KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 30, 2014

KATIBA YA SIMBA INA MAPUNGUFU-THADEO
Na: Genofeva Matemu – Afisa Mawasiliano Serikalini (WHVUM)

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imemaliza kupitia Rasimu ya Katiba ya Club ya Simba kwa ajili ya kuidhinisha katiba hiyo na kuifanya Club ya Simba kuendelea na taratibu za uchaguzi mkuu.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Leonard Thadeo alipokutana na waandishi wa habari kujibu hoja mbalimbali za waandishi leo jijini Dar es Salaam.

Akijibu moja ya hoja iliyomtaka kufafanua Wizara imefikia wapi katika upatikanaji wa Katiba ya Club ya Simba Bw. Thadeo amesema kuwa upitiaji wa Katiba umemelizika na kuonekana kuwa na mapungufu machache yanayohitaji kurekebishwa ili Wizara iweze kuidhinisha katiba hiyo.

“Mchakato wa upitiaji wa Katiba ya Club ya Simba umemalizika jana lakini kumekuwepo na mapungufu machache yanayohitaji kurekebishwa ili Wizara iweze kuidhinisha Katiba hiyo” amesema Bw. Thadeo.

Akifafanua zaidi Bw. Thadeo amesema kuwa mapungufu hayo yanalenga zaidi upande wa kisheria ambapo mtu anaweza kutafsiri neno vibaya hivyo kupata maana tofauti na Katiba ilivyokusudia hivyo kuitaka Club hiyo kufanya marekebisho hayo mapema na kurejesha Katiba hiyo Wizarani kwa ajili ya kuidhinishwa.

Aidha Bw. Thadeo amewataka waandishi wa habari pamoja na wanachama wa Club ya Simba kuwa na subira ili waweze kupata Katiba itakayokidhi malengo ya Club yao kwani mchakato wa upitiaji wa Katiba ulihitaji umakini.

DIAMOND AAHIDI MAKUBWA MTWARA KESHOKUTWANyota wa muziki wa Bongo flava nchini anayepasua anga ya Afrika, Rais wa wasafi kama wengi wanavyomuita, Diamond Platnum, Dangote ameahidi makubwa kwa mashabiki wake wote wa Mkoa wa Mtwara kuhusu show ya aina yake inayotarajiwa kufanyika katika umbi wa Makonde Club mjini Mtwara siku ya ijumaa tarehe 2 mwezi huu.


Msanii huyo aliyeafanikiwa kujizolea mamilioni ya mashabiki wa muziki wa Bongo flava atasindikizwa na kipenzi chake, Malkia wa Bongo Movie nchini, Wema Sepetu - 'Beautiful Onyinye' au Madame kama mashabiki wake wanavyopenda kumwita.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, katika ofisi za Vodacom Tanzania, ambao ndio wadhamini wa tamasha hilo amesema Mashabiki wakae mkao wa kula burudani ya nguvu ya muziki kutoka kwa kipenzi chao ambaye hafikirii kukosea wala kuwaangusha mashabiki wake katika show zake zote anazozifanya.

"Mashabiki wote waliopo Mtwara watashuhudia nikiimba live nyimbo yangu mpya ya My number One remix niliyomshirikisha Davido kutoka nchini Nigeria. Kwa kawaida huwa sipendi kuwaangusha mashabiki zangu hivyo basi nawaahidi makubwa sana katika tamasha hilo na ningependa kuwaona wengi wakihudhuria show hiyo kwani kutakuwepo na mengi ambayo hawakutarajia kuyaona" Alisema Diamond.

Msanii Diamond ambaye kwa sasa ndiyo mwenye mafanikio makubwa ya kimuziki nchini amekuwa ni kivutio kikubwa kwa mashabaiki wa ndani na nje ya nchi kila mahali anapoalikwa kufanya shoo na hivyo kujizolea sifa lukuki na hata kuchaguliwa kuwania tuzo mbali mbali za muziki barani Afrika.

Kwa upande wao wadhamini wa tamasha hilo Mkuu wa kitengo cha masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa amesema mtandao wao unajivunia kudhamini tamasha kubwa kama hili kwani hakuna kitu ambacho wanakijali kama wateja wao haijalishi wapo kona gani ya Tanzania.

"Tunajivunia kuwa sehemu ya Wadhamini wa Tamasha hili kubwa, Vodacom siku zote tumekuwa tukitoa kipaumbele kwa wateja wetu, Kipindi cha Pasaka tulifanya Tamasha pale coco beach na sasa ni zamu ya watu wa Mtwara" alisema Twissa na kuongeza.

"Tutawafikia wateja wetu popote pale walipo na kuwapa burudani Vodacom imekuwepo nchini kwa zaidi ya miaka kumi sasa na kwa kipindi chote hicho watanzania wameonyesha kutuunga mkono na kutufanya tuwe mtandao unaaongoza siku zote Hivyo hatuna budi kuwafanyia yale ambayo wanaweza wakafurahi ikiwemo kuwaletea burudani kama hii".

"Ili kuwarahisishia wateja wetu na wananchi kwa ujumla, mteja anaweza kununua tiketi yake kwa njia ya M-pesa kwa kutuma pesa kwenda 0754 980 769. Na atapatiwa ufafanuzi wa jinsi ya kupata tiketi yake. Wateja watakaotumia njia hii watapata punguzo la asilimia 20 (20%). Wateja wa Vodacom na Mashabiki wote kwa ujumla wasiache kuhudhuria shoo hiyo ambayo itakuwa na kishindo kikubwa na kwa aina yake". Alisema.

Aidha, "Vodacom tunaahidi kuenedelea kuwaunga mkono wasanii wetu wa Kitanzania na kujivunia kilicho chetu, wote ni mashahidi kwa namna ambavyo tumekuwa msitari wa mbele kuwaunga mkono wasanii wetu na tutaendelea na jitihada hizo na kufikia viwango vya wasanii wengine wa kimataifa," alihitimisha Twissa.

KAVUMBAGU ATUA AZAM


AZAM FC, mabingwa wa Tanzania Bara wameingia Mkataba wa mwaka mmoja na Nahodha wa Burundi, Didier Kavumbangu wenye kipengele cha kuongezewa mwaka mwingine, iwapo atafanya vizuri katika mwaka wake wa kwanza.

Mshambuliaji huyo aliyemaliza Mkataba wake wa miaka miwili na waliokuwa wapinzani wakuu wa Azam FC katika mbio za ubingwa msimu huu, Yanga SC, amesaini mchana wa leo mbele ya Katibu Mkuu wa klabu, Nassor Idrisa makao makuu ya klabu, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Katibu Nassor alisema; “Tumepata mshambuliaji mzuri, ambaye tayari ana uzoefu wa kucheza Ligi Kuu ya Tanzania kwa misimu miwili, mchezaji huyu ni chaguo la kocha wetu Joseph Omog, ambaye alivutiwa naye baada ya kumuona akichezea klabu yake zamani, Yanga SC.”

Kwa upande wake, Kavumbangu alisema; “Mimi ni mchezaji, kazi yangu ni mpira. Nimemaliza mkataba Yanga, lakini viongozi hawaniambii kitu, nimepata ofa nzuri Azam nikaamua kusaini,”.

Mshambuliaji huyo mrefu mwenye nguvu amesema sasa akili yake anaipeleka kwa mwajiri wake mpya, Azam FC ambako pia amepania kwenda kushinda mataji na kuiwezesha timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika.

“Mimi sasa ni mchezaji wa Azam, nafurahi kujiunga na klabu hii kubwa. Kawaida yangu huwa nashabikia klabu nayochezea, sasa mimi ni mshabiki namba moja wa Azam,”amesema.

Kavumbangu alitua Yanga mwaka 2013 akitokea Atletico ya Burundi na katika mechi misimu miwili ya kuichezea klabu hiyo, amefunga mabao 31 katika mechi 63 za mashindano yote, moja tu la penalti.

Sunday, April 27, 2014

AZAM YATISHIA KUJITOA KOMBE LA KAGAMEAZAM FC itashiriki michuano mipya ya klabu inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) iwapo tu itasogezwa mbele.


Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa Mohammed ‘Father’ amesema kwamba wamepata mwaliko wa CECAFA kuombwa kushiriki michuano hiyo ya Mei mwaka huu, lakini wametoa jibu kwa muda uliopangwa, hawataweza.

“Tumewasiliana na CECAFA baada ya kutuomba tutume orodha ya watakaokwenda Sudan, na tumewaambia wazi kwamba muda ambao michuano imepangwa kufanyika, hatutaweza, ila kama watasogeza mbele, tunaweza kujipanga na kwenda,”alisema Father.

Father alisema kwa sasa wachezaji wa Azam FC wapo likizo hadi Juni 15 baada ya kumaliza msimu vizuri na ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wakati michuano hiyo mipya itakayoshirikisha mabingwa wa Kombe la FA au washindi wa pili wa Ligi Kuu itafanyika nchini Sudan kuanzia Mei 20 hadi Juni 5.

Azam imemaliza Ligi Kuu na pointi 62 dhidi ya 56 za waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC na kuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo.

Wachezaji wa Azam FC wamepewa likizo hadi Juni 15, mwaka huu baada ya kumaliza msimu vizuri wakitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Wachezaji na viongozi wa Azam FC jana walikuwa na kikao maalum na bodi kwa ajili ya kupongezana na kuagana kwa likizo hiyo ndefu, wakajipange kwa ajili ya msimu ujao.

Katibu wa klabu, Nassor Idrissa Mohamed ‘Father’ amesema benchi la Ufundi kwa pamoja na wachezaji wanakwenda likizo vizuri baada ya mafanikio ya msimu huu.

Azam imemaliza Ligi Kuu na pointi 62 dhidi ya 56 za waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC na kuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo.

Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.

Wakati huo huo: Wachezaji wa akademi ya Azam nao pia wamepewa likizo hadi Mei 8, mwaka huu watakaporejea kuenedelea na mafunzo ya soka ya kisasa

CECAFA YAANZISHA MICHUANO MIPYA, INAITWA KOMBE LA NILE, YANGA KUIWAKALISHA TANZANIABARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limeanzisha mashindano mapya yatakayojulikana kwa jina la Nile Basin Cup.

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo jana imeeleza kuwa, timu zitakazoshiriki kwenye michuano hiyo ni zile zilizoshika nafasi za pili katika ligi za kila nchi zilizo wanachama.

Michuano hiyo imepangwa kuanza Mei 20 hadi Juni 5 mwaka huu nchini Sudam na tayari wenyeji kwa kushirikiana na CECAFA wamepata wadhamini watakaogharamia usafiri wa kwenda na kurudi kwa timu zote, malazi, usafiri wa ndani na zawadi za fedha.

Katika michuano hiyo, Tanzania itawakilishwa na Yanga, ambayo imeshika nafasi ya pili katika michuano ya mwaka huu ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Mbali na michuano hiyo, CECAFA pia imeamua kuanzisha mashindano ya vijana wa chini ya umri wa miaka 23 inayotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu nchini Sudan.

Taarifa hiyo imesema lengo la michuano hiyo ni kuzipa maandalizi nchi wanachama kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016. Imesema serikali ya Sudan imejitolea kudhamini michuano hiyo.

Katika hatua nyingine, michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame, imepangwa kufanyika Agosti nchini Rwanda.

