KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, December 18, 2012

CANNAVARO, CHOLO, MORRIS WAFUNGIWA MWAKA MMOJA


CHAMA cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kimewafungia kucheza soka kwa mwaka mmoja wachezaji tisa wa timu ya Zanzibar Heroes iliyoshiriki katika michuano ya Kombe la Chalenji, iliyomalizika hivi karibuni mjini Kampala, Uganda.

Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya ZFA kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa chini ya Mwenyekiti wake, Amani Makungu.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa, wachezaji hao tisa wamefungiwa kutokana na kitendo chao cha kukataa kurejesha fedha za zawadi, ambazo timu hiyo ilipewa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa kutwaa nafasi ya tatu.

Zanzibar Heroes ilizawadiwa dola 10,000 za Marekani kutokana na kushika nafasi ya tatu katika michuano huyo, lakini wachezaji, wakiongozwa na nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' na msaidizi wake, Aggrey Morris, waliamua kuzipoka fedha hizo kutoka kwa kiongozi wa msafara wa ZFA na kugawana.

Kutokana na kupata kiwango hicho cha pesa, wachezaji wa Zanzibar Heroes, ambao waliitoa Tanzania Bara kwa njia ya penalti tano tano, waligawana dola 500 kila mmoja.

Mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji ya ZFA aliyehudhuria kikao hicho ameieleza blogu ya liwazozito kuwa, wachezaji wote waliofungiwa nile wale wanaocheza soka katika klabu za ligi kuu ya Tanzania Bara.

Aliwataja wachezaji hao, klabu zao zikiwa kwenye mabano kuwa ni Nadir Haroub 'Cannavaro' (Yanga), Nassoro Masoud 'Cholo' (Simba), Selemani Selembe (Coastal Union), Twaha Mohamed (Mtibwa Sugar), Amir Haji (JKT Oljoro), Khamis Mcha, Mwadini Ally, Aggrey Morris na Samir Haji Nuru (wote Azam).

Mjumbe huyo alisema tayari ZFA imeshaandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuliarifu kuhusu kufungiwa kwa wachezaji hao kucheza soka ndani na nje ya nchi kwa mwaka mmoja.

Aliongeza kuwa, ZFA imeitaka TFF kuhakikisha kuwa, adhabu hizo zinatekelezwa ikiwa ni pamoja na kutoichezea timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambayo inajiandaa kumenyana na Zambia katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayopigwa Desemba 23 mwaka huu mjini Dar es Salaam.

"Tumeiandikia TFF kuiomba itusaidie kuhakikisha kwamba, wachezaji hawa tisa hawaichezei Taifa Stars na pia hawatacheza katika ligi kuu ya Tanzania Bara kwa kipindi chote cha mwaka mmoja. Isipofanya hivyo, itakuwa imetangaza mgogoro kati yake na ZFA,"alisema mjumbe huyo.

Aliongeza kuwa, wachezaji wengine 12 waliokuwemo kwenye kikosi cha Zanzibar Heroes, wamerejesha fedha walizogawana, lakini nao wamepewa adhabu ya kusimamishwa kucheza soka kwa muda usiojulikana.

Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Suleiman Hamad (Black Sella), Abdalla Juma (Kipanga), Aziz Said Ali (KMkM), Mohammed Juma Azan (JKU), Ali Mohammed Seif (Mtende Rangers), Hamad Mshamata (Chuoni), Ali Bakar (Mtende Rangers), Is-haka Mohammed (JKU) na Saad Ali Makame (Zanzibar All Stars).

Wengine ni Makame Gozi (Zimamoto), Issa Othman Ali (Miembeni), Aleyuu Saleh (Black Sella), Jaku Juma Jaku (Mafunzo), Abdallah Othman (Jamhuri), Nassor Juma (JKU) na Faki Mwalim (Chipukizi).

"Hawa wachezaji 12 wamerejesha fedha walizogawana, lakini tumeamua kuwasimamisha kucheza soka ili liwe fundisho kwa sababu walikaidi kurejesha fedha hizo walipokuwa Uganda, badala yake wamezirejesha baada ya kurejea Zanzibar. Huu ni utovu wa nidhamu,"alisema mjumbe huyo.

No comments:

Post a Comment