'
Monday, March 18, 2013
AZAM YAJIWEKA PAZURI KOMBE LA SHIRIKISHO
AZAM FC imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kucheza raundi ya tatu ya michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho baada ya kuichapa Barrack Young Controllers ya Liberia mabao 2-1.
Katika mechi hiyo ya awali ya raundi ya pili iliyochezwa jana kwenye uwanja wa Antonette Tubman mjini Monrovia, Azam ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0.
Kwa matokeo hayo, Azam sasa inahitaji sare yoyote katika mechi ya marudiano itakayochezwa wiki mbili zijazo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Seif Abdalla Karihe aliibuka shujaa wa Azam baada ya kuifungia bao la pili na la ushindi dakika ya 90. Seif aliingia uwanjani dakika 10 kabla ya kufunga bao hilo, akichukua nafasi ya Kipre Tchetche.
Barrack ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 44 lililofungwa na Junior Barshall.
Bao la kusawazisha la Azam lilifungwa na Humphrey Mieno dakika 10 baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Jabir Azizi na Khamis Mcha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment