'
Tuesday, July 7, 2015
MKWASA AWASHUKURU WATANZANIA
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Charles Boniface Mkwasa amewashukuru watanzania wote waliowapa sapoti katika mchezo wa marudiano dhidi ya Uganda uliochezwa mwishoni mwa wiki jijini Kampala.
Mkwasa amesema kujitolea kwa wachezaji wa Taifa Stars (uzalendo) katika mchezo huo kulipelekea kuwapa wakati mgumu wenyeji, huku watanzania waliojitokeza kuja kushuhudia mchezo huo wakiwashangilia muda wote wa mchezo.
“Kiukweli japo timu haikuweza kupata matokezo mazuri sana, lakini tunamshukuru mungu ndani ya wiki moja ya maandalizi, tumeweza kuwapa maelekezo vijana na kuyafanyia kazi, japo wengine walikua wakicheza kwa mara ya kwanza timu ya Taifa walicheza vizuri, kijumla wote kwa pamoja walifanya vizuri sana katika mchezo dhidi ya Uganda” alisema Mkwasa.
Aidha Mkwasa amesema kwa sasa wataomba kupata nafasi ya japo siku 10 kufanya mazoezi kwa pamoja kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) dhidi ya Nigeria Septemba 5 mwaka huu, na kuwaomba watanzania wote kuwaunga mkono katika maandilizi hayo.
MWESIGWA AFUNGUA SEMINA YA AIRTEL
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Mwesigwa Selestine leo amefungua semina ya makatibu wakuu wa vyama vya soka vya mikoa nchini (FA's) kuhusu maandalizi ya michuano ya airtel.
Katika ufunguzi wa semina hiyo, Mwesigwa amewaomba viongozi hao kuzingatia kanuuni na mahitaji katika michuano ya Airtel inayoshirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17 ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi hivi karibuni.
Mwesigwa amesema viongozi hao wakichagua vijana wenye umri sahihi wa kushiriki kwenye michuano hiyo itatoa fursa kwa makocha kuchagua wachezaji wenye umri halisi kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa nchi yetu.
Aidha Mwesigwa ameipongeza kampuni ya simu za mkonono ya Airtel kwa kuendesha michuano hiyo kila mwaka, ambapo kwa sasa vijana watatu wapo katika kituo cha mpira miguu kilichopo Dakar - Senegal wanaposoma masomo ya kawaida na kufundishwa mpira wa miguu, huku wakitafutiwa timu za kucheza nje ya Afrika na kufanya majaribio sehemu mbalimbali Ulaya.
CECEFA KAGAME CUP MEDIA ACCREDITATION
Maombi ya vitambulisho vya waandishi wa habari kwa ajili ya michuano ya CECAFA Kagame Cup 2015 yamefunguliwa rasmi kuanzia leo tarehe 7 Julai, 2015 katika tovuti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF.
Kila Kampuni ya Habari (Media House) inaombwa kuomba vitambulisho vitano (5) vya waandishi wa habari watakaofanya kazi wakati wa michuano ya kombe la Kagame Cup kwenye tovuti ya TFF (tff.or.tz) kisha kuchagua KAGAME CUP, ACCREDITATION na kujaza fomu ya maombi ya kitambulisho na kuambatanisha na picha ya muombaji.
Mwisho wa kuomba kitambulisho kwa waandishi wa habari ni jumatano tarehe 15 Julai, 2015 saa 6 kamili usiku.
Waombaji wa vitambulisho hivyo wote wanaombwa kufanya maombi hayo mapema ili kuondokana na usumbufu wakati michuano ya Kagame itakapokua imeanza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment