KIPA namba moja wa klabu ya Simba, Juma Kaseja amegoma kujiunga na timu hiyo hadi atakapolipwa pesa zilizobaki za usajili wake wa msimu uliopita.
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, kipa huyo alilipwa pesa nusu za usajili msimu uliopita na kuahidiwa kuwa, angemaliziwa baadaye.
Hata hivyo, haikuweza kufahamika mara moja kiasi cha fedha alichoahidiwa kulipwa kipa huyo, fedha alizolipwa awali na zilizobaki.
Lakini uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, Kaseja aliahidiwa kulipwa sh. milioni 25 na Simba baada ya kusajiliwa msimu uliopita akitokea Yanga.
Kabla ya kurejea Simba, Kaseja aliichezea Yanga mwaka juzi baada ya kusajiliwa kwa kitita cha sh. milioni 45.
“Kaseja ameapa kwamba hatajiunga na kambi ya Simba hadi atakapomaliziwa pesa zake zilizobaki, ambazo aliahidiwa na uongozi uliopita,” kilisema chanzo cha habari ndani ya klabu hiyo.
Licha ya kutojiunga na kambi ya timu hiyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, Kaseja amekuwa akifanya mazoezi binafsi kwenye gym na viwanja mbalimbali vya soka.
Mbali na Kaseja, uchunguzi zaidi umebaini kuwa beki Kelvin Yondani naye hajaripoti kwenye kambi ya timu hiyo kutokana na kutomaliziwa baadhi ya pesa anazoidai klabu hiyo.
Wachezaji wengine wanaowaumiza vichwa viongozi wa Simba kutokana na kushindwa kuripoti kambini ni Emmanuel Okwi, Joseph Owino na Patrick Ochan, ambaye amesajiliwa msimu huu.
Simba ilianza kambi wiki iliyopita kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Agosti 21 mwaka huu.
Alipoulizwa kuhusu kutoripoti kwa wachezaji hao, Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uongozi hauna taarifa zozote.
Ndimbo alisema uongozi umeshaanza kufanya mawasiliano na wachezaji hao ili kujua matatizo yao kabla ya kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Hata hivyo, Ndimbo alisema baadhi ya wachezaji wa kigeni wameshawasili nchini na kuanza mazoezi na wenzao. Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Hilary Echessa na Jerry Santo kutoka Kenya.
Ndimbo alisema mazoezi ya timu hiyo yanafanyika chini ya Kocha Msaidizi, Amri Said kabla ya kurejea kwa Kocha Mkuu, Patrick Phiri, aliyeko Zambia kwa mapumziko. Alisema Phiri anatarajiwa kurejea nchini mwishoni mwa wiki hii.
No comments:
Post a Comment