KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, December 31, 2015

SERIKALI YAMFAGILIA MBWANA SAMATTA

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye(kushoto) akiongea na Mchezaji wa Timu ya TP Mazembe Mbwana Samatta(kulia)  jijini Dar es salaam.Mbwana  amemtembelea waziri Nape ofisini kwake na kuomba baraka za wizara katika kinyanganyiro cha kugombea uchezaji bora wa Afrika anayechezea ligi za ndani  na pia kumpa habari njema za yeye kutegemea kujiunga na timu ya Ubelgiji ya Genk.

Wednesday, December 30, 2015

AZAM YAREJEA KILELENI LIGI KUU


Goli pekee la team captain John Bocco JB ‘Adebayor’ limeipa Azam FC nafasi ya kuongoza ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara kwa kuiondoa Yanga kwenye nafasi hiyo baada ya kufikisha jumla ya pointi 35 wakiwa wamecheza mechi 13 sawa na Yanga yenye pointi 33 baada ya kucheza mechi 13 pia.

Azam wamekwea kileleni mwa VPL baada ya kuifunga Mtibwa Sugar kwa goli 1-0 kwenye mchezo wao wa kipolo uliopgwa leo kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.Mchezo wa leo ulikuwa mgumu kwa upande wa Azam kutokana na kubanwa na Mtibwa Sugar kila sehemu kwa dakika zote za mchezo huo. Mtibwa walimiliki mchezo kwa dakika zote lakini walishindwa kupachika mabao kutokana na nafasi ambazo walitengeneza.

Wakati kila mtu akiamini mchezo huo utamalizika kwa sare ya bila kufungana (0-0), ndipo nahodha huyo na mkongwe wa Azam FC akaifungia goli timu yake na kuipaisha hadi kileleni mwa msimamo wa ligi. Bocco alifunga goli hilo kwa mpira wa adhabu ndogo baada ya yeye mwenyewe kuchezewa ndivyo sivyo nje kidogo ya eneo la hatari.

Bocco alipiga shuti kali ambalo lilijaa wavuni moja kwa moja na kumwacha golikipa wa Mtibwa Sugar Said Mohamed akiwa hana la kufanya.


Winga wa Azam FC Farid Musa akijaribu kumtoka mchezaji wa Azam FC Winga wa Azam FC Farid Musa akijaribu kumtoka mchezaji wa Azam FC

Matokeo hayo ya ushindi kwa Azam ni habari mbaya kwa Yanga kutokana na kushushwa kwenye nafasi ya kwanza hadi ya pili hasa katika kipindi hiki ambacho ligi ya Vodacom Tanzania bara itasimama kwa muda tena kupisha mashindano ya Mapinduzi Cup yanayotarajia kuanza January 3, 2016 visiwani Zanzibar ambapo timu tatu kutoka Tanzania bara zitashiriki mashindano hayo.

CHANZO CHA HABARI. BLOGU YA SHAFFIE DAUDA

MALINZI ATUMA SALAMU ZA MWAKA MPYA KWA WADAU WA SOKA


Ndugu zangu, Kwa niaba ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania kupitia kwenu wanahabari ninaomba nitoe salam za mwaka za Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF.

Awali ya yote tumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametulinda kwa mwaka mzima na kupitia Baraka zake tumeweza kuwa na nguvu, uwezo na hekima za kutimiza majukumu yetu mbalimbali katika kipindi hiki cha mwaka 2015. Tuzidi kumuomba atuvushe salama mwaka 2015.

Ninaomba nichukue fursa hii kuwapongeza Watanzania wenzangu kwa kukamilisha mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Ninampongeza Mh. Dr John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hongera sana Mama Samia Suluhu kwa kuwa Makamu wa Rais na hongera kwa mwanamichezo mwenzetu Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kushinda ubunge jimbo la Ruangwa na kwa uteuzi wa kuwa Waziri wetu Mkuu. Hongera za kipekee kwa Mheshimiwa Nape Nnauye kwa uteuzi wa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na hongera pia kwa Mama Anastasia Wambura kwa kuteuliwa kuwa naibu waziri wa wizara hii muhimu kwa mustakabali wa afya na ajira kwa vijana na utangazaji wa jina la Nchi yetu ya Tanzania nje ya mipaka ya nchi. Ninashukuru Mh. Waziri Nnauye majuzi alinipatia fursa ya kuwa mmoja wa viongozi wa kwanza wa vyama vya Kitaifa vya michezo ya kukutana naye na kujitambulisha rasmi kwake, ahsante sana.

Ndugu zangu, Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania lipo kwa ajili ya kuendeleza na kusimamia mpira wa miguu Tanzania. Tunafanya hivyo kwa niaba ya Watanzania wote wapenzi wa mpira wa miguu. Kwa kutambua uzito na umuhimu wa jukumu hili ndio maana wakati wote TFF inafanya jitihada za dhati kuhakikisha timu zetu za Taifa zinafanya vizuri. Kwa sasa tunazo timu za Taifa kumi ambazo ni za soka la ufukweni wanawake na wanaume, umri chini ya miaka 17 wanawake na wanaume, umri chini ya miaka 20 wanawake na wanaume, umri chini ya miaka 23 wanawake na wanaume na mbili za wakubwa za wanawake na wanaume.  Katika kuingiza timu kwenye mashindano ya kimataifa tumekuwa tukizingatia vigezo kadhaa lakini kikubwa ikiwa ni utayari wa timu kushiriki mashindano na uwezo wa kugharamia mchezo wenyewe. Kwa wastani gharama za kushiriki mkondo mmoja wa mechi ya Kimataifa kwa kucheza nyumbani na ugenini ni takribani shilingi million mia moja (USD 50,000.-), hii inajumuisha gharama za kambi, usafiri kwenda ugenini, posho, nauli na posho za waamuzi na kamisaa, malazi ya waamuzi na kamisaa nk. Kwa kuwa timu yenye udhamini kwa sasa ni timu ya Taifa wanaume tuu hivyo TFF imekuwa inabeba yenyewe gharama nyingine zote kwa timu zote zilizobakia. Imani yetu ni kuwa mwaka 2016 utashuhudia ufadhili unapatikana kwa timu zetu nyingine za Taifa.

Ninaomba sasa nichukue fursa hii kuzungumzia maeneo kadhaa ambayo yamehusu mpira wetu na taasisi yetu kwa mwaka 2015:

1.   Timu ya Taifa ya wanaume “Taifa Stars”

Baada ya timu yetu ya Taifa, Taifa Stars kutofanya vizuri katika michuano ya COSAFA huko Afrika Kusini mwezi Mei mwaka huu na baadae kufuatia kufanya vibaya katika mchezo wa kwanza katika mtoano wa mashindano ya CHAN, Kamati ya Utendaji ya TFF ilichukua maamuzi ya kusimamisha ajira ya kocha wa kigeni Martin Nooj na badala yake kuingia mkataba na makocha wazawa Boniface Charles Mkwasa akisaidiana na Hemed Morocco. Tangu walimu hawa wamechukua timu ya Taifa Stars tumefungwa mechi mbili tuu za mashindano dhidi ya Algeria na Malawi ugenini, tumetoka sare na Uganda ugenini, tumetoka sare na Nigeria na Algeria nyumbani na kuwafunga Malawi nyumbani. Aidha timu ya Kilimanjaro Stars chini ya kocha Abdalla Kibadeni na msaidizi wake Juma Mgunda katika mashindano ya CECAFA  Challenge katika mechi nne ilizocheza Ethiopia haikufungwa hata mechi moja kwa muda wa mchezo (Open Play) ingawa ilitolewa kwa penati tano tano katika hatua ya nusu fainali. Katika mashindano hayo Taifa Stars ilishinda mechi mbili na kutoka sare mbili. Kipindi chote ambacho tumekuwa na makocha hawa wazawa kiwango cha Tanzania FIFA kimekuwa kikipanda mara zote. Tunawapongeza sana makocha wetu hawa na benchi zima la ufundi. Kwa sasa tunajiandaa na mechi mbali mbali za kufuzu kucheza fainali za Afrika Afcon 2017 nchini Gabon. Mechi hizi ni dhidi ya Tchad tarehe 25/03/2016 ugenini Ndjadema na mechi ya marudiano siku tatu baadae hapa Dar es Salaam tarehe 28/03/2015. Imani yetu ni kuwa timu yetu itaendeleza wimbi la ushindi. Katika kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Nigeria, Taifa Stars iliweka kambi nchini Uturuki na pia timu iliweka kambi Afrika Kusini kujiandaa na mechi dhidi ya Algeria. Kambi hizi zimesaidia sana kuimarisha timu yetu kabla ya mechi hizi kubwa mbili. Katika kujiandaa na mechi dhidi ya Tchadi mwezi Machi mwakani ratiba ya ligi kuu ikiruhusu timu itaweka kambi pia nje ya nchi.

2.   Timu ya Taifa Wanawake “Twiga Stars”.

Timu yetu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars chini ya kocha Rogasian Kaijage ilifanikiwa kuiondoa Zambia na hivyo kufuzu fainali za michezo ya Afrika Kusini Kongo Brazaville. Katika fainali hizi Tanzania ilifungwa na Ivory Coast na Nigeria na kutoka sare na Congo, hivyo kutolewa kaika hatua za makundi. Tunaamini uzoefu uliopatikana katika mashindano hayo utaimarisha timu na kufanya Twiga Stars iweze kushiriki fainali ya Afrika ya mpira wa wanawake nchini Cameroon mwaka 2016.

Hatua ya awali Tanzania itapambana na Zimbabwe mwezi Machi 2016 na mshindi wa michezo huo atacheza hatua ya pili dhidi ya mshindi kati ya Namibia na Zambia.

3.   Udhamini na michuano mipya.

Kwa kipindi hiki cha mwaka 2015 tumefanikiwa katika maeneo yafuatayo:

3.1  Kufufua Kombe la Shirikisho Azam Sports Federation Cup.

Kwa kushirikiana na mdhamini Azam Sports Kombe la Shirikisho limefufuliwa na kuboreshwa. Kwa mwaka huu tumeanza na timu 64 ambazo ni za ligi kuu (16), Ligi daraja la kwanza FDL (24) na Ligi daraja la pili SDL (24). Ili kupanua uwigo wa ushiriki wa Mikoa yote kwa misimu ya usoni timu mabingwa wa mikoa (RCL) nazo zitashirikishwa katika mashindano haya ili kila mkoa wa Tanzania upate fursa ya kushiriki katika mashindano haya. Fainali itachezwa mwezi Mei na bingwa wa Kombe hili ataiwakilisha Tanzania katika kombe la Shirikisho la Afrika CAF Confederation Cup.

3.2   Udhamini Ligi daraja la kwanza.

Tumefanikiwa kupata wadhamini wawili kwa ligi daraja la kwanza FDL. Tumempata STARTIMES ambayo ni mdhamini mkuu wa ligi na pia kampuni ya Television ya Sahara Media kupitia STAR TV imepewa haki za kuonyesha mechi hizi moja kwa moja. Haya ni mafanikio makubwa kwa ligi ya daraja la kwanza. Tunaishukuru kampuni ya Geita Gold kwa kuidhamini timu ya daraja la kwanza ya Geita Gold Sport na tunazidi kutoa wito kwa washirika wengine wazidi kujitokeza kudhamini timu zetu.

3.3    Mkataba wa Vodacom na Ligi Kuu.

Kampuni ya Vodacom baada ya mazungumzo marefu tuliafikiana na kutuliana saini ya mkataba mwingine wa miaka mitatu wa udhamini wa ligi kuu wenye ongezeko la thamani ya udhamini kwa asilimia 40%. Jitihada zimefanyika kuvutia wadhamini wengine nao waje waongeze udhamini kwa ligi kuu. Tunaishukuru kampuni ya ACACIA ambayo imejitolea kuidhamini klabu ya ligi kuu ya Stand United haya ni mafanikio makubwa kwa ligi yetu na tunazidi kuvipa moyo vilabu vizidi kupata wadhamini zaidi. Tunayashukuru sana makampuni yote ambayo yamejitokeza kudhamini vilabu mbali mbali na tunazidi kutoa wito kwa makampuni mengine yajitokeze kutoa udhamini ikiwa ni sehemu ya kutangaza biashara na kukuza jina la chapa zao.

