KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 20, 2010

Ngasa: Nipo tayari kwa lolote

MSHAMBULIAJI Mrisho Ngasa wa Yanga amesema yupo tayari kwa uamuzi wowote utakaochukuliwa katika kikao cha pamoja kati ya viongozi wa klabu hiyo na Azam.

Ngasa amesema kwa sasa anasubiri hatma ya kikao hicho kilichotarajiwa kufanyika jana kwenye hoteli ya Movenpick mjini Dar es Salaam.

“Mimi nipo tayari kuichezea timu yoyote, itakayokuwa tayari kunilipa dau ninalolitaka,”alisema Ngasa alipozungumza na Burudani kwa njia ya simu mjini Dar es Salaam.

“Kwa sasa siwezi kufahami ni timu ipi nitakayoichezea msimu ujao. Kikao cha pamoja kati ya viongozi wa Yanga na Azam ndicho kitakachotoa hatma yangu,”aliongeza.

Ngasa ameelezea msimamo wake huo siku moja baada ya uongozi wa Yanga kusema, hautakuwa tayari kumruhusu ajiunge na Azam kwa vile bado ana mkataba na klabu hiyo hadi mwaka 2010.

Mbali na kutakiwa na Azam, mshambuliaji huyo mwenye kasi na chenga za maudhi, pia anawindwa kwa udi na uvumba na klabu ya APR ya Rwanda, alikokwenda kufanya majaribio wiki iliyopita.

Wakati huo huo, Mwandishi Wetu Charles Mganga ameripoti kutoka Rwanda kuwa, timu ya APR imesema bado haijakata tamaa ya kumsajili Ngasa.

Kocha Msaidizi wa APR, Nshimiyimana Eric alisema juzi mjini hapa kuwa, wameshamalizana na Ngasa kwa ajili ya kumsajili msimu ujao.

Eric alisema hakuna kilichowakwamisha kumsajili mchezaji huyo ambaye tangu atue Jangwani, amekuwa mwiba mchungu kwa timu pinzani kwenye ligi kuu soka Tanzania Bara.

“Tulishakutana na Ngasa mjini hapa na kufanyanaye mazungumzo, ambayo yalifikia hatua nzuri. Alitueleza anachotaka nasi tukakubali na kumwambia ofa zetu. Mpaka anaondoka, mambo yetu na yeye yalikuwa yameshamalizika," alisema kocha huyo.

Eric alisema kilichobaki kwao ni uongozi wa APR kukutana na viongozi wa Yanga ili kukubaliana kuhusu malipo ya ada ya uhamisho wa mchezaji huyo.

"Siwezi kusema kwamba tumekwama, tunachofanya kwa sasa ni kutafuta muda ili tuweze kwenda Tanzania kuongea na viongozi wa mchezaji huyo," aliongeza Eric.

Kocha huyo alisema, wana nia ya dhati ya kumnasa mchezaji huyo na kamwe wasingependa kumkosa kutokana na uwezo wake na kipaji alichonacho cha kusakata kabumbu.

Awali, APR ilikuwa tayari kumlipa Ngasa dau la sh. milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wake, lakini mchezaji huyo aligoma na kutaka alipwe sh. milioni 40 na mshahara wa sh. milioni 1.5 kila mwezi.

No comments:

Post a Comment