KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, May 30, 2016

MKWASA: MECHI YETU NA MISRI ITAKUWA FAINALI



Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba mchezo ujao kati ya Mapharao wa Misri na Taifa Stars, utakuwa ni fainali ya kuamua taifa litakalofuzu katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON hapo mwakani kutoka kundi G.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo kati ya Harambee Stars ya Kenya na Taifa Stars ya Tanzania Mei 29, 2016, uliofanyika Uwanja wa Moi Kasarani, Mkwasa maarufu kama Master anasema kwa msimamo na hali ilivyo kwa sasa, “Najua Misri wanatufuatilia. Na hata Kenya kwa siku zote tatu walikuwako. Najua  Misri wanahitaji sare ili wafuzu kwa fainali hizi, lakini hawataipata Tanzania.”

Mkwasa anasema mchezo dhidi ya Misri, ana uhakika vijana wake watajitahidi ili kupata matokeo mazuri baada ya Jumapili kufanya vema dhidi ya Harambee Stars waliocheza mechi hiyo mbele ya mashabiki wao wachache ambao pia hawakuchangamka kama wale wa Tanzania ambao licha ya kuwa ugenini walichangamsha mji na uwanja.

Wakati Misri wana pointi saba, Taifa Stars ina pointi moja na hivyo wa kuibania au kupindua matokeo ya Misri isiende AFCON mwakani, basi ni Tanzania hasa kama itawafunga Mapharao Jumamosi kabla ya kwenda Nigeria Septemba, mwaka huu kucheza na Nigeria.

“Kama nilivyosema, Misri wanakujawanahitaji pointi moja. Lakini sisi tunahitaji pointi tatu. Mchezo wa leo unatosha kuona mapungufu (upungufu). Maana ilikuwa mechi ngumu iliuyojaa nyota wote wa Kenya ambao ni professionals, lakini mimi nilikuwa na local based players na matokeo yamekuwa hayo.

“Tilianza kufunga bao, lakini wakarudisha. Bora mchezo umeishia hivi maana najua Wakenya hawana uvumilivu, tungewafunga hapa sijui kama tungetoka salama,” amesema Mkwasa ambaye baadhi ya waandishi, hususani wale wa Kenya walianguka kicheko kuashiria kuwa kuna matatizo katika utawala wa soka.

Mkwasa anasema ana taarifa namna ambavyo Misri wanaifuatilia Taifa Star hususani ukusanyaji wa video kwa ajili ya kuona aina ya soka la Tanzania, huku akisema: “Hawatafanikiwa kwa sababu soccer is the game of different approach (Soka ni mchezo wenye mifumo tofauti). Hivyo tulivyocheza na Kenya sivyo nitakavyocheza na Misri, nitakuwa na approach yake.”

Anasema ushindi wa Jumamosi ijayo ni wa kuvuna pointi tatu ili kupata kasi ya kushinda mchezo dhidi ya Nigeria na kufungua ukurasa mpya wa Taifa Stars kutengeneza mazingira mazuri ya kuwashinda Nigeria katika mchezo wa mwisho hatua ya makundi utakaofanyika Septemba, mwaka huu.

“Tunaomba Wakenya mtuombee. Nasi tunawaombea ili kama wote inatokea mwaka huu tunakosa mafasi, basi iwe kheri kwa kipindi kijacho. Sisi tumekuja kucheza kwenu katika mji wenu wenye baridi basi nanyi karibuni siku moja dar es Salaam, Tanzania katika mji wetu wetu wenye joto, huenda mkaambulia sare vile vile,” anasema.

Mkwasa alipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (FKF), kwa kuandaa mchezo huo angalau kwa asilimia 70 kwa kushirikiana na Tanzania iliyojazia gharama za juu sambamba vijana wake kwa kucheza kwa kujituma licha ya kuwakosa nyota wake wa kulipwa na hivyo kupata picha na mbinu sahihi za kuivaa Misri Jumamosi ijayo.

“Bado tunaendele kujenga timu yetu, wengi ni vijana kama mlivyoona na wengine ni mara ya kwanza wanacheza. Nimewapa nafasi na mmeona uwezo wao, bila shaka tutafanya vema maana wengine ni under 21 wako kwenye kikosi. Huko mbele tutakuwa na timu nzuri,” anasema Mkwasa akimtolea mfano Shiza Ramadhani ambaye alipewa nafasi kwa mara ya kanza katika kikosi cha kwanza akichukua winga ya kulia.

 VICTOR WANYAMA
“Kwa hiyo tayari tumeona kitu gani cha kuongeza,” anasema Mkwasa hoja yake iliyoungwa mkono na Nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama ambaye kwa dakika chache, alizungumza na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania na kuhoji: “Unasema leo hamkuwa na professional pale uwanjani?” alipohakikishiwa ukweli huo, akasema:

“Basi mna kikosi kizuri. Wengi ni vijana, wanaweza kama mkicheza kwa kutubana kama mlivyobana hapa, Misri mnaifunga na hata hao Nigeria, si ajabu nikasikia mnakwenda AFCON mwakani. Ninaitakia kila la kheri timu hii, nawatakiwa kila la kheri Watanzania katika harakati zao.

"Sisi mwaka huu tumepotea kabisa, hatuna matumaini tena, tunajipanga ndiyo maana nimekuja kutetea taifa langu, hata kama tumekosa nafasi,” alisema Wanyama anayekipiga Southampton ya England.

Katika mchezo huo, Taifa Stars iliwakosa nyota wake Mbwana Samatta anayechezea Genk ya Ubelgiji kwa kuwa alikuwa na mchezo muhimu wa kupa nafasi timu yake ama icheze Ligi ya Uropa au ibaki nje katika michezo ya kimataifa ngazi ya klabu Ulaya.

Shirikisho la Soka Tanzania na Kocha Mkwasa walimruhusu kama ilivyo kwa Thomas Ulimwengu anayekipiga TP Mazembe waliokuwa na mchezo mkali dhidi ya AS Vita ambao wana utani na ushindani mkali wa soka huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

MWINYI KAZI MOTO
Naye Nahodha wa Taifa Stars katika mchezo huo, Mwinyi Kazimoto amesema kwamba mchezo dhidi ya Kenya, umeonesha picha ya kinachotakiwa kufanyika katika michezo ijayo inayoikabili timu hiyo baada ya kusifu maandalizi, mapokezi mazuri na sapoti nzuri kutoka kwa mashabiki wa Kitanzania, hasa wale waliosafiri umbali mrefu kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi, Kenya kuishangilia Stars. Nahodha wa Taifa Stars ni Mbwana Samatta anayesaidiwa na John Bocco ambao katika mchezo huo, hawakucheza. Bocco ni Majeruhi.

MCHEZO WA HARAMBEE STARS, TAIFA STARS
Katika mchezo huo, kipindi cha kwanza mashabiki walishuhudia mabao 1-1 kwa kila upande na ndiyo yaliyokuwa matokeo ya mwisho katika dakika 90, lakini kipindi cha pili wadau wa soka walishuhudia mabadiliko ya kila timu kujaribu nyota wake kwa mujibu wa sheria na taratibu za Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA), linaloruhusu kubadili wachezaji hadi wachezaji sita. Lakini hakukuwa na mabadiliko ya matokeo.

Kuhusu mabao ni Elias Maguli ndiye aliyetangulia kuifungia Taifa Stars bao katika dakika ya 30 kwa kichwa baada ya kupokea krosi murua kutoka kwa Juma Abdul kutoka Mashariki ya Uwanja wa Moi Kasarani kabla ya dakika saba baadaye kumfanyia madhambi Winga Ayub Masika ndani ya eneo la hatari hivyo Mwamuzi, Brian Nsubuga kutoka Uganda, kuamuru penalti iliyokwamishwa wavuni na Victor Wanyama.

Katika mchezo huo ambao wakati wote ulikuwa ni wa kushambuliana kwa timu zote mbili, Taifa Stars iliwapumzisha kipa Deogratius Munishi na nafasi yake ikachukuliwa na Aishi Manula na kwa wakati mmoja kuwatoa Jonas Mkude na Shiza Ramadhani na nafasi zao kuchukuliwa na Farid Mussa na Mohammed Ibrahim baadaye Kocha Mkwasa alimwingiza Jeremiah Juma kuchukua nafasi ya Maguli.

Kenya wao waliwatoa Humphrey Ochieng kwa kuingia Cliford Miheso; akatolewa tena Jesse Were kwa Wyclif Ochomo; Ayub Masika akapumzishwa na John Makwata akapewa nafasi kama alivyopumzishwa Anthony Agay na nafasi yake kuchukuliwa na Mayeko Mohammed. Pamoja na mabadiliko hayo, matokeo yalibaki vilevile 1-1 hadi dakika ya 90 katika mchezo ambao Wanyama alipewa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Kazimoto.