3.4   Udhamini tarajiwa.

Tunatarajia kupata wadhamini kwa ajili ya Ligi Kuu ya vilabu vya wanawake (Women Premier League) pamoja na ligi kya vilabu vya ligi kuu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (U-20).

Jambo hili likifanikiwa matumaini yetu ni kuwa tutaanzisha ligi mpya mbili mwaka 2016, Ligi ya vilabu vya wanawake (Women Premier League) na ligi ya vilabu vya ligi kuu ya vijana umri chini ya miaka 20 (U-20). Mechi hizi nazo zitakuwa zinaonyeshwa moja kwa moja kwenye television.

Kwa matarajio haya sasa ni vyema uongozi wa kila mkoa kufanya jitihada za kuhakikisha vilabu vya mpira vya wanawake vinaanzishwa ili tuweze kuwa na ligi ya ushindani.

Ninaomba nichukue fursa hii kuwashukuru washirika wetu wote, ambao kama sio kujitolea kwa haya mafanikio tusingeweza kuyafikia/kuyapata.

Ahsante Kampuni ya Bia Tanzania kwa kupitia bia ya Kilimanjaro Lager.

Ahsante Vodacom.

Ahsante Azam Tv kwa kupitia channel ya Azam Sports HD.

Ahsante Startimes Media kwa kupitia king’amuzi cha STARTIMES.

Ahsante Sahara Media kwa kupitia Star Tv.

Ahsante AIRTEL kwa kutuletea Airtel Raising Star kwa mara nyingine mwaka huu.

Ahsante Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF.

4.   Soka la Vijana.

4.1   Fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 17 (U-17) mwaka 2017 Madagascar.

Kikosi chetu cha Taifa cha vijana chini ya umri wa miaka 17 (U-17) kinachojiandaa na hatua za mtoano mwezi Juni, 2016 ilikuwa kifanye ziara ya kimichezo katika nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, lengo ilikuwa kuwapatia vijana hao uzoefu wa Kimataifa. Wakati tayari kikosi kimejiandaa na kukabidhiwa bendera, akaunti za TFF zilifungiwa na mamlaka za mapato TRA na hivyo safari kuvunjika kwa ukosefu wa fedha. Mpango mkakati ni kuwa mwezi Aprili, 2016 timu hii itaweka kambi nje ya nchi ili kujiandaa na hatua ya mtoano (qualifiers).

4.2  Fainali za Afrika U-17 mwaka 2019.

Maandalizi ya fainali hizi ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji yanaendelea vizuri vikao na Wizara tayari vimeanza kwa ajili ya kufanya maandalizi muhimu ya awali ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Pia maandalizi ya timu itakayoshiriki fainali hizi yameanza kwa vijana umri chini ya miaka 13 (U-13) kujumuishwa pamoja katika shule ya Alliance jijini Mwanza. Imani yetu ni kuwa Tanzania tutafanikiwa kuandaa mashindano mazuri mwaka 2019 na pia kunyakua kombe hili.

4.3   Vituo vya mikoa vya kukuza na kuendeleza vipaji.

Azma ya TFF ni kuhakikisha kuwa kila chama cha mpira wa miguu cha mkoa kinakuwa na kituo mama cha kukuza na kuendeleza vipaji vya mpira. Mkataba wa mfano (template) umekwisha pelekwa katika kila mkoa ili vyama vya mkoa ambavyo havina vituo vyake basi viingie mkataba wa ushirikiano na kituo kimoja kwa lengo la kukifanya kiwe kituo mama cha mkoa. Kupitia vituo hivi TFF itaweza kuratibu shughuli za maendeleo ya mpira wa vijana katika mikoa yetu, kuongeza nguvu kwa kuvipatia vifaa na walimu. Mipira 5,000 ya 3 na 4 ya ukubwa (size), koni 3,000, beeps 2,000 tayari vimeagizwa toka nje ya nchi kwa kutumia vyanzo vya fedha vya TFF yenyewe bila kuomba msaada kutoka popote kwa ajili ya kuendeleza program hii. Tayari kila mkoa una mwalimu angalau mmoja aliyefanya kozi ya FIFA ya ukocha wa vijana isipokuwa mikoa miwili tu ya Manyara na Njombe, jitihada zitafanyika nao wapate walimu stahiki. Hivyo mtaji wa kutosha tunao wa kuanzisha vituo hivi. Pindi vituo hivi vikiimarika yataanzishwa mashindano ya kiumri (age categories) baina ya vituo hivi kuanzia ngazi ya mkoa, kanda na hatimaye Taifa. Ninatoa wito kwa viongozi wenzangu  wa mikoa tujizatiti tuweke nguvu katika uwanzishwaji na uendelezaji wa vituo hivi ambavyo vitakuwa chachu kuu ya kutoa wachezaji  wa Taifa wa kike na wakiume. Baada ya mazungumzo haya nitawakabidhi viongozi wa vyama vya mpira vya mkoa wa Manyara na Dar es Salaam mpira mmoja mmoja ikiwa ni ishara ya kuanzishwa rasmi kwa program hii ya kitaifa.

5.  Kozi mbalimbali.

Kwa kushirikiana na CAF na FIFA Shirikisho letu limeandaa, kuratibu na kutoa kozi mbali mbali za waamuzi na makocha katika ngazi mbalimbali. Jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha mikoa iliyokuwa na hazina ndogo ya makocha na waamuzi inapewa fursa ya kuratibu kozi hizi. Tunashukuru viongozi wote wa mikoa na wilaya ambao tumeshirikiana nao kutimiza azma hii. Juhudi zinaendelea ili tuweze kupata makocha, waamuzi, madaktari wa michezo na watawala zaidi. Ninaomba tuwape moyo wakina mama wazidi kujitokeza kwa wingi kufanya kozi hizi maana wao ndio nguzo kuu ya kuendeleza mpira wa wanawake nchini mwetu. Ninatoa rai kwa waajiri, hasa wakurugenzi wa Halmashauri ambao ni waajiri wa walimu wanaofundisha mpira mashuleni, wazidi kutupatia ushirikiano kwa kutoa ruhusa kwa waajiriwa wao pindi wanapoomba kuhudhuria kozi mbalimbali zitolewazo na TFF.

6.   Bodi ya Ligi na Vilabu.

Utendaji katika bodi yetu umeimarishwa kwa kutoa ajira kwa mtendaji mkuu Ndugu Boniface Wambura. Mipango ya kuimarisha sekretariet ya Bodi ikiwa ni pamoja na kupata nafasi kubwa zaidi ya kufanyia kazi iko mbioni. Matarajio yetu ni kuwa chombo hiki kikiweza kuimarika kitakuwa ni chachu ya kuandaa ligi zilizo bora zaidi na zenye ushindani.

Pamoja na jitihada za kutafuta wadhamini wa mashindano mbalimbali yanayohusisha vilabu, jitihada pia zinaendelea kufanyika kuhakikisha vilabu vyetu vinaimarisha utawala bora. Kufuatia CAF na FIFA kuanzisha utaratibu wa kutoa leseni kwa vilabu (Club Licencing) jitihada sasa zinafanyika kuhakikisha vilabu vinaelimishwa kwa kina juu ya mahitaji ya leseni hizi. Katika utaratibu wa leseni za vilabu, vilabu vyetu sasa vitalazimika kuwa na ofisi, watendaji wa kuajiriwa, kuwa na maeneo ya kufanyia mazoezi, kuwa na program ya maendeleo ya vijana, kuajiri walimu wenye sifa n.k. Tunaamini utaratibu wa leseni za vilabu ukitekelezwa ipasavyo uendeshaji wa vilabu vyetu utaboreshwa na hivyo kuongeza tija kwa vilabu vyetu.

7.   Tiketi za Eletroniki.

Kutokana na matatizo yaliyojitokeza matumizi ya tiketi za eletroniki yalisimamishwa na mmiliki wa uwanja wa Taifa ambaye ni Serikali. Baada ya mazungumzo na mtoa huduma ambaye ni Benki ya CRDB ilikubaliwa atafutwe mshauri mwelekezi (Consultant) kwa kupitia mfumo mzima ili kubaini matatizo na baadae kutoa ushauri wa namna ya kuboresha mfumo huo. Tenda ya kumpata mshauri huyu ilikwishatangazwa na kinachofuatia ni TFF kwa kushirikiana na CRDB kuteua mshauri huyo. Imani yetu ni kuwa kazi ya mshauri ikikamilika basi mwongozo utapatikana ili utekelezaji wa uboreshaji wa mfumo ukamilike na matumizi ya tiketi za eletroniki yaweze kuendelea.

8.   Mfuko wa Maendeleo ya Mpira (Football Development Fund).

Baada ya mfuko huu kuanzishwa kikatiba katika mkutano mkuu uliopita, kamati ya utendaji ya TFF iliteua wajumbe wa kamisheni ya uendeshaji wa mfuko huu chini ya Mwenyekiti Ndugu Tido Mhando na Mtendaji Mkuu Henry Tandau. Mfuko huu tayari umefanikiwa kupata ofisi yake na shughuli zake zitaanza punde baada ya kuwekewa vitendea kazi. Lengo la mfuko huu kama ilivyoanishwa ni kuwa chanzo kikuu cha kupata rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu nchini mwetu. Ninaomba tuwaunge mkono na kuwapa ushirikiano watendaji wa mfuko huu huku tukitambua kuwa maendeleo ya mpira yanahitaji rasilimali nyingi.

9.   Kufungiwa akaunti za TFF.

Kutokana na madeni ambayo yamekuwa kwenye mafaili ya mamlaka ya mapato kwa kipindi karibia miaka mitano iliyopita, mamlaka ya mapato nchini TRA iliamua kuzifungia akaunti zetu na pesa yote kuhamishiwa Benki kuu. Mazungumzo yanaendelea kati ya TFF, Mamlaka ya mapato na Wizara husika ili fedha hizi ziweze kurudishwa. Tunaushukuru uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambao wametusaidia kutuongoza namna ya kukabiliana na changamoto hii.

 OMBI  KWA SERIKALI.

Duniani kote, iwe katika nchi tajiri au maskini, michezo huendelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na taasisi zinazoendesha shughuli za michezo husika. Tunaiomba serikali tuzidi kushirikiana kwa karibu katika kuandaa timu zetu za Taifa, kuboresha miundo mbinu ya kuchezea mpira, kusaidia upatikanaji wa vifaa vya michezo kwa gharama nafuu, kuto fursa kwa waajiriwa wake, hasa walimu, wafanye kozi mbalimbali za ukocha na uamuzi. TFF itafarikika sana iwapo itapewa fursa na Serikali ya kuratibu na kusimamia mpira wa miguu katika mashindano ya Taifa ya shule za msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA). Tunaamini TFF ikipewa fursa hiyo itaongeza uweledi katika usimamizi wa mashindano hayo na kuhakikisha vipaji vinaibuliwa kila mwaka kuliko ilivyo sasa.

Ndugu zangu, wakati tunauaga mwaka 2015 na kuelekea kuingia mwaka 2016 ninaomba nimalizie kwa kutoa wito kwa wadau wote wa mpira wa miguu Tanzania tuzidi kushirikiana, penye makosa tukosoane japo kwa staha na penye kuhitaji ushauri tushauriane.

Imani yetu ni kuwa mwaka 2016 utakuwa ni mwaka wa mafanikio kwa mpira wetu.

Mungu Ibariki Tanzania.

Mungu Ibariki Afrika.

Ahsanteni,

 Jamal Malinzi

Rais wa TFF
Dar es Salaam.
30 Desemba, 2015.

Saturday, December 26, 2015

YANGA YACHANJA MBUGA, SIMBA YASONONESHA MASHABIKI WAKE


YANGA SC imetanua mbawa kileleni mwa Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 33, baada ya kucheza mechi 13, wakati Azam FC iliyocheza mechi 12, ina pointi 29.
Mrundi Amissi Tambwe aliifungia Yanga SC mabao mawili mfululizo, la kwanza dakika la 37 akimalizia pasi ya winga Simon Msuva na la pili dakika ya 65 akimalizia krosi ya Mwinyi Hajji Mngwali, kabla ya kumpasia kwa kichwa Mzimbabwe Thabani Kamusoko kufunga la tatu dakika ya
66.
katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, Simba SC imelazimishwa sare ya 1-1 na Mwadui FC ya kocha Jamhuri KIhwelo ‘Julio ’Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.


Mwadui walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Nizar Khalfan dakika ya 77, kabla ya Brian Majwega kuisawazishia Simba SC dakika ya 86.

CHANZO CHA HABARI: BLOGU YA BINZUBEIRY

Friday, December 25, 2015

TFF YAIDHINISHA USAJILI WA DIRISHA DOGO


 Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Richard Sinamtwa, jana Jumatano ilikaa na kupitia malalamiko/pingamizi za usajili wa wachezaji yaliyokuwa yamewasilishwa TFF mara tu baada ya usajili wa dirisha dogo uliofungwa Disemba 15, mwaka huu.

Kamati hiyo imeweza kupitia na kupitisha usajili kwa vilabu mbalimbali, huku pia kamati hiyo ikizuia baadhi ya usajili wa wachezaji waliosajiliwa, mpaka pande hizo mbili zitakapomalizana ndipo mchezaji husika ataweza kuitumikia klabu yake mpya.

Ifuatayo ni taarifa kamili ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji,A. USAJILI

1. Kamati imepitisha usajili wa wachezaji walioombewa kwa vilabu vifuatavyo vya ligi kuu

1. AZAM FC - mchezaji mmoja Ivo Philiph Mapunda (huru)2. COASTAL UNION - wachezaji watatu

i. Omary Wayne Maunda-Mkopo toka Azam

ii. Miraji Adam Seleman-mkopo toka Simba

iii. Ramadhani Ali Thabit-huru

 3. MGAMBO SHOOTING

i. Mudathir M. Khamis-Yanga

ii. Nurdin Mkomeni-huru

iii. Godson Mmasa-alikuwa mchezaji wa Mgambo, wameomba kumsajili tena4. MTIBWA SUGAR

i. Alex Mwambisi-huru

ii. Boniface Maganga-Mkopo kutoka Simba

iii. Kelvin Iddi Friday-Mkopo kutoka Azam

iv. Abdallah Said Makangana-alisahaulika usajili uliopita ni mchezaji anayendelea

5. MWADUI SCi. Abdallah Mfuko-huru

ii. Ismail Gambo-Mkopo kutoka Azam FC6. NDANDA SC

i. Braison Raphael-Mkopo kutoka Azam

ii. Jackson John Nkwera-Sinza Srtars7. MBEYA CITY

i. Ramadhani Selemani Chombo-huru

ii. Abdallah Salum Juma-Toto Africans

iii. Deogratius Julius-Kagera Sugar

8. TANZANIA PRISONS

i. Baraka Majogoro-Wenda FC9. TOTO AFRICANS

i. Shija Hassan Mkina-huru

ii. Frank B Kimati-huru

iii. Ladslaus Mbogo-huru

iv. Yusuf Seleman Mpili-huru

v. Maneno Steven Shaban-huru10. SIMBA SC

i. Kiongera Raphael-Amerudishwa toka KCB alikokuwa anacheza kwa mkopo

ii. Novaty Lufunga-African Sports

iii. Haji Mohamed Ugando-Jaki Academy

iv. Brian Majegwa-Azm FC

11. STAND UNITED

 i. Assouman N’gueassan David-FC Olympic Sports Abobo12. YOUNG AFRICANS

i. Issoufou Boubacar-

ii. Paul Nonga-Mwadui13. JKT RUVU

i. Waziri Shaban Iddi-huru

ii. Hamis Thabit-African Lyon

iii. Hassan Dilunga-Stand United14. MAJIMAJI

 i. Kennedy Stainley Kipepe-Njombe Mji

ii. Abubakar B Bakari-huru

iii. Sixmund Ally Mwakasekaga-huru

iv. Paulo Maona Terry-huru15. KAGERA SUGAR

i. Ramadhani Mzee Kipalamoto-Kagera Sugar

ii. Samwel Donald Ngassa-huru

iii. Shaaban Ibrahim Sunza-Mshikamano

iv. Martin Lupart Mlolere-Abajalo, Dar es Salaam

 v. Juma Jabu Hamis-huru 16. AFRICAN SPORTS

i. Hamis Twairu Juma-U20, huru

ii. Hamad Nathaniel Mbumba-Polisi Tabora

iii. Hamad Nathaniel Mbumba-African Lyon

iv. Charles Martin Ilamfya-Mkopo toka Mtibwa

v. Rajab Isihaka-huru

vi. Reyna Mgungira-huru

USAJILI UFUATAO UMEZUILIWA KWA MAELEZO YAFUATAYYO

1. AFRICAN SPORTS

i. Karim Hamud Juma aliyeombea kusajiliwa na African Sports akitokea PolisiTabora usajili wake

ii. Michael Victor Mgimwa kamati imezuia usajili wake mpaka hati ya uhamisho wa kimataifa umezuiwa mpaka timu mbili zitakapofikia makubaliano itakapotumwa toka Thailand, mchezaji huyu alikuwa anaitumikia Rio United ya Thailand.

2. MAJIMAJI SPORTS CLUB

i. Danny David Mrwanda na Lulanga Andrew Mapunda-kamati imezuia usajili wake mpaka vilabu viwili vya Majimaji inayotaka kumsajili na Lipuli iliyokuwa inawamiliki wachezaji hao zitakapokubaliana na kutuma kwa maandishi makubaliano yao TFF.

 3. MBEYA CITY

i. Kamati baada ya uchunguzi imejiridhisha kwamba mchezaji Tumba Sued aliyewekewa pingamizi na Coastal Union alisaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu na Coastal Union siku ya tarehe 12 June, 2014 na mkataba huu ulienda kushuhudiwa kwa mwanasheria siku ya tarehe 23 Agosti 2014, kushuhudiwa huku hakukubatilisha mkataba uliosainiwa tarehe 12 June 2014.

Hivyo kamati inamtangaza Tumba Sued kuwa mchezaji huru toka tarehe 11 Desemba na kwa sasa ni mchezaji halali na amepitishwa kuichezea Mbeya City ya Mbeya.

ii. Kamati pia inatoa onyo kali kwa klabu ya Mbeya City na imeagiza kesi hii ipelekwe kwenye kamati ya nidhamu kwa kuongea na mchezaji Ditram Nchimbi ambaye ni mchezaji halali wa Majimaji ya Songea ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili na Majimaji  tarehe 20 Oktoba 2014 hivyo mkataba wake utaisha tarehe 19 Octoba 2016. Mbeya City wameongea na mchezaji mwenye mkataba uliozidi miezi 6 bila kuomba ridhaa ya klabu inayommiliki ambayo ni Majimaji.

4. JKT RUVU

JKT Ruvu iliomba kumsajili mchezaji Hassan Dilunga kutoka Stand United kwa kufata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kuongea na klabu yake ya Stand United na kupata kibali cha kumsajili Dilunga kutoka kwa uongozi halali wa Stand United kupitia kwa mwenyekiti na katibu wa Stand United. Pamoja na ruhusa kutoka kwa Stand United bado kuna mtu anayeitwa mratibu wa Stand United aliiandikia barua TFF akipinga usajili wa mchezaji huyu.

Kamati imesikitishwa na kiendo cha mtu huyu ambaye hatambuliki na TFF na wala siyo mtu anayepaswa kuwasiliana na TFF kwa kuingilia maamuzi ya viongozi halali wa Stand United na imeamuru mtu huyo anayeitwa Mbasha Matutu apelekwe kamati ya maadili kwa kupora mawasiliano ya Stand United wakati viongozi halali wanaotambulika kikatiba wa Stand United wapo.

Kamati imeamua mratibu Mbasha Matutu apelekwe kamati ya maadili kufuatia kutofata na kuheshimu uongozi halali wa klabu ya Stand United.

5. NDANDA SC-RAMADHANI KIPALAMOTO

Klabu ya Ndanda SC ilileta maombi ya kumsajili mchezaji Ramadhani Salim Kipalamoto amabye alikuwa anachezea Abajalo SC ya Dar es Salaam, maombi haya yamekataliwa kwa kuwa mchezaji husika alikuwa pia ameombewa kusajiliwa na Kagera Sugar na klabu yake ya Abajalo ikatoa ridhaa ya mchezaji huyu kwenda Kagera Sugar ya mkoani Kagera.

6. NDANDA SC-IBRAHIM IS-HAAK

Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji  imeridhia ombi la mchezaji Ibrahim Is-haki aliyedai klabu yake ya Ndanda SC kuvunja mkataba wake kwa kutomlipa hela yake ya usajili kama walivyokubaliana.

Mchezaji huyu amevunja mkataba wake baada ya maombi yake TFF kukubaliwa na mwakilishi wa klabu yake ya Ndanda SC, Edmund Njowoke ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Ndanda SC, na kamati imeridhia maombi ya timu ya Geita SC ya kutaka kumsajili.

Mchezaji Ibrahim Is-haak amepitishwa kuichezea timu ya Geita Gold SC ya Geita.

7. MWADUI SC

Kamati imeridhia pingamizi la klabu ya KMC ya Kinondoni kumzuia mchezaji Emmanuel Memba aliyeombewa kusajiliwa na Mwadui Sc kwa kutofata utaratibu. Kamati inaiagiza klabu ya Mwadui kuongea na KMC wamiliki wa mchezaji ili wawaruhusu kumtumia mchezaji husika.

8. KIMONDO SC

Klabu ya Kurugenzi ya Mafinga imeleta pingamizi dhidi ya Kimondo FC kwa kumsajili mchezaji wao George Mpole bila kufata utaratibu. Kamati inaishauri Kimondo SC kufata utaratibu wa usajili kwa kuongea na Kurugenzi.

9. GEITA GOLD SC

TFF imepokea ombi la pingamizi kutoka kwa timu ya Rhino Rangers kwa Geita Gold SC kumsajili mchezaji wao Pius Kisambale bila kufuata utaratibu. Geita inatakiwa kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kuongea na uongozi wa timu ya Rhino SC ya Tabora

10. POLISI MOROGORO

Imeleta ombi la pingamizi la wachezaji wao wawili

i. Anafi Selemani Ally

ii. Mohamed Kapeta kusajiliwa na timu yoyote kwa kuwa ni wachezaji wao. Ombi la pingamizi kwa wachezaji hao limekubaliwa na kamati

LIGI DARAJA LA KWANZA SASA KUONYESHWA LIVELigi Daraja la Kwanza nchini (StarTimes First Division League) mzunguko wa pili unaanza kutimua vumbi siku ya Jumamosi katika viwanja tisa mbalilimbali, huku michezo ya ligi hiyo ikianza kuonyeshwa moja kwa moja na kampuni ya Sahara Media kupitia kituo chake cha luninga cha StarTV.

Akiongea na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa TFF, Meneja Masoko wa kampuni ya StarTimes Tanzania, Damien Li amesema anashukuru michezo ya Ligi Daraja la Kwanza inaanza kuonekana moja kwa moja kwenye luninga.

Damien alisema StarTimes wanafarijika kuwa wadhamini wa kwanza kabisa wa ligi  wa daraja la kwanza nchini tangu kuanzishwa kwake, na sasa wanaviomba vilabu vyote vinavoshiriki ligi hiyo kutumia nafasi hiyo kujitangaza ndani na nje pamoja na wachezaji wao.

StarTimes ilingia udhamini wa Ligi Daraja la Kwanza wenye thamani ya milioni 900 (mia tisa) za kitanzania kwa kipindi cha miaka mitatu, huku kituo cha StarTV kikiongeza milioni 450 (mia nne hamsini) na kufanya udhamini huo kwa jumla kuwa ni bilioni 1.25 kwa kipindi cha miaka mitatu.

StarTv wataanza kuonyesha moja kwa moja mchezo wa Jumamosi, Disemba 26 kati ya Friends Rangers dhidi ya Polisi Dar mchezo utakaochezwa uwanja wa Karume, huku Jumapili Disemba 27 wakionyesha moja kwa moja mchezo kati ya Kiluvya United hidi ya Ashanti United Uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Naye Afisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, amevitaka vilabu vya Ligi Daraja la Kwanza kuitumia vizuri nafasi hiyo kujitangaza kimataifa, kwa kuheshimu taratibu na kanuni zinaondesha ligi hiyo.

Kizuguto amesema ligi hiyo itakuwa ikirushwa moja kwa moja na kampuni ya Sahara Media kupitia kituo chake cha StarTV, ambapo zaidi ya nchi 50 barani Afrika na Asia watapata nafasi ya kushuhudia michezo hiyo.

Wednesday, December 23, 2015

SERIKALI YAUPATIA UFUMBUZI MGOGORO WA TIMU YA SOKA YA STAND UNITEDWaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua zilizofikia katika kutatiua mgogoro baina ya Timu ya Stand Unite ya mjini Shinyanga na kamati ya uendeshaji ya timu hiyo iliyopo chini ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa leo jijini Dar es Salaam.Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,WHUSM.

Na: Frank Shija, WHUSM

Serikali imeagiza kumalizika kwa mgogoro uliopo baina ya Timu ya mpira wa miguu ya Stand United na Kamati ya uendeshaji wa timu hiyo iliyopo chini ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Agizo hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye mara baada ya kumaliza kikao na uongozi wa Stand United.

Nape amesema kuwa imefika wakati vilabu vikapewa uhuru wa kujiendesha kwa kutumia katiba zao badala ya kingiliwa na chombo kingine chenye  maslahi binafsi.

“Wizara itasaidia kuona mgogoro huu unaisha kwa Stand United kupewa uhuru wa kujiendesha yenyewe na uongozi uliokuwapo kupewa mamlaka yake ya kusimamia na kuendesha shughuli za Timu yao kwa mujibu wa Katiba”

Aidha aliongeza kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusimamia uendeshaji wa mchezo wa mpira wa miguu kwa kuzingatia sheria ,kanuni na taratibu za mchezo huo ili kuepuka migogoro isiyokuwa na tija.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Timu ya Stand United Bw. Aman Vicent ameishukuru Serikali kupitia Wizara yenye dhamana na masuala ya michezo kwa kuona umuhi wa kushughulikia na kumaliza mgogoro wao.

Aman amesema kuwa kutokana na makubaliano waliyofikia katika kikao hicho imani yao ni kuwa suala hili litamalizika mapema kwa kuwa Waziri mwenye dhamana ameonyesha nia na utayari wa kuhakikisha suala hili linaisha kwa wakati ili Timu iweze kusonga mbele katika kujiletea maendeleo.

Kikao baina ya Waziri na uongozi wa Timu hiyo kimefanyika ikiwa ni matokeo ya juhudi za uongozi wa Timu ya Stand Uinted kuinusuru timu yao baada ya kujikuta katika mgogoro usiokuwa na tija zaidi ya maslahi binafsi kutoka na udhamini walionao.

DIAMOND KUFANYA MAKAMUZI YA NGUVU DAR LIVE KRISMAS


STAA wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amewaahidi shoo ya nguvu mashabiki wake na kuwataka waje kwa wingi katika shoo kali ya kufunga mwaka itakayopigwa Dar Live, Mbagala Zakhem, Dar katika Sikukuu ya X-mas na kuwa hatawaangusha.

Diamond anayetamba na ngoma ya Utanipenda ameyaongea hayo leo kwenye mkutano maalum uliofanyika Karume, Dar ambao ulihusisha waandishi wa habari na wapenzi wa muziki kwa ajili ya kuzungumzia shoo hiyo kubwa kuliko inayojulikana kama Funga Mwaka Concert.
 

“Itakuwa ni Sikukuu ya Krismasi, sasa kwa nini tusifurahi pamoja, kama MTV wameamua kunipa tuzo ya Mtumbuizaji Bora Afrika kwa hiyo sihitaji kuongea sana shoo itakuwaje siku hiyo, naomba mje kwa wingi kwa kweli sipendi kuwaudhi, nawaahidi sitawaangusha,” alisema Diamond au Baba Tiffah.

Pia waandaji wakuu wa shoo hiyo, Global Publishers Ltd, kupitia kwa Meneja Mkuu, Abdallah Mrisho, naye alizungumza machache pamoja na kutambulisha listi ya wasanii wengine watakaoambatana na Diamond siku hiyo.

“Mbali na Diamond pia kutakuwa na Msagasumu, Wakali Dancers, Staric pamoja na burudani nyingine nyingi. Haitakuwa shoo ndogo, Diamond ameamua kufurahi na mashabiki wa muziki siku ya Krismasi kwa kufunga na kuukaribisha mwaka mpya. Shoo zitaanza asubuhi kwa watoto mpaka saa 12 jioni kisha baada ya hapo ni watu wazima mpaka alfajiri,” alisema Mrisho.

Viingilio ni Sh 15,000 na kwa V.I.P ni Sh 30,000 lakini wadhamini wakuu wa shoo hiyo, Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel wakaamua kutoa ofa ya punguzo la bei kwa tiketi 1,000 za awali kwa watakaokata kupitia kadi mpya za Airtel Money Tap Tap zenye mfumo mpya wa kulipia bili mbalimbali.

“Kadi za Tap Tap zinazorahisisha kufanya malipo zaidi popote ulipo bila ya gharama yoyote tayari zipo zinapatikana maeneo ya Temeke na Ilala lakini kuwa nayo unapaswa kuwa na kadi ya Airtel na kwa wateja 1,000 wa kwanza wenye Tap Tap watakaokata tiketi kupitia kadi hiyo watakuwa na punguzo la Sh 5,000 yaani kwa 15,000 itakuwa 10,000 na 30,000 itakuwa 25,000,” alisema Meneja Uhusiano Msaidizi wa Airtel Tanzania, Jane Matinde. .

Tuesday, December 22, 2015

MABADILIKO YA JINA LA BLOGU
WAPENZI WASOMAJI.

BLOGU YAKO PENDWA YA CCMNUMBERONE, ILIYOKUWA MAALUMU KWA KURIPOTI HABARI ZA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2015, SASA IMEBADILISHWA JINA NA ITAJULIKANA KWA JINA LA TANZANIAKWANZADAIMA. ITAKUWA MAALUMU KWA KURIPOTI HABARI ZA KISIASA, KIUCHUMI, BIASHARA, ELIMU NA MAMBO MENGINE YA KIJAMII.

INAPATIKANA KWA ANWANI IFUATAYO:
www.tanzaniakwanzadaima.blogspot.com

KARIBUNI TUENDELEZE LIBENEKE.
Sunday, December 20, 2015

AZAM YAIKOSESHA RAHA MAJIMAJI


AZAM FC imepata ushindi muhimu wa ugenini, baada ya kuifunga mabao 2-1 Majimaji Uwanja wa Majimaji Songea jioni ya leo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Ushindi huo unaifanya Azam FC ifikishe pointi 29 baada ya kucheza mechi 11 na kuendelea kubaki nafasi ya pili, nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 30 na mechi moja zaidi. 
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Didier Kavumbangu alianza kuifungia Azam FC dakika ya 10, kabla ya Ame Ally ‘Zungu’ kufunga la pili dakika ya 20.
Bao pekee la wenyeji, Majimaji lilifungwa na Alex Kondo dakika ya 55.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Serge Wawa, David Mwantika, Farid Mussa, Frank Domayo, Jean Mugiraneza, Ame Ally/Allan Wanga dk85, John Bocco na Didier Kavumbagu.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, JKT Ruvu imelazimishwa sare ya 2-2 na Coastal Union Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, wakati Mbeya City nayo imelazimishwa sare ya 1-1 na Mgambo JKT Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

MECHI ZIJAZO…
Desemba 23, 2015
Azam FC vs Mtibwa Sugar
Desemba 26, 2015
Ndanda FC vs JKT Ruvu
Yanga SC vs Mbeya City
Majimaji vs Prisons
Mwadui FC vs Simba SC
Mtibwa Sugar vs Mgambo JKT
Coastal Union vs Stand United
Desemba 27, 2015
Azam FC vs Kagera Sugar
Toto Africans vs African Sports

IMETOLEWA BLOGU YA BINZUBEIRY

NAPE KUMWAKILISHA SAMIA TAMASHA LA PASAKA


Na Mwandishi Wetu

WAZIRIwa Habari,Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye anatarajia kumwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwenye Tamasha la Krismasi  linalotarajia kufanyika Desemba 25 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti  wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, Makamu huyo wa rais alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo lakini kutokana na majukumu mengine ya kikazi, hivyo tunaendelea na maandalizi ya tamasha hilo.

Msama alisema  wanamshukuru Nape kukubali kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo ambalo lina mlengo wa kurudisha shukrani kwa Mungu baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.

“Ni nafasi yetu kama Kampuni na Watanzania kurudisha shukrani kwa Mungu baada ya kipindi ambacho kilikuwa kigumu katika maendeleo ya Tanzania, alisema Msama.

Aidha Msama alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha hilo kwa sababu ya kufikisha shukrani kwa Mungu baada ya uchaguzi Mkuu.

Alitaja viingilio kwa VIP ni shilingi 50,000, viti maalum shilingi 10,000, viti vya kawaida shilingi 5000 na watoto shilingi 2000.

Msama aliwataja waimbaji watakaopanda jukwaani siku hiyo ni pamoja na Rebecca Malope (Afrika Kusini), Solomon Mukubwa, Sarah K, Faustin Munishi (Kenya), Rose Muhando, Upendo Nkone, Jesca BM, Joshua Mlelwa, Kwaya ya Wakorintho Wapili na KKKT Yombo.

“Maandalizi yamefanyika kwa kiasi kikubwa yamefanyika, hivyo nawaomba Watanzania tujitokeze kwa wingi siku hiyo ili kufanikisha asante kwa Mungu,” alisema Msama.

Saturday, December 19, 2015

AMISI TAMBWE AIPAISHA YANGA


STRAIKA Amissi Tambwe raia wa Burundi leo amefanya yake kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kupiga hat-trick timu yake ya Yanga ilipoilaza Acacia Stand United bao 4-0.

Acacia Stand United ilikosa nafasi nyingi za wazi huku Yanga wao wakitumia vizuri nafasi walizozipata na kufanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao matatu pamoja na pointi tatu zilizowafanya waendelee kukaa kileleni wakiwa na pointi 30.

Tambwe alianza kucheka na nyavu za wapinzani wao dakika ya 18 baada ya Thaban Kamusoko kupiga mpira uliomkuta kipa wa Stand, Frank Muwange ambaye alirudisha mpira ndani na kumkuta Tambwe aliyetupia nyavuni.

Dakika ya 29, Elius Maguli aliikosesha timu yake bao baada ya kupiga shuti lililotoka nje kidogo ya goli ambapo Tambwe alicheka tena na nyavu dakika ya 36 bao alilofunga kwa kichwa.

Acacia Stand United, ilikosa bao lingine kupitia kwa kiungo wao Harun Chanongo ambaye pia alipiga shuti kali na kugonga mwamba akiwa yeye na kipa Deogratius Munishi 'Dida'.

Tambwe aliwainua tena mashabiki wa Yanga katika dakika ya 45 na kuifanya Yanga ambao ni Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao hayo matatu.

Dakika ya 66, Kamusoko aliipatia Yanga bao la nne ambalo alifunga kwa kichwa ukiwa ni mpira wa krosi na ndipo kocha wa Acacia Stand United, Patrick Leiwig aliamua kufanya mabadiliko ya kuwatoa Maguli, Amri Kiemba na Abuu Ubwa ambao nafasi zao zilichukuliwa na Frank Khamis, Jeremiah Katula pamoja na Seleman Mrisho

Kocha wa Yanga, Hans Pluijm aliamua kuwatoa Donald Ngoma na Kelvin Yondan nafasi zao zilichukuliwa na  Matheo Anthony na Pato Ngonyani

Mwamuzi wa mchezo huo Ludovic Charles alitoa kadi nyekundu kwa mchezaji wa Stand United, Katula katika dakika ya 90 baada ya kumfanyia madhambi Tambwe.

IMETOLEWA KUTOKA BOIPLUSBLOGSPOT.COM

SIMBA YABANWA MBAVU NA TOTO AFRICAN SPORTS


SIMBA leo imeshindwa kuonyesha makucha yake mbele y Toto African ya jijini Mwanza baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 22 kupitia kwa mshambuliaji wao Danny Lyanga huku Toto ikisawazisha dakika za nyongeza mfungaji akiwa ni Evarist Bernard ambaye aliingia kuchukuwa nafasi ya Miraji Athuman dakika ya 71.

Hiyo ni sare ya pili mfululizo kwa kikosi cha Simba baada ya kulazimishwa sare kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya Azam wakienda sare kwa kufungana bao 2-2 uwanja wa taifa.

Katika Uwanja wa Mwadui Complex, wenyeji Mwadui wameifunga Ndanda FC mabao 2-1, mabao ya Mwadui yalifungwa na Jerry Tegete na Jabir Azizi wakati bao la Ndanda lilifungwa na Atupelek Green huku Kagera Sugar ikiifunga African Sports bao 1-0, bao lililofungwa kwa penalti na Salum Kanoni.

Azam wao wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 26 na wamecheza mechi 10 ambapo kesho watacheza na Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji uliopo Songea.

MICHUANO YA LIGI YA MKOA WA DAR ES SALAAM KUANZA JUMATATU DESEMBA 21


Michuano ya ligi ya mkoa wa Dar es salaam kwa msimu wa mwaka 2015/2016 inaanza kutimua vumbi siku ya jumatatu desemba 21,kwa michezo minne kupigwa katika viwanja tofauti.

Timu ya Sifapolitan wataikaribisha timu ya Ninja, Katika uwanja wa S/msingi Kigamboni,timu ya Inter Milan watacheza dhidi ya timu ya Red Coast katika uwanja wa M/nyamala,timu ya Kijitonyama watakipiga dhidi ya Azania Ngano kwenye uwanja wa Kunduchi,huku timu ya Mkunguni wakioneshana ubabe dhidi ya timu ya Magereza kwenye uwanja wa Magereza.


Ligi hiyo ya mkoa wa Dar es salaam inashirikisha jumla ya timu 32 zilizopangwa a katika makundi manne, ambapo kila kundi linaundwa na timu 9,zitakazomenya kusaka washindi watatu kila kundi watakaoingia kucheza hatua ya pili,na washindi watatu wa jumla watakaopatikana,majina yao yatapelekwa Tff kwaajili ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa wa mikoa.


Kamati ya mashindano ya chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA,imethibitisha kukamilika kwa maandalizi yote ya ligi hiyo,ikiwa ni pamoja na kuzipa kanuni na taratibu klabu zote zinazoshiriki.


DRFA ina imani kuwa kama ilivyokuwa katika misimu iliyopita,mashindano hayo yataleta ushindani wa kweli na hatimaye kuwajenga kiuwezo wachezaji watakaojihakikishia kupata nafasi katika vilabu vinavyoshiriki ligi daraja la kwanza na ligi kuu hapo baadaye.

TFF YAMFIKISHA JERRY MURO KWENYE KAMATI YA MAADILIShirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litamfikisha kwenye Kamati ya Maadlili mapema Mwakani baada ya sikukuu ya mwaka Mpya 2016, Mkuu wa Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Jerry Muro kutokana na kauli zake za kibaguzi dhidi ya Mkuu wa Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara.

Muro alimshambulia kwa maneno ya kibaguzi Manara wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika mkutano uliofanyika jana makao makuu ya klabu ya Yanga jijini Dar es Salaam.

Kauli ya Muro dhidi ya Manara ni kinyume na Katiba ya TFF, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambao zinapiga vita vitendo vya ubaguzi wa aina yoyote katika mpira wa miguu.

Mapema mwaka huu, Muro alifikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kutokana na kumshambulia na kumdhalilisha kupitia vyombo vya habari aliyekuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Fatma Abdallah. Kamati ya Nidhamu ilimwadhibu kwa kumpiga faini ya sh. milioni 5.

Friday, December 18, 2015

RATIBA YA MECHI ZA LIGI KUU LEOMwadui FC vs Ndanda FC (Mwadui Complex-Shinyanga)

Kagera Sugar vs African Sports (Ali Hassan Mwinyi-Tabora)

Tanzania Prisons vs Mtibwa Sugar (Sokoine Stadium-Mbeya)

Toto Africans vs Simba SC (CCM Kirumba-Mwanza)

Majimaji FC vs Azam FC (Majimaji Stadium-Ruvuma)

TFF YAFANYA MAREKEBISHO YA KANUNI ZA USAJILI


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya marekebisho ya kanuni za usajili ambapo sasa mchezaji ambaye usajili wake utakuwa umepita kwenye mfumo wa mtandao wa Transfer Matching System (TMS) atapewa leseni na kuitumikia moja kwa moja timu yake mpya.

TFF itatoa leseni ya usajili wa mchezaji ambaye amethibitishwa kupitia mtandao wa TMS baada ya kuwepo nyaraka zote; mkataba uliomalizika, barua ya kuvunja mkataba, barua ya kuachwa (release letter), mkataba mpya na uthibitisho wa makubaliano kati ya klabu zinazohusika.

Licha ya mchezaji kupata leseni, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji bado itakuwa na mamlaka ya kushughulia upungufu, malalamiko ya kiusajili, pingamizi na uhalali wa kimkataba kati ya pande mbili (mchezaji na klabu).

Wachezaji wote wa kigeni waliosajiliwa kwa ajili ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) wanapaswa kulipiwa dola za kimarekani U$ 2,000 kwa kila mmoja kabla ya kupatiwa leseni na kuanza kuzitumikia klabu zao katika michuano ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.

Pia TFF kupitia kamati ya sheria na hadhi za wachezaji inaweza kumruhusu kwa kipindi maalum mchezaji mwenye dosari acheze kwa leseni ya muda (provisional license) hadi dosari hizo kati ya klabu na klabu zitakapomalizwa. Iwapo dosari hizo hazitakuwa zimemalizwa, mchezaji anaweza kuzuiwa kucheza na klabu husika kuadhibiwa.

Timu zote za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili zinatakiwa kufuatilia TFF kujua wachezaji ambao hawana pingamizi na leseni za wachezaji waliopitishwa wanaweza kuanza kutumika kuanzia kesho tarehe 18/12/2015 na kwenye michezo ya kombe la Shirikisho (FA Cup) kama hawakuwa wamecheza raundi ya kwanza kwenye vilabu vya zamani.

MBEYA WAANDAA KOZI YA UKOCHA YA LESENI C


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa kushirikiana na Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (MREFA) wameandaa kozi ya makocha wa mpira wa miguu Leseni C, itakayofanyika jijini Mbeya kuanzia Disemba 21- 04 Januari, 2016.

Jumla ya makocha 46 kutoka katika kanda ya Nyanda za Juu Kusini wanatazamiwa kushiriki kozi hiyo ya wiki mbili, ambayo itaendeshwa na wakufunzi Kidao Wilfred na Salum Madadi.

Washiriki wa kozi hiyo ni Mussa Kasalika, Steven Viera, Golya, Mlekwa, Matokeo Sigalla, Ernest Nkandi, Felix A. Sosteness, Michael Mwamaja, Daniel Mwaisabila, Deus Nsheka, Albert Gama, Joseph Abiero, Simon Mwapili, Bahati Mwaipopo, Willy Ngailo, Charles Makwaza, Paul Msyahila, Osward Morris, Jacob Ndago, Castor Mahona, Ambilikile Albion, Jumanne Nsunye, Gowdin Mulenga.

Wengine ni Abel Shizya, Matatizo Abdallah, Michael Kasekenya, Thomas Kasombwe, James Wanyato, Rose Njobelo, Amos Chiwaya, Baraka Kibanga, Mohamed Dondo, Josephat Digna, Shabani Mwaibara, Lucas Kibaja, Yusuph Mlekwa, Joel Makitta, Josiah Steven, Rashid Kasiga, Charles Njango, Alex Lusekelo, Shabani Kazumba, Ismail Suleiman, Ibrahim Kasegese, Simon Bernard, Anthony Mwamlima, Christian Simkoko.

Wednesday, December 16, 2015

YANGA YAREJEA KILELENI LIGI KUU


Na Mohammed Slim, TANGA
YANGA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo.
Shukrani kwake, kiungo wa kimataifa wa Zimbabwe, Thabani Scara Kamusoko aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 90 na ushei na kuwarejesha wana Jangwani hao kileleni.
Kamusoko alifunga bao hilo kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya kichwa ya Mzimbabwe mwenzake, Donald Dombo Ngoma ambaye naye alipokea krosi ya winga Godfrey Mwashiuya.
Na kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 27, baada ya kucheza mechi 11, ikiizidi pointi moja Azam FC yenye mechi moja mkononi, ambayo sasa inashukia nafasi ya pili.
Mchezo wa leo ulikuwa mgumu haswa kwa Yanga SC na ilibaki kidogo tu itoe sare ya pili mfululizo Uwanja wa Mkwakwani, baada ya Jumamosi kulazimishwa sare ya 0-0 na Mgambo JKT
Ni mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm yaliyoisaidia Yanga SC kuongeza kasi ya mashambulizi hadi kupata bao.
Pluijm anayesaidiwa na mzalendo, Juma Mwambusi aliwatoa washambuliaji Mrundi Amissi Tambwe na Deus Kaseke dakika za mwishonin na kuwaingiza Malimi Busungu na Mwashiuya waliokwenda kuipasua ngome ya Sports.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Malimi Busungu, Donald Ngoma na Deus Kaseke/ Godfrey Mwashiuya.
African Sports; Ramadhani Mwaluko, Mwaita Ngereza, Khalfan Twenye, Juma Shemvuni, Rahim Juma, Mussa Chambega/Ally Ramadhani ‘Kagawa’,
Mussa Kizenga/James Mendi, Pera Ramadhani, Hassan Materema, Mohammed Mtindi/Hussein Issa na Mohamed Issa.

IMETOLEWA BLOGU YA BINZUBEIRY

MKUTANO MKUU TFF WAAHIRISHWA


Mkutano Mkuu wa kawaida wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) uliokuwa ufanyike Tanga ikiwamo shughuli ya uwekaji jiwe la msingi kwenye kiwanja cha TFF jijini Tanga sasa umeahirishwa kwa muda usiojulikana.

Mwishoni mwa mwezi Novemba 2015, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) mkoa wa wa Ilala ulitoa agizo la kufungwa na kuchukuliwa fedha kutoka kwenye akaunti za Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) ili kulipa fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.6, sehemu kubwa ikiwa ni malipo ya kutoka kwenye mishahara (PAYE) ya makoch Jan Poulsen, Kim Poulsen, na Jacob Michelsen na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mchezo kati ya Tanzania na Brazil mwaka 2010.

