KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 27, 2015

TANZANIA KUANDAA FAINALI ZA AFRIKA U-17 2019Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika -CAF leo hii limeipa Tanzania uenyeji wa fainali za michuano ya Afrika ya vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.


Uenyeji huu ni hatua muhimu sana kwa Tanzania katika kukuza soka la vijana na kwa hatua hii Tanzania itacheza moja kwa moja fainali hizi.

Katika kuandaa kikosi bora cha kushiriki fainali hizi Tanzania, mwezi Juni mwaka huu TFF itaandaa mashindano ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 13 na wachezaji bora wa mashindano haya wataunda kikosi cha mwanzo cha Taifa kuelekea fainali za mwaka 2019.

TFF inamshukuru sana Rais Jakaya Kikwete na Mh. Fennela Mukangara Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kufanikisha maamuzi haya, na inaamini ushirikiano huu wa Serikali na wadau wengine utafanikisha mashindano haya mwaka 2019.

SAMATTA ANUNUA GARI LA BEI MBAYA


Gari aliloposti Samatta ni Range Rover lenye rangi ya damu ya mzee ambalo lina namba za usajili za Tanzania na linakua gari la pili la thamani ambalo Samatta ameliweka hadharani baada ya mwaka 2013 kulionyesha gari lake aina ya Chrysler Crossfire ambalo lilikuwa na thamani ya takribani millioni 50 za kitanzania.

Tuesday, May 26, 2015

STARS KUINGIA KAMBINI KESHO


Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajiwa kuingia kambini kesho jumatano katika hoteli ya Tansoma iliyopo eneo la Gerezani jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri kuwania kufuzu kwa AFCON.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars Mart Nooij, amewaita wachezaji 16 kuingia kambini kesho siku ya jumatano kwa ajili ya kupimwa afya zao na kujua maandeleo yao kabla ya kuwajumisha katika kikosi cha pamoja kitakachokua kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Misri.

Wachezaji walioitwa kuingia kambini kesho ni, Mohamed Hussein, Peter Manyika, Hassan Isihaka, Jonas Mkude (Simba SC), Salum Telela, Juma Abdul, Nadir Haroub (Yanga SC), Aishi Manula, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Kelvin Friday (Azam FC), Rashid Mandawa, Atupele Green (Kagera Sugar), Haroun Chanongo (Stand United) Malimi Busungu (Mgambo JKT) na Emmanuel Simwanda (African Lyon).

Mara baada ya kurejea kutoka nchini Afrika Kusini, kocha wa Stars Nooij aliwapa mapumziko ya siku 10, wachezaji waliokua kwenye michuano ya Cosafa mpaka Juni Mosi ambapo ndipo watajumuika na wachezaji wengine waliopo kambini.

Ifikapo Juni Mosi, 2015 Taifa Stars itaanza kambi ya moja kwa moja kujiandaa na mechi dhidi ya Misri itakayochezwa jijini Alexandria katika uwanja wa Borg El Arab Juni 14, 2015 ikiwajumuisha pia wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Congo DR.

Kabla ya kuelekea nchini Misri, Taifa Stars inatarajiwa kuweka kambi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kuanzia tarehe 4,Juni 2015 kwa muda wa wiki moja kabla ya kuelekea nchini Misri kwenye mchezo huo dhidi ya Mafarao.

Juni 20, 2015 Taifa Stars itawakaribisha Uganda kwenye uwanja wa Aman mjini Zanzibar katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN, zitakazofanyika nchini Rwanda 2016, na mchezo wa marudiano kufanyika baada ya wiki mbili nchini Uganda.

Monday, May 25, 2015

TFF YAMWEKA KIKAANGONI KOCHA WA STARSKamati ya utendaji ya TFF imesikitishwa na mwenendo mbovu wa Taifa Stars Rais wa TFF, Jamal Malinzi kwa niaba ya kamati ya utendaji amewaomba radhi wapenzi wa mpira kwa matokeo mabaya ya Taifa Stars kwenye michuano ya  Cosafa.

Kikao cha kamati ya utendaji kilipokea taarifa juu ya mwenendo wa timu ya Taifa.

Baada ya majadiliano ya kina, ilikubaliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa, Mart Nooij apewe changamoto maalumu ya kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN na asipofanikisha jambo hilo mkataba wake utasitishwa mara moja.

Maamuzi haya yamezingatia hali halisi ya timu ya Taifa ambayo inakabiliwa na michuano mbalimbali ya kimataifa ndani ya kipindi kifupi.

Aidha katika kuliimarisha benchi la ufundi la timu ya Taifa, Leopald Tasso Mkebezi ameteuliwa kuwa meneja mpya wa timu ya Taifa.

Mkebezi amewahi kuwa meneja wa timu ya Taifa katika kipindi cha mwaka 2006 - 2012.

WAMBURA MKURUGENZI MTENDAJI MPYA WA BODI YA LIGI KUU


Kamati ya Utendaji ya TFF imemteua Boniface Wambura kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Bodi ya Ligi Kuu nchini kuanzia tarehe 01, Juni 2015.

Wambura kabla ya uteuzi huo alikua mkurugenzi wa mashandano  TFF.

TFF inampongeza Wambura kwa uteuzi na inaamini atatoa mchango mzuri katika kukuza na kuzitangaza ligi zetu.

Kamati ya utendaji imemteau Martin Chacha (mratibu wa timu za Taifa) kukaimu nafasi ya mkurugenzi wa mashandano TFF.

TFF YAPITISHA KANUNI ZA KUENDESHA MFUKO WA FDF
Leo jumapili tarehe 24, Mei 2015 Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF imeketi katika ukumbi uliopo makao makuu ya Shirikisho uwanja wa Karume.

Kamati ya Utendaji imepitia masuala mbalimbali na kutoa maamuzi yafuatayo:

CLUB LICENCING (Leseni za vilabu)
Kamati ya Utendaji imeiagiza sekretarieti ivisisitize vilabu vya Ligi Kuu umuhimu wa kukamilisha maombi yao ya ushiriki wa ligi kuu kwa msimu wa 2015/16 kwa kuwasilisha fomu za maombi ya Leseni za vilabu TFF. Klabu ambayo haitakamilisha mchakato huo haitaruhusiwa kushiriki ligi kuu ifikapo msimu wa 2015/16.

KOMPYUTA - Kutokana na maamuzi ya mkutano mkuu wa TFF uliofanyika Morogoro ambao uliagiza wanachama wake wapya wapewe kompyuta, agizo hilo limetekelezwa na kompyuta hizo watakabidhiwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanaotoka kanda hizo ili waziwakilishe maeneo husika. Mikoa hiyo ni Geita, Katavi, Manyara, Njombe na Simiyu.

MFUKO WA FDF - Kufuatia mkutano mkuu wa TFF kuingiza kipengele cha FDF katika katiba yake, kikao cha Kamati ya Utendaji wa mujibu wa katiba kimepitisha kanuni za uendeshaji wa mfuko huo.

Aidha kikao hicho kimeteua wajumbe wafuatao wawe wajumbe wa
tume hiyo

(i)Tido Mhando - Mwenyekiti,
(ii) Deogratius Lyatto - Makamu mwenyekiti
(iii)Ephraim Mafuru - mjumbe, 
(iv)Beatrice Singano - mjumbe,
(v)Joseph Kahama - mjumbe
(vi)Ayoub Chamshana - mjumbe.
Pia Henry Tandau ameteuliwa kuwa katibu mtendaji wa mfuko huo.

Monday, May 18, 2015

TAIFA STARS YAANZA VIBAYA KOMBE LA COSAFA


Simon Msuva wa Tanzania (kushoto) akimtoka Sanele Mkweli wa Swaziland katika mchezo huo

Watanzania waishio miji mbalimbali Afrika Kusini walijitokeza kwa wingi Jumatatu usiku Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace kuishangilia timu yao ya taifa, Taifa Stars ikicheza na Swaziland katika mchezo wa kwanza wa Kundi B Kombe la COSAFA mjini Rusternbug, Afrika Kusini. Bahati mbaya Taifa Stars ilifungwa 1-0.

Na Mahmoud Zubeiry, RUSTENBURG
TANZANIA, imeanza vibaya michuano ya Kombe la COSAFA, baada ya kufungwa bao 1-0 na Swaziland katika mchezo wa kwanza wa Kundi B, usiku huu Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace mjini hapa.

