LONDON, England
HALI ya mwanamuziki Cheryl Cole wa Uingereza bado tata na ilikuwa almanusura apoteze maisha kutokana na kuugua ugonjwa wa malaria.
Rafiki mmoja wa karibu na mwanamuziki huyo, alilieleza gazeti la Daily Mail la Uingereza wiki hii kuwa, hali Cheryl bado haijawa nzuri.
Cheryl (27) alipatwa na ugonjwa huo alipokuja Tanzania kwa mapumziko akiwa na rafiki yake mpya wa kiume, Derek Hough wiki tatu zilizopita
Kwa mujibu wa rafiki huyo, Cheryl amewekewa vifaa maalumu vya kumsaidia kupumua, kuongezwa maji mwilini na kwamba hawezi kuzungumza. Rafiki huyo alisema Cheryl amelazwa kwenye hospitali moja binafsi ya mjini London, alikopelekwa wiki iliyopita kwa ajili ya matibabu.
“Ilikuwa bado kidogo tumpoteze na bado anaendelea kutibiwa. Amedhoofika sana na ugonjwa huu nusura uyaondoe maisha yake,”alisema rafiki huyo.
“Tunamshukuru Mungu kwamba ugonjwa huu uligundulika mapema. Hadi sasa hawezi kuzungumza. Baadhi ya wakati anakuwa kwenye hali mbaya na wakati mwingine anapata nafuu, anachoweza kufanya ni kulia,”aliongeza rafiki huyo.
Rafiki huuo alisema ilikuwa vigumu kutoa taarifa za maendeleo ya hali ya mwanamuziki huyo kwa sababu ilikuwa ikibadilika mara kwa mara. Alisema walishindwa kuwahakikishia mashabiki kuhusu hali yake.
“Ukweli ni kwamba ilikuwa almanusura tumpoteze mtu wa pekee. Hawezi hata kuzungumza wala kuelewa kinachoendelea kwake. Inasikitisha,”alisema.
“Inasikitisha kumuona Cheryl akiwa katika hali hii. Angeweza kupoteza maisha. Bado hajapona, na wala hajakaribia kupona. Bado yupo kwenye hali mbaya,”aliongeza rafiki huyo.
Aliongeza kuwa, tangu alipolazwa kwenye hospitali hiyo siku sita zilizopita, amekuwa akisaidiwa kupumua kwa kutumia mashine maalumu na amekuwa akiwekewa chupa za maji mara kwa mara.
Kwa mujibu wa rafiki huyo, kinga za mwili za mwanamuziki huyo zimepungua na hawezi kupambana na magonjwa makubwa kama vile malaria.
“Hana kumbukumbu ya leo wala jana. Analia muda wote na huwa hataki mama yake awe mbali naye,”alisema rafiki huyo.
Awali, Cheryl alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya Chuo Kikuu cha London kabla ya kuhamishiwa kwenye hospitali moja binafsi ya mjini humo.
Mbali na wauguzi, watu wengine pekee wanaoruhusiwa kumuona mwanamuziki huyo ni mama yake mzazi, Joan Callaghan na rafiki yake wa karibu, Derek (25), ambaye amehamia kwenye nyumba ya Cheryl.
Baadhi ya marafiki wa mwanamuziki huyo wamekuwa wakimshutumu mumewe wa zamani, Ashley Cole, mchezaji wa klabu ya Chelsea ya England kuwa ndiye aliyemsababishia hali hiyo baada ya kutengana.
Cole, ambaye aliichezea England katika fainali za Kombe la Dunia zilizomalizika hivi karibuni nchini Afrika Kusini, yupo mjini California, Marekani alikokwenda kwa mapumziko na hajawahi kwenda hospitali kumjulia hali mwanamuziki huyo.
Mwanasoka huyo alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, kwa sasa Cheryl sio sehemu ya maisha yake na ameamua kumsahau moja kwa moja.
No comments:
Post a Comment