KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 30, 2010

APR bingwa Kombe la Kagame



WACHEZAJI wa timu ya APR ya Rwanda wakiwa na kombe la ubingwa wa michuano ya soka ya Kombe la Kagame walilolitwaa juzi baada ya kuichapa St George ya Ethiopia mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Amahoro mjini Kigali. (Picha ya CECAFA).

Na Mwandishi Wetu, Kigali

APR ya Rwanda juzi ilitawazwa kuwa mabingwa wapya wa michuano ya soka ya Kombe la Kagame baada ya kuichapa St George ya Ethiopia mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Amahoro mjini hapa.

Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane katika muda wa nyongeza wa dakika 30 baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa suluhu.

APR ilihesabu bao lake la kwanza dakika ya 93 kupitia kwa Chiukepo Msowoya kabla ya Victor Nyirenda kuongeza la pili dakika ya 95.

Kwa ushindi huo, APR ilizawadiwa kitita cha dola 30,000 za Marekani, zilizotolewa na mdhamini wa michuano hiyo, Rais Paule Kagame wa Rwanda. St George ilizawadiwa dola 20,000.

Mabingwa wa mwaka jana, Atraco ya Rwanda walimaliza michuano hiyo wakiwa wa nne baada ya kupata kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Sofapaka ya Kenya.

Ushindi huo uliiwezesha Sofapaka kuzawadiwa kitita cha dola 10,000 kwa kushika nafasi ya tatu. Rais Kagame hudhamini michuano hiyo kila mwaka kwa kutoa dola 60,000 za Marekani kwa ajili ya washindi watatu wa kwanza.

Sofapaka ilitawala sehemu kubwa ya pambano hilo na kupata bao la kuongoza dakika ya 19 lililofungwa na Akinyemi Abass. Alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi kutoka kwa Bob Mugalia.

Atraco ilisawazisha dakika ya 37 kwa bao lililofungwa na Birory Dady kabla ya Laurent Tumba kuiongezea Sofapaka bao la pili na la ushindi dakika ya 40.

Mechi ya fainali ilihudhuriwa na watazamaji wapatao 40,000 wakiongozwa na Rais Kagame. Mechi hiyo pia ilishuhudiwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, anayechezea klabu ya Inter Milan ya Italia, MacDonald Mariga.

Katika michuano ya mwaka huu, mshambuliaji Msowoya wa APR aliibuka kuwa mfungaji bora baada ya kupachika wavuni mabao saba.

Jumla ya timu 11 kutoka nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), zilishiriki katika michuano ya mwaka huu.

No comments:

Post a Comment