'
Friday, May 14, 2010
Manji amvuruga Papic
HALI imeendelea kuwa si shwari ndani ya klabu ya Yanga baada ya kuzuka tena tafrani kubwa kati ya mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yussuf Manji na Kocha Mkuu, Kostadin Papic.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Papic sasa amefikia uamuzi wa kufungasha virago kurejea kwao Serbia huku akiapa kwamba hatarejea tena katika klabu hiyo.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya klabu hiyo kimeeleza kuwa, Papic amekerwa na tabia ya Manji kuwa kigeugeu katika masuala yanayohusu usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Manji amekubali kutoa fedha za usajili kwa wachezaji wote wazalendo, lakini amekataa kufanya hivyo kwa wachezaji wa kigeni waliotafutwa na Papic.
“Imefika hatua sasa Papic haelewi nini la kufanya kwa sababu Manji ndiye aliyemwambia atafuta wachezaji na kumpelekea ripoti, lakini ameikataa,” alisema mtoa habari wetu.
“Wachezaji wote wazalendo ameshawasainisha mikataba mipya na kuwalipa haki zao na wengine amewaongeza mishahara, lakini ajabu ni kwamba ameyakataa majina yote ya wachezaji wa kigeni yaliyopendekezwa na Papic,” aliongeza.
Chanzo hicho cha habari kiliongeza kuwa, Manji amemtaka Papic ayapeleke majina ya wachezaji hao wa kigeni kwa uongozi wa Yanga ili watafute fedha za kuwasajili.
Uchunguzi zaidi umebainisha kuwa, viongozi wa Yanga nao wapo njia panda kwa vile hawaelewi lengo la mfadhili huyo kwa vile kauli zake zimekuwa zikiwachanganya.
“Kwa kweli hata sisi sasa hatumuelewi na hatujui tufanye nini kwa sababu amekuwa akitoa kauli tofauti kwa Papic,” alisema kiongozi mmoja wa Yanga, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.
“Kama hataki kuendelea kuifadhili Yanga ni bora aweke mambo wazi kwa wanachama kuliko kuendelea kutuweka njia panda. Hivi anavyofanya, anatuchanganya,” aliongeza.
“Kama ni kocha, yeye ndiye aliyemtafuta na kuingia naye mkataba, sasa iweje hawaelewani? Hapa kuna kitu kinajificha, tunamuomba Manji aweke mambo hadharani,” alisema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo alisema hawaelewi kwa nini Manji alimtaka Papic awapelekee orodha ya usajili wa wachezaji viongozi wa klabu hiyo wakati ambapo sio wanaotoa fedha hizo.
“Kwa hali ilivyo, Papic anaweza kuondoka nchini wakati wowote na ameshaanza kuwaaga watu wake wa karibu kwa kuwaeleza kwamba, huenda asirudi tena nchini,”alisema.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, upo uwezekano mkubwa kikao cha kamati kuu ya Yanga kilichopangwa kufanyika leo kikaahirishwa kutokana na viongozi wengi kutokuwepo Dar es Salaam.
“Hivi ninavyozungumza na wewe, Mwenyekiti (Iman) Madega yupo Dodoma kwa shughuli zake binafsi, (Emmanuel) Mpangala amefiwa kwao Mbeya na (Patrick) Fatah hatakuwepo,”alisema.
Kikao hicho kilipanga kujadili mambo mbalimbali yanayoihusu Yanga, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya katiba na tarehe za kuitishwa kwa mkutano mkuu wa wanachama na uchaguzi wa viongozi wapya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment