KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, June 5, 2016

DUNIA YAOMBOLEZA KIFO CHA MUHAMMAD ALI



Mazishi yake kufanyika Ijumaa, nyumbani kwake Lousville
Bintiye Hana asimulia dakika za mwisho za baba yake
Obama, Tyson, Foreman, Mywether waelezea walivyoguswa
Aliagiza mazishi yake yawe wazi kwa watu wa aina zote

WASHINGTON, Marekani

WAKATI dunia ikiomboleza kifo cha bingwa wa zamani wa ndondi za uzani wa juu duniani, Muhammad Ali, imeelezwa kuwa mazishi yake yafanyika Ijumaa wiki hii.

Ali, bondia wa kwanza maarufu mwenye asili ya Kiafrika, alifariki juzi asubuhi akiwa na umri wa miaka 74.

Ali, ambaye alijizolea sifa nyingi kutokana na machachari yake awapo ulingoni, alifariki katika jini la Phoenix Arizona, ambako alilazwa hospitali Alhamisi iliyopita kutokana na matatizo ya kupumua.

Taarifa iliyotolewa na familia yake jana, ilieleza kuwa ibada ya mazishi itafanyika nyumbani kwake Lousville Kentuck.

Msemaji wa familia hiyo, Bob Gunnel alisema mazishi ya Ali yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali maarufu nchini Marekani, akiwemo Rais wa zamani wa nchi hiyo, Bill Clinton.

Gunnel pia alidokeza kuwa Ali hakupata msukosuko wowote wakati anakata roho na kwamba, muda  wote alikuwa amezungukwa na familia yake, ambayo ilikesha ikimsomea Quraan.

Kwa mujibu wa Gunnel, mwanamasumbwi huyo aliagiza watu wa rika zote waruhusiwe kuhudhuria maisha yake kwa sababu yeye alikuwa raia wa dunia.

Meya wa Jiji la Lousville, Greg Fischer alitangaza jana kuwa, mji huo umeandaa siku maalumu ya maombolezo ya kifo cha bondia huyo wa zamani, yatakayofanyika Jumamosi.

Mara baada ya kifo chake, bintiye Hana aliandika kupitia mtandao wa twitter akisema, familia yake ina furaha kwa sababu  baba yao kwa sasa yuko huru.

Hana pia alielezea jinsi baba yake alivyopambana kabla ya mauti kumkumba na kuwashukuru watu wote waliokuwa wakimuunga mkono.

"Nyoyo zetu zimeumia. Lakini tuna furaha kwamba hatimaye baba sasa yuko huru," alieleza Hana kupitia mtandao huo.

"Sote tulijaribu kuwa jasiri na kumnong'oneza masikioni tukimwambia, 'Sasa unaweza kwenda. Tutakuwa salama. Tunakupenda. Asante baba. Sasa unaweza kurejea kwa Mungu," alieleza Hana.

"Sote tulikuwa tumemzunguka, tukiwa tumemkumbatia na kumbusu huku tukiishika mikono yake na kusoma aya za kiislamu. Kwa sekunde 30 moyo wake ulikuwa ukipiga kwa kasi," alieleza Hana kupitia ujumbe huo.

Hana, ambaye ni mtunzi wa kitabu cha 'The Soul of a Butterfly and More Than a Hero Life Lessons from Ali', kinachoelezea maisha ya baba yake, pia aliweka picha mbalimbali za baba yake kwenye mtandao wa Instagram.

"Tuiombee roho yake ipumzike mahali pema na kumuombea safari ya furaha huko aendako. Mungu akubariki baba. Wewe ni kipenzi cha moyo wangu," alieleza Hana kupitia mtandao huo.

Ali alizaliwa Januari 17, 1942 na kupewa jina Cassius Marcellus Clay, kabla ya kuamua kubadili dini kutoka mkristo kuwa mwislamu.

Alianza kucheza ndondi akiwa na umri wa miaka 12 na baadaye akaishia kushinda dhahabu katika uzani wa light-heavyweight katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika mjini Roma mwaka 1960.

ASEMAVYO TYSON

Bingwa wa zamani wa ndondi hizo, Mike Tyson, amemuenzi Ali kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia anwani yake ya Tweeter akisema, "Mungu alikuja kumchukua bingwa wake''.

OBAMA ANENA
Rais wa Marekani, Barrack Obama amewaongoza viongozi mbalimbali katika kumuenzi Muhammad Ali kwa kusema enzi za uhai wake, Ali aliushangaza ulimwengu kutokana na staili yake ya upiganaji.

Obama pia amesema ulimwengu umekuwa bora kwa sababu ya Ali. Rais huyo wa Marekani pia amesema yeye na mkewe, Michelle wanaomba bingwa huyo wa zamani akalale mahali pema peponi.

