KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 13, 2015

NGASA AMWAGA WINO FREE STATE STARS YA AFRIKA KUSINI

Na Mahmoud Zubeiry, BETHELEHEM
KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa amesaini Mkataba wa miaka minne kujiunga na klabu ya Free State Stars ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini leo.
Ngassa, mume wa Radhia na baba wa Farida (8) na Faria (6) aliwasili jana jioni mjini hapa na leo asubuhi baada ya kukamilisha mazungumzo, akasaini Mkataba huo mnono.
“Nimefurahi kusaini timu hii, ambayo kaka yangu Nteze John amewahi kuchezea pamoja na wachezaji wengine wakubwa kama Tshabalala na Mweene,”alisema Ngassa.
“Sasa najiandaa kwa maisha mapya baada ya kucheza Tanzania kwa muda mrefu, hii ni changamoto mpya kwangu, mpira wa Afrika Kusini upo juu sana ukilinganisha na pale kwetu (Tanzania). Nataka kutumia fursa hii kuitangaza soka ya Tanzania, ili klabu zisijifikirie tena kusajili wachezaji wa Tanzania,”amesema Ngassa.

 Kocha Kinnah Phiri (kushoto) akimkabidhi Ngassa jezi ya Free State Stars leo, makao makuu ya klabu hiyo, Mtaa wa 22B President Boshoff mjini Bathlehem baada ya kusaini Mkataba wa miaka minne kuichezea timu hiyo

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa timu hiyo maarufu kama Ea Lla Koto, Mmalawi Kinnah Phiri amesema kwamba amekuwa akimpenda Ngassa kwa muda mrefu na kukutana naye FS ni kutimia kwa ndoto zake za kufanya kazi na kijana huyo siku moja.
Katika Mkataba huo ambao Ngassa, mtoto wa kiungo wa zamani wa Simba SC, Khalfan Ngassa atakuwa analipwa karibu mara tatu ya mshahara aliokuwa anapata Yanga SC, atapatiwa nyumba ya kuishi na familia yake, gari na huduma nyingine muhimu, ikiwemo bima.
Ngassa anakuwa Mtanzania wa pili kuichezea Free State, baada ya Nteze John Lungu ‘mwana Mwanza’ pia aliyeichezea timu hiyo enzi hizo inaitwa Qwa Qwa Stars mwaka 1997 hadi 1999.  
Ngassa anatua Free States akitokea Yanga SC, ambayo ameichezea jumla ya mechi 186 katika awamu mbili, na kuifungia jumla ya mabao 86.
Ngassa aliyetimiza miaka 26, Aprili 12 mwaka huu, alijiunga na Yanga SC kwa mara ya kwanza mwaka 2006, akitokea Kagera Sugar iliyomuibua mwaka 2005 kutoka timu ya vijana ya Toto Africans ya Mwanza.
Mwaka 2010 alihamia Azam FC kwa dau la rekodi wakati huo, dola za Kimarekani 40,000 (Sh. Milioni 80).
Kabla ya hapo, akiwa Yanga SC, Aprili mwaka 2009, Ngassa alikwenda kufanya majaribio klabu ya Ligi Kuu England, West Ham United wakati huo chini ya kocha Mtaliano Gianfranco Zola.
Hata hivyo, pamoja na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Zola kuvutiwa na uwezo wa mchezaji huyo kisoka, akasema Ngassa anahitaji kurejea Afrika kuongeza lishe.
Julai mwaka 2011, Ngassa alikwenda kufanya majaribio Seattle Sounders FC ya Ligi Kuu ya Marekani na akatumiwa katika mchezo wa kujiandaa na msimu dhidi ya Manchester United ya England.
Hata hivyo, Azam FC haikuwa tayari kumuuza mchezaji huyo. Ngassa alicheza Azam FC hadi mwaka 2012 alipohamia Simba SC kwa mkopo na mwaka 2013 akarejea timu yake kipenzi, Yanga SC ambayo, ameiaga baada ya msimu akiiachia ubingwa wa Ligi Kuu.
Mfungaji huyo bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, pia amewahi kuwa Mchezaji Bora wa Tanzania mara mbili mwaka 2010.
Mwaka 2005 akiwa Kagera Sugar alishinda Kombe la Tusker wakiifunga Simba SC katika fainali na alipohamia Yanga SC alishinda mataji ya Ligi Kuu katika misimu ya 2008, 2009 na 2015.
Ameshinda pia mataji ya Tusker mwaka 2007 na 2009 akiwa na Yanga SC, wakati akiwa na Azam FC aliiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka 2012.
Amekuwa Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2010–2011 akiwa na Azam FC na mfungaji bora wa Kombe la Challenge mwaka 2009.
Huyo ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu mwezi Apirli mwaka huu, ambaye ana nafasi kubwa ya kuwa pia Mchezaji Bora wa jumla wa Ligin Kuu msimu huu.
Amekuwa mchezaji muhimu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars tangu mwaka 2007 na hadi sasa amiechezea timu hiyo mechi 82 na kuifungia mabao 22.
KUHUSU FREE STATE;
Free State Stars ni timu yenye maskani yake mjini Bethlehem, Free State ambayo inacheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini, maarufu kama PSL.
Haswa ilianzishwa mwaka 1977 katika mji mdogo wa Makwane katika zama za QwaQwa, na ikafanikiwa kupanda Ligi Kuu mwaka 1986.
Timu hiyo ikashinda Kombe la Ligi, michuano ambayo baadaye ikabadilishwa jina na kuwa Kombe la Coca Cola.
Baada ya kuteremka daraja kufuatia kuyumba kiuchumi, mwaka 2003 klabu hiyo iliuzwa kwa
Mike Mokoena na familia yake ambaye aliifufua ikianzia Daraja la kwanza kabla ya kufanikiwa kurejea Ligi Kuu mwaka 2005 baada ya kushinda Kombe la Ligi ya Mvela Golden.
Lakini katika msimu wake wa kwanza Ligi Kuu ilishika mkia na kuteremka tena, lakini ikafanikiwa kurejea tena PSL msimu wa 2007–2008. Pia walifanikiwa kushinda taji la Kombe la Baymed Desemba 2006 baada ya kuifunga FC AK katika fainali.
Tangu hapo, timu hiyo ambayo wamepita nyota kadhaa waliotamba katika soka ya Afrika Kusini kama Bunene Ngaduane wa DRC, Jonathan Mensah wa Ghana, Kennedy Mweene wa Zambia na watoto wa nyumbani, John Tlale, Siphiwe Tshabalala na Thabo Matlaba imekuwa imara katika PSL, msimu huu ikimaliza nafasi ya tisa.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

No comments:

Post a Comment