KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 6, 2013

AFANDE SELE AHUBIRI AMANI, AKEMEA UDINI




MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Selemani Msindi 'Afande Sele' amegeuka muhubiri wa amani nchini baada ya kuibuka na kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la Dini tumeletewa.

Katika kibao chake hicho, Sele anazungumzia umuhimu wa Watanzania kuheshimiana licha ya kila mtu kuwa na dini yake, kabila lake na imani yake.

Akizungumza kwa njia ya simu wiki hii kutoka Morogoro, Sele alisema watanzania wanapaswa kuishi kwa amani na upendo kwa sababu dini ni kitu kilicholetwa na wageni kutoka nje.

Alisema tangu enzi na enzi, upendo, umoja na ushirikiano ndiyo dini ya watanzania hivyo wanapaswa kuiendeleza.

"Kabla ya ukoloni, wazee wetu waliishi kwa upendo, hawakuwa na dini, walisali popote na Mungu aliitikia sala zao. Walimwamini Mungu ndio kama ulimwengu, hakukuwa na kanisa wala msikiti, "alisema Sele.

"Walisali sala zao kwa miungu yao, dua zao silisikika kabla ya mwaka kumalizika, mvua kubwa ilinyesha hata kama sio masika,"aliongeza msanii huyo, ambaye aliwahi kutwaa taji la mfalme wa mashairi.

"Miaka inavyokwenda, dini zinaongezeka, nyingine toka mashariki ya mbali. Yule anajiona sahihi kuliko mwingine. Wenyewe kwa wenyewe tunaitana makafiri, dini zinasababisha ndugu kwa ndugu tunauana, ndugu wa baba na mama tunauana, kisa yule anaitwa Salehe mwingine Willy, Waafrika tunaonekana hatuna amani,"alisema msanii huyo.

Afande Sele alisema siku zote Mungu ni yule yule, isipokuwa majina ya wanaomwabudu ndiyo yanayotofautiana, ambapo kuna wengine wanaomwita Jah, Allah, Maulana, subhana na Jehova.

Alisema iwapo wazungu wasingekuja barani Afrika kutangaza dini zao, waafrika wote wangeitwa wapagani kwa sababu wasingekuwa na dini zaidi ya kuabudu dini zao za asili.

Msanii huyo alijifananisha na Nabii Suleiman na kudai kuwa, ameletwa nchini kwa ajili ya kuhubiri amani hivyo aliwataka watanzania kuwa makini katika kipindi hiki, ambacho zimeanza kujitokeza chokochoko za kidini.

Afande Sele alisema kibao cha Dini tumeletewa ni miongoni mwa vibao sita vitakavyokuwemo kwenye albamu yake mpya, anayotarajia kuitoa hivi karibuni. Alisema albamu hiyo itajulikana kwa jina la wimbo huo.

Afande Sele alisema licha ya mauzo ya albamu kwa wasanii nchini kwa sasa kusuasua, hatajali mauzo ya albamu yake hiyo mpya yatakuwaje.

"Lengo langu ni kuielimisha jamii, sio kupata maslahi. Sitofikiria soko kama litalipa au vipi, ninachohitaji ni kuwapa elimu watanzania,"alisema msanii huyo aliyetengeneza nywele zake kwa mtindo wa rasta.

Msanii huyo amewahi kurekodi vibao vingi, ambavyo vilimpatia sifa na umaarufu kutokana na ujumbe wake kugusa maisha ya kila siku ya jamii.

Baadhi ya vibao hivyo ni Mkuki moyoni, Kama nikipata ukimwi, Ndugu zangu, Mtu na pesa, Darubini kali, Malaria na nafasi ya mtu.

Mapema mwaka jana, Afande Sele alidokeza kuwa anatarajia kugombea mojawapo ya nafasi kubwa za kisiasa katika uchaguzi mkuu wa 2015. Japokuwa hakutaka kuitaja nafasi hiyo, lakini kuna habari kuwa amepanga kuwania ubunge.

No comments:

Post a Comment