MAYWEATHER
Bondia Floyd Mayweather Jr naye ameandika kupitia akaunti yake ya tweeter akisema: "Leo moyo wangu unanung'unika kwa kumpoteza mwanzilishi, bondia hodari, bingwa na shujaa kwa vyovyote vile. Hakuna siku niliingia katika ulingo wa ndondi bila kukukumbuka. Ucheshi, uzuri wako na vinginevyo ni vitu tutakavyovienzi."

FOREMAN
George Foreman, ambaye aliwahi kupambana na Ali katika pambano la karne lililofanyika mwaka 1974, amesema:
"Muhammed Ali alikuwa na ushawishi wa kukufanya akupende. Iwapo usingempenda, angekufanyia vituko ili umchukie."

KENT
Aliyekuwa bondia wa kimataifa nchini Kenya, Muhammad Abdallah Kent, anasema ameshangazwa na kifo cha Muhammad Ali na hakuweza kujizuia machozi yake wakati dadake alipompingia simu na kumueleza kuhusu kifo hicho.

Kent aliiwakilisha Kenya katika ndondi za kulipwa kuanzia
mwaka 1973 hadi 1986. awali akiwa anapigana katika uzani wa kati na baadaye uzani wa juu.

Alipigana na Ali katika pambano la raundi nne mwaka 1980, mjini Nairobi wakati Ali alipozuru Afrika kwa lengo la kuyashawishi baadhi ya mataifa kujiondoa katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Moscow, ikiwa ni siku chache baada ya Urusi
kuvamia  Afghanistan.

ALIVYOJIUNGA NA NGUMI
Muhammad Ali ajiunga na mchezo wa ngumi kwa bahati wakati akiwa na umri wa miaka 12. Ofisa wa polisi, Joe Martin ndiye aliyemshawishi ajiunge na mchezo huo kwa ahadi ya kumsaidia kumtafuta mwizi aliyemwibia baiskeli yake. Alipofikisha umri wa miaka 18, akafanikiwa kushinda medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Rome, Italia.

Muhammad Ali alikuwa mtu wa kujigamba kupita kiasi, lakini alikuwa na kila sababu ya kufanya hivyo. Alikuwa na kipaji cha pekee kwenye ndondi. Alikuwa na kasi na nguvu. Alianza kujulikana aliposhinda medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya Roma mwaka 1960.

Alianza kucheza ngumi za kulipwa mwaka 196 na kushinda mapambano 18 mfululizo kabla ya kusafiri kwenda London, mwaka 1963, ambako alishinda pambano lake la kwanza ugenini dhidi ya Henry Cooper wa Uingereza. Alimshinda Cooper kwa knockout ya raundi ya tano.

Katika pambano hilo la kihistoria, Cooper alimbwaga Ali raundi ya nne, lakini Mmarekani huyo alitimiza ubashiri wake kwa kumshinda raundi ya tano mbele ya watazamaji 55,000, waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Wembley.

Ushindi wa Ali dhidi ya Tony Liston ulikuwa na bado ni moja ya matokeo ya kushangaza zaidi katika historia ya ndondi. Baada ya pambano hilo, Ali alijisifu kwa kusema: "Mimi ndiye bingwa zaidi! Mimi ndiye bora zaidi! Mimi ni mfalme wa dunia!".

Ali alishinda Liston kwa kumpiga kwa knock-out, dakika ya kwanza ya raundi ya kwanza. Hadi leo, watu wengi duniani wanaamini Liston aliuza pambano hilo, lakini Ali alikuwa akisisitiza kwamba, alishinda kwa njia safi.

Ali alirejea London kupigana na Henry Cooper kwa mara ya pili Mei, 1966 kwenye Uwanja wa zamani wa klabu ya Arsenal wa Highbury.  Mashabiki wake wa Uingereza, ambao hawakuwa wamemtambua mara ya kwanza, walimshabikia sana kiasi cha kumpa mapokezi mazito.

Angelo Dundee ndiye aliyekuwa msaidizi wa Ali kila alipopanda ulingoni. Alikuwa akimsaidia Ali tangu alipoanza kucheza ndondi.

"Kuna Cassius Clay mmoja," alikuwa akipenda kusema Dundee. "Namshukuru Mungu."

Bondia wa kwanza kumshinda Ali alikuwa Joe Feazier, lakini aliweza kulipa kisasi kwa kushinda pambano la marudiano.

Hata hivyo, pambano pekee lililosifika ni lile dhidi ya George Foreman, lililofanyika mwaka 1974 nchini Zaire, lililojulikana kama  'Rumble in the Jungle", ikiwa na maana "Mngurumo Msituni". Ali alikaa raundi nane za kwanza akiwa amejibanza kwenye kamba, mbinu aliyoiita 'rope-a-dope'.

Marehemu Ali aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa Parkinson (ugonjwa wa kutetemeka) mwaka 1984, lakini alikabiliana na hali hiyo kwa ujasiri na staha. Mwaka 1996, alitazamwa na mabilioni ya watu akiwasha mwenye wa Olimpiki mjini Atlanta.

No comments:

Post a Comment