KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 13, 2012

ARSENAL YAMNYATIA DROGBA

LONDON, England
KOCHA Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger ameamua kusikiliza kilio cha mashabiki wa klabu hiyo wanaotaka kuwepo kwa mabadiliko kwa kusajili wachezaji nyota na wanaotamba katika mchezo huo duniani.
Wenger amesikiliza kilio hicho kwa kutamka wazi kuwa, anamtaka kwa udi na uvumba mshambuliaji nyota wa zamani wa Chelsea, Didie Drogba kutoka klabu ya Shanghai Shenhua ya China.
Arsenal inahaha kusaka mfungaji hodari wa mabao kwa ajili ya kuziba pengo la nahodha wake wa zamani, Robin Van Persie aliyetua Manchester United. Tayari RVP ameshafunga mabao manne katika mechi tatu alizoichezea Manchester United.
Wenger anapima upepo kama anaweza kumpandia dau nahodha huyo wa Ivory Coast, aliyejiunga na Shanghai Shenhua majira ya kiangazi, lakini huenda akakumbana na changamoto ya kumlipa mshahara wa milioni 400 kwa wiki anaoupata kutoka kwa matajiri hao wa China.
Drogba (34) anatajwa kutaka kujiunga na Liverpool katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani baada ya kutokea mzozo wa uongozi ndani ya klabu hiyo tajiri ya Kichina.
Kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho, aliyemsajili mwaka 2004, pia anamtolea jicho nyota huyo mwenye kipaji cha kufunga mabao.
Wakati huo huo, 'Kibibi Kizee' cha Turin, klabu ya Juventus ya Italia imethibitisha kutaka kumng'oa winga wa Arsenal, Theo Walcott.
Kuondoka kwa Walcott huenda kukawa pigo zaidi kwa Arsenal, kufuatia kuondokewa na wachezaji wake nyota wawili katika msimu mmoja.

No comments:

Post a Comment