni. Kituo hicho ni Uwanja wa Karume, ulioko Ilala jijini Dar es Salaam ambako mchezo wa kwanza utaanza saa 8.00 mchana wakati mwingine utaanza saa 10.00 jioni.

Ratiba inaonesha kwamba siku ya Februari 18,mwaka huu kutakuwa na mchezo Kati ya JKT Queens na Mlandizi saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 kutakuwa na mchezo kati ya Fair Play na Sisterz.

Februari 20, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Marsh Academy na Panama saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Mlandizi na Fair Play.

Februari 22, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Sisterz na Marsh Academy saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Panama na JKT Queens.

Februari 24, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Fair Play na JKT Queens saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Marsh Academy na Mlandizi Queens.

Februari 26, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Panama na Sisters saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya JKT Queens na Marsh Academy.

Februari 28, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Sisters na Mlandizi Queens saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Panama na Fair Play.

Machi 2, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Marsh Acedemyna Fair Play saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Mlandizi na Panama.

Machi 3, mwaka huu kutakuwa na mchezo mmoja tus aa 10.00 jioni ambako JKT Queens watamaliza na Sisterz.

SIMBA YAPANIA KULIPA KISASI DHIDI YA AFRICAN LYON KOMBE LA AZAM FC


Raundi ya Sita ya mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) yaani Azam Sports Federation Cup – 2016/17, itaanza Februari 16, 2017 badala ya Februari 24, mwaka huu. Mchezo huo awali ulipangwa kufanyika Machi mosi, 2017.

Kutakuwa na mchezo mmoja kabla ya kuendelea tena Februari 24, mwaka huu, kwa michezo minne kuchezwa kwa siku hiyo kuanzia saa 10.00 jioni kasoro mchezo mmoja tu utakaopigwa saa 1.00 jioni.

Michezo hiyo kwa mujibu wa ratiba inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), itakuwa ni kati ya Madini FC ya Arusha na JKT Ruvu yaP wani watakaocheza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Kagera Sugar itacheza Stand United ya Shinyanga Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Mechi nyingine itakuwa ni kati ya The Mighty Elephant ya Ruvuma na Ndanda FC ya Mtwara zitakazopambana kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ilihali Azam naMtibwa Sugar watacheza Chamanzi –Mbagala – mchezo utakaofanyika saa 1.00 usiku.

Jumapili Februari 26, mwaka huu timu yaM bao FC itacheza na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Tanzania Prisons itacheza na Mbeya City zote za Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Machi 7, mwaka huu Young Africans SC itacheza na Kiluvya United kwenyeUwanja waTaifa jijini Dar Es Salaam.

MAYANGA AKABIDHI PROGRAMU YA MIEZI SITA YA TAIFA STARS KWA TFF


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea programu ya miezi sita ya timu ya taifa, Taifa Stars kutoka kwa kocha wa muda, Salum Mayanga, anayekaimu nafasi iliyoachwa wazi na Charles Boniface Mkwasa ambaye kwa sasa ni Katibu wa Yanga SC.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema kwamba programu hiyo itahusisha kambi za mazoezi na michezo ya kirafiki.
Mapunda amesema kwamba kwa ujumla Mayanga amewasilisha programu ya maandalizi ya kufuzu kwa Fainali za Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
“Michezo ya kirafiki ni kocha Mayanga ndiye atapendekeza ichezwa nje ya nchi au ndani, lakini pia programu hiyo inaelezea juu ya maandalizi ya mechi ya CHAN ya 2018 na AFCON ya 2019 Cameroon,”amesema Lucas.
Taifa Stars itaanza na Rwanda katika kuwania tiketi ya CHAN mwakani nchni Kenya na mechi ya kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kati ya Julai 14 na 16 kabla ya timu hizo kurudiana Uwanja wa Amahoro, Kigali kati ya Julai 21 na 23.
Ikifanikiwa kuitoa Rwanda, Tanzania itamenyana na mshindi kati ya Uganda na ama Sudan Kusini au Somalia katika Raundi ya Tatu ya mchujo mechi ya kwanza ikichezwa kati ya Agosti 11, 12 na 13 na marudiano kati ya Agosti 18, 19 na 20, mwaka huu.
Tanzania imewahi kushiriki mara moja tu fainali za CHAN, ambayo ilikuwa ni mwaka 2009 zikifanyika kwa mara ya kwanza kabia.
Kwa upande wa AFCON, Taifa Stars imepangwa Kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho.
Mshindi wa kila kundi atafuzu moja kwa moja AFCON ya 2019, wakati timu nyingine tatu zitakazomaliza nafasi ya pili na wastani mzuri zaidi ya nyingine zitafuzu kama washindi wa pili bora.
Tanzania imewahi kucheza mara moja tu fainali za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilitolewa hatua ya makundi.

Monday, February 13, 2017

YANGA YAWATEMBEZEA KICHAPO KIKALI WACOMORO


WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya soka ya klabu bingwa Afrika, Yanga jana walianza vyema michuano hiyo baada ya kuitandika Ngaya FC ya Comoro mabao 5-1 mjini Coron.

Wafungaji wa mabao ya Yanga walikuwa Justin Zullu, Amis Tambwe, Juma Mahadhi, Simon Msuva na Obrey Chirwa.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa inahitaji sare ya aina yoyote katika mechi ya marudiano ili iweze kusonga mbele katika michuano hiyo.

Timu mbili hizo zinatarajiwa kurudiana Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


TAMASHA LA BUSARA LAFANA ZANZIBAR

Vijana wa Rico & the band ya zanzibar wakitumbuiza siku ya pili ya Tamasha la sauti za Busara kwenye ukumbi wa Ngomekongwe mjini Zanzibar jana.

Msanii Mirza wa Rico & the band ya zanzibar akichekecha muziki kwenye ukumbi wa Ngomekongwe jana.
Wanamuziki wa bendi ya Loryzine kutoka Reunion wakicheza kwenye jukwaa mbele ya mashabiki kwenye ukumbi wa Ngomekongwe mjini Zanzibar jana.
Wapenzi wa muziki wakiwashangilia vijana wa Loryzine jana usiku.

AROBAINI YA DIAMOND YAFANA DAR, AMUONYESHA MTOTO WAKE HADHARANI




Sunday, February 12, 2017

SIMBA YAREJEA KILELENI LIGI KUU


SIMBA imerejea kwenye uongozi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara kwa kishindo baada ya kuibugiza Prisons mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo iliyoonekana kuwa ya upande mmoja, Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo, hasa safu ya kiungo kutokana na Kocha Joseph Omog kuwapanga wachezaji wengi wa safu hiyo.

Iliwachukua Simba dakika 18 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Juma Luizio baadaya kuunganisha wavuni krosi kutoka kwa beki Javier Bokungu.

Ibrahim Ajib aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 28 baada ya gonga safi kati yake na Laudit Mavugo. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Mavugo aliihakikishia Simba ushindi dakika ya 68 baada ya kufunga bao la tatu, akisindikiza wavuni krosi kutoka kwa Ajib.

Wednesday, February 8, 2017

KEMONDO SUPER FC KUSHUSHWA DARAJA



Timu ya Kimondo Super SC imeshushwa madaraja mawili (hadi Ligi ya Mkoa), na matokeo ya mechi zake zote ilizocheza katika kundi la B yamefutwa kwa kushindwa kufika uwanjani kucheza mechi dhidi ya JKT Mlale bila sababu za msingi.

Mechi hiyo namba 47 (JKT Mlale vs Kimondo Super SC), ilitakiwa kuchezwa Januari 28, 2017 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, lakini Kimondo Super SC haikutokea uwanjani wala kutoa taarifa yoyote hadi Februari 1, 2017 ilipotuma taarifa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), na kutoa sababu ambazo hazikukubaliwa na Kamati.

 Pia Kimondo Super SC imetozwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili) ambapo kati ya hizo sh. 1,000,000 (milioni moja) itachukuliwa na TPLB, na sh. 1,000,000 (milioni moja) italipwa JKT Mlale. Adhabu dhidi ya Kimondo Super SC ni utekelezaji wa Kanuni ya 28(1) na (2) ya Ligi Daraja la Kwanza.

RAUNDI YA SITA AZAM SPORTS FEDERATION CUP 2016/2017

Raundi ya Sita ya mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) yaani Azam Sports Federation Cup – 2016/17, itaanza Februari 24, 2017 kwa michezo minne kuchezwa kwa siku hiyo kuanzia saa 10.00 jioni kasoro mchezo mmoja tu utakaopigwa saa 1.00 jioni.

