KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 7, 2010

SOKA LIBERIA IMEKUFA

MONROVIA, Liberia
CHAMA cha Soka cha Liberia (LFA), kimekiri kuwa mchezo wa soka nchini humo umekufa.
Rais wa LFA, Musa Hassan Bility aliieleza BBC wiki hii kuwa, jitihada zinahitajika ili kuunusuru mchezo huo.
Musa ameliomba Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) na lile la Afrika (CAF), kuisaidia nchi hiyo katika jitihada zake za kuinua soka.
Rais huyo mpya wa LFA alitarajia kukutana na Rais wa FIFA, Sepp Blatter wiki hii kujadili tatizo hilo, ambalo limeifanya timu ya taifa ya nchi hiyo na za klabu kupoteza umaarufu.
“Soka imekufa Liberia na tunatafuta njia za kuifufua,”alisema Musa, aliyeukwaa wadhifa huo baada ya kushinda uchaguzi mkuu.
“Hapa ndipo nchi pekee ya Afrika iliyotoa mwanasoka bora wa dunia (George Weah), kunapaswa kuwepo na kitu fulani kizuri kuhusu nchi hii,”aliongeza.
“Bahati mbaya ni kwamba, Liberia ni moja ya nchi zenye kiwango cha chini kisoka miongoni mwa nchi za Afrika,”alisema.
Timu ya taifa ya Liberia, Lone Star inashika nafasi ya 152 kwa ubora wa viwango vya soka duniani, miongoni mwa nchi 202 zilizo wanachama wa FIFA. Mwaka 2001, nch hiyo ilikuwa ikishika nafasi ya 66.
“Tunaamini FIFA na CAF zinaweza kutusikiliza na kutusaidia kuinua tena kiwango cha soka,”alisema Musa.
Musa alisema wanahitaji msaada wa kifedha na kiufundi na kuongeza kuwa, ataomba wapatiwe programu ya miaka miwili kwa ajili ya kufufua mchezo huo.
Alisema kwa sasa, chama chake kinatafuta makocha wa kigeni kwa ajili ya kuinoa Lone Star, lakini pia watajaribu kuwaendeleza makocha wazalendo.
“Lengo letu kwanza ni kuiweka nyumba yetu kuwa katika hali nzuri na kuiwezesha nchi kufuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika,”alisema.

No comments:

Post a Comment