KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, May 4, 2015

SIMBA YAFUFUA MATUMAINI YA KUCHEZA KOMBE LA SHIRIKISHO


TIMU ya soka ya Simba jana ilifufua matumaini ya kucheza michuano ya klabu za Afrika mwakani baada ya kuichapa Azam mabao 2-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Licha ya ushindi huo, Simba bado ipo nyuma ya Azam kwa tofauti ya pointi moja. Azam ni ya pili ikiwa na pointi 45 wakati Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 44.

Hata hivyo, Simba italazimika kuiombea mabaya Azam ipoteze mechi zake mbili zilizosalia,ikiwemo dhidi ya Yanga na yenyewe ishinde mechi yake ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu.

Iliwachukua Simba dakika 48 kuhesabu bao lake la kwanza kupitia kwa Ibrahim Ajibu, aliyeunganishwa kwa kichwa mpira wa krosi kutoka pembeni ya uwanja.

Azam ilisawazisha bao hilo dakika ya 57 kupitia kwa Mudathir Yahaya baada ya kuunganisha wavuni krosi kutoka kwa Kipre Tchetche.

Bao la pili na la ushindi la Simba lilifungwa na Ramadhani Singano dakika ya 74 baada ya kufyatua  shuti la mbali lililotinga moja kwa moja wavuni.

Azam ililazimika kumaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji 10 baada ya kiungo wake, Salum Abubakar kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya beki Mohamed Hussein wa Simba.

No comments:

Post a Comment