KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

Utafiti kubaini umri wa wachezaji wakamilika

MCHAKATO wa kutafiti umri sahihi wa wachezaji, unaosimamiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), umepangwa kumalizika kesho.

Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Dk. Sylvester Faya alisema, utafiti huo ulioanza mwanzoni Mei mwaka huu, uliwashirikisha wachezaji wa kike.

Alizitaja shule mbili, ambazo wachezaji wake walifanyiwa utafiti huo, wilaya zilipo zikiwa kwenye mabano ni sekondari ya Benjamini Mkapa (Ilala) na sekondari ya Kibasila (Temeke).

Dk. Faya alisema lengo la utafiti huo ni kubaini udanganyifu wa umri wa wachezaji, ambao hufanywa na viongozi klabu ama timu za vijana, hasa wa umri wa chini ya miaka 17.

"Tunakaribia kumaliza utafiti wetu wa kuhakiki umri sahihi wa wachezaji vijana kwa kutumia kipimo cha MRI, ambacho licha ya ughali wake, lakini kina uwezo mkubwa wa kung'amua umri sahihi wa mchezaji," alisema.

Akifafanua zaidi, Dk. Faya alisema FIFA imeamua kutumia kipimo hicho, kutokana na urahisi na ubora wake kwa mtumiaji ikilinganishwa na aina zingine za vipimo hivyo.

Alisema kupitia mifupa ya mwanasoka kijana na kulingana na umri wake, MRI inaweza kubaini umri sahihi bila ya kumuathiri mpimwaji hata kama atapimwa zaidi ya mara moja.

"Tunashukuru TFF kwa kutusaidia kwa namna moja au nyingine hadi kukamilika kwa mchakato wetu, ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi tano duniani zilizoendesha utafiti huo," alisema.

Faya amesema ni sifa kubwa kwa nchi kuteuliwa na FIFA kuwa miongoni mwa nchi zilizofanyiwa utafiti huo.

Mbali ya Dk. Faya kutoka TFF, utafiti huo pia ulimshirikisha Mjumbe wa Kamati ya Tiba ya FIFA, Yacine Zerguin, ambaye anatoka Algeria. Mbali na Tanzania, nchi zingine zilizofanya utafiti huo ni
Thailand (Asia), Brazil (Amerika Kusini), Canada (Amerika Kaskazini) na Ubelgiji (Ulaya).

No comments:

Post a Comment