KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 30, 2010

Van Vicker afanya kioja cha mwaka Nollywood



LAGOS, Nigeria

MWIGIZAJI filamu nyota wa Ghana, Joseph Van Vicker amefanya kioja cha mwaka baada ya ‘kuingia mitini kiaina’ wakati yeye na waigizaji wenzake wa Nigeria walipokuwa wakipiga picha za filamu katika mji wa Asaba.

Habari kutoka katika mji huo zimeeleza kuwa, Vicker alifikia uamuzi huo bila kutoa taarifa, hali iliyowachanganya na kuwaweka kwenye wakati mgumu watayarishaji wa filamu hiyo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Vicker alikutwa baadaye akiwa kwenye uwanja wa ndege wa mjini Lagos, akijiandaa kurejea nyumbani Ghana.

Baada ya kumsubiri kwa saa kadhaa bila ya kujua mahali alipo, mtayarishaji wa filamu hiyo aliamua kwenda hotelini kwake kumuulizia.

Kwa kuhofia kuwa, huenda mwigizaji huyo ametokewa na kitu chochote kibaya, uongozi wa hoteli hiyo uliamua kuvunja mlango wa chumba chake ili kujua kulikoni.

Lakini kwa mshangao mkubwa, maofisa wa hoteli pamoja na mtayarishaji wa filamu hiyo, walikikuta chumba kikiwa kitupu, hali iliyozidi kuwapa wasiwasi.

Mbali na kukikuta chumba kikiwa kitupu, mwigizaji huyo aliamua kuchukua kila kilichokuwa chake. Juhudi za kumtafuta kwa njia za mkononi hazikuzaa matunda kwa sababu simu yake ilikuwa imezimwa.

Baada ya kumkosa hotelini, mtayarishaji wa filamu hiyo aliamua kupiga simu kwa mkewe, lakini naye hakuwa na taarifa zozote kuhusu mahali alipokuwa. Aliahidi kumtumia ujumbe iwapo angempata.

Baadaye, mtayarishaji huyo wa filamu alifanikiwa kumpata Vicker kwenye simu yake ya mkononi, ambapo alimweleza kwamba, alikuwa mjini Lagos akijiandaa kupanda ndege kurejea nyumbani.

Katika mazungumzo yao, Vicker alimweleza mtayarishaji huyo wa filamu kwamba, alikuwa na ahadi ya kufika kwenye ubalozi wa Marekani nchini Ghana asubuhi ya siku iliyofuata.

Majibu hayo yalimkera mtayarishaji huyo wa filamu, ambaye alimshutumu Vicker kwa kutokuwa mwaminifu na kuishindwa kuiheshimu kazi yake, ikiwa ni pamoja na kutomweleza mapema kwamba alikuwa na mipango ya kuondoka.

Vicker alimjibu ‘kibosile’ huyo kwa kumweleza kwamba, alitarajia upigaji wa picha za filamu hiyo ungemalizika kabla ya yeye kuondoka kurejea Ghana.

Lakini Vicker alikuwa amesahau kwamba, upigaji wa picha za filamu hiyo ulichelewa kuanza kutokana na yeye kuwa na mkataba wa kupiga picha za filamu nyingine katika mji mwingine tofauti kwa wakati mmoja.

Kutokamilika kwa filamu hiyo mapema pia kulichangiwa na tabia ya Vicker kufika eneo la kupiga picha akiwa amechelewa.

Mbali na Vicker, mwigizaji mwingine aliyedaiwa kuchelewesha upigaji wa picha za filamu hiyo ni Mercy Jonhnson, ambaye aliomba ruhusa ya kuhudhuria sherehe za harusi ya Mike Ezuruonye mjini Enugu.

Kitendo cha Vicker kuingia mitini kabla ya filamu hiyo kukamilika, kimemkera mtayarishaji wake kwa sababu alishalipwa Naira 600,000 kwa ajili ya kazi hiyo na alitaka alipwe kwanza kabla ya kuanza kazi.

Vicker ni mmoja wa waigizaji nyota wa Ghana waliojipatia sifa kubwa barani Afrika kutokana na kushiriki kucheza filamu nyingi zilizotayarishwa nchini Nigeria.

Mwigizaji huyo aliyezaliwa Agosti Mosi, 1977, amewahi kushinda tuzo mbili za mwigizaji bora na ya mwigizaji bora anayechipukia za African Movie Academy Awards mwaka 2008.

Mama wa mwigizaji huyo asili yake ni nchini Liberia na baba yake ni raia wa Uholanzi. Baba yake alifariki wakati Vicker akiwa na umri wa miaka sita.

Vicker amekuwa akikakariwa mara kadhaa kwenye vyombo vya habari akisema kuwa, amelelewa zaidi na mama yake. Kutokana na kifo cha baba yake, Vicker amekuwa karibu zaidi na mama yake na amekuwa akimwelezea kama mtu shujaa.

Kabla ya kuwa mwigizaji, Vicker alikuwa mtangazaji wa kituo cha televisheni cha Metropolitan. Mwaka 2003, alionekana kwa mara ya kwanza kwenye kipindi cha televisheni cha Suncity, kikielezea maisha yake.

Filamu yake ya kwanza inajulikana kwa jina la Divine Love, akiwa mwigizaji msaidizi. Filamu hiyo pia iliwashirikisha waigizaji wenzake wa Ghana, Jackie Aygemang na Majid Michel, ambaye walisoma pamoja shule ya sekondari.

Vicker amekuwa akipewa nafasi zaidi ya kucheza filamu zinazohusu mapenzi, akiwa na waigizaji wengine nyota wa Ghana kama vile Nadia Buari na Jackie. Mashabiki wengi wa filamu wa Ghana na Nigeria wamekuwa wakimfananisha na Ramsey Nouah.

Mwigizaji huyo ameoa na ana watoto wawili. Kwa sasa anamiliki kampuni ya wakala wa matangazo, inayojulikana kwa jina la Sky & Orange na kampuni ya matukio, inayoitwa Babetown. Pia anamiliki taasisi ya Van Vicker Foundation.

No comments:

Post a Comment