KOCHA maarufu wa soka nchini, Abdalla ‘King’ Kibadeni,
ameamua kuweka mambo hadharani kwa kusema kuwa viongozi wengi wa sasa wa mchezo
huo ‘bomu’.
Kibadeni, ambaye alipewa jina la King miaka ya 1970,
alipokuwa akiicheza Simba, akifananishwa na Pele wa Brazil, amesema viongozi
wengi wa soka nchini hawana mapenzi ya dhati na klabu zao na wameweka mbele
zaidi maslahi yao binafsi.
Mbaya zaidi, Kibadeni amesema baadhi ya viongozi wa
klabu hawapendani, hawana uzalendo na wamekuwa wakiwadhulumu wachezaji haki zao
za msingi.
Mshambuliaji huyo nyota wa zamani wa Simba na timu ya
Taifa, Taifa Stars, alisema hayo mjini Dar es Salaam hivi karibuni, alipokuwa
akizungumzia maendeleo ya mchezo huo nchini na mustakabali wake kisoka.
Kibadeni, ambaye alipewa hadhi ya ‘Chifu Mputa’,
alipokuwa akiifundisha Majimaji ya Songea,amesema kushindwa kufanya vizuri kwa
timu za Tanzania katika michuano ya kimataifa, kunachangiwa kwa kiasi kikubwa
na uzembe wa viongozi.
Amesema katika miaka ya nyuma, timu za Tanzania zilikuwa
zikifanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kutokana na viongozi wake kuwa
makini katika maandalizi na kuwahudumia wachezaji.
“Zamani haikuwa ajabu kwa Simba, Yanga, Pan African na
Taifa Stars kuzifunga timu za Afrika Magharibi. Hawakuwa wakitusumbua,”alisema.
Amesema ajira ya ukocha kwa klabu za Tanzania haina
heshima kutokana na kutimuliwa bila sababu za msingi na pia baadhi ya viongozi
kuingilia kazi zao, ikiwa ni pamoja na kupanga wachezaji katika mechi muhimu.
“Viongozi kuingilia kazi za kocha ni jambo la kawaida.
Unaweza ukaletewa memo siku ya mechi ikikuelekeza timu inayopaswa kucheza siku
hiyo na ukikataa kufuata maelekezo, unajiweka kwenye matatizo,”amesema kocha
huyo aliyewahi kuzifundisha timu za Majimaji, Moro United, Manyema, Ashanti na
Simba.
“Wakati mwingine unaweza kupigiwa simu siku ya mechi, ukaambiwa
fulani usimchezeshe, ameonekana mahali fulani akichukua pesa, lakini ukimuuliza
iwapo ana ushahidi, hana. Sasa fikiri umemfundisha mchezaji wiki nzima kwa
ajili ya maandalizi ya mechi, halafu unaambiwa usimchezeshe,”aliongeza.
Kocha huyo amesema yeye na Julio (Jamhuri Kihwelo), walitimuliwa
Simba mwaka jana bila sababu za msingi na kwamba kitendo hicho kiliwahuzunisha.
Amesema kumdhulumu mtu haki zake ni dhambi na pale
anapohuzunika, dua yake hupokelewa na Mungu.
Kwa mujibu wa Kibadeni, kufundisha timu ndogo kuna
changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na malipo kidogo, lakini kocha anakuwa huru
katika kufanyakazi yake.
“Lakini ukifundisha timu kubwa, kama hauko sawasawa,
utashindwa. Timu ikifanya vizuri utaonekana wa maana, lakini ikivurunda
unashushwa thamani,” amesema.
Ili kocha aweze kulinda hadhi na heshima yake, Kibadeni
amesema ni bora kuondoka mapema timu inapofanya vibaya badala ya kusubiri
kutimuliwa.
Hata hivyo, Kibadeni amesema wachezaji wamekuwa
wakichangia makocha kutimuliwa holela kutokana na kushindwa kucheza kwa kufuata
maelekezo wanayopewa.
“Mara nyingi wachezaji wamekuwa wakipaniki mapema katika
mechi muhimu na kucheza kivyao, lakini mwisho wa siku, lawama zinamuangukia
kocha,”amesema.
Kibadeni amesema katika miaka ya nyuma, makocha walikuwa
na heshima kubwa katika klabu za Simba na Yanga, ikiwa ni pamoja na kutumiwa na
wanachama kutafuta viongozi bora wakati wa uchaguzi na ushauri wao
uliheshimiwa.
Akizungumzia ushiriki wa timu za Tanzania katika
michuano ya kimataifa, Kibadeni amesema tatizo kubwa ni maandalizi duni na
viongozi kushindwa kuzitumia vyema mechi za nyumbani kupata ushindi.
Amesema ushindi wa nyumbani ni muhimu kwa vile unarahisisha
matokeo ya ugenini.
Kwa mujibu wa Kibadeni, waarabu wanapocheza ugenini,
hutumia mbinu ya kuchelewesha muda na kucheza kwa kujihami ili kuwachanganya
wapinzani wao, lengo lao kubwa likiwa ni kutumia kila mbinu kushinda nyumbani.
Amesema viongozi wa Simba walitumia vyema mbinu hizo
katika michuano ya Kombe la CAF mwaka 1993, ambapo walishinda karibu mechi zote
za nyumbani na kulazimisha sare ugenini na hatimaye kufuzu kucheza fainali.
Amesema hadi sasa hana hakika ni vipi Simba ilishindwa
kutwaa kombe hilo nyumbani baada ya kutoka suluhu na Stella Abidjan ya Ivory
Coast ugenini. Katika mechi hiyo ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa
Uhuru, Simba ilichapwa mabao 2-0.
“Mengi yalisemwa kuhusu mechi hiyo. Wengine walisema
ilikuwa ni mbinu ya mfadhili (Azim Dewji) kupita mlango wa nyuma baada ya
kushindwa kununua KIA alizoahidi kwa wachezaji.
“Ninachoweza kusema sina hakika. Inawezekana ikawa kweli
ama isiwe kweli. Hata mimi nilishindwa kuelewa. Kwao tulitoka sare, tukatawala
mchezo, huku tukafungwa!” Alieleza kwa mshangao Kibadeni, ambaye alikuwa kocha
msaidizi wa Simba wakati huo, akimsaidia Eshente kutoka Ethiopia.
Kocha huyo amesema timu nyingi zinazoshiriki michuano ya
ligi kuu Tanzania Bara, lengo lao kubwa huwa ni kubaki katika ligi hiyo, na si
kutwaa ubingwa. Amesema hali hiyo ndiyo inayotoa mwanya kwa Simba, Yanga na
sasa Azam kutawala ligi hiyo.
Kibadeni ameelezea kusikitishwa kwake na uamuzi wa Azam
kumtimua kocha wake, Joseph Omog kutoka Cameroun, baada ya timu hiyo kutolewa
na El-Merreikh ya Sudan katika michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka huu.
Amesema uamuzi huo haukuwa wa busara na ulichangia
kuifanya Azam ipoteze mwelekeo katika kutetea taji la ligi kuu msimu huu,
ambalo limetwaliwa na Yanga.
Akizungumzia mipango yake ya baadaye, Kibadeni amesema
ni kukuza vipaji vya vijana kupitia kituo chake cha kuendeleza soka chenye
vijana wa umri wa miaka 14 hadi 16.
“Nawakaribisha vijana wa umri huo wenye vipaji waje
kwenye kituo changu. Nawaandaa kuwa wachezaji wa timu za taifa za vijana wa
umri mbalimbali. Sitarajii kuwauza Simba au Yanga, nitawauza nje,”amesema.
Licha ya kuanzisha na kumiliki kituo hicho, Kibadeni
amesema hajawahi kuwaona viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
waliopewa jukumu la kusimamia soka ya vijana, wakimtembelea au kumpatia msaada
wowote.
Amesema anakerwa kuona viongozi wa Simba, Yanga na Azam,
wakitumia mamilioni ya pesa kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi, wakati wapo
vijana wengi wenye vipaji, isipokuwa wanatakiwa kuendelezwa.
Licha ya kuwepo kwa vijana wengi wenye vipaji vya
kucheza soka nchini, Kibadeni amesema hakuna usimamizi mzuri katika soka ya
vijana. Amesema hali hiyo ndiyo inayosababisha hadi sasa kusitokee vijana
walioweza kufikia kipaji chake.
“Bado hajatokea mchezaji wa aina yangu hadi sasa, ndio
sababu nilipewa majina ya heshima kama vile King, nikifananishwa na Pele na
Mputa, nililopewa kama heshima na viongozi wa mkoa wa Ruvuma kutokana na kuinua
soka ya mkoa huo,”amesema Kibadeni.
No comments:
Post a Comment