KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

Twiga Stars yapewa milioni 10/-

TIMU ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars imekabidhiwa kitita cha sh. milioni 10taslimu kutoka kwa mlezi wake, Rahma Al - Kharoosi.

Makabidhiano hayo yalifanyika jana kwenye ukumbi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambapo fedha hizo zilipokelewa kwa niaba ya Twiga Stars na meneja wake, Furaha Francis.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rahma pia aliahidi kuipeleka Twiga Stars nchini Marekani iwapo itaitoa Eritrea na kufuzu kucheza fainali za michuano ya Afrika. Rahma anamiliki Kampuni ya RBP Oil & Industrial Technology (T) Limited.

Alisema kampuni yake imeguswa na kibarua kizito kinachoikabili Twiga Stars, ambayo ili iweze kufuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza, italazimika kushinda mechi zote mbili. Fainali za michuano hiyo zimepangwa kufanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini.

"Mabinti wa Twiga tayari wameonyesha nia ya kutaka kucheza fainali hizo, hasa ni baada ya kuwang'oa kinadada wa Ethiopia. Nikiwa mlezi wa vijana hao, nimeguswa ndio sababu nimeamua kutoa kiasi hicho cha fedha ili kiwe changamoto ya ushindi kwao," alisema.

Rahma alisema pia kuwa, kampuni yake imepokea mwaliko kutoka kwa timu ya wanawake ya Washington Freedom ya Washington DC nchini Marekani kwa ajili ya Twiga Stars kwenda huko kwa mazoezi ya wiki mbili.

Hata hivyo, alisema safari hiyo itafanyika iwapo tu Twiga Stars itaitoa Eritrea na kusonga mbele. Alizitaja timu, ambazo Twiga itacheza nazo itakapokuwa Marekani kuwa ni pamoja na wenyeji wao, Washington Freedom.

Zingine ni Seattle Woman, White Caps Woman na mechi ya mwisho watapangiwa na wenyeji wao.

Akipokea fedha hizo, Furaha alimshukuru mlezi huyo wa Twiga Stars na kuongeza kuwa, wamezipata kwa wakati mwafaka kwa vile zitawasaidia katika maandalizi yao dhidi ya Eritrea.

Pambano la awali kati ya timu hizo limepangwa kufanyika Mei 23 mwaka huu mjini Dar es Salaam na la marudiano wiki mbili baadaye mjini Asmara.

No comments:

Post a Comment