Tayari Rais Paul Kagame wa Rwanda ameshajitolea kudhamini michuano hiyo kwa kutoa dola 60,000 za Marekani kwa ajili ya fedha za zawadi kwa washindi.

Wakati Kombe la Kagame litachezwa Rwanda, michuano ya Kombe la Chalenji imepangwa kufanyika kati ya Novemba na Desemba mwaka huu nchini Ethiopia.

Ujumbe wa CECAFA unatarajiwa kwenda Ethiopia baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mwisho na kutafuta wadhamini.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) limeandaa semina ya mawasiliano kwa nchi wanachama wa CECAFA itakayofanyika Aprili 30 hadi Mei 2 mwaka huu mjini Dar es Salaam.

Semina hiyo itahudhuriwa na maofisa wa habari, wakurugenzi, wenyeviti wa vyama vya mikoa, makatibu wakuu na vyama vyote vilivyo wanachama wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Semina hiyo inatarajiwa kufunguliwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke, anayetarajiwa kuwasili nchini hivi karibuni.

Katika hatua nyingine, CECAFA imeingia mkataba mpya wa miaka minne na kituo cha televisheni cha Supersport cha Afrika Kusini. Mkataba huo umeanza 2014 na utamalizika 2017.

Kwa mujibu wa mkataba huo, Supersport itaonyesha live michuano yote inayoandaliwa na CECAFA.

NGORONGORO YAITOA KENYA KWA MATUTA


TIMU ya soka ya Taifa ya vijana wa chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro

Heroes imeitoa Kenya katika raundi ya kwanza ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za
Afrika.

Ngorongoro imesonga mbele katika michuano hiyo baada ya kuishinda Kenya kwa penalti 4-3, kufuatia timu hizo mbili kushindwa kufungana katika mechi zote mbili za nyumbani na ugenini.

Kwa matokeo hayo, Ngorongoro inayofundishwa na kocha mzalendo John Simkoko
sasa itamenyana na Nigeria katika hatua inayofuata.

Penalti za Tanzania zilikwamishwa wavuni na Mohammed Hussein, Kevin Friday,
Mange Chagula na Iddi Suleiman wakati Mudathir Yahya alikosa.

Penalti za Kenya zilifungwa na Geoffrey Shiveka, Timonah Wanyonyi na Victor Ndinya,
wakati Evans Makari na Harison Nzivo walipoteza.

Hakuna kipa aliyeokoa penalti bali wapigaji walikosa kwa kupiga nje.

Mechi hiyo ilikuwa kali na ya ushindani na makipa wa timu zote mbili, Aishi Manula wa
Tanzania na Farouk Shikhalo wa Kenya aliyeanza kabla ya kumpisha Boniface Barasa
dakika ya 88 walifanya kazi nzuri ya kuokoa michomo ya hatari.

TISA WAONGEZWA STARS

KOCHA mpya wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Mart Nooij ameongeza wachezaji
tisa katika kikosi hicho kinachojiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi (The
Flames).

Timu hizo mbili zinatarajiwa kumenyana Mei 4 mwaka huu katika mechi ya kirafiki ya
kimataifa itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Wachezaji walioongezwa ni Edward Charles Manyama (JKT Ruvu), Elias Maguli (Ruvu
Shooting), Hassan Dilunga (Yanga), Hussein Javu (Yanga), John Bocco (Azam), Kelvin
Friday (Azam), Oscar Joshua (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe
(AC Cannes, Ufaransa).

Beki Kelvin Yondani wa Yanga, ambaye aliitwa awali, ameondolewa katika kikosi hicho
kwa vile ameshindwa kuripoti kambini.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Pemium Lager, inaingia kambini leo (Aprili
28 mwaka huu) jijini Mbeya kujiandaa kwa mechi hiyo dhidi ya Malawi.

SIMBA WAOMBOLEZA KIFO CHA MUCHACHO

MWENYEKITI wa Simba SC, Mhe; Ismail Aden Rage, ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa, marafiki na familia ya Marehemu Abdulrahman Muchacho (66), aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam na kuzikwa jana katika makaburi ya Kisutu jijini.

Muchacho ni miongoni mwa wanachama wenye historia ya kipekee ndani ya klabu kwani akiwa Timu Meneja wa Timu ya Simba mwaka 1976, Simba iliifunga Yanga mabao 6-0, ambao ndiyo mshindi mnono zaidi kuwahi kutokea katika historia ya mechi za Watani wa Jadi na akiwa Mweka Hazina wa Timu katika miaka ya 1990, Simba ilicheza katika Fainali ya Kombe la CAF.

Mwanachama huyu ndiye pia chachu ya kuanzishwa kwa kundi la ushangiliaji la Muchacho ambalo ndilo chimbuko la makundi yote ya ushingilijiaji katika viwanja vya soka hapa nchini.

"Kwa kweli msiba huu umenigusa sana hasa ukizingatia kwamba niliona utendaji wake wakati mimi nikiwa mchezaji wa Simba na baadaye katika uongozi. Msiba wa Muchacho ni mkubwa kwa klabu kwa sababu jina lake litabaki kuwa sehemu ya historia iliyotukuka ya Simba SC.

"Muchacho anatoka katika familia ya wana Simba. Baba yake alikuwa shabiki mkubwa wa Sunderland na mrehemu alikuwa mrithi mzuri wa mapenzi haya ya baba yake. Kwa sababu ya mambo ambayo wameifanyia klabu, jina la Muchacho na Simba vitaendelea kudumu, daima na milele," alisema Rage.

MSAJILI.
KLABU ya Simba inapenda kukanusha upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kupitia vyombo vya habari kwamba Katiba ya Simba bado haijapelekwa katika Ofisi za Msajili.

Katiba ya tayari iko kwa Msajili kwa Zaidi ya wiki moja sasa na kilichobaki ni taratibu za kawaida za serikali kuhakikisha kwamba mchakato huu unamalizika kwa faida ya pande zote.

Simba SC inatumia nafasi hii kuwaomba wanachama na wapenzi wake kuwa watulivu wakati wakisubiri Ofisi ya Msajili wa Vyama na Vilabu kufanya kazi yake. Tangu mwanzo tulikubali kwamba Katiba yetu itatumika mara tu baada ya kupitishwa na TFF na Ofisi ya Msajili ambao wanafanya kila kitu kwa taratibu zao.

Ni vema pia watu wakaacha kueneza maneno ya uongo kuhusu Katiba kutopelekwa kwa Msajili kwa vile taarifa kama hizo zina lengo tu la kupotosha na kutaka kusababisha rabsha hata pasipo na sababu.

Mchezo wa mpira ni wa kistaarabu na ni vema wastaarabu wote wakatulia na kusubiri majibu kutoka katika Ofisi ya Msajili.

Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Katibu Mkuu
Simba SC

MOGELLA, MZIBA WATEMBELEA KLINIKI YA AIRTEL RISING STARS


Wachezaji nyota wa zamani wa timu ya Taifa, Taifa Stars Zamoyoni Mogella na Abeid Mziba, wakisalimiana na washiriki wa kliniki ya soka ya Kimataifa ya Airtel Rising Stars inayoendelea kwenye Uwanja wa Azam Complex.Mchezaji nyota wa zamani wa timu ya Taifa, Taifa Stars Zamoyoni Mogella, akiongea na washiriki wa kliniki ya soka ya kimataifa ya Airtel Rising Stars wakati walipowatembelea kwenye kliniki hiyo inayofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex.


Shirikisho la mpira wa miguu nchi (TFF), imetakiwa  kuhahakisha inawalea vijana waliopata nafasi ya kushiriki kliniki ya soka ya Kimataifa ya Airtel Rising Stars ili waweze kulisadia taifa kwa hapo baadae.

Wachezaji wa zamani wa timu ya Taifa Abeid Musiba na Zamoyoni Mogella walitoa kauli hiyo
kwenye uwanja wa Azam wa Complex jijini Dar es Salaam jana, alipokwenda kuwatembelea
washiriki wa kliniki ambayo ina washiriki 72 kutoka nchi 12 Barani Afrika huku Tanzania
ikiwakilishwa na washiriki 19.

‘Ninayo furaha kuona mwekezaji kama Airtel kwa kushirikiano na Klabu ya Manchester United
ya Uingereza, zimejitokesa kusaidia maendeleo ya soka, hatuna budi kuhakikisha vipaji hivi
vinaendelezwa pamoja na kukuzwa zaidi,’ alisema Mogella.

Mogella alisema kuwa hana uhakika serikali imeweza kutoa miundo mbinu inayowezesha
michezo kufanyika, hivyo jukumu la kuhakikisha vipaji na elimu wanayoipata vijana hawa inabaki
kwa TFF.

"Kwa siku za karibuni serikali imekuwa ikitoa mazingira kwa wawekezaji kama hawa ili waweze
kufanya kazi yao vizuri. Na kwa maana hiyo nayo watahamasika na kuwekeza zaidi kwenye sekta
za michezo. Wakati sisi tunacheza mambo kama hayo hayakuwepo," alisema Mziba.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya Yanga Africans alisema Tanzania na hata baadhi ya
nchi za Afrika zilikuwa hazifanyi vizuri kwenye michuano ya kimataifa sio kwa sababu hazina
vijana wenye vipaji vya soka, bali ni kutoka na ukosefu wa programu madhubuti za kuendeleza
vijana ambao ndio muhimili wa maendeleo ya soka.

WACHINA KUUKARABATI UWANJA WA MAO TSE TUNGBalozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Yunliang akiwasilisha agizo la Serikali yake kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi la kuridhia na kukubali kusaidia Ujenzi wa uwanja wa Michezo wa Mau Tse Tung uliopo Mtaa wa Mperani - Kikwajuni Mjini Zanzibar
Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imeridhia na kukubali kugharamia ujenzi wa Kiwanja cha michezo kilichopewa jina na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la Mau Tse Tung kilichopo miperani Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bw. Xie Yunliang wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ofisi yake iliyomo ndani ya Jengo la Msekwa Bungeni Mjini Dodoma.


Balozi Xie Junliang alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Timu ya wataalamu wa China inatarajiwa kukifanyia utafiti na uchunguzi kiwanja hicho baadaye mwaka huu sambamba na utiwaji saini Makubaliano ya ujenzi wa kiwanja hicho unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka ujao.

Alisema ujenzi wa uwanja huo uliopewa heshima ya Jina la Kiongozi muasisi wa Taifa la China Marehemu Mao Tse Tung utajumuisha kiwanja cha mchezo wa soka pamoja na michezo mengine ya ndani mfano mchezo wa Table Tennis.

“ Tunatarajia ujeni wa kiwanja cha Mao utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wanamichezo wa michezo tofauti ukiwemo ule unaopendwa zaidi wa soka “. Alisema Bwana Xie Junliang.

Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uhusiano wa kidugu uliopo kati ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla pamoja na China unastahiki kuenziwa zaidi.

Alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Jamuhuri ya Watu wa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika harakati zake za kujikwamua kiuchumi.

Alisema matengenezo makubwa ya ujenzi wa Hospitali ya Abdulla Mzee iliyopo Mkoani Kisiwani Pemba, ujenzi wa maegesho ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar pamoja na matayarisho wa matengenezo ya chumba cha wagonjwa mahututi { ICU } mwezi Juni mwaka huu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ni miongoni mwa uthibitisho wa uhusiano wa pande hizo mbili.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Jamuhuri ya Watu wa China kwa moyo wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika miradi ya Kiuchumi na Maendeleo.

Balozi Seif alisema mchango wa Serikali ya China kwa Zanzibar umesaidia kuiwawezesha asilimia kubwa ya Jamii Zanzibar kustawika Kijamii na hata kiuchumi kupitia miundo mbinu iliyowekwa na Serikali kwa msaada wa Nchi hiyo rafiki.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitolea mfano msaada mkubwa uliotolewa na China katika ujenzi wa skuli za Wilaya za Sekondari katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Alisema mradi huo mkubwa wa sekta ya Elimu umekuja kufuatia ongezeko kubwa la idadi wa wanafunzi wanaofanikiwa kujiunga na masomo ya Sekondari katika maeneo tofauti ya Zanzibar.

“ Kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi hasa eneo la Wilaya ya Magharibi katika Kisiwa cha Unguja tumelishuhudia hivi karibuni katika skuli ya Kijitoupele na Serikali kupitia Wizara ya Elimu tunaliangalia tatizo hilo kwa mtazamo wa kujenga skuli mpya katika Mtaa wa Pangawe “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza China kupitia Balozi wake huyo kwa mchango wake mkubwa katika Nyanja ya Elimu mchango ambao tayari watoto wa Zanzibar wanaendelea kufaidika nao.

NGORONGORO HEROES KURUDIANA NA KENYA LEO


TIMU ya soka ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo itamenyana na vijana wenzaao wa Kenya katika mechi ya marudiano Raundi ya Kwanza kuwania tiketi ya fainali za Afrika mwakani nchini Senegal.


Mechi hiyo itakayochezewa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni ndiyo itakayoamua timu itakayocheza raundi inayofuata katika michuano hiyo dhidi ya Nigeria.

Ngorongoro Heroes inayofundishwa na John Simkoko ilitoka suluhu na Kenya katika mechi ya kwanza iliyochezwa Machakos, Kenya wiki tatu zilizopita, na imekuwa kambini jijini Dar es Salaam kwa wiki mbili kujiwinda kwa mechi hiyo.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 2,000 na sh. 5,000 ambapo Kenya iliyowasili nchini jana (Aprili 25 mwaka huu) usiku imefanya mazoezi yake ya mwisho jana (Aprili 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa.

Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Burundi wakiongozwa na Pacifique Ndabihawenimana wakati Kamishna ni Tarig Atta Salih kutoka Sudan. Kila la heri Ngorongoro Heroes.

MALINZI: KOCHA MPYA STARS HATAINGILIWA, AISHUHUDIA STARS IKICHAPWA 3-0 NA BURUNDIRAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) amesema kwamba atahakikisha kocha mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars Mholanzi Mart Nooij haingiliwi katika utendaji wake.

Malinzi aliyasema hayo jana wakati akimtambulisha mwalimu huyo mpya kwa Waandishi wa Habari Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya mchezo dhidi ya Burundi ambao Taifa Stars ilitandikwa mabao 3-0.

Akiwa amefuatana na Makamu wake Wallace Karia, amesema anafurahi kumtangaza Nooij na ana matarajio kuwa Tanzania itanufaika na uzoefu wake mkubwa wa ukocha, hasa katika bara la Afrika.
“Nawaahidi Watanzania kuwa sitomuingilia kocha katika kazi yake. Kama mimi sitomuingilia kocha, basi hakuna mtu yeyote atakayemuingilia. Tumemwajiri yeye kwa vile ni mtaalamu, hivyo hakuna sababu ya kumuingilia,” amesema Rais Malinzi.

Naye Nooij ambaye amepewa mkataba wa miaka miwili amesema yeye ni mtu wa maneno mafupi, hawezi kuahidi kitu lakini ana matarajio ya kuifanya Taifa Stars ifanye vizuri katika mashindano mbalimbali.

Amesema kabla ya kukubalia kufundisha Taifa Stars alikuwa na klabu ya St. Georges ya Ethiopia, lakini vilevile amewahi kufundisha mpira wa miguu barani Afrika katika nchi za Burkina Faso, Mali na Msumbiji.

Nooij alikuwa jukwaani jana wakati Stars inachapwa mabao 3-0 na kesho anatarajiwa kwenda na timu hiyo Mbeya kambini kuanza kazi ya kuleta mabadiliko.

Thursday, April 24, 2014

AZAM KULAMBA MIL. 75/ ZA VODACOM, TAMBWE KUKOMBA MIL 5.2MSHAMBULIAJI Amisi Tambwe wa Simba atalamba Sh. milioni 5.2 za zawadi ya mfungaji bora zitakazotpolewa na wadhamini wakuu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kampuni ya huduma ya simu ya Vodacom Tanzania baada ya kuibuka mfungaji bora wa msimu wa 2013/14 wa ligi hiyo.

Aidha, timu yenye nidhamu italamba Sh. milioni 16 ikiwa ni ongezekon la Sh. milioni moja ikilinganishwa na ilivyokuwa msimu uliopita.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania, Salum Mwalim katika mkutano na waandishi wa habari muda mfupi uliopita kwenye ofisi za Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zilizopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

ZAWADI ZA WASHINDI LIGI KUU BARA 2013/2014
Bingwa: Sh. Milioni 75
Mfungaji Bora: Sh. Milioni 5.2
Timu yenye Nidhamu; Sh. Milioni 16
Kipa Bora: Sh. Milioni 5.2
Refa Bora; Sh. milioni 5.2
  Mwalim amesema mabingwa Azam FC watazawadiwa Sh. milioni 75 ikiwa ni ongezeko la Sh. milioni 5 ikilinganishwa na ilivyokuwa msimu uliopita.   Kipa bora, mwamuzi bora watapata Sh. milioni 5.2 kila mmoja ikikwa ni ongezeko la Sh. 200,000.Timu yenye nidhamu italamba Sh. milioni 16, ikiongezeka kutoka Sh. 15 ya msimu uliopita zilizochukuliwa na Yanga.   Silas Mwakibinga, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), aliyekuwa amefuatana na Mwalim kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, alisema tarehe ya kutolewa kwa tuzo hizo itatangazwa baada ya wiki moja.

Wednesday, April 23, 2014

KIINGILIO STARS, BURUNDI BUKU TANO J'MOSI


KIINGILIO cha chini katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Burundi (Intamba Mu Rugamba) itakayochezwa Aprili 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000.

Mechi hiyo itakuwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kiingilio hicho ni kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa wa VIP A kiingilio kitakuwa sh. 20,000 wakati VIP B na C ni sh. 10,000.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari ipo kambini kwenye hoteli ya Kunduchi Beach kujiandaa kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka nchini Kenya.

Burundi inatarajia kuwasili nchini keshokutwa (Aprili 22 mwaka huu) tayari kwa ajili ya mechi hiyo inayotajiwa kuwa ya kusisimua. Mechi hiyo imepangwa kuanza saa 10 jioni.

Wachezaji wa Taifa Stars waliopo kambini ni Deogratias Munishi, Mwadili Ali, Aidan Michael, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Hassan Mwasapili, Kelvin Yondani, Said Moradi, Amri Kiemba, Frank Domayo, Himid Mao, Jonas Mkude, Athanas Mdamu, Haruna Chanongo, Juma Liuzio, Khamis Mcha, Mrisho Ngasa, Ramadhan Singano na Simon Msuva.

Wengine ni Benedicto Mlekwa, Emma Simwanda, Joram Mgeveje, Omari Kindamba, Edward Mayunga, Shiraz Sozigwa, Yusuf Mlipili, Said Ally, Abubakar Mohamed, Hashim Magona, Omari Nyenje, Chunga Zito, Mohammed Saidi, Ayoub Lipati, Abdurahman Ally na Paul Bundara.

Monday, April 21, 2014

SIMBA YATOA TAARIFA YA 2013/2014SIMBA SPORTS CLUB

P.O.BOX 15318
TEL+255 222183330
FAX +255 222183330
MSIMBAZI/MCHIKICHI STREET
DAR ES SALAAM
TANZANIA
EMAIL simbasportsclub@yahoo.com
WEBSITE www.simbatz.co.tz
AFFILIATED TO TFF, DRFA and IDFA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UONGOZI wa Simba SC unapenda kuwashukuru wanachama na washabiki wake wote hapa nchini kutokana na mshikamano mkubwa waliounyesha wakati wa kuelekea kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu.

Ingawa matokeo hayakuwa mazuri siku zote, lakini mapenzi ambayo washabiki walionyesha kwa klabu yao lilikuwa ni jambo la faraja kwa uongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji.

Wachezaji wa Simba pia wameelezea kufurahishwa kwao na namna washabiki waliokwenda kwenye Uwanja wa Taifa kutazama pambano la Watani wa Jadi Jumamosi iliyopita, walivyowashangilia kwa dakika zote tisini.

Uongozi wa Simba unapenda kuwaahidi washabiki wake kwamba utafanya kila uwezalo kuhakikisha kwamba klabu inajiandaa vya kutosha kufanya vizuri msimu ujao.

Makosa ambayo yalisababisha timu isifanye vizuri msimu uliomazika yatatazamwa na kufanyiwa upembuzi yakinifu ili yasijirudie tena katika msimu unaokuja na mingine.

Simba SC inaamini kwamba wanachama wake watakuwa bega kwa bega na uongozi kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri msimu ujao.

MAPATO

Msimu huu ulikuwa na changamoto kubwa sana za kimapato. Katika mechi baina ya Simba SC na Ashanti iliyochezwa jijini Dar es Salaam, mgawo kwa Simba SC ulikua ni zaidi kidogo ya shilingi laki tatu. Hii ni rekodi katika historia ya Simba.

Hili lilisababishwa zaidi na kutofanya vizuri kwa timu. Hata hivyo, uongozi ulijitahidi kwa kadri ilivyowezekana kupambana na changamoto hizi kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani na ubunifu.

Pamoja na changamoto zote hizo, uongozi ulijitahidi kuisimamia timu na hata katika mechi ya Watani wa Jadi iliyofanyika Jumamosi iliyopita, timu iligharamiwa na viongozi waliopo pasipo kupata msaada wowote kutoka nje ya uongozi.

Kupitia uzoefu uliopatikana msimu huu kwenye eneo la mapato, uongozi sasa utabuni namna nyingine za kuongeza mapato ili kupambana na changamoto za kupungua kwa mapato ya milangoni.

TIMU

Mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu, klabu imevunja kambi na wachezaji wote wamepewa ruhusa ya kupumzika hadi katika wiki ya kwanza ya mwezi Julai mwaka huu ambapo timu itaanza mazoezi kujiandaa na msimu ujao.

Na kama ilivyo katika vitabu vya Sayansi ya Michezo, Simba itafanya mazoezi ( Pre Season) kwa walau wiki sita kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu ujao. Simba haitakuwa na mechi yoyote ya kirafiki na wala haitashiriki mashindano yoyote yatakayokuwa yameandaliwa katika kipindi cha kati ya mwezi Juni au Julai; labda kama benchi la ufundi litaona inafaa.

KOCHA LOGARUSIC

Uongozi wa Simba unaendelea na mazungumzo na kocha wake, Zdravko Logarusic, kuhusu kumuongezea mkataba wake na mazungumzo hayo yatafikia tamati mwishoni mwa wiki hii.

Klabu itatoa tamko rasmi kuhusu endapo itaendelea au haitaendelea na mkataba wake na kocha huyo baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo. Kwa sasa, haitazungumzia lolote kuhusu hilo hadi mwishoni mwa wiki hii.

Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Katibu Mkuu
Simba SC

AZAM YAMETIMIA, SIMBA, YANGA HAKUNA MBABE

PAZIA la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara limefungwa rasmi leo kwa Azam FC kutimiza ndoto za kumaliza ligi hiyo bila kupoteza mechi baada ya ushindi wa 1-0 jioni hii Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mganda, Brian Umony ndiye aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 78 na kwa matokeo hayo, Azam FC inamaliza na pointi 62 na wametawazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa Bara, wakiipokonya taji Yanga SC iliyomaliza katika nafasi ya pili na pointi 56 baada ya sare ya 1-1 jioni hii na watani wao, Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nahodha wa Azam FC akiwa ameinua cheti cha kutambuliwa na FIFA kama mabingwa wapya wa Bara baada ya kukabidhiwa na Jamal Malinzi leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Azam ilijihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu Jumapili iliyopita, baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kufikisha pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi ambazo zisingeweza kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho leo.

Licha ya kuwa timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine Aprili 13, mwaka huu, Azam FC pia inakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo

Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.

Mechi ya leo ilihudhuria na Wakurugenzi wa Azam, Abubakar, Omar na Yussuf, watoto wa Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa ambao waliketi jukwaa kuu pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Malinzi alimkabidhi Kombe la ubingwa Nahodha wa Azam, John Bocco baada ya mechi hiyo pamoja na cheti maalum kutoka FIFA, ambacho kinatolewa kwa mara ya kwanza mwaka huu na Azam inakuwa timu ya kwanza kupata.

Wachezaji wote walivalishwa Medali baada ya mechi na baada ya hapo sherehe za ubingwa zilichukua nafasi yake Uwanja wa Azam Complex.

Taifa; Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mechi ya watani wa jadi ilimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, Simba wakitangulia kupata bao dakika ya 77 kupitia kwa Haroun Chanongo, kabla ya Simon Msuva kuisawazishia Yanga SC dakika ya 86.

Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Ashanti United iliendeleza rekodi yake ya kushuka msimu ule ule waliopanda Ligi Kuu, baada ya kufungwa 1-0 na Prisons ya Mbeya- bao pekee la Peter Michael dakika ya 54, wakati JKT Oljoro na Mtibwa Sugar zimetoka sare ya 1-1 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, na Mbeya City wameilaza 1-0 Mgambo JKT, bao la Saad Kipanga dakika ya 75.

Coastal Union pia imemaliza ligi na kipigo cha 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, bao pekee la Themi Felix dakika ya 50, wakati Ruvu Shooting imeshinda mabao 2-0 dhidi ya Rhino Rangers.

Ashanti United ya Ilala, Dar es Salaam inayomaliza ligi na pointi 25, inaungana na JKT Oljoro ya Arusha iliyomaliza na pointi 19 na Rhino Rangers ya Tabora pointi 16 kuipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu msimu wa 2013/2014 na nafasi zao zinachukuliwa na Ndanda FC ya Mtwara, Polisi ya Morogoro na Stand United ya Shinyanga zilizopanda kwa ajili ya msimu ujao.

Mbali na Azam kumaliza kileleni na pointi 62, Yanga SC pointi 56 nafasi ya pili, Mbeya City ya Mbeya imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake 49, Simba SC ya nne pointi 38, Kagera Sugar ya tano pointi 38 pia, Ruvu Shooting ya sita pointi 38, Mtibwa Sugar ya saba pointi 31, JKT Ruvu ya nane pointi 31 Coastal Union ya tisa pointi 29, Prisons ya 10 pointi 28 na JKT Mgambo ya 11 pointi 26.   IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY

Thursday, April 17, 2014

OKWI, NIYONZIMA, KASEJA KUIKOSA SIMBA J'MOSI


Yanga imerejea jana jijini Dar es salaam na kuendelea na maandalizi ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya timu ya Simba SC mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Uwanja wa Taifa siku ya jumamosi majira ya saa 10:00 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.


Kikosi cha Young Africans kimeweka kambi eneo la Bahari Beach kujiandaa na mchezo huo ambao ni muhimu kwa watoto wa Jangwani kuhakikisha wanafanya vizuri na kupata ushindi mzuri wa kumalizia ligi.

Kocha Mkuu wa Young Africans amesema vijana wake wapo katika hali nzuri kuelekea mchezo wa jumamosi, kwani hakuna majeruhi hata mmoja katika kikosi chake cha wachezaji 20 walioingia kambini kujiandaa na mchezo huo.

Hans amesema Vijana wake wanazidi kuonyesha mabadiliko makubwa kiuchezaji, mafunzo yake wanaonekana kuyaelewa vizuri hivyo kikubwa anaomba waendelee kuwa katika hali nzuri kuelekea mchezo na ana imani kikosi chake kitaibuka na ushindi."Nina uzoefu na michezo wa watani wa jadi, huwa inakua migumu kwa kila timu kutokana na kila timu kutaka kuonyesha wapenzi, washabiki na wanachama wake kuwa wako vizuri, Simba ni timu nzuri lakini bado sioni kikwazo cha kutuzuia tusiibuke na ushindi katika mchezo huo" alisema Hans.

Leo jioni kikosi kitafanya mazoezi katika Uwanja wa Bko Beach Veterani ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo huo wa jumamosi ambapo kikosi cha Young Africans mpaka sasa kinashika nafasi ya pili kikiwa na pointi 55 huku kikiwa kimecheza michezo 25, Simba wakiwa nafasi ya nne na pointi 37 huku wakiwa wamecheza michezo 25.

Kikosi cha Young Africans kilichoingia kambini kujiandaa na mchezo huo ni:

Walinda milango: Deogratias Munish "Dida" na Ally Mustafa "Barthez"

Walinzi: Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Ibrahim Job, Rajab Zahir, Kelvin Yondani na Nadir Haroub "Cannavaro"

Viungo: Frank Domayo, Hassan Dilunga, Salum Telela, Hamis Thabit, na Nizar Khalfani

Washambuliaji: Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa, Jerson Tegete, Hamisi Kizza, Hussein Javu na Saimon Msuva.

16 WAONGEZWA KIKOSI CHA STARS
KOCHA Msaidizi wa Taifa Stars, Salum Mayanga ametangaza majina ya wachezaji 16 waliochaguliwa katika maboresho ya timu ya Taifa Taifa Stars kwenye hoteli ya Hill View jijini Mbeya.

Wachezaji hao ni kipa Benedicto Tinoko Simwanda (Temeke), mabeki wa kati; Emma Namwondo Simwanda (Temeke) na Joram Nason Mgeveje (Iringa). Walinzi wa pembeni ni Omari Ally Kindamba (Temeke), Edward Peter Mayunga (Kaskazini Pemba) na Shiraz Abdallah Sozigwa (Ilala).

Kikosi cha maboresho ya Taifa Stars kikiwa mjini MbeyaViungo ni Yusuf Suleiman Mlipili (Temeke), Said Juma Ally (Mjini Magharibi), Abubakar Ally Mohamed (Kusini Unguja), Hashim Ramadhan Magona (Shinyanga), Omari Athumani Nyenje (Mtwara) na Chunga Said Zito (Manyara).

Washambuliaji ni Mohammed Seif Saidi (Kusini Pemba), Ayoub Kasim Lipati (Ilala), Abdurahman Othman Ally (Mjini Magharibi), Paul Michael Bundara (Ilala). Wachezaji wa U 20 ni Mbwana Mshindo Musa (Tanga) na Bayaga Atanas Fabian (Mbeya).

Alisema mpango huu wa kuboresha timu ya Taifa ambayo inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ni endelevu na kusisitiza kuwa hata wale 18 walioachwa watafuatiliwa na TFF na kuitwa panapokuwa na mahitaji.

“Hawa wote wapo kwenye database ya TFF na hawataachwa tu hivi hivi wapotee,” alisema kocha Mayanga.

Wachezaji ha0 waliingia kambini mjini Tukuyu, Machi 21 mwaka huu na wamefanya mazoezi kwa pamoja kwa karibu wiki nne sasa kabla ya kuchujwa.

Wachezaji 16 waliochaguliwa wanatarajiwa kuondoka Tukuyu kesho (Aprili 18 mwaka huu) na kwenda kwenye kambi ya Taifa Stars katika Hoteli ya Kunduchi ambapo wataungana na wachezaji wa Taifa Stars wa siku zote.

Baadaye watachujwa tena ili ipatikane timu moja ya Taifa iliyoboreshwa.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjro Premium Lager inaunga mkono utaratibu huu wa maboresho ya Taifa na imewekeza zaidi ya dola milioni 2 kwa mwaka kudhamini Taifa Stars. Huu ndio udhamini mkubwa zaidi ambao Stars imewahi kupata tangu kuanzishwa kwa TFF/

Wednesday, April 16, 2014

UCHAGUZI MKUU YANGA JUNI 15


Kikao cha Kamati ya Utendaji kilichoketi tarehe 10 Aprili 2014 Makao Makuu ya klabu kiliazimia kuwa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa YANGA SC utafanyika tarehe 15 Juni 2014.


Taarifa za taratibu za Uchaguzi zitatangazwa hapo baadae na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Mh Alex Mgongolwa.

Imetolewa:
Young Africans SC
14 Aprili,2014

MAELFU YA MASHABIKI WAILAKI AZAMMASHABIKI wa Azam FC wamejitokeza kwa wingi jioni ya leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kuilaki timu yao, ikitokea Mbeya ambako jana iliifunga Mbeya City na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.


Msafara wa wa Azam uliwasili kwa ndege ya Fats Jet Saa 12:00 jioni hii na kupokewa na mamia ya wapenzi wake kabla ya kupanda basi lao la kisasa kuelekea makao yao makuu, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Ilikuwa hoi hoi, nderemo na vifijo katika mapokezi ya timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake katika mapokezi yake baada ya mabingwa hao wapya wa Bara kutua JNIA.

Azam ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana, baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine mjini hapa, huku waliokuwa wapinzani wao katika mbio za taji hilo, Yanga SC wakishinda 2-1 dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha jana pia.

Azam imefikisha pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho Aprili 19, mwaka huu. Yanga SC yenye pointi 55 sasa ikiifunga Simba SC wiki ijayo itafikisha 58.

Mabao ya Azam jana yalifungwa na Gaudence Mwaikimba na John Bocco, wakati la Mbeya City lilifungwa na Mwagane Yeya.

Licha ya kuwa timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wake jana, Azam FC pia inakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo

Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.

Monday, April 14, 2014

KOCHA OMOG WA AZAM FURAHA TUPU


KOCHA Mcameroon, Joseph Marius Omog amefurahia ushindi wa jana wa mabao 2-1

dhidi ya wenyeji Mbeya City Uwanja wa Sokoine ulioihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara timu yake, Azam FC, lakini amewaambia wachezaji wake, pati
ni baada ya mechi ya mwisho Aprili 19, mwaka huu.