Matokeo hayo yanaiweka Stars inayofundishwa na Mholanzi, Mart Nooij katika mazingira magumu ya kwenda Robo Fainali- baada ya Madagascar kuifunga 2-1 Lesotho katika mchezo wa kwanza.

Stars sasa lazima ishinde mechi zake mbili zijazo dhidi ya Lesotho na Madagascar ili kuangalia uwezekano wa kwenda Robo Fainali.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Nelson Emile Fred wa Shelisheli, aliyesaidiwa na Akhtar Nawaz Rossaye wa Mauritius na Isaskar Boois wa Namibia, hadi mapumziko tayari Swaziland walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.

Bao hilo lilifungwa na Sifiso Mabila kwa shuti kali dakika ya 42 baada ya kutanguliziwa pasi kwenye njia na Xolani Sibandze aliyemtoka Oscar Joshua upande wa kushoto.

Tanzania ilitengeneza nafasi tatu nzuri kipindi cha kwanza, ambazo kwa bahati mbaya mbili Simon Msuva alishindwa kuzitumia na moja John Bocco alipoteza pia.

Kipindi cha pili, Swaziland walitawala zaidi mchezo, lakini safu ya ulinzi ya Stars ilikuwa imara kutoruhusu mabao zaidi.

Nafasi pekee nzuri ambayo Stars walipata kipindi cha pili ilikuwa ni dakika ya 65, baada ya Said Ndemla kupiga juu ya lango akiwa ndani ya boksi kufuatia pasi nzuri ya John Bocco. 

Swaziland waliizidi ufundi uwanjani Stars leo, ambayo haikucheza kwa malengo. Stars haikuwa na madhara kabisa kwenye eneo la hatari la Swaziland.

Tony Tsabedze alitajwa mchezaji bora wa mechi baada ya mchezo huo.

Taifa Stars; Deo Munishi ‘Dida’, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Salum Mbonde, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Mrisho Ngassa/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dk75, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Said Ndemla/Juma Luizio dk65 na Simon Msuva/Ibrahim Hajibu dk82.

Swaziland; Mphikileli Dlamini, Sifiso Mabila, Siyabonga Ndluli, Sanele Mkhweli, Zweli Nxumalo/Mxlosi Lukhele dk67, Mthunzi Mkhontfo, Siboniso Malambe, Machawe Dlamini, Njabulo Ndhlovu/Sifiso Nkambule dk62, Tony Tsabedze na Xolani Sibandze/Sabelo Ndzinisa dk80.

Sunday, May 17, 2015

TAIFA STARS KUWAVAA WASWAZI KESHO


Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mchezo wake wa kwanza  wa kombe la COSAFA siku ya jumatatu dhidi ya Swaziland katika uwanja wa Royal Bafokeng pembeni kidogo ya jiji la Rustenburg kuanzia majira ya saa 1:30 jioni kwa saa za Afrika Kusini.

Awali michezo ya kundi B ilikuwa ifanyike katika uwanja wa Olympia Park, lakini waandaji wa michuano ya COSAFA Castle wamesema kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wao michezo hiyo imeshindikana kufanyika katika uwanja huo.

Uwanja wa Royal Bafokeng ni miongoni mwa viwanja viliyotumika katika Fainali za Kombe la Dunia 2010 chini Afrika kusini, ukiwa na uwezo wa kubeba watazamaji  42,000 huku timu ya Platinum Stars iliyopo Ligi Kuu ikiutumia kama uwanja wake wa nyumbani.

Jana asubuhi Taifa Stars ilifanya mazoezi katika uwanja wa shule ya Rustenburg chini ya kocha mkuu Mart Nooij, na wachezaji wote wapo katika hali nzuri kuelekea katika mchezo huo wa jumatatu.

Leo jioni Taifa Stars ifanya mazoezi saa jioni katika uwanja wa Rolay Bafokeng kwa ajili ya kuuzoea uwanja kabla ya mchezo wenyewe dhidi ya Swaziland.

Akiongelea hali ya hewa, kocha mkuu wa Taifa Stars Mart Nooij amesema vijana wake wanaendelea kuizoea hali ya hewa, japokuwa kuna baridi hakuna mchezaji aliyeshindwa kufanya mazoezi kutokana na hali ya hewa.

MKUTANO MKUU WA WANACHAMA COASTAL UNION LEOMKUTANO Mkuu wa Dharura wa Wanachama wa Klabu ya Coastal Union
unatarajiwa kufanyika leo kwenye ukumbi wa Bwalo la
Polisi Mkoani Tanga.

Sababu za Mkutano huo kufanyika katika Ukumbi la Polisi Mesi ni
kutokana na makao makuu ya klabu ya Coastal Union kuendelea mchakato
wa uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa na upigaji picha wananchi
kwa ajili ya vitambulisho hivyo.

Akizungumza leo,Ofisa Habari wa Coastal Union,Oscar Assenga  alisema
maandalizi ya mkutano huo yanaendelea vizuri na unafanyika kufuatia
vikao vya maridhiano ya Uhakikiwa wanachama wa Klabu ya Coastal Union
ulioongozwa na Mjumbe wa Kamati
ya Utendaji ya Shirikisho la soka nchini (TFF) Ahmed Iddi Mgoyi.

Ambapo alisema  baada ya kumalizika vikao hivyo,Katibu Mkuu wa TFF,
Mwesigwa Selestine aliiandikia barua Klabu ya Coastal Union akiiagiza
klabu hiyo kuitisha mkutano mkuu wa dharura wa wanachama tarehe 17 Mei
mwaka 2015.

Alisema kuwa matokeo  ya maamuzi haya yamepatikana baada ya kikao cha
usuluhishi cha amani kilichoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
TFF, Ahmed Iddi Mgoi aliyekuwa ameongozana na Makamu Mkurugenzi wa
Sheria na Uanachama shirikisho la soka nchini (TFF) Eliud Peter Mvella
kilichofanyika April 13 mjini hapa.

Aidha alisema kuwa tayari shirikisho la soka nchini (TFF) ilishatuma
orodha tatu za majina Wanachama stahiki,Wanachama waliobainika kuwa
wanadosari na inabidi wathibitishwe na wanachama stahiki.

Orodha nyengine ni waombaji wapya wa  wa uanachama watakaohakikiwa na
wanachama stahiki ambapo utaratibu huo ndio ulioagizwa kutumika .

Hata hivyo alisema kuwa orodha zote zimekwisha kubandikwa kwenye ubao wa
Matangazo wa Klabu ya Coastal Union tayari kwa ajili ya mkutano huo wa
kesho(leo)

Wednesday, May 13, 2015

NGASA AMWAGA WINO FREE STATE STARS YA AFRIKA KUSINI

Na Mahmoud Zubeiry, BETHELEHEM
KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa amesaini Mkataba wa miaka minne kujiunga na klabu ya Free State Stars ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini leo.
Ngassa, mume wa Radhia na baba wa Farida (8) na Faria (6) aliwasili jana jioni mjini hapa na leo asubuhi baada ya kukamilisha mazungumzo, akasaini Mkataba huo mnono.
“Nimefurahi kusaini timu hii, ambayo kaka yangu Nteze John amewahi kuchezea pamoja na wachezaji wengine wakubwa kama Tshabalala na Mweene,”alisema Ngassa.
“Sasa najiandaa kwa maisha mapya baada ya kucheza Tanzania kwa muda mrefu, hii ni changamoto mpya kwangu, mpira wa Afrika Kusini upo juu sana ukilinganisha na pale kwetu (Tanzania). Nataka kutumia fursa hii kuitangaza soka ya Tanzania, ili klabu zisijifikirie tena kusajili wachezaji wa Tanzania,”amesema Ngassa.

