KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, December 20, 2012

NUSU FAINALI KOMBE LA UHAI KUPIGWA KARUME




Mechi za nusu fainali ya michuano ya Kombe la Uhai 2012 inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom zitachezwa kesho (Desemba 21 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Nusu fainali ya kwanza ya michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai itazikutanisha timu za Mtibwa Sugar ya Morogoro na Azam na itafanyika kuanzia saa 2 kamili asubuhi.
Simba na Coastal Union zitacheza nusu fainali ya pili kuanzia saa 10 kamili jioni kwenye uwanja huo huo. Mtibwa Sugar imepata tiketi ya nusu fainali baada ya kuichapa African Lyon mabao 3-1 wakati Simba iliilaza Oljoro JKT mabao 2-0.
Nayo Azam iliindoa JKT Ruvu kwenye robo fainali kwa bao 1-0 huku Coastal Union ikipata ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mechi ya mwisho ya robo fainali.
Mechi ya fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Mechi ya mshindi wa tatu itaanza saa 2 kamili asubuhi wakati ya fainali itakuwa saa 10 kamili jioni.

No comments:

Post a Comment