“Ni furaha sana, tumepambana sana, haikuwa kazi nyepesi, tumepitia mechi ngumu
tangu naanza kazi hapa, lakini tulibaki kwenye dhamira yetu na tukaendelea kupambana
hatimaye tumetimiza malengo. Sote tuna furaha sasa, kila mtu ana sababu ya kufurahia
kazi yake kati yetu,”alisema Omog.

Omog amewataka wachezaji wake kutobweteka na matokeo ya jana, na badala yake
waelekeze nguvu zao katika mchezo wa Aprili 19, ili washinde na kukabidhiwa Kombe
kwa furaha. “Nasikia Yanga walikata rufaa, hata kama haina maana, lakini lazima
tushinde mechi ya mwisho, wachezaji wangu wanajua hilo, nimewaambia,”alisema.

Mabao ya Gaudence Mwaikimba na John Bocco ‘Adebayor’ kila kipindi jana yalitosha
kuihakikishia Azam FC ubingwa wa Ligi Kuu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya dhidi ya
bao la Mwagane Yeya.

Ushindi huo, umeifanya Azam ifikishe pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi
ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho Aprili 19, mwaka
huu.

Nafasi ya pili tayari ni Yanga SC yenye pointi 55 sasa baada ya jana kuifunga JKT
Oljoro 2-1 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha ambayo kama itawafunga pia na
Simba SC wiki ijayo itafikisha pointi 58, ambazo haziwezi pia kufikiwa na timu za chini
yake.

Azam FC itacheza mechi ya mwisho nyumbani, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam Jumamosi wiki hii, dhidi ya JKT Ruvu ikiwa na
dhamira ya kushinda ili kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bila kupoteza
mechi.

Kikosi cha Azam kinaondoka leo Saa 10:00 mjini Mbeya kwa ndege kurejea Dar es
Salaam na wachezaji watapewa mapumziko ya siku moja kabla ya kukutana kwa
maandalizi ya mchezo wa kufungia pazia la msimu.

JK ATUMA RAMBIRAMBI KIFO CHA GURUMO

RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutokana na kifo cha mwanamuziki maarufu na wa siku nyingi, Muhidini Gurumo kilichotokea juzi mjini Dar es Salaam.

Gurumo alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliomsumbua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Kikwete alisema mchango wa marehemu Gurumo kwa Taifa ni mkubwa na wa kupigiwa mfano kupitia kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu ambacho alikitumia kikamilifu kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Gurumo ambaye alikuwa mmoja wa wasanii wa muziki wa dansi nchini waliolitumikia Taifa hili kwa bidii tangu miaka ya sitini kupitia sanaa ya muziki,

Katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi kuanzia Bendi ya NUTA Jazz, Mlimani Park Orchestra, Orchestra Safari Sound (OSS) na Msondo Ngoma ambayo ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013,”alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alimuomba Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kumfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya marehemu Gurumo kwa kumpoteza kiongozi na mhimili wa familia yao.

Alisema anaungana na familia ya marehemu kuomboleza msiba huo mkubwa kwa kutambua kuwa msiba wao ni wa wote, na anamuomba Mwenyezi Mungu.

Aliwaomba wanafamilia ya marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba wa mpendwa wao kwa kutambua kwamba yote ni mapenzi ya mola.

0000
National Arts Council BASATA

Yah: Salaam za Rambirambi

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii nguli wa tasnia ya muziki wa Dansi nchini Muhidini Maalimu Ngurumo

“ Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Muhidini Maalimu Ngurumo ambaye mchango wake katika muziki wa dansi ni mkubwa mno na unahitajika sana, pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wake bado unahitajika katika tasnia hii.” Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini, aidha tunawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.

Mwenyezi Mungu aipumzishe mahala pema peponi roho ya marehemu. Baraza liko pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Imetolewa na
Godfrey Mngereza
Kaimu Katibu Mtendaji
Baraza la Sanaa la taifa.

Sunday, April 13, 2014

AZAM YAIVUA UBINGWA YANGA, SIMBA YAPIGWA NA ASHANTIAZAM jana ilifanikiwa kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwa mara ya kwanza baada ya kuichapa Mbeya City mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.


Azam imetwaa ubingwa huo huku ikiwa na mechi moja mkononi baada ya kufikisha pointi 59, ambazo haziwezi kufikiwa na mabingwa wa mwaka jana, Yanga ambayo jana iliichapa JKT Oljoro mabao 2-1 mjini Arusha.

Yanga imesaliwa na mechi moja dhidi ya Simba itakayochezwa Aprili 19 mwaka huu mjini Dar es Salaam na iwapo itashinda, itafikisha pointi 58.

Iliwachukua Azam dakika 44 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Gaudence Mwaikimba baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Mbeya City.

Mbeya City ilisawazisha dakika ya 70 kwa bao lililofungwa na Mwigane Yeya kwa tiktak.

Wakati mashabiki wakidhani mechi hiyo ingemalizika kwa sare, John Bocco alibadili matokeo dakika ya 84 baada ya kuifungia Azam bao la pili.

Pambano kati ya Yanga na JKT Oljoro lilikuwa na ushindani mkali kutokana na timu hizo mbili kucheza kwa kukamiana.

JKT Oljoro ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 68 lililofungwa na Jacob Masawe baada ya kupokea pasi kutoka kwa Shija Mkina.

Yanga ilisawazisha dakika ya 75 baada ya Rajabu Zahir, aliyeingia badala ya Ibrahim Job kufunga bao.

Bao la pili na la ushindi la Yanga lilifungwa na Mrisho Ngasa dakika ya 71 baada ya kupokea krosi kutoka kwa Simon Msuva.

Wakati huo huo, timu kongwe ya soka nchini, Simba jana ilipigwa mweleka wa bao 1-0 na Ashanti katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao pekee na la ushindi la Ashanti lilifungwa na Mohamed Nampaka dakika ya 17 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Hassan Kabunda.

BURIANI MUHIDIN MAALIM GURUMONA RASHID ZAHOR
NYOTA imezimika. Mbuyu umeanguka. Ndivyo unavyoweza kukielezea kifo cha mwanamuziki mkongwe nchini, Muhidin Maalim Gurumo.

Mkongwe huyu wa muziki nchini aliiaga dunia jana mchana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, ambako alikuwa amelazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia yake, Gurumo alipelekwa kwenye hospitali hiyo juzi baada ya kupatwa na shinikizo la damu.

Taarifa za kifo cha Gurumo zilianza kusambaa kwenye mitandao na ujumbe wa simu za mkononi kama moto uwakao nyikani. Wapo walioziamini, lakini wengine walidhani ni uzushi uliozoeleka katika siku za hivi karibuni, hasa kwa wasanii na watu maarufu.

Binafsi nilipopata taarifa hizo nilishtuka. Ni baada ya kuzungumza na baadhi ya wanamuziki wa bendi yake ya Msondo Ngoma, akiwemo msemaji wa bendi hiyo, Super Deo ndipo nilipoanza kuamini.

Ni kweli kwamba kifo huua mwili wa binadamu ukabaki kuwa vumbi kaburini, lakini yote aliyoyafanya hapa duniani, yatabaki kuwa kumbukumbu ya milele kwa vizazi vya sasa na vitakavyokuja baadaye.

Kwa mara ya mwisho nilikutana ana kwa ana na marehemu Gurumo mwaka jana nilipokwenda nyumbani kwake Ubungo Makuburi, Dar es Salaam. Lengo la kumtembelea Gurumo lilikuwa kuandika makala juu ya masha yake kimuziki.

Makala hiyo ya Gurumo, iliyotoka kwenye gazeti la Burudani, ambalo ni gazeti dada la magazeti ya Uhuru na Mzalendo, ni sehemu ya makala nne za muziki wa dansi na kizazi kipya, ambazo niliandika kwa ufadhili wa Tanzania Media Fund (TMF).

Wakati huo Gurumo alikuwa ametoka kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa moyo na mapafu. Lakini siku hiyo alionekana kuwa na afya njema. Alizungumza kwa ucheshi na kuzungumzia mambo mengi kuhusu maisha yake kimuziki na hata kutoa somo kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya.

Baada ya mahojiano hayo yaliyodumu kwa saa mbili, nikiwa na mwandishi wa zamani wa gazeti la Mfanyakazi, Michael Magembe, mkongwe huyo wa muziki alitusindikiza kutoka nyumbani kwake hadi kituo cha mabasi cha Gereji kisha akaendelea kutembea kwa miguu hadi zilipo ofisi za gazeti la Mwananchi.

Njiani nilijaribu sana kumsihi Mzee Gurumo asifike mbali kwa kuwa alikuwa ametoka kuugua kwa muda mrefu, lakini hakutaka kukuubaliana na mimi.

"Mbona sasa hivi nipo fiti kabisa. Hii ni sehemu ya mazoezi. Huku kote najulikana, ukiuliza tu kwa Gurumo wanakuleta mpaka nyumbani kwangu,"alinieleza Gurumo huku akitabasamu.

Wakati mimi na mwenzangu tukisubiri basi kurudi mjini, Gurumo aliendelea kutembea taratibu kwenda zilipo ofisi za Mwananchi. Tulibaki tukimkodolea macho kwa mshangao.

Marehemu Gurumo alitangaza kustaafu kazi ya muziki mwaka jana baada ya kuifanya kazi hiyo kwa miaka 53.

Gurumo (74), alitangaza uamuzi wake huo Agosti 22, mwaka jana alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), mjini Dar es Salaam.

Mkongwe huyo wa muziki alisema aliamua kustaafu kutokana na umri wake mkubwa.

Licha ya kujihusisha na muziki katika sehemu kubwa ya maisha yake, Gurumo alisema hakupata mafanikio makubwa kimaisha, licha ya kujenga nyumba anayoishi na familia yake, iliyoko Ubungo Makuburi, Dar es Salaam.

Katika kipindi alichopiga muziki katika bendi za NUTA, JUWATA, OTTU na Mlimani Park, Gurumo alitunga nyimbo zaidi ya 200.

Alijiunga na NUTA 1964 akiwa mmoja wa waanzilishi kabla ya kuhamia Mlimani Park 1978 na Orchestra Safari Sound (OSS) kuanzia 1985 hadi 1990.

Marehemu Gurumo alikuwa kipaji cha kutunga nyimbo zenye ujumbe kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Alikuwa gwiji katika uimbaji na jina la Gurumo halikuwa la utani kwa sababu ya kuimba kwa sauti nzito, bali ni jina lake halisi.
Aliposimama jukwaani kuimba katika bendi za Msondo Ngoma, OSS na Mlimani Park Orchestra, mashabiki waliburudika kutokana na sauti yake nzito, ambayo ilikolezwa na nyingine za Hassan Bitchuka, marehemu Moshi William, Thobias Chidumule, hayati Hamisi Juma na Maxi Bushoke.

Katika wimbo wa Kassim aliouimba akiwa Mlimani Park, Gurumo akishirikiana na Hamisi Juma (sasa marehemu), aliimba na kutoa picha halisi ya mlevi wa pombe aliyeanza kufilisika na kubana matumizi, wakati Hamisi aliimba kama mwanamke, aliyezoea kupewa ofa na Gurumo.

“Na mie moja Kassim,” anaimba Hamisi katika wimbo huo.

“Sina hela ya mchezo,” anajibu Gurumo.

Wimbo mwingine uliompa sifa Gurumo ni Celina aliouimba akiwa na Mlimani Park. Katika wimbo huo, Gurumo anasikika akiimba: ‘Na kwa sababu imekuwa hivyo Celina, sioni haja ya kutaka ujiue kwa ajili yangu”. Wimbo huo ulitungwa na marehemu Joseph Mulenga, aliyekuwa akipiga gitaa la solo.

Akiwa OSS, alipata umaarufu kupitia wimbo wa Chatu mkali. Katika wimbo huo, sauti yake nzito inasikika alipoimba: ‘Natoa onyo kwa yeyote anayemchezea chatu ni hatari, atakuwa asipate lolote la manufaa, na ajali imkute bila ya kutegemea, atakuja adhirika ajute na dunia.

Nyimbo zingine, ambazo zinakumbusha kazi ya Gurumo tangu alipojitosa kwenye fani ya muziki ni ‘Salima’, ‘Bwana Abdul’, ‘Dada Fatuma’, ‘Kulima Hadeka’ (umelima bondeni) na ‘Agweti Chole’ (Mwenzangu Twende) zilizoimbwa kwa lugha ya Kizaramo. Alitunga nyimbo hizo alipokuwa Kilwa Jazz.

Gurumo alizaliwa 1940 katika kijiji cha Masaki, Kisarawe mkoani Pwani. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Sungwi na kumaliza darasa la saba 1956. Pia alipata mafunzo ya dini ya Kiislamu katika madrasa ya kijiji alichokuwa akiishi.

Baada ya kumaliza shule, aliamua kujiunga na bendi ya Kilimanjaro Chacha iliyokuwa na maskani Ilala, Dar es Salaam. Alifanya kazi na bendi hiyo hadi 1961 alipojiunga na Rufiji Jazz pia ya Dar es Salaam.

Alidumu na bendi hiyo hadi 1963 alipojiunga na Kilwa Jazz, iliyokuwa maarufu enzi hizo chini ya uongozi wa marehemu Ahmed Kipande. Bendi hiyo ilikuwa na makundi mawili, Kilwa A na B, Gurumo alikuwa kundi B.

Gurumo hakupendezwa na uamuzi wa marehemu Kipande kumuweka katika kundi B, wakati alijiona ana uwezo mkubwa wa kuimba kuliko baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi A. Hali hiyo ilimfanya ajiunge na NUTA Jazz 1964.

Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Jumuia ya Wafanyakazi Tanzania na baadaye ilibadili majina na kuitwa JUWATA na OTTU Jazz. Baada ya jumuia hiyo kujitoa katika kuendesha bendi, ilikabidhi vyombo kwa wanamuziki, ambao waliamua kuibadili jina na kuiita Msondo Ngoma.

Akiwa OTTU hadi Msondo Ngoma, alitunga nyimbo nyingi ukiwemo wa ‘Wosia kwa Watoto’.

Gurumo ndiye muasisi wa mitindo ya muziki ya Msondo, akiwa na NUTA, JUWATA na OTTU Jazz, Sikinde akiwa na Mlimani Park na Ndekule akiwa na OSS, ambayo ilizipatia umaarufu mkubwa bendi hizo.

Mitindo hiyo ya muziki ilitokana na majina ya baadhi ya ngoma za kabila la Wazaramo na huchezwa kama ilivyo ngoma ya Vanga.

Tofauti ni kwamba, wachezaji wa ngoma hizo huvaa mavazi ya asili, wakati wale wa muziki wa dansi huvaa mavazi ya kawaida.

Kabla ya uamuzi wa kustaafu muziki, Gurumo alishauriwa na daktari aliyekuwa akimtibu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, kujiweka kando na masuala ya muziki baada ya kuugua ugonjwa wa moyo na kulazwa hospitali mara kadhaa.

Ugonjwa wa moyo hutokana na kupungua damu inayoingia kwenye mishipa ya moyo, ambao haukumpata Gurumo kwa sababu ya kuimba.

“Sijapatwa na ugonjwa huu kwa sababu ya kuimba kwa miaka mingi. Baada ya kupata tiba, madaktari walinishauri nipumzike kwa sababu ya umri kubwa mkubwa, siwezi tena kusimama jukwaani kwa muda mrefu na kuimba,” anasema. Alianza kusumbuliwa na maradhi mwaka 2011.

Gurumo ni mmoja wa wanahisa wa bendi ya Msondo. Wengine ni Saidi Mabela, Saidi Kibiriti (meneja), Ramadhani Zahoro, Abdul Ridhiwani, Roman Mng'ande na Huruka Uvuruge.

Wanamuziki hao wanamiliki kiwango sawa cha hisa na malipo yao kwa mwezi ni makubwa ikilinganishwa na waajiriwa.

Hata hivyo, Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti, hakuwa tayari kutaja viwango vya malipo wanavyolipana.

Kwa Gurumo, muziki wa dansi, ambao wanamuziki hutumia ala mbalimbali, kama vile magitaa, tumba, ngoma, tarumbeta na vinanda katika kuupamba na kuufanya uwe na mvuto wa aina yake, utatoweka iwapo vituo vya redio na televisheni nchini vitaendelea kuacha kupiga nyimbo hizo.

"Ukifungua televisheni yoyote, kuanzia asubuhi hadi jioni, nyimbo zinazopigwa ni za bongo fleva tu. Huwezi kusikia nyimbo za muziki wa dansi. Hii maana yake ni kwamba, vyombo hivi vinaua muziki wetu makusudi," anasema.

Hata hivyo, Gurumo alisema wapo watunzi na waimbaji wengi wazuri wa nyimbo za muziki wa dansi na alikuwa anavutiwa na Hassan Bitchuka wa Mlimani Park na Hussein Jumbe wa Talent Band.

Mkongwe huyo alisema muziki wa kizazi kipya, ambao hutengenezwa studio kwa kutumia kompyuta, na kuimbwa katika miondoko mbalimbali kama vile, hip hop, R&B na Zouk, ukichezwa kwa kurukaruka na kujinyonganyonga mwili, ni mzuri kwa wakati uliopo, hususan kwa vijana.

Hata hivyo, alisema hauwezi kudumu kwa vile wasanii wanatumia zaidi kompyuta kuutengeneza.

Gurumo alisema wasanii wa muziki huo wanapata mafanikio tofauti na zama zao, kwani hivi sasa sheria ya hatimiliki inawalinda.

Alisema muziki umemwezesha kujuana na kufahamiana na watu wengi, wakiwemo viongozi wa serikali. Alitoa mfano wa Rais Jakaya Kikwete, ambaye alikwenda kumjulia hali alipokuwa amelazwa Muhimbili.

Mke wa mwanamuziki huyo, Pili Kitwana, ambaye alikuwepo wakati wa mahojiano hayo alisema, mumewe ana jina kubwa kimuziki, lakini maisha yake ni ya kawaida. Pili na Gurumo walifunga ndoa mwaka 1967 na wamezaa watoto wanne.

Mpiga gita la solo wa Msondo Ngoma, Mabela, anasema Gurumo ameshiriki kuimba nyimbo na pia kutunga zingine, zikiwemo Shaba imelia, Kilimo cha kufa na kupona, Ikiwa kama hunitaki, Nimuokoe nani, Heko Mwalimu Nyerere na Baba nipeleke kwa mama.

Kwa mujibu wa Mabela, watunzi wa nyimbo nyingi za bendi hiyo walikuwa yeye, marehemu Joseph Lusungu, Khalfan Mabruki na Hassan Bitchuka.

Kwa upande wake, Bitchuka anasema Gurumo alikuwa kiongozi msikivu na alitoa ushauri kwa wanamuziki wenzake.

"Gurumo hakuwa mtu wa kuchezewa. Kama hujui muziki, hawezi kuwa rafiki yako na kama unaujua, atakuwa rafiki yako mkubwa," anasema.

Bitchuka anasema Gurumo alikuwa kiongozi jasiri, asiyeyumba, mwenye msimamo na alitunga nyimbo nyingi, hususan akiwa bendi za Mlimani Park na OSS.

Kiongozi wa bendi ya Extra Bongo, Ally Choki, anasema Gurumo ni mwanamuziki aliyekuwa makini katika kazi yake.

"Kwa mtu wa umri wake, isingekuwa rahisi kupanda jukwaani hadi sasa na kuimba. Ni wa kupigiwa mfano na vijana wanaochipukia kimuziki," anasema.

Anasema alihamasika kurekodi albamu na Gurumo kutokana na kuvutiwa na uwezo wake kimuziki.

Albamu hiyo ina nyimbo sita, tatu zimetungwa na Gurumo na tatu za Choki. Albamu hiyo inajulikana Choki/Gurumo remix.

Nyimbo za Gurumo zilizomo kwenye albamu hiyo ni Nipeleke kwa baba, Ikiwa kama hunitaki na Nimuokoea nani.

Kutokana na kilio cha marehemu Gurumo cha kutaabika kimaisha, msanii wa muziki wa kizazi kipya Nasib Abdul, Diamond alimkabidhi gari mkongwe huyo.

Diamond alimkabidhi mzee huyo gari hilo wakati wa hafla ya kuzindua video ya wimbo wake mpya uitwao My Number One iliyofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.

Baada ya kuizungumzia video yake hiyo na changamoto aliyokutana nazo wakati wa kutengeneza video hiyo, ndipo alipomuita stejini mzee Gurumo na kuweka wazi namna ambavyo amekuwa akimpenda na kumheshimu nguli huyo huku akisisitiza kuwa amesikitishwa na namna mzee huyo anavyohangaika.

Ndipo Diamond alipomuita jukwaani na kumkabidhi ufunguo wa gari, hali iliyosababisha wageni waalikwa kupiga kelele za kushangilia baada ya kuguswa na tukio hilo.

Baada ya zoezi hilo, Diamond alimshika mkono mzee huyo na kisha wakiongozana na wageni waalikwa kwa pamoja walitoka nje na kwenda kuliangalia gari hilo kabla ya kurejea ndani na kuendelea na ratiba kama kawaida.

NSSA YAPONGEZWA KUVIUNGANISHA VYOMBO VYA HABARIWAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangala amelipongeza Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuviunganisha vyombo vya habari anuai nchini Tanzania kupitia tasnia ya michezo.

Dk. Mukangala ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia kwa niaba ya waziri, alipokuwa akifunga rasmi Mashindani ya 11 ya NSSF yanayoshirikisha vyombo vya habari anuai katika mchezo wa mpira wa miguu na mpira wa pete kwa wasichana.

Dk. Mukangala alisema kwamba mashindano hayo yamekuwa yakivikutanisha vyombo anuai vya habari kutoka Tanzania Bara na Visiwani hivyo kujenga uhusiano mzuri kwa washiriki kupitia michezo, huku yakiimarisha uhusiano kati ya vyombo hivyo na shirika la NSSF ambalo hudhamini mashindano hayo kila mwaka kwa muda wa miaka 11 mfululizo hivi sasa.

"...Hakuna ubishi kwamba miaka 11 sio michache kwa kuendesha mashindano kama haya, lakini kwa sababu uongozi wa NSSF unaheshimu na kukubali nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha jamii ni wazi kwamba mtaendelea kutenga bajeti ya mashindano haya kila mwaka," alisema Dk. Mukangala.