 Kocha Kinnah Phiri (kushoto) akimkabidhi Ngassa jezi ya Free State Stars leo, makao makuu ya klabu hiyo, Mtaa wa 22B President Boshoff mjini Bathlehem baada ya kusaini Mkataba wa miaka minne kuichezea timu hiyo

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa timu hiyo maarufu kama Ea Lla Koto, Mmalawi Kinnah Phiri amesema kwamba amekuwa akimpenda Ngassa kwa muda mrefu na kukutana naye FS ni kutimia kwa ndoto zake za kufanya kazi na kijana huyo siku moja.
Katika Mkataba huo ambao Ngassa, mtoto wa kiungo wa zamani wa Simba SC, Khalfan Ngassa atakuwa analipwa karibu mara tatu ya mshahara aliokuwa anapata Yanga SC, atapatiwa nyumba ya kuishi na familia yake, gari na huduma nyingine muhimu, ikiwemo bima.
Ngassa anakuwa Mtanzania wa pili kuichezea Free State, baada ya Nteze John Lungu ‘mwana Mwanza’ pia aliyeichezea timu hiyo enzi hizo inaitwa Qwa Qwa Stars mwaka 1997 hadi 1999.  
Ngassa anatua Free States akitokea Yanga SC, ambayo ameichezea jumla ya mechi 186 katika awamu mbili, na kuifungia jumla ya mabao 86.
Ngassa aliyetimiza miaka 26, Aprili 12 mwaka huu, alijiunga na Yanga SC kwa mara ya kwanza mwaka 2006, akitokea Kagera Sugar iliyomuibua mwaka 2005 kutoka timu ya vijana ya Toto Africans ya Mwanza.
Mwaka 2010 alihamia Azam FC kwa dau la rekodi wakati huo, dola za Kimarekani 40,000 (Sh. Milioni 80).
Kabla ya hapo, akiwa Yanga SC, Aprili mwaka 2009, Ngassa alikwenda kufanya majaribio klabu ya Ligi Kuu England, West Ham United wakati huo chini ya kocha Mtaliano Gianfranco Zola.
Hata hivyo, pamoja na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Zola kuvutiwa na uwezo wa mchezaji huyo kisoka, akasema Ngassa anahitaji kurejea Afrika kuongeza lishe.
Julai mwaka 2011, Ngassa alikwenda kufanya majaribio Seattle Sounders FC ya Ligi Kuu ya Marekani na akatumiwa katika mchezo wa kujiandaa na msimu dhidi ya Manchester United ya England.
Hata hivyo, Azam FC haikuwa tayari kumuuza mchezaji huyo. Ngassa alicheza Azam FC hadi mwaka 2012 alipohamia Simba SC kwa mkopo na mwaka 2013 akarejea timu yake kipenzi, Yanga SC ambayo, ameiaga baada ya msimu akiiachia ubingwa wa Ligi Kuu.
Mfungaji huyo bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, pia amewahi kuwa Mchezaji Bora wa Tanzania mara mbili mwaka 2010.
Mwaka 2005 akiwa Kagera Sugar alishinda Kombe la Tusker wakiifunga Simba SC katika fainali na alipohamia Yanga SC alishinda mataji ya Ligi Kuu katika misimu ya 2008, 2009 na 2015.
Ameshinda pia mataji ya Tusker mwaka 2007 na 2009 akiwa na Yanga SC, wakati akiwa na Azam FC aliiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka 2012.
Amekuwa Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2010–2011 akiwa na Azam FC na mfungaji bora wa Kombe la Challenge mwaka 2009.
Huyo ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu mwezi Apirli mwaka huu, ambaye ana nafasi kubwa ya kuwa pia Mchezaji Bora wa jumla wa Ligin Kuu msimu huu.
Amekuwa mchezaji muhimu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars tangu mwaka 2007 na hadi sasa amiechezea timu hiyo mechi 82 na kuifungia mabao 22.
KUHUSU FREE STATE;
Free State Stars ni timu yenye maskani yake mjini Bethlehem, Free State ambayo inacheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini, maarufu kama PSL.
Haswa ilianzishwa mwaka 1977 katika mji mdogo wa Makwane katika zama za QwaQwa, na ikafanikiwa kupanda Ligi Kuu mwaka 1986.
Timu hiyo ikashinda Kombe la Ligi, michuano ambayo baadaye ikabadilishwa jina na kuwa Kombe la Coca Cola.
Baada ya kuteremka daraja kufuatia kuyumba kiuchumi, mwaka 2003 klabu hiyo iliuzwa kwa
Mike Mokoena na familia yake ambaye aliifufua ikianzia Daraja la kwanza kabla ya kufanikiwa kurejea Ligi Kuu mwaka 2005 baada ya kushinda Kombe la Ligi ya Mvela Golden.
Lakini katika msimu wake wa kwanza Ligi Kuu ilishika mkia na kuteremka tena, lakini ikafanikiwa kurejea tena PSL msimu wa 2007–2008. Pia walifanikiwa kushinda taji la Kombe la Baymed Desemba 2006 baada ya kuifunga FC AK katika fainali.
Tangu hapo, timu hiyo ambayo wamepita nyota kadhaa waliotamba katika soka ya Afrika Kusini kama Bunene Ngaduane wa DRC, Jonathan Mensah wa Ghana, Kennedy Mweene wa Zambia na watoto wa nyumbani, John Tlale, Siphiwe Tshabalala na Thabo Matlaba imekuwa imara katika PSL, msimu huu ikimaliza nafasi ya tisa.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

Tuesday, May 12, 2015

TAIFA STARS KWENDA AFRIKA KUSINI KESHOTimu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kesho jumatano inatarajiwa kusafiri kuelekea nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki michuano ya kombe la COSAFA.

Michuano ya COSAFA inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei 17 mpaka Mei 30, 2015 katika viwanja vya Olympia Park na Moruleng  jimbo la North West Province nchini Afrika Kusini ikishirikisha nchi za Kusini mwa Afrika huku Tanzania na Ghana zikiwa ni nchi waalikwa.

Taifa Stars itaondoka jijini Dar es salaam kesho majira ya saa 1 jioni, kwa usafiri wa shirika la ndege la Fasjet na kufika jijini Johanesburg saa 5 usiku.

Mara baada ya kupimwa afya jana na madaktari wachezaji Aishi Manula, Isihaka Hassan, Haroun Chanongo, Kelvin Friday na nahodha Nadir Haroub wamekutwa na majeruhi ambayo yamepelekea kutokuwepo katika kikosi kitakachosafiri kesho, watabakia nchini wakiendelea kufanya mazoezi chini ya ungalizi mpaka timu itakaporejea kutoka Afrika Kusini na kuungana kwa ajili ya maandalizi ya AFCON, huku Amri kiemba akipewa ruhusa kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia.

Msafara wa Taifa Stars utaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF, Ephaphra Swai ukijumuisha wachezaji 20 na benchi la ufundi, timu inatarajiwa kufikia katika hoteli ya Sun City iliyopo pembeni kidogo ya jiji la Rusterburg.

Kesho siku ya Alhamis kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 7 mchana ni muda wa mapumziko, waandishi wa habari mnakaribishwa katika kambi ya timu ya Taifa iliyopo Tansoma Hotel kuweza kuongea na wachezaji, kocha mkuu na daktari wa timu kabla ya kuanza safari jioni.

Monday, May 11, 2015

NDUMBAROKUENDELEA KUTUMIKIA ADHABU YA TFFBaada ya mahojiano kati ya mrufani Dk. Damas Ndumbaro na Wakili wa TFF,  Emmanuel Muga, pamoja na Wajumbe wa Kamati ya rufaa ya nidhamu kuwahoji wote, mrufani na wakili wa TFF, kamati ya rufaa ya nidhamu ilichukua uamuzi ufuatao:-


    Hoja ya kwanza ya rufaa, kwamba kamati ya nidhamu haikuwa na nguvu za kisheria kusikiliza shauri lake, Kamati ya rufaa ya nidhamu baada kusikiliza hoja za pande zote mbili, kwa uamuzi wa Wajumbe wote kwa maana ya kuwa zote nne za Wajjumbe wa kamati ya rufaa ya nidhamu, ilitupilia mbali hoja hiyo na kuona kwamba kamati ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa mkata rufaa ni afisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF kwa mujibu wa Katiba ya TFF ya 2013. Uamuzi katika hoja hii uliamuliwa kwa kura 3 dhidi ya moja.
    Hoja ya pili inayosema kwamba kamati ilikosea kisheria kwa kutompa muda wa kuleta utetezi wake wala vielelezo vyovyote vile kwenye shauri lake.

