KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, December 17, 2012

AZAM YALAZIMISHWA SARE NA DRAGONS



Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, (CAF), Azam FC wameanza na sare ya 1-1 dhidi ya Dragons ya hapa katika mchezo wa Kundi B kuwania Kombe la Hisani kwenye Martyrs mjini hapa.

Hadi mapumziko, wenyeji walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na mshambuliaji wao hatari, Nkate Jason dakika ya 24.Nkate alifunga bao hilo baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Azam, ambao walichanganyana na kipa wao, Mwadini Ally.

Pamoja na kufungwa, Azam walicheza vizuri katika dakika 45 za kwanza na zaidi walikosa mipango tu ya kumalizia.Hata hivyo, mashambulizi ya pembeni ya wapinzani wao yalilitia misukosuko ya kutosha lango la Azam katika ngwe hiyo.

Kipindi cha pili Azam walirudi na kikosi kile kile, lakini walibadilika kiuchezaji na iliwachukua dakika nne tu kukomboa bao, kupitia kwa Nahodha mpya, Jabir Aziz aliyeunganisha pasi ya Abdi Kassim ‘Babbi’.

Baada ya bao hilo, Azam waliendelea kushambulia lango la wapinzani wao, lakini safu ya ulinzi ya Dragons ilisimama imara kudhibiti mashmbulizi hayo.

Katika dakika ya 76, kipa Mwadini alipangua kwa uhodari mkubwa mkwaju wa penalti wa Mukinzi Mawesi, baaada ya mchezaji huyo huyo kuangushwa kwenye eneo la hatari na Ibrahim Mwaipopo.

Baada ya hapo Azam walihamia langoni mwa Dragons, ambao safu yao imara ya ulinzi iliwanusuru adhabu hii leo.

Azam ilicheza mechi ya leo bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall na Msaidizi wake, Kali Ongala ambao wamebaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche kutokana na kukosa viza za kuingia DRC.

Azam ambao ni washindi wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na Ligi Kuu, wamepangwa katika Kundi B pamoja na Dragons na Shark FC, ambayo watacheza nayo Desemba 17.

Ikifuzu kwenye kundi lake, Azam itaingia Nusu Fainali moja kwa moja, ambazo zitachezwa Desemba 25 na Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu. Kundi B, lina timu za DC Motema Pembe, Diables Noirs, FC MK na Real De Kinshasa.

Kikosi cha Azam leo kilikuwa; Mwadini Ally, Himidi Mao, Waziri Salum, Luckson Kakolaki, David Mwantika, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Abdi Kassim, Gaudence Mwaikimba, Abdallah Seif/Humphrey Mieno na Uhuru Suleiman/Zahor Pazi.

No comments:

Post a Comment