VIKOSI VYA TIMU ZOTE
Vikosi vya kwanza katika mchezo, Kenya: 1. Boniface Oluoch, 9. Joakins Otieno Atudo, 5. Abud Omar Khamis, 12. Eugene Ambuchi Asike, 8. David Owino Odhiambo, 14. Anthony Akumu Agay, 15. Victor Mugubi Wanyama, 23. Ayub Timbe Masika, 19. Humphrey Mieno Ochieng’ 16. Eric Johanna Omondi, 29. Jesse Jackson Were

Wachezaji wa akiba: 3. David Okello Abongo, 10. Eric Ouma Otieno, 6. Mayeko Musa Mohammed, 24. Victor Ali Abondo, 27, Wycliff Okello Ochomo, 20. John Mark Makwata, 21. Clifford Miheso Ayisi

Tanzania XI: 1. Deo Munishi, 6. Juma Abdul Jafari, 2. Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, 13. Aggrey Morris, 15. Erasto Edward Nyoni, 17. Jonas Gellard Mkude, 7. Himid Mao Mkami, 16. Shiza Ramadhan Yahya, 12. Mwinyi Kazimoto Mwitula, 10. Elias Mrugao Maguli, 4. Deus David Kaseke

Wachezaji wa akiba walikuwa: 18. Aishi Salum Manula, 5. David John Mwantika, 9. Farid Mussa Shah, 11. Jeremiah Juma Ally, 8. Abrahim Hajibu Migomba, 3. Mwinyi Haji Mngwali, 14. Mohammed Ally Ibrahim.

MUSSA WA JKT RUVU MCHEZAJI BORA WA MWEZI MEI



Mshambuliaji Abdulrahman Musa wa JKT Ruvu ameibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Mei 2016.

Musa katika kinganyiro hicho aliwapiku Donald Ngoma wa Yanga na Ali Nassoro wa Mgambo Shooting. Katika mwezi huo uliokuwa na raundi tatu, Musa alicheza mechi zote tatu za timu yake na kufunga jumla mabao manne; mawili katika kila mechi.

Kwa kushinda tuzo hiyo ya Mei ambayo ni ya mwisho kwa msimu huu kwa wachezaji bora wa mwezi, Musa atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom.

Washindi wengine wa tuzo hiyo ya mwezi kwa msimu huu wa 2015/2016 ambao mechi zake za mwisho zilichezwa Mei 22 mwaka huu ni Hamisi Kiiza wa Simba (Septemba), Elias Maguli wa Stand United (Oktoba), Thaban Kamusoko wa Yanga (Desemba), Shomari Kapombe wa Azam (Januari), Mohamed Mkopi wa Tanzania Prisons (Februari), Shiza Kichuya wa Mtibwa Sugar (Machi) na Juma Abdul wa Yanga (Aprili).

LIGI YA SDL YAENDELEA KUTIMUA VUMBI



Michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) msimu wa 2015/2016 inaendelea vizuri katika vituo vinne vya Kagera, Morogoro, Singida na Njombe ambapo itafikia tamati Juni 6 mwaka huu.

Timu sita zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu wa 2016/2017. Timu hizo ni zile zitakazoongoza kila kundi, na washindwa bora (best losers) wawili kutoka makundi mawili tofauti.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeweka waangalizi wake katika kila kituo, na litawachukulia hatua watu wote watakaobainika kutumia michuano hiyo kuchafua viongozi.

Mtwivila City ya Iringa inaongoza kituo cha Njombe ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi tatu. Katika kituo hicho kesho (Mei 31) kutakuwa na mechi kati ya Jangwani FC ya Rukwa na Nyundo FC ya Katavi kwenye Uwanja wa Amani.

Timu inayoongoza kituo cha Morogoro ni Namungo FC ya Lindi yenye pointi saba kwa mechi tatu. Kesho (Mei 31) ni mechi kati ya Makumbusho FC na Sifapolitan, zote za Dar es Salaam itakayofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Kitayose ya Kilimanjaro inaongoza kituo cha Singida ikiwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu ilizocheza. Kesho (Mei 31) kwenye kituo hicho kutakuwa na mechi kati ya Stand FC ya Tabora na Murusgamba ya Kagera itakayochezwa Uwanja wa Namfua.

Mpaka sasa vinara wa Kituo cha Kagera ambacho mechi zake zinachezwa Uwanja wa Vijana mjini Muleba ni Mashujaa FC ya Kigoma yenye pointi saba.

TAIFA STARS YATOKA SARE BAO 1-1 NA HARAMBEE STARS

Kikosi cha kwanza cha timu ya Soka ya Tanzania -Taifa Stars kilichoanza dhidi ya Harambee Stars ya Kenya jana.
Winga wa Taifa Stars, Shiza Ramadhani akichuana na beki Joakins Atudo wa Harambee Stars katika mchezo huo.
Mshambuliaji wa Taifa Stars, Elias Maguli (Kulia) akichuana na David Odhiambo wakati wa mchezo wa kirafiki wa Kimataifa uliofanyika Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi Kenya. timu hizo zilitosahana nguvu kwa kutoka sara ya 1-1.

Sunday, May 29, 2016

REAL MADRID VIDUME BARANI ULAYA

WACHEZAJI wa Real Madrid ya Hispania wakishangilia baada ya kuibuka na ushindi kwa njia ya matuta dhidi ya ndugu zao wa Atletico Madrid, katika mechi ya fainali iliyopigwa jana mjini Milan,Italia.

WAGANDA KUZUICHEZESHA STARS NA HARAMBEE STARS LEO, AZAM KURUSHA ‘LIVE’


Waamuzi watatu wa soka kutoka Uganda, ndio wakaochezesha mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Taifa Stars ya Tanzania na Harambee Stars ya Kenya utakaofanyika Uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi, Kenya.

Waamuzi hao watakaochezesha mchezo huo utakaoanza saa 10.00 jioni na kurushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Azam Tv kwa kushirikishi na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) ni Brian Nsubuga atakayepuliza kipenga na wasaidizi wake ni Bugembe Hussein upande wa kulia (line 1) na Katenya Ronald kwa upande wa kushoto (line 2)

Kamishna wa mchezo atakuwa Amir Hassan kutoka Somalia ambako Meneja wa Uwanja wa Moi Kasarani, Lilian Nzile amesema kwamba mazingira uwanja ni mazuri na mipango yote ya mchezo huo imekaa vema ikiwa ni pamoja na usalama uliothibitishwa pia na Kanali wa Jeshi la Polisi, Muchemi Kiruhi OCS wa Kasarani.

Kwa upande wa Kocha Mkuu Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro inayozalishwa na Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL), Charles Boniface Mkwasa atawakosa washambuliaji wake watatu katika kikosi ambacho kitaivaa Harambee Stars.

Washambuliaji hao ni Mbwana Samatta kutoka Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na John Bocco ambaye ni majeruhi wa mguu aliumia wakati wa fainali za Kombe la FA kati ya Yanga na Azam Jumatano wiki hii.

“Madaktari wamempa Bocco saa 72 za mapumziko. Bila shaka kabla ya kucheza na Misri atakuwa amepona,” alisema Mkwasa leo Mei 28, 2016 asubuhi na kuongeza kuwa Samatta ametuma taarifa kukosa mchezo dhidi ya Kenya kwa kuwa ana ratiba ya kucheza mchezo muhimu Mei 30, mwaka huu na matarajio ni kujiunga na timu Juni 1, 2016 kabla ya kuivaa Misri Juni 4, mwaka huu.

Kwa upande wa Ulimwengu, uongozi wa TP Mazembe nao waliomba kumtumia Ulimwengu katika mchezo wa ushindani wa mpinzani wake AS Vita. TP Mazembe na AS Vita ni timu pinzani huko DRC Congo na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ukaridhia na Mkwasa sasa amejipanga kukiandaa kikosi bila nyota hao mahiri.

“Katika mchezo huu sitakuwa na professionals (wachezaji wa kulipwa),” alisema Mkwasa ambaye jioni ya leo ameahidi kutoa kikosi cha nyota 11 watakaonza dhidi ya Kenya kesho.

Kwa sasa anaangalia namna ya kuipanga vema safu yake ya ulinzi baada ya kumkosa Kelvin Yondani anayetumikia adhabu ya kuonywa mara mbili kwa kadi ya njano hivyo kutojumuishwa kwenye mipango mchezo dhidi ya Misri. Mabeki anaotarajiwa kuanza nao ni Juma Abdul upande wa kulia na Mohammed Hussein upande wa kushoto.

Walinzi wakaoachukua nafasi ya Yondani na Nadir Haroub Cannavaro ambaye hakuongozana na timu katika safari ya Kenya ni Erasto Nyoni, Aggrey Morris na David Mwantika huku viungo wa kati wanaotarajiwa kupangwa ni Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude na pembeni ni Farid Mussa na Shiza Kichuya. Washambuliaji watakaotikisa Kenya katika mchezo wa kesho ni Elisu Maguli na Ibrahim Ajib.

“Kipa anaweza kuanza Dida (Deo Munishi) au Aishi Manula. Lakini hao niliokutajia ni proposed team (kikosi tarajiwa), lakini hasa nani anaaza kesho nitakutajia jioni ya leo mara baada ya mazoezi pale Moi Kasarani,” alisema Mkwasa aliyeonekana kujiamini na mipango yake kama lilivyo jina lake la umaarufu la Master.

“Nimeiandaa timu kucheza mifumo miwili ambayo ni 4-3-3 ambao ni mfumo wa kushambuliaji na pale tutakapokuwa tuna-defense (tunazuia) basi mfumo utakuwa ni 4-5-1,” alisema Mkwasa.

Katika mchezo wa kesho Mkwasa anayesaidia na Hemed Morocco na Manyika Peter anayewanoa makipa atapata nafasi ya kubadili wachezaji hadi sita ambao ni utaratibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa mechi za kirafiki za kimataifa kadhalika makubaliano katika mkutano wa kabla ya mchezo wa kesho.

