KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

Papic: Ngasa APR si saizi yako

KOCHA Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amesema timu ya APR ya Rwanda haimfai Mrisho Ngasa kwa sababu kiwango chake hakina tofauti na timu za Tanzania.

Papic alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, Ngasa anapaswa kwenda kucheza soka ya kulipwa katika klabu zenye kiwango cha juu zaidi.

Kocha huyo alitoa kauli hiyo baada ya kuwepo na taarifa kwamba, Ngasa amekwenda Rwanda kufanya majaribio ya kuichezea APR.

Kuna habari kuwa, APR ilitaka kumsajili Ngasa kwa kitita cha sh. milioni 20, lakini mchezaji huyo aligoma na kutaka alipwe sh. milioni 35.

Papic alisema kama Ngasa ana kiu ya kwenda nje kucheza soka ya kulipwa, ni vyema aende katika klabu kubwa kama za Afrika Kusini na za Ulaya.

"Pale Rwanda sifahamu vizuri soka yao, lakini kwa ushauri wangu, naona ni vyema mchezaji huyo angefanya mipango ya kwenda Afrika Kusini au Ulaya,"alisema kocha huyo, ambaye ni raia wa Serbia.

Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu ya Azam umesema kuwa, hauna mpango wa kumsajili mshambuliaji Mrisho Ngasa kutoka Yanga.

Mmoja wa viongozi wa Azam, Mohamed King alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, watasajili washambuliaji wapya kutoka klabu zingine na siyo Yanga.

King alisema hawajawahi kufanya mazungumzo na Ngasa kwa ajili ya kumsajili msimu ujao na kuongeza kuwa, taarifa hizo wamekuwa wakizisoma kupitia kwenye vyombo vya habari.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Azam alikiri kuwa, wamefanya mazungumzo ya awali na beki Nadir Haroub ‘Canavaro’ wa Yanga kwa ajili ya kumsajili msimu ujao.

"Ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba, ni kweli tumefanya mazungumzo na Canavaro, lakini kwa upande wa Ngasa, hilo jambo halipo,"alisema King.

Tayari uongozi wa Yanga umekaririwa ukisema kuwa, milango ipo wazi kwa Canavaro kujiunga na Azam, lakini anapaswa kufuata taratibu za usajili.

No comments:

Post a Comment