KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, March 25, 2013

RAGE BADO MWENYEKITI HALALI SIMBA-TFF



MKUTANO Mkuu wa Dharura ulioitishwa na wanachama wa Simba, Machi 17 mwaka huu na kuuondoa uongozi wa klabu hiyo si halali kwa vile haukufuata taratibu, na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halitambui Kamati za Muda.


Uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana mjini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa.

Kamati imebaini kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 22(2) ya Katiba ya Simba, Mkutano Mkuu wa Dharura unaitishwa na Kamati ya Utendaji baada ya wanachama wasiopungua 500 kuwasilisha ombi hilo kwa maandishi na kujiorodhesha.

Mkutano huo haukuitishwa na Kamati ya Utendaji ya Simba.

Utaratibu huo haukufuatwa ambapo barua ya Mkutano huo iliandikwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo badala ya Kamati ya Utendaji ya Simba ambayo ndiyo matakwa ya Katiba ya Simba.

Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, Kamati ya Utendaji ndiyo inayoitisha Mkutano Mkuu wa Dharura baada ya kuhakiki uhai na uhalali wa wanachama waliojiorodhesha kuomba mkutano huo.

Kamati imesisitiza kuwa Katiba za wanachama wote wa TFF hazina kipengele cha kura ya kutokuwa na imani na uongozi (vote of no confidence), ndiyo maana uko nyuma wanachama wa Yanga, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) walipiga kura hiyo, na TFF kutotambua uamuzi wao.

Hata Katiba ya Simba haitoi mamlaka kwa Mkutano Mkuu wa Dharura kufukuza uongozi uliochaguliwa.

Katiba za wanachama wote wa TFF zimezingatia katiba mfano za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambazo zinasema kiongozi ataingia madarakani kwa uchaguzi, na si kuteuliwa (Kamati ya Muda).

Pia Kamati imesema endapo wanachama wa Simba wangefuata taratibu na uongozi ukakataa kuitisha mkutano, wanachama wangetuma ombi hilo TFF kupitia Kamati ya Sheria ili kutoa mwongozo kwa uongozi wa Simba .

TFF ina mamlaka ya kutoa adhabu kwa viongozi wa wanachama wake wanaokwenda kinyume cha Katiba zao. Pia Kamati imesisitiza kwa wanachama wa TFF kuitisha mikutano yao kwa mujibu wa taratibu na Katiba zao, na wale ambao muda umefika wafanye hivyo haraka.

No comments:

Post a Comment