KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 6, 2010

SIMBA VURUGU TUPU

MICHAEL Wambura


Wambura afungua kesi Kisutu

Aichongea TFF kwa FIFA

MGOMBEA uenyekiti aliyeenguliwa katika uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba, Michael Wambura amefungua kesi kwenye mahakama ya Kisutu ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Simba.
Mbali na kesi hiyo, Wambura ameandika barua kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), akilifahamisha kuhusu mgogoro wa Simba uliopo mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Wambura alisema ameamua kufungua kesi ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi wa Simba ili haki itendeke. Alifungua kesi hiyo jana.
Akifafanua kuhusu uamuzi wake huo, Wambura alisema haoni vipengele vyovyote ndani ya katiba ya Simba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) vinavyomzuia kugombea uongozi katika klabu hiyo.
Wambura alisema anataka apate ufafanuzi wa kina wa kisheria kuhusu kipengele cha ‘kukosa uaminifu’ kilichotumiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika kumuengua kugombea wadhifa huo.
Wambura ni miongoni mwa wagombea wawili walioenguliwa na kamati hiyo, kufuatia rufani zilizowasilishwa na wanachama Asha Kigundula na Daniel Kamna. Mgombea mwingine aliyeenguliwa ni Zacharia Hanspope.
“Lazima tuelewe kwamba binadamu anaishi kwa misingi ya sheria. Katika mpira wa miguu, tuliweka utaratibu, tukikataza masuala ya mpira kwenda mahakamani. Lakini huwezi kumzuia mtu kama hujamwambia haki yake ataipata wapi,”alisema.
“Unapotaka kumzuia mtu kwenda mahakamani, unamweleza kuna utaratibu fulani unaotakiwa kufuata, ikishindikana huko ndio uende mahakamani. Usipofanya hivyo, unakuwa umemfunga mtu mikono asipate haki yake,”aliongeza.
Wambura alisema kipengele kilichotumiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kumuengua kugombea uongozi wa Simba ni batili na kinapaswa kutumiwa kwa vyama vilivyo chini ya shirikisho hilo, kama vile vya mikoa na si klabu.
Alisema katiba ya Simba ibara ya 55 inaeleza wazi kuwa, kutakuwepo na kamati maalumu ya kushughulikia migogoro ndani ya klabu hiyo, hivyo suala hilo halikupaswa kushughulikiwa na TFF.
Wambura alisema asingeweza kuwasilisha malalamiko yake kwa Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) kwa sababu suala hilo linapaswa kushughulikiwa na vyombo vya chini kwanza kabla ya kufika huko.
“Katiba ya Simba inasema kwamba, wanachama wanaunganishwa kwa muundo wa chombo cha kushirikisha wanaofuata sheria za Tanzania, hivyo inatambua mamlaka za kisheria na haiwezekani kumzuia mtu kwenda mahakamani,” alisema.
“Mimi nasema kwenda mahakamani ni halali kwa mujibu wa sheria za nchi hii na huwezi kumzuia mtu kwenda kukata rufani katika vyombo ulivyovifungua wewe mwenyewe,” aliongeza.
Wambura alisema pia kuwa, ameamua kuiandikia FIFA kuieleza kuhusu kesi zilizopo mahakamani na nakala yake ameituma kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Alisema katika barua hiyo, ameeleza kwa kina sababu za yeye kuenguliwa kugombea uongozi ndani ya Simba na mchakato mzima ulivyokuwa na kuliomba shirikisho hilo liwasaidie wawaruhusiwe kugombea.
Uchaguzi wa Simba umepangwa kufanyika Jumapili, lakini kufuatia kufunguliwa kwa kesi hiyo na ile iliyofunguliwa na mwanachama Juma Mtemi kwenye mahakama ya Ilala, huenda ukasogezwa mbele.

No comments:

Post a Comment