KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, December 27, 2012

SIMBA YAPIGA MARUFUKU MKUTANO ULIOITISHWA NA WANACHAMA DESEMBA 30



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

HERI ya Krismas na Mwaka mpya kwenu nyote.

Uongozi wa klabu ya Simba leo unapenda kutoa taarifa zifuatazo kwenu.

1. Mkutano wa Wanachama uliopangwa kufanyika Desemba 30 mwaka huu.
UONGOZI umepata taarifa kuwa kuna kundi la wanalojiita wanachama wa Simba waliopanga kufanya mkutano wa wanachama siku ya tarehe 30 Desemba mwaka huu (Jumapili hii) kwa lengo la kujadili mambo ya klabu.

Mkutano huo, kwa mujibu wa Katiba ya Simba ni batili. Ubatili huo unatokana na ukweli kwamba wale walioutisha mkutano huo hawana Locus Standi (nguvu au mamlaka) ya kufanya hivyo. Katiba ya Simba iko wazi kuwa mtu anayeitisha mkutano wa wanachama ni MWENYEKITI wa klabu pekee na si vinginevyo.

Mkutano huo wa wanachama haujaitishwa na Mwenyekiti wa klabu na hivyo hauna uhalali wowote wa kisheria.

Uchunguzi uliofanywa na klabu umebaini kwamba zaidi ya nusu ya walioitisha mkutano huo pia si wanachama halali wa Simba. Wengine hawajawahi kulipa ada zao za uanachama katika kipindi cha hadi miaka 10 iliyopita !

Matendo yanayofanywa na kundi hili yanaashiria watu wanaotaka tu kuleta vurugu klabuni. Kundi hili linafanya hivi wakati Rais Jakaya Kikwete ametoka kutoa kauli kuhusiana na namna vurugu zinavyosababisha kushuka kwa michezo hapa nchini.

Kundi hili linaandaa vurugu katika kipindi ambacho uongozi upo katika mikakati kabambe ya kuiboresha timu ikiwamo kuipeleka nje ya nchi kufanya mazoezi, jambo ambalo halijawahi kufanyika katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Linaandaa vurugu katika kipindi ambacho Simba ndiyo bingwa mtetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania na ikiwa imeongoza ligi katika msimu huu kuanzia mechi ya kwanza hadi ya 11 katika mechi 13 za kwanza.

Klabu inaomba wapenzi na wanachama wake kukaa mbali na kundi hili la waleta vurugu. Huu ni wakati ambapo tunatakiwa kuwa pamoja kwa vile klabu inatakiwa kutetea ubingwa wake na pia kuliwakilisha taifa katika michuano ya kimataifa mapema mwakani.

Huu ni wakati wa wanachama, wapenzi na uongozi kuwa kitu kimoja. Uongozi uko tayari kukosolewa wakati wowote ule lakini haukubaliani na waleta vurugu.

Uongozi unapenda kusisitiza lifuatalo, Mkutano wa Desemba 30 ni batili na wale wote wenye mapenzi mema na klabu wanatakiwa kukaa mbali nao na kutojihusisha kwa chochote na wanaopanga vurugu.

2. Safari ya Oman
MWENYEKITI wa Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, amerejea Dar es Salaam akitokea Falme za Kiarabu alikoenda kuandaa ziara ya timu ya Simba kwenda kufanya maandalizi ya Ligi Kuu ya michuano ya kimataifa.

Taarifa kamili kuhusu ziara hiyo atazitoa wakati wowote kuanzia kesho.

3. Mazoezi
WACHEZAJI wa Simba wataendelea na mazoezi kesho Alhamisi Desemba 27 katika Uwanja wa Sigara, Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Timu haikufanya mazoezi katika siku mbili za Desemba 25 na 26 mwaka huu ili kutoa nafasi kwa wachezaji na benchi la ufundi kupumzika na familia zao kwenye sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Simba iko mazoezi kwa takribani wiki tatu nne –wiki mbili za kwanza ikijifua katika gym, wiki iliyopita wakifanya mazoezi ya ufukweni na wiki hii ndiyo wameanza ya uwanjani.

Mpaka sasa hakuna mchezaji yeyote majeruhi na mazoezi yanaendelea vizuri kabisa. Wachezaji waliokuwa na timu ya taifa wataanza mazoezi mara baada ya mapumziko ya sikuu za Krismasi na Boxing Day.

4. Zawadi ya Kombe la Uhai
KUFUATIA kupewa zawadi ya mshindi wa tatu katika mashindano ya Kombe la Uhai yaliyomalizika hivi karibuni, uongozi wa Simba umeamua kuwapa wachezaji wake fedha zote (Sh laki tano) za zawadi kwa mshindi wa nafasi hiyo wagawane.

Hatua hii ya uongozi ina lengo la kuwafanya wachezaji walioshiriki mashindano hayo wajitume zaidi katika mashindano mengine ambayo watahitajika kuitumikia klabu ya Simba.

5. Heri ya Krismas na Mwaka Mpya
UONGOZI wa Simba unawatakia wapenzi na wanachama wake sherehe njema za Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.

Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

No comments:

Post a Comment