KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 8, 2010

REDONDO: Nitatisha zaidi nikiwa Azam FC




WAKATI usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara ukiendelea, mashabiki wengi wa soka wameanza kuitabiria makubwa Azam FC kutokana na kusajili wachezaji wengi nyota. Miongoni mwa wachezaji hao, ni kiungo mshambuliaji, Ramadhani Chombo ‘Redondo’. Katika makala hii iliyoandikwa na Mwandishi Wetu Athanas Kazige, mchezaji huyo kutoka Simba, anaelezea mambo mbalimbali kuhusu maisha yake kisoka.

SWALI:Nini kimekufanya uondoke ndani ya kikosi cha Simba wakati msimu ujao ungepata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya klabu bingwa Afrika?
JIBU: Nimeondoka Simba kwa ajili ya kutafuta maslahi mazuri zaidi, ambayo nimeahidiwa na uongozi wa Azam FC. Kama ni nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, naamini nitaipata nikiwa Azam kwa kushirikiana na wenzangu kutwaa ubingwa wa ligi msimu ujao.
SWALI: Inaelekea viongozi wa Azam wamekuahidi donge nono maana ulipata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa klabu ya Haras Al-Hadoud ya Misri, lakini umeitolea nje.
JIBU:Siwezi kukupa jibu la swali hilo kwa sababu linahusu masuala yangu binafsi na mwajiri wangu. Lakini safari ya kwenda Misri bado haijakufa. Bado naendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo hadi sasa.
SWALI: Umejifunza nini katika kipindi chote ulichoichezea klabu ya Simba, ambayo ni miongoni mwa klabu mbili kongwe hapa nchini?
JIBU: Yapo mambo mengi niliyojifunza ndani ya Simba. Lakini kikubwa ni changamoto ya kujituma ili kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Lakini pia nimeweza kuingia kwenye historia ya klabu hiyo kwa kuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Simba kuweka historia ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu kabla haijamalizika.
Hakuna jambo, ambalo ninajivunia zaidi kama kuchangia ushindi wa Simba katika ligi kuu kwani tuliweka rekodi ya kutofungwa hata mechi moja. Hili kwangu ni jambo kubwa. Naamini mchango wangu ulisaidia mafanikio haya.
SWALI: Kwa nini klabu hizi kubwa zinapofungwa, huwa kunatokea tuhuma kwa baadhi ya wachezaji kwamba wamehujumu timu? Ulikuwa ukijisikiaje ulipohusishwa na tuhuma za aina hii?
JIBU:Namshukuru Mungu kwamba haijawahi kutokea hata siku moja mimi kuhusishwa na tuhuma za kuhujumu timu ama kupanga matokeo. Binafsi nafahamu vyema maana ya uaminifu na uadilifu katika kazi ndio sababu pia sijawahi kugombana hata siku moja na kiongozi, mchezaji ama mwanachama wa klabu hiyo.
SWALI: Umesema kuondoka kwako Simba kumekufanya uwe huru. Je, ni kipi kilichokuwa kinakupa wakati mgumu katika klabu hiyo?
JIBU: Hakuna kilichokuwa kikinipa wakati mgumu Simba, isipokuwa kulikuwa na watu wenye tabia ya kuwakatisha tamaa wenzao. Ninachoweza tu kusema ni kwamba hivi sasa nipo huru na ninaamini nitaonyesha uwezo mkubwa zaidi katika ligi kuu ya msimu ujao.
SWALI: Kipi kilichowahi kukukera na kukunyima raha katika kipindi chote ulichokuwa ukiichezea Simba?
JIBU:Kwa kweli hakuna kitu kama hicho. Lakini kama wapo watu, ambao kwa namna moja ama nyingine nilitokea kuwaudhi, nawaomba wanisamehe kwa vile hakuna binadamu aliyekamilika. Inawezekana kabisa niliwafanyia maudhi bila kujitambua.
SWALI: Una matarajio gani katika timu yako mpya ya Azam, ukiwa na wachezaji wenzako wapya kama vile Mrisho Ngasa na Jabir Azizi?
JIBU: Nina hakika msimu ujao wa ligi nitacheza kwa kiwango cha juu zaidi ili niweze kupata ofa ya kujaribiwa nje ya nchi na pia kuipa ubingwa timu yangu mpya. Nina ndoto kubwa ya kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi.
Kinachonifurahisha zaidi ni kuona kwamba ndani ya Azam wapo wachezaji wengine wazuri wengi kama vile Ngasa, Jabir, John Boko, Salum Swedi na wengineo. Naamini tukishirikiana vyema, hakuna kitakachoikosesha Azam ubingwa.
Kadhalika nina furaha kubwa ya kuona ndani ya kikosi cha Azam kuna wachezaji wengi wazuri wakiwemo Ngasa,Boko,Salum Sued na wengine ambao nina hakika tutaweza kuifikisha mbali kwenye ligi kuu.
SWALI:Una maoni gani kuhusu kumalizika kwa mkataba wa kocha mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo?
JIBU: Binafsi nitamkumbuka sana kocha huyu kwani ameweza kutupa mafanikio makubwa wachezaji wa Tanzania na pia kutuelewesha vyema jinsi, ambavyo mchezo huu unavyoweza kuwa na manufaa kwetu kimaisha, tofauti na miaka ya nyuma, ambapo wengi tuliichukulia soka kama burudani.
Chini ya Maximo, tuliweza kucheza na timu nyingi ngumu za Afrika kama vile Cameroon, Senegal na Ivory Coast na kufanya vizuri. Pia tuliweza kucheza na mabingwa wa zamani wa dunia, Brazil na japokuwa tulifungwa, tuliweza kujifunza mengi kutoka kwao.
Pia napenda kuwapongeza Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwa kufanikisha ujenzi wa uwanja mpya wa Taifa wa Dar es Salaam na Rais Jakaya Kikwete kwa kuhamasisha kwa kiasi kikubwa mashabiki wa soka nchini kuipenda timu yao ya taifa. SWALI: Una maoni gani kuhusu tuhuma zinazotolewa dhidi ya waamuzi nchini kwamba wamekuwa wakipindisha kwa makusudi sheria za mchezo huo kwa sababu ya rushwa ama mapenzi kwa timu kubwa?
JIBU: Ni kweli baadhi ya waamuzi nchini wamekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya mchezo huo kutokana na kuvurunda katika uchezeshaji wao. Wengi wanashindwa kuheshimu sheria 17 za soka kwa sababu tu ya mapenzi ama kuhadaiwa na rushwa.
Nawashauri waamuzi wetu wabadilike kwa sababu wakiendelea hivyo, soka ya Tanzania itaendelea kudumaa badala ya kusonga mbele. Hatutaweza kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa kwa sababu timu zetu zimezoea kubebwa katika ligi za nyumbani.
Ni vizuri bingwa wa nchi apatikane kutokana na uwezo wake kisoka ili aweze kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa. Akipatikana bingwa kwa kubebwa, ni rahisi kuvurunda kwenye michuano ya kimataifa kwa sababu huko hakuna kubebwa.

No comments:

Post a Comment