KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

Mourinho aikana Real Madrid



MILAN, Italia

KOCHA Mkuu wa Inter Milan ya Italia, Jose Mourinho amekanusha madai kuwa, amekuwa akifanya mazungumzo kwa ajili ya kuwa kocha mkuu wa Real Madrid ya Hispania msimu ujao.

Mourinho alisema mjini hapa juzi kuwa, kwa sasa hana mpango huo na kusisitiza kuwa, ameelekeza nguvu zake katika kukabiliana na changamoto zote zinazoikabili Inter Milan.

Inter Milan inachuana vikali na AS Roma katika kuwania taji la ligi ya Serie A ya Italia na inatarajiwa kuteremka dimbani keshokutwa kumenyana na Siena. Mechi hiyo ndiyo itakayoamua bingwa wa ligi hiyo.

Mbali na kibarua hicho, Inter Milan pia inakabiliwa na mtihani mwingine mgumu wa kupambana na Bayern Munich ya Ujerumani katika mechi ya fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya, itakayocheza Mei 22 mwaka huu.

“Sijafanya mazungumzo na klabu nyingine yoyote, na kama ilivyo kwa mashabiki wote wa Inter Milan, nafikiria mechi zetu mbili muhimu dhidi ya Siena na Bayern Munich,”alisema kocha huyo, ambaye amebatizwa jina la ‘Special One’.

“Hizi ni siku za ajabu, tumeelekeza akili na nguvu zetu katika mechi hizi mbili na hakuna yeyote ndani ya Inter Milan, anayefikiria kuhusu nini watakachokifanya baada ya mechi ya fainali ya ligi ya mabingwa. Huo ndio ukweli wenyewe,”aliongeza.

Mourinho alisema ameshamweleza wakala wake, Jorge Mendez kwamba hatajadili suala hilo hadi Mei 23 baada ya mechi ya fainali ya ligi ya mabingwa.

Hata hivyo, Mourinho alikiri kwamba bado ana mambo muhimu ya kufanya katika soka na kuongeza kuwa, moja ya mipango yake ya baadaye ni kufundisha kabumbu nchini Hispania ama kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ureno.

“Lakini hayo nitaweza kuyafanya nitakapokuwa mtu mzima zaidi, inawezekana katika miaka 15 ama 20 ijayo,”alisema.

Alipoulizwa iwapo siku moja angependa kuwa kocha wa mshambuliaji Cristiano Ronaldo wa Real Madrid, kocha huyo alisema: “Vema, Nimesema nataka kuwa kocha wa Ureno katika kipindi cha miaka 15 au 20 ijayo.”

Mapema wiki hii, Rais wa Inter Milan, Massimo Moratti alitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikikanusha madai kuwa, anamsaka mrithi wa Mourinho.

No comments:

Post a Comment