Stars iliwasili Nairobi, Kenya jana asubuhi na kupokewa na wenyeji Shirikisho la Soka Kenya iliyowapeleka hoteli ya Nairobi Safari Club iliyoko mtaa wa Koinange, katikati ya jiji la Nairobi ambako mchana kabla ya kwenda mazoezi ilitembelewa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. John Haule aliyewahakikishia usalama  timu hiyo licha ya kuwako kwa taarifa za kuvamiwa.

“Msaada wowote mnaotaka na chochote mnachohitaji tunaomba mtutaarifu tujue namna ya kuwasaidia. Msiwe na wasiwasi kabisa. Hata kama hamjaipenda hoteli, semeni,” alisema Dk. Haule ambaye aliitakia timu mafanikio mazuri katika mchezo wa dhidi ya Harambee na ule wa Mafarao wa Misri.

Viongozi wa msafara wa Taifa Stars, Ahmed Mgoyi na Omar Walii walimweleza Balozi DK. Haule kuridhika na kambi na kwamba hawakupata tatizo lolote hali ilivyo hadi sasa.

REKODI YA SERENGETI YAWAVUTIA WAKENYA

Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyorejea nchini kutoka ziara ya India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016), imerudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki.

Serengeti Boys imecheza mfululizo michezo 7 ya kimataifa bila kufungwa dhidi ya Misri (2), India, Kore, Malaysia, na Marekani (USA). Kabla ya hapo timu hiyo ilicheza michezo kadhaa ya ndani na timu za chini ya umri wa miaka 20 bila kupoteza hata mchezo mmoja.

Mratibu wa timu ta Tanzania kutoka Shirikisho la Soka la Kenya, Anthony Achia, amesema walikuwa wanafuatilia michuano hiyo na mafanikio ya Serengeti. “Timu imefanya vema, ikitunza hii inaweza kuitoa Afrika Mashariki kimasomaso. Unajua sisi sote ni wa East Africa (wa Afrika Mashariki). Sasa ukiona mwezako anafanya vema, lazima useme. Endeleeni. Itakuja kuirithi hii”

Katika mashindano ya AIFF, timu hiyo pekee kutoka Afrika na ambayo ilikua kipenzi cha mashabiki katika jiji la Goha ilicheza na timu ambazo ziko juu katika hatua za juu katika mtoano wa kuwania kushiriki Kombe la Dunia kupitia mabara yao yaani CONCACAF (USA) na AFC (India, Korea na Malaysia). Haishangazi nchi nyingi za Ulaya, Asia na Marekani zimeulizia uwezekano wa timu hii kutembelea nchi zao kwa michezo ya kirafiki.

Awali timu ya Serengeti Boys ilipewa nafasi ndogo ya kufanya vizuri kwa sababu ya rekodi zilizokuwa zinaiweka Tanzania katika viwango vya chini katika umri huo kwa nchi za Afrika Magharibi na Kaskazini zilikuwa juu zaidi na vilevile ukweli wa kwamba timu kama USA, Korea, Malasyia na India zilikuwa na bajeti kubwa iliyogharamiwa na Serikali zao na walikuwa na vifaa vya kila namna kiasi cha kuomba magari kwa ajili ya vifaa vya mazoezi na mechi.

Kikosi cha Serengeti kinavunja kambi kabla ya kurejea siku si nyingi ili kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Afrika chini ya miaka 17 (Madagascar 2017) dhidi ya Ushelisheli hapa tarehe 25 Juni katika uwanja wa Taifa Dar es salaam.

Benchi la ufundi limeahidi kuendelea kukiimarisha kikosi hiki na vilevile kutengeneza mpango endelevu wa kuwa na wachezaji bora zaidi kila mwaka.

Serengeti Boys ilimaliza Mashindano ya AIFF katika nafasi ya tatu kwa kuifunga Malaysia mabao 3-0.

Serengeti Boys na Bingwa Korea hawakupoteza mchezo hata mmoja na awali walipokutana walitoka sare ya 2-2.

MBEYA CITY YAPATA NYOTA WAPYA 44




ZOEZI kusaka nyota wapya (vijana) ambao wataingizwa kwenye timu  mbili za Mbeya City Fc U20 na ile ya wakubwa limefikia kwenye hatua nzuri hivi sasa baada ya wachezaji 44 kupatikana kwenye mchujo wa awali  uliolifanyika  leo ikiwa ni baada ya  siku nne   za mazoezi.

Akizungumza na mbeyacityfc.com, mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya leo (Clinic day 5) kwenye uwanja wa Sokoine kocha msaidizi wa City, Mohamed Kijuso amesema kuwa Vijana 44 wamefanikiwa kuvuka  kwenye mchujo wa kwanza  hivyo wataingia kwenye wamu ya pili inayotaraji kuanza hapo kesho kwenye uwanja wa Sokoine.

“Tulikuwa na kundi kubwa la wachezaji zaidi ya 106, baada ya mchujo leo, tumefanikiwa kupata  44 ambao wataingia kwenye awamu ya pili hapo kesho,  lengo letu ni kuona tunapata Cream nzuri kwa ajili ya timu yetu ya vijana na pia  wachezaji saba ambao watakuwa tayari kucheza kwenye timu kubwa msimu ujao”, alisema.

Kuhusu lini itakuwa siku ya mwisho, kocha huyo kijana alitanabaisha kuwa, mchakato huu wa kuska vipaji ulikuwa ufikie tamati hapo kesho lakini uongozi wa City umeamua kusogeza mbele mpaka siku ya jumamosi  ambapo wachezaji watakaopatikana kwenye mchujo wa kesho  watapata nafasi ya kucheza mchezo mmoja wa  kirafiki na timu ya  Ilemi Fc.

“Ilikuwa tuhitimishe kesho lakini tumesogeza mpaka jumamosi ambapo vijana wetu wapya watakaopatikana watacheza mchezo wa kirafiki , na baada ya hapo zoezi litafungwa tayari wa kusubiri maandalizi ya msimu mapema mwezi ujao” alimaliza.

CAF YAMTEUA MICHAEL WAMBURA


Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), limemteua Michael Richard Wambura kuwa Kamishna wa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Rwanda na Msumbiji unaotarajiwa kufanyika jijini Kigali, Juni 3, 2016.

Wambura ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), atakuwa Balozi mzuri katika mchezo huo unaokutanisha timu ambazo nchi imepana nazo. Msumbiji iko Kusini mwa Tanzania wakati Rwanda iko Magharibi mwa Tanzania.

TFF KUTOANDAA KOMBE LA KAGAME


Shirikisho a Soka Tanzana (TFF), limetangaza kutoandaa michuano ya kuwania Kombe la timu za nchi wanachama wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), maarufu kama Kombe la Kagame kwa mwaka 2016 kama ilivyopendekezwa.

Sababu za TFF ya kutoandaa fainali hizo ni kwa kubanwa na ratiba ya michuano ya kitaifa na kimataifa.

Awali mkutano mkuu wa CECAFA, uliamua Zanzibar iwe mwenyeji wa michuano ya Kagame.

Baadaye kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa ilionekana Zanzibar hawataweza kufanya.

Baada ya hapo TFF ilianza kuangalia uwezekano wa mashindano haya kwa kumshirikisha mabingwa wa 2015/16 ambao ni Yanga.

Kutokana na ratiba ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAFCC) iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), kipindi ch Juni hadi Agosti, 2016 Yanga watakuwa na kwenye michuano ya CAF hatua ya makundi hivyo ushiriki wao CECAFA utakuwa mgumu ilihali michuano ya CECAFA imepangwa kufanyika Juni na Julai, mwaka huu.

MBEYA CITY YAANZA KUSAKA NYOTA WAPYA



SIKU  chache baada ya pazia  la ligi kuu ya soka Tanzania  bara kufungwa,Kocha mkuu wa Mbeya  City Fc  Kinnah Phiri ameanza zoezi maalumu la kusaka nyota wapya ambao atawajumuisha  moja kwa moja kwenye vikosi vya timu yake  msimu ujao.

Akizungumza muda mfupi baada ya majaribio ya siku ya kwanza  kwa wachezaji wapya vijana waliofika kujaribu bahati zao kwa kuonyesha  vipaji walivyonavyo navyo, afisa habari wa City Dismas Ten amesema kuwa muitikio umekuwa mzuri katika siku hii kwanza ambayo nyota hao wa baadae wamefika kuonysha  uwezo wao mbele ya kocha huyo raia wa malawi.

“Leo ni siku ya kwanza, kitu kizuri mwitikio umekuwa mkubwa, takribani vijana 50 wamejitokeza kujaribu  bahati zao kulingana na vipaji walivyonavyo, haya ni majaribio ambayo kocha Phiri ameyaitisha ili kusaka vipaji vipya ambavyo moja kwa moja vitaingia kwenye timu yetu kubwa na ile ya U20, alisema.

Akiendelea zaidi, Ten  alisema kuwa,  hii  imekuwa ni kawaida kwa City kila inapofika mwisho wa msimu kuwaleta  pamoja vijana wote wanaoamini wanauwezo wa kucheza mpira, kufichua  vipaji vyao ili waje kuwa wachezaji wakubwa  baadae.