Michezo hiyo kwa mujibu wa ratiba inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), itakuwa ni kati ya Madini FC ya Arusha na JKT Ruvu ya Pwani watakaocheza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Kagera Sugar itacheza Stand United ya Shinyanga Uwanja wa kaitaba mjini Bukoba.

Mechi nyingine itakuwa ni kati ya The Mighty Elephant ya Ruvuma na Ndanda FC ya Mtwara zitakazopambana kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ilihali Azam na Mtibwa Sugar watacheza Chamanzi –Mbagala – mchezo utakaofanyika saa 1.00 usiku.

Jumapili Februari 26, mwaka huu timu ya Mbao FC itacheza na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Tanzania Prisons itacheza na Mbeya City zote za Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Jumatano Machi 1, 2017 Simba SC itacheza na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam wakati Machi 7, mwaka huu Young Africans SC itacheza na Kiluvya United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam.

KOCHA MOROCCO AFUNGIWA MECHI TATU



Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72), imemfungia Kocha wa Stand United, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kushiriki michezo mitatu uwanjani na faini ya Sh 500,000 (laki tano).

Katika mechi Na. 160 ya Ligi Kuu ya Vodacom uliozikutanisha timu za JKT Ruvu na Stand United iliyochezwa Januari 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Morocco aliondolewa kwenye benchi (Ordered off) kwa kosa la kupiga maamuzi ya mwamuzi na kutoa lugha chafu.

Kamati hiyo ya Saa 72 imechukua hatua hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 40 (11) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa Makocha. Morocco hata kama atakuwa amemaliza mechi tatu nje ya benchi, hataruhusiwa kukaa kwenye benchi hadi awe amelipa faini hiyo.

Adhabu hiyo ya Morocco itaendelea kumhusu hata kama utakuwa umehamia kwenye timu nyingine na katika msimu mwingine wowote.

Saturday, February 4, 2017

SIMBA YAIPUMULIA YANGA


 Timu ya Simba imekoleza mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuifanyia mauaji Majimaji kwa kuifunga mabao 3-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Alikuwa Ibrahim Ajibu aliyewanyanyua mashabiki wa Simba dakika ya 19, akifunga bao kwa kichwa, akimalizia pasi ya Shiza Kichuya. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko, ambayo hata hivyo yaliisaidia zaidi Simba iliyofanikiwa kuongeza bao la pili dakika ya 64 kupitia kwa Said Ndemla.

Zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo kumalizika, Laudit Mavugo aliiongezea Simba bao la tatu na kuifanya itofautiane kwa pointi moja na vinara wa ligi hiyo Yanga.

YANGA YAZIDI KUCHANJA MBUGA LIGI KUU, YAITANDIKA STAND UTD MABAO 4-0

MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, wameendelea kung'ara baada ya kuitandika Stand Utd ya Shinyanga mabao 4-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya Yanga yalifungwa na Donald Ngoma, Simon Msuva, Obrey Chirwa na beki Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Kutokana na ushindi huo, Yanga inaendelea kuongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 49 baada ya kucheza mechi 21, ikifuatiwa na watani wao wa jadi Simba, wenye pointi 44 baada ya kucheza mechi 20.

Dalili za Yanga kuibuka na ushindi zilianza kujionyesha mapema baada ya Ngoma kuifungia bao la kuongoza dakika ya 17, alipounganisha wavuni kwa kichwa krosi ya Msuva.

Msuva, ambaye kwa sasa anaongoza kwa ufungaji mabao katika ligi hiyo, aliongeza bao la pili dakika ya 26 baada ya kuunganisha wavuni krosi kutoka kwa Haruna Niyonzima. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Mzambia, Chirwa aliiongezea Yanga bao la tatu dakika ya 46 baada ya kupokea pasi kutoka kwa kiungo Thabani Kamusoko, kabla ya Cannavaro kuongeza la nne dakika ya 68, akimalizia kona iliyopigwa na beki Juma Abdul.

SERENGETI BOYS YAFUZU FAINALI ZA KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA

Timu ya Taifa ya Tanzania ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys, imefuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo.

Taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), imethibitisha hilo pasi shaka kwamba Tanzania ndiyo yenye nafasi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Aprili 2, mwaka huu huko Gabon baada ya Madagascar kuenguliwa kutokana na kutoandaa vema fainali hizo.

Taarifa hizo za CAF kutoka Libreville, nchini Gabon zinathibitisha kwamba Kamati ya Utendaji ya CAF imeipa ushindi Tanzania dhidi ya timu ya Jamhuri ya Congo ambayo katika michuano ya kufuzu, ilimchezesha mchezaji Langa Lesse Bercy aliyezidi umri kinyume cha kanuni za kanuni za michuano hiyo.

Serengeti Boys iliyosimamiwa na Kamati ya Utendaji ya TFF chini ya Rais Jamal Malinzi, sera kubwa ilikuwa ni kuangalia kuendeleza mpira wa miguu kwa vijana, ilikusanywa na kuandaliwa kwa michezo mingi ya kimataifa ambako kwa mwaka moja tu 2016, ilicheza mechi zisizopungua 16 ya kimataifa.

Katika michezo hiyo ya kirafiki na ushindani, Serengeti Boys ilipoteza mchezo wa 16 tu dhidi ya Congo ilihali kulikuwa na rufaa kuhusu mmoja wa wachezaji wa Congo ambaye alionekana kuwa na umri mkubwa. Mchezaji huyo ni Langa Lesse Bercy.

CAF, kwa nyakati tofauti ikiwamo Novemba 10, 2016 na Desemba 15, mwaka jana walitoa agizo kwa Congo Brazzaville kumpeleka kijana huyo Cairo, Misri kwa ajili ya vipimo vya MRI ili kuthibitisha au kupangua madai ya Tanzania. Congo Brazzaville hawakupeleka.

Januari 12, mwaka huu 2017 iliamriwa kwa mara nyingine kijana huyo kupelekwa jijini Libreville, Gabon ili kufanyiwa vipimo vya MRI, lakini hakupelekwa na katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya CAF, kimeamua kumaliza suala hilo na kuipa ushindi Tanzania.

Siku 10 ziliisha Januari 23, mwaka huu lakini tangu hapo kumekuwa na maswali ya kutosha kuhoji nafasi ya Tanzania yakitoka kwa Watanzania kupitia wanahabari, lakini TFF ilisimama kidete kutangaza kuwa tunasubiri uthibitisho wa CAF ambayo leo Februari 3, mwaka huu imetangaza rasmi kuwa Tanzania itacheza fainali hizo.

 

Thursday, February 2, 2017

FIFA YAIAMURU YANGA KUMLIPA BRANDTS DOLA 11,000 ZA MAREKANI




Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), limeitaka Klabu ya Young Africans ya Dar es Salaam kulipa mara moja deni la aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ernst Wilhelmus Johannes Brandts – Raia wa Uholanzi waliyevunja naye mkataba miaka miwili iliyopita.
Klabu ya Young Africans imetakiwa kulipa dola 11,000 za Marekani kama ambavyo iliamriwa Juni 30, 2015 na Kamati ya Hadhi ya Wachezaji ya FIFA.    
Kutolipa deni hilo kwa wakati, imetafsiriwa kwamba Yanga imevunja Kanuni ya 64 inayozungumzia Nidhamu katika FIFA yaani FDC (FIFA Disciplinary Committee).
Yanga inakabiliwa adhabu za kupigwa faini zaidi ya awali, kukatwa pointi katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoendelea kwa sasa au kushushwa daraja.
Kamati hiyo ya Nidhamu inatarajiwa kukutana wakati wowote wiki ijayo na suala la Nidhamu ya Yanga litakuwa ajenda ili kama hawakulipa, watachukua hatua kama adhabu zinavyojieleza hapo juu
TFF imeagizwa haraka kufuatilia suala la deni hilo katika klabu ya Yanga na kurudisha majibu FIFA. TFF kupitia Katibu Mkuu, imeagizwa kupeleka barua ya FIFA katika Makao makuu ya Klabu hiyo, yaliyoko kwenye makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.
“TFF tumeliweka wazi suala hilo kama ‘Tahadhari kabla ya hatari’, kwani tungeweza kufanya mawasiliano kati ya shirikisho (TFF) na klabu (Young Africans) kwa siri tu, lakini ikitokea huko mbele klabu inakutana na adhabu mojawapo, lawama hushuka TFF kwa madai kwamba tumekalia taarifa muhimu ya kuchukuliwa hatua haraka,”imesema taarifa ya TFF leo.