Kamati ya rufaa ya Nidhamu kwenye Shauri hili, baada ya kufanya maamuzi kwa kupiga kura, kura za Wajumbe watatu zilitupiliwa mbali hoja yake na kura moja kati ya kura nne ilikubaliana na hoja yake kwa uamuzi huo, kamati ya rufani ya nidhamu ilitupilia mbali hoja hiyo kwa uamuzi wa wingi wa kura kwa maana ya kuwa tatu dhidi ya kura moja.


Sababu za kutupilia mbali hoja hizo ni kwamba mrufani alipata wito wa kwenda kwenye shauri, na akawakilishwa na wakili wake ( Nestory Peter Wandiba ) kwenye Shauri hilo. Shauri liliposikilizwa kwa mara ya kwanza tarehe 10/10.2014 shauri lilipangwa kusikilizwa tarehe 11/10/2014 Lakini siku hiyo ya pili si wakili wala Dr Ndumbaro alifika kwenye shauri hilo kwa maana hiyo basi shauri lililazimika kusilikizwa upande mmoja kwa mujibu wa kanuni za nidhamu za TFF ibara ya 94 (3).


3. Hoja ya tatu linalosema kwamba kamati ilikosea kusiliza shauri upande mmoja bila ya mtuhumiwa kuwepo, ni kukiuka haki yake ya msingi ya  kusikilizwa.


Kamati baada ya kusikiliza utetezi kutoka pande zote mbili kamati ilifanya uamuzi kwa kupiga kura, na kura tatu (wajumbe watatu) walitupilia mbali hoja hiyo, dhidi ya kura moja (mjumbe mmoja) aliyeikubali hoja hiyo. Sababu za kutupilia mbali hoja hiyo ni kutokana na ukweli kwamba mrufani alipata wito wa kuhudhuria shauri hili na akamtuma wakili wake, lakini mrufani alishindwa kuonyesha vielelezo vya kuonyesha kwamba angesafiri kwenda nje ya nchi ili kamati ya nidhamu iweze kuahirisha shauri mpaka wakati ambao angekuwa amerejea lakini hakufanya hivyo.


Hata hivyo kwa mujibu wa Ibara 144(2) (3) za kanuni ya nidhamu za TFF, mrufani  angeweza pia kuomba kamati ya nidhamu ibatilishe uamuzi iliyoutoa dhidi yake ili aweze kusikilizwa utetezi wake pia hakufanya hivyo na aliamua kukata rufaa.


4. Hoja ya nne inayosema kwamba kamati ilikosea kisheria katika uchambuzi wa ushahidi wa mlalamikaji na hatimaye kutoa uamuzi uliomtia hatiani.Kamati ya rufani ya nidhamu ilisikiliza kwa umakini hoja za pande zote mbili na kujiridhisha kwamba mrufani alifanya makosa kwa kutoa taarifa isiyosahihi na kupotosha maamuzi ya TFF kinyume na kanuni ya 41 (6) ya kanuni za ligi kuu ya Tanzania toleo la 2014 (4) na pia kushawishi, kupotosha au kuzuia maamuzi/utekelezaji wa maamuzi ya TFF kinyume na kanuni ya 41(16) ya kanuni za ligi kuu za Tanzania ya (2014).


Wakati wa kufanya maamuzi, wajumbe watatu(3) kwa maana ya kura tatu zilitupilia mbali hoja hiyo, na kura moja, kwa maana ya mjumbe mmoja alikubaliana na hoja hiyo. Kwa maana hiyo, kamati ya rufaa ya nidhamu ya TFF imetupilia mbali hoja hiyo.


Kwa uamuzi huu kamati inadhibitisha uamuzi wa kamati ya nidhamu iliyosomwa tarehe 13/10/2014, uamuzi huu umefikiwa baada ya wajumbe kupiga kura na uamuzi kupitishwa kwa wingi wa kura za wajumbe watatu, dhidi ya mjumbe mmoja wa kamati hii kwa hoja ya 2,3 na 4 na wajumbe wote 4 walikubaliana kutupiliwa mbali hoja ya kwanza.


Kwa hiyo Dr Damas Ndumbaro ataendelea kutumikia adhabu yake kwa kutojihusisha na shughuli yoyote ya Mpira wa Miguu (Soka) kwa kipindi cha miaka saba.


Hata hivyo mrufani Dr Damas Ndumbaro anayohaki ndani ya siku 10 kuanzia leo tarehe 10/05/2015 ya kuomba marejeo ya uamuzi huu mbele ya kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya TFF chini ya Ibara 142 ya kanuni za nidhamu za TFF ya mwaka.

Kila upande utabeba gharama zake Hukumu inasomwa leo tarehe 10/05/2015/

Revocatus L. K. Kuuli.
MAKAMU MWENYEKITI.

WANAMUZIKI WA TANZANIA WANAKOSA UBUNIFU-BELLA
MWIMBAJI nyota wa muziki wa dansi nchini na kiongozi wa bendi ya  Malaika, Christian Bella, amesema sababu kubwa inayowafanya wanamuziki wa Tanzania kushindwa kupata mafanikio kimataifa ni kukosa ubunifu.
Bella amesema wanamuziki wa Tanzania wanashindwa kwenda na wakati na kwa miaka mingi sasa wamekuwa wakipiga muziki uleule, bila kuubadili na kuweka vionjo vipya.
“Wanamuziki wa Tanzania hawataki kwenda na wakati, wanakosa ubunifu. Wanataka kupiga muziki ule ule wa miaka ya 80,”amesema.
Bella, ambaye nyimbo zake nyingi zimetokea kugusa hisia za mashabiki wa muziki nchini, alisema hayo wiki hii, alipokuwa akizungumzia maendeleo yake kimuziki na hali ya muziki nchini.
Amesema licha ya kumiliki bendi ya Malaika, amekuwa akirekodi nyimbo zake binafsi kwa lengo la kujitangaza na kukuza kipaji chake.
“Bendi ni yangu, lakini haiwezi kuimarika bila mimi kujitangaza,”amesema mwanamuziki huyo mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Amesema uamuzi wake huo hauna maana kwamba anaidharau bendi hiyo au kuitelekeza, bali amepania kula sahani moja na wakali wa muziki wa bongo fleva kama Ali Kiba na Naseeb Abdul ‘Diamond.
Amesema nyimbo zake zimekuwa zikipendwa na mashabiki wengi wa muziki nchini kutokana na kuwa na mashairi yenye mvuto na pia kuweka vionjo vipya mara kwa mara.
“Naimba na kupiga nyimbo zangu kwa kuchanganya aina tofauti ya muziki. Nachanganya bongo fleva, dansi na pia naangalia wenzangu wanafanya nini,”amesema Bella, ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa bendi ya Akudo Impact.
“Hakuna kipya katika muziki, aina zote za muziki zinazopigwa sasa, zilishawahi kupigwa miaka ya nyuma.
“Hata Koffi Olomide na Fally Ipupa wanaiga vionjo vya muziki vya Kitanzania. Katika muziki, hakuna kitu kinachoitwa kuiga muziki wa bendi au mwanamuziki fulani,”amesema mwanamuziki huyo, ambaye amekuwa na ushirikiano mkubwa na wasanii wa bongo fleva.
Bella amekiri kuwa binafsi anavutiwa na muziki wa kizazi kipya kutokana na ukweli kwamba wasanii wake ni wabunifu na amekuwa akipata vitu vingi kutoka kwao.
Mwimbaji huyo mwenye sauti yenye mvuto, inayopanda na kushuka mithili ya mawimbi baharini, amesema baadhi ya wanamuziki wa Tanzania hawapendi maendeleo ya wenzao na wamekuwa wakipenda kufuatilia maisha na kazi za wenzao.
“Wapo wanaoweza kukufuatilia kila siku kutaka kujua umefanya nini. Hata ukifanya kitu kizuri, utaona wanakukosoa, lakini ukiwaambia waingie studio kurekodi, hawawezi,”amesema.
Bella amesema wakati alipoanzisha bendi ya Malaika, baadhi ya wanamuziki walimponda na kumtabiria kwamba haiwezi kufika mbali, lakini alijipa moyo.
“Ningekuwa na moyo dhaifu, ningekata tamaa mapema, lakini nilijipa moyo kwamba nitafanikiwa, na kweli nimefanikiwa kwani bendi ipo juu kuliko zile zilizoanzishwa miaka mingi,”amesema.
Amekanusha madai kuwa, amekuwa akiwabania wanamuziki wenzake katika bendi ili wasipate umaarufu. Lakini amekiri kuwa msimamo wake ni kwamba haiwezekani bendi ikawa na mastaa kibao. Amesisitiza kuwa staa katika bendi huwa ni mmoja.
“Kila mtu anataka kuwa staa, hilo haliwezekani. Mwanamuziki anaweza kuwa na nyimbo alfu moja kwenye kabati, lakini hakuna hata moja iliyowahi kushika chati. Lazima wanamuziki watofautiane,”amesisitiza.
“Kama ni kweli nimekuwa nikiwabania wanamuziki wenzangu, mbona baada ya kuondoka Akudo Impact, bendi imeshindwa kuendelea. Kwa nini wale waliobaki wameshindwa kuiendeleza na kutumia nafasi ya kuondoka kwangu kuonyesha vipaji vyao?” Alihoji.
Bella amesema katika bendi yake ya Malaika, hatoi ruhusa kwa kila mwanamuziki kurekodi nyimbo zake binafsi kwa vile kufanya hivyo kutaidhoofisha bendi.
Amesema kama suala ni kutaka kupata umaarufu, amekuwa akiwaachia wanamuziki wake saa tatu kila wanapofanya maonyesho, kupiga nyimbo za utangulizi ili kuonyesha makali yao kabla ya yeye kupanda stejini.
“Huwa tunaanza maonyesho yetu saa tatu usiku. Nawaacha wanaimba kwa saa tatu, mimi naimba kuanzia saa sita usiku,” amesema.
“Umaarufu unaanzia kwenye maonyesho, sio kwenye TV. Wale mashabiki wanaoingia ukumbini tangu saa mbili usiku ndio wanaokupa umaarufu,”amesema.
Bella amesema kwa sasa anajiandaa kwa safari ya kwenda Ufaransa kwa ajili ya kuingia mkataba na promota mmoja maarufu wa wanamuziki kutoka DRC ili kurekodi nyimbo zake katika sura ya kimataifa na kujitangaza zaidi duniani.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja jina la promota huyo na pia kueleza lini anatarajia kwenda safari hiyo.

ABDALLA KIBADENI: VIONGOZI WENGI WA SOKA BOMU
KOCHA maarufu wa soka nchini, Abdalla ‘King’ Kibadeni, ameamua kuweka mambo hadharani kwa kusema kuwa viongozi wengi wa sasa wa mchezo huo ‘bomu’.
Kibadeni, ambaye alipewa jina la King miaka ya 1970, alipokuwa akiicheza Simba, akifananishwa na Pele wa Brazil, amesema viongozi wengi wa soka nchini hawana mapenzi ya dhati na klabu zao na wameweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.
Mbaya zaidi, Kibadeni amesema baadhi ya viongozi wa klabu hawapendani, hawana uzalendo na wamekuwa wakiwadhulumu wachezaji haki zao za msingi.
Mshambuliaji huyo nyota wa zamani wa Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars, alisema hayo mjini Dar es Salaam hivi karibuni, alipokuwa akizungumzia maendeleo ya mchezo huo nchini na mustakabali wake kisoka.
Kibadeni, ambaye alipewa hadhi ya ‘Chifu Mputa’, alipokuwa akiifundisha Majimaji ya Songea,amesema kushindwa kufanya vizuri kwa timu za Tanzania katika michuano ya kimataifa, kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na uzembe wa viongozi.
Amesema katika miaka ya nyuma, timu za Tanzania zilikuwa zikifanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kutokana na viongozi wake kuwa makini katika maandalizi na kuwahudumia wachezaji.
“Zamani haikuwa ajabu kwa Simba, Yanga, Pan African na Taifa Stars kuzifunga timu za Afrika Magharibi. Hawakuwa wakitusumbua,”alisema.
Amesema ajira ya ukocha kwa klabu za Tanzania haina heshima kutokana na kutimuliwa bila sababu za msingi na pia baadhi ya viongozi kuingilia kazi zao, ikiwa ni pamoja na kupanga wachezaji katika mechi muhimu.
“Viongozi kuingilia kazi za kocha ni jambo la kawaida. Unaweza ukaletewa memo siku ya mechi ikikuelekeza timu inayopaswa kucheza siku hiyo na ukikataa kufuata maelekezo, unajiweka kwenye matatizo,”amesema kocha huyo aliyewahi kuzifundisha timu za Majimaji, Moro United, Manyema, Ashanti na Simba.
“Wakati mwingine unaweza kupigiwa simu siku ya mechi, ukaambiwa fulani usimchezeshe, ameonekana mahali fulani akichukua pesa, lakini ukimuuliza iwapo ana ushahidi, hana. Sasa fikiri umemfundisha mchezaji wiki nzima kwa ajili ya maandalizi ya mechi, halafu unaambiwa usimchezeshe,”aliongeza.
Kocha huyo amesema yeye na Julio (Jamhuri Kihwelo), walitimuliwa Simba mwaka jana bila sababu za msingi na kwamba kitendo hicho kiliwahuzunisha.
Amesema kumdhulumu mtu haki zake ni dhambi na pale anapohuzunika, dua yake hupokelewa na Mungu.
Kwa mujibu wa Kibadeni, kufundisha timu ndogo kuna changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na malipo kidogo, lakini kocha anakuwa huru katika kufanyakazi yake.
“Lakini ukifundisha timu kubwa, kama hauko sawasawa, utashindwa. Timu ikifanya vizuri utaonekana wa maana, lakini ikivurunda unashushwa thamani,” amesema.
Ili kocha aweze kulinda hadhi na heshima yake, Kibadeni amesema ni bora kuondoka mapema timu inapofanya vibaya badala ya kusubiri kutimuliwa.
Hata hivyo, Kibadeni amesema wachezaji wamekuwa wakichangia makocha kutimuliwa holela kutokana na kushindwa kucheza kwa kufuata maelekezo wanayopewa.
“Mara nyingi wachezaji wamekuwa wakipaniki mapema katika mechi muhimu na kucheza kivyao, lakini mwisho wa siku, lawama zinamuangukia kocha,”amesema.
Kibadeni amesema katika miaka ya nyuma, makocha walikuwa na heshima kubwa katika klabu za Simba na Yanga, ikiwa ni pamoja na kutumiwa na wanachama kutafuta viongozi bora wakati wa uchaguzi na ushauri wao uliheshimiwa.
Akizungumzia ushiriki wa timu za Tanzania katika michuano ya kimataifa, Kibadeni amesema tatizo kubwa ni maandalizi duni na viongozi kushindwa kuzitumia vyema mechi za nyumbani kupata ushindi.
Amesema ushindi wa nyumbani ni muhimu kwa vile unarahisisha matokeo ya ugenini.
Kwa mujibu wa Kibadeni, waarabu wanapocheza ugenini, hutumia mbinu ya kuchelewesha muda na kucheza kwa kujihami ili kuwachanganya wapinzani wao, lengo lao kubwa likiwa ni kutumia kila mbinu kushinda nyumbani.
Amesema viongozi wa Simba walitumia vyema mbinu hizo katika michuano ya Kombe la CAF mwaka 1993, ambapo walishinda karibu mechi zote za nyumbani na kulazimisha sare ugenini na hatimaye kufuzu kucheza fainali.
Amesema hadi sasa hana hakika ni vipi Simba ilishindwa kutwaa kombe hilo nyumbani baada ya kutoka suluhu na Stella Abidjan ya Ivory Coast ugenini. Katika mechi hiyo ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Simba ilichapwa mabao 2-0.
“Mengi yalisemwa kuhusu mechi hiyo. Wengine walisema ilikuwa ni mbinu ya mfadhili (Azim Dewji) kupita mlango wa nyuma baada ya kushindwa kununua KIA alizoahidi kwa wachezaji.
“Ninachoweza kusema sina hakika. Inawezekana ikawa kweli ama isiwe kweli. Hata mimi nilishindwa kuelewa. Kwao tulitoka sare, tukatawala mchezo, huku tukafungwa!” Alieleza kwa mshangao Kibadeni, ambaye alikuwa kocha msaidizi wa Simba wakati huo, akimsaidia Eshente kutoka Ethiopia.
Kocha huyo amesema timu nyingi zinazoshiriki michuano ya ligi kuu Tanzania Bara, lengo lao kubwa huwa ni kubaki katika ligi hiyo, na si kutwaa ubingwa. Amesema hali hiyo ndiyo inayotoa mwanya kwa Simba, Yanga na sasa Azam kutawala ligi hiyo.
Kibadeni ameelezea kusikitishwa kwake na uamuzi wa Azam kumtimua kocha wake, Joseph Omog kutoka Cameroun, baada ya timu hiyo kutolewa na El-Merreikh ya Sudan katika michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka huu.
Amesema uamuzi huo haukuwa wa busara na ulichangia kuifanya Azam ipoteze mwelekeo katika kutetea taji la ligi kuu msimu huu, ambalo limetwaliwa na Yanga.
Akizungumzia mipango yake ya baadaye, Kibadeni amesema ni kukuza vipaji vya vijana kupitia kituo chake cha kuendeleza soka chenye vijana wa umri wa miaka 14 hadi 16.
“Nawakaribisha vijana wa umri huo wenye vipaji waje kwenye kituo changu. Nawaandaa kuwa wachezaji wa timu za taifa za vijana wa umri mbalimbali. Sitarajii kuwauza Simba au Yanga, nitawauza nje,”amesema.
Licha ya kuanzisha na kumiliki kituo hicho, Kibadeni amesema hajawahi kuwaona viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), waliopewa jukumu la kusimamia soka ya vijana, wakimtembelea au kumpatia msaada wowote.
Amesema anakerwa kuona viongozi wa Simba, Yanga na Azam, wakitumia mamilioni ya pesa kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi, wakati wapo vijana wengi wenye vipaji, isipokuwa wanatakiwa kuendelezwa.
Licha ya kuwepo kwa vijana wengi wenye vipaji vya kucheza soka nchini, Kibadeni amesema hakuna usimamizi mzuri katika soka ya vijana. Amesema hali hiyo ndiyo inayosababisha hadi sasa kusitokee vijana walioweza kufikia kipaji chake.
“Bado hajatokea mchezaji wa aina yangu hadi sasa, ndio sababu nilipewa majina ya heshima kama vile King, nikifananishwa na Pele na Mputa, nililopewa kama heshima na viongozi wa mkoa wa Ruvuma kutokana na kuinua soka ya mkoa huo,”amesema Kibadeni.

