MSANII nyota wa filamu na vichekesho nchini, Steve Mengele amesema kukithiri kwa tabia ya kihuni miongoni mwa wasanii wa filamu wa Tanzania kunasababishwa na wasanii wachache.
Steve, maarufu zaidi kwa jina la Nyerere, amesema wapo baadhi ya wasanii wa kike wa fani hiyo wanaojiheshimu na kuipenda kazi yao, lakini wengine wamekuwa wakiitumia vibaya.
"Nidhamu kila mtu anatoka nayo kwake. Na inategemea malezi aliyopata mtu kutoka katika familia yake,"amesema msanii huyo alipokuwa akizungumzia tabia ya kihuni inayofanywa na baadhi ya wasanii wa kike wa fani hiyo nchini wiki hii mjini Dar es Salaam.
"Zipo familia zingine, mama akiamka asubuhi anamwambia mwanawe toka nenda katafute bwana. Lakini familia zingine mama akimuona mwanaye amerudi shule, atamuuliza huna la kufanya, huna homework," aliongeza msanii huyo.
Steve alisema kinachosababisha fani hiyo igubikwe na vitendo na matukio ya kihuni ni ukweli kwamba, wasanii wametoka katika maeneo tofauti na wamepata makuzi yanayotofautiana.
"Tumekutana kwenye fani hii sote tukiwa watu wazima. Kila mmoja ana maamuzi yake kichwani,"alisema msanii huyo, ambaye kuna wakati aliwahi kujitosa kwenye fani ya siasa.
Hata hivyo, Steve alisisitiza kuwa, wasanii wanaoivuruga fani hiyo ni wachache na ndio wanaowaharibia wenzao wenye sifa na mwenendo mzuri.
Alisema wapo baadhi ya waigizaji wa kike waliojitosa kwenye fani hiyo kwa lengo la kutafuta wanaume baada ya kushindwa kuwapata mitaani.
Steve alisema wasanii wa aina hiyo ni wale wasiokuwa na kipaji cha fani hiyo zaidi ya kuigiza kwa kujilazimisha ili wauze sura.
"Lakini wapo ambao filamu ni maisha yao ya kila siku, wanaiheshimu na kuipenda. Nao wapo wachache sana,"alisema.
Ili kukomesha tabia hiyo, Steve amesema ni vyema Shirikisho la Wasanii wa Filamu Tanzania, liweke kanuni na sheria zitakazowabana wanachama wake kujihusisha na mambo ya kihuni.
Alisema moja ya kanuni hizo ziweke wazi kwamba, msanii atakayebainika akifanya vitendo vya kihuni na kuipaka matope fani ya filamu, afungiwe kwa mwaka kati ya mmoja na mitano.
Pendekezo lingine lililotolewa na msanii huyo na kuwepo kwa sheria itakayowazuia wauzaji wa filamu nchini, kuuza filamu ya msanii atakayejihusisha na vitendo vya kihuni ili liwe funzo kwa wengine.
Alipoulizwa sababu ya kutumia majina ya kiingereza kwenye filamu za kibongo, Steve alisema lengo ni kuwavutia mashabiki wa fani hiyo wasiofahamu lugha ya kiswahili.
Alisema soko la filamu za kitanzania kwa sasa limepanuka na zimekuwa zikiuzwa hadi katika baadhi ya nchi za Ulaya, ambako hawafahamu lugha hiyo.
Kwa sasa, Steve anatamba na filamu yake mpya inayojulikana kwa jina la Get Out, ambaye ameicheza akiwa na wasanii Sinta, Shamsa Ford na Lisa.
Katika filamu hiyo, Steve amecheza kama mlinzi wa getini wa akina dada hao watatu, ambao wanajihusisha na biashara haramu ya kuuza dawa za kulevya na kushiriki katika vitendo vya kihuni.
Licha ya akina dada hao kumdharau Steve, ambaye katika filamu hiyo anatumia jina la Kalulu, wanamtumia kama kipozeo wanapokuwa na hamu za kimapenzi na pia kufahamu mambo mengi juu ya maisha yao.
Steve alianza kutamba kwenye gemu ya filamu baada ya kuibuka na filamu yake ya kwanza inayojulikana kwa jina la My Son. Baadaye aliibuka na filamu ya Mke mwema, Mwalimu Nyerere na Mr. President.
Hivi karibuni, Steve alitoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni tatu kwa watoto wa kituo cha kulea yatima cha Maunga Centre. Pia aliahidi kuwasomesha watoto wawili wa kituo hicho.
No comments:
Post a Comment