KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, February 4, 2017

YANGA YAZIDI KUCHANJA MBUGA LIGI KUU, YAITANDIKA STAND UTD MABAO 4-0

MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, wameendelea kung'ara baada ya kuitandika Stand Utd ya Shinyanga mabao 4-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya Yanga yalifungwa na Donald Ngoma, Simon Msuva, Obrey Chirwa na beki Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Kutokana na ushindi huo, Yanga inaendelea kuongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 49 baada ya kucheza mechi 21, ikifuatiwa na watani wao wa jadi Simba, wenye pointi 44 baada ya kucheza mechi 20.

Dalili za Yanga kuibuka na ushindi zilianza kujionyesha mapema baada ya Ngoma kuifungia bao la kuongoza dakika ya 17, alipounganisha wavuni kwa kichwa krosi ya Msuva.

Msuva, ambaye kwa sasa anaongoza kwa ufungaji mabao katika ligi hiyo, aliongeza bao la pili dakika ya 26 baada ya kuunganisha wavuni krosi kutoka kwa Haruna Niyonzima. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Mzambia, Chirwa aliiongezea Yanga bao la tatu dakika ya 46 baada ya kupokea pasi kutoka kwa kiungo Thabani Kamusoko, kabla ya Cannavaro kuongeza la nne dakika ya 68, akimalizia kona iliyopigwa na beki Juma Abdul.

No comments:

Post a Comment