KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 13, 2012

AKI, UKWA WANANIHOFIA-IBRO



LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu anayechipukia nchini Nigeria, Ibro Ibrahim Musa amesema amepata taarifa kwamba, wasanii anaofanana nao kwa kimo na umbo, Chinedu Ikedieze 'Aki' na Osita Iheme 'Ukwa' wameanza kumuhofia.
Ibro, ambaye ni mzaliwa wa jimbo la Benue, alisema wiki hii kuwa, kuchomoza kwake katika fani ya uigizaji filamu nchini humo, kumeanza kuwapa hofu Aki na Ukwa na kuwafanya wahisi kwamba anaweza kuwaangusha.
"Wanaamini nataka kuwazidi kwa umaarufu wakati hilo siyo lengo langu. Tasnia hii ni kubwa kiasi kwamba inaweza kuwajumuisha watu wenye vipaji vya kila aina. Nimepokea taarifa nyingi kutoka kwa watu, zote kupitia kwenye magazeti zikieleza jinsi wanavyojenga chuki na mimi,"alisema.
Ibro, ambaye ameshacheza zaidi ya filamu 60 za Kinigeria alisema, hajali maneno yanayosemwa na waigizaji hao wawili nyota na kuongeza kuwa, kinachomfanya aendelee kung'ara katika fani hiyo ni kipaji chake.
"Kipaji chako ndicho kitu muhimu. Uigizaji, mwonekano wako na kauli utakazopata kutoka kwa mashabiki vitakwambia kama unafanya vizuri au la. Hivyo ninachokifanya ni kuwaambia wasijali, haya ni mambo ya kawaida katika fani,"alisema msanii huyo.
"Nawaambia hivi kwa sababu wanao mashabiki wao na mimi ninao wa kwangu. Ninawaona na kuwachukulia kama kaka zangu,"aliongeza msanii huyo.
Ibro, ambaye alianza uigizaji mwaka 2001 alikiri kuwa, mafanikio yake yanaweza kupimwa na wakati fani hiyo ilipoanza kushika kasi nchini Nigeria.
Msanii huyo mchekeshaji alisema, kwake anaamini kuwa, fani ya uigizaji filamu imeyabadili maisha yake.
"Watu ninaotoka nao matembezini na kustarehe nao kwa sasa ni wafanyabiashara maarufu. Baadhi ya wakati huwa najiuliza iwapo nafasi niliyonayo sasa katika maisha yangu ningeweza kuipata bila kuwa mwigizaji,"alisema.
Ibro alisisitiza kuwa, hana bifu wala ushindani wowote na Aki na Ukwa na kuongeza kuwa, wote ni rafiki zake na wapo kwenye fani moja.
"Hakuna ukweli wowote kuhusu uvumi huu. Aki na Ukwa ni rafiki zake na waigizaji wenzangu,"alisema msanii huyo. "Itakuwa ni makosa kwa watu kuvumisha kwamba tupo kwenye ushindani. Wote wawili wanafanya vizuri, kama nilivyo mimi, hivyo hakuna kabisa sababu ya kuwepo kwa ushindani kati yetu,"alisisitiza.
Ibro alisema ipo nafasi ya kutosha kwa kila mmoja wao kung'ara kwenye fani hiyo na kutengeneza pesa bila kumsumbua mwingine. Alisema tasnia hiyo ni kubwa kwa kila mmoja wao na kusisitiza kuwa, binafsi anaifurahia.
Hivi karibuni, Ibro aliteuliwa kuwa balozi wa taasisi moja inayoongozwa na Olivier Cowell, kazi yake kubwa ikiwa ni kuwatahadharisha vijana wasijihusishe na vitendo viovu katika jamii kama vile umalaya na utumiaji wa dawa za kulevya.
Ibro alisema hatarajii iwapo kazi yake hiyo itamwathiri katika fani ya uigizaji filamu. Alisema atakachokifanya ni kucheza filamu nyingi zaidi zitakazotoa mafunzo kwa vijana kujiepusha na mambo hayo.

No comments:

Post a Comment