MWANAMUZIKI Johnson
Nguza (Papii Kocha), jana, aliangua kilio cha furaha, baada ya kupata taarifa
za kuachiwa huru kutokana na agizo la Rais Dk. John Magufuli.
Papii na baba yake,
Nguza Vicking (Babu Seya), ni miongoni mwa wafungwa walionufaika na msamaha wa
Rais Magufuli, alioutangaza jana, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 56 ya
uhuru wa Tanzania Bara.
Rais Magufuli
alitangaza kutoa msamaha kwa wafungwa 61, waliohukumiwa adhabu ya kifo na
kuwaachilia huru Babu Seya na mwanawe, Papii Kocha.
Wanamuziki hao walihukumiwa
kifungo cha maisha gerezani na Mahakama Kuu, mwaka 2004, baada ya kupatikana na
hatia ya kubaka na kulawiti wasichana 10, wa shule ya Msingi Mashujaa, iliyoko wilayani
Kinondoni, Dar es Salaam.
Hukumu hiyo ilizua
hisia tofauti miongoni mwa Watanzania huku idadi kubwa ya wananchi wakiamini
kuwa, wanamuziki hao hawakuhusika na tukio hilo.
Kufuatia kupewa hukumu
hiyo, wanamuziki hao waliamua kukata rufani, lakini Novemba 21, mwaka 2013,
Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali ombi lao la kuitaka ifanye marejeo ya uamuzi
wake wa awali wa kuwapata na hatia, kama ambavyo hukumu dhidi yao ilivyotolewa.
Mahakama hiyo baada ya
kufanya mapitio, ikiwa imeketi chini ya majaji watatu, iliamua warufani hao
wawili wana hatia, hivyo waendelee kutumikia adhabu yao.
Akitumia Ibara ya 45
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayotoa mamlaka kwa Rais kutoa
msamaha kwa wafungwa, Rais Dk. Magufuli alitangaza kutoa msamaha kwa Babu Seya
na mwanaye, kwenye sherehe za miaka 56 ya uhuru wa Tanzania Bara, zilizofanyika
katika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
“Sisi sote ni binadamu
na hata mimi huwa namuomba Mungu anisamehe, ingawa sisi wanadamu ni wagumu kusamehe.
Hivyo natangaza msamaha kwa familia ya Nguza Viking, maarufu kama Babu Seya na
watoke leo,” alisisitiza Rais Magufuli huku akishangiliwa na umati wa watu
waliohudhuria sherehe hizo.
Kuhusu wafungwa 61,
waliohukumiwa adhabu ya kifo, Rais Magufuli alitangaza kuwasamehe kutokana na
kukaa gerezani kwa miaka mingi.
Alisema baada ya
kufanyika uchunguzi, imegundulika wafungwa hao wamejutia makosa yao kwa kiasi
kikubwa na wamejirekebisha.
“Yupo mtu alifungwa
akiwa na miaka 18. Sasa ana umri wa miaka 60, akiwa gerezani. Mwingine Mganga
Matonya mwenye umri wa miaka 87, ambaye amekaa gerezani kwa miaka 44.
“Nitamkabidhi Waziri
Mkuu orodha ya wafungwa wote ili ahakikishe utaratibu unafanyika wa kuachiwa
huru leo au kesho. Na hii document (nyaraka) naisaini hapa hapa. Lisiongezwe
jina lingine au kupunguzwa,” alibainisha.
Alisema wafungwa hao
61, hawakuua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) wala kuhusika na vitendo vya
ujambazi, lakini alisisitiza serikali kuendelea kusimamia sheria kwani uwepo wa
ibara hiyo ya kikatiba haina maana sheria haitofuata mkondo.
Rais alitaja idadi ya
wafungwa waliosamehewa, kwenye gereza la Uyui (2), Butimba (5), Ukonga (19),
Isanga (15), Maweni (11) Kinguwila (5) na gereza la Ruanda wapo wafungwa wanne.
Vilevile, Rais Magufuli
alitoa msamaha kwa wafungwa 8,157, ambao kati yao, 1,828 walitakiwa kutoka
tangu jana na wengine 6,329, walipunguziwa muda wa kukaa gerezani.
Jijini Dar es Salaam,
mwanamuziki Papii alipata taarifa za kuachiwa kwao huru wakati akiwa anashiriki
kucheza mechi ya soka ya wafungwa wanaozishabikia Simba na Yanga, kwenye gereza
la Ukonga.