Sunday, May 10, 2015

TFF YAKUBALI UENYEJI KOMBE LA KAGAME


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), leo hii imekubali kuwa wenyeji wa  michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, ngazi ya klabu maarufu kama Kombe la Kagame.


Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ambalo ndio wamiliki wa mashindano haya, watatoa mialiko kwa klabu zenye sifa ya kushiriki.

Taarifa iliyotolewa na TFF leo mchana imeeleza kuwa, michuano hiyo inatarajiwa kuafanyika nchini kuanzia Julai 11 hadi Agosti 2,  2015.

DRFA YACHEKELEA TIMU ZAKE KUMALIZA TATU BORA LIGI KUU

Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimeonyesha furaha yake baada ya timu tatu zilizo katika himaya yake, kumaliza katika nafasi za juu kwenye ligi kuu Tanzania Bara, iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kamati ya Utendaji ya DRFA, chini ya Mwenyekiti wake, Almas Kasongo,imesema ni jambo la kufurahisha kuona mkoa wa Dar es salaam unafanya vizuri kisoka na kuwa mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine.

Timu hizo zimepongezwa kutokana na matayarisho waliyoyafanya tangu kuanza kwa msimu,ambapo mabenchi ya ufundi yameonyesha kuwa na nia ya dhati kuleta ushindani katika ligi.

Yanga na Azam ndizo zitakazoiwakilisha nchi katika michuano ya klabu barani Afrika,ambapo Yanga itakwenda huko kuwania kombe la klabu bingwa baada ya kutwaa uchampioni, huku Azam ikiwania kombe la Shirikisho baada kumaliza katika nafasi ya pili. Simba imemaliza katika nafasi ya tatu.

Aidha, DRFA imeipongeza TFF na kamati ya bodi ya ligi kwa usimamizi mzuri wa ligi msimu huu licha ya kuwepo na changamoto ndogondogo kwa klabu kulalamikia miundombinu ya vyumba vya kubadilishia nguo viwanjani na uonevu wa baadhi ya waamuzi.

DRFA imeishauri TFF kuangalia kwa kina na kuzifanyia kazi changamoto hizo zilizojitokeza msimu huu ili zisijirudie tena katika msimu ujao, kwa lengo la kuiboresha ligi ya Tanzania,ambayo kuanzia msimu ujao itakuwa na timu 16.

Pamoja na hayo DRFA imezishauri Yanga na Azam kujipanga vizuri kwa ajili ya mashindano ya klabu za Afrika msimu ujao, ili kuandika historia na kuleta vikombe hivyo kwa mara ya kwanza nyumbani.

POLISI MORO, RUVU SHOOTING ZASHUKA DARAJA

 MICHUANO ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara, ilimalizika rasmi jana kwa mechi saba zilizochezwa kwenye viwanja tofauti, huku ikishuhudiwa timu za Polisi Moro na Ruvu Shooting zikishuka daraja baada ya kupoteza mechi zao.

Ruvu Shooting ilishuka daraja baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Stand United katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati Polisi Moro ilichapwa idadi hiyo ya bao na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Tayari timu za Majimaji ya Songea, Toto Africans ya Mwanza na African Sports ya Tanga, zimeshapata tiketi ya kucheza ligi mkuu msimu ujao, ambayo sasa itakuwa na timu 16 badala ya 14.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Mgambo iliyokuwa kwenye wakati mgumu ilitoka suluhu na Azam kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, wakati Prisons na Kagera Sugar zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mabingwa wapya wa ligi hiyo, Yanga walipoteza mechi yao ya mwisho kwa kuchapwa bao 1-0 na Ndanda kwenye Uwanja wa Nang'wanda mjini Mtwara, Mtibwa Sugar ilichapwa bao 1-0 na Coastal Union mjini Morogoro.

NOOIJ AITA 28 STARS KUELEKEA COSAFA CUP

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mart Nooij leo ametangaza kikosi cha wachezaji 28 watakaoingia kambini katika hoteli ya Tansoma iliyo eneo la Gerezani jijini Dar es salaam, kujiandaa na michuano ya kombe la COSAFA na kuwania kufuzu kwa AFCON na CHAN mwezi Juni mwaka huu.


Akiongea na waandishi wa habari leo makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF amesema, wachezaji 28 aliowaita, amewaona kwa macho yake wakicheza, na katika wachezaji aliowaita amechanganya wanaochipukia (damu changa) na wenye uzoefu wa michuano ya kimataifa.


Nooij amesema katika orodha hiyo ya wachezaji 28 watakaoripoti kambini jumatatu mchana, watapimwa afya zao na madakatari wa timu ya Taifa, na kisha watakaokuwa fit atachagua wachezaji 20 watakaokwenda kwenye michuano ya COSAFA nchini Afrika kusini.


Aidha Nooij ameongeza wachezaji 8 watakaobakia nchini wanapaswa kuwa tayari wakati wowote wanaweza jumuishwa katika kikosi kutokana na Taifa Stars kukabiliwa na michuano mbalimbali ambayo pia inahitaji kuwa na wigo mpana wa wachezaji.


Wachezaji walioitwa na kocha Nooij ni magolikipa: Deogratius Munish (Yanga), Aishi Manula, Mwadini Ali (Azam), walinzi: Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam), Nadir Haroub, Oscar Joshua, Kelvin Yondani (Yanga), Abdi Banda, Hassan Isihaka (Simba), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Haji Mwinyi (KMKM).


Wengine ni viungo: Amri Kiemba, Salum Abubakar, Frank Domayo (Azam), Said Juma, Salum Telela, Hassan Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba), Haroun Chanongo (Stand United) na Mwinyi Kazimoto (Al Markhira).Washambuliaji ni Ibrahim Ajib (Simba), Mrisho Ngasa, Saimon Msuva (Yanga), John Bocco, Kelvin Friday (Azam) na Juma Luizio (Zeco United).