Baada ya hatua hiyo TFF iliwasiliana na TRA na kuweka bayana kwamba deni la walimu (makocha) na mchezo dhidi ya Brazil lilistahili kulipwa na serikali na haikuwa sahihi kulielekeza TFF.

Aidha TFF ilieleza athari ambazo zingetokea iwapo amri hiyo (Agent Order) ingetekeleezwa kuwa ni pamoja na kusitishwa kwa ziara ya timu ya vijana chini ya miaka 15 (U15) katika nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, kusimama kwa program za vijana na wanawake, Mkutano Mkuu, Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Kombe la Shirikisho.

Baada ya utekelezaji wa amri hiyo kuanza TFF ilifanya kikao na TRA na makubaliano ya kufungua akaunti yakafanikiwa. Hata hivyo akaunti zilifunguliwa zikiwa hazina fedha kwa kuwa zilishapelekewa Benki Kuu (BOT) na zoezi la madai haliwezi kukamilika kwa muda mfupi.

Baada ya hali hiyo kujitokeza, TFF ilifanya kila linalowezekana kuhakikisha Mkutano Mkuu unafanyika ikiwa ni pamoja na kutafuta ufadhili toka kwa  wadau wake, lakini zoezi hilo limeshindikana katika muda mfupi uliopo na hivyo Shirikisho  limeamua kuahirisha Mkutano Mkuu 2015 mpaka hapo hali itakaporuhusu.

MWESIGWA AFUNGUA KOZI YA MAKOCHA WA AWALI


Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Mwesigwa Selestine leo amefungua kozi ya waalimu wa mpira wa miguu ngazi ya chini (Grassroots) inayofayika katika ukumbi wa TFF uliopo Karume jijini Dar es slaam.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo ya siku tano, Mwesigwa amewaomba washiriki kuitumia vizuri nafasi hiyo waliyoipata kwa kwenda kuwafundisha na kuupenda mpira wa miguu watoto wadogo wenye umri kati ya miaka 6-12.

Mwesigwa amewaomba walimu hao kutoka shule za msingi za mikoa ya Dar es salaam, Mtwara, Lindi na Ruvuma kusaidia katika kukuza mpira wa miguu ambao chimbuko lake ni watoto wadogo kuupenda na kuucheza mpira huo.

Jumla ya washiriki 30 kutoka mikoa minne wanashiriki kozi hiyo, inayoendeshwa na mkufunzi wa FIFA kutoka nchini Mauritius, Govinden Thondoo ambaye ametoa pongezi kwa TFF kwa kuwa na maendeleo mazuri katika kozi ya Grassoot kulinganisha na nchi nyingine zilizopo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati wneye jumla ya nchi 15.

Jumla ya walimu 106 kutoka katika shule za msingi za mikoa mbalimbali nchini Tanzania zina makocha waliopata kozi za Grassoort katika kipindi cha miaka 2, na lengo likiwa ni kufikisha walimu 25,000.

TFF YAZITAKA KLABU KUHESHIMU KANUNI ZA USAJILI
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limevitaka vilabu vyote nchini vya Ligi Kuu (Vodacom), Ligi Daraja la Kwanza (StarTimes), na Ligi Daraja la Pili (SDL) kuheshimu utaratibu uliowekwa wa usajili na utekelezaji wake, kwani TFF haitapendelea klabu yoyote katika suala hilo.

TFF inachukua fursa hii kuwakumbusha viongozi wote wa vilabu kuhusu kalenda ya mwaka ya usajili ambayo ina vipindi viwili,

(i)  Dirisha Kubwa la Usajili  (Juni 15 – Agosti 20)

(ii)  Dirisha Dogo la Usajili (Novemba 15 – Disemba 15)

Baada ya usajili hufuatia kipindi cha pingamizi ambacho kuchukua wiki moja, kisha Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya TFF kupitia mapingamizi hayo na kupitisha usajili wa wachezaji wote waliosajiliwa.

Kipindi cha usajili wa dirisha dogo ulifunguliwa Novemba 15 na utafungwa kesho Disemba 15, kipindi hichi hutumika kwa ajili ya uhamisho, kutangaza wachezaji wanaoachwa kwa mujibu wa kanuni, kutangaza wachezaji waliositishiwa mikataba, na kipindi cha pingamizi Disemba 16 – 22, na kuthibitisha usajili Disemba 23, mwaka huu.

TFF inaviomba vilabu kufuata utaratibu uliopo kikanuni katika shughuli za uendeshaji wa mpira wa miguu nchini.

Saturday, December 12, 2015

MIAKA MITATU YA KIFO CHA REMMY ONGARA: BADO TUNAKUKUMBUKANa: Kiyungi Moshy:

SIKU kama ya leo, Desemba 13, 2012, ilikuwa ni siku ya majonzi kwa wapenzi wa muziki wa dansi hapa Tanzania, Afrika ya Mashariki na ulimwenguni kwa ujumla. Siku hiyo ilikuwa ni miaka miwili kamili toka kifo cha mwanamuziki nguli Ramadhan Mtoro Ongala ‘Dk. Remmy’ aliyefariki usiku wa kuamkia Jumatatu Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza, jijini Dar es Salaam.

Alikuwa kipenzi cha watu aliyewaacha wapenzi wake na wananchi kwa ujumla katika dimbwi la majonzi yasiyosahaulika kufuatia tungo za nyimbo zake zenye maudhui maridhawa, ambazo hadi leo zinarindima katika vituo vingi vya redio hapa nchini hata nje ya mipaka yetu.

Dk. Remmy alikuwa wa kwanza kupata ujasiri wa kukemea ngono zembe, akatunga wimbo ‘Mambo kwa soksi’ Lakini jamii ikambeza kwamba wimbo huo haukuwa na maadili mema. Baadaye  viongozi wa serikali,vyama na dini na wengine kwa ujumla walielewa nini alichokuwa akisema Dk. Remmy, wakaanza kuhubiri majukwaani  tahadhari hiyo.

Alizaliwa akiwa na meno mawili ya mbele kinywani mwake  na akaonekana kana kwamba ni  mtoto wa ajabu. Aidha hakuwahi kunyolewa nywele zake kwa miaka yote hadi alipokuja kuokoka akiwa hapa nchini Tanzania.

Dk. Remmy alijipatia umaarufu katika jiji la Dar es Salaam hususan maeneo ya Sinza. Alikuwa na gari yake ndogo ‘soloon’ lililokuwa la aina yake popote lipitapo watu walilishangaa. Lilikiwa na maandishi nyuma ya gari hilo yakisema ‘ Baba yako analo’?

Historia ya maisha ya Dk.Remmy Ongala yaelezwa kwamba mara Dk. Remmy Ongala alipozaliwa, wazazi  wake walimuita Ramadhani Mtoro Ongala. Alizaliwa mwaka 1947 katika mkoa wa Kivu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Familia yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu eneo ambalo halikuwa mbali sana kutoka mpakani na Tanzania.
Baba yake alikuwa ni mwanamuziki mashuhuri pia alikuwa mpiga ngoma kwa kutumia mkono na pia mbira. Baada ya kuzaliwa kwake haikuchukua muda mrefu familia yake ilihamia katika mji wa Kisangani huko DRC.

Ipo habari kwamba kabla ya kuzaliwa kwake, mama yake alipata ujauzito mara mbili lakini kwa bahati mbaya kila alipojifungua, mtoto alifariki. Alipopata ujauzito mara ya tatu alienda kwa mganga wa kienyeji kumuomba ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa asiiage dunia pia.

Bila kusita mganga wa kienyeji akampa ushauri wake. Akamwambia kwanza safari hii asiende kujifungulia hospitali bali akajifungulie maporini. Pia alipewa ushauri kwamba mtoto akishazaliwa asije akamkata nywele zake. Yote hayo yalitendeka na ndio kisa cha Dk. Remmy Ongala kutokata nywele hadi alipozidiwa na maradhi yaliyompelekea kuokoka ndipo aliponyoa nywele zake akiwa hapa nchini Tanzania.

Mwenyewe aliwahi kusema kwamba mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kwa kuwa na nywele ndefu namna ile. Lakini baadaye jina na taswira ya mfalme wa reggae ulimwenguni, hayati Bob Marley ilipopata umaarufu nchini Congo, ndipo alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza kuikubali na kuionea ufahari.

Pia inasemekana Remmy alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele kitu ambacho kilichukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji. Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana huo ndio mwanzo wa yeye kujulikana hapo baadaye kama Doctor Remmy Ongalla.

Baba yake ndiye aliyeanza kumfunza mambo ya muziki tangia akiwa mdogo kabisa. Jambo lililomfanya aamini kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine wamezaliwa kuwa madaktari, wanasheria, waalimu, wakulima nk, yeye alizaliwa ili awe mwanamuziki.

Kwa bahati mbaya baba yake huyo mwaka 1953 alifariki dunia na kumuacha Remmy akiwa na miaka sita, akiwa tayari ameshaanza shule. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake hakuweza kuendelea kumlipia karo za shule, Remmy ilibidi aache shule.

Ilipofika miaka ya 1960, Remmy tayari alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa.
Mwaka mmoja baada ya kifo cha Baba yake mzazi, mwaka uliofuatia wa 1964 ulikuwa si mzuri kwa Remmy kwani mama yake mzazi naye alifariki dunia jambo ambalo lilimuacha Remmy na mzigo wa kuwalea wadogo zake kwani yeye sasa ndio alikuwa mkuu wa familia licha ya umri wake mdogo.

Bila elimu na ujuzi mwingine wowote, alilazimika kuanza rasmi kujitafutia riziki kupitia muziki. Ujuzi wake wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya ajabu kitu ambacho kilimuwezesha kutumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa katika hoteli nyingi na  sehemu mbalimbali nchini ya Congo akiwa na bendi yake iliyokuwa imesheheni vijana wenzake iliyoitwa ‘Bantu Success’.

Kwa miongo kadhaa iliyofuatia Dk. Remmy Ongala alizunguka katika sehemu mbalimbali za Congo akiambatana na bendi kadhaa maarufu za wakati huo nchini Congo zikiwemo Success Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz nchini Uganda.

Japokuwa kwa ujumla Dk. Remmy alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, lakini aliwahi kukiri kwamba muziki wa kutoka nchini Cuba ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia umaarufu barani Afrika, ulimsaidia katika kupata staili ya pekee katika upigaji gitaa.

Kwa upande wa uimbaji anasema uimbaji wa Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ na ule  wa Franco Lwambo Makiadi ulimsaidia kupata staili yake ya uimbaji kama tulivyoizoea kusikia enzi za uhai wake.

Mwaka 1978 Remmy aliingia jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na mjomba wake mzee Kitenzogu Makassy  ili aje ajiunge na bendi maarufu ya wakati huo ya Orchestra Makassy, iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba wake huyo.

Huo ukawa ndiyo mwanzo wa maisha ya Dk. Remmy nchini Tanzania. Akiwa na bendi ya Orchestra Makassy, alitunga wimbo wake wa kwanza uliojulikana kama ‘Siku ya Kufa’, wimbo ambao aliuandika kumkumbuka rafiki yake aliyefariki. Wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu mkubwa na kujulikana kwa haraka hapa nchini.

Mzee Makassy  aliamua kuihamishia bendi yake keipeleka nchini Kenya, kitendo hicho cha mjomba wake kilichomfanya Dk. Remmy  kujiunga na bendi ya  Matimila baada ya kudumu kwa katika bendi ya Orchestra Makassy kwa takriban miaka mitatu hivi.

