KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, December 6, 2012

AZAM 'YAICHINJA' SIMBA



SAKATA la mshambuliaji Mrisho Ngasa limechukua sura mpya baada ya klabu yake ya zamani ya Azam kuvunja mkataba kati yake na Simba.
Azam imefikia uamuzi huo siku moja baada ya kutangaza kumuuza Ngasa kwa klabu ya El-Merreikh ya Sudan kwa kitita cha dola 50,000 za Marekani.
Mbali na kuvunja mkataba wa Simba na Ngasa, uongozi wa Azam umesema upo tayari kurejesha sh. milioni 25, ambazo mabingwa hao wa Tanzania walizitumia kumsajili mchezaji huyo kwa mkopo.
Katika barua yenye kumbukumbu namba Azam/Simba/MHS/1/12 ya Desemba 5 mwaka huu, iliyoandikwa na Makamu Mwenyekiti wa Azam, Shani Christoms kwenda kwa Katibu Mkuu wa Simba, Evod Mtawali, ambayo Uhuru inayo nakala yake, Azam imesema makubaliano kati yao kuhusu usajili wa mchezaji huyo yalikuwa ni mkopo.
Shani ameeleza katika barua hiyo kuwa, mkataba huo ulitiwa saini Agosti Mosi, 2012 kwa makubaliano kwamba, Ngasa aichezee Simba kwa mkopo kwa mwaka mmoja na Simba ilipe sh. milioni 25.
"Mchezaji ameieleza menejimenti ya Azam kwamba, amepata ofa nzuri kutoka El-Merreikh ya Sudan na ametuomba tumruhusu apewe uhamisho wa kwenda Sudan. Menejimenti ya Azam imelikubali ombi lake na kufikia makubaliano na El-Merreikh kuhusu suala hilo," imeeleza sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa kwa Simba.
"Kwa sababu ya maendeleo ya mchezaji na timu ya taifa, tumempa baraka zote. Hivyo tunakufahamisha kwamba, tunavunja mkataba wa mkopo kati yetu na tungependa kufahamu turejeshe sh. milioni 25 mlizolipa kwa mkopo kupitia akaunti ipi," imeeleza barua hiyo.
Uongozi wa Azam pia umeandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikieleza makubaliano waliyofikia na Simba kuhusu usajili wa mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Yanga.
Katika barua hiyo ya Desemba 6, 2012 yenye kumbukumbu namba Azam/TFF/Ngasa/6/12, iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiaha, Azam imesema imeshangazwa na kitendo cha uongozi wa Simba kumsainisha Ngasa mkataba mwingine wakati aliuzwa kwa klabu hiyo kwa mkopo.
"Azam iliiruhusu Simba kumsajili Ngasa kwa makubaliano ya mkopo. Mchezaji alipaswa kuichezea Simba kwa mwaka mmoja. Siku chache baada ya Simba kutia saini mkataba wa mkopo kati yake na Azam, ilikiuka makubaliano kwa kumsainisha mchezaji mkataba mwingine unaozidi ule wa mkopo.
"Mchezaji aliyesajiliwa kwa mkopo haruhusiwi kutia saini mkataba na klabu inayomtumia kwa mkopo kama mkataba wake na klabu inayommiliki upo hai kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita. Simba imekiuka makubaliano ya mkopo kwa kuingia mkataba mwingine na Ngasa," imeeleza sehemu ya barua hiyo.
"Japokuwa tulifahamu kwamba Simba imekiuka makubaliano ya mkataba, hatukutaka kumrejesha mchezaji haraka kwa sababu tulitaka kufanya hivyo wakati wa usajili wa dirisha dogo. Hivyo tunakufahamisha rasmi kwamba tunamrejesha Ngasa klabu ya Azam," imeongeza barua hiyo, ambayo Uhuru inayo nakala yake.
Barua hiyo pia imeifahamisha TFF kwamba, Ngasa anatarajiwa kuuzwa hivi karibuni kwa klabu ya El-Merreikh kutokana na kupewa ofa nzuri, ambayo Azam inaamini kwamba, itakuwa kichochea kizuri kwa mchezaji huyo kupata mafanikio makubwa zaidi kisoka.
Mapema jana, klabu ya Simba ilisema imeandika barua kwa TFF ikilitaka shirikisho hilo lisitoe hati ya uhamisho wa Ngasa kwa klabu ya El-Merreikh hadi suala lake litakapopatiwa ufumbuzi.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kitendo kilichofanywa na Azam kumuuza Ngasa kwa klabu ya El-Merreikh hakikuwa sahihi kwa vile kinakiuka makubaliano kati yao.
Kamwaga alisema Simba ilimsajili mchezaji huyo baada ya kuilipa Azam sh. milioni 25, hivyo klabu hiyo haipaswi kumuuza kabla hajamaliza mkataba wake wa kuichezea klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.
Alipoulizwa kuhusu sakata hilo, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema jana kuwa, bado hawajapata taarifa rasmi kuhusu kuuzwa kwa mchezaji huyo.
Hata hivyo, Angetile alisema iwapo ni kweli mchezaji huyo ameuzwa kwa El-Merreikh, ukweli utajulikana hivi karibuni kwa vile itabidi matajiri hao wa Sudan wamwombee uhamisho wa kimataifa kutoka TFF.
"Mimi nimesikia tu habari hizo kupitia vyombo vya habari, hivyo kwa sasa sina la kueleza zaidi ya kusubiri maombi ya ITC, hapo ndipo itajulikana wazi ni nani mwenye mkataba na mchezaji huyo,"alisema.
Kwa sasa, Ngasa yuko Kampala, Uganda, ambako anaichezea timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, inayoshiriki katika michuano ya Kombe la Chalenji, ambayo jana iliingia katika hatua ya nusu fainali.

No comments:

Post a Comment