Aidha aliwapongeza washindi wa mwaka huu kwa jitihada na nidhamu ya mchezo waliozionesha hadi kufanikiwa kutwaa ushindi, hivyo kuwataka wanahabari wote kuendelea kuyatumia mashindano hayo kwa kujenga mahusiano mazuri na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii.

Mwaka huu timu ya Kampuni ya Bussnes Times Limited (BTL) imefanikiwa kutwaa kombe la mpira wa miguu na kuzawadiwa fedha shilingi milioni nne na nusu baada ya kuishindilia Changamoto mabao matatu kwa mtungi, nafasi ya pili ilichukuliwa na timu ya Changamoto na kujinyakulia kikombe pamoja na kitita cha shilingi milioni tatu na nusu.

Mshindi wa tatu mpira wa miguu imeibuka timu ya wenyeji wa mashindano hayo NSSF baada ya kuifunga timu ya Mwananchi, hata hivyo NSSF walichukua kikombe na kusamehe kitita chao cha shilingi milioni 2 kilichokabidhiwa mshindi wa nne, yaani Timu ya Mwananchi.

Neema ya mashindano hayo mwaka huu iliiangukia kampuni ya BTL ambapo kwa upande wa mpira wa Pete pia timu ya wasichana ya kampuni hiyo ilifanikiwa kutwaa ubingwa na kukabidhiwa kombe na fedha shilingi milioni 4, nafasi ya mshindi wa pili imechukuliwa na timu ya Habari kutoka Zanzibar na kujinyakulia kiasi cha shilingi milioni tatu na nusu.

Washindi wa tatu mpira wa pete imeibuka timu ya NSSF ambao walitwaa kombe bila fedha ambazo zilichukuliwa na mshindi wa nne (Mwananchi).

Kikombe cha nidhamu kimenyakuliwa na timu ya Tumaini wamiliki wa Redio na TV Tumaini pamoja na gazeti la Tumaini Letu.

Jumla ya timu 20 za mpira wa miguu na 18 za mpira wa pete zimeshiriki mashindano hayo kwa mwaka huu idadi ambayo inazidi kuongezeka kila mwaka tangu kuanza kwa mashindano hayo.

Hafla ya kufunga mashindano hayo iliyofanyika katika viwanja vya Sigara (TCC) jijini Dar es Salaam pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Abubakar Rajabu, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau viongozi waandamizi wa shirika la NSSF pamoja na wageni mbalimbali waalikwa.

Thursday, April 10, 2014

YANGA RAHA TUPUMAMIA ya mashabiki wa Yanga jana walitoka uwanjani roho kwatu baada ya kuishuhudia timu yao ikipata ushindiwa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilicheza kwa kasi kubwa na kuweza kuvuna pointi zote tatu kutoka kwa wapinzani wao.

Kutokana na ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 52 na iko nafasi ya pili, nyuma ya vinara Azam wenye pointi 53. Mechi ya Azam na Ruvu Shooting haikuchezwa jana kutokana na mvua kubwa kunyesha mkoani Pwani.

Mechi hiyo, ambayo itaonyesha mustakabali wa timu ipi itakayotwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu, sasa itachezwa leo kwenye uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi.

Yanga sasa imebakiwa na mechi mbili dhidi ya JKT Oljoro itakayochezwa Aprili 13 mjini Arusha kabla ya kuvaana na watani wao Simba katika mechi ya mwisho itakayopigwa Aprili 19 mwaka huu.

Kwa upande wa Azam, baada ya mechi ya leo, itasaliwa na mechi zingine mbili dhidi ya Mbeya City itakayochezwa mjini Mbeya kabla ya kuvaana na JKT Ruvu.

Yanga ilihesabu bao lake la kwanza dakika ya tatu kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Simon Msuva.

Bao la pili la Yanga lilifungwa na Didier Kavumbagu dakika ya 34 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi kutoka kwa Msuva.

Kagera ilipata bao la kujifariji dakika ya 62 kupitia kwa mshambuliaji wake, Daudi Jumanne baada ya beki Oscar Joshua kumrejeshea mpira dhaifu kipa wake, Deogratius Munishi 'Dida.

BUSHIRI KOCHA BORA LIGI KUU ZANZIBAR

Makamu Mwenyekiti wa BMZ Khamis Said, kushoto akimkabidhi Cheki ya shilingi milioni moja Kocha Bora wa Ligi Kuu ya Grand Malt, Ali Bushiri wa Timu ya KMKM.

DRFA YAOMBOLEZA KIFO CHA JIMMY MHANGO


CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimetuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Mjumbe wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi, Jimmy Mhango aliyefariki juzi katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kutokana na presha.


Katibu Mkuu wa DRFA, Msanifu Kondo amesema leo (Oktoba 22) kwamba wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mjumbe huyo, ambaye pia aliwahi kuwa mchezaji mahiri katika timu ya Ushirika ya Moshi katika miaka ya tisini chini ya Kocha Dan Korosso.

Marehemu pia aliwahi kuzichezea timu za Pan Africans ya Dar es Salaa pamoja na timu ya Mkoa wa Kilimanjaro ‘Kilimanjaro Stars.

“DRFA imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Jimmy Mhango na inatoa pole kwa familia, ndugu jamaa na wanafamilia wote wa mpira wa miguu, tunawaomba wawe na subira katika kipindi hiki kigumu,” alisema.

Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya DRFA ambayo marehemu alikuwa mjumbe, inaongozwa na Roman Masumbuko (Mwenyekiti), Fahadi Kayuga (Makamu Mwenyekiti), Mohamed Mpili (Mjumbe) na Peter Nkwera (Mjumbe).

Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo (Jumanne)katika makaburi ya Ilala Mchikichini, Dar es Salaam saa kumi jioni. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema

Imetolewa na Mohamed Mharizo
Ofisa Habari
Chama Cha Mpira Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
Oktoba 22, 2013

TWANGA PEPETA YAINGIA MKATABA NA PRAIN PROMOTIONS


BENDI ya muziki wa dansi nchini ya African Stars 'Twanga Pepeta',
wameingia mkataba maalumu na kampuni ya Prain Promotions
Limited kwa ajili ya utengenezaji wa kazi zao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka, alisema mkataba
huo una manufaa kwa bendi hiyo kutokana na kutaka
kuwanufaisha wanamuziki na wasanii wa nchini kwa ujumla.

Baraka alisema kampuni hiyo ambayo awali ilikuwa
ikijishughulisha na usambazaji wa kazi za filamu, imeamua kuingia
mkataba na bendi yake kutokana na ubora wao.

Alisema wasanii nchini wanatakiwa kunufaika na kazi
wanayoifanya, na Prain wameihakikishia Twanga kuwa kazi zao
sasa zimetengenezwa kwa ubora wa hali ya juu kiasi cha
kumshinda mtu yeyote kuirudufu.

"Tunataka maendeleo ya wasanii, tumekuwa tukiwakumbatia
zaidi wasanii wa nje, lakini muunganiko wetu sasa utasaidia kuinua
hali ya kipato sahihi kwa wanamuziki tulionao," alisema Baraka.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Prain Promotions, Evance
Steven, alisema kampuni yao imeamua kuingia kwenye muziki na
kuichagua Twanga Pepeta kuwa bendi ya kwanza kutokana na
kazi yao wanayofanya katika burudani.

Steven alisema kazi kubwa waliyoanza nayo katika albamu ya
Twanga Pepeta ya Dunia Daraja ni kuhakikisha kuwa haiwezi
kunakiliwa (kurudufiwa) upya na maharamia wa kazi za kisanii
nchini kama ilivyozoeleka.

"Tumewahakikishia wenzetu wa Twanga Pepeta kuwa kazi zao
sasa ziko salama kuuzwa kihalali kutokana na kuziwekea programu
maalumu ya kushindwa kunakilika, hivyo kila mtu atanunua
kihalali kazi za bendi hii za Dunia Daraja," alisema ofisa huyo.

Twanga itaanza kuuza kazi hizo katika kila maonesho yao huku
zikionekana kufungwa katika ubora wa hali ya juu alipokuwa
akiwaonesha waandishi wa habari utofauti mkubwa uliofanywa
na Prain, ambapo pia zina stika maalumu za TRA (Mamlaka ya
Mapato Tanzania).

Wednesday, April 9, 2014

TFF YAWAPONGEZA MSHUJAA WA BRAZIL

Tunaipongeza timu ya Tanzania ya Watoto wa Mitaani kwa kutwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani baada ya jana (Aprili 6 mwaka huu) kuifunga Burundi mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Ushindi kwa timu hiyo ni fahari kwa Tanzania, lakini kubwa ni kwa kituo cha Mwanza ambacho ndicho kinachoiendesha pamoja na wadhamini na wafadhili walioiwezesha kushiriki fainali hizo kwa mara ya pili mfululizi.

Vilevile ushindi huo unatoa changamoto kubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kuwa watoto wa mitaani ni sehemu tu ya vipaji vilivyotapaa nchini, hivyo iliyopo ni kuvisaka na kuvibaini vipaji hivyo kwa ajili ya ustawi wa mchezo huo nchini.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tutaendelea kushirikiana na kituo hicho cha Mwanza, na vingine vyote ambavyo vinajishughulisha na mchezo huu, lengo likiwa ni kuundeleza na hata kutoa ajira kwa vijana hapo baadaye kupitia mpira wa miguu.

Timu hiyo inarejea nchini Alhamisi (Aprili 10 mwaka huu) ambapo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10 jioni kwa ndege ya Emirates

NGORONGORO HEROES KUINGIA KAMBINI LEO


Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngongoro Heroes) imereja nchini leo mchana (Aprili 7 mwaka huu) kutoka Kenya mechi ya michuano ya Afrika dhidi ya wenyewe, na itaingia kambini Alhamisi.


Ngorongoro Heroes ambayo imewasili saa 8.25 kwa ndege ya Kenya Airways ilitoka suluhu na Kenya katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kanyetta uliopo katika mji wa Machakos.

Kocha John Simkoko amesema benchi lake la ufundi linafanyika kazi upunguzi uliojitokeza ili wafanye vizuri kwenye mechi ya marudiano itakayochezwa Aprili 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Iwapo Ngorongoro Heroes itaitoa Kenya, raundi inayofuata itacheza na Afrika Kusini. Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 zitafanyika mwakani nchini Senegal.

Monday, April 7, 2014

NGORONGORO HEROES KUREJEA LEO


Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngongoro Heroes) inarejea nchini leo (Aprili 7 mwaka huu) kutoka Kenya ambapo jana (Aprili 6 mwaka huu) ilicheza mechi ya michuano ya Afrika.

Ngorongoro Heroes ambayo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8.25 mchana kwa ndege ya Kenya Airways ilitoka suluhu na wenye Kenya katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kanyetta uliopo mji wa Machakos.

Timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam wiki tatu baadaye ambapo itakayofuzu itacheza raundi ya pili dhidi ya Afrika Kusini. Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 zitachezwa mwakani nchini Senegal.