Jina la bendi hiyo ya  Matimila lilitokana na jina la kijiji kimoja kilichoko kusini mwa Tanzania. Kujiunga kwa  Remmy katika  bendi ya Matimila, alijiongezea umaarufu katika anga za muziki nchini Tanzania wakati huo. Chini ya uongozi wake Dk. Remmy aliisuka upya bendi hiyo na kuibadilisha  jina ikaitwa Orchestra  Super Matimila.

Miaka iliyofuatia Watanzania tulishuhudia umaarufu wa Remmy ukiongezeka hususan kutokana na mashairi ya nyimbo zake ambayo yaliegemea katika kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, afya, siasa , majanga ya Ukimwi nk.

Mafanikio ya Remmy na kundi lake zima la Orchestra Super Matimila hayakuishia nchini Tanzania kwani katika miaka ya mwishoni ya 1980 walianza kujipatia umaarufu nje ya mipaka ya Tanzania na Afrika.

Dk.Remmy Ongala aliwahi kusema kwamba kupata mialiko ya nje lilikuja kama mchezo tu. Kasseti yenye nyimbo zao rafiki yake mmoja mzungu aliyekuwa akiondoka nchini Tanzania kurejea kwao Uingereza.

Rafiki yake huyo alipofika huko aliwapatia jamaa wa WOMAD (World of Music, Arts and Dance) shirika linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za dunia ya tatu. WOMAD  walivutiwa na nyimbo zao, hivyo kuwapa mwaliko kushiriki katika maonyesho yao barani Ulaya ya mwaka 1988.

Baada ya kurudi kutoka Ulaya bendi ya Super Matimila ilitoa album yenye jina la ‘Nalilia Mwana’ ikiwa na  mkusanyiko wa nyimbo zao zilikuwemo nyimbo zilizopendwa sana kama vile ‘Ndumila Kuwili’ na ‘Mnyonge Hana Haki’

Mwaka 1989 Remmy na Matimila walirudi tena Ulaya kufuatia mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo huo ambapo walipata nafasi ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ya Stud Real World Studios,
ambayo ilikuwa inamilikiwa na mwanamuziki maarufu aitwaye Peter Gabriel.

Dk. Remmy aliwahi kufafanua kuwa wimbo maarufu ya ‘Kipenda roho’ aliuimba mahsusi kwa ajili ya mkewe ambaye ni ‘mzungu’ muingereza ambaye wakati huo tayari walikuwa wameshazaa naye watoto watatu.

Mwaka 1990, Remmy na bendi yake ya Super Matimila walirejea tena katika studio za Real World ambako walirekodi album nyingine yenye nembo ya ‘Mambo’  ambayo ilikuwa na nyimbo kama hiyo ya ‘Mambo’ ambayo aliimba kwa lugha ya kiingereza na kuweza kukidhi kiu ya wapenzi wake wasiojua Kiswahili. Zingine ni pamoja na ‘No money, no life’ na ‘One World’.

Umaarufu wake ulizidi kung’ara mwaka 1990 alipotoa wimbo wa ‘Mambo kwa soksi’ ingawa baadhi ya watu waliupinga kwa kusema kwamba haukuwa na maadili mema kwa jamii, ingawa kimsingi alikuwa anawaasa watu hususani vijana kutumia kondomu ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.

Akiwa Super Matimila Dk. Remmy alitoka na nyimbo ningi zikiwemo za ‘Bibi wa mwenziyo’, ‘Kipenda roho’, ‘Asili ya muziki’ na ‘Ngalula’. Zingine  ni pamoja na ‘Mwanza’, ‘Mama nalia’, ‘Harusi’, ‘Hamisa’, ‘Mnyonge hana haki’, ‘Ndumila kuwili’ na ‘Mataka yote’ ambazo  zilimuongezea sifa kubwa Dk. Remmy kufuatia maudhui yaliyokuwa yakikidhi jamii.

Baadaye Dk. Remmy Ongala akaanza kusumbuliwa na maradhi ya kisukari iliyompelekea kuamua kuachana na muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya kishetani.
Remmy akaokoka, akatubudu dhambi zake na akaanza kupiga muziki akimuimbia bwana.
Kabla ya kifo chake Dk. Remmy alitoa albamu yake ya Injili aliyooiita ‘Kwa Yesu kuna furaha’. Remmy alikuwa katika hatua  za mwisho za kukamilisha albamu yake ya pili, lakini mungu akampenda sana usiku wa kuamkia Jumatatu ya Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza. Eneo hilo alilokuwa akiishi lilipewa jina la ‘Sinza kwa Remmy’ kufuatia umaarufu wake alipokuwa hai.

Mungu aiweke roho yake pahala pema peponi, Amina.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA MOSHI KIYUNGI

SIMBA, AZAM ZASHINDWA KUTAMBIANA; YANGA YABANWA MBAVU NA MGAMBO JKT


Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
AZAM FC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo, yanaifanya kila timu ijiongezee pointi moja, Azam FC ikifikisha 26 na Simba SC ikitimiza 22 baada ya timu zote kucheza mechi 10.
Azam FC inaendelea kuwa kileleni baada ya Yanga SC nayo kulazimishwa sare ya 0-0 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo hivyo kufikisha pointi 24, wakati Simba SC ikibaki nafasi ya nne.
Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, Azam FC wakitangulia kupitia kwa Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ kabla ya Simba SC kusawazisha kupitia kwa Ibrahim Salum Hajib ‘Kadabra’
Bocco alifunga dakika ya kwanza baada ya kumzidi maarifa kipa wa Simba SC, Vincent Angban raia wa Ivory Coast kufuatia krosi ya winga Farid Mussa Malik, aliyempokonya mpira beki Mrundi, Emery Nimubona.
Azam FC iliweka kambi kwenye eneo la Simba SC kwa takriban dakika tano mfululizo baada ya bao hilo, lakini safu ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi ilihimili vishindo vyote bila kurusu mabao zaidi.
Hajib aliisawazishia Simba SC dakika ya 25 baada ya kumtoka beki Said Mourad na kumchambua vizuri kipa Aishi Manula, kufuatia pasi maridadi ya kiungo Said Ndemla.
Azam FC walionekana ‘kuchanganyikiwa’ baada ya bao hilo na kuruhusu mashambulizi zaidi ya Simba SC langoni mwao, lakini sifa zimuendee kipa Manula aliyeokoa takriban michomo miwili ya hatari, mmoja wa Danny Lyanga na mwingine wa Hajib.
Kipindi cha pili, timu zote zilirudi kwa tahadhari kuhofia kuwapa wapinzani nafasi ya kuongeza bao.
Hata hivyo, nyota ya Hajib iliendelea kung’ara uwanjani baada ya kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 68 kwa shuti kali baada ya kumtoka Mourad tena.
Bao hilo halikudumu sana, kwani Bocco tena aliifungia Azam FC bao la kusawazisha dakika ya 73 baada ya kuwatoka mabeki wa Simba SC.
Baada ya hapo, timu hizo zilirudi kucheza kwa kujihami zaidi licha ya mabadiliko yaliyofanywa na makocha wote, Waingereza, Stwart Hall wa Azam na Dylan Kerr wa Simba SC.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Said Mourad, Erasto Nyoni, Serge Wawa, Himid Mao/Kipre Balou dk46, Abubakar Salum/Didier Kavumbangu dk71, Jean Baptiste Mugiraneza, John Bocco, Kipre Tchetche/Mudathir Yahya dk81 na Farid Mussa.
Simba SC; Vincent Angban, Emery Nimubona/Kessy dk84, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murushid, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Said Ndemla, Jonas Mkude, Danny Lyanga/Kizza dk68, Ibrahim Hajib na Abdi Banda/Mwalyanzi dk81.
Wakati huo huo, Yanga imeshindwa kutwaa uongozi wa ligi hiyo baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Mgambo JKT katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY

MKUTANO MKUU WA BODI YA LIGI LEO


Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) itafanya Mkutano wake wa Pili wa Baraza Kuu (Governing Council) jijini Dar es Salaam, leo Jumapili, Desemba 13 mwaka huu.

Mkutano huo utahudhuriwa na Marais/Wenyeviti wa klabu zote 40, ambapo 16 ni za Ligi Kuu ya Vodacom na nyingine 24 za Ligi Daraja la Kwanza ya Startimes na kutoa mwelekeo wa Bodi kwa kipindi cha miezi 12 ijayo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel ndiye anayetarajiwa kufungua Mkutano huo utakaofanyika kuanzia saa 10 kamili asubuhi kwenye ukumbi wa Mikutano wa Uwanja wa Taifa.

MALINZI AMPONGEZA NAPE


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za pongezi mbunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye kufutia kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo katika serikali ya awamu ya tano.

Katika salamu zake, Malinzi amempongeza Nape na kusema TFF ina imani nae katika nafasi hiyo, na kuahidi kushirikiana katika michezo na haswa katika kusukuma gurudumu la maendeleoya mpira wa miguu nchini.

Aidha pia Malinzi amewapongeza Paschal Kihanga, Mwenyekiti wa chama cha soka moa Morogoro kwa kuchaguliwa kuwa Meya wa manispaa hiyo, na James Bwire mmiliki wa shule ya Alliance kwa kuchaguliwa meya wa manispaa ya Nyamgana.

Malinzi amewatakia kila la kheri katika nafasi hizo walizozipata za kuwatumikia watanzania, na kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini anawatakia kila la kheri na kuahidi kushirikiana nao.

Tuesday, December 8, 2015

KIKOSI CHA U 15 CHAREJEA DAR


Ziara ya timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U15) iliyoanzia kanda ya ziwa na kanda ya Magharibi kisha kuendelea katika nchi za Rwanda, Uganda na Kenya mwezi huu imesitishwa kutokana na kufungwa akaunti za Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Timu hiyo ya vijana iliondoka wiki iliyopita kuelekea jijin Mwanza, ambapo iliagwa na kukabidhiwa bendera ya Taifa na katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel, ilicheza mchezo mmoja wa kirafiki na timu ya Alliance kabla ya kuelekea mkoani Kigoma.

Ikiwa Kigoma U-15 ilicheza michezo miwili ya kirafiki na timu ya kombaini ya mkoa wa Kigoma U-15, jumapili ikacheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya Burundi U-17, na jana asubuhi kuanza safari ya kurejea jijini Dar essalaam.

Awali ziara ya timu hiyo ya U-15 ilikua iendelee katika mji wa Kigali kwa kucheza na U17 ya Rwanda, Kampala kucheza na Uganda U17, jijini Nairobi kwa kucheza na U17 ya Kenya na kumaliza ziara hiyo kwa kuchez ana U15 kombaini ya mkoa wa Arusha Disemba 23, na kurejea jijin Dar es salaam Disemba 24, 2015.

U-15 inajiandaa na michuano ya Viajana U17 kuwania kufuzu kwa Mataifa ya Afrika mwaka 2017 nchini Madagascar itakayoanza kutimua vumbi Juni 2016.

TFF YATUMA SALAMU KIFO CHA WILLIE CHIWANGO


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehem Willie Chiwango aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki na mazishi kufanyika eneo la Buguruni jijini Dar e salaam.

Katika salam zake, TFF inawapa pole familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na kusema kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini, wako pamoja katika kipindi hiki cha maombolezo.

Marehemu Willie Chiwango ni miongoni mwa waandishi wa habari wa michezo wakongwe kabisa, aliambatana na timu ya taifa ‘Taifa Stars’ iliyoshiriki michuano ya Mataifa Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria.

TFF ilimpa cheti cha heshima marehemu Chiwango katika zoezi la kuwakumbuka na kutambua mchango wa viongozi, wachezaji, waandishi wa habari za michezo waliojitoa katika sekta ya mpira wa miguu nchini.

Monday, December 7, 2015

KOMBE LA SHIRIKISHO KUENDELEA DESEMBA 15

Michezo ya Kombe la Shirikisho nchini (Azam Sports Federation Cup) mzunguko wa pili unatarajiwa kuendelea kuanzia Disemba 15 mwaka huu, ambapo jumla ya timu 32 zitachuana kusaka nafasi ya kuingia mzunguko wa tatu wa kombe hilo.

Mzunguko wa kwanza uliochezwa mwezi Novemba, jumla ya timu 32 zilichuana kutoka Ligi Daraja la Pili, na timu 16 kusonga mbele hatua ya pili inayozikutanisha timu za Ligi Daraja la Kwanza (StarTimes League) 16 na kufanya idadi ya timu 32 zinazosaka kufuzu kwa hatua ya mzunguko wa tatu.

Timu zilizofuzu kwa mzunguko wa pili kutoka mzunguko wa awali ni Abajalo FC, Mshikamano FC, Green Warriors, Villa Squad (Dar), Mvuvuma FC (Kigoma), Madini FC (Arusha), Sabasaba FC (Morogoro), Alliance, Pamba FC (Mwanza), Mighty Elephant (Songea), Kariakoo FC (Lindi), Wenda (Mbeya), Singida United (Singida).

Timu za Daraja la Kwanza zinaoanza kucheza mzunguko wa pili ni Polisi Tabora, Rhino Rangers, Burkinafaso, Friends Rangers, KMC, African Lyon, Ashanti United, JKT Oljoro, Panone FC, Kiluvya United, Lipuli FC, Kurugenzi, Mbao FC, Geita Gold, JKT Mlale, Njombe Mji, Kimondo, Mji Mkuu na JKT Kanembwa.

Friday, December 4, 2015

TRA YAFUNGA AKAUNTI ZOTE ZA TFF


Juma lililopita Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliaga timu ya Taifa ya Vijana Chini ya umri wa miaka 15 (U15) ikianza ziara yake ya Afrika Mashariki kuanzia kucheza na Burundi mjini Kigoma na baadaye Kigali, Rwanda, Kampala, Uganda na mwisho Nairobi Kenya.

Bahati mbaya ziara hiyo itaishia Mwanza na Kigoma kufuatia Mamlaka ya Kodi ya Mapato (TRA) mkoa wa Ilala kuzuia fedha kwenye akaunti zote za Shirikisho kwa madai ya kulipwa kiasi cha Shilingi 1,637,334,000 (bilioni 1.6 tshs) ikiwa ni kodi kwa kipindi cha 2010 – 2013 sehemu kubwa ikiwa ni makato kwenye mishahara (PAYE) ya walimu wa kigeni, Jan Poulsen, Kim Poulsen na Jacob Michelsen na vilevile kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mchezo wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Brazili uliofanyika mwaka 2010.

Walimu wa Timu za Taifa wamekuwa wakilipiwa mishahara na Serikali na hivyo TFF haikuwajibika kuwakata kodi. Aidha, mchezo kati ya Tanzania na Brazil ulisimamiwa na kamati maalum ya Serikali na fedha zake hazikuingizwa katika akaunti za TFF.

Kutokana na hatua hii ya TRA shughuli nyingine za mpira zitakazohathirika nazo ni:

1. Kulipia madeni ya usafiri, chakula na posho za Timu za Taifa zilizoshiriki mtoano wa kombe la Dunia na mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Challenge Cup)

2. Program za mpira wa Wanawake na vijana zitalazimika kusimama.

3. Mashindano ya kombe la Shirikisho raundi ya pili iko kwenye hatihati kwani hakuna fedha za kugharimia michezo hiyo.

4. Mashindano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoendelea yatalazimika kusimama vilevile. Mashindano haya TFF imekuwa ikiyaendesha bila mdhamini.

5. Vifaa vya michezo (Mipira) kwa ajili ya shule za msingi na vituo vya maendeleo (Regional Football Development Centres) vinatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote na TFF haitakuwa na uwezo wa kulipia usafirishaji na ushuru wake.

6. Malipo ya gharama za kambi na karo kwa ajili ya vijana wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 13 walioko shule ya Alliance Academy ya jijini Mwanza.

7. Huduma za kiutawala ikiwa ni pamoja na utunzaji viwanja na majengo, maji, umeme, ulinzi pamoja na mishahara na stahiki nyingine za wafanyakazi

8. Mwelekeo na mwitikio mzuri wa wadhamini uko kwenye hatari ya kupotea pindi mashindano na shughuli wanazozidhamini zitakapofubaa au kusimama kabisa.

9. Mkutano Mkuu wa kawaida wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) wa Mwaka 2015 uliopangwa kufanyika Tanga 19-20 Desemba 2015 sasa una hatihati ya kuweza kufanyika.

Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu wa ulipaji kodi na wajibu wa Mamlaka ya Mapato katika kuhakikisha kodi inakusanywa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Taifa,TFF ipo katika mawasiliano na TRA katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala hili ikiwa ni pamoja na kupitia upya mahesabu ili kujua wajibu halisi (net liability) wa TFF na namna ya kulipa au kulipwa kutegemea ulali wa mahesabu.

Hii si mara ya kwanza hili kujitokeza, lilijitokeza Oktoba 2012 na shilingi 157,407,968 iliyokuwa mgawo wa vilabu kuchukuliwa na TRA. Kufuatia tukio hilo, yalifanyika mazungumzo kati ya TFF na serikali ambamo ilikubaliwa kwamba fedha hizo zitarudishwa TFF na mpaka sasa TFF inafuatilia fedha hizo.

Kwa taarifa hii TFF inaomba utulivu kwa wanamichezo wote pamoja na ushirikiano wa karibu kutoka katika vyombo vyote husika ikiwemo TRA na wadau wengine ili jambo hili lipate ufumbuzi wa kudumu utakaoleta tija kwa serikali ya awamu ya tano ikiwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika maendeleo ya mpira wa miguu na michezo kwa ujumla wake.

MKUTANO MKUU TPLB DESEMBA 13


Mkutano Mkuu wa Pili wa Kawaida wa Baraza Kuu (Ordinary Governing Council) la Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) utafanyika Jumapili, Desemba 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mkutano wa Kawaida ambao wajumbe wake ni klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza utafanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Uwanja wa Taifa kuanzia saa 4 kamili asubuhi.

Ajenda za Mkutano huo ni Kufungua mkutano, Kuhakiki akidi, Kuthibitisha ajenda, Kuthibitisha Muhtasari wa Mkutano uliopita, Yatokanayo na Mkutano uliopita, Hotuba ya Mwenyekiti, Kupokea Taarifa za Utekelezaji kutoka kwa Wanachama, Kuthibitisha Taarifa ya Utekelezaji ya Kamati ya Uongozi, Kuthibitisha Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu, na Kupitisha Bajeti ya 2016.

Mkutano huo utakuwa chini ya Mwenyekiti wake Hamad Yahya Juma

LIGI DARAJA LA PILI KUENDELEA WIKIENDI HII


Ligi Daraja la Pili (SDL) inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa timu 24 za makundi A, B, C na D kucheza katika viwanja 12 mbalimbali nchini, kusaka nafasi nne za kupanda Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao (StarTime First League).

Kesho Jumamosi Kundi A, Singida United watakua wenyeji wa Mvuvuma FC katika uwanja wa Namfua mkoani Singida, Green Warriors watacheza dhidi ya Mirambo FC uwanja wa Mabatini Mlandizi - Pwani, huku maafande wa Trasnit Camp wakiwakaribisha Abajalo FC ya Tabora katika uwanja Kambarage Shinyanga.

Kundi B, jijini Mwanza timu ya Alliance FC itawakaribisha ndugu zao Pamba FC katika uwanja wa CCM Kirumba, Madini FC ya mkoani Arusha ikiwakaribisha Bulyanhulu FC uwanja wa Mbulu, huku AFC wakicheza dhidi ya JKT Rwamkoma katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Kundi C, Abajalo FC ya jijini Dar es salaam watawakaribisha Changanyikeni FC katika uwanja wa Karume, huku kundi D, Mbeya Warriors watakua wenyeji wa Wenda FC uwanja wa Sokoine – Mbeya, Sabasaba FC dhidi ya Mkamba Rangers uwanja wa Jamhuri Morogoro, na The Mighty Elephant watakuwa wakicheza dhidi ya African Wanderes kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Jumapili kutakua na mchezo mmoja kati ya  Vill Squad dhidi ya Karikaoo ya Lindi kwenye uwanja wa Karume, Jumatatu Cosmopolitan FC watawakaribisha Mshikamano FC katika uwanja wa Karume yote ikiwa michezo ya Kundi C.

MKUTANO MKUU WA TFF KUFANYIKA TANGA


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) linatarajia kufanya mkutano wake Mkuu wa Mwaka kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Regal Naivera jijini Tanga ambapo wajumbe wa mkutano huo tayari walishatumiwa taarifa za mkutano.

Akiongea na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa TFF, Kaimu Mkurugenzi wa Sheria na Wachama, Elliud Mvela amesema maandalizi ya mkutano huo yanaendelea vizuri.

Mvella amesema ajenda za mkutano mkuu wa kawaida ni zile zilizopo kikatiba, ila itaongezeka ajenda ya marekebisho ya katiba ambayo ni mapendekezo yaliyotolewa na FIFA.

Agenda za mkutano mkuu ni:

1.Kufungua Mkutano

2. Uhakiki wa Wajumbe

3. Kuthibitisha Ajenda.

4. Kuthibitisha Muhtsari wa Mkutano Mkuu uliopita.

5. Yatokanayo na Mkutano uliopita.

6. Hotuba ya Rais.

7. Ripoti kutoka kwa Wanachama

8. Kuthibitisha ripoti ya utekelezaji wa Kamati ya Utendaji.

 9. Kuthibitisha ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu 2013.

10. Kupitisha bajeti ya 2016

11. Marekebisho ya Katiba

12. Mengineyo

13. Kufunga Mkutano.

Monday, November 30, 2015

KILI STARS YATOLEWA KOMBE LA CHALENJI, YAFUNGWA KWA MATUTA NA WENYEJI ETHIOPIA


Na Mwandishi Wetu, ADDIS ABABA
TANZANIA Bara imetolewa katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 na wenyeji Ethiopia, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
Katika mchezo huo wa Robo Fainali uliofanyika Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa, Tanzania Bara walikuwa wa kwanza kupata kupata bao liliofungwa na Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyemalizia krosi ya Deus Kaseke dakika ya 25.
Ethiopia walisawazisha kwa penalti ya utata iliyofungwa na Nahodha wake, Panom Gathouch baada ya Mohammed Naser kujiangusha wakati akidhibitiwa na Shomary Kapombe dakika ya 57.
Stars walionekana kutaka kupagawa baada ya wapinzani wao kusawazisha bao na kuanza kuwaletea ubabe marefa, lakini baadaye wakatulia na kuendelea kucheza mpira.
Hata hivyo, bado bahati haikuwa yao, kwani baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1, walitolewa kwa matuta.
Beki Shomary Kapombe na kiungo Jonas Mkude walikwenda kupoteza penalti zao, wakati waliofunga kwa upande wa Kilimanjaro Stars ni kiungo Himid Mao, mshambuliaji Bocco na beki Hassan Kessy.
Waliofunga penalti za Ethiopia ni Panon Gathouch, Mohammed Naser, Ashalew Tamene na Behaylu Girima. 
Katika Robo Fainali ya Kwanza, Uganda imeifunga 2-0 Malawi mabao ya Farouk Miya na Ceasar Okhuti na sasa itakutana na Ethiopia katika Nusu Fainali, wakati Kili Stars inarejea nyumbani Dar es Salaam.
Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Said Mohamed, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kevin Yondan, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Simon Msuva, Himid Mao, John Bocco, Said Ndemla na Deus Kaseke.
Ethiopia; Abel Mamo, Yared Bayeh, Aschalew Tamane, Anteneh Tesfaye, Aschalew Girma, Eliyas Mamo, Zekariyas Tuji, Gothuoch Panom, Beneyam Belay, Mohammed Naser na Bereket Yisshak.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY