KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 6, 2010

DROGBA, ROONEY WACHUANA KUWANIA KIATU CHA DHAHABU

WAYNE Rooney

DIDIER Drogba


LONDON, England
WAKATI ligi kuu ya soka ya England ikiwa inafikia ukingoni Jumapili, washambuliaji Didier Drogba wa Chelsea na Wayne Rooney wa Manchester United wanachuana vikali kuwania tuzo ya kiatu cha dhahabu, inayotolewa kwa mfungaji bora.
Mbali na washambuliaji hao wawili, ambao timu zao zinapambana vikali kuwania ubingwa, pia wamo Darren Bent wa Sunderland na Carlos Tevez wa Manchester City.
Kabla ya mechi za jana, Drogba na Rooney walikuwa wamefungana kwa kufunga mabao 26 kila mmoja, huku timu zao zikiwa zimebakiwa na mechi moja kila moja kumaliza ligi hiyo.
Hatma juu ya mfungaji bora wa ligi hiyo atajulikana baada ya mechi za mwisho za timu hizo, ambapo mabingwa watetezi Manchester United watamenyana na Stoke City wakati Chelsea itavaana na Wigan.
Wachezaji wengine wenye nafasi ya kunyakua kiatu hicho cha dhahabu ni Bent mwenye mabao 24 na Tevez mwenye mabao 23. Wachezaji hao wawili wanaweza kutwaa tuzo hiyo, iwapo wataongeza mabao wakati Sunderland itakapomenyana na Wolves na Manchester City itakapovaana na West Ham.
Kiungo Frank Lampard wa Chelsea anashika nafasi ya tano kwa kufunga mabao 21 akifuatiwa na Jermaine Defoe wa Tottenham na Fernando Torres wa Liverpool waliofunga mabao 18 kila mmoja.
Cesc Fabregas wa Arsenal anashika nafasi ya nane kwa kufunga mabao 15, akifuatiwa na Emmanuel Adebayor wa Manchester City aliyefunga mabao 14. Louis Saha wa Everton na Gabriel Agbonlahor wa Aston Villa wamefunga mabao 13 kila mmoja.
Waliofunga mabao 12 kila mmoja ni Florent Malouda wa Chelsea na Dimitar Berbatov wa Manchester United wakati waliofunga mabao 10 kila mmoja ni Craig Bellamy wa Manchester City, John Carew wa Aston Villa, Carlton Cole wa West Ham, Cameron Jerome wa Birmingham na Hugo Rodallega wa Wigan.
Wachezaji waliofunga mabao tisa kila mmoja ni Steven Gerrard wa Liverpool, Nicolas Anelka wa Chelsea, Dirk Kuyt wa Liverpool, Andrei Arshavin wa Arsenal.
Waliofunga mabao nane kila mmoja ni Tim Cahill wa Everton, Bobby Zamora wa Fulham, Matthew Taylor wa Bolton, David Dunn wa Blackburn, Kevin Doyle wa Wolves, Steven Fletcher wa Burnley, Kenwayne Jones wa Sunderland na Aruna Dindane wa Portsmouth.
Wakati huo huo, Chelsea imedhihirisha kuwa na washambuliaji wenye uchu zaidi wa kufunga mabao msimu huu, baada ya kupachika wavuni mabao 95.
Mabingwa watetezi Manchester United wanashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao 80, wakifuatiwa na Arsenal, iliyofunga mabao 78 na Manchester City iliyofunga mabao 72.
Tottenham inashika nafasi ya tano kwa kufunga mabao 64, ikifuatiwa na Liverpool iliyotikisa nyavu mara 61, Everton iliyofunga mabao 59, Sunderland iliyofunga mabao 47 na West Ham iliyofunga mabao 46.
Burnley ndiyo timu yenye ukuta mbovu kuliko zote baada ya kuruhusu mabao 80, ikifuatiwa na Hull City iliyofungwa mabao 73 na Wigan iliyofungwa mabao 69.
Bolton inashika nafasi ya nne miongoni mwa timu zenye ukuta mbovu baada ya kuruhusu lango lake kufungwa mabao 66, ikifuatiwa na Portsmouth na West Ham zilizofungwa mabao 65 kila moja na Wolves iliyofungwa mabao 55.
Kipa Edwin van der Sar wa Manchester United ndiye aliyedhihirisha kuwa kipa bora zaidi msimu huu baada ya kuruhusu lango lake kufungwa mabao machache. Kipa huyo hadi sasa amefungwa mabao 28.
Petr Cech wa Chelsea anashika nafasi ya pili kwa kufungwa mabao 28, akifuatiwa na Pepe Reina wa Liverpool aliyefungwa mabao 35 na Brad Friedel wa Aston Villa aliyefungwa mabao 38.

No comments:

Post a Comment