'
Wednesday, December 5, 2012
UHURU SELEMANI APASUA YA MOYONI
MSHAMBULIAJI Uhuru Selemani aliyejiunga na Azam akitokea Simba, amesema hakuna kitu kilichowahi kumuumiza moyo wake kama kuwekwa benchi msimu mzima.
Akihojiwa katika kipindi cha Amplifaya cha Clouds FM juzi, Uhuru alisema kiongozi mmoja wa Simba, ambaye hakutaka kumtaja jina lake, hakuwa akipenda maendeleo yake.
“Nafikiri huyo mtu alikuwa karibu sana na mwalimu na alikuwa na nafasi ya kuzungumza sana na mwalimu kwa hiyo alikuwa anapanga mimi nisitumike kwenye timu, sijui ni kwa sababu gani na sijawahi kukorofishana naye,” alisema Uhuru.
Mshambuliaji huyo machachari alisema aliwahi kumuuliza Kocha Milovan Cirkovic kuhusu uamuzi wake huo, lakini hakumjibu chochote zaidi ya kumwambia kwamba yeye ni mchezaji bora, anatakiwa kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii.
“Mwalimu alikuwa halioni hilo. Viongozi wa juu wa timu waliliona, lakini walinyamaza. Kama rais wa timu, ananijua nina mchango gani kwenye timu, lakini hakuwahi kuuliza hata siku moja kwa nini Uhuru hachezi,” alisema Uhuru.
Mshambuliaji huyo alisema kukaa benchi kwa muda mrefu kumemuuma na angependa mashabiki wa soka nchini wafahamu ukweli huo kwa sababu hakutarajia kitu kama hicho.
"Sikutegemea kama Simba wanaweza kunifanyia kitu kama hicho kwa sababu nimeifanyia mambo mengi makubwa. Nimeipa taji la ubingwa mara mbili, makombe mbalimbali na ngao za hisani," alisema nyota huyo wa zamani wa Coastal Union ya Tanga.
Uhuru alilitaja tukio lingine, ambalo liliiumiza moyo wake kuwa ni kifo cha kiungo wa zamani wa Simba, Patrick Mafisango, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari mapema mwaka huu maeneo ya Chang'ombe, Dar es Salaam.
Alisema alihuzunishwa sana na kifo hicho kwa vile Mafisango alikuwa rafiki wa kila mtu na alitoa mchango mkubwa katika klabu hiyo katika kipindi kifupi alichoichezea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment