KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 30, 2010

GERRARD: Zitakuwa fainali za mwisho kwangu



LONDON, England

KIUNGO wa kimataifa wa England, Steven Gerrard amesema, fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Afrika Kusini, huenda zikawa za mwisho kwake.

Akizungumza wiki hii mjini hapa, Gerrard alisema anafikiria kustaafu soka ya kimataifa mara baada ya kumalizika kwa fainali hizo, zinazotarajiwa kuanza Juni 11 mwaka huu.

Gerrard (29) alisema hana hakika iwapo atakuwa na uwezo wa kucheza fainali za mwaka 2014, zilizopangwa kufanyika nchini Brazil, akiwa na umri wa miaka 33.

Kiungo huyo anayechezea klabu ya Liverpool ya England amesema, hatarajii iwapo ataweza kutwaa tuzo yoyote akiwa na timu ya taifa ya nchi hiyo baada ya kumalizika kwa fainali za mwaka huu.

“Nafikiria kuzifanya fainali za mwaka huu kuwa za aina yake kwa England kwa sababu huenda zikawa za mwisho kwangu. Natarajia kutimiza miaka 30 wiki hii na kamwe huwezi kuelewa nini kitatokea baadaye,”alisema kiungo huyo.

Gerrard ameshindwa kutwaa tuzo yoyote akiwa na kikosi cha Liverpool, hivyo amepania kufanya kila linalowezekana ili kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa dunia akiwa na England.

“Kamwe sikuwahi kufikiria kustaafu kuichezea England, lakini wachezaji wengi wana umri mkubwa hivi sasa na watakuwa na wiki tatu au nne za mapumziko baada ya Kombe la Dunia kabla ya kufikiria mustakabali wao,”alisema.

Hata hivyo, Gerrard alisema hayo yote yatategemea jinsi England itakavyofanya vizuri katika fainali hizo na jinsi Kocha Fabio Capello atakavyokuwa akifikiria.

“Unapofikisha umri wa miaka 30, ni wakati ambao napaswa kufikiria soka ya kimataifa, nini nitakachokifanya ili kusonga mbele na pia mafanikio niliyoyapata,”alisema Gerrard.

“Sitaki kujiondoa katika soka ya kimataifa kama sijapata mafanikio yoyote. Kama tutafanya vizuri, huenda itasaidia kubadilisha fikra zangu, lakini sijalipa sana uzito hilo,” aliongeza.

Gerrard alisema kutokana na viwango vya wachezaji walio nyuma yake, hana hakika iwapo atakuwemo kwenye kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 kitakachoteuliwa na Capello kucheza fainali za
mwaka huu.

“Napaswa kulifikiria hilo, lakini nashukuru kwamba nipo fiti na mwenye uwezo wa kuwemo kwenye kikosi hicho. Nataka kutoa mchango mkubwa katika fainali hizi , hasa ikizingatiwa huenda zitakuwa za mwisho kwangu,”alisema.

Kiungo huyo wa England alikataa kuzungumzia mustakabali wake ndani ya Liverpool, aliyoichezea kwa miaka 11 sasa, lakini alisema hana wasiwasi wa kuihama klabu hiyo.

Alisema ataamua kuhusu hatma yake ndani ya klabu hiyo mara baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia.

Gerrard amekuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na klabu ya Real Madrid ya Hispania, lakini amekuwa akikanusha mara kadhaa kuwepo kwa mipango hiyo.

Mara baada ya kumalizika kwa fainali za Mataifa ya Ulaya mwaka 2004 na fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006, Gerrard pia alihusishwa na mipango ya kujiunga na Chelsea.

Mbali na Real Madrid, klabu nyingine iliyoonyesha nia ya kumsajili kiungo huyo ni Manchester City, ambayo imesema ipo tayari kuilipa Liverpool dau lolote inalotaka ili imwachie mchezaji huyo.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka wameeleza kuwa, upo uwezekano mkubwa kwa Gerrard kuihama Liverpool msimu ujao kutokana na klabu hiyo kukabiliwa na hali ngumu kifedha.

Sababu nyingine iliyotajwa na wachambuzi hao kwamba huenda ikamlazimisha Gerrard kuhama ni hali ya kutokuelewana kati ya mchezaji huyo na Kocha Rafael Benitez.

“Kwa sasa sifikirii kuhusu mustakabali wangu au nini kitanitokea Liverpool hadi baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia,”alisema.

Alisema hataki kujiingiza kwenye mtego wa fainali zilizopita za kombe hilo, ambapo nusura awe chizi kwa kufikiria hatma yake ya baadaye. Alisema safari hii, hataki kufanya kosa kama hilo.

“Kumekuwa na tetesi nyingi kuhusu hatma yangu katika kipindi cha miezi miwili au mitatu, lakini imekuwa hivyo kwa miaka mingi sasa.

“Natumaini kuna vitu huenda vikatokea nitakapokuwa sipo. Huenda kukawa na wachezaji watakaojiunga na Liverpool ili kuiongezea nguvu timu.

“Napaswa kusubiri na kuona, lakini kwa sasa sifurahishwi na mambo yanavyokwenda Liverpool. Naelekeza akili yangu katika fainali za Kombe la Dunia,”alisema.

No comments:

Post a Comment