KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, May 18, 2015

TAIFA STARS YAANZA VIBAYA KOMBE LA COSAFA


Simon Msuva wa Tanzania (kushoto) akimtoka Sanele Mkweli wa Swaziland katika mchezo huo

Watanzania waishio miji mbalimbali Afrika Kusini walijitokeza kwa wingi Jumatatu usiku Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace kuishangilia timu yao ya taifa, Taifa Stars ikicheza na Swaziland katika mchezo wa kwanza wa Kundi B Kombe la COSAFA mjini Rusternbug, Afrika Kusini. Bahati mbaya Taifa Stars ilifungwa 1-0.

Na Mahmoud Zubeiry, RUSTENBURG
TANZANIA, imeanza vibaya michuano ya Kombe la COSAFA, baada ya kufungwa bao 1-0 na Swaziland katika mchezo wa kwanza wa Kundi B, usiku huu Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace mjini hapa.

Matokeo hayo yanaiweka Stars inayofundishwa na Mholanzi, Mart Nooij katika mazingira magumu ya kwenda Robo Fainali- baada ya Madagascar kuifunga 2-1 Lesotho katika mchezo wa kwanza.

Stars sasa lazima ishinde mechi zake mbili zijazo dhidi ya Lesotho na Madagascar ili kuangalia uwezekano wa kwenda Robo Fainali.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Nelson Emile Fred wa Shelisheli, aliyesaidiwa na Akhtar Nawaz Rossaye wa Mauritius na Isaskar Boois wa Namibia, hadi mapumziko tayari Swaziland walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.

Bao hilo lilifungwa na Sifiso Mabila kwa shuti kali dakika ya 42 baada ya kutanguliziwa pasi kwenye njia na Xolani Sibandze aliyemtoka Oscar Joshua upande wa kushoto.

Tanzania ilitengeneza nafasi tatu nzuri kipindi cha kwanza, ambazo kwa bahati mbaya mbili Simon Msuva alishindwa kuzitumia na moja John Bocco alipoteza pia.

Kipindi cha pili, Swaziland walitawala zaidi mchezo, lakini safu ya ulinzi ya Stars ilikuwa imara kutoruhusu mabao zaidi.

Nafasi pekee nzuri ambayo Stars walipata kipindi cha pili ilikuwa ni dakika ya 65, baada ya Said Ndemla kupiga juu ya lango akiwa ndani ya boksi kufuatia pasi nzuri ya John Bocco. 

Swaziland waliizidi ufundi uwanjani Stars leo, ambayo haikucheza kwa malengo. Stars haikuwa na madhara kabisa kwenye eneo la hatari la Swaziland.

Tony Tsabedze alitajwa mchezaji bora wa mechi baada ya mchezo huo.

Taifa Stars; Deo Munishi ‘Dida’, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Salum Mbonde, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Mrisho Ngassa/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dk75, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Said Ndemla/Juma Luizio dk65 na Simon Msuva/Ibrahim Hajibu dk82.

Swaziland; Mphikileli Dlamini, Sifiso Mabila, Siyabonga Ndluli, Sanele Mkhweli, Zweli Nxumalo/Mxlosi Lukhele dk67, Mthunzi Mkhontfo, Siboniso Malambe, Machawe Dlamini, Njabulo Ndhlovu/Sifiso Nkambule dk62, Tony Tsabedze na Xolani Sibandze/Sabelo Ndzinisa dk80.

No comments:

Post a Comment