“Hii ni kawaida yetu, kila tunapomaliza msimu huwa tunafanya hivyi, vijana wote wenye umri kuanzia miaka 17-22 ni fursa kwao kujitokeza, zoezi hili la kusaka vipaji  litakuwepo kwa juma zima, leo hatukuwa na kocha Phiri kwa sababu  alikuwa kwenye majukumu mengine lakini kesho tutakuwa  kwenye uwanja Sokoine na mwalimu  atakuwa, kwa hiyo vijana wote ndani ya jiji la Mbeya na mikoa ya jirani waje kujaribu bahati zao.

Kwa upande wa vijana waliojitokeza siku ya leo, walishukuru kuwepo kwa zoezi hili kwa sababu limerahisisha  uwezekano wa vipaji walivyonavyo kuonekana mapema hatimaye waweze kutimiza ndoto zao za kuwa wachezaji wakubwa  siku za usoni

Thursday, May 26, 2016

YANGA BINGWA KOMBE LA FA


MABINGWA wa soka wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana walifanikiwa kuongeza taji lingine baada ya kuibwaga Azam mabao 3-1.

Yanga, ambayo imefuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika, imetwaa Kombe la FA, baada ya kuibuka na ushindi huo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Yanga imezawadiwa kitita cha sh. milioni 50, ikiwa ni siku chache baada ya kuzaliwa sh. milioni 80, kutokana na kutwaa ubingwa wa ligi kuu.

Mshambuliaji Amis Tambwe aliendelea kuibeba Yanga baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu. Bao lingine lilifungwa na Deus Kaseke.

Bao la kufutia machozi la Azam lilifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Didier Kavumbagu, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya John Bocco.

Tuesday, May 24, 2016

KUZIONA YANGA, AZAM BUKU TANO



KIINGILIO cha chini katika Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Yanga SC na Azam FC kitakuwa ni Sh.5,000.
 

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema leo kwamba kiingilio cha Sh. 5,000 kitahuus majukwaa yote ya mzunguko. Lucas ametaja viingilio vingine kuwa ni Sh 25,000 kwa VIP A na Sh 20,000 kwa VIP B na C.

Sherehe za mchezo huo zitaanza rasmi saa 8.00 mchana kwa mchezo wa awali wa kuburudisha kuzikutanisha timu za soka za kituo cha Televisheni cha Azam ‘Azam Tv’ na wafanyakazi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kurushwa live na kituo hicho kilichotokea watazamaji wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

YANGA YAPANGWA KUNDI MOJA NA TP MAZEMBE




YANGA SC imepangwa kundi la A katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa na timu za
TP Mazembe ya DRC, MO Bejaia ya Algeria na Medeama ya Ghana.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo hatua ya makundi, iliyopangwa leo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kundi B linaundwa na timu za Kaskazini mwa Afrika, ambazo ni mabingwa watetezi, Etoile du Sahel ya Tunisia, Ahly Tripoli ya Libya, FUS Rabat na Kawkab zote za Morocco.
 

Monday, May 23, 2016

WAAMUZI 40 KUCHEZESHA LIGI YA MABINGWA WA MIKOA



Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeteua waamuzi 40 watakaochezesha Ligi ya Mabingwa Mikoa (RCL) inayoanza leo Mei 23 katika vituo vinne tofauti hapa nchini.

Ligi hiyo inayoshirikisha timu 27, imegawanywa katika makundi manne ambako bingwa katika kila kundi atapanda daraja hadi Ligi Daraja la Pili msimu wa 2016/17 ngazi ya taifa kabla ya kutafuta nafasi ya kucheza Ligi daraja la Kwanza msimu wa 2017/18.

Timu tano zitapanda daraja hadi Ligi Daraja la Pili ambako mbali ya washindi katika vituo vyote vinne, mshindwa bora katika vituo vya Njombe, Morogoro na Singida nayo itapanda daraja kwa kuangalia vigezo vya wingi wa pointi, wastani wa mabao, mabao kufunga na mabao ya kufungwa. Kituo cha Kagera hakijajumuishwa kwa kuwa kina timu shiriki sita.

Waamuzi walioteuliwa kuchezesha ligi hiyo kwa kituo cha Njombe ni Elasto Msaliwa, Klement Manga, Mashaka Lulambo, Lazaro Mbogoro, Michael Mkongwa, Alex Chitalula, Maulid Makiwa, Michael Kilango, Edina Ndelwa na Haidal Kisingile.

Timu zinazoshiriki ni Mkali Stars ya Ruvuma, Mtwivila (Iringa), Sido FC (Mbeya), Jangwani FC ya Rukwa, Nyundo FC ya Katavi, Mawezi ya Morogoro na Zimamoto ya Ilala, Dar es Salaam.

Kituo cha Morogoro walioteuliwa ni Athuman Lazi, Mohammed Theophil, Seleman Kinugane, Fikiri Yusuph ‘Magari’, Nicolaus Makangara, Mwarabu Mumba, Emmanuel Muga, Herry Shao, Shaban Juma na Makongo Katuma na timu zinazoshiriki ni Stend  FC ya Pwani, Mbuga FC (Mtwara), Namungo FC(Lindi), Muheza United ya Tanga, Stand Misuna FC ya Singida, Makumbusho ya Kinondoni na Sifa Politan SC ya Temeke, Dar es Salaam.

Kituo cha Singida wako Meshack Suda, Abdallah Mwinyimkuu, Sarah Bongi, Lucas Mathias, Amani Mwaipaja, Siyachitema Kawinga, Theophil Tegamaisho, Shaaban Msangi, Aboubakar Irume na Frederick Ndahani na timu shiriki ni Veyula FC (Dodoma), Pepsi SC (Arusha), Kitayosce FC (Kilimanjaro), Stand FC (Tabora), Murusagamba FC (Kagera), Fire Stone (Manyara) na Tomato FC (Njombe).

Kituo cha Kagera walioteuliwa ni Jonesia Rukyaa, Jamada Ahmada, Ringston Rwiza, Grayson Buchard, Grace Wamala, Edgar Lyombo, Yahaya Juma, Adrian Karisa, Getrude Kahawa na Ahmada Simba na timu shiriki ni Geita Town Council Fc (Geita), Gold Sports Academy (Mwanza), Kabela City (Shinyanga), Ambassador FC (Simiyu), Igwe FC (Mara) na Mashujaa (Kigoma).

ISRAEL MUJUNI KUZIHUKUMU YANGA NA AZAM KESHO


Mwamuzi mahiri nchini, Israel Mujuni Nkongo wa Dar es Salaam, Jumatano Mei 25, 2016 ameteuliwa kuwa mwamuzi atakayechezesha mchezo wa fainali za Kombe la Shirikisho maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayozikutanisha timu za Young Africans na Azam FC; zote za jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo utakaoanza kesho saa 10.30 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam waamuzi wasaidizi watakuwa Ferdinand Chancha wa Mwanza (line 1) na upande wa pili ni Soud Lila wa Dar es Salaam (line 2) na mwamuzi wa akiba mezani ni Frank Komba wa Dar es Salaam pia. Kamishna wa mchezo huo anatakuwa Juma Mgunda wa Tanga.

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu msimu 2015/16, mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu 2015/16 wataiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2016/17. Nafasi hiyo imechukuliwa na Young Africans.

Kadhalika Azam ina tiketi tayari ya kushiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kufika fainali za ASFC ingawa kanuni zinataka bingwa ambako kwa upande wa Yanga wana tiketi ya michuano ya juu zaidi ya shirikisho. Mvuto wa mchezo wa Jumatano ni ushindani wa soka na zawadi kwa bingwa.

Fainali za Kombe la Shirikisho zinakuja baada ya mchuano ulioshindanisha timu 64 za Ligi Kuu Tanzania Bara - VPL (16); Ligi Daraja la Kwanza -FDL (24), Ligi Daraja la Pili – SDL (24).

DRFA,YAJIVUNIA KLABU ZAKE KUMALIZA MSIMU 2015/2016 KWENYE NAFASI ZA JUU


Chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA imezipongeza klabu zake tatu za ligi kuu kwa kumaliza katika nafasi za juu kwenye michuano ya ligi kuu soka tanzania bara.


Timu hizo ni Yanga SC iliyomaliza katika nafasi ya kwanza,Azam FC iliyomaliza katika nafasi ya pili na Simba SC  iliyomaliza katika nafasi ya tatu.
 

Mwenyekiti wa DRFA,Almas Kasongo amesema mafanikio hayo wanayapeleka moja kwa moja kama zawadi kwa mkuu wa mkoa wa Dar  es salaam Mh .Paul  Makonda,ambaye ameonesha mchango mkubwa kwa kuhimiza watu kupenda michezo.
 

Amesema kama chama hawana budi kujivunia mafanikio hayo na kuwapongeza wachezaji,walimu na viongozi wa vilabu vyote vitatu kwa hatua hiyo inayozidi kuupamba mkoa wa Dar es salaam kisoka.

MAKUMBUSHO,SIFA POLITAN,ZIMA MOTO ZATAKIWA KILA LA KHERI LIGI ZA MIKOA.
 

DRFA,inazipongeza timu za Makumbusho FC,Sifa Politan na Zima Moto kwa kufanikiwa kuingia katika ligi za mikoa baada ya kufanya vizuri katika michezo yao.
 