Taifa Stars inatarajiwa kuondoka nchini siku ya jumatano, Mei 13 saa 1 jioni kwa shirika la ndege la Fastjet kuelekea nchini Afrika Kusini katika mji wa Rusterburg - North West Province ambapo ndipo michuano ya COSAFA CUP itafanyika kuanzia Mei 17 mpaka Mei 31 mwaka huu.


Mchezo wa kwanza wa Taifa Stars iliyopo katika kundi B katika michuano ya COSAFA, itacheza dhidi ya Swaziland Mei 18, Mei 20 (Madagascar Vs Tanzania) na Mei 22 ( Tanzania vs Lesotho), mshindi wa kundi B atacheza robo fainali dhidi ya timu ya Taifa kutoka Ghana.


Mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, Taifa Stars itarejea nchini kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa AFCON 2017, dhidi ya Misri utakaopigwa Juni 13 nchini Misri, kisha kurejea nchini kucheza na Uganda Juni 21 kuwania kufuzu kwa fainali za wachezaji wa ndani CHAN.


Mart Nooj amesema ataitumia michuano ya COSAFA kama sehemu ya maandalizi ya michezo ya kuwania kufuzu kwa AFCON na CHAN.

JERRY MURO APIGWA FAINI MILIONI 5

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF iliyoketi jumanne tarehe 5 Mei, 2015 imempiga faini ya sh. 5,000,00 (milioni tano), Afisa Habari wa klabu ya Yanga SC Jerry Muro kwa kutoa kauli za chuki, kisirani na uchochezi dhidi ya uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) nchini na TFF.

Akitoa utetezi wake mbele ya Kamati ya Nidhamu, Jerry Muro alikiri na kujutia kufanya kosa hilo na kudai ilitokana na ugeni wake katika uongozi wa michezo, kwa kuzingatia hilo kamati ilimuepusha na adhabu ya kufungiwa..


Kwa mujibu wa Ibara ya 53 (2)ya Kanuni za Nidhamu za TFF toleo la 2012, kwa kuidhalilisha TFF na Bodi yake ya Ligi mbele ya umma, kamati imemtoza faini ya sh. 5,000,000 (millioni tano), Jerry Muro na kuwaonya viongozi wengine wa familia ya mpira wa miguu kutojihusisha na vitendo vya matamshi ya aina hiyo.


Shitaka linalomhusisha mchezaji wa Yanga, Amissi Tambwe kumshika kwa kumdhalilisha mchezaji wa Simba SC Juuko Mursheed, na kiongozi wa Friend Rangers Hery Chibakasa wa Friends Rangers kuhamasisha vurugu katika mchezo wa timu yake na dhidi ya Majimaji ya Songea Januari 29, 2015, kamati imeahirisha mashitaka hayo mpaka tarehe nyingine itakapopangwa.


Kamati iliahirisha malalamiko dhidi ya Mohamed Hussein, Muhibu Kanu, Manfred Luambano, Venance Joseph, Mussa Senyange, Saleh Ali, Shafii Maganga na Ismail Salim baada ya kupokea taarifa za udhuru zilizosbabishwa na mgomo wa madereva wa mabasi ya abiria ya mikoani.KUMRADHI WANAHABARI


Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Mwesigwa Selestine ameomba radhi kwa vyombo kufuatia madai ya waandishi wa habari kupata usumbufu wakati wa utoaji wa Zawadi kwa Mabingwa na washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom.


Mwesigwa alisema kwa niaba ya TFF anaomba radhi kwa usumbufu wowote uliowapata waandishi na wadau wote walioshindwa kushuhudia vema tukio hilo.


“TFF na FIFA vinatambua umuhimu na nafasi ya wanahabri na vyombo vya habari si tu katika kuutangaza mchezo, bali pia katika kutia chachu maendeleo ya mchezo wenyewe “ alisema Mwesigwa.


Hali mbaya ya hewa ilivuruga utaratibu uliokuwa umepangwa awali kuanzia itifaki ya shughuli za kabla na wakati wa mchezo na zile za utoaji tuzo.


Aidha Mwesigwa alisema TFF itaendelea kushirikiana vema na jumuiya ya wanahabari ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wana mazingira mazuri wanapofanya kazi kwenye matukio ya mpira wa miguu.Thursday, May 7, 2015

AZAM YATIBUA SHEREHE ZA UBINGWA YANGA


WACHEZAJI wa Yanga wakishangilia kombe la ubingwa wa michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya mechi kati yao na Azam. Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilichapwa mabao 2-1 na Azam.


Winga wa Azam FC, Brian Majwega akimtoka beki wa Yanga SC, Juma Abdul jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

AZAM FC imekata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mabingwa Yanga SC jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo, unaifanya Azam FC ifikishe pointi 48 baada ya kucheza mechi 25, nyuma ya mabingwa, Yanga SC wenye pointi 55 za mechi 25.

Simba SC ipo nafasi ya tatu kwa pointi zake 44 na hata ikishinda mechi yake ya mwisho itafikisha 47, hivyo kwa mwaka wa tatu mfululizo Wekundu wa Msimbazi watakosa michuano ya Afrika

Azam FC ilitoka nyuma kwa 1-0 baada ya Mbrazil Andrey Coutinho kutangulia kuifungia Yanga SC dakika ya 12 na Bryson Raphael akasawazisha dakika ya 14 kabla ya Aggrey Morris kufunga la ushindi dakika ya 85.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Gadiel Michael, Shomary Kapombe, Aggrey Morris, Mudathir Yahya, Brison Raphael, Frank Domayo, Gaudence Mwaikimba, Kipre Tchetche na Brian Majwega. 

Yanga SC; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Pato Ngonyani, Saum Telela, Danny Mrwanda, Nizar Khalfan, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho.

HABARI, PICHA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY

Wednesday, May 6, 2015

WAAMUZI WA KIKE WA TANZANIA WAULA


Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika - CAF limewateua waamuzi wa kike kutoka Tanzania kuchezesha mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake U-20 mwaka 2016 kati ya Congo DR dhidi ya Gabon.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa jumamosi tarehe 09.05.2015 jijini  Kinshasa - Condo DR, mwamuzi wa kati ni Jonesia Rukya, akisaidiwa na washika vibendera Dalila Jafari na Sophia Mtongoli huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Hellen Mduma.

Wakati huo huo Elizabeth Kalinga ameteuliwa kuwa kamisaa wa mchezo kati ya Kenya dhidi ya Botswana kuwania kufuzu kwa michuani ya Olympiki, mchezo utakaofanyika Mei 31, 2015 nchini Kenya.


NB: Alhamisi ya tarehe 07 Mei, 2015, saa 5 kamili asubuhi, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars) Mart Nooij ataongea na waandishi wa habari katika Ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume, waandishi wote wa habari mnaombwa kuhudhuria bila kukosa.

YANGA, AZAM NI SHIIIIDA LEO
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja utakaopigwa katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, wenyeji timu ya Azam FC watawakaribisha Mabingwa wapya wa ligi hiyo msimu huu timu ya Young Africans.

Mechi hiyo no. 141 itachezeshwa na mwamuzi wa kati Jacob Adongo kutoka Mara, akisaidiwa na washika vibendera Frednand Chacha (Mwanza), Hellen Mduma (Dsm), huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Hussein Kalindo (Dsm) na Kamisaa wa mchezo huo ni Damian Mabena kutoka Tanga.

Katika mchezo huo timu ya Young Africans itakabidhiwa Kombe lake la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2014/2015, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dr Fennela Mkangara.

Mchezo huo wa kesho unatarajiwa kuanza majira ya saa 11 kamili jioni, kwa saa za Afrika Mashariki na kati ili kutoa fursa kwa wadau, wapenzi na mashabiki wa mpira wa miguu nchini kujitokeza kushudia mchezo huo pamoja na shamrashamra za kukabidhiwa kikombe.

Young Africans watakabidhiwa Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu na mgeni rasmi, huku wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom wakimkabidhi zawadi mchezaji bora wa mwezi Aprili Mrisho Ngasa na fedha taslimu sh. millioni moja.

COASTAL UNION YAAGIZWA KUITISHA MKUTANO WA DHARULAKatibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine ameiandikia barua Klabu ya Coastal Union akiiagiza klabu hiyo kuitisha mkutano mkuu wa dharura wa wanachama tarehe 17 Mei mwaka 2015.

Matokeo ya maamuzi haya yamepatikana baada ya kikao cha usuluhishi cha amani kilichoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ahmed Iddi Mgoi aliyekuwa ameongozana na Makamu Mkurugenzi wa Sheria na Uanachama shirikisho la soka nchini (TFF) Eliud Peter Mvella kilichofanyika April 13 mwaka huu katika hotel ya Tanga Beach Resort Tanga mjini.

TFF imeahidi kutuma orodha tatu za majina
(A) Wanachama stahiki.                                                                       
(B) Wanachama waliobainika kuwa wanadosari na inabidi wathibitishwe na wanachama stahiki naa.
(C) Waombaji wapya wa wanachama watakaohakikiwa na wanachama stahiki.

Orodha hizi zinapaswa kubandikwa kwenye ubao wa Matangazo wa Klabu, katika kikao cha ufunguzi cha kuleta usuluhisho huo, mbali na kuhudhuriwa na kamati ya Utendaji ya Coastal Union chini ya Makamu wake Mwenyekiti Steven Mguto pia kilihudhuria na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF,Khalid Abdallah, Mwenyekiti wa Chama cha soka Mkoa wa Tanga,Said Soud.

Wengine waliohudhuria kikao hicho walikuwa ni Afisa Michezo wa Mkoa wa Tanga, Digna Tesha, Katibu wa Chama cha soka Mkoa wa Tanga, Beatrice Mgaya, Afisa Utamaduni Jiji la Tanga, Peter Semfuko na Katibu wa Chama cha soka wilaya ya Tanga (TDFA) Salim Carlos.

Monday, May 4, 2015

SIMBA YAFUFUA MATUMAINI YA KUCHEZA KOMBE LA SHIRIKISHO


TIMU ya soka ya Simba jana ilifufua matumaini ya kucheza michuano ya klabu za Afrika mwakani baada ya kuichapa Azam mabao 2-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Licha ya ushindi huo, Simba bado ipo nyuma ya Azam kwa tofauti ya pointi moja. Azam ni ya pili ikiwa na pointi 45 wakati Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 44.

Hata hivyo, Simba italazimika kuiombea mabaya Azam ipoteze mechi zake mbili zilizosalia,ikiwemo dhidi ya Yanga na yenyewe ishinde mechi yake ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu.

Iliwachukua Simba dakika 48 kuhesabu bao lake la kwanza kupitia kwa Ibrahim Ajibu, aliyeunganishwa kwa kichwa mpira wa krosi kutoka pembeni ya uwanja.

Azam ilisawazisha bao hilo dakika ya 57 kupitia kwa Mudathir Yahaya baada ya kuunganisha wavuni krosi kutoka kwa Kipre Tchetche.

Bao la pili na la ushindi la Simba lilifungwa na Ramadhani Singano dakika ya 74 baada ya kufyatua  shuti la mbali lililotinga moja kwa moja wavuni.

Azam ililazimika kumaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji 10 baada ya kiungo wake, Salum Abubakar kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya beki Mohamed Hussein wa Simba.

Sunday, May 3, 2015

MAYWEATHER ALIVYOMDUNDA PACQUIAO KWA POINTI


YANGA YATOLEWA NA ETOILE YA TUNISIA KLABU BINGWA AFRIKANa Prince Akbar, SOUSSE
SAFARI ya Yanga SC katika Kombe la Shirikisho Afrika imefikia tamati usiku huu.
Hiyo inafuatia Yanga SC kufungwa bao 1-0 na wenyeji Etoile du Sahel katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Olimpiki mjini Sousse, Tunisia.

Kwa matokeo hayo, Yanga SC inatolewa kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya awali kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani Dar es Salaam. Etoile sasa watacheza na timu moja iliyotolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania nafasi ya kupangwa katika makundi ya Kombe la Shirikisho.

Etoile walipata bao hilo kipindi cha kwanza, mfungaji Ammar Jemal, kwa kichwa akimalizia krosi ya Alkhali Bangoura dakika ya 24. Jemal aliurukia mpira uliompita kipa Deo Munishi ‘Dida’ akiwa peke yake pembezoni mwa lango na kuutumbukizia nyavuni kiulaini

Pamoja na Yanga SC kutangulia kufungwa, lakini walicheza vizuri na kukosa mabao kadhaa ya wazi.
Etoile ndiyo walioanza kulitia misukosuko lango la Yanga SC, baada ya Soussi Zied kushindwa kumalizia kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Tej Marouen dakika ya saba.

Kevin Yondan alifanya kazi nzuri dakika ya tisa baada ya kuokoa mpira ambao tayari ulikuwa umempita kipa wake, Dida uliopigwa na Soussi dakika ya tisa.

Dakika ya 18 Mouhbi Youssef alipoteza nafasi baada ya shuti lake kutoka nje kidogo kufuatia krosi ya Naguez Hamdi.

Yanga SC ilifanya shambulizi la kwanza dakika ya 26, lakini mpira wa kichwa uliopigwa na mshambuliaji Amissi Tambwe uligonga mwamba kufuatia krosi ya Juma Abdul.

Mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman alipiga juu ya lango dakika ya 33 baada ya kupokea krosi nzuri ya Mrisho Ngassa.

Etoile ilipata pigo dakika ya 42, baada ya kiungo wake tegemeo, Mcameroon Frank Kom kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu.

Kom alionyeshwa kadi hiyo na refa Dennis Batte wa Uganda baada ya kumchezea rafu winga Simon Msuva, wakati tayari alikuwa ana kadi ya njano aliyoonyeshwa mapema dakika ya tisa kwa kumchezea rafu Ngassa.

Kipindi cha Yanga SC walikianza vizuri wakipeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Etoile, ambayo ilionekana dhahiri kuathiriwa na kupoteza mtu mmoja, tena muhimu, Kom.

Katika kuhakikisha wanaulinda ushindi, Etoile wakaanza kucheza mchezo wa kujihami na kufanya mashambulizi ya kushitukiza.

Hiyo iliwapa Yanga nafasi ya kutawala mchezo, lakini hawakuwa na madhara kwenye eneo la hatari la wapinzani wao hao.

Kikosi cha Etoile su Sahel kilikuwa; Aymen Ben Ayoub, Naguez Hamdi, Abdelrazek Ghazi, Boughattas Zied, El Jemmal Ammar, Frank Kom, Ben Amine, Bangoura Alkhaly, Tej Marouen, Mouihbi Youssef na Soussi Zied/Brigui Alaya dk48.

Yanga SC; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Mbuyu Twite, Saidi Makapu, Simon Msuva, Salum Telela/Andrey Coutinho dk82, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa na Kpah Sherman/Hussein Javu dk65.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY

Saturday, May 2, 2015

NGASA, AMBROSE WACHEZAJI BORA WA MWEZI LIGI KUU


Mchezaji James Mwasote Ambrose wa timu ya Tanzania Prisons FC amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Machi 2015 kufuatia kuwapiku wachezaji wengine waliokua wakiwania nafasi hiyo.

Jopo la maalum la makocha ambao hutafuta wachezaji bora kwa kila mchezo na kisha kujumlisha alama za mchezaji kwa kila mchezo na kumpata mchezji bora wa mwezi, ndio hufanya kazi ya kuchagua mchezaji bora kwa kila mwezi.

Mshambuliaji wa Young Africans Mrisho Ngasa amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom mwezi Aprili kufuatia kuwapiku Amos Edward, Frank Domayo na Emmanuel Okwi baada ya kupata alama nyingi za jumla za mchezaji bora kwa kila mchezo.

Kwa kuibuka wachezaji bora wa mwezi Machi na Aprili, James Ambrose na Mrisho Ngasa watazawadiwa fedha taslimu sh. milioni moja kwa kila mmoja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodaom.


NB: Kesho jumamosi tarehe 02 Mei 2015, kutakua na mkutano na waaandishi na habari saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa TFF - Karume, waandishi wote wa habari mnaombwa kuhudhuria bila kukosa.