KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 29, 2015

COASTAL UNION YAMREJESHA MESSI WA SIMBA

Meneja wa timu ya Coastal Union, Akida Machai (kushoto) akimkabidhi jezi ya klabu hiyo
winga mpya wa kulia, Ibrahim Twaha 'Messi' mara baada ya kutua saini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia timu hiyo.

TIMU ya Coastal Union ya Tanga imeendelea kufanya usajili wa nguvu ili  kujiimarisha vilivyo katika safu mbalimbali ambapo jana ilifanikiwa kuingia mkataba wa kuitumikia timu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili aliyekuwa winga wa kulia wa Simba,Ibrahim Twaha “Messi”

Utiaji saini wa mkataba huo ulifanyika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mjini hapa na kushuhudiwa na viongozi waandamizi akiwemo Katibu Mkuu Kassim El Siagi na Meneja wa timu hiyo,Akida Machai.

Akiuzngumza mara baada ya kumalizika utiaji saini huo,Katibu Mkuu wa Coastal Union,Kassim El Siagi alisema kuwa wameamua kumsajili mchezaji huyo kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao hasa anapokuwa uwanjani .

Alisema kuwa winga huyo ana vitu adimu ambavyo akishirikiana na wachezaji wengine ambao wamesajiliwa katika timu hiyo itakuwa chachu ya kuipa maendeleo timu hiyo katika msimu mpya wa Ligi kuu Tanzania bara msimu ujao.

“Niseme tu safari hii tumedhamiria kuleta mabadiliko makubwa kwenye michuano ya Ligi kuu soka Tanzania bara na hili tunalifanya kuhakikisha tunarudisha kombe mkoani hapa ambalo tulilichukua mwaka 1988 “Alisema El Siagi.

Kwa upande wake,Ibrahim Twaha “Messi”mara baada ya kusaini mkataba huo alihaidi kuipa mafanikio timu hiyo kwa kushirikiana na wachezaji wengine katika safari za kuwania Ubingwa wa Ligi kuu msimu ujao.

“Sasa ni kama nimerudi nyumbani kwa sababu awali nilikuwa naitumikia timu hii hivyo najisikia faraja kubwa kurudi tena Coastal Union mi nihaidi kushirikiana nao kwa lengo la kuipa mafanikio “Alisema Messi.

Awali, Meneja wa Coastal Union,Akida Machai alisema kuwa msimu huu timu hiyo imedhamiri kufanya usajili nzuri ambao utaiwezesha kutwaa ubingwa na kurudisha makali yao ya miaka ya nyuma.

Sunday, July 26, 2015

YANGA HIYOOO ROBO FAINALI KOMBE LA KAGAME



WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya soka ya Kombe la Kagame, Yanga jana walifuzu kucheza robo fainali baada ya kuichapa Khartoum ya Sudan bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao pekee na la ushindi la Yanga katika mchezo huo lilifungwa na mshambuliaji Amis Tambwe dakika ya 19 baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Haruna Niyonzima.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa itakutana na ndugu zao wa Azam katika mechi ya kwanza ya robo fainali itakayochezwa Jumatano kwenye uwanja huo wakati Gor Mahia ya Kenya itapambana na KCCA ya Uganda kesho.

Gor Mahia ilitinga hatua hiyo baada ya kushinda mechi yake ya mwisho ya kundi A jana kwa kuichapa Telecom ya Djibouti mabao 3-0.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall, amesema kikosi chake kina kila sababu ya kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame.

Azam imetinga robo fainali ya michuano hiyo baada ya kuongoza kundi B ikiwa na pointi tisa, ikifuatiwa na KCCA ya Uganda yenye pointi saba.

Akizungumza baada ya Azam kuicharaza Adama City ya Ethiopia mabao 5-0, Hall alisema kikosi chake kimefanya vema katika mechi zote za hatua ya makundi kutokana na maandalizi mazuri.

"Hatuna sababu ya kukosa ubingwa wa Kombe la Kagame mwaka huu,"alisema kocha huyo raia wa Uingereza.

YANGA, KAHRTOUM KAZI IPO LEO KOMBE LA KAGAME

Hatua ya makundi ya michuano ya Vilabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup 2015) inatarajiwa kukamilika leo kwa michezo miwili kupigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku macho na masikio ya wapenzi wa soka yakiwa katika mchezo kati ya Yanga SC dhidi ya Kahrtoum ya Sudan.

 Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 10 kamili jioni, ambapo Yanga SC watashuka dimbani kusaka ushindi wake wa tatu mfululizo katika michuano hiyo, hali kadhalika timu ya Khartoum ikihitaji ushindi wake wa tatu katika mechi hiyo inayosuburiwa kwa hamu kubwa.

 Kuelekea katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa wa vuta ni kuvute kufuatia timu ya Yanga SC kuhitaji ushindi katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuongoza kundi lake, huku pia Khartoum wakihitaji ushindi katika mchezo huo ili kuweza kuongoza kundi A.

 Utamu wa mchezo huo unaletwa na makocha wa timu hizo mbili, Hans Van der Pluijm wa Yanga na James Kwesi Appiah wa Khartoum ambao wote wamewahi kufanya kazi nchini Ghana kwa vipindi tofauti.

 Hans ambaye ametwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanznaia msimu huu, anasifika kwa kucheza soka safi la kasi na kushambulia muda wote, huku akiwa na mafanikiko nchini Ghana baada ya kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na timu ya Berekum Chelsea miaka miwili iliyopita.

 Kwa upande wa James Appiah alikuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Ghana, ambapo alikua kocha wa kwanza mwafrika kuipeleka timu ya Afrika katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Brazil mwaka 2014.

 Licha ya kufuzu kwa fainali za kombe la Dunia, Appiah pia aliwahi kuichezea timu ya Taifa ya Ghana kwa miaka 7 akiwa nahodha, pia aliiwezesha timu ya Vijana ya Ghana chini ya miaka 23 kufuzu kwa fainali za Michezo ya Afrika na kutwaa Ubingwa huo mwaka 2011.

 Katika kikosi chake cha Khartoum kinachoshiriki michuano ya Kagame, Appiah amejumuisha wachezaji wa kimataifa kutoka nchini Cameroon na Ghana, na malengo yake ni kutwaa Ubingwa wa Kagame Cup kwa mara ya kwanza.

Mpaka sasa Khartoum inaongoza kundi A ikiwa na pointi 7 sawa na Gor Mahia lakini Wasudani hao wakiwa juu kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa, huku Yanga wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi sita.

 Kabla ya mchezo huo kati ya Yanga SC dhidi ya Khartoum kutakua na mchezo wa kwanza utakaoanza majira ya saa 8 kamili mchana kati ya Gor Mahia ya Kenya dhidi ya  Telecom ya Djibout.

 Mpaka sasa timu zilizofuzu hatua ya robo fainali ni Khartoum, Gor Mahia na Yanga kutoka kundi A, huku APR na Al Shandy zikitoka kundi B, na Azam FC ikiwa timu ya kwanza kufuzu kutoka kundi C, na timu mbili kati ya Adama City, KCCA na Malakia zitaingia hatua ya robo ya fainali.

 Hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la Kagame itachezwa Jumanne, Julai 28 na Jumatano Julai 29 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Thursday, July 23, 2015

LIGI KUU BARA KUANZA SEPTEMBA 12



Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) itaanza Sept 12 badala ya Agosti 22 ili kumpa Charles Mkwasa fursa ya kuendelea na program yake kuelekea mechi ya Taifa Stars vs Nigeria itakayochezwa Sept 5.

Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) itakayozikutanisha Azam FC dhidi ya Yanga SC sasa itachezwa Agosti 22 badala ya Agosti 15.

Ratiba ya Ligi Kuu iliyokuwa imeandaliwa, sasa inafanyiwa marekebisho kwa ajili ya tarehe mpya ya kuanza, ambapo pamoja na mambo mengine mechi sasa zitachezwa wikiendi na katikati ya wiki na wikiendi ya Oct 25 hakutakuwa na mechi kupisha Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge.

Klabu za Ligi Kuu zimeandikiwa barua kujulishwa tarehe mpya ya kuanza ligi, na dirisha la usajili linabaki kama lilivyo.

Wamiliki wa viwanja vyenye upungufu wmeandikiwa barua kutakiwa kurekebisha upungufu katika muda maalumu, vinginevyo havitaruhusiwa kutumika kwa ajili ya PL na FDL.

Timu ya Madini ya Arusha imeruhusiwa kutumia Uwanja wa Nyerere uliopo Mbulu mkoani Manyara kwa mechi za SDL kwa masharti upungufu uliopo kwenye uwanja huo urekebishwe kwanza.

YANGA YAICHAPA TELECOM 3 -0


Mabingwa mara tano wa michuano ya Kombe la Kagame timu ya Young Africans (Yanga SC) leo imeibuka na ushindi wa mabao 3- 0 dhidi ya timu ya Telecom kutoka nchini Djibout, katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Mabao ya Yanga yalifungwa na mshambuliaji Malimi Busungu aliyefunga mabao mawili, na Geofrey Mwashiuya  aliyefunga bao la tatu kwa kombora kali umbali wa mita 20 na kupeleka kilio kwa timu ya Telecom.

Katika mchezo wa leo Yanga walipoteza penati mbili zilizopigwa na washambuliaji wake Amissi Tambwe na Saimon Msuva zilizookolewa na mlinda mlango wa Telecom Nzokira Jeef.

Baada ya ushindi huo wa leo kocha mkuu wa Yanga, mholanzi Hans Van der Pluijm amesema vijana wake leo wamecheza vizuri na ndio manaa wameweza kuibuka na ushindi huo wa mabao 3- 0.

Aidha kocha huyo amesema kwa sasa wanajiandaa na mchezo wa siku ya ijumaa dhidi ya KMKM utakochezwa saa 10 kamili ijumaa, ukitanguliwa na mchezo kati ya Gor Mahia dhidi ya Khartoum utakoanza saa 8 kamili mchana.

Katika mchezo wa uliotangulia mapema saa 8 mchana, timu Khartoum ilibuka na ushindi wa mabao 2- 1 dhidi ya KMKM, huku katika uwanja wa Karume KCCA ya Uganda ikiibuka na ushindi wa bao 1-1 dhidi ya Adama City ya Ethiopia.

 KAGAME KUENDELEA LEO
Michuano ya Kombe la Kagame inayoendelea kutimua vumbi jijini Dar es salaam itaendelea leo siku ya Alhamisi katika uwanja wa Taifa, ambapo Mabingwa mara tatu wa michuano hiyo timu ya APR SC watacheza dhidi ya LLB ya Burundi, mechi itakayoanza majira ya saa 10 kamili jioni.

Mchezo wa kwanza utazikutanisha timu ya Heegan FC ya Somalia itakayocheza dhidi ya Al Shandy ya Sudan.

Wednesday, July 22, 2015

TANZANITE KUWAFUATA YOUNG SHE-POLOPOLO LEO


Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania wenye umri chini ya miaka 20 (Tanzanite) imeondoka nchini leo asubuhi kwa ndege ya Rwanda Air kwenda Zambia kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Young She-Polopolo.

Tanzanite inayowania kufuzu kwa Fainali za Kombe Dunia mwaka 2016 nchini Papua New Guinea, itacheza mchezo huo wa marudano siku ya Jumamosi, Julai 25, jijini Lusaka.

Katika mchezo wa awali uliofanyika takribani wiki mbili zilizopita, Tanzanite ilipoteza mchezo wake nyumbani baada ya kufungwa kwa mabao 4 – 0, hivyo kuhitaji kushinda zaidi ya mabao 5 – 0 ili kuweza kusonga katika hatua inayofuata.

Msafara wa Tanzanite utaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Blassy Kiondo, utajumuisha makocha Rogasian Kaijage (kocha mkuu), Edna Lema (kocha msaidizi), Peter Manyika (kocha wa makipa), Christina Luambano (Daktari), Mwanahamis Abdallah (mtunza vifaa) na Meneja Furaha Francis.

Wachezaji watakaosafiri ni Stumai Abdallah, Shelder Boniface, Donisia Minja, Najiat Abbas, Neema Kiniga, Happyness Mwaipaja, Jane Lucas, Anastazia Katunzi, Anna Mwaisura, Janet Pangamwene, Gelwa Rugomba, Blandina Ambros, Amina Ramadhan, Asha Shaban, Maimuna Hamis, Zuwena Hamis, Amisa Athuman na Wema Richard.

COASTAL UNION YASAJILI WAPYA 13


KLABU ya Coastal Union imeweza kusajili wachezaji 13 ambao wataitumikia timu hiyo katika michuano ya Ligi kuu msimu ujao Tanzania bara unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba mwaka huu hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,Ofisa Habari wa Coastal Union,Oscar Assenga amesema kuwa wachezaji ambao wamesajiliwa wametoka timu mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi.

Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Abasalim Chidebele ambaye ni mshambuliaji kutoka timu ya Stand United, Kiungo Mkabaji Adeyum Salehe kutoka JKU ya Zanzibar,Kiungo Mshambuliaji Nasoro Kapama kutoka Ndanda FC ya Mtwara,Beki wa kati Ernest Mwalupani kutoka Ndanda FC ya Mtwara.

Wengine ni Beki wa Kushoto ,Yassin Mustapa Salim kutoka Stand United,Kiungo Sultan Juma kutoka klabu ya African Sports,Mshambuliaji Ahmde Shiboli kutoka Klabu ya African Sports,Mohamed Hamis Mititi ambaye ni mchezaji huru.

Assenga amewataja wachezaji wengine kuwa ni Benedict Haule ambaye alisajiliwa akiwa kama mchezaji huru ambaye ni mlinda mlango,Mshambuliaji Ismail  Mohamed Suma kutoka Stand United, winga wa kushoto ambaye ni mchezaji huyo Patrick Protas Kamuhagile.

Amesema wachezaji wengine ni Jackson Sabweto ambaye ni Mlinda Mlango kutoka Klabu ya VILLA FC ya nchini Uganda amesaini mkataba wa miaka miwili,Yossouph Sabo kutoka Klabu ya Younde FC ya Cameroon ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja.

Wachezaji wa zamani waliobaki kutimukia klabu hiyo kuwa ni Bakari Mbwana “Kibacha”,Abdallah Mfuko,Hamadi Juma,Ibrahim Chuma,Ike Bright Obina,Abdulhalim Humud,Godfrey Wambura,Ayoub Semtawa na Sued Tumba.

Wakati huo huo wachezaji uongozi wa Coastal Union umewapandisha wachezaji watano kutoka timu ya vijana ya Coastal Union kutokana na uwezo wao kuwa mzuri na wa kuridhisha.

Waliopandishwa ni Mohamed Shekuwe,Sabri Sabri,Tumaini Bakari,Fikirini Suleiman na Mtenje Albano


MBEYA CITY YATANGAZA ZABUNI YA KUUZA VIFAA VYAKE VYA MICHEZO


TANGAZO LA ZABUNI LA UAGIZAJI NA UUZAJI WA VIFAA VYA CLUB.

Mbeya City Council F.C inakaribisha kampuni zenye uwezo wa kufanya kazi na
club yetu.

Kazi zinazotangazwa ni kama ifutazo:
I.      Kuwa mwagizaji wa vifaa mbalimbali vya club
II.     Kuuza vifaa mbalimbali vya club
Zabuni hii inafuati utekelezaji wa club kutaka kukuza mapato yake ili
iweze kujijenga msingi imala ya mapato na hivyo kuiwezesha kuendesha
shughuli zake mbalimbali.

Mwombaji anatakiwa atimize masharti yafuatayo.
1. Awe na Leseni hai ya biashara husika
2. Awe amesajiliwa kama mlipa kodi
3. Maelezo ya kampuni yaani Company profile ikieleza aina ya kampuni au
biashara unayoifanya na eneo ilipo.

4. Waombaji wawe ni makampuni yaliyosajiliwa kisheria na waambatanishe
vivuli vya nyaraka zinazoonyesha uhalali wa uwepo wa mwombaji. Pia
muombaji aonyeshe anwani ya ofisi yake (physical address).

5.Bahasha zenye zabuni zifungwe na lakiri zikionyesha jina na namba ya
zabuni inayoombwa zikielekezwa kwa anuni ya Katibu Mkuu Mbeya City Council
F.C, S.L.P 149, Mbeya na ziwasilishwe ofisi ya Timu iliyopo Ukumbi wa
Mkapa.
         Kwa maelezo wasiliana na;
         Katibu Mkuu
         Mbeya City  Council F.C
         S.L.P 149,Mbeya.
          Simu  N0: 0718732626

6.Mwisho wa kupokea maombi ni tarehe 03.08.2015 saa 4.00 asubuhi.

Katibu Mkuuu
Mbeya City Council F.C

Wednesday, July 15, 2015

CECAFA KUENDESHA MTIHANI WA UTIMAMU WA MWILI KESHO

Baraza la Vyama Vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kesho Alhamis tarehe 16 Julai, 2015 litaendesha mtihani wa utimamu wa mwili (Pysical test) kwa waamuzi wa watakochezesha michuano ya kombe la Kagame inayoanza mwishoni mwa wiki huu.

Zoezi hilo la utimamu kwa waamuzi watakochezesha mashindano ya Kagame, litafanyika kuanzia saa 2 asubuhi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam litasimamiwa na kamati ya waamuzi yay a CECAFA.

Waamuzi wanaotarajiwa kuhudhuria zoezi hilo ni Ali Ahmed, Suleiman Bashir (Somalia), Ahmed Djama (Djibout), Yetayew Belachew (Ethiopia), Kakunze Herve (Burundi), Davis Omweno, Peter Sabata (Kenya), Issa Kagabo, Hakizimana Louis (Rwanda), Ahemd El Faith (Sudan), Lee Okelo na Mashood Ssali (Uganda), Israel Mjuni na Ferdinand Chacha (Tanzania).

AL SHANDY, MALAKIA, KMKM KUWASILI KESHO
Timu ya Al Shandy kutoka nchini Sudan, Al Malakia kutoka Sudan Kusini na KMKM kutoka Visiwani Zanzibar zinatarajiwa kuwasili kesho jijini Dar es salaam tayari kwa ushiriki wao kwenye michuano ya kombe la Kagame.

Al Shandy wanatarajiwa kuwasili kesho Alhamisi saa 3 kamili asubuhi kwa usafiri wa shirika la Ndega la Kenya (KQ), KMKM wakitarajiwa kuwasili majiraa ya saa 5 kamili asubuhi kwa boti ya Kilimanjaro, na Al Malakia wakitarajiwa kuwasili saa 10 jioni kwa ndege ya Rwanda Air.

Viwanja vya mazoezi vitakavyotumika kwa timu zinazoshiriki michuano ha Kagame ni Chuo cha Ualimu (Duce), TCC – Chang’ombe, Sekondari ya Loyola, Bora Kijitonyama, Polisi Kurasini, Chamazi, Uwanja wa Uhuru.

Timu 11 zitafikia katika hoteli za Durban (Mnazi Mmoja), Chichi (Kinondoni) Ndekha, Grand Villa, Travertine (Magomeni), wakati wenyeji Azam na Yanga watakua na kambi zao kwa ajili ya mashindano hayo.

Wasifu wa Al Khartoum:
Al Khartoum ni kati ya wawakilishi wawili wa Sudan kwenye kombe la Kagame. Al Khartoum ni kiboko ya vigogo  katika Ligi ya Sudan kutokana na kutoa upinzani mkali katika ligi ya nchi hiyo inayozijumuisha timu za Al Hilal, El Merreikh na Al Shandy.

Wachezaji wa kuangaliwa:
Mshambuliaji Ismail Baba ambaye ni mchezaji wa zamani wa Coton Sports ya nchini kwao, Kameruni anategemewa kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hii kutoka jiji la Khartoum.

Kiungo mshambuliaji, Dominic Aboy, raia wa Sudani Kusini anategemewa kuonesha ufundi katikati ya dimba. Salah Al Amini ni mchezaji mwingine wa kutupiwa jicho.

Benchi la ufundi:
Katika kujaribu kufurukuta kutoka kwenye ubabe wa timu mbili maarufu za Sudan, Al Merriekh na Al Hilal, wawakilishi hawa wa Sudani walivuka mipaka na kumuajiri kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Ghana, Kwesi Appiah.

Huu utakuwa mtihani wa pili mkubwa kwa kocha Kwesi Appiah baada ya kushindwa kufurukuta kwenye mashindano ya kombe la Shirikisho mbele ya Power Dynamos ya Zambia.

Kundi ililopo:
Al Khartoum iko kwenye kundi A la michuano ya kombe la Kagame kwa mwaka huu ikijumuishwa pamoja na Yanga, Gor Mahia ya Kenya, KMKM ya Zanzibar na Telecom ya Djibout.

Bila shaka ni kundi gumu kwenye michuano ya mwaka huu.

Rekodi kombe la Kagame:
Al Khartoum ni wageni wa mashindano haya. Rekodi ya kubwa nje ya Sudan, ni kufanikiwa kufika kwenye hatua ya kumi na sita bora ya mashindano ya Kombe la shirikisho la CAF mnamo mwaka 2011.

Wasifu wa KMKM
Klabu ya KMKM  itawaiwakilisha Tanzania kwa upande wa Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Jumamosi kwenye viwanja vya Taifa na ule wa Karume.

Historia ya KMKM kwenye Kombe la Kagame:
Imeshiriki mara kadhaa bila kushinda taji hili. Ushiriki wao  haukuwa mzuri kwenye michuano ya mwaka jana iliyofanyika jijini Kigali, Rwanda.

Hata hivyo, KMKM wameonesha nia ya kufanya vizuri mwaka huu kwa kufanya maandalizi mapema.

Tayari wamecheza mechi tatu mfululizo za kirafiki kama sehemu ya maandalizi yao ya kujaribu kufungua ukurasa mpya wa kufanya vyema kwenye mashindano ya Kagame.

Benchi la Ufundi:
KMKM iko chini ya kocha mzoefu Ali Bushiri.

Wachezaji wa kuangaliwa:
Kiungo mshambuliaji, Juma Bwawa, mshambuliaji Matheo Anthony na Hamisi Ally ni miongoni mwa wachezaji wanaopewa nafasi ya kuisadia klabu hii. Wengine ni pamoja na mlinzi Khamisi Ally, na Musa Saidi.

TFF YAUNDA KAMATI YA USHAURI YA LIGI

Rais wa Shirikiso la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Jamal Malinzi ameteua Kamati ya ushauri ya Ligi Kuu (VPL) na ligi Daraja la Kwanza (FDL) nchini.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Alhaj Ahmed Mgoyi na katibu wa Kamati ni mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi nchini (TPLB) na wajumbe wengine saba.

1. Alhaji Ahmed Idd Mgoyi (Mwenyekiti)
2. Boniface Wambura (Katibu)
3. Kennedy Mwaisabula- Mjumbe
4. Idd Mshangama- Mjumbe
5. Amiri Mhando- Mjumbe
6. Grace Hoka- Mjumbe
7. Ibrahim Kaude (Vodacom)- Mjumbe
8. Baruan Muhuza (Azam Media)- Mjumbe
9. Peter Simon- Mjumbe

Kazi za kamati hiyo zitakuw
a ni:
(i) Kufuatilia mwenendo wa Ligi
(ii) Kuishauri Bodi/TFF namna ya kuboresha Ligi
(iii) Masoko
(iv)  Leseni za Vilabu (Club Licensing)
(v)  Mipango ya Maendeleo ya Vilabu
(vi) Viwanja vya mazoezi
(vii) Utoaji wa tuzo za ligi mbalimbali
(viii) Kutengeneza vigezo (criteria) vya washindi wa tuzo

MAGUFULI MGENI RASMI UFUNGUZI WA KAGAME

Waziri wa Miundombinu nchini Tanzania, John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa michuano ya Kombe la Kagame siku ya Jumamosi, Julai 18 2015 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Magufuli baada ya kufungua rasmi michuano hiyo, atashuhudia mchezo wa ufunguzi rasmi wa mashindano ya Kagame, mechi itakayowakutanisha miamba ya Afrika Mashariki timu ya Yanga dhidi ya Gor Mahia kutoka nchini Kenya.

Michuano ya Kagame inatarajiwa kuanza kutimua vumbi siku ya jumamosi kwa michezo mitatu, ukindoa mecho ya Yanga Vs Gor Mahia, mechi zingine zitakua ni kati ya APR dhidi ya Al Shandy uwanja wa Taifa saa 8 mchana, KMKM Vs Telecom saa 10 jioni uwanja wa Karume.

Kuanzia leo tutakua tunawaleta kwa ufupi timu zinazoshiriki michuano hiyo mwaka huu, na kwa kuanza tunaanza na kundi A;

Mchezo wa ufunguzi  kati ya Yanga dhidi ya Gor Mahia unaonekana kuteka hisia za wapenzi wa soka kwa ukanda wa Afrika Mashariki, kwani ni takribani miaka 19 timu hizo mbili haziwaji kukutana katika ardhi ya Tanzania.

Mara ya mwisho mwaka 1996 katika michuano ya Cecafa, timu hizo zilikuwa katika kundi moja, katika mchezo wa awali zilitoka sare ya bao 1- 1, wakati zilipokutana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, Gor Mahia iliibuka na ushindi wa mabao 4 -0.

Gumzo la wadau wa soka nchini kwa sasa ni kuhusu uwezo wa klabu za Tanzania, Yanga, Azam na KMKM kuweza kuhakikisha kombe la michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki haliondoki kwenye ardhi ya

Tanzania.
Kwa upande wa Yanga, matumaini ya kulibakiza kombe kwenye ardhi ya Tanzania yatachagizwa na historia yao nzuri ya miaka ya hivi karibuni pindi Kombe la Kagame linapoandaliwa nchini. Yanga iliibuka kidedea mara mbili mfululizo mwaka 2011 na 2012 mashindano hayo yalipoandaliwa nchini.

Yanga mabingwa mara tano wa michuano hio watakuwa na kazi moja tu ya kujaribu kuifikia rekodi ya Simba, inayoongoza kutwaa Kombe hilo mara nyingi, ikiwa imeweza kufanya hivyo, mara sita.

Kocha: Hans van Pluijm ( Uholanzi)
Yanga iko chini ya mtaalam kutoka Uholanzi, Hans van Pluijm anayesifika kwa kuwa mfuasi asiyetetereka  wa soka la kushambulia.

Nyota wa kutazamwa:
Yanga ina wachezaji kadhaa inaowategemea ili kufanya vizuri. Macho na masikio yataelekezwa kwa Donald Ngoma,  mshambuliaji aliyesainiwa kutoka Platinum Fc ya Zimbabwe kuona kama ataendeleza kasi yake ya ufungaji aliyoanza nayo.

Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Nadir Haroub na Amissi Tambwe ni kati ya wachezaji ambao wanatarajiwa kuendelea kuwa nguzo za Yanga kwenye michuano hii.

Rekodi kwenye Kombe la Klabu Bingwa:
Yanga imebahatika kutwaa ubingwa mara tano; (Mwaka 1975, 1993, 1999, 2011, na 2012).

Pia Yanga imemaliza kama washindi wa pili mara mbili, mwaka 1976 ilipofungwa na Gor Mahia 2-1 jijini Kampala na mwaka 1992 ilipolala kwa mikwaju ya penati mbele ya watani wao wa jadi, Simba.

Kuanzishwa:
Yanga ilianzishwa mwaka 1935, na kuwa moja ya klabu kongwe kabisa kwenye ukanda huu na bara la Afrika kwa ujumla.

Gor Mahia: Wababe wa Kenya waliojipanga upya kurudisha heshima.

Gor Mahia hawakufanya vizuri katika michuano ya mwaka jana, ila wanatarajiwa kutoa ushindani katika mashindano ya mwaka huu.

Licha ya kupotea kwa muda mrefu kabla ya kuibuka na kushindwa kufurukuta kwenye michauno ya mwaka jana jijini Kigali, Gor Mahia wanajipa moyo Zaidi kutokana na mwenendo wao kwenye Ligi ya

Kenya. 
Mabingwa hao wa Kenya hawajapoteza mechi msimu huu huku wakionesha dalili za kutangaza ubingwa mapema kabisa.

Kundi lake:
Gor Mahia iko kwenye kundi A la michuano ya mwaka huu ikijumuishwa na Yanga, Al Khartoum ya

Sudan, KMKM ya Zanzibar na Telecom ya Djibout. Ni kundi ambalo ni gumzo kuu likdaiwa  kuwa na mechi zenye msisimko Zaidi na ushindani mkubwa.

Wachezaji wa kuangaliwa:
Kwa wafuatiliaji wa soka nchini Kenya, hakuna anayepinga kuwa kwa sasa timu yenye wachezaji bora zaidi ni Gor Mahia.

Wachezaji kama Khalid Aucho, chipukizi Micheal Olunga anayetajwa kuwa mrithi wa mshambuliaji bora kuwahi kutokea nchini Kenya, Dennis Oliech, na Meddie Kagere wamekuwa ni kiungo muhimu kwenye timu hii.

Wachezaji wengine ni pamoja na mlinda mlango Boniface Oluoch zake kutikiswa kwenye ligi ya Kenya inayoendelea kwa sasa.

Mlinzi wa Uganda Cranes, Godfrey Walusimbi na George Odhiambo wakiongeza chachu kwenye timu hiyo.

Benchi la Ufundi:
Gor Mahia inaongozwa na kocha Frank Nuttal, raia wa Uskochi. Benchi lao la ufundi linajumuisha pia mlinda mlango wa zamani wa kimataifa wa Harambe Stars, Mathew Ottamax ambaye ana jukumu la kuwanoa walinda mlango, Boniface Oluoch na Jerim Onyango.

 Rekodi Kombe la Kagame:
Mara ya mwisho Gor Mahia ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1985, lakini imetwaa ubingwa huo mara 5 (1976, 1977, 1980, 1981, 1985).

Wakati huo huo kuelekea kuanza kwa michuano ya Kagame siku ya jumamosi, waamuzi wa michezo hiyo wanatarajiwa kuwasili kesho siku ya jumatano sambamba na kamati ya ufundi kwa ajili ya mitihani ya utimamu wa mwili (Physical Test) siku ya alhamis, na kamati ya ufundi watakua wakikagua viwanja na kuweka vipimo kabla ya ufunguzi rasmi wa michuano hiyo siku ya Jumamosi.

MICHUANO YA KAGAME KUANZA JUMAMOSI



Michuano ya Kombe la Vilabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Kagame Cup) inatarajiwa kuanza kutimua vumbi siku ya Jumamosi tarehe 18 Julai 2015 jijini Dar es salaam, kwa kushirikisha timu 13 kutoka nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na kati.

Mashindano ya CECAFA Kagame Cup ni mashindano makongwe barani Afrika ambayo yalianza mwaka 1967 kwa kushirikisha timu za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, na mwaka huu ni mashindano ya 40 tangu kuanza kwa michuano hiyo

Klabu ya Simba ndio timu inayoongzoa kwa kutwaa ubingwa huo mara sita (6) ikifuatiwa na Yanga, Gor Mahia zilizotwa mara (5), APR ya Rwanda ikiwa imetwaa ubingwa huo mara tatu (3). Yanga na Gor Mahia zina nafasi ya kufikia Simba SC endapo zitafanikiwa kutwaa Ubingwa msimu huu.

Mechi ya ufunguzi ufunguzi siku ya jumamosi uwanja wa Taifa itawaktanisha APR ya Rwanda dhidi ya Al Shandy ya Sudan saa 8 kamili mchana, KMKM kutoka Visiwani Zanzibar watacheza dhidi ya Telecom ya Djibout  uwanja wa Karume saa 10 jioni, huku wenyeji timu ya Yanga wakiwakaribisha Gor Mahia kutoka Kenya saa 10 jioni.

Kuelekea kwenye mashindano hayo, waandaji wa michuano hiyo CECAFA kwa kushirikiana na wenyeji Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya michezo hiyo, ambapo Uwanja wa Karume kiingilio kitakua shilingi elfu mbili (2,000) na uwanja wa Taifa kiingilio cha chini kitakua ni shilingi elfu tano (5,000) na kiingilio cha juu ni elfu 20,000 (20,000).

Timu zinazoshiriki michuano hiyo

Kundi A: Yanga (Tanzania Bara), Gor Mahia (Kenya), Telecom (Djibout), KMKM (Zanzibar), Khartoum-N (Sudan).

Kundi B: APR (Rwanda), Al-Shandy (Sudan),LLB AFC (Burundi), Heegan  FC (Somalia).

Kundi C: Azam FC (Tanzania), Malakia (Sudan Kusini), Adama City (Ethiopia) na KCCA (Uganda).

Michuano hiyo ya CECAFA Kagame Cup itaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha luninga cha Supersport.


UCHAGUZI TWFA
Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Soka cha Wanawake chini (TWFA) inatangaza kuwa wafuatao wamepita katika mchujo wa awali katika nafasi walizoomba kama ifuatavyo:

1.   Amina Ali Karuma  - Mwenyekiti
2.   Devotha John Marwa – Mwenyekiti
3.   Cecilia Makafu – Katibu Msaidizi
4.   Somoe Roberst Ng’itu – Katibu Msaidizi
5.   Debora Ernest Mkemwa – Mjumbe Kamati ya Utendaji
6.   Mwanaheri Kalolo – Mjumbe Kamati ya Utendaji
7.   Theresia Reginald – Mjumbe Kaamti ya Utendaji

Hivyo mtu yeyote mwenye pingamizi anaombwa aliwasilishe katika ofisi za TFF – Karume kuanzia tarehe 15/07/2015  mpaka 20/07/2015.

Friday, July 10, 2015

KUZIONA TANZANITE, YOUNG SHE-POLOPOLO 2000



Timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake cwenye umri chini ya miaka 20 (Tanzanite) kesho siku ya jumamosi itashuka dimbani uwanja wa Azam Complex kucheza na timu ya Taifa ya Zambia chini ya miaka 20 (Young She-Polopolo).

 Viingilio vya mchezo wa kesho kati ya Tanzanite dhidi ya Young She-Polopolo ni shilingi elfu mbili (2,000/=) kwa jukwaa la mzunguko, na shilingi  elfu tatu (3,000/=) kwa Jukwaa Kuu.

 Mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Wanawake za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Papua New Guinea, utachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Sudan,unatarajiwa kuanza saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki na kati.

 Timu ya Young She-Polopolo tayari imeshwasili nchini jana jioni, na leo wakitarajiwa kufanya mazoezi mepesi leo jioni katika uwanja wa Azam Complex kw ajaili ya mchezo huo. Waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Sudan tayari wameshawasili.

Wakati huo huo Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetoa usafiri wa mabus mawili kwa ajili ya kikundi cha ushangiliaji cha timu za Taifa (Taifa Supporters) kitachokwenda kesho Chamazi kuipa sapoti timu ya Tanzanite.

 Mabasi hayo mawili yataondoka ofisi za TFF zilizopo Karume saa 6 kamili mchana kuelekea Chamazi kwa ajili ya kuishangilia timu ya Taifa ya wanawake  chini ya miaka 20 (Tanzanite).



TWIGA STARS YAPANGWA NA WENYEJI



Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) leo limetoa ratiba ya fainali ya michezo ya Afrika (All African Games), ambapo Timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars) imepangwa kundi A pamoja na wenyeji Congo-Brazaville.

Katika droo iliyochezwa leo makao makuu ya CAF - Cairo na kupanga makundi ya fainali hizo za michezo ya Afrika, Tanzania imepangwa kundi A pamoja na wenyeji Congo - Brazaville, Nigeria na Ivory Coast, huku Kundi B likiwa na timu za Cameroon, Afrika Kusini, Ghana na Misri.

Kundi B lenye timu ya Twiga Stars linaonekana kuwa ndio kundi gumu zaidi kutokana na kuwa timu ya Nigeria, mabingwa mara mbili wa michuano hiyo, wenyeji Congo -Brazzavile washiriki mara mbili wa fainali hizo na timu ya Ivory Coast.

Twiga Stars ilifanikiwa kukata tiketi ya kucheza fainali hizo baada ya kuiondoa timu ya Taifa ya Zambia ya wanawake (She-Polopolo) kwa jumla ya mabao 6-5.

Fainali hizo za michezo ya Afrika zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi nchini Congo - Brazzaville Septemba 3 - 18 mwaka huu.

Tuesday, July 7, 2015

KOZI YA MAKOCHA WA MAGOLIKIPA JULAI 13


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF litaendesha kozi ya makocha wa magolikipa nchini itakayofanyika Julai 13 - 17, 2015 jijini Dar es salaam

Jumla ya makocha wa magolikipa 29 wanatarajiwa kuhudhuria kozi hiyo itakayofanyika katika ofisi za TFF zilizopo Karume.

Orodha ya Makocha watakaohudhuria kozi hiyo na timu wanazotokea kwenye mabano ni

Rafael Mpangala (Mgambo JKT), Adam Abdallah Moshi (Simba SC ), Khalid Adam Munnisson (Mwadui FC), Choke Abeid (Toto African), Mussa Mbaya (Ndanda FC), Idd Abubakar Mwinchumu (Azam FC), Herry Boimanda Mensady (Tanzania Prisons), Kalama Ben Lwanga (Stand United), Patrick Mwangata (Mtibwa Sugar), Juma Pondamali (Young Africans).

Wengine ni Abdi Said Mgude (Coastal Union), Razack Siwwa (African Sports Tanga), Josia Steven Kasasi (Mbeya City), Ramadhani Juma (Kagera Sugar Kagera),Abdallah Said Ngachimwa (JKT Ruvu), John Bosco (Majimaji FC Ruvuma), Fatuma Omary (Twiga Stars), Juma Kaseja Juma (Premier League), Athuman Mfaume Samata (Ilala), Peter Manyika John (Taifa Stars).

Hussein Tade Katadula (African Lyon), Juma Mohamed Bomba (Kinondoni), Mwameja Mohamed Mwameja (Ilala),  Agustino Malindi Mwanga (Kigoma), Mohamed Abbas Silima (Police SC. Zanzibar), Bakari Ali Kilambo (Kizimbani SC Zanzibar), Hafidh Muhidin Mcha (Zanzibar Heroes), Elyutery Deodatusy Mholery (Kinondoni), Salim Waziri (Tanga)



MKWASA AWASHUKURU WATANZANIA


Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Charles Boniface Mkwasa amewashukuru watanzania wote waliowapa sapoti katika mchezo wa marudiano dhidi ya Uganda uliochezwa mwishoni mwa wiki jijini Kampala.

Mkwasa amesema kujitolea kwa wachezaji wa Taifa Stars (uzalendo) katika mchezo huo kulipelekea kuwapa wakati mgumu wenyeji, huku watanzania waliojitokeza kuja kushuhudia mchezo huo wakiwashangilia muda wote wa mchezo.

“Kiukweli japo timu haikuweza kupata matokezo mazuri sana, lakini tunamshukuru mungu ndani ya wiki moja ya maandalizi, tumeweza kuwapa maelekezo vijana na kuyafanyia kazi, japo wengine walikua wakicheza kwa mara ya kwanza timu ya Taifa walicheza vizuri, kijumla wote kwa pamoja walifanya vizuri sana katika mchezo dhidi ya Uganda” alisema Mkwasa.

Aidha Mkwasa amesema kwa sasa wataomba kupata nafasi ya japo siku 10 kufanya mazoezi kwa pamoja kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) dhidi ya Nigeria Septemba 5 mwaka huu, na kuwaomba watanzania wote kuwaunga mkono katika maandilizi hayo.

MWESIGWA AFUNGUA SEMINA YA AIRTEL
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Mwesigwa Selestine leo amefungua semina ya makatibu wakuu wa vyama vya soka vya mikoa nchini  (FA's) kuhusu maandalizi ya michuano ya airtel.

Katika ufunguzi wa semina hiyo, Mwesigwa amewaomba viongozi hao kuzingatia kanuuni na mahitaji katika michuano ya Airtel inayoshirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17 ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi hivi karibuni.

Mwesigwa amesema viongozi hao wakichagua vijana wenye umri sahihi wa kushiriki kwenye michuano hiyo itatoa fursa kwa makocha kuchagua wachezaji wenye umri halisi kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa nchi yetu.

Aidha Mwesigwa ameipongeza kampuni ya simu za mkonono ya Airtel kwa kuendesha michuano hiyo kila mwaka, ambapo kwa sasa vijana watatu wapo katika kituo cha mpira miguu kilichopo Dakar - Senegal wanaposoma masomo ya kawaida na kufundishwa mpira wa miguu, huku wakitafutiwa timu za kucheza nje ya Afrika na  kufanya majaribio sehemu mbalimbali Ulaya.

CECEFA KAGAME CUP MEDIA ACCREDITATION
Maombi ya vitambulisho vya waandishi wa habari kwa ajili ya michuano ya CECAFA Kagame Cup 2015 yamefunguliwa rasmi kuanzia leo tarehe 7 Julai, 2015 katika tovuti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF.

Kila Kampuni ya Habari (Media House) inaombwa kuomba vitambulisho vitano (5) vya waandishi wa habari watakaofanya kazi wakati wa michuano ya kombe la Kagame Cup kwenye tovuti ya TFF (tff.or.tz) kisha kuchagua KAGAME CUP, ACCREDITATION na kujaza fomu ya maombi ya kitambulisho na kuambatanisha na picha ya muombaji.

Mwisho wa kuomba kitambulisho kwa waandishi wa habari ni jumatano tarehe 15 Julai, 2015 saa 6 kamili  usiku.

Waombaji wa vitambulisho hivyo wote wanaombwa kufanya maombi hayo mapema ili kuondokana na usumbufu wakati michuano ya Kagame itakapokua imeanza.



DR. TWAHA MWENYEKITI MPYA COASTAL UNION


Uchaguzi uliofanyika jana tarehe 5/7/2015 matokeo yalikuwa kama ifuatavyo:

1.MWENYEKITI:
 Jumla ya wapiga kura 207.
Kura zilizopigwa  205.
Kura zilizo haribika  2.

Ahmed Ally Twaha -192
Steven Mnguto  11.

2.MAKAMU MWENYEKITI:
Jumla ya wapiga kura 207.
Kura zilizopigwa 203.
kura zilizoharibika- 4

Salim Amir-
Kura za NDIYO-193
Kura za HAPANA- 9.

3.WAJUMBE KAMATI YA UTENDAJI.
Waliochaguliwa na kura zao:

1.Hassan Omary Bwana-190.
2.Hassan Ramadhan Muhsin-190.
3.Abdallah ZubeiryAlly-188.
4.Hussein Ally Mwinyi Hamis-185
5.Aggrey Ally Mbapu-179.
6.Mohamed Rajabu-179.
7.Omary Hassan Mwambashi -144.
8.Waziri Mohamed-31.
Kwa kuwa walikuwa wanatakiwa wajumbe saba tu kwa hiyo wajumbe walioshinda ni kuanzia  moja mpaka saba.

Kwa kawaida uchaguzi ulifanyika kwa utulivu ukiacha vurugu za hapa na palele wakati wa kuingia ukumbini.

Kesho siku ya jumatano saa 5 kamili asubuhi kocha mkuu wa timu wa Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Charles Mkwasa ataongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume.

Waandishi wote wa habari mnaombwa kuhudhuria bila kukosa.

Friday, July 3, 2015

CECAFA YATANGAZA RATIBA YA KOMBE LA KAGAME 2015


Rais wa Baraza la Vyama vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, Leodgar Tenga leo ametangaza kuanza kwa michuano ya kombe la Kagame itakayoanza kutimua vumbi Julai 18, 2015 na kumalizika Agosti 2 mwaka huu jijii Dar es salaam.

Akiongea na waandishi wa habari leo katika ofisi za TFF zilizopo Karume, Tenga ameishukuru serikali ya Tanzania na TFF kwa kukubali kuwa wenyeji wa michuano hiyo mikubwa, vyombo vya habari na wapenzi wa mpira wa miguu nchini kwa sapoti yao na kuipokea kwa mikono miwili michuano hiyo.

Lengo la CECAFA ni kuona vilabu vya ukanda huu vinapata nafasi ya kucheza michezo mingi na kujiandaa kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Naye Rais wa TFF, Jamal Malinzi amewashukuru CECFA kwa kuipa Tanzania uenyeji huo na kuahidi TFF itahakikisha michuano hiyo inafanya nchini katika hali ya amani na usalama toka mwanzo mpaka mwisho wa michuano hiyo.

Timu zilizothibtisha kushiriki michuano hiyo ni Yanga, Azam (Tanzania), APR (Rwanda), Gor Mahia (Kenya), Telecom (Djibout), KMKM (Zanzibar), Khartoum-N (Sudan), Al Shandy (Sudan) LLB AFC (Burundi), Heegan FC (Somalia), Malakia (Sudani Kusini), Adama City (Ethipia) na KCCA (Uganda).

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholaus Musonye ametangaza ratiba ya michuano ya Kombe la Kagame itakayoanza kutimua vumbi Julai 18, 2015 jijini Dar es salaam ikishirikisha timu 13 kutoka nchi wanachama wa CECAFA.

Mechi ya ufunguzi tarehe 18 Julai, 2015 Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam itashuhudia wenyeji Yanga SC wakicheza na Gor Mahia ya Kenya, huku APR ya Rwanda ikicheza na Al Shandy ya Sudan na KMKM ya Zanzibar wakifungua dimba na Telecom ya Somalia.