Wednesday, February 1, 2017

MKWASA ATEULIWA KUWA KATIBU MKUU MPYA YANGA



MCHEZAJI na kocha wa zamani wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa leo ametambulishwa rasmi kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, akichukua nafasi ya Baraka Deusdedit anayerejea kwenye Idara yake ya Fedha.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kwamba Mkwasa anaanza majukumu yake rasmi Februari 1, mwaka huu.
Sanga alisema kuwa sababu kubwa ya kumchagua Mkwasa ni kuhimarisha safu ya uongozi wa klabu hiyo  ambapo aliyekuwa kaimu katibu mkuu, Baraka Deusdedit anarejea katika nafasi yake ya zamani ya Ukurugenzi wa Fedha.
“Najua wadau wa soka wanajiuliza kwa nini Mkwasa ameshika nafasi hiyo ya Ukatibu Mkuu kwa sabab ya taaluma yake inayojulikana ni ufundisha mpira wa miguu, siyo kweli, Mkwasa anauzoefu mkubwa katika kazi hiyo tofauti na watu wanavyomuelewa,”
“Na hii si mara ya kwanza, hata Zambia, Kalusha Bwalya amewahi kuwa katibu mkuu wa chama cha soka nchini humu huku wakijua kuwa ni mchezaji mstaafu au kocha, Yanga tumemuona Mkwasa ni bora ya zaidi katika nafasi hiyo,” alisema Sanga.
Mkwasa alishukuru kushika nafasi hiyo na kuahidi kuifikisha Yanga katika malengo yaliyowekwa. “Naomba nieleweke wazi kuwa mimi ni Katibu Mkuu wa Yanga na wala siyo kocha, najua kuna watu watafikiria kuwa narejea kwa mlango wa nyuma, kamwe sitaingilia masuala yoyote ya ufundi zaidi ya kufanya yale yaliyomo katika majukumu yangu,” alisema Mkwasa.
“Ninaomba ushirikiano kutoka kwa wanachama, mashabiki, viongozi wenzangu, sisi sote tupo hapa Yanga kwa ajili ya kuiletea maendeleo na si vinginevyo,” alisema.

Mkwasa anarejea Yanga ndani ya mwezi mmoja tangu aondolewe timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na nafasi yake kupewa Salum Mayanga.
Mkwasa aliifundisha Taifa Stars tangu Julai, mwaka 2015, baada ya kurithi nafasi ya Mholanzi, Mart Nooij na katika kipindi chake aliiongoza timu hiyo katika mechi 13, ikishinda mbili, kufungwa sita na sare tano.

SIMBA, YANGA ZAGOMA KUCHEZA NA MAMELODI SUNDOWN



KLABU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga zimegoma kucheza mechi za kirafiki za kimataifa na mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Yanga imegoma kucheza na vinara hao wa soka barani Afrika kwa kile kilichodaiwa kuwa, Kocha wake, George Lwandamina, amekataa kwa kuhofia wachezaji wake kuumia.

Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Lwandamina aligomea mechi hiyo kwa madai kuwa mchezo huo ungeingilia programu zake za maandalizi ya mechi za ligi kuu.

“Hatutacheza na Mamelodi kwa sababu kocha ameukataa huo mchezo, amesema unaingilia programu zake, kama unavyojua kwa sasa tupo kwenye hatua ngumu ya Ligi Kuu na wakati huo huo tunaingia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika,” kilisema chanzo cha habari.

Kufuatia Yanga kugomea mchezo huo, waandaaji wa mechi hiyo mbali na kusikitishwa na uamuzi huo, wamefanikiwa kuishawishi Azam kuchukua nafasi ya mabingwa hao wa soka nchini.

Mamelodi ilikuwa icheze na Simba jana kabla ya kuivaa Yanga kesho. Kutokana na mabadiliko hayo, mabingwa hao wa Afrika Kusini sasa kesho watacheza na Azam.

Mamelodi imekuja nchini kwa mwaliko wa klabu ya African Lyon, inayomilikiwa na Rahim Kangezi, kwa ajili ya kushiriki kampeni ya kupiga vita ujangili.

Kwa upande wa Simba, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu', amesema Kocha Joseph Omog aliwasilisha mapendekezo ya kugomea mechi hiyo.

Kaburu alimkariri Omog akisema kuwa, kwa sasa Simba haiwezi kucheza mechi hiyo kwa vile inashiriki kwenye ligi kuu na mechi zake zote zilizosalia ni muhimu.

Kiongozi huyo wa Simba alisema mchezo huo ulikuwa mzuri na muhimu kwao, lakini tatizo ni kwamba, umekuja katika wakati mbaya hivyo wanalazimika kuuacha.

SERIKALI YAZIPONGEZA TFF, KAMATI YA OLIMPIKI



SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema kwamba inaunga mkono juhudi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika programu za maendeleo ya vijana, hususani nia yake ya dhati kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo, Japan mwaka 2020.

Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Omari alisema hayo mara baada ya kusikia program za TFF kutoka kwa Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi na Makamu Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau katika hafla ya uzinduzi wa kampeni maalumu za kuifanikisha Tanzania kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki.

“Nimesikia programu mbalimbali za TFF, naona zinakuja wakati mwafaka. Nimewapongeze kwa mipango yenu mizuri kwa sababu inaleta matumaini. Jambo kubwa ambalo linanisukuma na kuwapongeza ni kuwa na program ya vijana, hatuwezi kufanikiwa kama hatutakuwa na program ya vijana.

“Serikali inatambua haya yote mnayofanya. Na ili kuboresha, Serikali imetenga shule 55 ambazo zitakuwa ni maalumu kwa ajili ya vijana, lengo ni kupata vipaji bora ambavyo vitakuwa vikiendelezwa, huku wakiwa wanapata elimu.

“Watanzania wana kiu kubwa ya mafanikio, lakini tunafikaje katika katika safari hii tunayoianza leo? Tutafika tu, iwapo kutakuwa na ushirikiano licha ya kutoangalia aina ya usafiri ambao tutatumia,” alisema Singo huku wadau wa mpira wa miguu wakimsikiliza kwa makini.

Aliendelea kusema: “Nasikia mmeunda Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu hususani vijana. Ni jambo zuri, lakini rai yangu ni kwamba watakaunda kamati ya mfuko huo wawe watu respected ili wananchi waipende na ikiwa hivyo itafanikiwa. Sisi Serikali tutafanya kazi bega kwa bega na kamati hiyo. Jambo kubwa, ni kwamba lazima tukutane mara kwa mara.”

Kabla ya Mkurugenzi Singo kuzungumza, Makamu Rais wa TOC, Ndugu Tandau, alipongeza pia harakati za kuanza mapema akisema: “Shukrani TFF kwa kuthamini TOC. Ni vizuri tumeanza mapema. Michuano ya Olimipiki ni mikubwa na inahitaji timu zenye viwango vya juu kufanikiwa kufuzu.”

Alieleza hadhara iliyohudhuria hafla hiyo, kuwa TOC inakuwa na Mawasiliano ya maandalizi Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki inayoitwa ‘Olympic Solidarity Program’ ambayo hutoa sehemu ya fungu ya maandalizi na kwamba TFF haina budi kuwasilisha program yake kwa ajili ya kuingia kwenye bajeti ambayo inaitwa ‘Team Support Grant’.

“Sasa tuwe kitu kimoja toka huu mwanzo na mambo yaende kwa uwazo na kupeana taarifa kila wakati,” alisema Tandau.

Awali kabla ya viongozi hao kuzungumza, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema kinachofanywa sasa na Shirikisho si kutafuta miujiza kwenye matokeo badala yake ni kujenga timu (Maandalizi) kwa dhana kwamba “Timu za Taifa haziokotwi kama embe dodo.”

“Mhe. Mkurugenzi, kujenga timu hizi ni gharama kubwa. Hata matunda ambayo tunasubiri moshi mweupe ya timu ya vijana, hayakutokea hivi hivi ni maandalizi. Si ajabu kabla ya mwisho wa wiki hii tukaona moshi mweupe,” alisema Malinzi.

Alisema ili vijana wa Tanzania waweze kufanya vema, hakuna budi wadau wakiwamo Serikali, Kampuni, Mashirika ya umma na watu binafasi kusapoti mbio hizo za kwenda Tokyo, Japan pamoja na timu nyingine za taifa. “Program nzima ni gharama kubwa,”

Kadhalika, ili kutekeleza programu hiyo, Rais Malinzi alizungumzia utulivu katika kufanya kazi kwa sasa kwa kuwa historia inaonesha kuwa kumekuwa na nia ovu ya baadhi ya wadau kutaka kutibua mambo mazuri yanayofanywa na uongozi wa mpira wa miguu.

“Naomba tuelekeze mafanikio yetu kwa kushirikiana na kuutendea haki mpira wa miguu kwa kushirikiana kwa sababu soka ni furaha na ili kufanikiwa linahitaji juhudi za pamoja,” alisema Malinzi.