Klabu ya Zima Moto itakwenda kucheza mkoani Njombe,wakati Makumbusho na Sifa Politan wanakwenda kucheza mkoani Morogoro.
 

Pia klabu ya Abajalo FC  nayo imepongezwa kwa mafanikio ya kutinga ligi daraja la kwanza,na kuwataka kuzidisha mapambano ili wapige hatua nyingine zaidi ya kufika ligi kuu.

JUMA ABDUL MWANASOKA BORA WA MWEZI APRILI


Beki wa kulia wa timu ya soka ya Young African ya Dar es Salaam, Juma Abdul ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Aprili, 2016 baada ya kura zake kuwashinda Donald Ngoma ambaye pia anakipiga Young Africans na Hassan Dilunga wa JKT Ruvu ya Pwani.

Katika rekodi za Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) iliyoketi Jumamosi Iliyopita, imeonesha kwamba Abdul alicheza mechi zote tano za Ligi Kuu kwa mwezi Aprili ambapo pia aliifungia timu yake bao katika harakati za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/16.

Rekodi hizo pia zinaonyesha kwamba beki huyo hakuonyeshwa kadi hata moja katika michezo hiyo mitano sambamba na kutoa mchango mkubwa katika michezo aliyoshiriki kwa mwezi Aprili, 2016. Abdul atazawadiwa fedha Sh. 1,000,000 (milioni moja) na wadhamini wa Ligi hiyo, Kampuni ya mahiri ya simu za mkononi ya Vodacom.

Uwezo aliouonyesha Abdul ulisababisha Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kumjumuisha katika kikosi chake kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Harambee Stars ya Kenya kadhalika Mapharao wa Misri katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Juni 4, mwaka huu.

Wachezaji bora wa miezi minne iliyopita ni kiungo Thaban Kamusoko wa Young Africans (Desemba 2015), beki Shomari Kapombe wa Azam (Januari 2016), Mshambuliaji Mohamed Mkopi wa Tanzania Prisons (Februari 2016) na Shiza Ramadhani Kichuya wa Mtibwa Sugar (Machi 2016).

RAIS WA FIFA AIPONGEZA YANGA



Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ameipongeza timu ya soka Young Africans ya Dar es Salaam, kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2015/16.

Young Africans imetwaa ubingwa huo kwa msimu wa pili mfululizo, lakini ikiwa ni mara ya 26 tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara mwaka 1965.

Katika salamu zake, kupitia barua yake ya Mei 18, 2016 kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi, Infantino ameelezea ubingwa wa Young Africans kwamba umetokana na kazi kubwa inayofanywa na uongozi wa timu hiyo, makocha, wachezaji pamoja na mashabiki.

“Yanga ndiyo mabingwa wa Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Young Africans na timu nzima isiyoshindika kwa mafanikio haya makubwa. Taji la Young Africans ni matokeo ya mshikamano ulioko ndani ya Young Africans,” amesema Infantino katika barua hiyo yenye kichwa cha habari kinachosema: Salamu za Pongezi kwa Young Africans.

Amesema pongezi zake ziende kwa uongozi wa klabu, makocha na benchi nzima la ufundi, wachezaji, madaktari pamoja na mashabiki wote wa Young Africans.

“Kwa niaba ya familia ya soka, napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Young Africans na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa jinsi mnavyopeleka ujumbe chanya wa soka kwa jamii ya michezo,” alisema Infantino katika barua hiyo iliyotua TFF Mei 21, mwaka huu.

Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikwisha kuipongeza Yanga ambayo imepewa Kombe na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji na kwa sasa wanasubiri zawadi ya fedha Sh 81,345,723.

AIRTEL YAPANGA MIKAKATI YA MAENDELEO SOKA LA VIJANA


Kampuni ya Airtel Tanzania jana Ijumaa Mei 20, 2016 imekutana na Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) kuzungumzia mipango ya maendeleo wa mpira wa miguu nchini ikiwa ni pamoja na michuano ya vijana chini ya umri 17 ya Airtel Rising Stars inayotarajiwa kuanza Juni mwaka huu.

Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa Selestine ambaye ndio aliongoza kikao hicho, alitoa shukrani ka kampuni ya Airtel kwa kuwekeza kwenye soka la vijana ambalo ndio msingi wa kukuza mpira wa miguu nchini. “Naamini ya kwamba kwa kuendelea kuwekeza kwenye soka la vijana, tutaweza kufika mbali kwa kupata matokeo mazuri.”

Tangu kuanzisha kwa michuano ya Airtel Rising Stars miaka mitano iliyopita, soka la vijana nchini imekuwa na mafanikio makubwa“Leo, Timu ya Taifa chini ya miaka 20 – Serengeti Boys, imeundwa na vijana ambao wamekuwa ni chimbuko la Airtel Rising Stars,” alisema Selestine na kuongeza kuwa hata timu ya Taifa ya Wanawake – Twiga Stars, Klabu za Liguu na zile zinazoshiriki ligi daraja ya kwanza, zinatumia wachezaji ambao wamekuzwa kwa michuano ya Airtel Rising Stars.

Airtel imeweza kuiwezesha TFF kufika maeneo ambayo yamekuwa ni vigumu kufika kutafuta vipaji. Kwa kufanya hivyo, tuweza kupata vijana wenye vipaji vingi na hata kwa sasa hivi, baadhi yao wako na Timu ya Taifa ya Vijana Serengeti kushiriki michuano ya Kimataifa inayoendelea India, alisema Mwesigwa.

Katibu Mkuu huyo wa TFF aliomba Airtel kuendelea kudhamini miradi ya soka ya vijana kwa vile ndio njia pekee Tanzania inaweza kuwa na timu bora na imara ya Taifa. Nchi nyingi zinazofanya vizuri kwenye michuano mbali mbali ya soka ni kwa vile waliweza kuwekeza kwenye program mbali mbali za vijana kama vile Airtel Rising Stars. Kwa kushirikiana na nyinyi, tutaweza kupata na kukuza vipaja vya soka ambazo watakuwa na msaada mkubwa kwenye timu ya Taifa.

Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema “kampuni yake itaendelea kudhamini program za soka la vijana ambazo zimeweza kuwa na mafanikio makubwa kwa miaka mitano iliyopita. Lengo letu ni kuwa na timu ya taifa bora kama vile Misri, Cameron, Nigeria, Ivory Coast na Ghana,” alisema Mmbando huku akisisitiza njia pekee ya kufikia mafanikio hayo ni kuwekeza na kukuza soka la vijana.

Airtel pia imetoa shukrani kwa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Michezo na Sanaa pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ushirikiano wao ambao umeifanya Airtel Rising Stars kuwa moja ya mashindano yenye mafanikio makubwa hapa Tanzania. Bila ushirikiano na serikali pamoja na wadau wa soka hapa nchini, Airtel Rising Stars hangeweza kufika hapa ilipo kwa leo, alisema Mmbando.

Mmbando alisema kwa mwaka huu, Tanzania haitashiriki kwenye michuano ya kimataifa ambayo huleta pamoja wachezaji waliong’ara kwenye nchi zao Barani Afrika kwa ajili ya kubadilisha uzoefu, bali itashirikiana na TFF kuweka mikakati  mingi zaidi ya kuwawezesha vijana hawa kufanya vyema hata baada ya mashindano ya Airtel Rising Stars kwisha.

Tayari Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi amepanga ratiba kamili ya michuano hiyo kwa mwaka huu ambako kwa sasa inajadiliwa na itatoa wakati wowote wiki ijayo.

YANGA, AZAM SASA KUKIPIGA KESHO FAINALI YA KOMBE LA FA


Fainali za kuwania Kombe la Shirikisho, maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), zitakazokutanisha timu za soka ya Young Africans na Azam FC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam sasa zitafanyika kesho (Mei 25, 2016) kama ilivyotangazwa awali.

Awali fainali hizo zilipangwa Juni 11, 2016 ili kuzipa muda wa kuajindaa timu mara baada ya michezo ya mwisho ya Ligi Kuu ya Vodacom inayotarajiwa kufikia ukomo Mei 22, 2016, lakini imeachwa tarehe ya awali ili kuenenda na kanuni ya tarehe ya mashindano kwani mwisho wa msimu ni Mei 31, mwaka huu.

Kadhalika tarehe ya awali ilipangwa kutokana ratiba kubana hasa ya timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambayo ina mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’ unaotarajiwa kufanyika Mei 29, mwaka huu. Mchezo huo unaingia kwenye kalenda ya FIFA.

Taifa Stars itacheza mechi hiyo ikiwa ni maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Misri unaotarajiwa kufanyika Juni 4, 2016 jijini Dar es Salaam kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Tayari TFF imefafanua iwapo Bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa msimu 2015/16 inayoendelea atashinda pia taji katika fainali za Kombe la Shirikisho la ASFC, ndiye atayeiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya mabingwa wa Afrika msimu wa 2016/17.

