MHARIRI wa gazeti la Burudani, Rashid Zahor (kushoto) akikabidhi fulana yenye nembo za magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani kwa kiongozi wa bendi ya Mlimani Park Orchestra, Habibu Abbas 'Jeff' (kulia) wakati wa onyesho la bendi hiyo lililofanyika juzi kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni msemaji mkuu wa bendi hiyo, Jimmy Chika na wa pili kulia ni mwimbaji, Hassan Kunyata. (Picha na Emmanuel Ndege).
KAMPUNI ya Uhuru Publications Limited (UPL), wachapishaji wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, imetoa fulana 20 kwa wanamuziki wa bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra.
Fulana hizo zilikabidhiwa kwa kiongozi wa bendi hiyo, Habibu Abbas ‘Jeff’ na Mhariri wa gazeti la Burudani, Rashid Zahor wakati wa onyesho lililofanyika juzi kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fulana hizo, Zahor alisema kampuni yake imefikia uamuzi huo ili kuonyesha jinsi ilivyo bega kwa bega na bendi za muziki wa dansi nchini katika masuala yanayohusu burudani.
Zahor, maarufu kwa jina la Ramoza alisema, kampuni hiyo kupitia magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, imejitolea kuchapisha mara kwa mara taarifa zinazohusu bendi hiyo ili mashabiki waweze kupata habari zake.
“Sikinde ni moja ya bendi kongwe na zinazoheshimika hapa nchini, ikiwa na wanamuziki wengi mahiri, hivyo kupitia magazeti yetu haya matatu, tutakuwa tukichapisha habari zake mara kwa mara,”alisema.
Kwa upande wake, Jeff aliishukuru UPL kwa kuonyesha mshikamano na bendi yake, ikiwa ni pamoja na kuwajali wanamuziki wake na kuripoti habari zake mara kwa mara.
“Msaada huu unaweza kuonekana ni mdogo, lakini kwetu sisi ni mkubwa kwa vile umeonyesha jinsi magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani yanavyoijali bendi yetu,”alisema.
Mbali na kuipatia Mlimani Park Orchestra fulana hizo, UPL pia iliwazawadia mashabiki wawili, fulana moja kila mmoja kutokana na kuonyesha mapenzi makubwa kwa bendi hiyo.
Mmoja wa mashabiki waliozawadiwa fulana hizo ni Shabani Jiwe, ambaye ni nadra kukosekana kwenye maonyesho ya bendi hiyo yanayofanyika kila Jumapili kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo.
Mwingine ni Kibibi Saidi, ambaye alitia fora katika onyesho la juzi kutokana na kujimwaga stejini kucheza vibao vyote vilivyopigwa na bendi hiyo. Stella alijitambulisha kuwa ni shabiki wa Sikinde tangu mwaka 1978.
Katika muda wote wa onyesho hilo, wanamuziki wa Mlimani Park Orchestra walikuwa wamevalia fulana zilizotolewa na UPL, zenye nembo ya magazeti ya Uhuru na Mzalendo.
Wakati huo huo, uongozi wa bendi ya Mlimani Park Orchestra, umeahidi kutunga wimbo maalumu kwa ajili ya magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha pamoja kati ya viongozi wa Mlimani Park Orchestra, uongozi wa kundi la Sikinde Family na kamati ya habari ya bendi hiyo.
Mkuu wa mirindimo wa bendi hiyo, Hassan Bitchuka alisema wakati wa kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni kuwa, wameamua kutunga wimbo huo kwa lengo la kuuenzi mchango wa magazeti hayo kwa Mlimani Park Orchestra.
No comments:
Post a Comment