Ratiba ya michuano hiyo imeziweka timu hizo katika makundi matatu ambapo kundi A lina timu za: Yanga (Tanzania), Gor Mahia (Kenya), Telecom (Djbiout), KMKM (Zanzibar) na Khartoum-N (Sudan)

Kundi B: APR (Rwanda), Al Shandy (Sudan), LLB AFC (Burundi) na Heegan FC (Somalia), Kundi C: Azam FC (Tanzania), Malakia (Sudan Kusini), Adama City (Ethiopia) na KCCA (Uganda)

Timu tatu zitakazoshika nafasi ya juu kutoka kundi A, timu mbili za juu kutoka kundi B & C, na mshindi mwenye wastani mzuri kutoka kundi B & C zitaingia katika hatua ya robo fainali.

BENDERA AIPONGEZA TFF
Mkuu wa mkoa wa Manyara Dokta, Joel Bendera ameipongezs TFF kwa kuandaa mashindano ya ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 13 (U-13),  na maandalizi ya timu hiyo kwa ajili ya kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika za vijana chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwaka 2019 nchini Tanzania.

 Bendera amesema hiyo ndiyo njia sahihi ya kuelekea kwenye mafanikio pia amepongeza juhudi za Chama cha Soka mkoa wa Manyara na TFF kwa kuandaa kozi za makocha na waamuzi, akisema huo ndiyo uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya soka mkoani Manyara.

Aidha aliwaasa makocha kutumia mbinu za kisasa za ufundishaji soka walizozipata kwenda kuendeleza vipaji vya wachezaji watakaowafundisha.

Pia Bendera amewahakikishia wakazi wa Manyara atahakikisha wanaandaa vipaji vitakvyowawezesha kuwa na timu bora itakayowakilisha mkoa wa Manyara.

ACCREDITATION FOR ALL AFRICAN GAMES:
Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) limetangza kufunguliwa kwa maombi ya vitambulilsho kwa wandishi wa habari kwenye fainali za michezo ya Afrika zitakazofanyika mwezi Septemba mwaka huu nchini Congo- Brazaville.

Waandishi wa habari wanaotajiwa kwenda kufanya kazi kwenye michuano hiyo wanaombwa kufanya maombi ya vitambulisho (Accrediatation) kuanzia Juni 29 mpaka Julai 7 mwaka huu.

STARS YAWAFUATA THE CRANES

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager inaondoka nchini leo jioni kuelekea Kampala - Uganda kwa ajili ya mchezo wake wa marudiano dhidi ya The Cranes siku ya jumamosi.

Kikosi cha Taifa Stars kinaondoka kikiwa na wachezaji 20, bechi la ufundi 7, pamoja na viongozi kwa shirika la ndege la Rwanda (Rwada Airi) ambapo wanatarajiwa kuwasili uwanja wa Entebe majira ya saa 3 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Mchezo wa jumamosi ni wa marudiano kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazofanyika nchini Rwanda, huku mechi hiyo ikichezwa saa 10 jioni katika uwanja wa Nakivubo.

Kocha mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema vijana wake wamefanya mazoezi vizuri katika kipindi chote cha maandalizi, na sasa wako tayari kwa mchezo huo, mipango ikiwa ni kupata ushindi siku ya jumamosi.

Aidha Mkwasa amesema watawakosa wachezaji wawili, Abdi Banda na Mohamed Hussein (Tshabalala) waliopata majeruhi jana wakati wa mazoezi yaliyofanyika uwanja wa Boko Vatereani, na kusema nafasi zao zitazibwa na wachezaji waliopo kambini.

Wachezaji wanaosafiri ni: Ally Mustafa, Mudathir Khamis, Juma Abdul, Shomari Kapombe, Haji Mngwali, Michael Aidani, Hassan Isihaka, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Frank Domayo, Mudathir Yahya, Salum Telela, Said Ndemla, Saimon Msuva, Deus Kaseke, Ramadhan Singano, Atupele Green, Rashid Mandawa, John Bocco na Ame Ally.

TFF YATUMA SALAM ZA RAMBI RAMBI KWA MWAKELEBELA, MWAMBUSI
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Mwesigwa Selestine ametuma salamu za rambi rambi kwa famili aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela kufuatia kufiwa na baba yake mzazi jana mjini Irinnga na mazishi yakitarajiwa kufanyika kesho mjini Iringa.

Aidha TFF imetuma salam za rambi rambi kwa kocha mkuu wa timu ya Mbeya City, Juma Mwambusi kufutia kufiwa na mama yake mzazi mjini Mbeya.

TFF pia imetuma salam za rambi rambi kwa familia ya mtangazi maarufu wa wa michezo nchini Ezekiel Malongo  aliyefariki dunia jana.

Katika salam zake kwa familia ya Mwakalebela, Mwambusi na Malongo, Mwesigwa amesema wanawapa sana pole wafiwa kwa kuondokewa na wapendwa wao na kusema kwa niaba ya TFF, familia ya mpira na watanzania wote wapo nao pamoja katika kipindi hichi cha maombolezo.

Wednesday, July 1, 2015

YANGA KUNDI MOJA NA GOR MAHIA KOMBE LA KAGAME



MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga SC wamepangwa Kundi A pamoja na Gor Mahia ya Kenya, Khartoum FC ya Sudan, Telecom ya Somalia na KMKM ya Zanzibar katika michuano ya 41 ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
Katika mkutano na waandishi wa habari leo makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, amesema mabingwa wa mwaka jana, Azam FC wamepangwa kundi C pamoja na Malakia ya Sudan Kusini, KCC ya Uganda na Adama City ya Ethiopia.
Mkutano huo uliohudhuriwa na Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga, Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ulishuhudia APR ya Rwanda ikipangwa kundi B pamoja na timu za Al Shandy ya Sudan, Lydia Ludic Burundi  ya Burundi na Elman ya Somalia.
Michuano hiyo inatarajiwa kufanyika mjini Dar es Salaam, Tanzania, kuanzia Jumamosi ya Julai 18 hadi Jumapili ya Agosti 2, mwaka huu.
Mabingwa watetezi, El Merreikh ya Sudan wamejitoa ili wapate fursa ya kushiriki vyema hatua ya makundi ya Ligi Mabingwa Afrika.

MAKUNDI KOMBE LA KAGAME 2015:
KUNDI A: Yanga (Tanzania), Gor Mahia (Kenya), Khartoum (Sudan), Telecom (Somalia), KMKM (Zanzibar)
KUNDI B: APR (Rwanda), Al Shandy (Sudan), LLB (Burundi), Elman (Somalia)
KUNDI C: Azam (Tanzania), Malakia (South Sudan), KCC (Uganda), Adama City (Ethiopia)