Kwa msingi huo, timu itayopoteza fungwa katika fainali hizo za Kombe la Shirikisho –ASFC linalodhaminiwa na kituo cha Televisheni cha Azam, ndiyo itakayowakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika katika msimu wa 2016/17

Fainali za Kombe la Shirikisho zinakuja baada ya mchuano ulioshindanisha timu 64 za Ligi Kuu Tanzania Bara - VPL (16); Ligi Daraja la Kwanza -FDL (24), Ligi Daraja la Pili – SDL (24)

MKWASA ATANGAZA KIKOSI KITAKACHOIVAA MISRI



Kocha Mkuu wa timu ya Soka ya Tanzania, Charles Boniface Mkwasa ameita kikosi cha wachezaji 27 watakaounda Taifa Stars ambacho kinajiandaa kucheza Misri Juni 4, 2016 katika mchezo wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON-2017).

Mkwasa maarufu kama Master, alitangaza kikosi cha timu hiyo leo Mei 18, 2016 mbele ya Kocha Msaidizi, Hemed Morocco na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kuiva Misri, kikosi hicho kitafunga safari hadi Kenya kucheza na Harambee Stars katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa ambao wenyeji wameuombea Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwamba utambulike na kuingia kwenye rekodi za kimataifa ikiwa ni pamoja na kuingia kwenye mchakato wa kupima viwango vya soka.

Katika kikosi hicho, Mkwasa amemuita beki Mlinzi mahiri wa Young Africans, Nadir Haroub maarufu kama Cannavaro huku akimwacha beki mwingine wa Young Africans, Kelvin Yondani kwa sababu ya sentahafu huyo anatumikia kadi mbili za njano alizoonywa katika michezo iliyopita.

“Yondani ana kadi mbili za njano,” amesema Mkwasa ambako katika kikosi chake amewateua makipa, Deogratius Munishi (Young Africans), Aishi Manula (Azam FC) na Benny Kakolanya (Tanzania Prisons) wakati mabeki ni Horoub, Mwinti Haji na Juma Abdul (Young Africans), Aggrey Moris, David Mwantika na Erasto Nyoni (Azam FC), Mohammed Hussein (Simba) na Vicent Andrew (Mtibwa Sugar).

Viungo ni Himid Mao, Farid Mussa (Azam), Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto (Simba), Mohammed Ibrahim na Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar), Ismail Issa (JKT Ruvu), Juma Mahadhi (Coastal Union) na Hassan Kabunda (Mwadui FC) wakati washambuliaji ni Thomas Ulimwengu (TP Mazembe), Mbwana Samatta (KDC Genk), Elias Maguli (Stand United), Ibrahim Ajib (Simba), John Bocco (Azam), Deus Kaseke (Young Africans) na Jeremiah Juma (Tanzania Prisons).

Saturday, May 7, 2016

TFF YATOA UFAFANUZI USHIRIKI WA MICHUANO YA KIMATAIFA




Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lingependa kutoa ufafanuzi kuwa iwapo Bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa msimu 2015/16 inayoendelea atashinda pia taji katika fainali za Kombe la Shirikisho maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), ndiye atayeiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya mabingwa wa Afrika msimu wa 2016/17.

Kwa msingi huo, timu ambayo itafungwa katika fainali hizo za Kombe la Shirikisho –ASFC linalodhaminiwa na kituo cha Televisheni cha Azam, ndiyo itakayowakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika katika msimu wa 2016/17

Fainali za Kombe la Shirikisho zinatarajiwa kufanyika baadaye mwezi ujao, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya mchuano uliohusisha timu 64 za Ligi Kuu Tanzania Bara - VPL (16); Ligi Daraja la Kwanza -FDL (24), Ligi Daraja la Pili – SDL (24).

YANGA, ESPERANCA KAZI IPO LEO


Uongozi wa Young Africans ya Dar es Salaam, umekamilisha maandalizi yote muhimu ya mchezo dhidi ya GD Sagrada Esperanca ya Angola wa kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho la Barani Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho Jumamosi Mei 7, saa 10:00 jioni.

Mchezo huo utakaochezeshwa na waamuzi kutoka Ghana ukisimamiwa na kamishna kutoka Ethiopia.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro ametaja viingilio vya mchezo huo kuwa Jukwaa la VIP “A” kuwa ni Sh 30,000; VIP “B” na “C” Sh 20,000 wakati jukwaa la viti Rangi ya chungwa ni Sh 7,000 wakati mzunguko wa viti vya bluu na kijani ni Sh 5,000.

Kwa mujibu wa Muro, Yanga itawakosa wachezaji mahiri wawili, Donald Ngoma na Thaban Kamusoko ambao watatumia mchezo huo kutumikia adhabu ya kadi mbili za njano walizoonywa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kushuka kucheza Kombe la Shirikisho.

“Tunawaomba wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga tujitokeze kwa wingi kesho kuishangilia timu yetu kwa nguvu na kasi kubwa,” amesema Muro ambaye alitumia nafasi hiyo kutamba kwamba Yanga ilisajili wachezaji 24 kwenye michuano inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).

FIFA YAITOZA FAINI SIMBA



Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), limeipiga faini ya Franc 2,000 za Uswisi (sawa na Sh 4,582,000 za Tanzania), Klabu ya Simba baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kupuuza maagizo ya Idara ya Utatuzi wa Migogoro (Desputes Resolution Chamber) ya shirikisho hilo.

Kamati ya idara hiyo iliyokutana na Aprili 20, 2016 huko Zurich, Uswis ilitumia Franc 500 (sawa na Sh 1,145,500) hivyo Simba pia imeagizwa kuzilipa ikiwa ni gharama za kikao cha kufuatilia utekelezaji sakata la mchezaji huyo, raia wa Kenya.

Simba imeelezwa kupuuza kumlipa mchezaji Donald Musoti Omanua kwa wakati tangu mkataba wake uvunjwe. Musoto aliyesajiliwa na Simba msimu wa 2014/15 na kuachwa alilalamika FIFA ambayo iliona ana hoja na hivyo Simba kutakiwa kumlipa dola 29,250 (sawa na Sh 62.8 milioni) na kiasi kingine anachodai ni Dola 600 (Sh 1,290,000) zilizobaki katika usajili ambapo jumla yake ni Sh 64.2 milioni. Pia Mosoti anamlipa Mwanasheria wake dola 2,000 (Sh 4.3 milioni) kwa ajili ya kusimamia kesi hiyo.

Felix Majani, Mwanasheria wa Musoti, ambaye pia ni mmoja wa wanasheria wa FIFA, alifungua kesi katika shirikisho hilo kuwashitaki Simba kwa kukiuka makubaliano ya mkataba na mteja wake.

Kwa kosa hilo Simba inatakiwa kulipa faini ya kiasi hicho cha fedha ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya kupokea barua hiyo ya FIFA iliyoandikwa Mei 3, mwaka huu na kufika Tanzania leo Mei 6, 2016. TFF imekuwa nakala na maagizo kuisimamia Simba inalipa kiasi hicho cha fedha.

Simba imeagizwa kulipa stahiki zote za Mosoti ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya kupokea barua hiyo ya FIFA iliyoandikwa Mei 3, mwaka huu na kufika Tanzania leo Mei 6, 2016.

Katika barua hiyo ambayo TFF ina nakala yake, Simba imepewa amri ya kuhakikisha inalipa na isipotekeleza agizo hilo mara moja itakatwa pointi tatu katika mechi zake Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara –VPL.

FIFA imekwenda mbali zaidi ikisema ikiwa klabu hiyo kama haitalipa katika muda uliopangwa yaani siku 30 kutoka sasa, FIFA itaishusha Simba daraja kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara hadi Ligi Daraja la Kwanza au zaidi.

Kwa upande wake, TFF imagizwa kuhakikisha uamuzi huo unasimamiwa vema utekelezwaji wa maagizo hayo vinginevyo itachukuliwa hatua stahiki ikiwamo kuiondoa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

MBEYA CITY YAIUNGA MKONO TFF KUIPOKA POINTI AZAM



Mwenyekiti wa Mbeya City  fc, Mussa Mapunda amelipongeza shirikisho la  soka Tanzania  TFF kwa hatua yake ya kuipoka  pointi 3 timu ya Azam Fc  kufuatia  makosa yaliyofanywa na timu hiyo ya  Chamazi Complex  kumchezesha mchezaji Erasto Nyoni aliyekuwa na zuio la kadi tatu za njano.

Muda mfupi uliopita Mapunda ameimbia mbeyacityfc.com kwamba kwa kosa  hilo City ilistahili kupata ushindi huo wa bao 3 na pointi 3 kama ambavyo kanuni za ligi  zinavyoelekeza na kutoa  angalizo kwa vilabu vyote vinavyoshiriki ligi kuu Tanzania  bara kuongeza umakini katika  kutunza  kumbukumbu  za adhabu  au makosa mbalimbali kwa wachezaji wake.

“Kwenye hili nalipongeza shirikisho, hakika wametenda haki, na ninawaomba  waendelee kusimama kwenye misingi ya haki, ni haki yetu kupata pointi 3 baada ya Azam fc kuchezesha mchezaji mwenye adhabu ya kadi 3 ambaye ni wazi hakustahili kucheza mchezo ule, hata sisi tumekutana na hali hii katika nyakati tofauti lakini hatukuwahi kuthubutu kumchezesha mchezaji  mwenye adhabu  hata kama alikuwa ni muhimu kikosini” alisema.

Akiendelea zaidi Mwenyekiti Mapunda alisisitiza vilabu kuwa makini na matukio ya aina hii  huku pia  akiikumbusha TFF kuendele kuchukua hatua kama hizi.

Katika hatua nyingine  Mapunda amesema kuwa  bado anaamini TFF itaitendea haki City kwa kuchukua hatua kama hizi kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union uliovunjika  dakika mwisho za kipindi cha pili baada ya kutokea kwa vurugu kubwa  uwanjani zilizosababishwa  na mashabiki wa timu hiyo ya Tanga .

“Naamini TFF watatutendea haki kwenye hili pia, kwa sababu  tushapeleka malalamiko muda mrefu,mchezo ule ulikuwa na matukio mengi ya ajabu ambayo yalimfanya mwamuzi kushindwa kumaliza mchezo, risasi za moto zilipigwa  uwanjani, , sisi bado tunasubiri pointi tatu zingine kutoka kwenye mchezo ule, kwa sababu mnyonge mnyongeni  haki yake mpeni”, alimaliza.

Friday, May 6, 2016

WAAMUZI KUTOKA GHANA KUZICHEZESHA YANGA NA ESPERANCA



Mwamuzi Joseph Odartei Lamptey, Jumamosi Mei 7, 2016 anatarajiwa kuwa mwamzi wa kati katika mchezo wa kimataifa kuwania Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaozikutanisha timu za Young Africans ya Dar es Salaam, Tanzania na GD Sagrada Esperanca ya Angola.

Lamptey kutoka jiji la Accra, Ghana atasaidiwa na raia wenzake wa nchi hiyo kuchezesha mchezo huo Na. 99. Mwamuzi Msaidizi Na. 1 (line 1) ni David Laryea wakati Mwamuzi Msaidizi Na. 2 (line 2) ni Malik Alidu Salifu.

Mwamuzi Msaidizi mezani (Fourth Official) ni Cecil Amately Fleischer huku Kamishna wa mchezo huo, akiwa ni Asfaw Luleseged Begashaw wa Ethiopia.

Viingilio na upatikanaji wa tiketi utatangazwa kesho Ijumaa Mei 6, 2016 na uongozi wa klabu ya Young African mara baada ya mkutano kati ya makocha wa timu zote mbili. Mkutano wa makocha hao utafanyika saa 5.00 mchana kwenye Ukumbi wa mikutano wa TFF.

AZAM YAPOKWA POINTI TATU ZA LIGI KUU


Timu ya Azam FC ya Dar es Salaam, imenyang'anywa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu uliyoupata katika mechi Na. 156 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City.

Uamuzi huo umetokana na Azam kumtumia mchezaji Erasto Nyoni kwenye mechi hiyo wakati akiwa na kadi tatu za njano. Mchezo huo ulifanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 37(4) ya Ligi Kuu Toleo la 2015 inayoelekeza kuwa mchezaji atakayeonywa kwa kadi ya njano katika michezo mitatu hataruhusiwa kucheza mchezo unaofuata wa timu yake. Hivyo kwenda kinyume na Kanuni husika.

Pia kwa kuzingatia Kanuni ya 14(37) ya Ligi Kuu Toleo la 2015, timu ya Mbeya City imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.

Kadhalika Bodi ya Ligi imelionya Benchi la Ufundi la timu hiyo kuongeza umakini katika utunzaji wa kumbukumbu za kadi za wachezaji wake. Pia imezikaribisha timu zote wakati wowote kuomba kumbukumbu zozote kila zinapozihitajika.

KANUNI ZA LIGI KUREKEBISHWA



Bodi ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka (TFF) imezipongeza timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushiriki na kufanya msimu wa Ligi Kuu Bara kuwa ya Vodacom 2015/16 kuwa wenye mafanikio.

Bodi hiyo imezifahamisha klabu zitakazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2016/17 kuwa mchakato wa wa utengenezaji kanuni umeanza.

Bodi ya Ligi kwa sasa inakaribisha maoni, mapendekezo, marekebisho kutoka klabu ili kuboresha uendeshaji wa ligi. Maoni hayo yanapokelewa kwa njia ya maandishi moja kwa moja kwenye ofisi za bodi au kwa njia ya barua pepe.

Thursday, May 5, 2016

FILAMU YA IMEBUMA YAPIGWA STOP


Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Joyce Fisso akizungumza na waigizaji wa filamu ya “Imebuma” (Hawapo Pichani) wakati wa ukaguzi wa filamu hiyo kabla ya kupelekwa sokoni kulia ni 2 Afisa Utamaduni Bw. Julius Tairo.

Na Shamimu Nyaki WHUSM

Bodi ya Filamu Tanzania imesitisha usambazaji wa filamu ya “Imebuma” mpaka pale maudhui yake yatakapofanyiwa marekebisho.

Akisitisha usambazaji wa filamu hiyo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi Joyce Fisso amesema mtengenezaji wa filamu hiyo hana kibali cha kutengenza filamu kutoka Bodi ya Filamu na hajazingatia Sheria na kanuni za utengenezaji wa filamu.

Bi Joyce Fisso amesema filamu hiyo imesitishwa kwenda sokoni kutokana na kukiuka vifungu vya kanuni za sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 2011 ambayo inakataza kuonesha namna yoyote ya udhalilishaji wa kibinadamu katika filamu na maigizo.

“Baada ya kuangalia kwa makini filamu hii na kuona mapungufu ambayo yanakinzana na Kanuni za Sheria ya filamu na Michezo ya kuigiza  nimeamua kuisitisha usambazaji wake mpaka pale wahusika watakaporekebisha maudhi yake” Alisema Bi Joyce.

Bi Joyce amefafanua kuwa filamu hiyo imeonesha baadhi ya matukio ya udhalilishaji wa kibinadamu, ushawishi wa matendo ya ngono na ushoga ambayo ni kinyume na madili ya mtanzania.

Aidha kwa upande wake Afisa Utamaduni kutoka Bodi ya Filamu Tanzania Bw. Julius Tairo amewataka waandaaji na waigizaji wa filamu nchini kufanya utafiti wa kutosha kuhusu maudhui ya filamu kabla ya kutengeneza ili kuondokana na  utengenezaji wa filamu zisizofata Sheria na kanuni za utengenezaji wa filamu Tanzania.

SERIKALI YAUFUNGIA WIMBO WA CHURA WA SNURA


Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Zawadi Msalla (katikati) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapopichani) wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu kusitishwa kwa wimbo wa Msanii Snura Mushi ujulikanao kwa jina la Chura kwa kukiuka maadili kushoto ni Mwanasheria wa wizara hiyo Bw. Patrick Kipangula na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utamaduni Bibi. Lily Beleko.
Serikali imesitisha wimbo na Video ya Muziki wa Chura wa Msanii Snura Mushi  kuchezwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuanzia leo mpaka pale msanii  huyo atakapoifanyia marekebisho video ya wimbo huo.

Usitishwaji huo umetokana na maudhui ya utengenezwaji wa Video hiyo ambayo haiendani na maadili ya Mtanzania.

Pia Serikali imesitisha maonyesho yote ya hadhara ya mwanamziki huyo mpaka pale atakapo kamilisha taratibu za usajili wa kazi zake za Sanaa katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Serikali inawataka wasanii kujiuliza mara mbili kabla ya kubuni kazi zao za Sanaa. Wafikirie wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zao watazipokeaje? Wavae nafasi ya wale wanaowadhalilisha, Waelewe kwamba Sanaa si uwanja wa  kudhalilisha watu hata kidogo..

Aidha Serikali imechukizwa na kazi hiyo ambayo si tu inadhalilisha tasnia ya Muziki bali inadhalilisha utu wa mwanamke na inaifanya jamii kuanza kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya Sanaa kwa ujumla.

Serikali inawakumbusha wananchi wote kutokujiingiza katika makosa ya sheria ya mtandao kwa kusambaza wimbo huu kwa njia yoyote ile ya kimtandao

Pia inavitaka Vyombo vya habari viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi yoyote ya Sanaa kabla ya kuwa mawakala wa uharibifu wa jamii kupitia kucheza kazi chafu za Sanaa.

Serikali inatoa wito kwa wasanii wote kuzingatia maadili ya Kitanzania kabla ya kutoa kazi zao kwani haitawavumilia ‘wasanii’ wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya Sanaa kuwa sehemu ya uvunjifu wa maadili.

Imetolewa na Zawadi Msalla

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

RAMADHANI CHOMBO AIONYA YANGA



KIUNGO wa Mbeya  City ,  Ramadhani Chombo ‘Rendondo’ ameionya  timu ya Yanga  ya jijini Dar Es Salaam  kuwa  ijiandae vya  kutosha itakapokuja  jijini hapa mwanzoni mwa juma lijalo kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania  bara kati ya timu hizo mbili uliopangwa  kuchezwa kwenye uwanja wa Sokoine, Mei 10 mwaka huu.

Akizungumza na mbeyacityfc.com mapema leo, Redondo  aliyekosa michezo miwili ya awali kupisha majeraha ya mguu kabla ya kurejea na kuichezea City kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar aliweka wazi kuwa ana imani kubwa na kikosi cha sasa cha timu yake, hasa baada ya ujio  kocha Kinnah Phiri aliyefanikiwa kuyaondosha ‘makandokando’ yote yaliyokuwa nasababisha timu kufanya vibaya kwenye michezo iliyopita.

Nadhani Yanga wanatakiwa wajiandae vizuri, wanakuja  kukutana na kikosi  cha City ambacho kiko kwenye  wakati mzuri  hivi sasa,hivyo wasitegemee mteremko,ujio wa kocha  Phiri  umeiimarisha zaidi timu yetu, ametupa muongozo mzuri na amefanya kazi kubwa  kuweka timu sawa, hivyo hao wanaokuja wajue watakutana na upinzani mkali,timu yetu  sasa inacheza tofauti sana na ilivyokuwa inacheza hapo mwanzo, alisema.

Akiendelea  zaidi Redondo, aliyewahi kucheza kwa mafaniko kwenye  timu za Ashanti, Simba na Azam Fc alisema kuwa  anafahamu mchezo huu utakuwa mgumu pande zote  kwa sababu kila timu inahitaji matokeo kulingana na  hali ilivyo kwenye msimamo, Yanga  ikitaka  kujihakikishia ubingwa na City ikihitaji kujiweaka kwenye mazingira mazuri zaidi licha ya kuwepo kwa uhakika kuwa itasalia kwenye ligi .

Kuhusu majaaliwa yake kwenye kikosi cha City Redondo alisema kuwa  anaimani kubwa  atakuwa sehemu ya kikosi msimu ujao, na kuweka wazi furaha yake  ya  kuwa mchezaji wa timu hii tangu alipojounga nayo mapema  mwezi Januari.

“Nilijiunga na City mapema mwezi januari, nakumbuka  ilikuwa ni wakati wa usajiri wa dirisha dogo,  binafsi nina furaha  hapa na nitaka kufanya  kazi zaidi  na kwa uwezo wangu wote kwa sababu  lengo langu ni kuendelea kuwepo, kwa ngumi mimi  hii ni timu nzuri  kuliko zote nilizowahi kucheza, kuna wakati najiuliza kwa nini sikuwa huku mapema  lakini  hii ni soka na maisha ya mchezo huu ndiyo yalivyo”  alimaliza 

Wednesday, May 4, 2016

UCHAGUZI MKUU YANGA SASA JUNI 25, FOMU KUANZA KUTOLEWA



KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetangaza Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Yanga kuwa utafanyika Juni 25, 2016 badala ya Juni 5, 2016.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imelazimika kufanya hivyo kwa kuzingatia ushiriki wa Yanga ambayo inashiriki michuano ya kimataifa.
Sekretarieti ya Yanga ambayo ingefanya kazi kwa pamoja na Kamati ya Uchaguzi kwa kushirikiana na TFF kwa sasa inashughulikia pia kuiandaa timu kwa ajili ya michuano ya kimataifa.
Yanga inatarajiwa kucheza na Esperanca ya Angola katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Mei 7, mwaka huu kabla ya kurudiana kati ya Mei 17 na 18, mwaka huu huko Angola.
Kwa mujibu wa ratiba mpya, fomu za kuwania uongozi wa Yanga zitaanza kuchukuliwa Mei 25, 2016 na kwamba uchaguzi huo utafanyika ndani ya muda ambao Serikali kwa kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) iliagiza uchaguzi kufanyika kabla ya Juni 26, 2016 hivyo uchaguzi utafanyika ndani ya wakati.
Katiba itakayotumika ni ya mwaka 2010 na kwamba Wanachama wa Yanga watatumia kadi za kawaida za uanachama na si za benki.


Wakati huo huo, Yanga itaanza kutoa fomu kwa ajili ya wanachama wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia Mei 27 badala ya leo kama ilivyotangazwa awali na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, amesema leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, kwamba mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu hizo utakuwa ni Mei 29.
Kiongozi huyo alisema kuwa baada ya zoezi hilo Kamati ya Uchaguzi itaanza kusikiliza pingamizi zitakazokuwa zimewasilishwa huku orodha ya mwisho ya wagombea waliopitishwa ikitarajiwa kutangazwa Juni Mosi.
Aliongeza kuwa Juni Mosi hadi 4 itakuwa ni kipindi cha kampeni kwa wagombea waliopitishwa na uchaguzi mkuu utafanyika Juni 5 kwenye ukumbi utakaotangazwa hivi karibuni.
Alisema kuwa uchaguzi huo utasimamiwa na TFF baada ya kushindwa kufanya uchaguzi tangu mwaka 2014 muda wa viongozi waliokuwa madarakani ulipomalizika.
Kufanyika kwa uchaguzi huo kutatoa nafasi kwa viongozi wapya kusimamia usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na kufanya mabadiliko mengine ya katiba kwa kufuata maelekezo ya TFF.

KIPA WA ZAMANI SIMBA AACHIWA HURU, RUFANI YA GEITA GOLD MINE YAGONGA MWAMBA


KAMATI ya rufaa ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfutia adhabu ya kufungiwa miaka 10 kipa wa Simba, Denis Dioniz Richard.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Wakili Levocatus Kuuli amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba, Dennis aliyeadhibiwa wakati anacheza kwa mkopo Geita Gold ya Daraja la Kwanza, amefutiwa adhabu kwa sababu hakuna ushahidi wa kutosha dhidi yake.
Wakili Kuuli amesema walipitia rufaa za washitakiwa nane kati ya 22 waliotiwa hatiani kwa upangaji matokeo wa mechi za Daraja la Kwanza.
"Denis Dioniz Richard, kipa wa Geita ameachiwa huru kutokana na mapungufu yalikuwepo katika vifungu vya sheria za TFF,"amesema Wakili Kuulu.
Katika hatua nyingine, Kocha Msaidizi wa Geita, Abeid Choki ataendelea na kifungo chake cha kutojihusisha na mpira maisha baada ya rufaa yake kugonga mwamba.
Geita Gold Mining wataendelea na adhabu ya kushushwa daraja baada ya kubadilisha vithibitisho katika rufaa yao.
Kamisaa Salehe Mang'ola ataendelea na kifungo chake cha kutojihusisha na mpira maisha baada ya rufaa yake kugonga mwamba.
Katibu wa Chama cha Soka Tabora (TAREFA), Fate Remtulah, ataendelea na kifungo cha kutojihusisha na mpira maisha baada ya rufaa yake kushindikana.
Mwenyekiti wa TAREFA, Yusuph Kitumbo ataendelea kutumikia kifungo cha kutojihusisha na mpira maisha a ya rufaa yake kugonga mwamba.
Polisi Tabora itaendelea kutumikia adhabu ya kushushwa daraja kutokana na rufaa yao kutupiliwa mbali, wakati JKT Oljoro adhabu yake ya kushushwa daraja itaendelea, bali watarudishiwa fedha yao ya rufaa shilingi milioni moja kutokana na kanuni kuwa na mapungufu.
Kamati hiyo imetoa siku 10 kuanzia leo kwa warufani kukata rufaa endapo hawakuridhika na hukumu hiyo.

YANGA YAZIDI KUNUSA UBINGWA


MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana walijiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea taji lao baada ya kuibanjua Stand United mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Washambuliaji wa kimataifa, Donald Ngoma na Amis Tambwe ndio walioiwezesha Yanga kuibuka na ushindi huo mnono baada ya kuifungia mabao hayo matatu.

Ngoma alifunga bao la kwanza dakika ya pili kabla ya kuongeza la pili dakika ya 45. Tambwe alifunga bao la tatu dakika ya 63.

Stand ilifunga baola kujifariji dakika ya 81 lililofungwa na mshambuliaji Elias Maguli kwa mkwaju wa penalti baada ya Thabani Kamusoko wa Yanga kucheza rafu kwenye eneo la hatari.

Kutokana na ushindi huo, Yanga inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 68, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 59 na Simba yenye pointi 58.


Monday, May 2, 2016

SIMBA, AZAM HAKUNA MBABE


MATUMAINI ya timu za Simba na Azam kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara, jana yaliingia doa baada ya kutoka suluhu katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Sare hiyo imezifanya Simba na Azam kuendelea kuwa nyuma ya Yanga, ambayo inaongoza kwa kuwa na pointi 65, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 59 na Simba yenye pointi 58.

Katika mchezo huo uliojaa ushindani wa kila aina, timu zote mbili zilicheza kwa kasi kwa lengo la kutafuta mabao, lakini umaliziaji mbovu ulikuwa kikwazo.

Mshambuliaji John Bocco ndiye aliyewanyong'onyeza mashabiki wa Azam baada ya kupoteza nafasi zaidi ya tatu nzuri za kufunga mabao, ambapo mashuti yake yalitoka nje ya lango.

Sunday, May 1, 2016

YANGA YAZIDI KUUFUKUZIA UBINGWA


MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana walizidi kujisafishia njia ya kutetea taji lao baada ya kuichapa Toto Africans mabao 2-1.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Toto Africans ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwabao 1-0.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa inazo pointi 65 baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 58 na Simba yenye pointi 57.

Iliwachukua Toto dakika 39 kufunga bao la kwanza, lililopachikwa wavuni na Williams Kimanzi, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Abdalla Seseme.

Baada ya kufungwa bao hilo, Yanga iliongeza kasi ya mchezo huku ikihaha kutafuta bao la kusawazisha, lakini ilikumbana na kizingiti kigumu cha mabeki wa Toto.

Juhudi za Yanga kusawazisha zilizaa matunda dakika ya 50 baada ya Amis Tambwe kufunga bao kabla ya Juma Abdul kuongeza la pili dakika ya 78.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo wakati miamba ya soka nchini, Simba na Azam itakapomenyana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.