Wakati wafungwa
wengine wakishiriki katika mechi hiyo, baadhi yao walikuwa wakitazama moja kwa
moja matangazo ya maadhimisho ya miaka 56 ya uhuru kupitia kwenye runinga
iliyokuwepo ndani ya gereza hilo.
Wakati Rais Magufuli
akitangaza kuwaachia huru Nguza na Papii, wafungwa waliokuwa wakifuatilia
matangazo hayo walilipuka mayowe ya kushangilia na kukimbilia uwanjani, ambako
walianza kumkimbiza Papii na hatimaye kumzingira.
Mmoja wa wanamuziki
wakongwe nchini, King Kikii, alisimulia mkasa huo jana, kwa waandishi wa
Mzalendo, baada ya kwenda kuwatembelea Babu Seya na Papii kwenye gereza la
Ukonga.
Kikii alisema alifika
kwenye gereza hilo baada ya kumsikia Rais Magufuli akitangaza msamaha huo kwa
Babu Seya na Papii, kupitia kwenye runinga, akiwa nyumbani kwake, Ubungo, Dar
es Salaam.
“Kwanza namshukuru
sana Rais Magufuli. Uamuzi alioufanya ni wa kihistoria. Nimefurahi sana. Siwezi
kusema lolote kwa sasa, isipokuwa
namshukuru Mungu na rais wetu. Mdogo wangu na mwanawe wamekaa gerezani
kwa miaka 10 na sasa wako huru,” alisema.
Akisimulia jinsi Babu
Seya na Papii walivyopokea taarifa hizo, Kikii alisema Papii ndiye aliyeonekana
kuwa na furaha kubwa, kutokana na kuzunguka gereza zima, akiwaaga wenzake kwa
furaha.
“Papii anasema alipita
kila chumba kuwaaga wenzake huku akiwashukuru kwa ushirikiano wao kwa muda wote
waliokuwa pamoja gerezani,” alisema Kikii.
Aliongeza kuwa,
kitendo cha wafungwa wenzake kumkimbiza na kumzingira, kilimshtua hivyo
alilazimika kuwahoji kulikoni, ndipo wakamjulisha kwamba, yeye na baba yake
wameachiwa huru na Rais Magufuli.
“Kuanzia hapo Papii
anasema alikuwa kama amepagawa kwa furaha. Mwanzoni aliangua kilio kwa kuwa
hakuamini, lakini baadaye alianza kufurahia kwa kuzunguka gereza lote
akishangilia na kuwaaga wenzake,”alisema.
Akimzungumzia Babu
Seya, alisema baada ya kupokea taarifa hizo, hakuwa na mengi ya kusema zaidi ya
kumshukuru Mungu na Rais Magufuli kwa uamuzi wake huo.
“Nguza (Babu Seya)
alikuwa akifuatilia matangazo hayo na wenzake gerezani, lakini hakuwa
akitarajia kitu kama hicho kutokea. Alichosema ni kwamba, anamshukuru Mungu na
Rais Magufuli kwa kuwaonea huruma,”alisema.
Mmoja wa askari wa
Magereza, aliyekuwepo kazini kwenye gereza la Ukonga, jana, alisema licha ya
Rais Magufuli kutoa agizo hilo, isingewezekana kwa Babu Seya na mwanawe
kutolewa siku hiyo kwa kuwa kuna taratibu za kisheria, zinazopaswa
kukamilishwa.
“Ni kweli mheshimiwa
rais ametoa agizo hilo, lakini kwa jinsi ninavyofahamu, kuna taratibu ambazo
lazima zifuatwe kabla ya kuwaachia huru. Inawezekana wakaachiwa kesho (leo),”
alisema askari huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Mapema wakati akitoa
takwimu za idadi ya wafungwa waliopo magerezani, Rais Magufuli alisema hadi
juzi, kulikuwa na wafungwa 39,000, kati yao wafungwa 37,000, ni wanaume na
wanawake ni 2,000.
Dk. Magufuli alieleza kuwa
wafungwa waliohukumiwa kunyongwa ni 522, kati yao wanaume 503 na wanawake 19.
Alisema wafungwa
waliohukumiwa kifungo cha maisha ni 666, kati yao wanaume 655 na wanawake 11.
“Kwa maana hiyo
wafungwa wengi waliopo magerezani ni wanaume, hivyo tuanze kujitambua ni
kwanini wanaume wanaongoza kwenye vitendo vya uhalifu,”alisema.
No comments:
Post a Comment