WATOTO WA MITAANI WA TANZANIA WATWAA UBINGWA WA DUNIATimu ya Taifa ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imetwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani baada ya jana (Aprili 6 mwaka huu) kuilaza Burundi mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Mshambuliaji Frank William alifunga mabao matatu katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja mkongwe na maarufu wa klabu ya Fluminense huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Fedha wa Uingereza, George Osborne.

Tanzania ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuitandika Marekani mabao 6-1 ambapo hadi mapumziko ilikuwa mbele kwa mabao 4-0.

Burundi ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuifunga Pakistan mabao 4-3 katika mechi ya nusu fainali ya pili.

Timu ya Tanzania inarejea nchini Alhamisi (Aprili 10 mwaka huu) ambapo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10 jioni kwa ndege ya Emirates


Tanzania boys win 2014 Street Child World Cup

Tanzania boys won the 2014 Street Child World Cup producing a powerful performance to beat their neighbours Burundi 3-1. After the game both teams joined together to stress that the Street Child World Cup was more than just a game, and to congratulate the players from all teams at the tournament.


Tanzania and Burundi had already faced each other in the 2014 Street Child World Cup in the opening fixture of the group stages. Tanzania had looked on course for an impressive opening victory, taking a two-goal lead, only for Burundi to demonstrate their remarkable resilience to mount a second half comeback and get a draw.

So when Tanzania were 2-0 up at half time in the final they were very aware that the game was far from over. But instead of letting Burundi back into the game, this time Tanzania scored the first goal of the second half, completing a hat-trick for Frank, to put the game out of Burundi’s reach. Although Burundi got a consolation goal, it was too late to change the outcome of the game.

In the first half despite having the better of the opening exchanges Burundi failed to get a shot on target. Burundi moved the ball around with familiarly impressive passing, but failed to test the Tanzania keeper. Then after seven minutes a clever sidestep by Frank left him in space and he fired home into the top corner. The goal against the run of play began a passage of end-to-end action, which only ended when Frank bagged his second goal from a tight angle.

After the game the Tanzania team were quick to congratulate the Burundi team for their performance, and Tanzania captain Deograutis said it was a demonstration of the bonds developed between squads throughout the Street Child World Cup: “We are friends and neighbours with the Burundi team, and know what it is like to lose the final, so we wanted to show them our support.

“We’re happy because in 2010 we were in the final but didn’t win the cup. We’re representing all the children in Tanzania, and we hope we’ve made them proud.”

Team Tanzania is organised by Tanzania Street Children Sports Academy which works with around 300 street children. TSCSA works in three areas; outreach through street-based work, using sport as an educational tool through work in schools and running a football academy.

TSCSA President Altaf Hirani thinks all the Street Champions have demonstrated their talents and exuberance throughout the tournament: “These children have shown what they can do if they are given opportunities and the chance to flourish. The Street Child World Cup has been a great way to raise awareness of the global campaign to protect children. We would like to thank the organisers and the volunteers, who have been fantastic right from the start.”

Tanzania coach Suleiman Jabir added that TSCSA hope winning the Street Child World Cup will be a vehicle to increasing their deliver of support to children: “We hope we can use this as a stepping stone, to help more children in Tanzania and to campaign to the government to pass policies to support children. But this isn’t just about Tanzania, this is about children everywhere.”

Team Burundi is organised by New Generation, which is fostering relations between boys from different ethnic backgrounds in a country scarred by civil war. The players are former street children, who New Generation are working to get back into the community and education.

Burundi coach Teddy Bright thinks his team demonstrated the values New Generation tries to foster in its players: “It’s important to play together, to know each other as friends and trust each other. We’re really happy to be at this event to raise awareness for street children, not just in Burundi but all over the world.”

Sunday, April 6, 2014

WATOTO WA MITAANI WATINGA FAINALI BRAZIL


Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil baada ya jana kuifunga Indonesia kwa jumla ya mabao 5-3.

Hadi muda wa kawaida wa mchezo huo unamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2 ndipo ikatumia mikwaju ya penalti kuamua mshindi. Tanzania ilipata penalti tatu dhidi ya moja ya wapinzani wao.

Kwa matokeo hayo, Tanzania sasa itacheza mechi ya nusu fainali leo dhidi ya Marekani ili kupata timu zitakazocheza mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu. Mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa kesho (Aprili 6 mwaka huu).

Timu nyingine zilizoingia nusu fainali na mechi zake zinachezwa leo (Aprili 5 mwaka huu) ni Burundi itakayocheza na Pakistan.

Katika mechi zilizopita, Tanzania ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi, ikaitandika Argentina mabao 3-0 ikailaza Nicaragua mabao 2-0 na ikafungwa na Philippines mabao 2-0.

TAIFA STARS, BURUNDI KUCHEZA APRILI 26Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mechi ya kirafiki na Burundi (Intamba Mu Rugamba) Aprili 26 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya ikijiandaa kwa ajili ya mechi hiyo ikiwa na wachezaji waliopatikana katika programu maalumu ya kusaka vipaji.

Baadaye wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wapo nje ya programu ya kusaka vipaji wataungana na wenzao kabla ya kutengeneza kikosi cha mwisho kitakachoivaa Burundi.
Mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachezeshwa na waamuzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kutoka nchini Kenya.

21 KUCHEZA RCL


Timu 21 kati ya 27 zitakazocheza Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kutafuta tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao tayari zimejulikana.

Timu hizo ni Abajalo SC (Dar es Salaam), AFC (Arusha), African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Geita Veterans (Geita), JKT Mafinga (Iringa), JKT Rwamukoma (Mara), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United (Pwani), Milambo SC (Tabora) na Mshikamano FC (Dar es Salaam).

Nyingine ni Mvuvumwa FC (Kigoma), Navy SC (Dar es Salaam), Njombe Mji (Njombe), Pachoto Shooting Stars (Mtwara), Panone FC (Kilimanjaro), Singida United (Singida), Tanzanite (Manyara), Town Small Boys (Ruvuma), Ujenzi FC (Rukwa) na Volcano (Morogoro).

WATANO WAFANYA MTIHANI WA UWAKALA WA WACHEZAJI
Watanzania watano wamefanya mtihani wa uwakala wa wachezaji wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambao ulifanyika jana (Aprili 3 mwaka huu) duniani kote.

Watahiniwa katika mtihani huo ambao ulikuwa na maswali kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) walikuwa Godlisten Anderson, Jesse Koka, Lutfi Binkleb, Rwechungura Mutahaba na Silla Yalonde.

NAVY SC, ABAJALO, MSHIKAMANO KUIWAKILISHA DAR LIGI YA MABINGWA WA MIKOA


CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimetangaza timu tatu zilizofanikiwa kucheza Ligi ya Mabingwa wa Mikoa baada ya kufanya vizuri katika Ligi Daraja la Pili Mkoa wa Dar es Salaam iliyomalizika Jumapili iliyopita.

Ofisa Habari wa DRFA Mohamed Mharizo amesema timu hizo ni Navy SC ya Temeke iliyokua vinara baada ya kujizolea pointi 34 ikifuatiwa na Abajalo ya Sinza iliyojikusanyia pointi 31 na Mshikamano ya Temeke iliyokua na pointi 30.

“Ligi yetu naweza kusema ilikua bora nay a ushindani kwa sababu tulianza raundi ya kwanza tukiwa na timu 32 na baadae zikabaki timu 16 ambazo katika hizo tatu ndio zimefanikiwa kuwakilisha mkoa wetu wa Dar es Salaam katika Ligi ya Mabingwa wa mikoa inayotarajia kuanza Aprili 20 mwaka huu.

“Kwa niaba ya uongozi wa DRFA, tunazipongeza timu hizi na tunaamini kwa dhati kabisa kuwa zitatuwakilisha vyema katika Ligi ya Mabingwa wa mikoa na hatimaye kufuzu kucheza Ligi Daraja la Kwanza,” alisema Mharizo.

Imetolewa Aprili 4, 2014
Mohamed Mharizo
Ofisa Habari
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).

Thursday, April 3, 2014

KOCHA AZAM ATAMBA UBINGWA NI WAOKOCHA Mkuu wa Azam FC, Joseph Marius Omog amewataka wachezaji wake kutobweteka kwa ushindi wa jana dhidi ya Simba SC, kwani vita ya ubingwa bado ni kali na Mbeya City na Yanga SC nao pia wote wana nafasi ya kubeba taji.

Azam FC jana iliifunga Simba SC mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kufikisha pointi 53 baada ya kucheza mechi 23 mbele ya Yanga SC yenye pointi 46 za mechi 22 na Mbeya City yenye pointi 45 za mechi 23.

Omog ambaye ni raia wa Cameroon amewataka wachezaji wake kuendelea kupambana kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizosalia kama wanataka kusherehekea ubingwa. “Hakuna mechi nyepesi katika hatua hizi, hata timu inayotaka kushuka daraja inaweza kukufunga, lazima tutilie mkazo mechi zote,”alisema Omog.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon amewapongeza wachezaji wake kwa ushindi wa jana katika mchezo mgumu na akawataka sasa kuhamishia fikra zao katika mchezo ujao dhidi ya Ruvu Shooting Aprili 6, Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Ikitoka Mlandizi, Azam FC itakwenda Mbeya kucheza na Mbeya City Aprili 13 Uwanja wa Sokoine kabla ya kumalizia Ligi Kuu msimu huu kwa kumenyana na JKT Ruvu Aprili 19, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

YANGA YAKANA KUWATIMUA KASEJA, CHUJI NA YONDANIYoung Africans itashuka dimbani siku ya jumapili kucheza na JKT Ruvu katika muendelezo wa michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara mzunguko wa pili raundi ya 23 mchezo utakaofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.


Ligi Kuu ya Vodacom inaelekea ukingoni na sasa kila timu ikijitahid kufanya vizuri ili kuweza kujiweka katika mazingira mazuri aidha ya kubakia Ligi Kuu, kupata Ubingwa au kujinusuru kutoshuka daraja.

Young Africans yenye pointi 46 imebakisha michezo minne ambapo ikiweza kushinda yote itafikisha pointi 58 ambazo zinaweza kupitwa na vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Azam FC peke kama itashinda michezo yake yote miatatu iliyosalia.

Baada ya kupoteza mchezo wake dhidi ya Mgambo JKT mwishoni mwa wiki jijini Tanga, Kikosi cha mhoalanzi Hans Van der Pluijm kimeingia kambini jana jioni katika Hoteli ya Kiromo huku kikiendelea kufanya mazoezi katika Uwanja wa Boko Beach Veterani.

Mlinda mlango Deoragtias Munish "Dida" aliyekua majeruhi kwa takribani wiki mbili kwa sasa ameshapona majeraha aliyokuanayo na ameungana na wenzake kambini tayari kwa maandalizi ya mchezo huo wa siku ya jumapili.

Katika mchezo wa awali wa mzunguko wa kwanza timu hizi zilipokutana, Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 4-0

Aidha taarifa zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya kawamba wachezaji Athuman Idd, Kelvin Yondani na Juma Kaseja wamesimamishwa kutokana na timu kufungwa mchezo dhidi ya Mgambo JKT hazina ukweli, wachezaji hao hawajafukuzwa na wapo wanaendelea na mazoezi pamoja na wenzao.

Tunaomba vyombo vya habari kuwa wanatoa taarifa za ukweli na sio kupotosha jamii na mwisho wa siku kuwapa usumbufu viongozi kufanya kazi ya kukanusha.